John Komba kafanya Ubabe huu na hajaguswa je angalifanya Zitto leo ingalikuwaje ?

Lunyungu

JF-Expert Member
Aug 7, 2006
8,873
1,894
Msanii mkuu wa CCM avamia mkutano wapinzani, polisi wamshusha jukwaani
*Helkopita ya Mbowe yawatia kiwewe CCM
*Jitihadha za RC, DC kuizuia zakwama
Na Waandishi Wetu Kiteto na Dar
MBUNGE wa Mbinga Magharibi na Mkurugenzi wa Kikundi cha Sanaa cha Tanzania One Theatre (TOT), Kapteni John Komba akiwa na baadhi ya wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) jana kuvamia eneo la mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kuanza kupiga muziki.
Kutokana na kitendo hicho ambacho kilizua vurugu kubwa baina ya wafuasi wa Chadema na CCM, askari polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) walilazimika kumshusha jukwaani kwa nguvu.
Komba ambaye pia ni Mjumbe wa Halmshauri Kuu ya CCM, jana majira ya saa nne asubuhi alivamia eneo la Kata ya Kijungu lililopangwa na Tume ya Uchaguzi (NEC) kwa ajili ya Chadema kufanya mkutano wa hadhara na kuanza kupiga nyimbo za kampeni kwa lengo la kumnadi mgombea wa CCM katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kiteto.
Vurugu hizo zilizoanza majira ya saa nne asubuhi hadi saa saba mchana, zilichochewa na Jeshi la Polisi kushindwa kuchukua hatua za haraka kudhibiti hali hiyo, licha ya viongozi wa Chadema kuwasilisha malalamiko hayo kwa jeshi hilo.
Katika hali ya kushangaza viongozi wa CCM na Serikali waliofika katika eneo hilo, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Henry Shekifu pia walishindwa kumzuia Komba na kundi lake la TOT kupiga muziki, hatua iliyofanya wananchi kupandwa na hasira na kuanza kuwazomea.
Kikosi cha FFU kiliongozwa na Mkuu wa Kikosi cha Upelelezi Mkoa wa Manyara, Mrakibu Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (ASP), Ernest Sakawa kilipowasili kilitumia zaidi ya saa moja kumsihi Komba kusitisha kupiga muziki, lakini aligoma.
Hata hivyo mara baada ya kuwasili Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, John Henjewele na kufanya mazungumzo na maafisa hao wa polisi, walifanikiwa kumshawishi Komba kushuka jukwaani na kufanya mazungumzo ambayo yalizaa matunda na kundi hilo kuacha kupiga muziki.
�Tunakuomba uzime mziki MheshimiwaKomba na kushuka chini,� alisikika mmoja wa
maafisa wa polisi akimweleza Komba ambaye baada ya kuimba nyimbo za CCM kwa muda
ndipo alishuka.
Awali, akizungumza na waandishi wa habari kijijini hapo, Shekifu alisema ameonea tatizo hilo na kuahidi serikali itachukuwa hatua kwa kundi ambalo limevamia mkutano.
�Mimi nimeona, lakini sio jukumu langu kuzuia mkutano, kuna vyombo husika, nadhani wamepewa taarifa na watakuja,�alisema Shekifu akiwa njiani kuelekea kijiji jirani cha Langatei.
Awali Shekifu ambaye yupo katika ziara ya kukagua na kuhamasisha miradi ya maendeleo, aligoma kupigwa picha wala kuzungumza na waandishi wa habari kwa maelezo kuwa hajatoa ruhusa na ni makosa kumpiga picha bila idhini yake.
Katika vurugu hizo hali ingeweza kuwa mbaya zaidi, kama si jitihada za Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa kuwaomba vijana waliokuwa tayari wamebeba mawe kushambulia kundi la TOT kuwa wavumilivu.
Dk Slaa aliwaeleza vijana hao ambao walikuwa katika Uwanja wa Shule ya Msingi
Kijungu kuwa vurugu zinazofanywa na CCM
zinalenga kusababishwa kusogezwa mbele kwa uchaguzi.
�Vijana wangu kuweni wapole tu, hawa wanataka tuwavamie na kuwaondoa kwa nguvu ili
vurugu zitokee wapate sababu za kuahirishwa kwa uchaguzi huu,� alisema Dk Slaa.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kushuka jukwaani na kuzima
muziki, Komba alisema kilichotokea ni masuala ya siasa na ni kweli Chadema ndio walikuwa na mkutano katika eneo hilo.
Hata hivyo, alidai kuwa hawakuwa na nia ya kufanya mkutano hapo bali kupiga muziki ambao ulikuwa unaisadia Chadema kuwaita watu.
Baada ya TOT kuondoa majira ya saa saba ndipo Chadema walianza kufanya mkutano wao
ambapo, mgombea wa Ubunge Victor Kimesera aliwaomba wananchi wa Kijungu kumchagua
ili aongeze nguvu katika vita dhidi ya mafisadi na kuwaletea maendeleo.
Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kiteto, Festo Kang�ombe alisema kuwa Chadema ndio walipaswa kufanya mkutano katika eneo hilo kwa mujibu wa ratiba na alilaumu Jeshi la Polisi kushindwa kudhibiti vurugu zinazotokana na kukiuka ratiba za mikutano ya kampeni.
�Chadema ndio walipaswa kufanya mkutano Kijungu leo(jana), kama CCM walikuwepo na
ratiba haiwatambuwi, hivyo vyombo vya dola vilipaswa kuwaondoa,�alisisitiza.
Tukio hilo limekuja siku chache tu baada ya viongozi 6 wa Chadema kuvamiwa na kupigwa na vijana wa CCM na polisi katika kijiji hicho hata hivyo hadi jana hakuna mtuhumiwa ambaye alikuwa amekamatwa na polisi.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe jana alianza
kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kiteto kwa kutumia helkopta licha ya
jitihada kubwa za CCM na serikali ya mkoa wa Manyara kuizuwia helkopta hiyo .
RC, DC walia na helkopta ya Mbowe
Katika hatua nyingine na ya kushangaza Mkuu wa Mkoa wa Manyara na Mkuu wa
wilaya ya Kiteto jana walifika kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Kijungu ambapo helkopta ya Chadema ilipangwa kutua na kuwaeleza viongozi wa chama hicho kuwa helkopta hiyo haitakiwi kutumika hapo.
Shekifu alisema serikali mkoani Manyara haijakubali kutumika kwa helkopta hiyo kwenye kampeni.
�Hapa leo (Alhamisi) helkopta haitashuka kwani tumeipinga na hatuna taarifa nayo,� alisema.
Naye Mkuu wa Wilaya hiyo, alifanya kikao na viongozi wa Chadema na maafisa wa
polisi waliofika katika eneo hilo la kutuliza ghasia na kusisitiza kuwa helkopta hiyo haitakubaliwa kutua katika wilaya yake.
�Jambo hili tumelijadili na msimamizi wa uchaguzi na tumekubaliana kuzuwia helkopta hii kutumika katika kampeni,� alisema Henjewele.
Awali, Komba aliwatangazia wananchi wa kijiji cha Kijungu kuwa helkopta ya Chadema ambayo walikuwa wanaisubiri haitatua katika uwanja huo na kama ikitua wananchi wa Kijungu wasiichaguwe CCM.
�Nugu zangu hiyo helkopta tumeizuia na kamwe haitakuja Kiteto na kama ikija hapa
basi msiichaguwe CCM,� alisema Komba.
Hata hivyo, Msimamizi wa Uchaguzi jimbo la Kiteto, Kang�ombe alikanusha jana
kukutana na viongozi wa serikali akiwepo mkuu huyo wa wilaya na kupiga marufuku
kutumika kwa helkopta hiyo.
�Hakuna sheria ambayo inazuia kufanya kampeni kwa helkopta hata kama ukitaka
kufanya kwa baiskeli ni juu yako, sheria ipo kimya katika masuala ya usafiri kwenye
kampeni,� alisema Kang�ombe.
Hata hivyo, mara baada ya saa mbili helkopta hiyo ilifika katika uwanja huo
licha ya kuwepo askari wa FFU lakini walishindwa kuzuia kutua hivyo kuibuwa shangwe kwa wananchi waliokuwa na hamu ya kuiona.
Akizungumza mara baada ya kutua, Mbowe alisema jitihada za CCM kuizuia helkopta hiyo zisingewezekana kwa kuwa wamefuata taratibu zote na kisha kuwaomba wananchi kumchagua mgombea wa Chadema Kimeresa
Tendwa aliwashutumu Polisi
Katika hatua nyingine, Msajili wa vyama vya Siasa Nchini John Tendwa amesema hakuridhishwa na kauli za Jeshi la polisi kuwa vurugu zilizotokea katika kampeni za uchaguzi mdogo Jimbo la Kiteto mkoani Manyara zilifanywa na wananchi wa kawaida na kwamba si wafuasi wa vyama vya siasa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Tendwa alilitaka Jeshi la Polisi nchini kuwakamata na kuwafikisha mbele ya sheria watu wote waliohusika katika vurugu hizo kabla ya uchaguzi kufanyika.
Alisema vitendo vya vurugu vinapaswa kulaaniwa kwa nguvu na hafurahishwi na matamshi ya jeshi hilo kwamba chama fulani hakiusiki katika kvurugu hizo.
�Nimesoma kwenye gazeti kwamba waliohusika na vitendo hivi ni morani fulani, morani fulani gani hao? Morani ndani ya nchi yetu ni wananchi na kama ni wahalifu wakamatwe," alisisitiza na kuongeza:
�Tukipuuza yaliyotokea Kiteto, yanaweza kutokea kama yaliotokea Kenya kwa sababu tukishindwa kuzuia cheche zilizotekea Kiteto, zinaweza kuwasha pori zima�.
Naye Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu Lewis Makame amesema amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za vurugu ambazo zimetokea katika Jimbo la Kiteto wakati maandalizi ya Uchaguzi Mdogo utakaofanyika 24 Februari 2008 yanaendelea.
Alisema kuwa Tume inakemea vitendo vyovyote ambavyo vinafanyika kwa lengo la kuathiri, kuvuruga au kuchafua mchakato wa Uchaguzi Mdogo huona kuwakumbusha wadau wote, wakiwamo wagombea, vyama vya aiasa na wafuasi wao kuzingatia na kuheshimu Sheria, maelekezo ya Tume na Maadili ya Uchaguzi wakati huu wa Kampeni za Uchaguzi na siku ya Upigaji Kura.
Imeandikwa na James Magai, Muhib Said na Musa Juma
 
Back
Top Bottom