Hili la warioba ni la kweli? Wana jf simwelewi?

Kiumbemzito

Member
Nov 25, 2008
31
1
AWALAUMU WATU WANAOPINGA MALIPO YA DOWANS, ATAKA MAHAKAMA ZIHESHIMIWE
Raymond Kaminyoge


WAZIRI Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba amesema haoni nia ya dhati kwa viongozi wa ngazi za juu wa serikalini kupambana na ufisadi badala yake, suala hilo limekuwa likizungumzwa kisiasa.“Viongozi wa ngazi za juu wanazungumzia mafisadi lakini hawawachukulii hatua za kisheria, huu ni upungufu mkubwa katika utawala wetu,” alisema Jaji Warioba Dar es Salaam jana alipokuwa akizindua Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Chama cha Majaji Wastaafu Tanzania (Tarja).

Warioba ambaye aliwahi kuongoza Tume ya Kero ya Rushwa wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu ya Benjamin Mkapa alisema viongozi wa Serikali wanashindwa kutofautisha masuala ya kisiasa na ya kisheria: “Sheria ni kuchukua hatua siyo kuhutubia kwenye majukwaa. Nawaasa majaji wenzangu wastaafu tujitahidi kutoa ushauri kwa viongozi na wananchi kuhusu umuhimu wa kufuata sheria,” alisema.

Kauli ya Jaji Warioba imekuja kipindi ambacho jamii ya Watanzania imegawanyika kuhusu vita dhidi ya ufisadi kutokana na watuhumiwa kutofikishwa katika vyombo vya sheria kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kukosekana kwa ushahidi dhidi ya tuhuma zinazowakabili.

Dowans walipwe
Katika hotuba yake, Jaji Warioba pia alizungumzia suala la malipo ya Kampuni ya Dowans akisema Serikali inawajibika kutekeleza amri ya Mahakama kwa kuilipa kampuni hiyo ya Costa Rica na kwamba kufanya hivyo ni kuzingatia utawala bora na wa sheria lakini akataka mafisadi waliohusika wachukuliwe hatua.

Kauli hiyo ya kwanza ya Jaji Warioba kuhusu sakata hilo la Dowans imekuja kipindi ambacho Watanzania wengi wakiwamo wanaharakati wanapinga malipo hayo ya Sh110 bilioni kwa Dowans kiasi cha kutaka kuandamana kuyapinga.

Wakati wanaharakati hao wakiwamo wanasheria kutoka Kituo cha Msaada wa Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) wakipinga malipo hayo, jana Jaji Warioba alitofautiana nao akisema jambo hilo si la kisiasa bali kisheria.

Jaji Warioba aliwashangaa baadhi ya viongozi wanaosimama hadharani na kupinga hukumu hiyo ya Mahakama.

Ingawa hakuwataja kwa majina, lakini viongozi wa kisiasa ambao wamekuwa wakipinga malipo hayo kwa nguvu zote ni pamoja na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Samwel Sitta na Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe.

“Nashangaa viongozi wa nchi inayofuata utawala bora na wa sheria wanapinga hukumu iliyotolewa na Mahakama isitekelezwe, tunaonyesha mfano gani kwa jamii tunayoiongoza? Leo tunaikataa hukumu ya kesi ya Dowans, kesho haijulikani tutaikataa kesi gani, hii itatufanya tuwe na jamii ya watu wasiofuata sheria.”

Warioba ambaye aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), alitoa mfano mwingine wa kesi ya uhaini katika utawala wa Awamu ya Kwanza ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere akisema katika kesi hiyo, wananchi walilalamikia adhabu iliyotolewa na Mahakama kuwa ilikuwa ndogo mno.

“Hata Serikali ilikiri kuwa kweli adhabu hiyo iliyotolewa kwa wahaini ilikuwa ndogo, lakini haikuchukua hatua ya kuikataa adhabu hiyo, iliheshimu uamuzi wa Mahakama,” alisema Warioba.

Alizishangaza pia taasisi zinazojihusisha na masuala ya haki za binadamu kupinga malipo hayo kwa kampuni ya Dowans.Mahakama Kuu ya Tanzania iliisajili Tuzo ya Dowans iliyopewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Kibiashara ( ICC) ya kutaka kulipwa Sh94 bilioni na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Baada ya kupitia tuzo hiyo iliyokuwa imesajiliwa na Dowans katika Mahakama hiyo, ilitoa uamuzi wa kutaka kampuni hiyo iliyorithi mkataba wa kifisadi wa Richmond ilipwe Sh110bilioni ikiwamo riba kwani hukumu ya ICC iliyotolewa Novemba, mwaka jana imezingatia masharti ya kisheria ya mkataba kati ya pande mbili.
Hata hivyo, hatua hiyo imekuwa ikipingwa vikali na kina Sitta na Dk Mwakyembe ambao wamepata nguvu ya wanaharakati ambao sasa wanaandaa maandamano makubwa nchi nzima.

Uhuru wa mahakama
Akizungumzia Mahakama, Jaji Warioba alisema chombo hicho kitakuwa huru kikipata uhuru wa kuwa na bajeti wanayoweza kujipangia wenyewe nini cha kufanya.Alisema utaratibu wa sasa wa kuomba fedha Hazina katika kila shughuli zinazotakiwa kufanywa na chombo hicho unakwamisha uhuru wake.

“Bunge liko huru kwa sababu wana bajeti yao ambayo wao wenyewe wanaigawanya kutekeleza majukumu yao, katika Katiba Mpya hilo lipewe kipaumbele,” alisema.

Kuhusu Katiba Mpya, Waziri Mkuu huyo mstaafu alisema maoni ya wananchi katika uandaji wake ni ya muhimu kwa sababu wao ndiyo wenye uwezo wa kueleza ni Tanzania ya aina gani wanayoitaka.

“Lakini ukiwahoji viongozi hasa wa kisiasa kuhusu Katiba, wao watakueleza madaraka makubwa ya Rais au Tume ya uchaguzi iwe huru mambo ambayo hayawezi kumaliza matatizo ya wananchi,” alisema.
Rais wa Tarja, Jaji Robert Mihayo alisema ingawa nchi inafuata misingi ya utawala bora na wa sheria, vitendo vinavyofanyika vinakiuka misingi hiyo.

Kuhusu mpango huo wa miaka mitano, Jaji Mihayo alisema utakifanya chama hicho kuwa mwelekeo mzuri wa kiutendaji. “Chama kitakuwa na ratiba ya shughuli za kufanya katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2011 hadi 20015.”

Alisema hiyo itawafanya hata wafadhili wenye nia ya kukisaidia kufahamu shughuli zake ambazo alisema ni pamoja na utoaji wa ushauri na mafunzo kwa mahakimu na majaji nchini ili kuimarisha utawala bora na wa sheria.

“Unajua Hakimu akifanya kosa wakati akitekeleza majukumu yake kama vile kupokea rushwa inakuwa aibu yetu kwa sababu naye anaweza siku moja kuwa jaji ndiyo maana inabidi kuwa karibu nao,” alisema Jaji Mihayo.Mpango mkakati huo umefadhiliwa na Mfuko wa Asasi za Kiraia na Taasisi ya 2000 Agenda Participation.




NAOMBA COMMENTS ZENU.
 
Huo ndio ukweli tatizo lako lipo wapi? Cha msingi kama wananchi/serikali tuwachukulie hatua watu/viongozi (walioaminiwa na wananchi (trusted) wakaenda kusaini mikataba feki?.
 
Back
Top Bottom