HOJA KUHUSU NCHI YA WATZ, nani anafuatilia haya, Hayupo

Kisendi

JF-Expert Member
Jan 29, 2009
699
178
dugu zanguni,
wakati fulani haya mambo yanakatisha tamaa sana. Nakuonea huruma Helen huko uliko
maana hupati undani wa mambo tunayoyapata wenzio huku. Deus pia anakosa maana kaenda
bondeni. Ukweli ni kuwa wananchi na sisi wanaharakati tunajua fika kinachoendelea na
tunafahamu kuwa sote ni mateka wa mafisadi kwa namna moja au nyingine. Tatizo ni
kwamba hata ukiongea nani anakusikiliza? Nani anajali? Nani anachukua hatua? na hata
pale hatua zinazoitwa hatua zikichukuliwa ndizo muafaka?
Suala la Richmond limebaki danadana hadi kesho. Wabunge wachache walipoacha kuhoji
hatua za serikali ndo umekuwa mwisho wake. Nani wa kuliendeleza?
Kesi hizo za EPA na nyinginezo nawaapia kuwa zitaisha baada ya uchaguzi wa 2010.
Nani azishughulikie? Kwa maslahi gani?
Agenda za muhimu kuhusu madini unazisikia tena? Tumeshafanyiwa kiini macho tuamini
Rais anashughulikia yameishia hapo kama huamini suburi uone kama hiyo sera mpya ya
madini itasaidia kitu. nani atekeleze? tena karibu na 2010 akose kura?

Kule Kilwa kampuni moja la Kidachi limepewa msitu lianzishe shamba la BIofuels
lakini kabla ya hapo inafanyika kwanza biashara ya magogo iliyopigwa marufuku ili
kusafisha eneo nani anajali?

Kama kuna wanadamu wamefanyiwa unyama hapa nchini hakuna aliyefikia kiwango cha
wafugaji waliotoka Ihefu na baadae wa Kilosa. Mtu anaporwa ng'ombe zaidi ya elfu
moja, na baadae analazimishwa kuwauza kwa bei mchekea ya hadi elfu thelathini
badala ya laki tatu au nne ili alipe faini ya zizi la bandia lililowekwa mahsusi
kwaajili hiyo unalichukuliaje hilo?

Mimi naamini kabisa kuwa yote haya yanajulikana sana na wananchi na wanaharakati
wamejitahidi sana lakini bado hatujafikia mateso ya kutuwezesha kuzinduka na kupiga
hatua moja zaidi ya hizi tunazofanya ili hao walioziba maskio wayazibue
watusikilize. Wabunge ndio hata siwaamini kabisa maana ukiwa pale Dodoma wengine
wanatoa hadi machozi kwa huruma na kuahidi makubwa sana. Baada ya hapo, ndani ya
bunge wanabadilika. walifanya hivyo mwaka 1998 wakati wa sheria za ardhi, walifanya
hivyo 2002 wakati wa sheria ya NGOs na wameendelea kufanya hivyo juzi kwa suala la
wafugaji wanaoporwa mifugo yao.

Masuluhisho
Mwenye kuandika kwenye mtandao aendelee kuandika. HIi inasaidia kuendelea kujielimisha

Wenye fursa katika vyombo hivyo hivyo vya mafisadi wazitumie kusema wanachoweza
kusema na tuliobaki tuwape nguvu. Japo hili ni gumu sana maana siku hizi tumeishiwa
kweli kama huamini jaribu kutafuta wazungumzaji kwenye vipindi vya redio na TV kila
mtu anatoa udhuru wanarudia walewale. Ngoja tu tuendelee hivyo hivyo maana huwa
wanatusikia na kutuona japo hawatusikilzi

Tufufue mitandao yetu inayochechemea ijadili mambo ya maana badala ya kuendeleza
agenda zao hao hao. BAWATA imerejea nini kinafuata baada ya ushindi wa miaka 12?
Natambua pia kuwa FemAct karibu itajitokeza kwa mshindo mkuu, wakati CCNC na
mitandao mingine ikifuatia. Sitaki kuamini kuwa UDASA ilizikwa pamoja na Chachage
japo kuna kila dalili kuwa huo ndo ukweli.

Kwa kuanzia, nawakaribisha katika kongamano la kitaifa la masuala ya ardhi ambapo
mwaka huu tutafanya tathmini ya miaka kumi ya sheria za ardhi 1999 -2009. Tumesikia
vilio vya wanachi maeneo ya madini, misitu, wanyamapori na sasa vijijini dhidi ya
wawekezaji wakati sheria za ardhi zipo. kwanini? Tunatarajia zaidi ya washiriki mia
moja wengi wakitoka mikoani katika maeneo ya harakati na baadhi ya wawakilishi
kutoka nchi jirani. wengine ni ninyi wenyewe. Ni mwezi huu tarehe za mwishoni.
karibuni sana, mengine mtajulishwa.

Tuendelee kujadili tutafika tu
Yefred
 
Back
Top Bottom