Kahama: Wananchi wakichoka wataingia mitaani

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,319
33,125
Fidelis Butahe
MWANASIASA mkongwe nchini, Sir George Kahama ameishauri CCM kutambua kuwa ili nchi itawalike lazima pawepo demokrasia ya kweli kinyume na hapo, umma utachoka na hatimaye kuleta vurugu.Sir Kahama (82)alitoa kauli hiyo hivi karibuni kwenye mahojiano maalumu na Mwananchi Jumapili nyumbani kwake Dar es Salaam, kuhusu mustakabali wa kisiasa maendeleo ya mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini.
Mwanasiasa huyo mstaafu aliyewahi kuwa waziri katika Baraza la Kwanza la Mawaziri baada ya Tanganyika kupata uhuru wake Desemba 9, 1961 alisema hivi sasa Tanzania imeingia kwenye mfumo wa vyama vingi vya siasa wenye nguvu unaotoa nafasi kwa wananchi kuchagua chama kutokana na sera zake.

Sir Kahama aliyewahi kulitumikia taifa katika nyadhifa mbalimbali kuanzia awamu kwanza hadi ya tatu , zikiwamo uwaziri na ubalozi, aling’atuka kwenye viambaza vya siasa mwishoni mwa utawala wa Awamu ya Tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa mwaka 2005, akiwa Mbunge wa Karagwe na Waziri wa Ushirika na Masoko.

Kahama alisema anaamini kwamba, mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini una manufaa makubwa katika kuharakisha maendeleo ya taifa licha ya baadhi ya kuwa na mtazamo tofauti.
“Tutaendelea na hali hii, lakini itafika wakati watu wataelewa tu maana ya kuwepo wa vyama vingi, hiyo ndio demokrasia na binafsi sioni kama kuna tatizo,” alisema Sir Kahama

Alionya: “Mkitaka kuwa salama lazima muwe na kitu kama hiki, wananchi watachagua chama kwa sera zake na chama kikiingia madarakani kikaboronga watakiondoa. Mbali na hilo watu wakichoka wataingia mitaani na hali itakuwa mbaya,”.

Kauli hiyo ya Sir Kahama inakuja wakati malumbano ya kisiasa kati ya CCM na vyama vya upinzani yakiendelea baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi mdogo Jimbo la Igunga, mkoani Tabora uliofanyika hivi karibuni kufuatia kujiuzulu kwa mbunge wa zamani, Rostam Aziz.
Sir Kahama alisisitiza kuwa, mfumo wa sasa wa vyama vingi vya siasa umebadili mitazamo ya wananchi kisiasa tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma wakati wa mfumo wa chama kimoja.

“Ikumbukwe kuwa Tanzania ilikuwa na chama kimoja, sasa tuko kwenye vyama vingi, ndiyo maana kuna mambo mengi yanaibuka na kuzungumzwa kila mara, hilo ni jambo la kawaida, tulikuwa watu wa chama kimoja, sasa ni tofauti.” Alisema pamoja na Serikali kupitisha sheria kuruhusu mfumo wa vyama vingi vya siasa na kuanza kutumika rasmi Julai mosi, 1992, watu wengi waliendelea kubaki na mawazo ya chama kimoja hali inayowafanya kushindwa kwenda sambamba na mazingira ya sasa kisiasa.

Alisema katika kipindi cha miaka 19 tangu kuanza kwa mfumo huo, vyama vya upinzani vimeendelea kukua siku hadi siku hali inayotoa changamoto kwa CCM kutokana na changamoto mbalimbali vinavyoibua.

“Mwaka 2010 kiliibuka Chadema na kupata viti zaidi bungeni na kuonekana kuwa na nguvu, ndio maana CCM tukaanza kujihami,” alisema Sir Kahama na kuongeza:

“Nchi kuwa na vyama vingi ni jambo la kawaida, hii ni demokrasia ambayo inaweza kuwepo nchi yoyote, hata Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kwamba, chama kimoja kikibweteka kingine kinaweza kushika kasi.” Alisema Tanzania ni nchi yenye umoja na amani na kwamba kinachoikumba CCM ni mshtuko wa kushika kasi kwa vyama vya upinzani. Alieleza kuwa sasa nchi imeingia katika mfumo wa vyama vingi wenye nguvu na mwelekeo thabiti.

Kauli ya mwanasiasa huyo ni ya pili ndani ya kipindi cha miezi mitatu tangu alipokaririwa akielezea wasiwasi wake juu ya kutekelezwa kwa ahadi ya serikali ya Maisha Bora kwa kila Mtanzania ambayo alisema ni kitendawili kinachosubiriwa na Watanzania wengi kuteguliwa.
Katika waraka wake wa Julai mwaka huu kuhusu mafanikio na changamoto ilizopata Tanzania katika kipindi cha Miaka 50 ya Uhuru, Sir Kahama alikaririwa akisema kuwa, pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana ni vema pia kukiri kwamba, safari ya kufikia lengo la kuwa na maisha bora kwa kwa kila Mtanzania bado ndefu.

“Asilimia 36 ya Watanzania bado hawajaweza kumudu kupata mahitaji yao ya msingi. Asilimia 86 hawapati umeme wa gridi ya taifa …Wananchi wengi bado wanaishi katika nyumba zilizojengwa kwa miti, fito na matope na kuezekwa kwa makuti au nyasi.” Alisema Kahama.

chanzo: Gazeti la Mwananchi
 
Ccm hawashauriki hawaambiliki ni sawa na sikio la kufa lisilosikia dawa na pia mtu kupoteza muda wako kuwashauri ni sawa na kumpigia mbuzi gitaa kwani kamwe hatocheza, ilopo nikuwataarifu wajiandae na kitakachotokea wakati wowote
 
Back
Top Bottom