Katiba mpya ni sawa na kupindua nchi - Nimrod Mkono

Jana nilimsikiliza mh Dr Slaa akikosoa utaratibu uliopendekezwa na mheshimiwa Raisii wa kuunda Tume ya Katiba. Kwa maoni yake, isingekuwa busara na salama kama maoni juu ya katiba mpya yakikusanywa na Tume iliyoundwa na Raisi na badala yake kazi hiyo ingefanywa na Bunge. Kwa upande wa pili, alionesha mapungufu yaliyomo katika Katiba yetu yanayohalalisha mahitaji ya Katiba mpya. Kwa ufupi, alizungumzia matatizo makuu matatu. La kwanza, mgawanyo wa madaraka katika ya mihimili mikuu ya dola (Bunge, Mahakama na Utawala). Kwamba Katiba iliyopo haiweki vizuri mipaka na madaraka ya vyombo hivi. Pili alizungumzia kuhusu mapungufu yaliyomo katika masuala ya haki za binaadamu. Na mwisho alizungumzia madaraka ya Raisi na kusema ni makubwa zaidi yanahitaji kurekebishwa. Alitia msisitizo kwamba hayo mambo ni mhimu kuzingatiwa kwa kuwa katiba si mali ya Serikali bali ni mkataba kati ya watawala na watawaliwa.

Naomba nichangie hoja nzuri za mheshimiwa Dr Slaa kama ifutavyo. Kwanza, kuhusu Bunge kuunda Tume ya kukusanya maoni juu ya mabadiliko ya katiba, mimi naona itakuwa ni vigumu kiutekelezaji. Kama Dr Slaa anakusudia kwamba Bunge liunde Tume toka miongoni mwa wabunge, haitakuwa na maana kubwa kidemokrasia ukizingatia kwamba wabunge wengi ni wa chama kimoja na mbali ya maslahi ya wananchi wanaowawakilisha pia wanafungwa na maslahi ya chama. Na kama alikusudia kwamba Bunge iunde Tume hiyo toka kwa wananchi wasio wabunge tatizo litakuwa katima maeneo mawili. Ni nani atakayependekeza wanaofaa kuwemo katika Kamati hiyo. Kama kutakuwa na tofauti za maslahi ya kisiasa katika upendekezaji huo, maamuzi ya kura yatatoa muelekeo sahihi kuhusu uwezo, uaminifu na uhuru wa wana tume? Labda sehemu nayoweza kukubaliana na DR SLAA labda angesema kwamba Raisi ateuwe wajumbe wa Tume hiyo toka kwa wawakilishi mbalimbali wa kijamii, kitaaluma na kisiasa kama alivyopendekeza na baadae apeleke Bungeni kwaajili ya kupitishwa.


Kuhusu mapungufu yaliyomo katika katiba iliyopo, mimi tatizo ninaloliona ni kwamba wanasiasa wako mbele zaidi katika kuunga mkono misimamo yao bila kwenda hatua moja zaidi kuhalalisha kihoja misimamo yao. Nionavyo mimi, pande zote mbili zinakubali kwamba kuna matatizo katika Katiba yetu. Kiini cha ubishi ni kama matatizo yamaweza kuondolewa kwa kuwa na katiba mpya au marekebisho? Ili kuwaweka wananchi wa kawaida katika nafasi nzuri ya kuamua ni bora tukawapa faida ya kuwa na katiba mpya badala ya kurekebisha iliyopo na kinyume chake.

Ukisema katiba iliyopo inatoa madaraka makubwa kwa Raisi na haiweki vizuri mipaka ya mihimili ya dola, mtu anaweza kusema kwamba hilo linaweza kurekebishwa kwa kuondoa vifungu vinavyompa zaidi mamlaka Raisi na kuweka vifungu vingine vinavyotowa mamlaka hayo kwa watu na mihimili mimgine ya dola, kadili utashi wa watu utakavyoelekeza. Kama suala la Haki za Binaadamu, katiba yetu ina sura nzima ya haki za binaadamu. Mapungufu yaliyomo katika vifungu vya haki za binaadamu kama vile vifungu vinavyohalalisha unyimwaji wa haki kwa vigezo ya maslahi ya umma, hiyo ianaweza kurekebishika kwa kuvifuta vifungu hivyo na kuongeza haki zingine za binaadamu kadili utashi wa watu utakavyoamua. Ilikuwa ni mhimu kwa wanasiasa kuonesha ugumu wa matatizo haya kuondolewa kwa njia ya marekebisho ya Katiba.

Kuamua tu kwamba matatizo ya kikatiba yanapaswa kuondolewa kwa kuandika katiba mpya au kurekebisha iliyopo bila kutoa hoja za msingi za kuhalalisha ni kuingilia uhuru wa wananchi wa kuamua kwa kuwafanya baadhi ya wanasiasa au wanaharakati kuwa wasemaji wa wananchi. Kazi ya kwanza ya Tume huru itakayoundwa kwa maoni yangu, ingekuwa ni kukusanya maoni ya wananchi kama wanataka katiba mpya au marekebisho ya Katiba. Na hilo lifanyike baada ya kuwaelimisha watu juu ya mapungufu yaliyomo katika Katiba yetu. Hili litawafany wananchi kuwa sehemu ya mchakato mzima wa mageuzi ya katiba badala ya kuwashirikisha nusu nusu wakati tayari mmeshawaamlia kwamba inatakiwa katiba mpya au hii iliyopo kutiwa viraka. Umhimu wa kuwashilikisha wananchi katika hilo unatokana na ukweli kwamba kuna sauti kinzani zisizorasmi katika mitizamo hii miwili. Na pili ni kutokana na uelewa mdogo wa watu wengi kuhusiana na mapungufu na mazuri yaliyomo katika Katiba yetu.

Nakubaliana kabisa na Dr Slaa kwamba Katiba sio mali ya Serikali. Naongezea kwamba Katiba pia sio mali ya Bunge, sio mali ya Mahakama, sio mali ya wanasiasa wala sio mali ya wasomi na wanaharakati. Katiba ni mali ya watu. Katiba, kwa maoni yangu, sio mkataba kati ya watawala na watawaliwa kama wanafalsafa wa zama za kale walivyoielezea, bali ni amri na muongozo wa watawaliwa (watu) kwa watawala. Tukisema Katiba ni mkataba kati ya watawala na watawaliwa tunamaana kwamba katiba ni mali ya watawala na watawaliwa. Moja kati ya nguzo mhimu za mkataba ni uhuru na usawa kati ya pande mbili za mkataba kuhusiana na yaliyomo katika mkatba. Mkataba unabadilishwa kwa ridhaa ya pande zote mbili. Watawaliwa wana uwezo wa kusema kwamba hawataki katiba iliyopo na wanataka nyingine hata kama watawala hawataki. Watawaliwa wanaweza kuwaondoa watawala madarakani lakini watawala hawawezi kuwaondoa watawaliwa.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom