Jk ataka bei ya mafuta ishuke haraka sana

Pdidy

JF-Expert Member
Nov 22, 2007
50,956
22,139
JK ataka bei ya mafuta ishuke

• EWURA yataka bei za bidhaa zishushwe
• Akiri kuwepo kwa magendo makonyo ya karafuu Pemba
* Amwagiza Ngeleja kukutana na EWURA
* Ahoji bei kupaa nchini, tofauti na soko la kimataifa

NA JOSEPH BURA

RAIS Jakaya Kikwete amemuagiza Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, kukaa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), kuangalia uwezekano wa bei ya mafuta kushuka.

Agizo hilo alilitoa jana alipohutubia Baraza la Iddi el Haji, kwenye viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam.

Rais alisema inashangaza kuona bei ya mafuta katika soko la dunia ikiwa imeshuka kwa kiwango kikubwa, lakini nchini tangu ilipopanda kwa kasi mwaka jana, imeendelea kuwa hivyo.

Alisema mwaka 2005 bei ya pipa moja la mafuta katika soko la dunia ilikuwa dola za Marekani 50, lakini tangu mwaka jana bei imekuwa ikipanda hadi kufikia dola 147 kwa pipa katika soko hilo.

Hata hivyo, katika soko la dunia bei ya pipa moja imeshapungua kwa sasa na kuuzwa kwa dola 46, lakini bei ya mafuta nchini imeendelea kuwa juu.

"Nimemwagiza Waziri wa Nishati na Madini kuwasiliana na EWURA, kuwabana wauza mafuta kujua kwa nini kasi ya kupanda kwa bei ya mafuta haiendi sawa na kasi ya kushuka kwa bei hiyo, bei ikipanda kidogo kwenye soko, asubuhi ukienda kituo cha Mwembechai wameshapandisha bei, kwa nini hiyo kasi isitumike bei inaposhuka," alihoji Rais Kikwete.

Alifafanua kuwa, taratibu zilizopo ni kwamba EWURA ndiyo wasimamizi, hivyo watimize wajibu wao.

"Kama wanakuwa hodari wa kupandisha bei basi wawe hodari pia katika kushusha ili vyote viwe sawa. Wazungumze nao haraka iwezekanavyo ili tuelewane.

"Nimewaambia waende Botswana wakaone mfano kwa wenzetu wanavyokabiliana na hali hiyo wakati hali inapokuwa si tengefu," alisisitiza Rais Kikwete.

Wakati huo huo, mwandishi wetu anaripoti kuwa, imeelezwa kuna uwezekano mkubwa wa bei ya mafuta kushuka kuanzia mwakani kutokana na EWURA kuamua kuingilia kati suala hilo.

Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Haruna Masebu, alisema jana ofisini kwake kuwa, kutokana na bei ya mafuta kutoshuka na kuendelea kulalamikiwa, watakutana na wadau kesho kwenye ukumbi wa
Karimjee, Dar es Salaam kwa ajili ya kupata maoni yao.

Masebu alisema baada ya kupata maoni ya wadau watatumia siku 21 kuyafanyia uchambuzi na kuyawasilisha kwenye bodi ya wakurugenzi, ambayo itatoa uamuzi kuhusu bei zitakazotumika.

Kutokana na mtiririko huo, huenda bei mpya za mafuta ambazo zitakuwa za chini zitaanza kutumika Februari, mwakani.

Hata hivyo, Masebu alitahadharisha wananchi kuwa, bei inayotangazwa na kuonekana kushuka katika soko la dunia ni ya mafuta yasiyosafishwa na kuwa EWURA wanajihusisha na yale yaliyosafishwa.

Katika hatua nyingine, Rais Kikwete alisema uchumi wa nchi bado ni imara, licha ya kuyumba duniani, kwa kuwa haujafungamanishwa na masoko ya fedha ya dunia.

Alisema Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imechukua hatua za tahadhari kuimarisha mfumo wa usimamizi ili kulinda uchumi.

"Uchumi wa dunia ulipoanza kuyumba watu walianza kununua dola kwa wingi ili kuhifadhi fedha zao kwa dola hali iliyosababisha thamani ya shilingi kushuka kwa kasi.

"Lakini BoT nayo ikauza dola za kutosha kuonyesha kuwa wanao uwezo wa kuhimili misukosuko thamani ya shilingi ikarejea, msihofu tuna hazina ya kutosha ya fedha za kigeni, BoT wanakaa kila siku kuangalia hali ya uchumi," alisisitiza Rais Kikwete.

Alisema athari hizo zimeanza kuonekana kwenye sekta ya utalii, ambapo idadi ya watalii wameanza kupungua na pia wawekezakaji wameanza kupungua kwa sababu ya kukosa mikopo kwenye nchi zao kwa kuwa taasisi za fedha zinaogopa kuwakopesha.

Alitoa mfano kuwa, kuna wawekezaji walikubali kuwekeza katika kiwanda cha kutengeneza bidhaa za mabati, mkoani Mtwara na kuahidi kufika nchini mwezi ulipita, lakini kutokana na mgogoro wa taasisi za kifedha duniani, wameshindwa kupata mkopo kwa shughuli hiyo.

Rais alisema kimsingi bado wawekezaji hao wana nia ya kuwekeza, na kwamba wana kiwanda kikubwa cha namna hiyo nchini Msumbiji, ambacho kwa mtu kukitembelea kwa miguu yaweza kumchukua siku mbili.

Alisema wawekezaji hao walisema kiwanda chao kingetumia umeme wa megawati 600, hivyo ikapendekezwa kijengwe Mtwara, ambapo wangetumia umeme wa gesi.

Rais Kikwete alisema hata ujenzi wa barabara utaathirika kwa sababu riba ya mikopo mikubwa katika benki za kimataifa imeongezeka, hivyo kwa ushauri wa kitaalamu kwa sasa imeonekana ni vyema kuahirisha hadi zitapopungua.

Alitoa mfano kuwa, nchi ambazo zilikopa kabla ya mgogoro huo wa kifedha zilipata fedha kwa riba ndogo ya kati asilimia sita hadi nane, ambapo kwa sasa ni asilimia 11 hadi 15.

Rais alifafanua kwamba, Ghana walikopa dola za Marekani milioni 700 wakafanikisha ujenzi wa mtandao wa barabara na Gabon ilikopa dola bilioni moja kwa riba ya asilimia sita, ambayo imepanda na kuwa asilimia 11.

Hii ni mara ya pili kwa Rais Kikwete kualikwa kuwa mgeni rasmi katika Baraza la Iddi, ambapo mwaka 2006 alihudhuria baraza hilo lililofanyika mkoani Arusha.
 
Mtanisamehe kauliza za huyu jamaa JMK zinanifanya nijizuie kucheka.Anyway mate wake huyu hapa
borat_lebanon0109.jpg
 
Hiyo ndiyo maana ya SOKo HURIA. Huwezi kulazimisha bei ishuke ati kwa kuwa soko la Dunia imeshuka. Market forces ndizo zitaamua ishuke au la. Njia rahis kama serikali ilivyotaka kuanza, sijui imeishia wapi, ni kuanzisha au kufufua shirika la maendeleo ya Petrol ili ku-compete. Otherwise, bei kushuka ni story hiyo. Wauzaji wenyewe wa bongo?!!

Mbona sijawahi sikia hata siku moja serikali ikipiga kelele kuhusu nauli za boat DSM-Zanzibar. Umbali wa kilometer 78 watu wanalipa 22,500! Umeona wapi hiyo? Wale jamaa wamefanya cartel na wanauza wanavyotaka kupata super profits. Wadhitiwe wale
 
Mbona sijawahi sikia hata siku moja serikali ikipiga kelele kuhusu nauli za boat DSM-Zanzibar. Umbali wa kilometer 78 watu wanalipa 22,500! Umeona wapi hiyo? Wale jamaa wamefanya cartel na wanauza wanavyotaka kupata super profits. Wadhitiwe wale[/COLOR]

Wauza mafuta a Dar sio untouchables, ni watu wadogo sana ikilinganishwa na wamiliki wa boti. Unajua jinsi nchi yetu inavyoendeshwa.
 
Hiyo ndiyo maana ya SOKo HURIA. Huwezi kulazimisha bei ishuke ati kwa kuwa soko la Dunia imeshuka. Market forces ndizo zitaamua ishuke au la. Njia rahis kama serikali ilivyotaka kuanza, sijui imeishia wapi, ni kuanzisha au kufufua shirika la maendeleo ya Petrol ili ku-compete. Otherwise, bei kushuka ni story hiyo. Wauzaji wenyewe wa bongo?!!

Mbona sijawahi sikia hata siku moja serikali ikipiga kelele kuhusu nauli za boat DSM-Zanzibar. Umbali wa kilometer 78 watu wanalipa 22,500! Umeona wapi hiyo? Wale jamaa wamefanya cartel na wanauza wanavyotaka kupata super profits. Wadhitiwe wale
Wasipangiane🤣
 
Back
Top Bottom