Jakaya Kikwete 'alivyododa' Butiama

Sokomoko

JF-Expert Member
Mar 29, 2008
1,915
127
Na Saed Kubenea

PAMOJA na madaraka makubwa aliyonayo ndani na nje ya chama chake, Rais Jakaya Kikwete ameshindwa kupitisha kile alichokiamini, alichoombea misaada na ambacho serikali yake imeshiriki kugharimia kwa kipindi cha miezi 14.

Tarehe 30 Desemba 2005, wakati akifungua kikao cha Bunge mjini Dodoma, Rais Kikwete alisema anataka kumaliza kile alichokiita, “mpasuko wa kisiasa Zanzibar.”

Lakini hali haikuwa hivyo Butiama. Huko Kikwete alihojiwa. Alikaripiwa. Alidhalilishwa na alifedheheshwa kwelikweli.

Hakudhalilishwa na wafuasi wa vyama vya upinzani. Mara hii alidhalilishwa na wale waliomchagua. Wale walioapa kumlinda na kumtetea.

Ni hao ndio walimueleza, tena bila hata kumuangalia usoni, wakisema, “ondoka na ajenda yako. Hakuna serikali ya mseto wala shirikishi Zanzibar.”

Hakika, kikao cha Butiama hakikuwa kikao cha kujadili Mwafaka, au mambo mengine yenye maslahi kwa chama na taifa, bali kilikuwa kikao kilichoitwa na wengi kuwa cha “kuonyeshana ubabe.”

Kila mmoja anajua kwamba Kikwete alielemewa. Na hili linathibitishwa hata na hotuba yake aliyoitoa kwa wanachama wake mara baada ya kurejea kutoka Butiama.

Kikwete aliwaambia wana-CCM waliokusanyika katika ukumbi wa Diamond Jublee, jijini Dar es Salaam, kwamba kikao cha Butiama ndicho kilikuwa cha kwanza kwa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kupewa taarifa ya maendeleo ya mazungumzo ya Mwafaka.

Ni wazi kwamba Rais Kikwete, anaficha ukweli. Hasemi kwamba wajumbe wa Kamati Kuu na NEC ya CCM walikuwa wanajua kila kitu. Taarifa ya CCM iliyowasilishwa kwa wajumbe wa NEC, ambayo chama hicho kimeiita siri inasema wazi kwamba NEC ilikuwa inajulishwa hatua kwa hatua juu ya mazungumzo hayo.

Ukurasa wa tatu wa taarifa hiyo unasema: “Kamati ya mazungumzo na CUF imekuwa na utaratibu wa kutoa taarifa ya maendeleo ya mazungumzo na CUF kwenye Kamati Kuu ya Taifa mara kwa mara.

“Kamati Kuu, baada ya kuitafakari taarifa, imekuwa ikitoa maelekezo stahiki kwa maendeleo bora ya mazungumzo. Taarifa za maendeleo ya mazungumzo ya mwafaka zimekuwa zikifikishwa pia Halmashauri Kuu ya Taifa kwa madhumuni hayohayo.”

Hii ina maana kwamba NEC ilikuwa inajua kuwa Kamati ya mazungumzo inataka iwepo serikali shirikishi Zanzibar. Hivyo basi, upinzani uliotokea umesababishwa na mambo matatu makubwa.

Kwanza, udhaifu wa Kikwete katika kusimamia kile anachokiamini. Pili, wajumbe wengi, hasa kutoka Zanzibar, walitawaliwa na ubinafsi kuliko maslahi ya taifa. Tatu, walikuwapo wajumbe wengi walioshindwa kuchanganua mambo kwa haraka.

Kwa mfano, baadhi ya wajumbe walikuwa wanang’ang’ania kutokuwapo kwa serikali shirikishi Zanzibar, kwa hoja kwamba Zanzibar kuna Serikali ya Mapinduzi, na kwamba kuleta serikali shirikishi kutaifanya ile ya mapinduzi ifutike.

Ni kauli hii inayodhihirisha ufahamu mdogo wa wajumbe katika mambo ya msingi.

“Zanzibar kuna serikali ya Mapinduzi. Sasa mnataka kuleta serikali shirikishi, mtaitaje hii iliyokuwapo? Mtaita Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Shirikishi?” alihoji mjumbe mmoja wa NEC, akidhihirisha kwamba ameshindwa kupambanua kilichoelezwa.

Baadhi yao hawajui kwamba kinachobadilishwa si jina, bali ni mfumo wa uongozi; kwamba kwa sasa, chama kinachounda serikali ni kile kinachoshinda urais hata kama hakina wawakilishi wengi katika Baraza la Wawakilishi.

Kinachotakiwa ni kuwa na serikali ya pamoja kati ya wale walioshinda uchaguzi na wale walioshindwa lakini kwa karibu sana. Hiyo ndiyo serikali shirikishi inayotakiwa, jambo ambalo haliathiri kabisa jina la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Jina haliwezi kuondoka kwa kuunda serikali ya ushirikiano bila kuwapo makubaliano mengine ya kubadilisha jina hilo. Lakini kwa umbumbu wa wajumbe, suala hilo likawa hoja kuu hadi Kikwete akatokomea.

Lakini jambo hili Kikwete analijua vema. Anajua kuwa baadhi ya wajumbe wa vikao vyake hawana sifa ya kushika nafasi walizonazo. Hili tumeliandika sana huko nyuma.

Tumesema kwamba kutokana na CCM inavyoendesha uchaguzi wake ndani ya chama, uwezekano wa watu wasio na sifa, hadhi wala heshima ya kuwa viongozi, kupata uongozi ni mkubwa sana.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba chaguzi za sasa ndani ya CCM zimetawaliwa na hila, hadaa na ghiliba. Wanachama na viongozi wa chama hiki wanakiri kuwa si chaguzi tena, bali ushindani katika ununuzi wa kura.

Ukichukua tatizo hilo, ukachanganya na makundi yanayokitafuna chama, pamoja na udhaifu wa kibinadamu au wa kuendekeza wa mwenyekiti na watendaji wake, ni dhahiri kuwa huwezi kuwa na chama makini cha siasa.

Hapo patakuwa kijiwe cha watu waliojikusanya kwa lengo la kumkomoa huyu na kumkwamisha yule; maana kila mwenye akili timamu na anayefikiri vema, anajua kuwa Zanzibar kuna mpasuko wa kisiasa uliodumu kwa miaka mingi sasa.

Na wajumbe wa NEC na CC wanalijua vema jambo hili. Wanajua kwamba njia pekee ya kumaliza mpasuko huo ni kuwapo kwa serikali shirikishi.

Je, wanataka kutuambia kuwa hawajui kwamba hatua yao ya kumgomea mwenyekiti wao kupitisha hoja yake, imemshushia hadhi na heshima mbele ya jumuiya ya kimataifa?

Viongozi wengi makini wa CCM wanajua kuwa chama chao hakishindi uchaguzi Zanzibar, bali huwa kinatangazwa kuwa kimeshinda. Hakiendi kwa matakwa ya wananchi.

Lakini unapokuwa na chama ambacho watendaji wake wanakuwa wa kwanza kukana yale wanayoyasimamia, unatarajia nini?

Tayari Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba, amekana yale aliyotumwa. Anasema maamuzi ya jambo hili yalikuwa makubwa, hivyo hayawezi yakafanywa na yeye na Seif Shariff Hamad (Katibu Mkuu wa CUF) peke yao.

Je, Makamba anataka kusema kwamba awali hakujua kuwa hili ni jukumu zito? Au anataka kuthibitisha madai ya siku nyingi ya wapinzani wake kuwa hana uwezo wa kushika nafasi aliyopewa?

Kama nchi hii ingekuwa na utaratibu wa watu kuwajibika kutokana na kushindwa kazi, basi Makamba angekuwa wa kwanza kuondoka. Angesema mbele ya NEC, ‘siwezi kubakia katika nafasi hii. Mmeniabisha mimi na yule aliyenituma.’

Angekubali kuwa hawezi kubaki kwa sababu alichotumwa kukipigania usiku na mchana, wakati wa jua na mvua, kimekataliwa, tena bila hoja bali kwa ushabiki na uhafidhihina.

Angalau hiyo ingejenga heshima kwake na kwa mwenyekiti wake. Lakini kwa kuendelea kung’ang’ania madaraka, Makamba anamdhalilisha mwenyekiti wake, anamdhoofisha zaidi.

Katikla hali hii inaweza kufikia wakati wanachama wakaachana na kusita; wakatamka mara moja ba bila aibu wala woga, kwamba kwa udhaifu huu, Kikwete na makamba waondoke!

Si wajumbe wa NEC na CC tu waliokuwa wanalifahamu jambo hili la kuundwa kwa serikali shirikishi Zanzibar kwa mapana na marefu. Rais Amani Abeid Karume, ambaye wajumbe wa NEC na CC wanasema ndiye aliyeongoza uhafidhina katika kikao cha CC, alikuwa analifahamu kwa mapana na marefu.

Taarifa ya Kamati ya Mazungumzo ya CCM inathibitisha hili katika ukurasa wa tatu: Inasema: “…ujumbe wa CCM katika mazungumzo na CUF, pamoja na kutumia busara na ubunifu wake, ulifanya mashauriano na viongozi wakuu wa chama na serikali ili kuendeleza mazungumzo haya.

“Ujumbe ulifaidika sana kila ulipokutana na mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ndugu Jakaya Kikwete na vilevile ulipokutana na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar, Ndugu Amani Abeid Karume, kutokana na ushauri, maelekezo na mawazo mapana na ya kina waliyoyapata. Mazungumzo yamefika hapa yalipofika kutokana na michango yao hiyo,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Hii ina maana kwamba Kikwete na Karume walikuwa wanajua kinachoendelea, bali tangu mwanzo hawakutaka suala la serikali shirikishi.

Walisubiri kikao cha Butiama kuonyesha rangi zao halisi. Walikuwa na uwezo wa kushauriana mapema na Kamati ya Mwafaka kwamba suala hilo litekelezwe baada ya uchaguzi wa 2010.

Lakini kutokana na hila waliyokuwa nayo moyoni, walisubiri vikao vya Butiama ili wawaburuze wajumbe na kuwafanya ndio wameamua suala hilo.

Hapo ndipo Karume alilia na kusaga meno akisema Mwafaka huu unataka kufuta historia iliyojengwa na “baba yake.”

Lakini yote haya yametokana na Kikwete kukubali kutishwa na wajumbe wa Zanzibar waliofikia hata hatua ya kutaka kujitoa katika Muungano.

Huo ukawa ushindi wa kwanza kwa wapinzani wake, hasa wale waliokuwa wakihoji uwezo wake, si katika kuongoza chama tu, bali hata nchi pia.

Mwenyekiti wa CUF. Ibrahim Lipumba aliwahi kusema, mwaka 2005 kwamba Kikwete ana uwezo wa kuongoza wasanii, si kuongoza taifa.

Alisema: “Kikwete si mtu makini katika kusimamia mambo ya msingi yanayoweza kulikabili taifa.”

Nje ya CCM, wapo waliokuwa na mashaka juu ya uwezo wa Kikwete wa kukabiliana na mambo mazito, ingawa wengi pia walikuwa na matumani.

Wengine walimfananisha na Mwalimu Nyerere lakini leo hii, kwa udhaifu uliojitokeza, Kikwete amewadhihirishia mwenyewe kwamba hana uwezo.

Alilobakia nalo ni turufu moja tu - kuwaachia Zanzibar kufanya uchaguzi huru na wa haki bila kuingiliwa na vyombo ya ulinzi na usalama ambavyo ni mali ya Serikali ya Muungano.

Sharti kazi ya vyombo vya ulinzi ithaminiwe. Lakini kulinda chama kimoja – CCM – siyo kazi ya majeshi. Kazi yake ni kulinda raia na mali zao.

Nani asiyejua kuwa bila wizi wa kura, ghiliba, vitisho na hata kutumia majeshi kuonyesha ubabe wa watawala, CCM isingekuwa madarakani Zanzibar?

Source: MwanaHalisi
 
Hawaelewani kwa sababu wanaongoza nchi kutokana na dhambi ya kura za wizi zilizowapa ushindi,haya mambo yana mwisho na huwezi kuongoza kila siku kwa kutegemea ushindi wa wizi wizi tuu...waache wafanye wanachofanya lakini wanaokula vumbi kutokana na haya matatizo ni nchi nzima sio CUf peke yao!
 
Sasa wewe ndugu yangu sokomoko, hii mada mbona inafanana na ile ya "karume alia mbele ya Kikwete". Kilichoandikwa hapa hakina tofauti na kilichoandikwa katika nakala ya "karume alia mbele ya kikwete".
 
Sasa wewe ndugu yangu sokomoko, hii mada mbona inafanana na ile ya "karume alia mbele ya Kikwete". Kilichoandikwa hapa hakina tofauti na kilichoandikwa katika nakala ya "karume alia mbele ya kikwete".

I swear to GODsio mie nilioandika hizo makala ni Jamaa mmoja anaitwa Saed Kubenea kwenye Gaazeti la MwanaHalisi la Leo habari hii imechapishwa kwenye ukurasa wa 8 na ile ya Karume kulia imechapishwa kwenye ukurasa wa 3. Namba ya Kubenea ni 0784 440073 muulize au back to school utaona tofauti kati ya ile makala na hii.
Ahsante kwa kunisoma MWANAMALUNDI
 
I swear to GODsio mie nilioandika hizo makala ni Jamaa mmoja anaitwa Saed Kubenea kwenye Gaazeti la MwanaHalisi la Leo habari hii imechapishwa kwenye ukurasa wa 8 na ile ya Karume kulia imechapishwa kwenye ukurasa wa 3. Namba ya Kubenea ni 0784 440073 muulize au back to school utaona tofauti kati ya ile makala na hii.
Ahsante kwa kunisoma MWANAMALUNDI

Sokomoko , karibu sana sana hapa JF na leo kwa mchango wako na namba ya simu nimecheka sana hata mbavu sina .Duh!! Sokomoko unapenda vibaya na kuchukia vilivyo .
 
Sokomoko , karibu sana sana hapa JF na leo kwa mchango wako na namba ya simu nimecheka sana hata mbavu sina .Duh!! Sokomoko unapenda vibaya na kuchukia vilivyo .

Ahsante sana Lunyungu. ila nanapenda vizuri na kuchukia vibaya. teh teh teh teh.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom