Katiba Mpya Ni Tumaini Jipya Kwa Watanzania ( Makala, Raia Mwema)

maggid

JF-Expert Member
Dec 3, 2006
1,084
1,246
( Makala hii imechapwa kwenye Raia Mwema, juma hili)

Na Maggid Mjengwa


AFRIKA mvua hainyeshi ghafla, utanguliwa na mawingu . Ndio, hakuna mvua isiyo na dalili. Muhimu ni kusoma alama za nyakati.

Kwa wenyeji wa Pwani wanaelewa tabia za miti hii; mkwaju na mnazi. Upepo mkali ukivumia uliko mkwaju, basi, mti huo huwa na tabia ya kuinama kwa kufuata nguvu ya upepo. Upepo ukipita, mkwaju husimama tena. Mnazi ni tofauti, hushindana na nguvu ya upepo mkali. Upepo ukiwa mkali sana, mnazi utaanguka, hautasimama tena.

Kauli ya Waziri Mkuu, Mzengo Pinda juu ya Katiba, japo kwa wakati huu, inaitofautisha Serikali na tabia ya mnazi. Waziri Mkuu Pinda aliongea maneno ya hekima sana. Pinda alikubali kuwa hoja ya Katiba ni hoja ya msingi. Kwamba Serikali yetu ni sikivu, na kuwa yeye, kama Waziri Mkuu, atakwenda kumshauri Rais juu ya jambo hilo. Ningemshangaa sana Pinda kama angekurupuka na kutamka, kuwa Katiba iliyopo itabaki kuwa hiyo hiyo, haitarekebishwa. Pinda angekuwa ameonyesha udhaifu mkubwa katika uwezo wa kusoma alama za nyakati.

Maana, kwa sasa, upepo wa mabadiliko unavuma, si katika nchi yetu tu, hata nje ya mipaka yetu. Nilipata kuandika, kuwa matokeo ya uchaguzi mkuu uliopita yalituma ujumbe mmoja mkuu kutoka kwa wapiga kura; MABADILIKO, kwamba idadi ya Watanzania wenye kiu ya kutaka uwepo wa mabadiliko inaongezeka kila kukicha. Katika hali ya sasa, hali ya wengi kukata tamaa juu ya hali zao za maisha na hata kuwa na hofu ya mustakabali wa nchi yao, ujio wa Katiba Mpya imekuwa ni tumaini jipya kwa Watanzania.

Jaji Mstaafu Mark Bomani ameweza kuliweka hili la Katiba kwa namna yake; kuwa Katiba mpya itasaidia kuleta nafuu ya maisha ya Watanzania. Kwamba Katiba Mpya ni muhimu kwa sasa na kuwa kuna woga tu katika kuifanyia mabadiliko Katiba yetu.

Ni katika hilo alilozungumza Jaji Bomani ndipo tunapoona mawili katika Katiba mpya inayosubiriwa; tumaini kwa wananchi, na hofu kwa baadhi ndani ya mfumo uliopo. Tumaini la Katiba mpya kusaidia katika kuleta hali bora kwa mwananchi na hofu ya katiba mpya kupelekea kwa baadhi kupoteza mamlaka zao na hivyo maslahi yao binafsi au ya vikundi vya wachache.

Na umma nao una hofu, kuwa wanasiasa wachache, kwa kutanguliza maslahi yao. Wataogopa mabadiliko ya Katiba na kuwa tayari kuliingiza taifa katika machafuko, ilimradi wazidi kung’ang’ania madarakani, kwa maslahi binafsi. Umma una hofu ya amani na utulivu wetu kupotea kwa vile wachache wana hofu ya kupoteza maslahi yao.
Katiba mpya kwa sasa ni matakwa ya sehemu kubwa ya umma kwa maslahi ya umma. Si jambo la vyama vya siasa pekee. Inatuhusu sote kama taifa. Maana, hii ni nchi yetu sote, na inahusu mustakabali wa nchi yetu. Ni ukweli, kuwa Katiba yetu ya sasa haikidhi matakwa ya wakati uliopo. Haikidhi matakwa ya ujenzi wa taifa la kisasa.

Swali lisiwe; je, tubaki nayo kama ilivyo au irekebishwe? Bali ni nini kinahitajika na lini itaanza, kazi ya kuifanyia marekebisho makubwa katiba yetu?
Tumeanza kujikita katika kutafuta tafsiri ya nini tunachotakiwa kufanya; kuifanyia marekebisho Katiba au kuandika katiba mpya? Tunahangaika bure na misamihati. Maana, hata Rais akivunja Baraza lake la Mawaziri hupanga upya, huingiza sura mpya na nyingine za zamani hurudi. Bado tunasema baraza jipya la mawaziri. Upya hapa una maana pia wa kile kinachotoka baada ya kufanyiwa marekebisho. Hivyo basi, Katiba iliyofanyiwa marekebisho yaweza kuitwa Katiba Mpya.


Tunachotaka kufanya kama nchi ni kuifanyia marekebisho Katiba yetu. Swali hapa ni je, yafanyike marekebisho madogo au makubwa? Kwa tafsiri ya upepo unaovuma sasa, Watanzania tunahitaji mabadiliko makubwa ya Katiba. Kuna mambo muhimu yanatakiwa kufanyiwa marekebisho na kuwekwa wazi, kama vile mgawanyo wa madaraka ndani ya mihimili mitatu ya dola; Rais ( Utekelezaji) Bunge ( Sheria) na Mahakama ( Hukumu).

Inahusu pia haja ya uwepo wa Tume Huru ya Uchaguzi na mfumo wenyewe wa uchaguzi.
Maana, moja ya sababu kubwa ya nchi zetu hizi kubaki nyuma kimaendeleo ni ukweli kuwa zimekuwa zikitumia Katiba zilizotokana na wakoloni. Malengo makuu ya Katiba hizo yalikuwa ni kuonyesha namna mtawala atakamvyotawala mtaliwa bila mtaliwa kuwa na fursa ya kumdhibiti mtawala. Na mtawala kwa maana ya mkoloni lengo kuu la kuwa na koloni ni kuvuna rasilimali za koloni husika.

Hivyo basi, kwa kuendelea kutumia Katiba zilizotokana na katiba za kikoloni kumepelekea kutoa nafasi kwa wachache waliopewa dhamana za uongozi, kwa kutanguliza ubinafsi wao, kujilimbikizia mali na hata kutumika kama makuwadi wa kinachoitwa Soko Huria. Yote haya kwa gharama ya machungu makubwa kwa wana wa nchi.

Ndio maana, Katiba Mpya inayotokana na wananchi wenyewe inaweza kabisa kudhibiti kwa kiasi kikubwa wizi wa mali ya umma ikiwamo kuwadhibiti wale wenye kutuingiza kwenye mikataba mibovu na isiyo na maslahi kwa taifa na bado wakabaki salama kwa kulindwa na Katiba iliyopo. Maana, ni mapungufu haya ya Katiba ya sasa tunayoyazungumzia, ndio yamepelekea wananchi wenye uchungu wa nchi yao kuitwa ’ wenye wivu!’. Ni ajabu kubwa sana, mwenye mali anamkemea mwizi wa mali yake na mwizi anajibu; ” Una wivu wewe!” Eti uchungu umegeuka wivu kana kwamba mwizi huyo ameiba mume au mke wa mtu!

Kinachohitajika katika Katiba yetu ya sasa ni kufanyiwa marekebisho makubwa. Marekebisho madogo ndio yenye kutoa tafsiri ya ’ viraka’. Wananchi wamechoka na ’viraka’. Na katika hili la Katiba, haiyumkini kuwa yote yaliyomo katika Katiba ya sasa ni mabaya, la hasha. Kuna mazuri. Ni matumaini yetu, kuwa Serikali yetu sikivu itaunda jopo litakalotokana na wawalishi wa makundi mbali mbali ya kijamii kujadili namna njema tukavyopata Katiba mpya.

Kinachohitajika ni jopo shirikishi litakalopewa jukumu la kuipitia Katiba ya sasa ili wayaangalie mazuri na mapungufu yaliyopo. Waingize yale mapya muhimu kwa wakati tulio nao. Kisha waje na rasimu ya Katiba hiyo ili wananchi tusome, tujadili na hatimaye tuipigie kura ya kuikubali au kuikataa. Kujifunza huanzia kwa jirani. Hakuna ubaya kuiga mazuri waliyofanya jirani zetu wa Kenya.

Hata hivyo, Katiba Mpya haitakuwa muharobaini wa matatizo ya nchi yetu, bali, inaweza kabisa kusaidia kuleta nafuu ya maisha kwa Watanzania. Ndio, yawezekana kabisa tusipate Katiba bora sana, lakini, kwa kuilinganisha na hii ya sasa, Katiba Mpya tarajiwa na wengi itakuwa na afadhali mno.

Ndoto yangu, kama Mtanzania mzaliwa wa nchi hii, ni kuishi na kuja kuisoma rasimu ya Katiba Mpya na hatimaye kushuhudia kuzinduliwa kwa Katiba Mpya iliyotokana na matakwa ya Watanzania. Kwangu, hiyo itakuwa ni juzuu (kitabu) muhimu kabisa kuisoma maishani mwangu. Maana, nitakuwa nimeishi na kuona urithi wenye maana kubwa tutakaowachia watoto na wajukuu zetu. Urithi muhimu kwa vizazi vijavyo. Nahitimisha.

mjengwa
 
Back
Top Bottom