Katiba Mpya: Tunachotaka sasa

2015ready

JF-Expert Member
Feb 15, 2011
372
130
Katiba Mpya: Tunachotaka sasa



Na Mabere Marando - Imechapwa 20 April 2011
(Source - Mwanahalisi)


KUNA madai kwamba kinachohitajika sasa ni kuwaelimisha wananchi juu ya katiba iliyopo kabla ya kuandika katika mpya. Nina maoni tofauti.
Suala la leo si kujua katiba yetu ya sasa. Hoja ya sasa ni Watanzania kuzingatia kinachostahili kuwa katika katiba yao waliyoshiriki kuandika.
Katiba inakuwa na vipengele vingi. Hapa natataja baadhi ambavyo vinaweza kuchochea mjadala.

Fursa za kuchagua
Wananchi wawe na fursa kuchagua viongozi wao. Kwa sasa viongozi wenye nguvu ya utawala juu ya wananchi, huteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Chukua mfano wa wilaya moja ya Tanzania. Ina mbunge mmoja au pengine wawili, kwa zile wilaya zenye majimbo zaidi ya moja. Mbunge hana nguvu ya utawala wilayani.

Mbunge hawezi kuamuru polisi, usalama wa taifa au mgambo katika wilaya hiyo. Kiongozi mwingine ni Mwenyekiti wa Halmashauri wa wilaya au Meya wa Manispaa.
Hawa nao hawana nguvu za dola katika wilaya au manispaa inayohusika. Zaidi ya hapo, mwenyekiti au meya anachaguliwa na jopo dogo tu la madiwani, hana ridhaa ya wananchi wa wilaya au manispaa anayiiongoza.
Kiongozi pekee mwenye nguvu za dola katika wilaya ni Mkuu wa Wilaya. Huyu ni kiongozi wa kisiasa anayetokana na chama kinachotawala.

Huyu anateuliwa na rais. Utiifu wake wote ni kwa huyo aliyemteua. Hana sababu yoyote ya kuhofia hisia za wananchi wa wilaya juu yake.
Hata akiwa mzembe kiutendaji, wananchi hawawezi kumwondoa. Hata bei ya sukari, unga, maharage na vingine ziongezeke kwa kiwango gani, yeye hana msukumo wa kushughulikia hayo kwa sababu, wapigakura wa wilaya hiyo hawana mamlaka juu yake.

Leo hii, wakazi wa Dar es Salaam ni takribani milioni nne. Mkuu wa mkoa wao anatoka mikononi mwa rais.
Zanzibar, ambao ni kama watu milioni moja humpigia kura rais wao. Nchi ya Shelisheli (Seycheles) ina kama watu laki mbili, lakini wanachagua rais wao.
Inakuwaje wakazi wa Dar es Salaam, ambao ni milioni nne, wapewe kiongozi kutoka mikononi mwa rais?

Angalia hili. Wilaya ya Kinondoni ina watu karibu milioni mbili, lakini hawamchagui kiongozi wao mwenye mamlaka ya dola.
Kinondoni wanakabidhiwa mtawala na rais; na haimsumbui hata kidogo mtawala huyo, kama tuna umeme au hatuna; au kama viwanja vya wazi vinachukuliwa na matajiri.

Mkuu wa wilaya hajali kama mitaro ya eneo la Msasani imezibwa na matajiri; au mvua zikinyesha maji machafu yanaingia katika nyumba za wananchi.
Katika nafasi hii, mkuu wa wilaya au mkoa, hatishiki kwani hakuchaguliwa na wakazi wanaolia na kusaga meno. Hata watawala wanawajibika kwa yule aliyewateua.
Msimamo wa CHADEMA ni kwamba viongozi wote wa wananchi, wachaguliwe kwa kura ili wawajibike kwa wapigakura wao. Waogope kwamba wasipotatua kero za wananchi watatupwa nje katika uchaguzi unaofuata.
Hii ni sera tofauti na ile ya CCM. Ni sera inayokabidhi utawala wa nchi kwa wananchi. Tunataka Katiba yetu iwe na kipengele hicho.

Baraza la mawaziri
Kwa mujibu wa katiba ya sasa, baraza la mawaziri linateuliwa kutoka miongozi mwa wabunge. Katika Bunge la wabunge takribani 300, karibu wabunge 60 wanakuwa ni mawaziri na naibu mawaziri.
Athari yake mbaya ya kwanza ni kwamba mtindo huu unavuruga msingi wa mganganyo wa madaraka miongoni mwa mihimili mitatu ya Dola (serikali, bunge na mahakama).

Mawaziri ambao ni sehemu ya serikali wanakuwa vilevile ni sehemu ya mhimili wa kutunga sheria na wanapiga kura.
Kwa njia hii, nguvu ya bunge kusimamia/kudhibiti serikali, inapunguwa sana. Mgawanyo wa madaraka miongoni mwa mihimili unakuwa mgawanyo bandia; sema “danganya toto.”

Njia hii pia huwapa wale mawaziri nafasi kubwa ya kupendelea sehemu wanakotoka wakati wa kupewa fedha za maendeleo.
Katiba zenye kutekeleza kiukweli dhana ya mgawanyo wa mihimili, zinaweka vifungu vinanavyomwelekeza rais kuteua baraza la mawaziri kutoka nje ya bunge.
Katika kitabu chake kiitwacho “Tujadili Katiba Yetu,” Prof. G.M. Fimbo anasema:
“Katiba imuelekeze rais kuwapata mawaziri kutoka kwenye vyama vya siasa (si lazima wote wawe wanachama wa chama chake cha siasa), serikali taasisi za umma, vyama vya hiari, vyama vya wanataaluma. Katiba imuelekeza rais kuwakwepa wafanyabiashara wakubwa katika uteuzi wa mawaziri…”
Hayo ni mapendekezo sahihi ya wataalam wetu. Vilevile bunge liwe na madaraka ya kukosa imani na waziri yeyote, na ikitokea hivyo, basi rais analazimika kumuondoa na kumteua mwingine. Katiba ya namna hiyo itawapa wabunge nguvu ya kusimamia vema serikali.

Uchaguzi wa rais
Tangu enzi za chama kimoja, katiba ilizuia mtu yeyote kuwasilisha mahakamani malalamiko kupinga uchaguzi wa rais. CCM bado inatetea dhana hii wakati wananchi wameona jinsi kura za sasa zinavyopigwa kwa ushindani baina ya vyama.
Wananchi wanaona kabisa kwamba kuna taratibu za sheria katika uchaguzi wa rais. Nchi nyingi zinazothamini demokrasia zimetunga vipengele katika katiba vinavyoruhusu mtu yeyote kulalamikia uchaguzi wa rais kama anao ushahidi wa kuvunjwa kwa sheria za uchaguzi huo.

Huu nao ni msimamo wa CHADEMA; tofauti kabisa na msimamo wa CCM. Kinacotakiwa ni kuwekea mahakama muda maalum wa kupokea ushahidi na kumaliza kero za namna hiyo.
Usikilizaji wa kesi za namna hiyo uwe ndani ya muda usiozidi mwezi mmoja ili nchi isitetereke kiusalama. Majirani zetu Uganda na Kenya wana vifungu kama hivyo katika katiba zao, na chaguzi za maris wao zimehojiwa mahakamani.

Vifungu hivyo vinasaidia kupunguza tabia za vyama tawala kutumia mbinu chafu na maofisa wa usalama wa taifa, kuchakachua kura za urais kwa kuwa ushindi uliotangazwa na Tume ya Uchaguzi hauhojiwi mahakamani.
Rais kusaini sheria
Kwa mujibu wa katiba ya sasa, bunge lina mamlaka ya kutunga sheria, lakini muswada hauwi sheria kamili mpaka rais autie saini. Inaweza kutokea pia bunge likapitisha sheria na rais akakataa kutia saini.
Rais akikataa, muswada unarudishwa bungeni na maoni yake kwanini anaukataa. Kwa utaratibu wetu wa sasa, wabunge waking’ang’ania msimamo wao na kushindana na rais, basi rais anayo madaraka ya kuvunja bunge.
Ilitokea hivyo mwaka 1973, bunge lilipotofautiana na Rais Julius Nyerere juu ya muswada wa kodi ya mapato. Alikwenda bungeni na kuwatishia wabunge kuwa waking’ang’ania msimamo wao atavunja bunge.
Walipoitwa tena kwenda kujadili upya muswada huo, wabunge “walifyata mkia” na kuupitisha bila mjadala.

Hiyo siyo demokrasia. Pamoja na kwamba rais amechaguliwa na nchi nzima, lakini wabunge pia, kwa pamoja, wamechaguliwa na nchi nzima; na kwa pamoja ni wengi kuliko rais mmoja.
Kama kweli Bunge ndiyo mhimili wa tatu wa dola, wenye dhamana ya kutunga sheria, basi hapana budi liwe na kauli ya mwisho dhidi ya rais ambaye ni kiongozi wa serikali (Executive).
Kwa hiyo basi, katiba mpya sharti itamke kuwa, kama bunge likimrudishia rais muswada kwa mara ya pili, na bado anaukataa, basi mkataba huo utakuwa sheria kamili hata bila saini yake, baada ya kipindi fulani kitakachowekwa.
Hili laweza kufanyika chini ya kipengele kinachotambua kiuhakika mamlaka ya bunge kama mhimili wa tatu wenye dhamana ya kutunga sheria.
Jirani zetu katika Jumuia za Afrika Mashariki – Kenya na Uganda wanacho kifungu kama hicho. Sioni kwanini sisi tusiwe nacho.

Viongozi wanaoiba
Kuna viongozi wa kisiasa wanaoibia nchi zao utajiri wa maliasili badala ya kutumia utajiri huo kuendeleza nchi zao. Wananchi wanabaki maskini sana.
Msimamo wa CHADEMA ni kwamba katiba mpya ilinde maliasili na rasilimali za taifa; kwa kutamka wazi kwamba mikataba mikubwa inayohusu madini lazima, mafuta, gesi, misitu, iidhinishwe na Bunge.
Kwa mfano katika mapendekezo ya katiba mpya ya bunge Kenya kifungu cha 71 kilisema kwamba:
Mkataba utaidhinishwa na bunge kama utakuwa ni wa uchimbaji wa madini na maliasii za Kenya; na

Bunge litatunga sheria itakayoweka ni aina gani ya mkataba ambayo lazima utaidhiniswa na bunge.”
Katika nchi yetu tumeona malalamiko ya wananchi kuhusu madini yao yanavyoporwa. Makampuni ya Ulaya yanachimba dhahabu zetu na kutuachia mashimo matupu huku wale wanaotia saini mikatana hiyo wakineemeka.
Katika hili, mawaziri ambao ni viongozi wa kisiasa, wasiruhusiwe kutia saini mikataba kama hiyo. Hizo ni kazi za kiutendaji ambazo ni za makatibu wakuu na watendaji wengine.

Tume ya Uchaguzi
Tangu uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi kumekuwepo malalamiko. Tume ya uchaguzi imekuwa tume ya rais amabaye mwenyekiti wa CCM – chama kimojawapo miongoni mwa vyama vinavyoshindana. Watanzania wote wameshakubaliana kuwa tume hii siyo huru.
Mtendaji mkuu wa tume, Mkurugenzi wa Uchaguzi, naye anapewa ajira na rais, huyohuyo mwenyekiti wa CCM. Hakika wana kila sababu kuhakikisha mwenyekiti wa CCM anaendelea kuwa madarakani ili walinde ugali wao.
Katiba mpya iweke utaratibu tofauti kabisa juu ya kupatikana kwa wajumbe wa Tume ya uchaguzi. Wengine wanasema nafasi zitangazwe ili watu waombe, wasailiwe na wale wanaofaa waajiriwe kwa kipindi maalumu chini ya bunge.

Wengine wanasema wajumbe watokane na vyama vya siasa watakaopendekeza majina ambayo rais atateua bila kubadili; na mapendekezo mengine mengi.
Kwa vyovyote vile, ni muhimu mwenyekiti wa chama kilicho katika ushindani anyang’anywe madaraka ya kuteua wajumbe wa tume ya uchaguzi ambao hawatawekwa kiganjani mwa chama tawala.
Kwa maoni yangu hata tume ya uchaguzi Zanzibar haijawa huru, kwani ni ya vyama viwili vilivyoungana katika utawala.

Wakuu wa majeshi
Nafasi nyeti kama za Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Jaji Mkuu wa nchi, ni muhimu wanaozishikilia waidhinishwe na bunge ingawa rais bado anaweza kuwateua.
Hii itafanya wawakilishi wa wananchi kuwa na sauti juu ya kupatikana kwa viongozi katika nafasi nyeti. Aidha, kutazuia uwezekano wa rais kuteua watu kwa kuzingatia sifa zingine zisizohusiana na uwezo wao katika kazi wanazopewa.

Kumwondoa mbunge
Baadhi ya wabunge “hupotea” baada ya kuchaguliwa. Hawarudi majimboni mpaka wakati wa uchaguzi unaofuata. Ili kudhibiti hali hiyo, katiba mpya iwape wapigakura haki ya kumuondoa mbunge kama huyo kabla ya muda wake wa miaka mitano kuisha.

Fursa ya hoja binafsi
Chini ya katiba mpya, wananchi hata bila kupitia kwa mbunge wao, wawe na haki ya kuwasilisha hoja (right to petition parliament).
Makundi mbalimbali ambayo yanaweza kuona hayatandewi haki na wabunge hawajali, yapate haki ya kuwasilisha hoja (petition); na utaratibu uwekwe ili makundi kama hayo yaweze kuwasilisha hata miswada, ili wabunge waijadili na hata kuipitisha.

Viongozi wa vyama
Vyama vya siasa vina viongozi wenye uwezo. Lakini wakigombea ubunge au urais wanaweza kushindwa, ingawa wana hazina kuu ya maarifa ambayo ingenufaisha taifa kama wangekuwa bungeni.
Katiba mpya iweke mfumo ambao utahakikisha watu kama hao wanaingia bungeni.

Kwa mfano, badala ya rais kuteua watu kuingia bungeni kwa misingi isiyoeleweka kama ilivyo sasa, katiba itamke kuwa kiongozi wa chama ataingia bungeni iwapo chama chake kitapata asilimia fulani (kama tano), hata kama hakikushinda uchaguzi.
Hili litaimarisha demokrasia.
Sababu za msingi
Hapa nimetoa mifano michache tu ili wananchi wajue kwamba CHADEMA ina sababu za msingi inapodai Katiba Mpya.
Hadi sasa wananchi wengi wamekubaliana kwamba mapendekezo ya muswada wa CCM si sahihi na ni hatari. Ndiyo maana umma umelazimisha serikali kuuondoa.
Je, tume ya kukusanya maoni ya wananchi ipatikaneje? Iteuliwe na CCM au ipatikane kwa njia nyingine? Je, rasimu ya awali ya tume hii iwasilishwe kwa mwenyekiti wa CCM au itangazwe kwenye magazeti ili ijadiliwe na watu wote?
Je, vyama vya siasa vishiriki katika kampeni ya kura ya maoni au la? Haya ni maswali muhimu ambayo majibu yake yatapatikana katika mijadala inayoanza sasa. Wewe unasemaje?

Wana JF - Kwa maoni yangu, nakubaliana kabisa na Marando. Hivi ndio vipengele muhimu ambavyo ni lazima viwekwe kwenye katiba mpya. Tukifanikisha kuviweka vipengele hivi, tutakuwa na katiba ambayo inalingana kabisa na inchi zinazo heshimu demokrasia ya kweli.
Naomba tuijadili hii.
 
Back
Top Bottom