JK, Waziri wa EU wajadili uharamia Bahari ya Hindi

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,316
33,112
headline_bullet.jpg
Boti mbili za maharamia zazamishwa baharini kilomita 240 kutoka pwani Dar



Ashton.jpg

Baroness Catherine Ashton, Waziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya (EU) na Makamu wa Rais wa Tume ya Ulaya.



Rais Jakaya Kikwete, jana alikutana na kufanya mazungumzo na Baroness Catherine Ashton, Waziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya (EU) na Makamu wa Rais wa Tume ya Ulaya.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya mawasiliano ya Rais Ikulu, ilisema jana kuwa katika mkutano huo uliofanyika Ikulu, Dar es Salaam, viongozi hao wawili walizungumzia masuala mbalimbali ya kimataifa, na yale yanayohusu uhusiano kati ya Tanzania na EU.
Aidha, viongozi hao walijadiliana kuhusu jinsi gani Tanzania na EU zinavyoweza kushirikiana katika kupambana na uharamia katika eneo la Bahari ya Hindi.
Baroness Catherine Ashton ambaye aliwasili nchini jana akitokea Kenya yuko njiani kwenda Seychelles kuhudhuria Mkutano wa Mawaziri wa Mwambao wa Afrika Mashariki utakaojadili jinsi ya kupambana na uharamia wenye chimbuko lake katika Pwani ya Somalia.
Mkutano huo uliopangwa kuanza leo, umeandaliwa na Serikali ya Seychelles kwa kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Mambo ya Nje ya EU na Ofisi ya Makamu wa Rais wa Tume ya Ulaya.
Katika mkutano wake na Baroness Catherine Ashton, Rais Kikwete alisema kuwa Serikali yake inafurahishwa na kuridhishwa na uhusiano kati ya Tanzania na EU katika maeneo mbalimbali.
EU imekuwa inasaidia maendeleo ya Tanzania kupitia msaada wake katika Bajeti ya Tanzania ambako maeneo yanayolengwa ni sekta za usafirishaji, kilimo, utawala bora, nishati, tabianchi, Mpango wa Taifa wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini wa Mkukuta kwa upande wa Tanzania Bara na Mkuza kwa upande wa Tanzania Visiwani.
EU pia imekuwa inatoa misaada yake kwa taasisi na wabia wengine wa shughuli za maendeleo nchini wasiokuwa Serikali. Wakati huohuo, meli aina ya 22 HMS Chatham ambayo iliwekwa baharini siku za karibuni na Majeshi ya Kujihami (Nato) kwa ajili ya kukabiliana na maharamia, imeziharibu boti mbili baada ya kuzingira kikundi kinachotuhumiwa kuwa ni cha kiharamia katika ukanda wa Somalia.
Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya meli hiyo ya 22 HMS Chatham, kumaliza ziara yake jijini Dar es Salaam.
Habari tulizozipata wakati tukienda mitamboni jana usiku zilieleza kuwa, zoezi hilo lilifanikiwa kwa ushirikiano na ndege ya Jeshi la Majini la Umoja wa Ulaya (EU) inayofanya kazi zake nje ya visiwa vya Shelisheli ambapo helikopta ya meli ya HMS Chatham, iliiona meli kubwa takriban kilomita 240 kutoka pwani ya Tanzania Mei 14, mwaka huu ikiwa katika eneo maalum la ukanda wa kiuchumi wa Tanzania.
Baada ya kukiona chombo hicho usiku, maharamia hao walilazimishwa kujisalimisha kwa amri ya meli hiyo ya HMS Chatham pamoja na helkopta iliyokuwa na boti ziendazo kasi.
Timu ya wanamaji hao wa Nato waliwafuata maharamia hao ambao baada ya kuona hali hiyo, walianza kutupa baharini vifaa vyao mbalimbali zikiwemo silaha na vifaa vingine vinavyohusiana na uharamia.



CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom