Jenerali Ulimwengu na "wanasiasa" dili!!!

kindafu

JF-Expert Member
Nov 12, 2010
1,346
1,676
Wanasiasa feki hawafanyi siasa; wanafanya ‘dili’ kupata vyeo vya kufanyia ‘dili’
Jenerali Ulimwengu
KATIKA makala ya wiki jana nilieleza kwamba ‘wanasiasa’ waliomo ndani ya chama-tawala hawafanyi siasa bali wanafanya mambo mengine kabisa.
Nimeweka neno hili ‘wanasiasa’ katika alama za nukuu kuashiria kwamba hawa si wanasiasa hata kama wanaamini kwamba wanafanya siasa. Wiki hii nimekusudia kueleza kwa undani kidogo ninachomaanisha kwa kusema ninayoyasema.
Kwanza kabisa nianze kwa kueleza maana ya maneno siasa na mwanasiasa kadri ninavyoelewa maana yake. Siasa ni shughuli nzima inayohusu uendeshaji wa utawala wa jamii, ikiwa ni pamoja na mipangilio ya utawala, umiliki wa nguvu za umma, na maingiliano na mahusiano ya maslahi ya makundi mbalimbali yanayoshindana katika kutafuta na kuhodhi mamlaka ya serikali (tafsiri isiyo rasmi).
Mamlaka ya serikali au dola ni bidhaa muhimu na adimu kwa makundi mengi, ambayo daima yatashindana katika kuyasaka na kuyatumia kwa ajili ya kuendeleza maslahi ya makundi hayo. Ni muhimu kwa sababu aliye nayo anapata uwezo mkubwa wa kuamua na kutekeleza yale anayoamini kwamba yataendeleza maslahi ya kundi analoliwakilisha; ni adimu kwa sababu katika eneo moja kwa kawaida kutakuwa na serikali moja tu, na hii ina maana kwamba nafasi za kuingia katika utawala ni chache mno na mashindano ya kuingia huko yanalazimika kuwa makali.
Aidha, makundi ya kijamii, ambayo katika sura nyingine yanaweza kuwa ni matabaka ya kiuchumi yanayokinzana na kuhasimiana, huwa yanafanya siasa ili kusukuma maslahi yao mbele na kuyapa nguvu dhidi ya makundi mengine katika kile kinachoitwa ‘mapambano ya kitabaka’ (class struggle).
Uhasama huu ukikua, ukakomaa kiasi cha kutosha unaweza kusababisha vita ya kitabaka, kila tabaka likijaribu kuliengua jingine na kuhodhi mamlaka ya dola kwa faida ya tabaka hilo. Historia imejaa mifano ya vita za aina hii.
Makundi haya ya kijamii hujenga mitazamo ya kifalsafa inayotokana na hali zao na maslahi yanayoyatetea. Tofauti kubwa kati ya binadamu na hayawani ni kwamba binadamu anao uwezo wa kufikiri, kuwaza na kujenga dhana kutokana na uzoefu wa jamii anamoishi, mazingira yanayomgusa na ambamo vizazi vilivyomtangulia viliishi, vikapambana na mazingira hayo, vikajenga mahusiano, vikavuna na kulimbikiza ujuzi, maarifa, busara kadri vilivyopata uzoefu.
Kinachotokana na hazina hii kubwa ya karne kadhaa ndicho huwa msingi wa mtazamo wa kifalsafa unaoeleza jamii husika ni jamii ya aina gani, watu wake wanaenenda vipi, nini unaweza kutazamia kwao na nini huwezi kutazamia kwao, nini wamekikubali na nini hawakikubali.
Huu ndio msingi wa falsafa, ambao unaambaa katikati ya imani za kidini na uyakinifu wa kisayansi, kiasi kwamba si dini wala si sayansi; ni mtazamo, muono, namna ya kuuangalia na kuuelewa ulimwengu, na kuhusiana na walimwengu.
Juu ya mwamba huu wa kifalsafa, itikadi za kisiasa zitajengeka ambazo zinashabihiana na falsafa husika. Makundi na matabaka yanayotofautiana kifalsafa yatatofautiana kiitikadi vile vile. Palipomea falsafa kwamba binadamu wote hawawezi kuwa sawa itajengwa itikadi inayohubiri kwamba wanawake, au watu weusi, au walemavu, au makabila fulani hawana uwezo wa kufanya hili au lile, n.k.
Juu ya falsafa, na juu ya itikadi inayotokana nayo, ndipo tunapata programu za kisiasa, ambayo ni mipango ya kusambaza falsafa na itikadi, kuwashawishi wanajamii kwa wingi unaowezekana kuunga mkono falsafa na itikadi za kundi husika ili kujenga mazingira ya kushinda na kukamata nguvu za dola kama njia ya kutekeleza matakwa ya kundi au tabaka hilo. Hapa ndipo tunapopata mikakati, programu za utekelezaji, ilani na mbinu za kiuenezi.
Hali hii bila shaka inajenga utamaduni wa mabishano, mijadala, ujengaji wa hoja, upambanishaji wa hoja na kila aina ya malumbano yaliyojengeka katika misingi ya ujuaji na si kwa kupiga kelele. Tokea ujana wao vijana hujifunza kutafuta taarifa zinazowasaidia kujenga hoja, na hushiriki katika midahalo ya kila aina shuleni kwao au katika miji yao na vijiji vyao.
Kwa jinsi hii vijana huhuweza kunoa vipaji vyao vya kufikiri na kuzungumza hadharani, pamoja na kuandika kwa ufasaha mkubwa kutokana na kuwa na uzoefu mkubwa wa ki-mdahalo.
Hivyo ndivyo ilivyokuwa enzi za wanafalsafa wa kale mjini Athens na mjini Roma enzi za akina Plato na Marcus Aurelius. Ndivyo ilivyokuwa Marekani enzi za akina Thomas Jefferson na Patrick Henry. Ndivyo ilivyo Bara Hindi leo hii, enzi ya kitabu cha Amartya Kunar Sen, “The Argumentative Indian.” Pia ndivyo ilivyokuwa nchini Tanzania enzi za TANU Study Group, ‘Cheche’ na midahalo ya Umoja wa Vijana wa CCM.
Taratibu, huku wengine tukishuhudia, nchi hii imeua mijadala, hususan ndani ya chama-tawala. Inashangaza kwamba chama kilichokuwa na mijadala ya kila siku wakati kikiwa chenyewe katika ulingo wa siasa (bila mpinzani) sasa, wakati kina wapinzani kibao ndiyo kimeamua kukataa mijadala na kuendesha mambo yake bila mijadala.
Sasa, wanafanyaje siasa bila mijadala? Hawafanyi. Unaweza kufanya mambo mengi katika asasi rasmi bila mjadala, lakini hakuna siasa inayofanyika nje ya mijadala. Kwa hiyo kinachofanyika katika chama-tawala ni kitu kingine isipokuwa siasa. Ni nini hicho?
Ni kile ninachokiita mipangilio, usukaji wa mipango, dili.
Maelezo yangu hapo juu yanayoainisha siasa ni kitu gani, (kama yanakubalika angalau kwa maana ya juu juu) yanaweza kutusaidia kama kigezo cha kuangala ni nini kinachofanywa na chama-tawala hivi sasa ambacho tungeweza kukiita siasa. Sikioni.
Nchi hii imekumbwa na matatizo makubwa mno, na kila mtu anayajadili isipokuwa hao ‘wanasiasa.’ Wao wako katika sayari yao wenyewe. Wanapigana vikumbo bila kusema ni nini hasa kinawafanya wapigane vikumbo.
Wakati nishati ya umeme imekuwa ni adha kubwa kuliko wakati wo wote tangu tupate huo uhuru tunaousherehekea kinafiki (Tumethubutu….?) watawala wetu wanapigana ngwala eti kwa kutafuta urais wa 2015.
Maisha ya Watanzania yanazidi kuwa magumu kwa maana ya gharama za maisha zinazopanda kwa kasi kubwa. Vyakula vya msingi kabisa vinazidi kupanda bei huku kipato cha mwananchi kikipungua kutokana na kushuka kwa thamani ya sarafu yetu.
Bei ya mafuta ya peteroli, bei ya mafuta ya taa, bei ya sukari muhimu kwa nishati ya miili ya watoto wadogo wasiopata chakula cha kutosha zinazidi kupaa…
‘Wanasiasa’ wetu wamo katika kusuka mipango, kupanga dili za urais wa 2015. Mkuu wao naye anawaangalia kama anayeangalia sinema. Hatusikii akiwakemea. Hatumsikii akiwakumbusha kwamba jukumu lao kubwa ni kutafuta namna ya kuwasaidia Watanzania waweze kukabiliana na maisha magumu, na si kusaka urais.
Ni kwa nini urais unasakwa nje ya siasa na ni kwa nini unasakwa na ‘wanasiasa’ wasiofanya siasa? Kwa sababu urais wa nchi hii umekwisha kuwa ni bidhaa na mtaji kwa wakati mmoja.
Ni bidhaa kwa sababu anayeutaka anaweza kuununua. Nilikwisha kuonyesha jinsi ambavyo utawala wetu wote unavyoweza kununuliwa na tajiri mmoja tu, awe ni kutoka Marekani, Kipros au Abu Dhabi. Sasa inafanyika, kwa sababu, kama nilivyosema wakati ule, ukiisha kukipeleka kitu chochote sokoni, kitapata mnunuzi.
Ni mtaji pia, kwa kuwa anayeupata anakuwa amejiweka katika nafasi nzuri ya kufanya biashara nyingi na za kila aina kwa kutumia mtaji wa urais. Mke wake, watoto wake, ndugu zake na maswahiba zake wanaweza kuranda kila kona mjini wakiuza amana ya urais kwa kubadilishana na mali na fedha.
Urais wa aina hii, kama ilivyo pia kwa vyeo vingine kama uwaziri, ukuu wa mkoa na ukuu wa wilaya, hauhitaji kufanya siasa; ni dili tu…. Juma kaa hapa, John pale, Janet wewe nenda pale kisha Jamal atakaa hapa…tujenge mtandao… hapana hapo mwachie Issa anamaliza muda wake kule alikokuwa hatuna pengine pa kumuweka.. sasa na huyu Robert aliyeshindwa uchaguzi juzi? Ah, kweli, lakini usijali tunafungua ubalozi mpya Galapagos… mipangilio ya ulaji. Hamna siasa.

My take:
Hivi hawa "wanasiasa" wetu huwa wanasoma makala kama hizi kweli? Kama wanasoma wanajisikiaje nafsini mwao???
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom