KAMPUNI ya Reli (TRL) imetangaza kusimamisha huduma ya reli ya kati kuanzia leo kutok

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
KAMPUNI ya Reli (TRL) imetangaza kusimamisha huduma ya reli ya kati kuanzia leo kutokana na kuharibika kwa daraja lililoko kati ya stesheni za Bahi na Kintinku mkoani Dodoma.

Daraja hilo liliharibika usiku wa kuamkia jana na uongozi wa TRL umesema daraja hilo limeharibika kutokana na mkondo wa maji ya mto Bububu kutoka Kondoa kubadilisha mwelekeo wake wa asili.

Mhandisi Mkuu Ujenzi wa TRL, Mathias Massae alisema jana kuwa mkondo huo wa maji
umeathiri nguzo moja kati ya nne zinazoshikilia daraja la mto hilo na kusababisha sehemu ya kati ya daraja kutitia chini.

Alisema mto huo uliacha njia yake baada ya kuvunja kingo za mto na kuliathiri daraja hilo kwa kiasi kikubwa.

Hata hivyo hakueleza hasara iliyopatikana kutokana na kubomoka kwa daraja hilo. Pia hakuwa tayari kutaja kiasi cha fedha watakazotumia kukarabati daraja hilo.

“Kwa sasa hatujajua kiasi cha fedha tutakazotumia kwenye ukarabati, hadi pale tutakapomaliza kutoa maji eneo hilo na kujua ukubwa wa athari yenyewe,” alisema Massae.

Kutokana na athari hizo, Mhandisi Massae alisema watasimamisha huduma za treni kwa muda wa siku 10.

Alitaja shughuli watakazozitekeleza ni kutoa maji ili yarudi kwenye njia yake ya asili kazi itakayochukua siku tatu huku kazi za ujenzi wa daraja la muda utachukua siku saba.

Mhandisi huyo alisema tayari wahandisi wa kampuni hiyo wameshaenda eneo la tukio na kwamba Mkurugenzi wa TRL ameunda jopo la wahandisi wanaofanya tathmini za raslimali zinazohitajika kufanyia ukarabati daraja hilo ili njia iweze kufunguliwa ndani ya kipindi hicho.

Abiria wa treni iliyokuwa inatoka Kigoma ambao wamekwama katika stesheni ya Kintiku wamekodishiwa mabasi ya kwenda kuwachukua jana. Abiria 1,846 walikwama kwenye stesheni hiyo na walikodishiwa mabasi 28.

Jopo jingine la wahandisi na wataalamu wa TRL wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji linaondoka leo kwenda eneo la ajali kuongeza nguvu ya kasi ya ukarabati.
 
Back
Top Bottom