IJUMAA KUU: Maaskofu wahofia hatima ya nchi

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,005
IJUMAA KUU: Maaskofu wahofia hatima ya nchi Send to a friendSaturday, 23 April 2011 09:01


askofumala.jpg

Askofu mkuu wa kanisa la Kilutheri Tanzania (KKKT) Alex Malasusa mbele kulia akiongoza mamia ya wananchi waliojitokeza katika kanisa hilo usharika wa Azania kuangalia maigizo ya Ijumaa kuu jana jijini Dar es Salam

Waandishi Wetu
Mwananchi

MAASKOFU wa madhehebu mbalimbali ya Kikristo Tanzania, jana waliitumia Ibada ya Ijumaa Kuu ambayo ni ya kukumbuka mateso ya Yesu Kristo, wakielezea wasiwasi wao juu ya hatima ya nchi kutokana na kugubikwa na vitendo vya rushwa na suala zima la utoaji wa haki kwa wananchi.

Waliwataka waumini wa Kikristo na Watanzania kwa ujumla kuitumia Sikukuu ya Pasaka kurejea vitendo vyema ikiwa ni pamoja na kuheshimiana na kudumisha amani.
Waliozungumza jana ni Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana nchini, Dk Valentino Mokiwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Yuda Thadeus Ruwa'ichi, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Makanisa ya Pentekoste Tanzania (PCT), Askofu David Mwasota, Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Nestory Timaywa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Eusebius Nzigirwa.

Askofu Ruwa'ichi alilia na haki
Kwa upande wake, Ruwa'ichi ambaye ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza, alisisitiza umuhimu wa Serikali na dola kutoa haki kwa umma akisema: "Siyo lazima kelele ya wengi inaporindima ndiyo haki inatendeka."
Akihubiri kwenye ibada hiyo iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Epifania, Parokia ya Bugando, Askofu Ruwa'ichi alisema kila mmoja anawajibika kusimamia ukweli ili kuungana na Kristo katika kutenda haki.
Alisema watendaji wa Serikali wanapaswa kujihoji ni kwa kiasi gani wanatimiza mapenzi ya Mungu katika kuwatendea wenzao haki.

Rwaichi alihoji ni mara ngapi watu waliopo katika dola wamenawa mikono yao ili kutoa haki dhidi ya wanyonge. Aliwataka kumrudia Kristo kujutia dhambi zao ili watakasike.
Alikemea tabia ya baadhi ya watu kufanya mambo kisha kuwatwisha mzigo wengine ili kuokoa roho zao na kwamba tabia hiyo ni kinyume na Kristo ambaye hakuwa kigeugeu katika uamuzi wake.

"Ulimwengu wa leo umebadilika tunapofanya makosa tunatafuta njia za kuwatupia watu wengine mizigo ili kunusuru roho zetu huo siyo mfano ambao tulionyeshwa na Kristo," alisema Ruwa'ichi.
Mapema katika mahojiano na gazeti hili, Askofu Ruwa'ichi, alisema Watanzania wana wajibu wa kudumisha amani na kukwepa kila aina ya dalili zitakazoweza kuivuruga.

Askofu Mokiwa acharuka
Askofu Mokiwa katika mahojiano maalumu na Mwananchi alisema, Tanzania inaelekea pabaya na hali inaashiria kutoweka kwa amani katika taifa hili ambalo kwa miaka mingi, limekuwa kimbilio la wengi.
Askofu Mokiwa alitaja vitu vinavyotishia amani ya Tanzania kuwa ni pamoja na tabia ya wanasiasa kuchafuana na haki kukaa katika mikono ya watu wachache.

Alisema kupanda kwa gharama za maisha, viongozi kuacha kutawala na watu kukataa kutawaliwa, pia ni tatizo jingine linalotishia amani ya nchi.
"Zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania uwezo wao wa kutofautisha uongo na ukweli ni mdogo kuliko watoto wanaojifunza," alisema Askofu Mokiwa bila kufafanua.
"Kweli hali ya nchi hii inanitisha, vitendo vya uvunjifu wa amani, kusemana kumeongezeka, wabunge wanafanya mambo ya ajabu na kuzomeana bungeni, watu wanatajana majina hadharani na kuchafuana. Jamani tunataka tufike 2015 tukiwa na umoja na amani yetu," alisema Askofu Mokiwa.

Alisema kumekuwa na matumizi mabaya ya neno demokrasia, akisema baadhi ya watu wamekuwa wakilitumia kwa manufaa yao na kuwachafua wengine.
Alisema hali inayoendelea sasa ya kila mtu kusema kitu anachojisikia bila kujali athari yake kwa amani ya taifa, itaifikisha nchi pabaya.

"Lakini pia hata baadhi yenu mnaoshika hizi kalamu (waandishi wa habari), mnatumia vibaya fursa yenu ya kuelimisha watu. Umoja wa kitaifa sasa hivi unatishiwa, kila mtu akiendelea kuwa msemaji tutafika pabaya. Kwa kweli mimi naona taifa hili linaelekea pabaya," alisisitiza.
Askofu Mokiwa alishauri "Ili kuepuka hali hiyo, kila mtu awajibike. Vyombo vya kutoa haki vifanye kazi yake, wabaya waache ubaya wao na wabunge waache utoto wa kuzomeana. Kuna giza zito mbele, tusipolifanyia kazi tutafika pabaya."

Askofu Dar akemea rushwa
Kwa upande wake, Askofu Msaidizi Nzigirwa, alitoa wito kwa viongozi kuepuka rushwa na kutenda haki ili kujenga jamii yenye upendo, iliyostaarabika na kumjali Mungu.
Nzigirwa alitoa kauli hiyo juzi katika Ibada ya Alhamisi Kuu, iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.
Alisema si jambo zuri kupokea au kutoa rushwa kwa sababu ya kuzuia haki za watu na kwamba kufanya hivyo ni kumkosea Mungu.
"Ni lazima ujiulize kwa nini nazuia haki za watu? Nataka hadi nipewe rushwa ndipo niwapatie haki zao kwa nini?"alihoji.
Alisema maadhimisho ya Karamu ya Mwisho, yawe changamoto kwa watu kwa kuwa wanaambatana na upendo wa Yesu Kristo.

Askofu Mwasota na amani
Askofu Mwasota akizungumzia Ibada hiyo ya Ijumaa Kuu alisema ni vyema Wakristo wakatumia wakati huu wa Pasaka kutafakari ukombozi wa Yesu Kristo.
"Tunavyosema ukombozi tunamaanisha amani na matumaini aliyotupa Bwana Yesu alipotufia Msalabani. Pamoja na mijadala yote inayoedelea nchini, Watanzania tuikumbuke amani tuliyonayo na kuiombea ili iendelee kudumu zaidi."
Alisema katika wakati huu wa Pasaka, kila Mtanzania anatakiwa kuiangalia hali ya nchi ilivyo na kisha ajivike wadhifa wa urais, ili aweze kupima hali ilivyo na kisha kuona umuhimu wa kumwombea kiongozi huyo wa taifa.

"Kila mtu nyumbani kwake wakati huu wa Pasaka ni vyema akamwombea Rais ili Mungu ampe nguvu na kumwongoza vyema katika kuliongoza taifa," alisema Askofu Mwasota.
Aliwataka pia Watanzania kuiombea nchi yao na kumshukuru Mungu kwa kuliwezesha taifa hili kutimiza miaka 50 ya uhuru kwa amani.

Kwa mujibu wa Askofu Mwasota, pia Pasaka ni wakati mzuri wa kuiombea nchi ili iweze kuendelea katika miaka mingine 50 kwa amani na matumani kwa wananchi wake.
"Tukitumia pasaka hii kuyafanya hayo, litakuwa ni jambo jema kwa taifa na watu wake," alisema.

Askofu Timanywa azungumzia sumu ya nyoka
Mjini Bukoba, Askofu Timanywa aliwataka waumini kumuomba Mungu ili awaponye dhidi ya kile alichokiita: "Sumu ya nyoka wa nyakati hizi."
Katika mahubiri yake ya jana alasiri katika Kanisa la Rumuli, Askofu Timanywa alikumbusha umuhimu wa waumini kuomba na kusali ili waweze kuvuka salama.

"Tuwe tayari kukiri makosa yetu tunapotaka kuanza upya, tumwombe sana Mungu atuponye na sumu ya nyoka wa nyakati zetu," alisema bila ya kufafanua zaidi.
Jijini Dar es Salaam, Padre Novatus Mbaula wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph, amewaka wananchi kutenda haki na kuondoa chuki ili taifa liweze kuishi katika hali ya utulivu na amani.
Akizungumza wakati wa Misa ya Ijumaa Kuu jana, Padre Mbaula alisema vitendo vya kulipiza visasi vinaweza kuhatarisha amani na kushindwa kusameheana.

Alisema katika kipindi hiki, nchi nyingi za Afrika zinakabiliwa na changamoto ya maandamano: "Afrika inakabiliwa na changamoto za maandamano, inawezekana wanaofanya hivyo wana haki au hawana, walipaswa kuchunguza kwanza kile wanachokidai ndipo wafikie uamuzi wa kuandama, kutokana na hali hiyo wanachokitenda kinaweza kuongeza chuki na kuondoa haki," alisema Padre Mbaula.

Alisema kutokana na hali hiyo, wananchi wanapaswa kusameheana kwa sababu msamaha hauwezi kupimwa kisayansi, bali ni mtu na Mungu pekee.
Alisema ikiwa watatimiza hilo, wanaweza kujengeana upendo baina ya mtu na mtu, familia na familia ambao utadumisha haki miongoni mwao.
Habari hii imeandaliwa na Fredy Azzah, Patricia Kimelemeta na Elizabeth Ernest, Sheila Sezzy, Mwanza na Phihas Bashaya, Bukoba.
 
Back
Top Bottom