Jaji Warioba: Hatutaki shinikizo

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,319
33,125
Hakuna kikundi chenye mtu wake
headline_bullet.jpg
Wakabidhiwa ofisi, kazi yaanza



Funguo(1).jpg

Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue (kulia), akimkabidhi funguo za jengo Mwenyekiti wa Tume ya kuratibu maoni kuhusu muundo wa Katiba mpya, Jaji mstaafu, Joseph Warioba, katika hafla iliyofanyika makao makuu ya Tume, barabara ya Ohio jijini Dar es Salaam jana. Anayeshuhudia ni Waziri wa Sheria na Katiba, Celina Kombani.


Mwenyekiti wa Tume ya kukusanya na kuratibu maoni ya wananchi kuhusu Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jaji Joseph Warioba, amesema tume yake haitafanya kazi kwa shinikizo kutoka kwa mtu yeyote.

Alisema hayo alipozungumza katika hafla fupi ya makabidhiano ya jengo litakalotumiwa na tume kuwa ofisi, jijini Dar es Salaam jana.

“Waliotupendekeza watuache tufanye kazi kwa uhuru. Tumepewa kazi ya nchi. Hivyo, hatutaki kufanya kazi kwa presure (shinikizo) kutoka kwa mtu yeyote,” alisema Jaji Warioba na kuongeza: “Wasiseme tuna mtu wetu huku (kwenye tume), hapana. Kama kuna mtu mmemchagua, basi watu wote walioko huku ni wa Watanzania wote.”

Alisema jukumu la kukusanya na kuratibu maoni ya wananchi walilokabidhiwa rasmi na serikali jana, ni gumu na zito. Hata hivyo, alisema watatumia uwezo wao wote kutekeleza kama Watanzania wanavyohitaji.

Alisema mkutano wa kwanza wa tume utapanga jinsi ya kufanya kazi, ikiwa ni pamoja na kuweka utaratibu wa kuwafikia wananchi ili kupata maoni yao juu ya Katiba wanayoitaka.

Jaji Warioba alisema jambo kubwa linalotarajiwa na tume ni Watanzania wanataka Tanzania ya namna gani katika mchakato wa mabadiliko ya Katiba ya nchi.

Kutokana na hilo, aliitaka serikali kurahisisha mawasiliano wakati tume itakapohitaji msaada kutoka kwake (serikali) wa kuiwezesha kuwafikia wananchi hadi vijijini.

“Tukija kuomba msaada kuwe na mawasiliano kuweza kuwafikia wananchi kwenye vijiji na kata. Mmetupa kazi ya kusuka katiba. Wananchi watakuwa na hoja zao kuhusu upungufu na uzuri wa katiba ya sasa ili itengenezwe katiba mpya,” alisema Jaji Warioba.

Alisema tume pia itahitaji msaada wa watu wengi, hasa kutoka vyombo vya habari katika kutoa elimu na kupata maoni ya wananchi ambao alisema wameonyesha imani kubwa kwake (tume).

Jaji Warioba alisema ameridhika na jengo ambalo tume imepewa na serikali na kusema litawawezesha kufanya kazi zake kwa amani na utulivu.

HADIDU ZA REJEA

Kumekuwepo na taarifa za tume hiyo kutopewa hadidu za kama inavyoelezwa kwenye sheria ya Marekebisho ya Katiba ya mwaka 2011, inayompa rais mamlaka ya kuipatia hadidu hizo.

Hata hivyo, akizungumza na NIPASHE, Jaji Warioba alisema kifungu cha 17 cha sheria hiyo kinaeleza majukumu ya tume ambayo ndizo hadidu za rejea.

“Sheria imezieleza kwa hiyo haihitaji tena kupewa hadidu nyingine, kifungu cha 17 kinazitaja,” alisema.
Kifungu cha 17 cha sheria hiyo kinasema:
“(1) Kwa msingi wa mahojiano wa uchambuzi uliofanywa na kuzingatia kifungu cha 16, Tume itatayarisha ripoti itakayokuwa na:
a) muhutasari wa maoni ya wananchi kwa kila hadithi ya rejea;
b) mapendekezo ya Tume kwa kila hadithi ya rejea;
c)ripoti za wataalam welekezi ambao Tume iliwatumia;
d)Rasimu ya Maswada wa Katiba; na
e)Taarifa nyingine yeyote muhimu.
(2) Rasimu ya Muswada wa katiba itakuwa ni kiambatisho kwenye ripoti ya Tume.”

Katibu Mkuu Kiongozi: Ni kazi adhimu
Awali, akiikabidhi tume jengo hilo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alisema makabidhiano hayo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya ushirikiano mkubwa wa serikali kwa tume, iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete, aliyotoa wakati akiwaapisha wajumbe na kuizindua tume hiyo Aprili 13, mwaka huu.

Alisema ahadi hiyo ya Rais Kikwete ilitokana na kutambua kwamba kazi aliyoikabidhi tume ni muhimu, nzito na nyeti, ambayo thamani yake kwa taifa ni kubwa na haiwezi kuwekewa bei.

“Kwa hiyo, serikali yetu licha ya hali ngumu ya kiuchumi na kibajeti inayoendelea nchini na duniani kote, imekubaliana na wananchi kufanya kazi hii,” alisema Balozi Sefue. Jengo hilo ni mali ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Alisema maagizo aliyopewa na Rais Kikwete ni kufanya kila linalowezekana kuiwezesha tume kufanya kazi yake katika mazingira stahiki, kwa uhuru, utulivu, usalama na amani.

UHURU NA UTULIVU WA KUFANYA KAZI

Balozi Sefue alisema jengo ambalo tume imekabidhiwa jana ni zuri, lina ofisi zenye nafasi ya kutosha, samani nzuri na mazingira masafi na kwamba wanaamini itafanya kazi zake kwa uhuru na utulivu kwa sababu ni mali ya serikali na litakuwa halina mtumiaji mwingine isipokuwa tume peke yake.

ULINZI NA USALAMA

Alisema serikali kwa kuzingatia pia ahadi ya Rais Kikwete, imeandaa ulinzi wa kutosha kwenye eneo la jengo hilo, ambako utakuwapo ulinzi wa askari polisi na ulinzi unaotumia mitambo maalum ya kuhakikisha usalama wa wajumbe, watumishi wote na vifaa vya tume.

UTUNZAJI WA KUMBUKUMBU NA NYARAKA

Balozi Sefue alisema katika jengo hilo, serikali pia imeandaa nafasi ya kutosha ya utunzaji wa taarifa na nyaraka za tume na pia kuna vyumba maalum vya kutunzia nyaraka na kwamba, vifaa vya taarifa rasmi za tume (hansard) na kompyuta zinazofaa zimenunuliwa na kazi ya kuviweka vifaa hivyo inaendelea.

MAWASILIANO

Alisema pia serikali imehakikisha tume inakuwa na mfumo mzuri wa mawasiliano na kwamba, tayari sanduku la posta limesajiliwa, simu za mezani na fax tayari zimewekwa na mtandao wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) unawekwa na kwamba, taratibu za kuanzisha tovuti ya tume zinaendelea vizuri.

BAJETI YA TUME

Balozi Sefue alisema serikali imeanzisha fungu kwa ajili ya tume litakaloanza kutumika mwaka wa fedha wa 2012/2013 na kwamba kuwapo kwake kutaiwezesha tume kufanya kazi zake kwa uhuru zaidi.

USAFIRI WA WAJUMBE WA TUME

Alisema serikali inakamilisha taratibu za kununu magari mapya yasiyopungua 30 kwa ajili ya tume ambayo yana uwezo wa kustahimili safari zote zitakazopangwa na tume ili kuwafikia wananchi.

Katibu Mkuu Kiongozi alisema wakati magari hayo mapya yakisubiriwa, jana serikali ingeikabidhi magari yaliyotolewa na wizara na idara mbalimbali za serikali na mashirika ya umma ili yaanze kuwahudumia wajumbe wa tume kwa muda.

VITENDEA KAZI MUHIMU

Balozi Sefue alisema vitendea kazi muhimu vimeandaliwa ambavyo ni pamoja na nakala za sheria ya mabadiliko ya katiba toleo la 2012, machapisho mbalimbali ya sheria nyingine na taarifa za tume nyinginezo pamoja na katiba ya sasa.
Alisema serikali inaendelea kuviandaa vitendea kazi vingine ambavyo tume itavihitaji ili kufanikisha kazi zake.

UMEME

Balozi Sefue alisema pia serikali imekamilisha mpango wa kununua jenereta ili kuhakikisha kuwa kazi za tume hazikwami pale umeme kutoka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) unapokatika.

WATUMISHI

Alisema serikali inakusudia tume iwe na sekretarieti yenye utaalamu wote unaohitajika ili kufanikisha kazi zake na kwamba, zoezi hilo linaendelea vizuri ambapo kwa sasa wameteuliwa watumishi wachache watakaowezesha tume kuanza kazi na wengine wataajiriwa katika ziku chache zijazo.

NYUMBA
Balozi Sefue alisema kwa lengo la kuhakikisha usalama wa wajumbe wa tume na watumishi wa sekretarieti, wote ambao hawaishi Dar es Salaam, serikali itawapa nyumba mpya zenye samani watakazozitumia muda wote wakati wanafanya kazi za tume. Alisema kwa upande wa sekretarieti hiyo pia itarahisisha usafiri wao kwenda kazini na kurejea nyumbani.
Alisema nyumba mpya na nzuri zimepatikana na hivyo hakuna haja ya wale wanaotoka nje ya Dar es Salaam kuhangaika kutafuta mahali pa kuishi.

BARUA ZA UTEUZI


Alisema barua za uteuzi wa wajumbe wa tume zinazoeleza masharti na stahili za kila mmoja wao, zipo tayari na kwamba wangejabidhiwa katibu wa tume jana.

WAZIRI KOMBANI ANENA

Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani, alisema jukumu la tume ni kusimamia mchakato wa mabadiliko ya katiba kwa haki, uaminifu na uwazi.
Hata hivyo, alisema pamoja na mambo mengine, kufanikiwa kwa mchakato huo, kutategemea zaidi uelewa wa wananchi wa katiba ya sasa ya mwaka 1977 ambayo alisema wengi hawana uelewa wa kutosha.

Alisema baadhi ya sababu zinazofanya uelewa mdogo wa wananchi kuhusu katiba ni kiwango kidogo cha uchapishaji na usambazaji wa nakala za katiba kinachochangiwa na gharama kubwa za uchapishaji na pia ukosefu wa utamaduni wa kusoma miongoni mwa wananchi.

Alisema ili kukabiliana na hali hiyo, ni vema tume ikajipanga kutoa elimu kuhusu katiba ya sasa ili kuwapatia wananchi uelewa kuhusu katiba hiyo na kwamba serikali itaendelea kutoa elimu ili kuhakikisha kuwa wananchi wanashiriki kikamilifu katika utoaji wa maoni na pia katika hatua nyingine za mchakato wa mabadiliko ya katiba.

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA ZANZIBAR

Naye Waziri wa Katiba na Sheria wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Abubakar Khamisi Bakari, alisema tume ina kazi kubwa ya kuelimisha wananchi kwa sababu wengi wao hawaujui Muungano.

Aliitaka tume kuwaelimisha wananchi kuujua Muungano kuwa ni nini, una maana gani na uliopo ni wa namna gani na kusema iwapo elimu hiyo itatolewa na wananchi kuielewa, Watanzania watatunga katiba nzuri.

Wengine waliohudhuria hafla hiyo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, Naibu wake, George Masaju na Katibu Mkuu Kiongozi wa SMZ, Abdulhamid Yahya Mzee na baadhi ya makamishna (wajumbe) wa tume.





CHANZO: NIPASHE

 
Siyo statement nzuri..! Inalenga kuonyesha negative sense kwa wale watakaokuwa tayari kushauri tume:tutatoa maoni lakini kuna ushauri wa kitaaluma ambao wanauhitaji sasa haya maneno yatawafanya watu waogope kudhaniwa wameshinikiza tume.
 
Siyo statement nzuri..! Inalenga kuonyesha negative sense kwa wale watakaokuwa tayari kushauri tume:tutatoa maoni lakini kuna ushauri wa kitaaluma ambao wanauhitaji sasa haya maneno yatawafanya watu waogope kudhaniwa wameshinikiza tume.

huo ni ujumbe sahihi,wanapokea maoni sio mashinikizo, kama huwezi kutoa maoni bila ya vitisho vya maandamano changanya Kwato!
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom