Karume aizima NEC Dodoma

Hoja ya kuongeza muda wa Karume yawakoroga Wawakilishi wa CCM

Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, wamegawanyika kuhusu hoja binafsi ya kuundwa kwa Serikali ya mseto na Rais Amani Abeid Karume kuongezewa muda wa kubaki madarakani.

Uchunguzi wa Nipashe umegundua kuwa wajumbe hao wamegawanyika makundi mawili, wale wanaounga mkono na wanaopinga hoja hiyo, kwa madai inakwenda kinyume cha katiba ya Zanzibar na tamko la Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM la Butiama.

Hata hivyo, wajumbe wote 26 wa Chama Cha Wananchi (CUF) wanaonekana kuwa tayari kuunga mkono hoja hiyo na wamekuwa wakiwashawishi wajumbe wa CCM kuiunga mkono, wakisaidiwa na baadhi ya vigogo wa Serikali (SMZ).

Hoja hiyo inatarajiwa kuwasilishwa katika kikao kinachoanza leo na kiongozi wa upinzani katika Baraza, Abuubakar Khamis Bakari, ambaye amesema lengo la hoja hiyo ni kujenga umoja wa kitaifa kwa Wazanzibari.
Mwakilishi wa Mkwajuni, Ali Haji Ali (CCM), alisema suala hilo si jipya kwa vile limewahi kujitokeza katika muafaka wa CCM na CUF katika kikao cha Butiama.

Alisema hoja hiyo itakuwa na wakati mgumu kwa vile wajumbe wa CCM waliokataa kuundwa kwa Serikali ya mseto ndio hao hao watakaojadili na kutoa uamuzi.

Mwakilishi wa Mfenesini, Ali Abdallah Ali (CCM), alisema wawakilishi wa CCM wanaongozwa na msimamo wa chama na ndio maana wanasubiri msimamo utakaotolewa na kikao cha wawakilishi wa CCM chini ya Mwenyekiti wake, Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha, wakati utakapofika wa kulijadili suala hilo. "Sisi sote ni wawakilishi kupitia chama cha CCM suala hili limeletwa na chama cha siasa cha CUF, hivyo msimamo wa chama chetu ndio tutakaoufuata," alisema.

Alisema suala la serikali ya umoja wa kitaifa lilitakiwa kuletwa baada ya uchaguzi kwa kuwa kwa sasa kila chama kipo katika matayarisho ya kujiandaa na uchaguzi wa Oktoba.

Mkuu wa Mkoa Kaskazini Pemba, Dadi Faki Dadi, alisema hajaiona hoja hiyo, lakini kama imelenga kuwaunganisha Wazanzibari hakuna sababu ya kutoiunga mkono.

Alisema wakati umefika kwa Wazanzibari kusahau tofauti zao na kujenga umoja na mshikamano kwa vile maridhiano yaliyofikiwa kati ya Rais Karume na Maalim Seif yameleta ushirikiano. Mwakilishi wa Koani (CCM), Haji Mkema Haji, alisema watu wasiangalie ni suala la kupitishwa hoja au kutopitishwa isipokuwa wanapaswa kuangalia mambo yaliyopendekezwa kama yanaweza kuleta mafanikio katika utekelezaji wake.

Baadhi ya wajumbe ambao waliomba kuhifadhiwa majina yao walisema hoja ya kuundwa kwa serikali ya mseto na Rais Karume kuongezewa muda haiwezi kuungwa mkono na wajumbe wote wa CCM kwa vile inakwenda kinyume cha katiba ya Zanzibar na ilani ya uchaguzi ya CCM. "Suala hili tutalipinga kwa nguvu zote kwa vile linakwenda kinyume cha Katiba ya Zanzibar na ya Muungano, huwezi kubadilisha katiba ya Zanzibar bila ya kugusa katiba ya Muungano kwa kuwa ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano," alisema Mwakilishi mmoja wa Viti Maalum wa CCM.

Alisema ziko fununu kuwa kuna baadhi ya wajumbe wa CCM tayari wameshapewa Sh. milioni sita kila mmoja, ili kupitisha hoja hiyo, jambo ambalo linatia wasiwasi kwanini kuwepo na ushawishi wa fedha katika suala linalohusu katiba ya nchi. Waziri kivuli wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi Hamad Masoud, alisema hoja hiyo ina nafasi kubwa kupita kwani imelenga kujenga umoja miongoni mwa Wazanzibari.

Alisema tangu kufikiwa kwa maridhiano baada ya Rais Karume kukutana na Maalim Seif, wananchi wa Zanzibar wanaonekana kuwa wamoja ndio maana CUF imeona kuna haja ya kushirikiana na kuwa na Serikali ya umoja wa kitaifa.

"Kwa mtazamo wangu, suala hili litafanikiwa Wajumbe wengi wa Baraza wanaonekana kuunga mkono kwa maslahi ya wananchi wote wa Zanzibar, ingawa hoja yenyewe bado haijawasilishwa barazani," alisema Mwakilihi huyo na kuungwa mkono na Mwakilishi wa Viti Maalum Najma Khalfan (CUF).

Najma alisema ana matumaini kuwa Wajumbe wa CCM wataiunga mkono hoja hiyo kwani imelenga kujenga Zanzibar mpya.

Katibu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Ibrahim Mzee, alisema hadi jana hoja hiyo binafsi haikuwemo katika ratiba ya shughuli za Baraza, lakini alisema kwa mujibu wa kanuni, hoja binafsi inatakiwa kuwasilishwa kwa Spika saa 48 kabla ya kuwasilishwa barazani.

Ili hoja hiyo iweze kupita, inahitaji kuungwa mkono na theluthi mbili ya wajumbe 52 wakati sasa Baraza hilo lina wajumbe 78 baada ya mjumbe mmoja kufariki.

Wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi wanatakiwa wawe 81, lakini hivi sasa Baraza hilo lina wajumbe 78 kufuatia kifo cha aliyekuwa mwakilishi wa Wawi Soud Yussuf Mgeni (CUF), na nafasi mbili kuwa hazijateuliwa na Rais hadi sasa.

Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, Rais amepewa uwezo wa kuteua wajumbe 10, nafasi 15 kupitia viti maalum nafasi tano kupitia wakuu wa mikoa, Mwanasheria Mkuu na nafasi 50 kupitia majimbo ya Unguja na Pemba. CUF kina viti 26.

SOURCE: NIPASHE (IPPMEDIA.COM)
 
Naona kama vile CUF wameamua kula matapishi yao, kinachowasukuma kufanya hivyo lazima kina siri kubwa - yangu macho.
 
Mkuu uliyokuwa nayo ni dhana tu hakuna uthibitisho wowote. Unajua ni mambo gani yalikuwa kikwazo huko mbele na kutekeleza mambo haya mwishoni mwa kipindi chake? Hakuna anaejua sababu. Lakini kitu ambacho kiko wazi CCM bara hawataki kuona CCM Zanzibar inaungana na CUF.

Ikiwa mkuu wa nchi JK alishatoa kauli kuwa mpasuko wa Zanzibar ataushughulikia mwenyewe kwa kuwa athari zake ni kubwa mno, Iweje yeye mwenyewe alipokwenda Pemba na kuwaambia mutake musitake mupende musipende mtatawaliwa na CCM milele!! Unapata picha gani hapo??

Ninachokiunga mkono kwa nguvu zote ni kupatikana amani ya kudumu visiwani ifike wakati mambo mengine CCM Zanzibar waamue mambo wenyewe mazingira ni tofauti sana na bara.

Muungano uendeleee kuwepo ila kuna baadhi ya mambo yanapaswa yabadilike kutokana na mazingira halisi yanayotuzunguka!!

Sijui ni sababu gani za msingi walizokuwa nazo CCM bara Kuona Zanazibar inaendelea kuwepo bila amani ya kudumu. Ninashindwa kuelewa kabisa!! Au kuna watu wanaona faraja wenzao wakiendelea kuishi kwa chuki na uhasama?

Kinachotafutwa na kilichoombwa na Maaalim Seif na CUF kwa ujumla ni uchaguzi usogezwe mbele kwa angalau mwaka mmoja na nusu na siyo kuwa Karume aongezewe kipindi cha tatu kwa nia tu maridhiano yapewe muda ili kujenga mazingira mazuri ya hali ya kisiasa na amani kwa kizazi kijacho. Sasa tatizo liko wapi??

Ndugu yangu, wewe unasema hiyo ya kwangu ni dhana tu haya nami nakubali. Lakini hata ya kwako ni dhana tuu. Sioni makubaliano ya vyama, CUF na CCM, naona makubaliano kati ya Seif na Karume, ndo maana tunalazimisha karume kuongezewa muda. Kama ni makubaliano ya vyama kwa nini karume tu ndo aonekane ndo mwenye uwezo wa kulea hayo makubaliano? Hapa wenye akili lazima wakune vichwa hata kama hampendi! Kwani miafaka mingapi ilikubaliwa kwa zumari na filimbi halafu balaa likafuata baadaye? Mwenye akili inayofanya kazi vizuri hawezi kushindwa kujiuliza .... ni kitu gani kilifanya uhasama uendelee kuwepo miaka yote hiyo ikiwa jambo hilo lilikuwe jepesi yaani kiasi cha Seif tu na Karume kuonana na kuongea?

Ikiwa uhasama huu umemalizwa kwa mazungumzo ya faragha ya watu wawili tu, ni lazima tujiulize mchango wa watu hao katika uhasama huo ulikuwa nini!! Kwa nini hawakufanya hivyo walivyofanya wakati kuna nafasi ya kutosha na wameamua kuyafanya wakati nafasi inaonekana haitoshi. I mean lazima mtu ujiulize hivi mgogoro huo ilikuwa kumbe ni ugomvi tu kati ya viongozi hao wawili?

Ni lazima tufikirie sana badala ya kubeba majibu rahisi kwa maswali magumu. Lengo si kurudi nyuma bali kuzuia balaa lingine lisitokee kwani historia si maskini wa mifano!!!
 
Mwenye akili inayofanya kazi vizuri hawezi kushindwa kujiuliza .... ni kitu gani kilifanya uhasama uendelee kuwepo miaka yote hiyo ikiwa jambo hilo lilikuwe jepesi yaani kiasi cha Seif tu na Karume kuonana na kuongea?

Ikiwa uhasama huu umemalizwa kwa mazungumzo ya faragha ya watu wawili tu, ni lazima tujiulize mchango wa watu hao katika uhasama huo ulikuwa nini!! Kwa nini hawakufanya hivyo walivyofanya wakati kuna nafasi ya kutosha na wameamua kuyafanya wakati nafasi inaonekana haitoshi. I mean lazima mtu ujiulize hivi mgogoro huo ilikuwa kumbe ni ugomvi tu kati ya viongozi hao wawili?


Kitu kilichofanya uhasama uendelee ni kuwa walikuwa wanapeleka kesi ya ngedele kwa nyani CCM-bara sasa wameamua wayamalize wenyewe.

Tatizo la watanzania tunapenda kudadisi mno ndiyo maana hatuendelei waacheni kama wamefanya siri ni siri yao na ukichunguza sana kuku huwa anakula nini hutatamani kumla tena.
 
Back
Top Bottom