Jenerali Mdogo Kwenye Nchi Kubwa! ( Makala, Raia Mwema)

maggid

JF-Expert Member
Dec 3, 2006
1,084
1,246
Na Maggid Mjengwa,
VIONGOZI Afrika hawajui kusoma alama za nyakati. Tumeona juzi hapa, kiongozi mwingine wa Kiafrika akidhalilika na kulidhalilisha bara letu, si mwingine ni Laurent Gbagbo. Anaingia kwenye msururu wa viongozi wa Kiafrika ambao mwisho wao umekuwa wa aibu kubwa.



Na kule Ivory Coast inahusu kiongozi na Chama kung’ang’ania madaraka hata pale wananchi wanapowaondoa kwa kura. Afrika viongozi wa aina ya Laurent Gbagbo walikuwawapo na bado wapo. Lililo jema, umma wa Afrika ukiongozwa na vijana uko mstari wa mbele kupambana kuwaondoa akina Gbagbo. Ni aina ya viongozi ambao, wao ama vyama vyao, huingia madarakani kwa hila na wagumu kuachia madaraka.


Huu ni wakati wa mabadiliko barani Afrika


Katika nchi nyingi barani Afrika, viongozi na vyama tawala kandamizi viko mashakani. Ni katika wakati huu ambapo hila na ghilba zitatumika zaidi. Watawala Afrika watajitahidi pia kuwaficha watu wao wasione ukweli wa kinachoendelea kwengineko.


Mara kadhaa nimekumbushia kuwa historia ni mwalimu mzuri. Afrika tumepata kuwa na viongozi kama Mobutu wa iliyokuwa Zaire ya zamani ambaye hakuheshimiwa na watu wake, aliogopewa. Na sifa moja ya madikteta ni kuogopewa.


Mobutu hakujishugughulisha na chochote kinachoitwa ujenzi wa taifa. Kinyume chake, Mobutu alijaribu kuligawa taifa katika makundi kadri alivyoweza. Aliamini kuwa kwa namna hiyo ndivyo angeweza kuwatawala vema Wakongo.


Kwa asili Mobutu alitoka kijiji cha Badolite. Huko, alijenga Ikulu ya marumaru za dhahabu. Ikulu ya Badolite ilikuwa ni kama mji wa kisasa wenye kila kitu. Ilikuwa ni Ikulu ya kifahari kweli kweli. Ikulu iliyokuwa na vyote ikiwamo bwawa la kuogelea. Lakini, ukitoka Kilomita chache tu nje ya Ikulu hiyo, ulikutana na Wakongo walioshi katika umasikini wa kutisha.


Katika mwaka wa mwisho wa utawala wa Mobutu, wananchi masikini walioishi kandokando ya Ikulu ya Badolite walikuwa na mazoea ya kuusimamisha msafara wa Mobutu. Naye Mobutu alifahamu kuwa angesimamishwa, alichofanya Mobutu ni kuwaelekeza Wakongo wale waende kwenye gari la nyuma kwenye msafara wake. Huko kulikuwa na wapambe wa Mobutu waliokuwa na maboksi ya fedha za Kikongo, walizigawa. Wakongo wale walibaki wakizigombania, msafara wa Mobutu uliendelea.


Kitu ambacho Mobutu hakukitafakari ni ukweli kuwa kugawa kwake noti zile kwa Wakongo hakukuwa jawabu la matatizo ya Wakongo. Watu wake walishagawanyika, ni yeye Mobutu aliyechangia kuwagawa.


Mobutu aligawa utajiri wa raslimali za Wakongo kwa wachache. Na yeye akawa mfano wa ufujaji wa rasilimali hizo. Tofauti na wakati wa mkombozi Patrick Lumumba, utaifa na moyo wa uzalendo uliporomoka kwa kasi ya ajabu miongoni mwa Wakongo.


Hatimaye, msafara wa mwisho wa Mobutu haukusimamishwa, kila mmoja alijua kuwa ulikuwa ni msafara wa mwisho kuelekea uwanja wa ndege kutoka Ikulu yake ya Kinshasa. Mobutu aliikimbia Zaire na kufia Ughaibuni kwenye nchi ya Morocco. Inasemekana kuwa watu waliokwenda kumzika Mobutu hawakuzidi sita.


Kwa nini kuna viongozi Afrika wanaoishia kuzikwa Ughaibuni? Ni kutokana na ukweli kuwa viongozi wengi huingia madarakani wakiwa na umma nyuma yao. Lakini wakiwa madarakani, viongozi hawa hulewa madaraka. Huanza kujitenga na umma uliowaingiza madarakani au uliowaunga mkono. Huanza kujilimbikizia mali wao , familia zao na ‘wenzao’ wachache katika utawala.


Viongozi hawa hugeuka vibaraka badala ya kuwa watetezi wa walio wengi. Hawaamini katika kugawana madaraka ya uongozi. Hawaamini katika demokrasia yenye kutoa uhuru mpana kwa watu kujieleza na hata kushutumu. Watatumia vyombo vya dola kuwakandamiza watu wao.


Huishia kujenga ngome ngumu ya kuwalinda. Huingiwa hofu na wale wanaowaongoza. Viongozi hawa hushindwa kabisa kujenga utaifa. Hawataki Utaifa ambao ndio huzaa uzalendo.


Lakini cha kujiuliza ni kitu gani kilichopelekea nchi kubwa kama Zaire, nchi yenye utajiri mkubwa wa maliasili, kukosa utulivu na kubaki kuwa ni nchi yenye watu wengi mafukara na wanaokufa kwa njaa na vita? Historia ya Kongo ni ndefu. Walioanza kuiharibu Kongo ni wakoloni. Lakini kama wasemavyo wahenga_”mvunja nchi ni mwananchi”.


Walioshiriki kikamilifu kuiangamiza Kongo ni Wakongo wenyewe. Kongo ilikuwa na bahati kubwa ya kumpata kiongozi mzalendo na mwanamapinduzi, aliitwa Patrick Lumumba. Mataifa ya Magharibi yakiongozwa na Marekani yalibaini mapema kuwa Lumumba asingelinda maslahi yao isipokuwa maslahi ya Wakongo.


Njama za Shirika la Kijasusi la Marekani (CIA) zilihitimishwa na kukamatwa kwake, kudhalilishwa na kuuawa kwa Partick Lumumba. Aliyetumika kufanya kazi hiyo na hatimaye kuwekwa madarakani kama kibaraka ni aliyekuwa rafiki wa Lumumba na aliyemfanya kuwa Waziri wake wa Ulinzi, Joseph Mobutu.


Ni Mobutu huyu aliyekuja baadaye kubadili jina la nchi na la kwake mwenyewe. Nchi akaiita Zaire na yeye mwenyewe akajiita Mobutu Sese Seko Kuku wa Zabanga. Mobutu aliigeuza Kongo kama mali yake mwenyewe. Alijilimbikizia mali yeye na jamaa zake.


Utawala wa Mobutu ulifanana sana na kisa nilichopata kukisoma huko nyuma katika kitabu kinachoitwa ”Herufi Zilizofanya Maasi”. Alitokea jenerali mdogo, alikuwa ni mtu mdogo hata kwa maumbile, lakini mwenye mamlaka makubwa sana. Alikuwa mtawala wa kiimla, dikteta. Hakuruhusu fikra huru katika nchi yake. Alijifanya ni mwerevu wa kila jambo, ingawa hakuwa mwerevu. Alikuwa ni mtu mjinga aliyeupata utawala kwa bahati tu.


Na kwa vile alipenda sana kutawala na kuamua kila jambo, alidhani ana uwezo hata wa kuamua juu ya fikra na hisia za watu wa nchi ile. Hivyo basi, alitaka watu wa nchi ile wasikie tu kile anachotaka yeye wasikie, na zaidi habari nzuri juu yake na nchi yake. Hakupenda kabisa kusikia habari mbaya zenye shutuma dhidi yake au juu ya mwenendo wa nchi na hali za wananchi.


Alitaka udhibiti wa mambo, alipiga marufuku maandiko yote ikiwemo vitabu na magazeti. Hakukuwa na ruksa ya kusoma, kuandika wala kuchapisha maneno huru, fikra huru. Watu wa nchi ile walizipata habari zote juu ya nchi hiyo na za dunia kupitia baragumu la jenerali mdogo. Baragumu lilitangaza yale ambayo jenerali mdogo aliyaelekeza na alitaka wananchi wake wayajue.


Lakini katika nchi ile, aliishi bwana mmoja aliyeitwa Placido. Bwana huyu alikuwa msomaji mzuri wa vitabu, alipenda pia kuandika. Aliutaka na aliupenda uhuru wa kujiamulia mwenyewe juu ya fikra na hisia zake. Licha ya jenerali mdogo kupiga marufuku ya kusoma na kuandika, Placido aliyafanya yote mawili kwa usiri mkubwa. Alisambaza pia maandiko yake kwa usiri mkubwa. Alitaka watu wayasome, na watu walikuwa na kiu ya kusoma.


Mara Yule jenerali mdogo alipogundua kuna maandiko yanayosambazwa, maandiko yaliyosheheni habari zenye maarifa mbalimbali ikiwemo maarifa ya ukombozi, basi, amri ilitolewa kwa askari kusaka kila karatasi yenye maandiko. Ulifanyika msako wa nyumba kwa nyumba na mtaa kwa mtaa.


Placido, bwana yule mwandishi, naye alikamatwa na kufungwa gerezani. Karatasi zote zenye maandiko zilikusanywa, ikawa kama kichuguu kirefu. Zikawashwa moto. Majina ya watu, historia na mengineyo yenye kuelezea nchi ile, yote yaliteketea. Wengi walitokwa machozi, lakini hakuna chozi lenye kuzima moto uliowashwa na mtu mpumbavu, mtu mjinga.


Naam. Katika nchi zetu hizi, bado tuna watawala wenye kufanana sana na jenerali mdogo katika nchi kubwa. Katika hili tunaweza kuandika kuwa Jenerali Mobutu alikuwa ni jenerali mjinga katika nchi kubwa. Amechangia sana katika machungu waliyoyapata na wanayoendelea kuyapata watu wa Kongo.


Mobutu alipoingia madarakani alianza kudhibiti vyombo vya habari. Wasomi na waandishi wa vitabu walilazimika kukimbilia mafichoni. Waliobaki walikiona cha moto.


Jenerali Mobutu alijaribu kufuta yote yenye kumhusu mkombozi wa watu wa nchi hiyo, Patrick Lumumba. Alipiga marufuku Wakongo, sio tu kuzungumza habari za Lumumba, bali pia hata kutundika picha za kiongozi huyo hadharani na hata kwenye sebule za vyumba vyao.


Mobutu alitaka na alipenda Wakongo wamuimbe yeye. Wampigie makofi hata kwa kauli za kipumbavu. Hakuelewa kuwa, unaweza kumpekeka punda mtoni, lakini huwezi kumlazimisha kuyanywa maji. Kwamba unaweza kumlazimisha mwanadamu kukupigia makofi, lakini kamwe si kutabasamu toka moyoni.


Kuna walioengua vicheko kwenye hotuba za Mobutu, wakati mwingine tafsiri za vicheko hivyo zilikuwa ni kumdharau Mobutu kwa kauli zake za kipuuzi. Hakika Afrika tunao akina Laurent Gbagbo na Mobutu wengi., majenerali wadogo kwenye nchi kubwa!

MJENGWA - Picha, Habari & Matangazo
0788 111 765
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom