Karume alitaka mamlaka ya waliyo wengi na sio umwagaji damu

Jamhuri ya Zanzibar

Senior Member
Jul 17, 2012
126
195
KARUME ALITAKA MAMLAKA YA WALIYO WENGI NA SIO UMWAGAJI DAMU – WALIOUA NI WATANGANYIKA

Hapa kwanza ifahamike kwamba hakuna mipango yoyote ya awali ya kimapinduzi iliyobuniwa au kufanywa na Chama cha Afro Shirazi (ASP) au kiongozi wake wa juu Karume. Rais wa ASP, Abeid Amani Karume, alikuwa akipendelea mizozo ile ya siasa za kuelekea uhuru wa Zanzibar itatuliwe kwa njia za amani na alipendelea upinzani makini na wa kistaarabu na utii mkubwa bungeni uendelezwe ili kuepuka Serikali kutumia sheria na nguvu za dola dhidi ya chama cha ASP na wanachama wake.

Hii ina maana kwamba Karume hakutaka matumizi ya ghasia au malumbano na Serikali iliyokuwa madarakani nje ya Bunge. Kwa hivyo ni kusema kwamba aliitambua Serikali iliokuwa madarakani na alikuwa tayari kutekeleza wajibu wake wa kidemokrasia ndani ya Bunge kama mpinzani wa serikalikwa maendeleo ya Wazanzibari. Sheria mbili kati ya saba za chama cha Afro-Shirazi wakati huo zilikuwa zinasema hivi kuhusu malengo ya chama hicho:

1. Kutafuta uhuru na utawala kamili utaokuwa miongoni mwa Dola zilizomo katika Shirikisho la Udugu na Dola ya Kiingereza…
2. Kuifanya na kuiamirisha Serikali ya Kidimokrasi katika visiwa vya Unguja na Pemba chini ya utawala na utii kwa Bwana Seyyid Mtukufu.

Timu ya asili ya mipango ya mapinduzi bila shaka iliongozwa na akina Abdalla Kassim Hanga, Saleh Saadalla Akida, na Abdulaziz Twala(Ghassany 2010). Hoja pia zinatolewa kukanusha kuwepo kwa kamati ya watu 14 kabla ya Januari 12. Kamati ya Watu 14 walikuwa ni vijana wa Afro-Shirazi Party Youth League ambao wakichukuwa miongozo kutoka kwa akina Hanga. Ukweli ni kwamba akina Hanga, Saadalla, na Twala walikuwa ni viongozi wasomi na wakiupinga vikali uongozi wa Karume, wakati vijana wa Afro-shirazi Youtu League ambao takriban wote hawakusoma walikuwa ni maswahiba na Karume.

Katika kitabu chake cha The Partner-ship: Tanganyika Zanzibar Union: 30 Turbulent Years, Mzee Aboud Jumbe anakiri kwa kusema "ijapokuwa nilikuwa Katibu wa Mipango wa chama cha Afro-Shirazi, sikujuwa vizuri asubuhi ya tarehe 12 Januari 1964. Ilikuwa ni siri iliyohifadhiwa vizuri ambayo ilifahamika na uongozi wake tu. Mpaka hii leo hadithi kamili imefungwa ndani ya nyoyo na kumbukumbu zao" (Jumbe 1994). Pia Thabit Kombo ambaye alikuwa chini ya Karume pia ndani ya kitabu Masimulizi ya Sheikh Thabit Kombo Jecha kilichoandikwa na Minael-Hosanna O. Mdundo na chenye Utangulizi aliouandika Mwalimu J.K. Nyerere, amekiri utata wa kuhusika ASP katika mipango ya awali ya mapinduzi. Thabit Kombo anasema"Usiniulize vijana wetu walioendesha mapinduzi walipata wapi mafunzo, au nani hasa alivamia mahali gani, mimi sijui. Nasikia hadithi tu kila mmoja akijinasibu baada ya kushinda, mengi ya kweli na mengine ya uwongo mtupu" (Gassany 2010).

Timu ya asili ya mipango ya mapinduzi ni kwamba nayo ilikumbana na mapinduzi mapya muda mdogo baada ya Januari 12. Timu hii bila shaka ilikuwa na mahusiano na timu ya asili katika kuucheza mchezo huu lakini ghafla ilipinduliwa na hivyo basi uongozi mpya ukajitokeza kudai kuwa ndio hasa uliyohusika na mapinduzi hayo na baadae kumkabidhi uongozi wa juu Karume (Ghassany 2010).

Nyerere na serikali yake ndio wadhamini wa Mapinduzi

Zipo hoja zenye kuthibitishwa zinazomshirikisha Nyerere na serikali yake moja kwa moja na mapinduzi ya 1964. Nyerere, wakati huo akiwa rais wa Tanganyika alishiriki kwa asilimia mia basi si katika mapinduzi ya Zanzibar lakini kwa staili ya nyuma ya pazia. Aliamini kwamba wanzanzibari walio wengi ni watu wa asili za Tanganyika na hivyo Zanzibar ni ndugu ya Tanganyika. Nyerere kama ilivyokwisha kuelezwa huko nyuma alianza ushawishi wake tokea zilipoanza zama za siasa miaka ya 1950 (Gassany 2010).

Ripoti ya Helen-Louise Hunter, mtafiti na mtaalamu wa kiuchumi na kisiasa alikuwa mfanyakazi wa Shirika la Kijasusi la Kimarekani (CIA) kwa zaidi ya miaka ishirini inasema kuwa kiongozi wa vyama vya wafanyakazi, Abdalla Kassim Hanga, mwana wa ASP aliyeunga mkono ukomyunisti alikuwa na mipango hiyo ya kimapinduzi mapema zaidi bila ya mashirikiano na Babu. Inadaiwa kwamba lipofika katikati ya mwaka 1963 baadhi ya viongozi katika Afro-shirazi (Bila shaka wakiongozwa na Hanga) walikwenda kwa Rais wa Tanganyika Julius Nyerere na kumuomba msaada wa askari na silaha kwa ajili ya kutekeleza azma yao ya Mapinduzi. Katika kitabu chake cha "Kwaheri ukoloni kwaheri uhuru, Zanzibar na mapinduzi ya afrabia"

Harith Ghassany amemnukuu Mzee Mohammed Omar ambae pia alijulikana kama Mzee Mkwawa kwa kuhusiana na Chief Mkwawa akibainisha kwa kina jinsi Nyerere na serikali yake nzima walivyohusika na mapinduzi. Mzee Mkwawa anasema:

"……Hayo yalikuwa na watu wenyewe wa Jamhuri. Yako juu hayo. Vitu vote ni ngazi za juu kuanzia marehemu Nyerere, Kawawa, Kambona, Serkali nzima inajuwa hapo Sakura, na inajuwa, kwa sababu ilikuwa ni intelligence [usalama] ni siri kabisa. Kwa hivyo hivi vitu vinajulikana juu. Kwa sababu wasingeliweza kuwepo pale bila ya ngazi hizo hazielewi. Na sisi tunaelewa, mimi naelewa, kwa sababu ndizo ngazi zilikuwa lazima nizipitie. Kambona ndo alokuwa kiongozi wangu. Kwa sibabu yeye alikuwa ni Waziri wa Mambo ya Ndani. Ndo aloweza kutoa authority [amri] ya hii bahari kuitumia. Na nikapewa kiwango nikifika Chumbe pale mpakani basi huko litakalonikuta ni langu mwenyewe. Lakini huku nna hifadhi ya kupewa, wakati kule bado hakukuwa tayari na utawala. Mara ya mwanzo kusikia habari ya kambi ya Sakura ilikuwa kutoka kwa Maulidi Sheni na yule Mzee, Victor Mkello. Kwa sababu pale ndo ilokuwa kambi kuu. Pale ndo wafanyakazi wa mashamba ya mkonge walikuwa wakipelekwa. Kwa sababu pale ndo ilikuwa kambi kuu. Matajiri wa mashamba ya mkonge walikuwa ni Magirigi na Wahindi walikuwepo, akina Karimjee hawa. Kazi ya Chama cha Kazi kilikuwa kinakwenda kuchukuwa watu, watu wawili watatu, lakini wasikatwe mishahara yao. Katika wafanyakazi wa mashamba ya mkonge walokwenda Zanzibar walitokea sehemu za Tanganyika zaidi ni Wamakonde, Wangoni, Wahehe, Muha, Wahyao, Wahaya, ni mchanganyiko wa makabila. Walikuwa wanachukuliwa hawa watuikiwa wao wenyewe matajiri pia hawajuwi, walikuwa ni wasimamizi tu. [Matajiri] hawajuwi. Kwa sababu yeye achukuliwa mfanya kazi, yeye ajuwa mtu fulani hakuja kazini, ndani ya master roll [daftari la kuhudhuria kazi] wamejazwa. Tajiri yeye hawezi kujuwa. Hawajuwi matajiri. Lakini makarani wale wakubwa, kama mameneja, wakielewa. Kwa sababu msiwakate hawa, wanakwenda saidia umma. Maulidi Sheni khasa yeye ni mtu wa Unguja. Kwao ni Mlandege na nyumbani kwao palepale. Huu mti, ule Mlandege wenyewe uko chini ya nyumba yao. Kwa upande wa mama, nafikiri ni mtu wa Uzini. Yeye msomi. Yeye kenda mpaka Ujerumani bwana. Huyu alikuwa kwenye utawala. Utawala ndo usomi wake. Si alikuwa ni katibu huyu, wa Victor Mkello. Wenzake Maulidi Sheni mmoja ni bwana mmoja kwao Pongwe, ya hapa Tanga, lakini yuko Dar es Salaam. Alikuwa chini ya Maulidi Sheni. Huyu yuhai. Anakaa mtaa wa Magomeni pale. Tukimpata huyu atatwambia katika lile tawi lao. Wote ni wa Chama cha Wafanyakazi na wao ndio wakusanyaji. Victor Mkello alikuwa na Kambona, na mwengine marehemu ameshakufa, ni Issa Mtambo, wa hapa huyu, kwao ni Korogwe. Na huyu ni mmoja alohusika hapo. Ndo alokuwa akigawa mambo ya pesa. Akichukuwa kwa Kambona. Nyerere ilikuwa si rahisi yeye kuja kwenye mambo kama haya. Wengine waliowahi kufika Sakura ni akina [Mustafa] Songambele, kina Mzee Jangukire, John Rupia, walikuwa mstari wa mbele hao. Wao ndo walokuwa mstari wa mbele wanopanga. Songambele, alikuwa ni Area Commissioner wa Dar es Salaam. John Rupia ndo mwenyewe, ndo alokuwa tajiri kwa wakati ule, kifedha. Alokuwa IGP, Mzee Hamza Aziz, akijuwa…………."

Ijapokuwa Nyerere mwenyewe alikanusha sana kushiriki kwake lakini ushahidi upo wazi kuwa aliicheza vyema ngoma hii ya mapinduzi. Ni askari wake wapatao mia sita ndio waliotekeleza mapinduzi hayo. Katika video ya mapinduzi hayo iliyochukuliwa kwa siri na Mtaliana ambayo aliitengenezea filamu ya African Addio inawaonyesha wazi wazi askari walivalia mavazi rasmi ya askari wa Tanganyika.

Halkadhalika sauti za askari hao katika filamu hiyo zinadhihirisha wazi kuwa watu hao ni watanganyika. Meli ya silaha ikitokea Tanganyika ilitia nanga Unguja muda wa kiasi cha masaa 48 kabla ya mapinduzi na inasadikiwa Nyerere alihudhuria na kushiriki kuikagua meli hiyo mwenyewe kabla ya safari yake ya kwenda Zanzibar. Silaha nyengine zinasadikiwa kuletwa Unguja kupitia Pemba zikitokea Tanga (Gassany 2010). Hiyo ndiyo hoja wanayoitoa baadhi ya wadadisi kwamba mapinduzi ya Zanzibar yalikuwa ni uvamizi wa Tanganyika chini ya Nyerere dhidi ya Zanzibar kwa kutumia uhasama wa kisiasa wazanzibari uliokuwepo kabla.

Zoezi la mauwaji lilifanywa na watanganyika

Damu ya kizanzibari imejengeka kwa misingi ya ubinadamu na huruma. Utamaduni wa wazanzibari uliojengewa misingi ya itikadi ya uislamu inawakosesha ujasiri wa kudhamiria kushika silaha na kuuwana. Ijapokuwa wazanzibari walishiriki mipango ya mapinduzi lakini wengi wao hawakuweza kushika bunduki wala mapanga kuwakata vichwa na kuwaua wenzao.

Waliotekeleza vitendo vya mauwaji walikuwa ni makomred kwa mashirikiano na watanganyika, watu ambao walikosa itikadi ya kidini na huruma jambo lililowapa ujasiri wa kutekeleza mauwaji kwa mafanikio makubwa. Katika kitabu chake cha "Kwaheri ukoloni kwaheri uhuru, Zanzibar na mapinduzi ya Afrabia".

Harith Ghassany anamnukuu Mzee Issa Kibwana aliyekuwa mmoja wa viongozi wa juu wa kikundi cha Tupendane na aliyekuwa mwanachama wa Afro-shirazi. Hapo awali Tupendane kilikuwa kikundi cha wanyamwezi kilichowachukia waarabu na utawala wa sultani ambao shughuli zao kubwa zilikuwa ni kucheza ngoma na kunywa gongo. Mzee Issa anasema:

"Kwenye mapinduzi ya Zanzibar, mzalia wa Zanzibar, hakuaminika. Kabisaaa! Kwa sababu. Mzee Karume alisema, damu nzito kuliko maji! Mapinduzi yanataka kufanywa, wakishiriki watu Wazanzibari itavuja. Na sababu? Kuwadondowa watu wa bara. Alijuwa tu, hawa wakisema tufanye, watafanya. Mzanzibari akisema tufanye, atarudi nyuma. Na mfano mmoja ulionyesha. Hamid Ameir alisema, Muislamu kuuwa haramuu! Watu wakastaajabu. Muislamu huyu leo akaja kuwa Memba wa Baraza la Mapinduzi (MBM). Imekuwa vipi? Sasa hii pesa anayokula si haramu? Kumbe ilikuwa nini? Moga. Mikidadi ni mtu wa Tanga. Songorokirangwe ni mtu wa Donge, lakini ana asili ya kibara. Mzee Karume akisema, Wazanzibari waliokuwa hawaaminiki sio nlokuwa nao mimi mikokoni mwangu. Mizizi yao ya karibu si ya hapa Zanzibar. Inatoka bara. Hafidh Suleman Mdigo yule. Bavuai yule ni mtu wa hapa, kazaliwa hapa, kama si baba yake, basi babu yake si mtu wa hapa…Hawakuaminika watu wa kusini. Makunduchi. Na Pemba ndo kabisaa! Kwenye listi ya wazee wa mapinduzi, Mmakunduchi mle hayumo. Huyu Ibrahim Amani katiwa tu. Hakushiriki mapinduzi. Kabisaa! Bambi wako wapinduzi. Bambi hiyo, Kinyasini, Mkwajuni palikuwa na wasiwasi, wakadokolewa kidugu Kidoti, wakaja kudokolewa kidugu, wapi? Donge. Wakadokolewa kidugu Mfenesini. Wakaja dokolewa kidugu jimbo la kati hilo hapo, Dole hii mpaka kuja kufikia wapi? Bumbwi Sudi, mpaka Ndagaa. Kwa sababu kule ni mchanganyiko wa watu wa bara. Jimbo la Kati hilo. Sasa Wazanzibari watakuja itazama historia ya Ikulu. Kwa sababu zile picha zote zile wanajuwa huyu ni mtu wa wapi, huyu ni mtu wa wapi. Lakini wengi wao memba wa Baraza la Mapinduzi ni wabara. Mzee Thabit mapinduzi hakushiriki lakini kujuwa anajuwa. Lakini yeye huyu hakuwa memba wa Baraza la Mapinduzi. Sasa pale pameshajitenga. Sasa historia, chanzo chake, hawa kindakindaki [kutoka bara] ndo walolianza suala hili. Wazanzibari, kuwakera kitawakera lakini hilo suala limeshatendeka na wao hawakushiriki. Ndo ukweli wenyewe" (Ghassany 2010).

Pia Harith Ghassany amemnukuu Mzee Mohammed Omar ambae pia alijulikana kama Mzee Mkwawa kwa kuhusiana na Chief Mkwawa akibainisha kwa kina jinsi watanganyika walivyotekeleza mapinduzi. Mzee Mkwawa anasema:

"…………Tukateka. Kwanza ilianguka Mtoni. Yale mabomu zilikuwa ni tambi za kuvunjia mawe majabali ndo zilochomwa katika mageti. Tambi zimechukuliwa kutoka Tanganyika. Tukazipeleka. Kisiri chetu, bila ya serikali kuelewa. Mkono ni Tanga, mapitio ni Tanga. Na wengine kutoka Bwagamoyo, akawa ni Abdalla Kheri, kijana wa Unguja. Abdalla Kheri alikuwa akipeleka watu. Alikuwa mfanya kazi bandari Dar es Salaam. Lakini kwa hamasa ya uchungu wa kampeni kwa kuwa ni mwananchi alijitolea. Alikuwa anachukuwa watu kutoka bandarini, vijana wa Kiunguja, na vijana walio bandarini Dar es Salam, na vijana wa ki-Dareslam, wanaojuwa lafdhi nzuri. Akawapeleka Unguja na akawatafutia malazi pale mpaka siku za uchaguzi, mpaka mapinduzi. Basi kwa hivyo tukafanikiwa kupata serikali. La ukweli, utaweza kuona kuwa wengine hawaelewi, wakaona ramda Waunguja ndio msaada wamejitegemea wao peke yao kwenye mapinduzi. Lakini utakuta si kweli kwa sababu kama ni WaUnguja wenyewe hawawezi kitu. Kwa sababu kwanza ni waoga. Hawakuzowea mambo ya harakati. Kwa hivyo ilikuwa kama ni wao ilikuwa haina maana kwenda kusaidiwa kuandikisha kura, wala kusaidiwa Wamakonde kujitia, vijana kupinduwa, wakashirikiana. Kuna Wamakonde walokuweko kule, kuna Wamakonde walotoka Tanganyika. Na walikuwa wanatoka sehemu za Sakura, wanatoka Ruwazi, Amboni, makabila mengi tu.9 Kulikuwa na Wamakonde, Wangindo, Wayao, Wamwera, Wahehe, na Wanyamwezi wengine, wengi tu. Kama akina Khamis Darweshi ni Myao, Mohamed Kaujore, Mohammed Mfaume, Mmakonde, watu wa Mtwara. Kwa hivyo hao wote Mungu aliwajaalia mapinduzi walipata nafasi ya kupata vyeo. Technique [mbinu] za Afro-Shirazi ziliwafanya wote wapewe uwenyeji, uzalia, wawe ni wenyeji. Wanapewa mababu, wanafundishwa kupewa babu, na kumtambuwa Sheha wa zamani. Yule Sheha aliopo sasa, apewa Sheha wa zamanii asema "wewe ni mwenyeji." Haya yalikuwa ni mahoji ya katika kupiga kura, kufanywa mtu mwenyeji. Unaambiwa "Sheha wako nani." Fulani, Magaramwadi aliyemzaa fulani ndio babu yake fulani. Yule Sheha aliopo akitajiwa yule anaunganisha. Hawezi kuhoji. Katajiwa babu yake. Kwa kuona Tanganyika, visiwani, wote wanodai uhuru ni Waafrika, kwa hivyo walikaa viongozi wakawa wanakutana. Tutashinda au tutashindwa. Tukishindwa tufanyeje. Ndipo wazee wakakaa kitako wakaziba macho yao, na mashikio, wakaweza kuwaachia vijana walio na ari kuingia. Wakati huo kulikuwa hakuna serikali ya Tanganyika. Kulikuwa na serikali ya kikoloni, haijahama. Mwaka 61 Tanganyika inapata uhuru wake, kwa hivyo ikafumba jicho, ikawaachia uhuru bahari ile, vinavyokwenda, madhali vinakwenda upande wa Afro-Shirazi watu wazibe macho wasione, wala nini. Ili kuwapisha Waafrika wapate hatuwa ya kujitawala. Kwa hivyo, vijana waliingia, na shauri walikaa kitako, tukishindwa walikaa pamoja kupeana mawazo. Tufanyeje mpaka tushinde? Hakuna. Wakaamua hakuna. Kama hakuna tukiwavamia WaUnguja wana kitu gani? Basi, kikatokea kikundi, kikakaa kitako, cha Makomred na Youth League. Vijana wa Youth League ni vijana wa Afro-Shirazi. Wakaamuwa twajitolea, hali, mali. Nafsi zetu. Kwa hivyo wakaanza, ndipo kilichopangwa, hapo tena, kikundi cha kuingia watakuwa hivi, hawa watakwenda Bomani, hawa watakaa boma hili. Ikapangwa, ikaenea. Sasa ikawa watu wanakula doria katika sehemu zile kutizama utaratibu. Wakati huu vipi, kuna nani, kuna walinzi gani? Kwa hivyo wakapata fursa. Wakajuwa kumbe tukija hivi tufanye hivi, tutafanikiwa. Lakini humo ndani tuna watu pia, wanojuwa hilo litakalotokea, katika hiyo hiyo serikali ya Mfalme, kuwa kuna watu wetu. Kina marehemu kina Sheikh Daud Mahmud, kwao Kilwa, ni katika hao. Watu wengi karibu Unguja wamechangia suala hilo. Vimezikwa vitu tu mpaka njia za panda. Katikati. Watu wamepiga makafara ya kuwashona paka macho. Nia kubwa Waarabu wapumbaye serikali. Wasiwaze kabisa. Wadharau kila kitu. Hilo ndo lilofanikisha. Hakuna kitu kengine. Kikao kikuu cha kuweza vijana kuchukuwa mazowezi, wa kibara na wa kisiwani [Zanzibar], pamoja, yalifanyika mbuga ya Sakura. Tukichukuwa askari waliowacha vita, walostaafu, tukawapa bunduki, nne, tano, huku na kule, kufundisha namna ya kufetuwa bunduki. Japo ilikuwa hatuna bunduki lakini ilikuwa hayo mazoezi yalifanyika, pamoja na kina Jimmy Ringo [Juma Maulidi Juma]10 wakishaona kuwa hatuna vitu va kuvipata, ndo tulipoamuwa, tutakapovamia, tunapopata bunduki, iwe wawili watatu, wanaweza kuzitumia. Walikuwapo watu kama watu mia na hamsini kwenye mbuga. Walikuwa wanakwenda kikundi cha watu kumi, wanarudi, wanakwenda wingine, wanarudi, sio wote kwa pamoja wanashughulika hizo habari. Waloonekana wameshajuwa wanakwenda zao. Wanavushwa wanakwenda zao. Walozowea wanavushwa wanakwenda zao. Hawana silaha, hawana chochote. Kitu kilichotumika kupinduwa serikali ni mapanga, shoka, misharee! Na pinde hizi. Na hivo vimetoka ndani ya Zanzibar na Tanganyika. Vimenunuliwa na wakapewa watu. Walikuwepo kina Jimmy Ringo, akina Khamisi Hemedi, na vijana wengine. Viongozi wakubwa ni hao. Tulikuwa katika mwaka 1962, Jimmy Ringo alikuwa yuko Tanga barabara ya kumi na tatu kwa Fundi Kidere, halafu akarejea kisiwani Zanzibar. Ndani ya kufanya organisation [mipango] ya mapinduzi ikabidi yeye achaguliwe awe Sakura, yaani kuwashughulikia vijana watakaokwenda kupinduwa serikali ya Zanzibar, kwa hali na mali, wakiwa hawana silaha yoyote isipokuwa mapanga, marungu, mashoka, pamoja na wenzake kina Musa Maisara na Abdalla Kheri. Musa Maisara alikuwa ni kiongozi mkuu, wa pili ni Jimmy Ringo. Abdalla alikuwa akitokea katika safari zake Dar es Salaam anakuja Tanga, anafika Sakura, halafu yeye alikuwa ni msafirishaji pia vijana kutoka Bagamoyo kupitia Fumba, akaingiza mjini Zanzibar. Usaidizi wa kuweza kupinduwa serikali. Alipokuja Jimmy Ringo Tanga pale mwanzo mbuga ya Sakura ilikuwa haijaanza kufanya kazi ya maandalizi ya mapinduzi. YASU [Young African Social Union] ilikuja Tanga 1962 ili kuisadia Afro-Shirazi kupata pesa kwa ajili ya matumizi ya kampeni ya uchaguzi, badala kuwa kama tutashindwa ndio tukakaa kitako kikundi maalum, halafu ndipo tulipoamua tufanye hivo vitu. Uamuzi wa kuijenga kambi ya Sakura tuliufanya kiwiziwizi tu kwanza bila ya kufahamika, baada ya kufahamika sawasawa ni kwenye 1962 mwishoni. Kufikia 1963 watu walikaa wako tayari. Palikuwa na historia. Ile historia ilihusikana na kina Jumaane Abdalla, Regional Commissioner wa hapa, kuamua kuweka Sakura kwa kuwa ni karibu na Kipumbwi, pa kuvukia kwenda Zanzibar. Watu wakitoka pale waingie mojamoja kwenda zao, bila ya kuingia mjini tena. Kuhusu Sakura nilikuwa nikifahamu, kwa sababu nimefahamu kutoka kwa Jimmy Ringo na Musa Maisara, na kujuwa pia kwa kamati nzima kuwa [mimi] ni mbebaji wa watu kuwapeleka na kuwarudisha Zanzibar. Uamuzi mkubwa ulikuwa na kina Jumaanne Abdalla, mimi pia mawazo ya kupatia pesa, nauli, na nini, nachukuwa kwake. ………."

Waengereza na Mapinduzi


Zipo kauli nzito kwamba waengereza nao waliyabariki mapinduzi ya 1964. Wakijenga hoja hiyo wadadisi wa masuala ya mapinduzi wanadai kwamba waengereza waliupokea kwa mtazamo tofauti ule uasi wa majeshi uliuotokea Tanganyika na mapinduzi ya Zanzibar na hivyo kutoa majibu tofauti kuhusiana na matukio haya mawili, ambayo kinadharia yote ni matukio ya uasi dhidi ya serikali zilizokuwa madarakani. Kwa upande wa uasi wa Tanganyika, waengereza kwa haraka mno walituma vikosi ili kutuliza uasi huo na kumrudisha Nyerere madarakani.

Kwa upande wa Zanzibar lakini waengereza walimkatalia vikali Shamte na Jamshid kutoa msaada wao kwa madai kwamba mapinduzi ya Zanzibar hayakuwa ni uvamizi wa nje bali ni mambo ya ndani ya nchi. Jambo la kwanza la kushangaza ni kwamba uasi wa Tanganyika pia ulikuwa si uvamizi wa nje bali yalipangwa na Kambona ambae ni mtanganyika. Uengereza ilijuwa wazi kama Nyerere alikuwa na mkono wake katika mapinduzi hayo (Ghassany 2010). Mkono wa waengereza kwa mapinduzi ya 1964 yanaegemezwa zaidi upande wa udini. Hii inawezekana sana kwani serikali ya ZNP/ZPPP ilikuwa ikiupigia debe sana uislamu na kuahidi kuundeleza na kuuimarisha. Kauli kali za Sheikh Ali Muhsin dhidi ya ukristo inaweza kuwa ndizo zilizoifanya Uengereza kuyabariki mapinduzi ya 1964.



Wako na wengine wengi nje ya mipaka ya Zanzibar ambao walikuwa na mikono yao katika kuyafanikisha mapinduzi ya 1964. Kila mmoja katika hao alikuwa na lengo lake na maslahi yake. Majina kama ya Kambona aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani wa Tanganyika, aliyejaribu kufanya uasi dhidi ya Nyerere na Odinga Oginga, aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani ya Kenya yanahusishwa na mipango ya juu ya Mapinduzi na hivyo basi Kenya nayo kuwa na mchango wake muhimu katika mapinduzi ya Zanzibar.

Odinga sio tu alikataa kutoa msaada kwa Jamshid na Shamte lakini pia alikataa hata kutumika kwa bandari ya Kenya kupokelewa Seyyid Jamshid na hivyo Jemshid kulazimika kupitia Dar es Salaam kwa uombezi wa Muengereza. Mtu mwengine anaenasibishwa sana pia na mapinduzi ni Myahudi, mfanyabiashara aliyekua amewekeza Tanganyika na Zanzibar kwa wakati huo, ambaye alikuwa rafiki wa karibu wa Karume na aliyekuwa akikisaidia sana chama cha ASP, Misha Finsilber. Misha Finnsilber ndie aliedhamini na kusimamia zoezi lote la kurejeshwa Zanzibar kutokea Dar es Salaam akina Karume, Babu, Hanga, Ali Mahfoudh, Ali Nyau na Jimmy Ringo mara tu baada ya mapinduzi kufanikiwa. Hivyo basi Israel nayo haiku nyuma katika kuyabariki mapinduzi ya 1964 kufanikiwa (Ghassany 2010).
 
Back
Top Bottom