Hotuba ya waziri kivuli elimu na mafunzo ya ufundi

Mpaka Kieleweke

JF-Expert Member
Feb 27, 2007
4,132
1,571
HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI MHESHIMIWA CRISTOWAJA MTINDA (MB) KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA 2011/2012.


UTANGULIZI.Mheshimiwa Spika, Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na kuweza kusimama hapa mbele ya Bunge hili, kuwasilisha Maoni na Mapendekezo ya Kambi ya Upinzani kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa mwaka 2011/2012 kwa mujibu wa kanuni za Bunge, kanuni ya 99(7).

Mheshimiwa Spika, Kabla ya kuanza kutoa maoni yetu naomba nikishukuru chama changu cha Demokrasia na Maendeleo – CHADEMA. Vile vile na kwa umuhimu wa kipekee namshukuru Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni Mhe. Freeman Aikael Mbowe (Mb) kwa kuniteua kuwa Waziri Kivuli wa Wizara hii. Nami natoa ahadi kwao kuwa nitajitahidi kwa kadri ya uwezo wangu na kwa jinsi Mwenyezi Mungu atakavyonijalia, kuwatumikia wananchi na taifa langu

.
Mheshimiwa Spika, natoa shukrani zangu za dhati kwa Baraza la Wanawake Chadema (BAWACHA), kwa kunichagua kuwa miongoni mwa Wabunge wa Viti Maalumu kuiwakilisha Singida bungeni. Aidha, nakishukuru Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kubuni utaratibu uliotumika kutuchagua Wabunge wa Viti Maalumu wa chama chetu bila manung’uniko.
Mheshimiwa Spika, mwisho lakini kwa umuhimu mkubwa, napenda kuipongeza familia yangu pamoja na wazazi wangu Mchungaji na mama Mchungaji Gerson Mtinda kwa kunipa msaada mkubwa na kuniombea katika kazi hii ninayoifanya. Nasema Mungu awabariki sana!
MAJUKUMU YA WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imekabidhiwa majukumu ya kuweka viwango vya ubora wa elimu na mafunzo ya ufundi katika ngazi ya Elimu ya Awali na Msingi; Elimu ya Sekondari; Mafunzo ya Ualimu; Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi, Elimu ya Juu, Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi pamoja na Taasisi na Mabaraza yaliyo chini yake.
Aidha, Wizara ina jukumu la kusimamia utekelezaji wa utoaji wa elimu kwa kufanya ufuatiliaji na tathmini. Wizara, pia, ina wajibu wa kufanya mapitio, kuandaa na kutoa mapendekezo ya marekebisho ya sera, mipango, sheria na kanuni za elimu zilizopo, kulingana na mabadiliko ya dira ya Serikali na kuandaa mikakati ya utekelezaji wake.

ELIMU YA AWALI

Mheshimiwa Spika, elimu ya awali ni mafunzo ya awali ambayo humwandaa na kumjenga mtoto katika mchakato mzima wa shule. Ingawa Wizara imeshaandaa mtaala wa elimu ya awali, lakini elimu hii haijaenea sana vijijini. Taarifa ya hali ya uchumi ya mwaka 2010 inaonyesha ongezeko la asilimia 3.3% pekee ya wanafunzi waliojiunga na shule hizo za awali kutoka 896,146 mwaka 2009 hadi 925,465. Hili ni tatizo kwani tafiti zote zinaonyesha umuhimu wa elimu ya awali katika kumjengea mtoto msingi imari wa elimu katika ngazi zinazofuata. Vilevile, tafiti zimeonyesha kwa wazi kabisa umuhimu wa elimu ya awali katika makuzi bora na maendeleo endelevu ya watoto.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kuelewa umuhimu wa shule hizi za awali kwa maendeleo ya sekta ya elimu hapa nchini, hivyo basi ni bora shule hizi zikawekwa katika mfumo rasmi wa uendeshaji katika elimu ya msingi. Ni muhimu kabisa serikali ikaweka utaratibu rasmi wa kuhakikisha kuwa kila mtoto anapitia elimu ya awali kabla ya kujiunga na elimu ya msingi.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inashauri Serikali ijipange vizuri ili kila mtoto hapa nchini mwenye umri kati ya miaka 4 na 5 ahudhurie elimu ya awali kabla ya kujiunga na elimu ya msingi. Shule hizi au vituo hivi vya elimu ya awali vigharimiwe na serikali za mitaa, chini ya usimamizi wa Maafisa Watendaji wa serikali hizo, na kuongozwa na walimu wastaafu, hasa kina mama, ambao kwa ngazi hii wanafaa zaidi kuliko kina baba.

Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza hilo, Serikali inapaswa kujipanga vizuri ili kukabiliana na changamoto zilizopo. Kuna changamoto tatu; Ya kwanza ni uchache wa shule za awali zinazomilikiwa na Serikali.Ya pili ni upingufu wa walimu wenye taaluma ya mafunzo ya elimu ya awali, na changamoto ya, Tatu ni ukosefu wa vifaa vya kufundishia elimu ya awali (Picha/Michoro, vitabu vya kiada na ziada)

.
Mheshimiwa Spika, kutokana na takwimu zilizotolewa katika taarifa ya hali ya uchumi kwa mwaka 2010 kuwa kuna wanafunzi 883,667 katika shule za awali za Serikali 41,798. Hivyo basi, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa takwimu sahihi ya idadi ya waalimu halisi waliohitimu au ni wangapi ambao wapo wanaofundisha shule hizo za awali za Serikali na pia tunataka tuambiwe ni vyuo vingapi na ni vipi vinatoa mafunzo kwa waalimu wanaokwenda kufundisha katika shule hizo.

ELIMU YA MSINGI NA SEKONDARI

Mheshimiwa Spika, ni ukweli kabisa kuwa Serikali imerudisha jukumu la kuendesha na kusimamia elimu ya Msingi na Sekondari TAMISEMI. Hata hivyo rasilimali za kuendeleza elimu zimebakizwa Wizara ya Elimu. Kitendo hiki cha kugatua majukumu peke yake bila ya kugatua na rasilimali za utekelezaji wake zinakwamisha sana halmashauri zetu kutekeleza majukumu haya.

Mheshimiwa Spika, ili kukidhi matakwa ya elimu bora ni lazima kitengo cha ukaguzi wa elimu kwa ngazi zote, yaani elimu ya msingi na elimu ya sekondari kufanya kazi mara kwa mara. Kitendo cha kukiachia kitengo cha ukaguzi kutegemea mawasilisho ya makato ya ada ya shilingi mia tano kwa kila ada ya mwanafunzi kwa kila shule ni kukifanya kitengo cha ukaguzi kudumaa na kutokufanya kazi yake ipasavyo. Hii maana yake ni kwamba kwa zile shule ambazo hazitaweza kuwasilisha kiasi hicho cha pesa maana yake ni kwamba hazitaweza kukaguliwa.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali itenge bajeti kamilifu kwa kitengo hiki cha ukaguzi na ripoti yake iwe inafanyiwa kazi na vitengo husika ili kuweza kurekebisha kasoro zilizopo katika shule zetu.

Mheshimiwa Spika, wakati Waziri akijibu swali namba 66 hapa bungeni tarehe 14 februari 2011 alisema kwamba, nanukuu…. “Idara imeanzisha utaratibu wa ukaguzi wa shule kwa kuzingatia makundi ya ubora ambapo shule zilizo chini ya kiwango zitakaguliwa mara nyingi zaidi ili kuinua kiwango cha ubora. Vilevile Wizara katika utaratibu wake wa kuimarisha ukaguzi wa shule, imeandaa Mwongozo wa Usimamizi wa Shule kwa lengo la kuwawezesha Walimu Wakuu na Waratibu Elimu Kata kama Wakaguzi wa Ndani na wa karibu wa shule, kusimamia shule ili ziweze kujiletea maendeleo kwa kuzipatia msaada endelevu wa kitaalamu na kitaaluma”. Mwisho wa kunukuu

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaamini kabisa kuwa kazi ya ukaguzi haipaswi kufanywa na walimu wakuu wa shule, kwani hata mwalimu mkuu naye anatakiwa kukaguliwa, Je utaratibu upi utatumika? Na ifahamike kuwa huyu ndio msimamizi wa masuala ya shule hivi atakuwa tayari kujikosoa yeye mwenyewe?

Shule za Elimu ya Msingi.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani ina shauri Serikali kubadili mfumo wa elimu ya msingi ili iweze kujitosheleza kwa kuhakikisha kuwa wahitimu wanapata maarifa na stadi za maisha, zitakazowawezesha kujitegemea pindi watakapomaliza masomo yao na kukosa fursa za kujiendeleza zaidi kielimu.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani, inapendekeza maboresho yafuatayo ili kuweza kuinua na kuimarisha kiwango cha elimu ya msingi hapa nchini;
(i) Muda wa elimu ya shule ya msingi usogezwe kutoka miaka 7 ya sasa hadi kufikia miaka 9 au 10. Hii inamaanisha kuwa watoto watamaliza shule wakiwa na umri wa kati ya miaka 15 na 17, umri unaomwezesha kijana kukaribia sana kuanza maisha ya kazi, kwa mujibu wa sheria za nchi na sheria za kimataifa.Pia utaratibu huu utaenda sambamba na zoezi linaloendelea la Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhuisha mfumo wa mitaala kuweza kufanana na hivyo kuwa na elimu inayofanana na mpaka sasa ripoti ya awali imeshawasilishwa wizarani

.
(ii) Mtaala wa elimu ya msingi upanuliwe kwa kuingiza muhtasari wa kidato cha kwanza na cha pili cha sasa kuwa sehemu ya elimu ya msingi.
Aidha, katika upanuzi huu wa mtaala, fursa kwa vijana wengi kupata utaalam na stadi za kujitegemea mapema itazingatiwa, ikiwa ni pamoja na kuingiza katika mtaala huo, elimu ya uzazi na mahusiano, kuwiana na umri wa mwanafunzi na utawapatia vijana wa kike stadi za kuweza kujikinga na tatizo la kuanza ngono katika umri mdogo, na hivyo kupunguza au kumaliza kabisa tatizo la mimba za utotoni.

(iii) Ujenzi upya, uboreshaji na ukarabati wa shule zote za msingi nchini, kwani shule nyingi katika ngazi ya elimu ya msingi hazina vyumba vya madarasa vya kutosha, na zile ambazo zina vyumba vya madarasa vya kutosha, viko kwenye hali mbaya na hii inatokana na shule hizi kujengwa muda mrefu.Uboreshaji huu wa vyumba vya madarasa utakwenda sambamba na uchongaji wa madawati ya kutosha, ili kuondokana na utegemezi kwa wahisani kuzipatia madawati shule zetu za elimu ya msingi, ambalo linapaswa kuwa jukumu la serikali.

(iv) Uchimbaji wa matundu ya kutosha na ujenzi wa vyoo vya kisasa, hii itasaidia katika kulinda afya za watoto wetu, kwani hali ilivyo sasa shule nyingi za elimu ya msingi hazina vyoo vya kutosha, na zingine hazina kabisa huduma hii.

(v) Utoaji wa chakula cha mchana mashuleni, ili kukabiliana na wimbi la utoro na usinziaji darasani kwa sababu ya njaa miongoni mwa watoto wa shule, wizara irudishe huduma hii muhimu iliyokuwepo hapo zamani wakati wa Mwalimu Nyerere, na huduma hii igharimiwe na Halmashauri za Majiji, Miji na wilaya, kwani mtoto mwenye njaa, au asiye na uhakika wa lishe, hawezi kuambulia chochote darasani kimasomo. Kama alivyosema mwanazuoni maarufu Plato, kuwa akili yenye afya iko katika mwili wenye afya

.
b) Elimu ya Sekondari

.
Mheshimiwa Spika, Elimu ya Sekondari hutolewa katika ngazi mbili tofauti na hadi tarehe 30 Juni, 2011, jumla ya shule zote za Sekondari nchini zilikuwa 4,266. Kati ya hizo, shule 3,397 ni za serikali (3,308 za wananchi za kutwa, 89 ni shule kongwe za serikali) na 869 ni shule zisizo za serikali. Jumla ya wanafunzi katika shule za sekondari za serikali na zisizo za serikali nchini ni 1,638,699. Wanafunzi wa kidato cha 1 – kidato cha 4 ni 1,566,685 (wasichana 699,951).

Mheshimiwa Spika, Wanafunzi wa kidato cha 5 na 6 ni 72,014. Idadi hii ya wanafunzi waliopo shuleni ni kielelezo dhahiri kuwa kuna tatizo kubwa na la kimsingi, hasa kwenye mfumo wetu wa Elimu ya sekondari na haswa ikizingatiwa kuwa kuna ufinyu wa nafasi za kujiunga na elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi ambapo idadi ya wahitimu wa elimu ya msingi na sekondari kwa mwaka ni 639,700 wakati nafasi za mafunzo ya ufundi na ufundi stadi ni 84,000 tu.

Kambi ya Upinzani tunahoji vijana wanaomaliza kidato cha nne wanaenda wapi kwani ni wachache sana wanaopata fursa ya kwenda kidato cha tano, na ikizingatiwa kuwa tuna upungufu mkubwa sana wa Vyuo vya ufundi hapa nchini. Tunataka maelezo ya kina kuhusiana na suala hili na mpango mathubuti wa kukabiliana na hali hii.

Mheshimiwa Spika,Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005-2010 na ya mwaka 2010-2015 ilitamka wazi kuwa serikali itajenga vyuo vya VETA kwa kila Wilaya nchini .Jambo la kushangaza ni kuwa ahadi hii mpaka leo bado haijatekelezwa na badala yake wananchi wanaendelea kupewa ahadi hewa .
Kwa mwaka huu wa fedha kwenye kitabu cha bajeti ya serikali kitabu cha Maendeleo volume iv fungu 1003 kasma 4397 serikali imetenga shilingi 100,000,000 kwa ajili ya kuisaidia VETA kiwango ambacho ni kidogo zaidi mara tano ya fedha zilizotengwa mwaka jana.

Kambi ya Upinzani , inataka majibu kutoka serikalini je? Kutenga kiasi kidogo cha fedha za maendeleo kwa ajili ya VETA kitaweza kweli kujenga vyuo hivyo kila wilaya kama ambavyo serikali imekuwa ikiwaahidi wananchi?

Mheshimiwa Spika, kiwango cha ufaulu katika mitihani ya Kidato cha 4 mwaka 2010, idadi kubwa ya wanafunzi waliopata daraja la I – III ilishuka sana kwani kati ya watahiniwa 38,781 waliopata daraja la I-III katika mitihani ya Kidato cha 4 mwaka 2010, wanafunzi 19,126 wanatoka Shule za Sekondari za Kutwa. Aidha, wanafunzi 3,697 wametoka katika shule kongwe za sekondari za serikali na 15,958 wanatoka katika shule za sekondari zisizo za serikali.Takwimu zinaonyesha kushuka kwa ufaulu wa kidato cha nne kutoka asilimia 72.5 mwaka 2009 hadi 50.2 mwaka 2010.Kiwango cha kufeli kwa wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne ni hatari kwani kinaongeza tatizo juu ya tatizo la ajira. Kama asilimia zaidi ya 80% ya watahiniwa wote wanapata madaraja ya IV na 0, hii inamaanisha kuwa kundi hili ni kundi ambalo litakuwa haliajiriki. Kwa hiyo mfumo wetu wa elimu unazalisha watu ambao huko mbele hawawezi kuajirika kwa sababu watakuwa hawana maarifa na weledi wa msingi katika kuweza kujitegemea na kuajirika. Lazima hatua makini na za haraka zichukuliwe.

Mheshimiwa Spika ,Sababu za wanafunzi kufanya vibaya katika mitihani zinajulikana. Moja ya sababu za msingi, kwa mujibu wa tafiti za hivi karibuni kabisa, ni walimu kukataa tamaa na menejimenti mbovu za shule, na hasa katika shule za umma. Katika miaka ya karibuni serikali imewekeza fedha nyingi sana katima elimu ya sekondari kupitia mpango maalumu wa elimu ya sekondari (MMES I na II). Lakini, kwa mshangao mkubwa, katika maeneo 39 yanayolengwa kuboreshwa katika MMES II, ni maeneo mawili pekee yanayowalenga walimu kwa mbali. Aidha, katika utafiti wa hivi karibuni uliwahusisha walimu katika mikoa mbalimbali hapa nchini, ni asilimia 15.3 pekee waliohojiwa ndio walisema kuwa wamewahi kuhudhuria mafunzo kazini katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Mheshimiwa Spika, Tafiti pia zinaonyesha kuwa maslahi na mazingira ya kazi ya walimu ni magumu na duni zaidi kuliko wafanyakazi wote katika sekta ya uma hapa nchini, japokuwa wao ndio wamesoma zaidi kuliko kada nyingi hapa nchini. Haya ni mambo ambayo yanawakatisha tamaa walimu na kuacha kufanya kazi yao ipasavyo. Tafizi zimehitimisha kuwa tatizo la walimu Tanzania sio uhaba au upungufu wa walimu. Tatizo la msingi ni kukataa tamaa kwa walimu kulikotokana na kada ya ualimu kutelekezwa na kudharauliwa na waliokabidhiwa dhamana ya kuendesha sekta ya elimu.

Mheshimiwa Spika,Kwa mujibu wa taarifa za serikali ni kuwa hadi Juni, 2011, jumla ya shule zote za sekondari nchini zilikuwa 4,266. Kati ya hizo, shule 3,397 ni za serikali (3,308 kutwa, 89 ni shule kongwe za serikali) na 869 ni shule zisizo za serikali.Takwimu hizi maana yake ni kuwa kiwango cha ufaulu kwenye sekondari za kata ni sawa na kusema kuwa shule hizi zimefaulisha kwa wastani wa kila shule ni wanafunzi 6 tuu waliopata daraja la 1-III ,wakati shule kongwe zimefaulisha wastani wa wanafunzi 42 waliopata daraja la 1-III na shule za binafsi zimefaulisha wastani wa wanafunzi 18 kwa kila shule .

Mheshimiwa Spika, jambo lingine la msingi katika kuinua kiwango cha elimu ni upanuzi na uboreshaji wa mabweni ya wanafunzi. Tafiti zinaonyesha umuhimu wa kuwa na shule za Bweni kwani wanafunzi wanapata muda wa kutosha kusoma na pia kuwa na maeneo ya kusomea badala ya hali ilivyo kwa wanafunzi wa kutwa ambao wengi wao majumbani kwao wanakuwa na majukumu makubwa sana ya kazi mbalimabli.Kambi ya Upinzani, inahoji yapo wapi mafanikio ya shule za kata ambayo kila siku serikali imekuwa ikiyasifia hapa bungeni?

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inapendekeza kuwa mfumo wa elimu ya sekondari ufanyiwe mabadiliko kutoka miaka 6 ya sasa kuwa miaka 4, kwa kuunganisha mitaala ya vidato vya tatu, nne, tano na sita kuwa mtaala mmoja wa elimu ya sekondari. Hii itasaidia sana kuongeza idadi ya wanafunzi wanaopata sifa za kujiunga na elimu ya sekondari na, pamoja na badiliko hilo la msingi, wizara itilie mkazo mambo yafuatayo:

(i) Uimarishwaji wa ufundishaji wa lugha ya Kiingereza. Hili lifanywe kwa kuboresha mazingira mazuri ya kujifunzia lugha ya Kiingereza, ikiwemo kuzipatia shule walimu wenye ujuzi wa kufundisha lugha hiyo. Hii lengo lake ni kuhakikisha mwanafunzi anapoingia kidato cha pili anaifahamu vizuri lugha ya Kiingereza katika kuelewa, kuandika, kuongea na kujieleza. Kadhalika,Serikali ianzishe Taasisi ya kufundisha lugha za kigeni, ambapo lugha za Kiingereza, Kifaransa, Kijerumani,Kichina, Kijapani,Kiarabu, Kihindi na nyinginezo zitafundishwa kwa viwango vya kati na juu.

(ii) Uimarishwaji wa ufundishaji wa lugha ya Kiswahili. Pamoja na kutilia mkazo ufundishaji wa lugha za kigeni, wizara iweke msisitizo wa pekee katika kuifahamu lugha ya Kiswahili sanifu. Wanafunzi Watanzania ni lazima waimudu lugha yao ya taifa bila kujiona duni kwa kufanya hivyo, waweze kupambanua Kiswahili cha mtaani na Kiswahili sanifu, wakati huo huo wakijiimarisha katika lugha za kigeni. Kambi ya Upinzani inaamini kwamba wanafunzi wetu wanaweza kumudu vizuri lugha nyingi kwa kiwango kile kile, bila kuathiri kwa namna yoyote uzalendo wao kwa taifa letu.

(iii) Uimarishwaji wa ufundishaji wa masomo ya Sayansi na Hisabati. Katika kufanikisha azma hii wizara izingatie maandalizi ya walimu wa masomo haya kwa uhakika, ujenzi wa maabara za masomo haya na kuziwekea vifaa na nyenzo zote za msingi za kufundishia masomo haya, pamoja na kemikali zinazohitajika. Kuhusu somo la elimu viumbe, shule ziweke utaratibu wa kufuga wanyama wadogo wadogo na kutunza mimea ya aina mbali mbali kwa ajili ya kufundishia na kujifunzia.

Mheshimiwa Spika, katika fani hii ya masomo ya Sayansi, na hasa Hisabati, mbali na jitihada za makusudi za kuhamasisha wanafunzi wa kike kupenda kuchukua masomo haya, wizara iboreshe ufundishaji wake uendane na misingi yake ambayo inazingatia sayansi ya mantiki inayojengeka hatua kwa hatua, ili kuwavutia wasichana wengi, lakini pia kuinua kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wote kwa jumla, ili kuondokana na tatizo la kukaririshwa ambalo hupelekea kutofanya vizuri katika somo la Hisabati.

(iv) ) Uhimizwaji wa ufundishaji wa stadi za maisha na TEKNOHAMA, kwa kuhakikisha kuwa matumizi ya teknolojia ya kisasa yanaanza mapema kwa wanafunzi wetu, ili wafikie kwenye kiwango cha kimataifa cha elimu na ujuzi, mapema inavyowezekana. Aidha serikali itoe kauli ya kuhakikisha uendelevu wa mpango wa Elimu kwa Teknolojia ya Simu unaotekelezwa na Wizara kupitia mradi wa Bridge-It Tanzania katika shule mbalimbali baada ya kuisha kwa mchango wa wahisani.

(v) Ujenzi wa makusudi wa “utaifa” kwa Watanzania. Serikali ianzishe shule mpya za kitaifa za bweni za sekondari na shule hizi zichukue wanafunzi wote waliofanya vizuri zaidi katika mitihani yao ya mwisho ya elimu ya msingi kutoka sehemu zote za Tanzania. Katika kila mkoa kujengwe angalau shule moja ya kitaifa, itakayochukua wanafunzi kutoka katika mikoa mingine, kwa lengo la kujenga “utaifa” na “uzalendo” miongoni mwa wanafunzi.

(vii) Serikali irejeshe utaratibu wa usafiri wa “warrant” kwa wanafunzi. Ili kuondoa makali ya gharama za nauli kwa wazazi. Ni wazi kuwa utaratibu huu ni aghali, lakini Kambi ya Upinzani inaamini kuua “utaifa” ni aghali zaidi.

c) Elimu ya Juu na Vyuo VikuuMheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inashauri kubadilisha na kuboresha sekta ya elimu ya juu, ili iweze kuwa ya kisasa zaidi, na kumuandaa msomi wa Tanzania kushiriki katika kutumia elimu yake kuiletea Tanzania maendeleo, na vile vile kumpatia nyenzo za kisasa za kielimu zinazoendana na ulimwengu wa kisasa. Lengo hasa la dhamira hii ni kuhakikisha kuwa elimu ya juu inapatikana kwa kila mtanzania anayeitamani, na mwenye uwezo kiakili wa kuipata elimu hiyo, itakayokuwa ya kisasa, na mwenye nia ya dhati ya kutoa mchango wake kuliendeleza taifa letu, ikiwa ni njia ya kuirudishia jamii ujuzi atakaoupata huko chuoni.

Mheshimiwa Spika, katika kupanua wigo na kuboresha elimu ya juu nchini Kambi ya Upinzani inaitaka serikali kuchukua hatua zifuatazo:

(i) Kuanzisha mfuko wa elimu ya Juu “Uhuru Scholarship Fund” kwa ajili ya kugharimia masomo katika vyuo vikuu vya umma, kuhusu wanafunzi wanaofaulu kwa viwango vya Daraja la I na la II wasichana. Hawa hawatachukua mikopo, Badala yake wanafunzi hawa watalipiwa gharama zote kadri wanavyofaulu, na kupanda, kuelekea viwango vya juu vya taaluma zao, kwa muda wote watakaokuwa vyuoni.

(ii) Kuweka mfumo mpya wa kugharimia elimu ya juu kwa ajili ya wale watakaofaulu kwa viwango vya Daraja la III na la IV. Mfumo huu mpya uwekwe ili kuhakikisha kuwa gharama za elimu ya juu hazimkwazi mwanafunzi yeyote anayeitamani, na mwenye uwezo kiakili kuipata elimu ya Chuo Kikuu. Katika kutimiza azma ya uwekaji wa mfumo huu, Serikali ihakikishe kuwa kila Mkoa unaanzisha mfuko wa Elimu ya Juu, taasisi za dini na watu binafsi wahamasishwe kwa lengo hilo, na kuwekewa utaratibu wa kisheria, ili waweze kuanzisha mifuko ya elimu inayogharimia mafunzo hayo na kamwe isiwe mikopo, kwa ajili ya wanafunzi wa vyuo vikuu, kwa kuzingatia vigezo mahususi.

(iii)Kuvunja Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Mheshimiwa Spika, kutokana na muundo wake, uendeshaji mbaya, na mfumo wake mbovu kisheria, uongozi wa bodi hii ya mikopo ya elimu ya juu umeshindwa kuifanya elimu ya juu ipatikane kwa kila mwanafunzi anayeistahili. Aidha, bodi hii kutokana na uongozi usiofaa, imeshindwa kusimamia marejesho ya madeni kutoka kwa wanafunzi waliowahi kukopeshwa na hii inatokana na ukweli kuwa bodi iliyopo ilitoa mikopo kwa wanafunzi 91,568 wakiwemo 23,141 wanaochukua masomo ya sayansi. Aidha, ilifanikiwa kukusanya marejesho ya mikopo yenye thamani ya Sh. Bilioni 7.9 kati ya Sh. bilioni 21 zilizo tayari kukusanywa.

Mheshimiwa Spika, Kutokana na sababu hizo,serikali iazimie kuivunja bodi hii, pamoja na kufanya uchunguzi huru wa fedha zote zilizotumika chini ya bodi hii hadi hivi sasa na kujiridhisha kama waliopewa dhamana hii hawakutumia nafasi zao kujinufahisha binafsi, baada ya huu kukamilika ripoti iwekwe wazi kwa umma, na mapendekezo yake yafanyiwe kazi mara moja.

(iv) Kuundwa kwa chombo kipya cha kutoa na kusimamia mikopo ya Elimu ya Juu
Mheshimiwa Spika, baada ya bodi ya sasa ya mikopo ya elimu ya juu kuvunjwa, Serikali iunde chombo kipya kitakachojulikana kama Mamlaka ya Taifa ya Kugharimia Elimu ya Juu (Tanzania Higher Education Financing Authority – TAHEFA). Hiki ndicho kitakuwa chombo cha kifedha ambacho kitachukua majukumu yote ya bodi ya mikopo ya sasa, chini ya muundo mpya na sheria mpya, ambayo itaweka utaratibu mpya na wa kisasa wa utoaji wa mikopo ya elimu ya juu, ili kuhakikisha kwamba hakuna mwanafunzi anayeitamani na mwenye uwezo kiakili wa kuipata elimu ya juu, atakayeikosa.

(v) Uhuru wa Vyuo Vikuu Kujiendesha.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa fursa kwa vyuo vikuu kujiendesha kiutawala, na kitaaluma, bila kuingiliwa na serikali. Hii iwe ni pamoja na uhuru wa kujichagulia viongozi wao, na chini ya utaratibu huu, jukumu la wizara litakuwa ni kutunga sera za jumla za kuendeleza na kuilinda elimu ya juu, kwa kuzingatia umuhimu wa upatikanaji wa rasilimaliwatu iliyo bora, ingawa uendeshaji wa vyuo vikuu vyenyewe utaachwa mikononi mwa mabaraza ya vyuo hivyo.Na hii itakuwa ni kulitekeleza azimio la kitaaluma ambalo tulilisaini mwaka 1990 (Declaration on Academic Freedom). Aidha kambi rasmi ya upinzani imebaini kwamba vipo vifungu vya kanuni ya vyama vya wanafunzi vyuo vikuu (Universities students orginzation regulations, 2009) ambavyo vinaingilia uhuru na haki za msingi za kikatiba na kisheria hivyo serikali irekebishe kanuni husika kwa kupata ushauri wa kamati ya bunge ya sheria ndogo.

(vi) Ushiriki wa Wanafunzi katika Shughuli za Siasa.

Mheshimiwa Spika, Hii itasaidia kujenga uwanja wa demokrasia katika serikali za vyuo, na vile vile kuweka mazingira ambayo yatawawezesha wasomi wetu kuanza kujifunza mbinu na utendaji wa kisiasa katika mazingira ya elimu, ili waweze kujifunza kuishi pamoja, kupingana kwa hoja, na kujua jinsi ya kuvumiliana katika mazingira mbalimbali yenye tofauti za kiitikadi, imani, na mitizamo. Bila kuimarisha misingi ya demokrasia katika ngazi za taasisi za elimu hatuwezi kujenga Taifa linalopenda na kuheshimu misingi ya demokrasia na utawala bora. Kupiga marufuku ushiriki wa vijana wa elimu ya juu katika shughuli za kisiasa ni umbumbu wa elimu ya siasa kunakotokana na mazoea ya kukulia katika mfumo wa kiimla na hodhi.

(vii) Baraza la Taifa la Utafiti – ‘National Research Council’.

Mheshimiwa Spika, ili kuchochea ubunifu na kuvishirikisha Vyuo Vikuu vyetu kwenye nyanja za kimataifa, Serikali iimarishe Tume ya Sayansi na Teknolojia ambayo itaratibu na kusimamia tafiti mbalimbali za kisayansi na teknolojia; sera na sheria viboreshwe ili tume iweze kufanya kazi kwa ufanisi.

Mheshimiwa Spika, Majukumu mengine ya Tume hii yawe ni kuanzisha na kusimamia mashindano ya changamoto za kisayansi, ili kuchochea utafiti na ubunifu. Kwa usimamizi wa Tume hii, zawadi nono ya fedha taslimu itakuwa ikitolewa kila mwaka, kwa Chuo Kikuu na wabunifu mbalimbali wa vitu ambavyo havijabuniwa sehemu nyingine duniani. Katika kuunda Baraza hili baadhi ya taasisi mbalimbali zilizopo nchini zitaunganishwa na kuwekwa chini yake, ingawa zitaendelea kuwa huru kiutendaji, huku zikishirikiana na kutegemeana katika kuendesha tafiti zake, na kusimamia matumizi ya matokeo ya tafiti hizo.

(viii) Kuanzishwa kwa Vyuo Vikuu Vipya.

Mheshimiwa Spika, ili kuchochea kasi ya ukuaji wa sayansi na teknolojia nchini, Serikali sasa ivipandishe hadhi vyuo viwili vilivyopo na kuwa na hadhi ya kutoa shahada, navyo ni kimoja kilichoko Mbeya na kingine kilichoko Tanga. Vyuo hivyo ni Mbeya Institute of Science and Technology, ambacho kitabadilishwa kuwa Mbeya University of Science and Technology –MUST, na Chuo cha Ufundi Tanga, ambacho kitabadilishwa kuwa Chuo Kishiriki cha MUST.

(ix) Kuanzishwa kwa Vyuo vya Kati vya Jamii.

Mheshimiwa Spika, Pamoja na kuendelea kutoa elimu ya kiwango cha shahada ya chuo kikuu, utaratibu wa kuwa na Vyuo vya Kati vya Jamii – ‘Community Colleges’, ambavyo vitatoa elimu sawa na inayotolewa katika semista tatu za kwanza za chuo kikuu ni wa muhimu sana. Madhumuni ya kuanzisha vyuo hivi ni kuanza kutengeneza kundi la wasomi wa elimu ya kati, ambao kutokana na sababu mbalimbali, wasingeweza kupata elimu kamili ya Chuo Kikuu. Vyuo hivi vya jamii vitakuwa ni kiunganishi kati ya elimu ya sekondari na elimu ya Chuo Kikuu na vitakuwa na uwezo wa kutoa Shahada Shiriki.. Mhitimu wa vyuo hivyo akitaka baadaye anaweza kuendelea na elimu ya Chuo Kikuu katika taaluma yake, kwa kuendeleza pale alipoachia na siyo kudahiliwa na kuanza masomo kama mwanafunzi wa mwaka wa kwanza. Ili kufanikisha azma hii, baadhi ya vyuo vya jamii vilivyopo sasa, vipandishwe ngazi na kubadilishwa kuwa Vyuo vya Kati vya Jamii.

(x) Kuinua ari ya Wahadhiri wa Vyuo Vikuu

Mheshimiwa Spika, Ili kuhuisha ari ya utumishi miongoni mwa wahadhiri wa Vyuo Vikuu, Serikali ihakikishe kuwa katika bajeti yake madeni yote ya wanataaluma, ya posho ya pango kwa wanaostahili yanalipwa, na mpango wa kuboresha mafao ya wahadhiri ya uzeeni unatekelezwa kikamilifu. Lengo la azma hii ni kuwaondolea hofu ya maisha yao ya kila siku wanataaluma wetu ili waweze kujikita kweli katika kutoa elimu, kufanya utafiti kwa utulivu, na kutoa ushauri wa kitaalam ipasavyo

.
(xi) Kuongeza Muda wa Utumishi kwa Wanataaluma.

Mheshimiwa Spika, ili kuendelea kufaidika na utaalam na uzoefu wa maprofesa wetu hapa nchini, katika kuwanoa vijana wetu wa vyuo vikuu, tunashauri kuwa Serikali iangalie utaratibu wa kuanzisha majadiliano na wanataaluma, pamoja na mabaraza ya vyuo na seneti zao, kuangalia uwezekano wa kuongeza umri wa maprofesa kustaafu, kutoka miaka 60 ya sasa hadi 70, maadamu chuo husika kimejiridhisha kuwa Profesa husika bado utaalam wake anautumia kikamilifu na unahitajika kwa wakati huo.

USHIRIKIANO NA NCHI MBALIMBALI KWENYE ELIMU YA JUU

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2010/2011 serikali ilitekeleza utaratibu wa kubadilishana wanafunzi kati ya Tanzania na Msumbiji, na Tanzania na Uganda, ambapo wanafunzi watanzania 68 wanasoma Uganda na 29 wanasoma Msumbiji.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka huo huo wa fedha Serikali iliwawezesha wanafunzi 5 raia wa China kusomea kozi ya muda mfupi ya lugha ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam chini ya utaratibu wa skolashipu zinazotolewa na Serikali ya Tanzania kwa Serikali ya China katika kutekeleza mkataba wa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya China.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka huohuo wa fedha serikali ilipokea na kuratibu nafasi 132 kutoka Uingereza (12), China (72), Korea ya Kusini (2), India (20), New-Zealand (2), Urusi (15), Misri (5) na Cuba (4).

Kambi ya Upinzani inataka kujua ni vigezo/utaratibu gani huwa unatumiwa na wizara katika kuwapatia wanafunzi nafasi za kwenda kusoma nje ya nchi. Hii inatokana na ukweli kuwa yamekuwapo malalamiko mengi kutoka kwa wanafunzi mbalimbali kuwa kuna upendeleo wa wazi katika kushughulikia nafasi za wanafunzi kwenda nje ya nchi. Ni chombo gani kinahusika katika kuteua wanafunzi hawa ?

UPUNGUFU WA WALIMU KATIKA SEKONDARI ZA SERIKALI

Mheshimiwa Spika, hakuna asiyefahamu kwamba sekondari zetu hususani za kata zinakabiliwa na upungufu mkubwa wa walimu ambao wamehitimu katika ngazi ya stashahada na shahada. Tatizo hili linawafanya walimu wachache waliopo kufanya kazi katika mazingira magumu sana ikiwepo kufundisha masomo ambayo hawakusomea na kufundisha idadi kubwa ya wanafunzi bila kufuatilia “performance” ya mwanafunzi mmoja mmoja.

Kambi rasmi ya upinzani, inaona umefika sasa wakati wa serikali kuingia mkataba wa lazima wa miaka mitano kwa wanafunzi wanaosomea kozi ya ualimu na wanaopata mkopo kutoka bodi ya mikopo, kwa kuwapangia wanafunzi wanaomaliza shahada zao kwenda kufundisha katika shule za serikali. Mkataba huu uwe unasainiwa pindi mwanafunzi anapodahiliwa na masharti yawekewe kwamba pindi mwanafunzi anapohitimu ni lazima afundishe katika sekondari za serikali na atakapoacha kwenda hufundisha huko basi sheria imbane arudishe mkopo aliopewa na serikali mara moja.
Na kama hafanyi hivyo sheria ichukue mkondo wake. Nachelea kusema kwamba, pendekezo hili lisichanganywe na ile sheria ya utumishi ya kufanya kazi kwa miaka miwili kwa mtumishi yeyote kabla ya kuthibitishwa yaani “probantion period” maana hii inahusu kada zote za ajira na si mkataba wa makusudi kama nilivyouelezea hapo juu.

Mheshimiwa spika, pamoja na kupunguza uhaba wa walimu kwa kiasi kikubwa, njia hii itasaidia kuwabana wakopaji wote kuweza kurudisha mkopo kwa wakati na kuwapa nafasi na wahitaji wengine kunufaika na mkopo huu wa elimu ya juu. Sambamba na hili, serikali iweke mazingira mazuri ya kufundishia kwa walimu ikiwepo kuwajengea nyumba bora za kuishi na kuboresha maslahi yao ili wasipate tamaa ya kumezwa na soko la ajira na wao kukimbilia kufundisha shule za binafsi.

MIGOMO NA MAANDAMANO VYUO VIKUU NA UHURU WA KITAALUMA

Mheshimiwa Spika,Wanafunzi wa vyuo vikuu hapa Nchini wamekuwa wakiandamana kutokana na sababu mbalimbali na hasa kubwa ni kutokana na serikali kutowatendea haki na hili linaendana na ama kucheleweshewa fedha zao za mkopo na wengine kunyimwa fedha kwa ajili ya kwenda kufanya mafunzo kwa vitendo kama sehemu ya masomo yao.Pindi wanafunzi hawa wanapogoma ama kuandamana wamekuwa wakipigwa na wengine kuumizwa na jeshi la polisi na baadhi yao kuishia kufukuzwa vyuoni na au kusimamishwa masomo kama ambavyo imetokea katika Vyuo Vikuu vya Dodoma, Dar Es Salaam, Muhimbili, chuo cha Ardhi na vinginevyo vingi hapa nchini.

Mheshimiwa Spika,Historia ya Maandamano hapa nchini inaonyesha kuwa yalianza tangu kipindi kirefu kilichopita cha uongozi wa awamu ya kwanza na hata viongozi mbalimbali wa wanafunzi wakiwemo wengine ambao ni mawaziri humu bungeni walishiriki kikamilifu maandamano na migomo hiyo na hata kufikia wengine kuathibiwa na Hayati baba wa Taifa wakati wa urais wake .Hivyo sio sahihi hata kidogo kufikiri kuwa wanafunzi wa vyuo vikuu ambao wanagoma na kuandamana hapa nchini basi kuna msukumo wa kisiasa kama ambavyo wanataka taifa liamini kwani lilikuwepo tangu wakati wa chama kimoja .Suluhisho pekee ni kuondoa matatizo kwenye vyuo vyetu ili wanafunzi waweze kusoma bila matatizo kama ambavyo hali ipo hivi sasa.

Mheshimiwa spika , kwa mujibu wa kanuni ya mwaka 2009 iliyotangazwa kwenye gazeti la serikali namba 178 la tarehe 12/06/2009 inayojulikana kama Kanuni ya vyama vya wanafunzi vyuo vikuu (Universities students organization regulations ,2009) pamoja na mambo mengine kanuni hizo zimeelezea kwenye kifungu cha 14 juu ya haki za wanafunzi kufanya mambo yafuatayo:
a) Kukusanyika (assemble)
b) Kuandamana (demonstrate)
c) Kutoa maoni yao (express their opinions)

Mheshimiwa Spika, Pamoja na serikali yenyewe kutoa haki hizi kwa wanafunzi lakini la kusikitisha ni kuwa pindi wanafunzi hawa wanapokuwa wanaandamana kama njia ya kuweza kutoa maoni yao na kama ambavyo kanuni zimewapa haki hizo , bado serikali kwa kutumia jeshi la polisi wamekuwa wakiwapiga vijana hawa na hata wengine kuumizwa vibaya kama ilivyotokea hapa Dodoma kitendo kilichopeleka mwanafunzi mmoja anayeitwa Malumbu Ngata kuvunjwa mguu wa kulia na kulazwa Dodoma General Hospital (Ward 11 kitanda na.3) kutokana na kipigo cha polisi .

Mheshimiwa Spika, Hali ya polisi kuwapiga wanafunzi sasa imeenda mpaka kufikia ngazi za shule za sekondari kwani ni hivi majuzi tuu polisi waliwafyatulia risasi za moto wanafunzi wa shule ya sekondari ya Mbezi iliyopo jijini Dar Es Salaam na kupelekea wanafunzi wengi kuumia vibaya na kulazwa katika hospitali ya taifa ya Muhimbili, wakati walipokuwa wakidai haki zao za msingi.

Mheshimiwa Spika, Hali hii ni ya hatari kwa vijana wetu kwani kama imefikia mahali pa kuwafyatulia risasi za moto wanafunzi ambao hawana silaha yeyote na serikali imeendelea kukaa kimya bila kuchukua hatua zozote dhidi ya wanaofanya vitendo hivyo ni kitu ambacho hakikubaliki.

Kambi ya Upinzani, tunaitaka serikali itoe maelezo kuhusiana na mambo yafuatayo;i) Ni hatua gani serikali imechukua mpaka sasa dhidi ya wale wote ambao wanasababisha majeruhi kwa kuwapiga wanafunzi kinyume cha sheria kama ambavyo kanuni tajwa hapo juu zinawapa haki ya kuandamana?ii) Je? Serikali inatoa kauli gani kuhusu wanafunzi ambao wamesimamishwa masomo kutokana na kutumia haki yao ya kisheria ya kuandamana na ni lini watarejeshwa vyuoni kwa ajili ya kuendelea na masomo.iii) Je? Ni kesi ngapi ambazo mpaka sasa zinawakabili wanafunzi wa Vyuo na wa Sekondari kwa kuandamana na zipo Mahakama gani?iv) Ni hatua gani zimechukuliwa dhidi ya wale wote ambao wanasababisha kutokea kwa migomo hii vyuoni kwani mara nyingi watawala vyuoni wamekuwa wakihusishwa kutokana na kushindwa kutatua matatizo mbalimbali ndani ya vyuo husika.v) Je? Ofisi ya waziri mkuu imechukua hatua gani dhidi ya utawala wa Chuo Kikuu cha Dodoma baada ya Waziri Mkuu kuunda Tume kuchunguza malalamiko ya wanafunzi dhidi ya Mkuu wa Utawala wa Chuo hicho na vingine vingi nchini.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inasisitiza kuwa ni haki ya kikatiba ya wanafunzi kuandamana na kutoa maoni yao na kamwe hatutakaa kimya pindi haki za wanafunzi zinapokuwa zinavunjwa na vyombo vya serikali na vijana wetu kuendelea kuumizwa .

Kambi ya Upinzani tutalisimamia tamko la Ulimwengu la uhuru wa kitaaluma “the Declaration on Academic Freedom and Social Responsibility of Academics” ambalo Tanzania tulisaini mnamo tarehe 19 Aprili 1990. Kwani tunaamini kuwa taifa haliwezi kuendelea kamwe kama wanataaluma wake wananyanyaswa na kukosa uhuru wa kutoa maoni yao kwa uwazi na bila kipingamizi chochote.

Mheshimiwa Spika, Itakumbukwa kuwa Serikali iliunda Tume ya Prof.Maboko kwa ajili ya kuchunguza chanzo cha migogoro na migomo kwenye vyuo mbalimbali hapa nchini na Tume hizi ni muendelezo wa Tume nyingi ambazo ziliwahi kuundwa kwa miaka nenda rudi na kila mara tume hizi huja na majibu yanayoshabihiana kuhusiana na vyanzo vya migogoro na hatimaye migomo na maandamano kwenye Vyuo vya Elimu ya Juu hapa nchini.

Kambi ya Upinzani, tunataka kujua ni lini mapendekezo ya Tume ya Prof. Maboko yatawekwa hadharani kuhusiana na vyanzo vya migogoro hii na migomo kwenye vyuo vikuu ili matatizo hayo yaweze kutafutiwa ufumbuzi na hatimaye visingizio bandia vya vyanzo vya migomo na maandamano vyuo vikuu viweze kuachwa .

MKAKATI WA KUHAMASISHA WATANZANIA KUJISOMEA

Mheshimiwa Spika, taifa letu limekuwa likishuhudia kushuka kwa viwango vya ufaulu wa mitihani mwaka hadi mwaka, katika ngazi za elimu ya msingi na elimu ya Sekondari. Pamoja na mambo mengine, mtizamo wa Kambi ya Upinzani kuhusu hili ni kwamba hali hii inasababishwa kwa kiasi kikubwa na kukosekana kwa vifaa , waalimu,vitabu vya kiada na ziada ,maabara,motisha kwa waalimu, kiwango kidogo cha watoto kupenda kusoma, na kutokuwepo kwa utamaduni wa kusoma vitabu miongoni mwa watanzania kwa jumla.

Mheshimiwa Spika, hii ni changamoto kubwa kwa taifa letu, changamoto ya kujenga tabia za watoto wetu kupenda kusoma, na kwa njia hiyo hatimaye kukuza utamaduni huo miongoni wa watanzania, hatuna budi kuwafanya watoto wetu wapende kusoma na kuwafundisha kupenda vitabu tangu wanapokuwa wadogo.

Mheshimiwa Spika, Ziko faida nyingi za kumfanya mtoto apende vitabu. Mbali na kumjengea tabia ya kupenda elimu, kwa watoto walio wengi, kusoma kwa kujifurahisha kunaweza pia kuwaepusha na tabia nyingine ambazo huharibu watoto, kama vile kucheza michezo isiyo na maana kwenye kompyuta, ama kuangalia programu za hovyo kwenye runinga.

Mheshimiwa Spika, kama taifa tunapaswa kuandaa mkakati wa kuhamasisha wazazi kuwafundisha watoto wao kupenda vitabu tangu wakiwa wadogo. Ili mkakati huu uweze kufanikiwa lazima ianzishwe kampeni maalum ya kitaifa katika kumshirikisha kila mzazi, kwani ni sehemu muhimu sana ya malezi ya mtoto. Kila mzazi hana budi kufahamu ni vitu gani ambavyo mtoto wake anavipenda, na vipi anavichukia, ili kubaini aina ya vitabu ambavyo vitamfurahisha, na kwa njia hiyo, kumvuta na kumwingiza kwenye ulimwengu wa kusoma.

Mheshimiwa Spika, wengi wetu tuna mazoea ya kuwafanyia sherehe watoto wetu, kuadhimisha kumbukumbu za siku zao za kuzaliwa, na huwa tunawanunulia zawadi. Mzazi akisha baini kitabu anachokifurahia mtoto wake kukisoma, zawadi ya kitabu kama hicho kwenye sherehe kama hiyo ni ya maana zaidi ya zawadi zingine zote tulizozoea kuwapa watoto wetu. Mkakati huu ni changamoto kwetu ya kututaka tubadilike.

Mheshimiwa Spika, kila mwaka Baraza la Maendeleo ya Vitabu Tanzania (BAMVITA) huwa linaandaa na kuendesha tamasha la maonyesho ya vitabu jijini Daressalaam, na kila mkoa, nchi nzima.Ni budi sasa kwa wizara na serikali kuanzisha mkakati wa kuhamasisha watanzania wote kutembelea maonyesho haya mwaka huu, tukifuatana na watoto wetu, ili kuwapa fursa ya kuona vitabu mbali mbali, kuchagua wanavyopendezwa navyo na tuwanunulie.

Mheshimiwa Spika, ili mkakati huu uwe endelevu, Serikali inapaswa kuhamasisha kuundwa kwa vikundi vya watoto, na kuanzisha vyama vya watoto vya kusoma, vijulikanavyo kama Mahema ya Watoto ya Kusoma – “Childrens’ Reading Tents”. Vikundi hivi vitakavyoanzishwa kwenye ngazi ya kata, vitasimamiwa na serikali za mitaa, na kuendeshwa na walimu wastaafu, sambamba na shule ngazi ya elimu ya awali, ambazo nimeishazizungumzia.

Mheshimiwa Spika, katika azma hii ya kujenga tabia na kukuza utamaduni wa kupenda kusoma miongoni mwa watanzania, mbali na kuimarisha Maktaba Kuu ya Taifa na Maktaba za Mikoa, tuanzishe Maktaba Tembezi – ‘Mobile Libraries’, kuhudumia wananchi walioko vijijini.

USAFIRI KWA WANAFUNZI

Mheshimiwa Spika, kutokana na adha kubwa inayowakumba wananfunzi na haswa wanaosoma maeneo ya miji na Majiji imekiuwa ikitishia uhai wa kukua kwa kiwango cha elimu nchini mwetu. Hali hii inatokana na mradi wa mabasi ya wanafunzi uliokuwa ukitoa huduma hii ya usafiri kwa wanafunzi kuhujumiwa na kuangamizwa.

Kambi ya upinzani , tunaitaka serikali itoe majibu kuhusu mradi huu na ni hatua gani zimechukuliwa mpaka sasa kwa wale waliohusika na ambao mpaka sasa wengine ni viongozi , tunataka wahusika hawa wachukuliwe hatua kwani wameshiriki kwa kiasi kikubwa kuongeza mateso kwa wanafunzi hawa.Tunaishauri serikali kuwa kutokana na mradi wa mabasi yaendayo kasi DSM ni muda muafaka sasa wa kulifanya shirika la UDA kuwa ni kwa ajili ya kutoa huduma kwa wanafunzi ili kuweza kupunguza adha wanayokumbana nayo kila siku.

MALIMBIKIZO YA MADAI YA WAALIMU NA WATUMISHI

Mheshimiwa Spika, idara ya utawala na Rasilimali watu ilipokea madai ya watumishi mbalimbali yaliyowasilishwa wizarani. Hivi sasa, madai ya watumishi 3,050 yanachambuliwa na kuhakikiwa ili kuainisha yale yanayostahili kulipwa, ambapo inatarajiwa kuwa ifikapo mwisho wa Juni, 2011 madeni hayo yatakuwa yamehakikiwa yote na kuwasilishwa Hazina kwa ajili ya malipo.
Kambi ya Upinzani , inataka kupata majibu ni hatua gani imefikiwa mpaka sasa kuhusiana na uhakiki wa madeni ya watumishi hawa?

Mheshimiwa Spika, Kuanzia Julai 2010 hadi Aprili 2011 madeni yenye thamani ya shilingi 777,918,643 yaliyotokana na malimbikizo ya mishahara yaliwasilishwa Hazina kwa ajili ya malipo. Kambi ya Upinzani inataka kujua ni lini malimbikizo ya waalimu hawa yatalipwa na haswa ikizingatiwa kuwa waziri wa fedha kwenye hotuba yake alkoisema kuwa mwaka huu wa fedha waalimu hawatalipwa mafao yao. Hivi waalimu hawa ni kwanini wao tuu ndio wanyimwe haki hiyo ya kulipwa haki zao? Au mpaka wagome ndio serikali itoe vitisho na iwalipe waalimu hawa?

Mheshimiwa Spika,Kutokana na waalimu wetu kuendelea kuumia kutokana na tatizo la kiwango kidogo cha mishahara na ukizingatia kuwa wanakuwa na wakati mgumu sana kuweza kukopeshwa na Benki mbalimbali za kibiashara hapa nchini.

Kambi ya Upinzani, inaitaka Serikali sasa kuweza kuweka utaratibu maalum wa kuhakikisha kuwa mifuko ya hifadhi ya jamii ambayo waalimu ni wanachama wake waweke utaratibu maalum wa kuwakopesha waalimu kutokana na makato yao kwenye mifuko hiyo ili waweze kujenga nyumba na kuweza kujikwamua kwenye hali ngumu ya maisha.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi ya Upinzani naomba kuwasilisha.

……………………Christowaja Mtinda (Mb),Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani,Waziri Kivuli Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.19.07.2011
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom