Kama tunafuja fedha kwanini waendelee kutusaidia?

Ustaadh

JF-Expert Member
Oct 25, 2009
413
19
Padri Privatus Karugendo

KWA mtu yeyote mwenye akili timamu, awe amesoma uchumi au hakusomea uchumi, awe Mtanzania au mgeni, akiangalia mabango ya uchaguzi mkuu hawezi kusema hayo ni matumizi mazuri ya fedha.
Mabango yenyewe yana ubora wa hali ya juu na tutaambiwa mengine thamani yake inakwenda hadi milioni kumi kwa bango moja. Wanaofuatilia mambo, wanasema mabango haya yalitengenezwa Canada; moja ya nchi inayoisaidia Tanzania.
Kwa upande mmoja Serikali ya Canada inaisaidia Tanzania kwa vile inaamini nchi hii masikini na inahitaji msaada ili kuendelea na kwa upande mwingine makampuni ya Canada yanakubali kupokea kazi ya kutengeneza mabango ya gharama kubwa na kufyonza fedha ya Watanzania Masikini.
Ni kama mchezo wa kuigiza au mchezo wa kikatili; unatoa kwa mkono wa kulia na kupora kwa mkono wa kushoto. Inajionyesha wazi kwamba mchakato mzima wa kutengeneza mabango ya gharama kubwa na kuyasambaza nchi nzima ni ufujaji wa fedha za umma.
Ninatoa mfano wa mabango maana ndio yanaonekana wazi; barabara zimepambwa na mabango, nyumba zimepambwa na mabango, magari yamepambwa na mabango na watu wanavaa mabango; lakini kuna mifano mingi ya kudhihirisha ufujaji wa fedha wa kutisha katika kampeni hizi zinazomalizika.
Mfano T-shirt na kofia za CCM zilizosambazwa nchi nzima; walizigawa kabla ya kampeni, wamegawa wakati wa kampeni na kuna tetesi kwamba wataendelea kuzigawa hata baada ya kampeni, ni shehena kubwa sana ambayo ukifuatilia utakuta iliingizwa nchini bila kulipa kodi.
Mafuta yaliyotumika kuwasafirisha washabiki wa CCM kwenda kwenye mikutano vya kampeni; habari za kuaminika ni kwamba mtu yeyote aliyekubali gari lake lisombe washabiki wa CCM kwenda kwenye mikutano ya kampeni.
Magari hayo yalikuwa yakipewa mafuta kuanzia lita 20 na kuendelea na shilingi 10,000 za dereva; posho na fedha za kutunza msafara mkubwa wa mgombea urais kupitia CCM; makundi ya wasanii wa muziki wa kizazi kipya, makundi ya ngoma na vichekesho, wasaidizi wa rais, waandishi wa habari; ni matumizi makubwa na yasiyokuwa ya lazima ambayo huwezi kukwepa kuyaita ufujaji wa fedha za umma.
Mimi na wewe tunaweza kuelewa ama tusielewe. Kama tuna faida kwenye mchakato mzima na malengo ya Tanzania tuitakayo ni ile ya kushibisha matumbo yetu na familia zetu; hatuna haja kuyashangaa matumizi makubwa na ufujaji wa fedha.
Kwa Mtanzania ambaye anaangalia Tanzania ya leo, kesho na vijazi vijavyo ni lazima ajiulize umuhimu wa kutumia fedha nyingi hivyo kwenye kampeni wakati tunautangazia ulimwengu mzima kwamba sisi ni maskini.
Ni mantiki kutumia fedha zote hizo wakati tunasisitiza kwamba elimu ya bure haiwezekani? Ni mantiki kutumia fedha hizo zote kwenye kampeni za uchaguzi wakati bado tunakwenda nje kuomba fedha za kujenga choo? Na kama tunafuja fedha hivyo ni kwa nini waendelee kutusaidia?
Je, wajomba zetu wanaotusaidia wanafahamu kwamba fedha wanazotuletea tunazitumia vibaya kwa mambo ambayo si ya lazima? Hoja ninayoileta kwenye makala hii imetokana na mabishano yangu na Mzungu niliyekutana naye wakati wa kipindi cha kampeni.
Mzungu huyu alitumwa na nchi yake kuangalia mwenendo wa kampeni na upigaji wa kura hapa Tanzania. Hawa tunawaita waangalizi wa uchaguzi. Wanakuja wengi kutoka nchi za nje na pia kuna waangalizi wa ndani. Mzungu huyu alikuwa anatoka kwenye nchi inayotoa misaada mingi Tanzania.
Tulichokubaliana na Mzungu huyu ni kwamba Serikali (CCM) imetumia fedha nyingi kwenye kampeni na hasa mabango yaliyosambaa nchi nzima. Tulichotofautiana na kuzuka mjadala mkubwa ambao haukufika mwisho na kuishia kwa maneno yenye utata mkubwa; yeye akinibatiza mimi
“Mawazo mgando ya ukomunisti ulioshindwa” nami nikijibu.
“ Mawazo mgando ya Ubeberu na ukoloni mambo leo” ni pale nilipotaka Mzungu anieleze ni kwa nini kama tunafuja fedha nchi yake iendelee kutusaidia. Na je, kwa nini watusaidie? Kuna uhusiano gani kati yetu sisi na wao? Na ni kwa nini uchaguzi wetu uwavutie?
Kama Wazungu wanagundua kwamba fedha wanazozitoa zinatumika vibaya; wanaona wenyewe na wakati mwingine wanashiriki ufujaji wa fedha hizi pale wanapokuja na kuishi mwenye mahoteli ya kifahari na wakati mwingine kuandaliwa sherehe kubwa, ripoti zinaandikwa na ushahidi upo, kwa nini basi waendelee kutusaidia?
Ingawa mimi binafsi bado ninaamini kwamba Tanzania haiitaji msaada kutoka nje; sina maana kwamba tunaweza kujitosheleza kwa kila kitu; tunahitaji ushirikiano na mataifa mengine ili tuweze kuishi kwenye dunia ya leo ambayo imegeuka kuwa kijiji kimoja; hoja yangu ni kwamba sisi si masikini kihivyo!
Tuna rasilimali nyingi; madini, mbuga za wanyama, mbao, mazao ya chakula na ya kuuza, ardhi yetu bado ni nzuri na tuna mvua za kutosha. Umasikini wetu ni wa kimawazo zaidi; tunakubali unyonge wa kutengenezwa na kushindiliwa vichwani mwetu.
Na ninafikiri kwa vile sisi si masikini, ndio maana wajomba zetu wanajiweka mstari wa mbele kusukuma misaada mikubwa yenye masharti na ujanja mkubwa ili kutufumba macho; wanaleta kumi wanaondoka na ishirini.
Wanatumia maneno yale yale ya wenye hekima na busara kwamba wajinga ndiyo waliwao na kwamba usimwamshe aliyelala. Wako tayari kuwafumbia macho wale wote wanaofuja fedha za umma ili kesho na keshokutwa waje kuchota kiasi chao:
Wanaandaa mazingira mazuri ya makampuni yao, nafasi za ajira kwa vijana wao, viwanda vyao na uwekezaji mwingine unaoweza kuleta faida kubwa kwa nchi zao.
Hawaji kuangalia uchaguzi wetu kwa vile wanatupenda; hawaji kushuhudia jinsi demokrasia inavyofanya kazi au inavyovurugwa, hawaji kuangalia kama serikali iliyokuwa madarakani iliwahudumia Watanzania wa vijijini bali wakuja kushuhudia na kuhakikisha tunamchagua mtu anayeweza kuyalinda masilahi yao.
Na kwa msingi huu wako tayari kusaidia kwa nguvu zao zote ili kuhakikisha mtu wanayemuunga mkono anapita. Vinginevyo hakuna maelezo ya ni kwa nini tunafuja fedha, lakini wao wanaendelea kutusaidia na wanatusaidia wakati tunasikia kwao kuna upungufu wa ajira na uchumi unaendelea kuwa mgumu kiasi cha serikali zao kufanya maamuzi ya kupunguza matumizi.
Wataendelea kutusaidia, wataendelea kuja kushuhudia chaguzi zetu; wataona kasoro kubwa zinazojitokeza kwenye uchaguzi wetu; watashuhudia matumizi mabaya ya fedha na wataelezea dunia nzima kwamba uchaguzi ulikuwa huru na wa haki.
Wako makini kwa majibu yao, ili kuhakikisha tunapumbaa na kuendelea kusinzia wakati wao wakipora kila tulichonacho. Vinginevyo sioni mantiki ya kuendelea kutusaidia wakati tunafuja mali.
 
Back
Top Bottom