Hongera Abubakar?..

Tumain

JF-Expert Member
Jun 28, 2009
3,154
70
ALIPOJITAMBUA hana baba wala mama, aliichukulia elimu kuwa tumaini na mkombozi pekee wa maisha yake. Hivi ndivyo Abubakar Rashid (16) mwanafunzi kinara wa masomo ya Sayansi aliyeshika nafasi ya sita kitaifa katika mtihani uliopita wa kidato cha nne anavyoelezea maisha yake kama alivyohojiwa na mwandishi wetu Abeid Poyo


Swali: Wasomaji wetu wana shauku ya kujua matokeo yako yalivyokuwa?

Jibu: Kuhusu matokeo yangu ya kidato cha nne nimepata daraja la kwanza kwa pointi 1.8 nikiwa na alama A katika masomo ya Hisabati, Fizikia, Kemia, Kifaransa, Maarifa ya Uislam, na Kiarabu.


Pia nimepata alama B katika masomo ya Kiingereza, Uraia, Kiswahili na Jografia. Haya ndiyo matokeo yaliyonifanya niingie katika orodha ya wanafunzi kumi bora waliofanya vizuri kitaifa huku mimi nikishika nafasi ya sita.


Swali: Ulijisikiaje ulipogundua siyo tu ulifanya vizuri lakini Baraza la Mitihani lilikuchagua kuwa miongoni mwa wanafunzi bora?


Jibu: Baada ya matokeo kutangazwa sikuamini kama nimeweza kuwa miongoni mwa wanafunzi 10 bora hii inatokana na uchanga wa shule yangu ya Mivumoni. Unajua sisi ndiyo wahitimu wa kwanza wa kidato cha nne halafu kuna shule nyingi kongwe zenye rekodi nzuri za kitaaluma hawajatoa mwanafunzi katika 10 bora.


Pia nilikuwa na furaha kubwa kwani ndoto zangu zilitimia na zile kauli za walimu wangu kuwa naweza kufanya vizuri zilithibitika. Nakumbuka nilijiuliza nimweleze vipi bibi yangu ili ajue namna nilivyofaulu ili apate faraja na pia nidhihirishe thamani yangu kwake.


Swali: Umesema shule uliyosoma ni ngeni na nyinyi ndiyo wahitimu wa kwanza, umewezaje kufanya vizuri kwa kiwango hiki?


Jibu: Shule yangu imechangia kwa kiasi kikubwa katika mafanikio yangu. Kwa hakika huwezi kuzungumzia mafanikio yangu bila kuizungumzia Mivumoni Islamic Seminary.Tulikuwa na walimu wazuri, wenye ari na moyo wa kujituma huku wakifundisha kwa ufanisi mkubwa.


Hii shule iliweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kwamba tunafaulu ikiwemo kufanya mitihani mingi ya ndani, mitihani ya ushindani na shule nyingine, kambi yakujisomea na kwa sisi wanafunzi wa sayansi tulifanya practical (mazoezi ya vitendo) ya kutosha.


Swali: Tukiiacha shule na walimu wako, tueleze siri binafsi ya mafanikio yako?

Jibu: Kwa kweli siri kubwa ni kuwa na nidhamu bora, hii inajumuisha kushirikiana vema na wanafunzi wenzangu, kufuata ushauri wa walimu na walezi wangu na wanajamii wazuri kwa ujumla.


Nilisoma kwa bidiii nikiwa na nia ya kujiondoa katika umaskini ili niweze kuja kuwakomboa mayatima wenzangu na kuliokomboa taifa langu kutokana changamoto mbalimbali zinazozikabili jamii za Kiafrika.


Katika maisha ya shule sikuwa na muda wa kujihusisha na vikundi viovu au kukaa vijiweni.Pia niliepuka mambo yanayopunguza ufanisi wa kusoma kama kuwa na marafiki wa kike, kuangalia picha za ngono na mengineyo.


Swali: Kusoma kuna mikiki mikiki mingi, wewe ni yatima uliwezaje kusoma bila ya usimamizi wa wazazi?


Jibu: Pamoja na kuishi katika mazingira magumu ya kukosa wazazi na kuwa na mlezi hohehahe, maendeleo yangu kitaaluma yalikuwa mazuri sana.Hali hii ilichangiwa na malezi bora ya bibi aliyekuwa akinipa nasaha bila kujali umri wangu mdogo hivyo akili yangu ilipevuka nikiwa bado mdogo.


Kwa mfano niliamini kuwa mafanikio yangu kitaaluma ndiyo chachu ya mafanikio maishani mwangu na kuwa umaskini wangu hautakiwi kunikatisha tamaa badala yake uwe changamoto ya kusaka mafanikio.


Swali: Ukimtoa bibi kuna wengine waliokusaidia na kwa vipi?
Jibu: Naomba niwashukuru walimu wa shule ya msingi Ali Hassan Mwinyi walionivumilia kusoma nikiwa na madeni mpaka namaliza.


Kwa kuwa hawakutaka kuona ndoto zangu zinaishia hapo, mwalimu mkuu aliueleza wasifu wangu kwa uongozi wa msikiti wa Mtambani waliochukua jukumu la kunilea na kunisomesha.


Hii ilinisaidia kwani matatizo yalibaki kwa bibi aliyeendelea kupata mahitaji ya lazima kwa tabu na mara nyingi nilitumia pesa za walezi wangu kununua chakula nyumbani na hili nalifanya mpaka hivi sasa.


Kwa uongozi wa msikiti wa Mtambani wanaonilea mpaka hivi sasa sijui naweza kuwaambia nini, labda niwashukuru na kuwaomba kuwa waendelee na moyo wa aina hii kwa watoto wengine zaidi wanaohitaji misaada.


Swali: Kuna madai kuwa Hisabati ni somo gumu, nini mtazamo wako?


Jibu: Gumu kivipi? mbona tuko wengi tuliopata A nchini?. Mimi maoni yangu ni tofauti kidogo na madai hayo. Mimi nasema Hesabu sio somo gumu isipokuwa wanafunzi wengi aidha hawazijui ama hawazifuati kwa makusudi zile mbinu za kufaulu hesabu nikiwa na maana hawafanyi vile ambavyo hesabu inawataka wafanye.


Swali: Una maana gani unaposema wanafunzi hawafanyi vile ambavyo hesabu inawataka wafanye?


Jibu: Labda nitoe mifano miwili, hesabu inahitaji mazoezi mengi kila unapomaliza mada fulani, sasa wanafunzi wengi hili hawalifanyi na lingine hesabu si somo la kusubiria mtu ulisome wakati wa mitihani. Unalizimika kila siku ufanye hesabu mbalimbali ili uweze kujua mbinu na mitego yake.


Swali:Baada ya mafanikio haya, nini matarajio yako kielimu kwa siku za baadaye?


Jibu: Binafsi natarajia kusomea ualimu wa masomo ya Hisabati na Fizikia na malengo yangu ni kuwa karibu na vijana ili niweze kuwafunda wawe wazalendo kwa nchi yetu Tanzania. Nikiwa mwalimu nataraji kuanzisha taasisi za kielimu kama vile shule za msingi na sekondari zitakazotoa elimu kwa watoto yatima na wale wa maskini.Lakini pia nahitaji kushiriki katika kampeni za kuongeza wanafunzi wanaochukua masomo ya sayansi nchini na kisha waje kufaulu vizuri ili kuondoa yale madai kwamba masomo ya sayansi na hesabu ni magumu.


Ualimu ni kazi niipendayo na hilo linathibitishwa na historia yangu tangu nikiwa shuleni kwani nilikuwa nawafundisha wenzangu na niliwaomba walimu niwe nawafundisha wanafunzi wa mdaraja ya chini hususan somo la Hesabu na pia kuwapa mbinu mbalimbali za kufaulu. Kwa sasa nipo shuleni naendelea kuwaongoza wanafunzi wa kidato cha nne katika mijadala na vikundi vya masomo ya sayansi na mengine ili kuwapa mbinu za usomaji na kuwatatulia matatizo ya kitaaluma yaliyo ndani ya uwezo wangu.


Swali: Unatoa wito gani kwa watoto yatima wengine wanaopata fursa ya kusomeshwa na wafadhili?


Jibu: Napenda kuwashauri watumie vizuri fursa hizo kwani wapo wengi wanaozihitaji lakini hawazipati.Nawashauri wamg'ang'anie mkombozi elimu kwani mayatima wengine na jamii wanatutazama,waache kuiga tabia za ajabu zilizo kinyume na tamaduni za Kiafrika kwani kufanya hivyo ni kupoteza mwelekeo katika maisha yao.


Swali: Tueleze kwa ufupi kuhusu maisha yako?

Jibu: Wazazi wangu walifariki nikiwa na umri mdogo kwa mfano baba alifariki nikiwa sina ufahamu wa kutosha hivyo sijaonja ladha ya malezi ya baba hasa ninapokuwa na matatizo. Mama alifariki mwaka 2003, kifo chake kiliniathiri sana nilijiona kama kiumbe tofauti niliyeibuka kutoka kusikojulikana.Wenzangu niliwaona wazazi wao lakini wa kwangu hawapo. Ugumu wa maisha uliongezeka na mlezi wangu wa kwanza ambaye ni bibi alikuwa mjane asiye na chochote.

Kiujumla tangu nikiwa mdogo hali ya maisha katika familia yetu ilikuwa ngumu.Alipofariki mama hali ikawa ngumu zaidi, bibi akishindwa kunilipia ada na mahitaji mengine, tukawa mimi na bibi tunaenda kuomba kwa wenye fedha.Tulikuwa tunakosa na mara nyingine tunapata fedha zisizotosheleza mahitaji.


Anachosema mlezi (Sheikh Abdallah Mohammed Ally) Abubakar ni kijana wa ajabu, mara zote alikuwa changamoto kwa wenzake. Nilitambulishwa kwake alipomaliza darasa la saba na mtu aliyemsaidia sana elimu ya msingi akawa hana uwezo wa kumsaidia tena. Tulichukua kwa kuwa hii ndiyo kazi ya vituo kama hivi. Tutaendelea kumlea na wala hatuzuii wengine kuja kutusaidia kumwendeleza.
 
Hongereni waalimu, masheikh na taasisi zote mliofanya juhudi kumsaidia kijana huyu katika safari yake ndefu ya kielimu..Mwenyezi Mungu awaongezea
 
M/mungu hamtupi mja wake, jitahidi kijana usome kwa bidii na usije ukalewa sifa, kaza buti na ikiwezekana matokeo ya kidato cha sita uwe mwanafunzi bora wa kwanza Tanzania..... mimi huwa naamini "kila kitu kinatokea kwa sababu" hivyo m/mungu alikuwa na sababu ya kuwachukua wazazi wako wote wawili, na hiyo imeleta chachu ya maendeleo kichwani kwako na inshallah atakupa uwezo wa kusoma sana na baadae utakuja pata kazi nzuri na utaweza kumtunza bibi. Hongera kwa matokeo mazuri, m/mungu amekutunuku kwani kuna watoto wengi wenye wazazi wote wawili na kipato kizuri na lakini darasani wanaongoza kwa ufirauni na kushika namba za mwisho.

Hongera kijana.
 
Uende mbelezaidi kijana, upae kama kishada.
Lakini kumbuka, popote utakapofika huko mbele, jamii yako huku ulikotoka inakusubiri kwa hamu ili ugawane nao maarifa, ushauri, na mafunzo uliyopata!
God bless you young blood!
 
M/mungu hamtupi mja wake, jitahidi kijana usome kwa bidii na usije ukalewa sifa, kaza buti na ikiwezekana matokeo ya kidato cha sita uwe mwanafunzi bora wa kwanza Tanzania..... mimi huwa naamini "kila kitu kinatokea kwa sababu" hivyo m/mungu alikuwa na sababu ya kuwachukua wazazi wako wote wawili, na hiyo imeleta chachu ya maendeleo kichwani kwako na inshallah atakupa uwezo wa kusoma sana na baadae utakuja pata kazi nzuri na utaweza kumtunza bibi. Hongera kwa matokeo mazuri, m/mungu amekutunuku kwani kuna watoto wengi wenye wazazi wote wawili na kipato kizuri na lakini darasani wanaongoza kwa ufirauni na kushika namba za mwisho.

Hongera kijana.


Mimi ni Abuubakar, kijana aliyetajwa katika Article hapo juu, nilipenda kuwajulisha maendeleo yangu kwa kuwaeleza kuwa nimechanguliwa kujiunga na MIT, Massachusetts Institute of Technology in the fall of 2012, and currently, am studying the International Baccalaureate Diploma at an International school called United World College-USA.
 
Mimi ni Abuubakar, kijana aliyetajwa katika Article hapo juu, nilipenda kuwajulisha maendeleo yangu kwa kuwaeleza kuwa nimechanguliwa kujiunga na MIT, Massachusetts Institute of Technology in the fall of 2012, and currently, am studying the International Baccalaureate Diploma at an International school called United World College-USA.[/QUOTE


CJAKUPATA!!!!
 
Mimi ni Abuubakar, kijana aliyetajwa katika Article hapo juu, nilipenda kuwajulisha maendeleo yangu kwa kuwaeleza kuwa nimechanguliwa kujiunga na MIT, Massachusetts Institute of Technology in the fall of 2012, and currently, am studying the International Baccalaureate Diploma at an International school called United World College-USA.[/QUOTE


CJAKUPATA!!!!


I am the one who was talking in the interview on the article you were commenting on (Hongera Abubakar?), basically, I am the Abuubakar uliyempa hongera. And what I did is inform you all that I will be joining Massachusetts institute of technology in the fall.
 
Hongera sana Aboubakar. Watie moyo na pia waeleze wengine katika jamii iliyokuzunguka umuhimu wa elimu. Ili nao wajikomboe kama wewe. Sio lazima ukose baba na mama ndio utilie elimu msisitizo, wape motisha vijana wa kiislamu wasiopenda shule.
 
Back
Top Bottom