Mchungaji...Shukran...Naomba pia usisahau kuwa madhumuni halisi ya wewe kuanzisha thread hii ni baada ya kudai kuwa mimi kuliuliza suala hili kwenye ile thread nyingine haikufaa.
Na hivyo basi ningeomba Mnyika ajaribu kutowa maelezo ya kihistoria ili wengine wetu tuweze kuelewa kuwa usaliti huo wa Sina ni upi.
Siko hapa kuchaguwa upande upi ni mzuri ama upi ni mbaya...Inawezekana kweli ni msaliti na mimi sijui...Hivyo maelezo yangesaidia kwani ndio kuelimishana huko pamoja na kujengana kwa kuthamini na kueleweshana kuhusu historia ya Taifa letu kwa ujumla...Taifa nalo litanufaika pia na historia ya usaliti huo.....Usaliti ambao kwa kweli ni muhimu Mnyika auweke wazi kwani alisema ulisababisha damu ikamwagika dhidi ya Mdachi.
Ahsante.
Kwanza ningependa kuchukua fursa hii kumshukuru Mr Mushi kwa kuwa kisababishi cha kuanza mada hii ambayo imeleta na mengi katika kujifunza juu ya historia ya uchagani. Kutokuridhika kwako hukukaa kimya na kunung'unikia vitandani kama watanzania wengi walivyo, bali uliamua kutoa dukuduku lako ili kupata taarifa sahihi. Mimi naona hiyo ni hatua ya kijasiri na ya kishujaa. Mpaka sasa mheshimiwa Mnyika hajajitokeza kujibu tuhuma hizo hivyo inathibitisha kwamba ni kweli alisema na inaonekana hakuwa na uhakika na anachoongea. Mnyika ni miongoni mwa watu wengi katika jamii yetu ambao bila ya kuwa na taarifa sahihi iliyofanyiwa utafiti makini huibuka na kutoa matamko kwenye halaiki na hata kujiabisha kwa kudhani watanzania wote ni mbumbumbu. Sifahamu kabila lake au fani yake hasa ni nini lakini inaonekana dai alilolitoa dhidi ya mangi Sina wa Kibosho limetokana na kudandia historia asiyoijua mapana yake. Ni vizuri watu wakajifunza kuongea (hasa kwenye public) taarifa ambazo hata wakija kuulizwa baadaye watakuwa na uwezo wa kuzitetea kihoja na kuzithibitisha kitaalamu. Viongozi wa kwenye jamii ambao wanaongea tu chochote ni hatari kwa mustakabali wa taifa letu.
Nikirudi kwenye mada, hasa dai alilolitoa mheshimiwa Mnyika ni kwamba uhasama uliokuwepo kati ya mangi Sina na mangi Rindi (Mandara) wa old Moshi ni wa kihistoria. Hapo nyuma, yaani 1890, mangi Rindi kwa kuona kwamba alishindwa kukabiliana na nguvu zilizokuwa zikiongezeka kila kukicha za mangi Sina kule uchagani, aliamua kutumia fursa yake ya ukaribu na wakoloni kule kwenye boma lake kuwachochea dhidi ya mangi Sina na kuwaahidi kuwapa msaada wa askari na njia za kuendea Kibosho kumshambulia mangi Sina. Mangi Rindi alikuwa ameona fadhaa kubwa ya kushindwa kumsaidia mangi Ngamini kule Machame dhidi ya mdogo wake Shangali ambaye alikuwa akisaidiwa na askari wa mangi Sina kumwezesha kutawala Machame. Huku akimchochea kapteni Johannes ambaye naye alishakuwa amekereheshwa na kitendo cha mangi Sina kuchochea vita kule Machame kumng'oa Ngamini, mangi Rindi alifanikiwa kumshawishi kapteni Johannes mwaka ule wa 1890 kwenda kushambulia ngome ya mangi Sina huku akimsaidia kwa kumpa askari kadhaa. Katika vita hiyo mangi Sina alishindwa vibaya na kulazimishwa kujisalimisha ambapo aliingia mkataba na wakoloni wa kijerumani kuwa mtiifu na kuiunga mkono serikali hiyo. Mangi Rindi aliitumia hiyo nafasi kumtia adabu adui wake na hata kumchochea kapteni Johannes kwamba mangi Sina ayasalimishe kwa mangi Rindi pia maeneo ya Uru na Kirua-Vunjo aliyokuwa ameyaweka chini ya himaya yake, sharti ambalo kwa kusaini mkataba wa kujisalimisha ilibidi akubaliane nalo. Mangi Sina aliamriwa pia amwachie mangi wa Uru ambaye alikuwa amemkamata na kumweka kifungoni. Ingawa mangi Rindi aliona faraja kwa kumtia adabu adui wake wa siku nyingi, tatizo ni kwamba alikuwa ameshaanza kuwa mgonjwa na mwaka huo wa 1890 inasimuliwa kuwa muda mwingi alikuwa yuko kitandani akiugua (inasemekana alikuwa amepooza kutoka kiunoni kuelekea chini miguuni). Mangi Rindi Mandara alifariki baadaye mwaka huo wa 1890 na mtoto wake Meli Mandara akatawala.
Kwa hiyo utaona sababu vita ilipokuja baadaye kati ya mangi Meli na wakoloni wa kijerumani kwa nini mangi Sina aliwasaidia wakoloni dhidi ya mangi Meli. Ni mambo ya uhasama na visasi, lakini pia kumbuka mkataba ambao alilazimishwa kuusaini hapo nyuma kama sharti lake la kujisalimisha. Ni hayo tu kwa leo.