Hivi ndivyo tulivyochemsha Waswahili

AHAKU

Member
Jan 28, 2010
26
1
Ujamaa uliikosesha Tanzania ajira za Kiswahili Marekani

Bado Tanzania ina nafasi na uwezo mkubwa wa kuikuza lugha ya Kiswahili nje ya mipaka yake. Huu ndio mtazamo wa Profesa Pete Mhunzi, Mmarekani mwenye asili ya Afrika na mpenzi wa Kiswahili anayeelezea maendeleo ya lugha hiyo nchini Marekani kama alivyohojiwa na mwandishi wetu Abeid Poyo
Swali: Yakoje maendeleo ya Kiswahili nchini Marekani?
Jibu: Maendeleo ya Kiswahili Marekani yalianza kuporomoka baada ya mwaka 1970 hivi. Kipindi hiki kilitanguliwa na ule muda wa uhuru kwa nchi nyingi za Afrika ambao ulijumuisha pia harakati za kukomesha ubaguzi Marekani zilizokuwa zikiendeshwa na Waafrika tuliozaliwa Marekani.
Wengine tulijitambulisha kama Waafrika na kutangaza kuwa haki ya kisheria haikukidhi mahitaji ya utu wetu. Harakati za kundi letu ndizo zilizofungua milango ya Kiswahili kufundishwa shuleni hususan vyuo vikuu.
Swali: Wewe ulianza kujifunza Kiswahili lini?
Jibu: Kwa sababu tulipigania haki ya kuisoma historia yetu pamoja na harakati za kuikomboa Afrika za nyakati hizi, matokeo yake yalikuwa kufunguliwa kwa idara za masomo ya Kiafrika kwa sisi Wamarekani na kisha Afrika yenyewe kwenye vyuo vikuu na miongoni mwa masomo yakawa Kiswahili. Hivi ndivyo nilivyoanza kujifunza Kiswahili kuanzia mwaka 1970.
Swali:Je, Watanzania waliopo Marekani wanakitumia Kiswahili katika mazungumzo ya kawaida?
Jibu: Ndiyo wanakizungumza lakini wengi wao wanajiepusha na jukumu la kujifunza zaidi lugha hiyo kwa sababu hakiendani na taaluma wanazosomea ama wanazozifanyia kazi. Wanakiona kama msingi wa maisha ya nyumbani na pia kitu cha wazee wao na kwao hawana haja nacho katika dunia ya kazi au maisha ya hivi leo.
Swali: Kiswahili kinafundishwa sana Marekani, nini malengo ya Wamarekani wanaojifunza lugha hii?
Jibu: Siku hizi ni mfano wa kasumba kwa vile wengi wao wanatarajia kufaulu bila ya kutoka jasho. Wametulia katika ujinga wa kuyaona masomo yoyote yale yanayohusika na Afrika, Uafrika au Waafrika ni mambo yasiyo na undani, yasiyoweza kuchemsha bongo.
Vinginevyo, ninavyowaona wale wa mfano huu wa kasumba wanaojiita wanafunzi, katika Kiswahili changu ninasema hivi: Hawana ti wala pe!
Swali: Ulishawahi kufundisha Kiswahili, upi uzoefu wako katika hilo?
Jibu: Ni kweli niliwahi kufundisha ila ilikuwa kazi ya muda katika idara ya masomo ya Waafrika Wamarekani. Sikuwahi kukifundisha kama kazi ya kudumu katika idara za isimu ya lugha nikiwa kama mwalimu. Mimi nina shahada ya uzamili katika fani ya Biashara (MBA).
Swali: Unaonekana ulikuwa na mapenzi na Kiswahili kwa nini hukukisoma katika ngazi ya shahada ya tatu?
Jibu: Sikuwahi kusoma shahada ya uzamifu (PhD) katika Isimu ya lugha licha ya kutaka kufanya hivyo. Nilikatazwa kutokana na upendo wangu wa Kiswahili ukiwa pamoja na nia yangu kukiweka kiwe msingi ama kitovu cha masomo ya isimu ya lugha.
Mkuu wa idara ya isimu ya lugha alinifahamu vizuri kwa sababu nilikuwa mwanafunzi wake wa Kiswahili pamoja na masomo ya isimu ya lugha. Naye kabla ya kuwa profesa alikuwa mmisionari Tanzania. Huyu ndiye aliyenizuia kusomea PhD ya Isimu ya lugha kwa nia ya kunipunguzia nia yangu ya kujifunza Kiswahili na pia kujitambulisha kama Mwafrika. Hata hivyo Kadiri nilivyozidi kujifunza na kuendelea katika Kiswahili ndivyo alivyozidi kuchukia.
Swali:Kuna taarifa kuwa ajira nyingi za ualimu wa Kiswahili nchi za nje hususan Marekani zimemezwa na walimu kutoka nje ya Tanzania na wasio na ujuzi wa Kiswahili. Je, ni kweli?
Jibu: Ni kweli. Hebu nianzie na chimbuko la kukifundisha Kiswahili Marekani. Habari za Ulaya na kwingineko sina habari nazo. Kabla ya mwaka 1960 hivi, Kiswahili kilifundishwa kwenye vyuo vikuu kwa ajili ya majeshi, CIA pamoja na wamisionari, lengo lilikuwa kusaidia upelelezi, uchunguzi pamoja na usambazaji wa Ukristo.
Katika enzi hizo wanafunzi kutoka Afrika na sisi pia tulikuwa wachache sana katika vyuo vikuu kwa hivyo walimu kwa ujumla walikuwa wamisionari waliorudi Marekani baada ya muda wao Afrika Mashariki kumalizika.
Halafu baada ya Uhuru wanafunzi wakaanza kuja kutoka Afrika, wengi wao hasa Wakenya walipata kazi ya kufundishia Kiswahili. Miongoni mwao wakapata kazi katika idara za masomo ya Umajumui wa Afrika (Pan-African Studies ).
Na hizi kazi zilifunguliwa kutokana na harakati zetu,tulimwaga damu na wakati mwingine kufungwa magerezani.
Swali: Kwa maelezo haya kwa nini ajira zikawa kwa Wakenya pekee na si Watanzania au Waganda?
Jibu: Hawakuwa Watanzania kwa sababu Tanzania ilibaguliwa kutokana na siasa zake za Ujamaa. Ulikuwa ni Mpango wa serikali ya Marekani kutokana ya chuki dhidi ya siasa za Ujamaa na isitoshe harakati za Tanzania katika ukombozi wa Afrika Kusini na Msumbiji.
Aidha kulikuwa na Watanzania wachache waliokuwa wakisoma kwenye vyuo binafsi ambavyo vijana wa matajiri ndimo walipokuwa wakisoma.
Serikali ya Tanzania ilikuwa inalipa gharama huenda maradufu ya gharama za wanafunzi Wakenya waliosoma katika vyuo vya kiserikali. Isitoshe
idara za masomo ya Kiafrika nilizozitaja awali zilikuwa kwenye vyuo vikuu vya kiserikali ambavyo sisi tukawahi kusoma na kufungua idara zetu.
Jambo lingine, Wakenya wengi waliowahi kazi ya kufundisha Kiswahili walikuwa wanafunzi wa masomo ya isimu ya lugha.
Swali: Hapa Tanzania kuna mjadala kuhusu lugha inayofaa kufundishia katika madaraja yote ya elimu kati ya Kiswahili na Kiingereza. Wewe una maoni gani?
Jibu: Suala hili linanitatiza kupita kiasi. Mimi bila shaka ni mpenzi wa Kiswahili lakini siwezi kukipendekeza huku
nikisahau ama kuukanusha umuhimu wa Kiingereza katika dunia ya hivi leo, dunia ya utandawazi. Mimi nitajibu hivi: Tafadhalini ndugu zangu Watanzania someni lugha hizi zote mbili.

Swali:Unadhani Kiswahili kilivyo sasa kina nafasi ya kukua kimataifa na kuwa na hadhi kama Kiingereza?
Jibu: Nafasi ipo, uwezo upo lakini tunahitaji kurekebisha nia zetu. Lazima Kiswahili kiwe katika kitovu cha maadili ya Watanzania kwa ujumla. Tusikilinganishe Kiswahili na Kiingereza katika hadhi yake. Naomba tusisahau msingi wa umuhimu wa Kiingereza ni ukoloni na mtoto wake utumwa, sitaki Kiswahili kifuate njia hiyo.
Swali: Unadhani nini kinakwamisha maendeleo ya Kiswahili ndani na nje ya Tanzania?
Jibu: Swali hili limenikumbusha kitabu kimoja cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, nacho ni We Must Run While They Walk. Kanuni moja ya kimsingi Marekani ambayo inapinga siasa za Ujamaa ni: Wanadamu takriban wote ni wavivu. Sharti maadili ya jamii yatusukume kuboresha maisha yetu. Ni rahisi mno kuwa mfuasi kuliko kuwa kiongozi.
Swali:Unautazamaje mchango wa balozi za Tanzania katika kukuza Kiswahili nje ya mipaka ya Tanzania?
Jibu: Ninasikitika nao hasa huku Marekani kwa sababu zile zile zilizopo katika maelezo yangu ya mwanzo. Nikirejea harakati zetu za kujitambulisha kama Waafrika, mimi nasema; ‘’Hamna hamna ndimo mliwamo.’’
Swali: Wewe na hata Watanzania mnaoishi Marekani mna mpango wowote wa kuwasaidia kiajira walimu wa Kiswahili wanaopenda kuja Marekani kusomesha?
Jibu: Sijaona namna ya kuwasaidia ila nashauri hivi wanafunzi waliokwishapata shahada ya pili katika masomo ya isimu ya lugha wanaweza kujaribu kuomba kazi ‘watesti zali’
Wafanye utafiti kupata habari za vyuo vikuu vinavyotoa shahada za isimu ya lugha vikiwa pamoja na vingine ambavyo vina idara za Pan-African Studies ama Black Studies. Pia kuna serikali ya Marekani huenda kazi inapatikana lakini kawaida wanatafuta watu ambao tayari wapo Marekani ili wasije kuwalipia gharama za usafiri.

Swali:Una maoni gani kwa watumiaji wa Kiswahili hasa wa Tanzania?
Jibu: Naomba wajenge misamiati pamoja na istilahi za Kiswahili na kuzitumia. Wafutilie mbali tabia ya kuchanganya lugha mbili katika matumizi hali inayokifanya Kiswahili kidharaulike.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom