Hofu sasa yasambaa uchumi kuporomoka
na Mwandishi Wetu - Tanzania Daima
na Mwandishi Wetu - Tanzania Daima
KUMEKUWA na hisia za kuporomoka kwa hali ya uchumi miongoni mwa wananchi wa kada mbalimbali katika siku za hivi karibuni kutokana na taarifa mbalimbali za mwenendo wa mambo.
Moja ya kundi linaloonekana kukumbwa na wasiwasi huo ni la wanasiasa, hususan wa kambi ya upinzani, wabunge na wafanyabiashara, ambao katika miezi ya karibuni, wamekuwa wakifuatilia kwa karibu mwenendo wa mambo serikalini.
Hata hivyo, hali hiyo imekuwa ni tofauti kidogo kwa wanasiasa kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wale wa serikali, ambao wamekuwa wakifanya juhudi kubwa kuwatoa hofu wananchi.
Taarifa mbili za Waziri wa Fedha, Zakia Meghji kwa wabunge, akianzia na ile aliyoitoa mbele ya Kamati ya Fedha na Uchumi na ya hivi karibuni kabisa aliyoiwasilisha Dodoma siku chache baada ya kumalizika kwa vikao vya bunge, zote zimeonekana kuongeza maswali mengi kutoka kwa wawakilishi hao wa wananchi.
Aidha, ripoti za kila mwezi za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na ile ya miezi mitatu mitatu, ni jambo jingine ambalo limezusha udadisi mkubwa kuhusu mwenendo wa uchumi wa taifa katika siku za hivi karibuni.
Kama hiyo haitoshi, Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali iliyotolewa hivi karibuni na kusababisha Rais Jakaya Kikwete alazimike kuitisha kikao cha Baraza la Mawaziri kuijadili kabla ya kufanya hivyo tena na watendaji wakuu serikalini kutoka mikoa na wilaya zote nchini, ni suala jingine ambalo nalo limetia chachu ya maswali kuongezeka kuhusu hali ya sasa ya uchumi.
Katika kuonyesha kuendelea kuguswa na mwenendo huo wa mambo, kesho Jumatatu, Rais Kikwete kwa mara nyingine tena, anakutana na watendaji katika serikali za mitaa jijini Dar es Salaam ili kuijadili ripoti hiyo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali.
Mbali ya hilo, taarifa ya Machi mwaka huu ya BoT inayoonyesha kuwa mfumuko wa bei katika mwezi Februari ulipanda hadi kufikia asilimia 7.3 kutoka 7.0 mwezi Desemba, nayo imeendelea kuzusha maswali mengi kutoka miongoni mwa wadau wa uchumi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya BoT, matumaini kidogo yanayoonekana kuwapo, ni takwimu zinazoonyesha kwamba, kupanda huko kwa mfumuko wa bei hakukuhusisha bidhaa za vyakula ambavyo vyenyewe vilishuka kwa asilimia 1.1.
Hata hivyo, kupanda kwa mfumuko kwa bidhaa zisizo za chakula hata kutoka asilimia 7.4 mwishoni mwa Januari hadi kufikia asilimia 8.8 mwishoni mwa Februari, kunaweza kutoa picha ya kuendelea kupanda kwa vitu kama mafuta ya petroli na bidhaa nyingine zinazoagizwa kutoka nje ya nchi mbali ya chakula.
Taarifa nyingine kutoka katika mkutano wa wabunge wote uliokaa chini ya Waziri Mkuu Edward Lowassa mjini Dodoma hivi karibuni, zilionyesha hali ya wasiwasi miongoni mwa wabunge.
Kikubwa kilichowafikisha hapo, ni takwimu zilizotolewa na Meghji mbele yao, zilizokuwa zikionyesha kuwa, kupanda huko kwa mfumuko wa bei kumekuwa ni jambo linaloendelea kwa miezi 16 tangu Serikali ya Awamu ya Nne iingie madarakani.
Kupanda kwa mfumuko kutoka asilimia 5.7 mwishoni mwa mwaka 2005 na kufikia asilimia 5.9 Septemba mwaka jana, kabla ya kupanda zaidi na kufikia asilimia 7.3 mwezi Februari, ni mambo ambayo yalikuwa yakitoa picha kwamba, hatua zisipochukuliwa, basi ile ndoto ya kuendelea kuwa na mfumuko usiofikia asilimia 10 inaweza ikatoweka.
Aidha, kuzidi kuongezeka kwa deni la nje ambalo Tanzania inadaiwa kutoka sh trilioni saba hadi kufikia tisa, hata pamoja na mafanikio makubwa tuliyoyapata ya kufutiwa madeni na wahisani mbalimbali chini ya Mpango wa Kuzipunguzia Madeni nchi maskini zaidi duniani (HIPC), ni jambo jingine linaloongeza wasiwasi huo.
Meghji aliyekuwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Bajeti ya Serikali katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2006/2007, alizitaja sababu za kupanda kwa mfumuko wa bei kuwa ni ukame ambao ulisababisha upungufu wa chakula, mgawo wa umeme na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.
Taarifa hiyo ya Meghji ilionyesha pia kwamba, mapato ya nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2006/2007 yalifikia sh bilioni 1,311.697 kiasi ambacho ni asilimia 53 ya lengo kwa mwaka mzima.
Aidha, katika kipindi cha Julai mwaka jana hadi Februari mwaka huu, mapato ya ndani yalipanda hadi kufikia sh bilioni 1,733.085 kiwango ambacho ni asilimia 70.4 ya makadirio ya mwaka mzima.
Hata kabla ya taarifa hiyo ya Meghji, kikubwa ambacho kimeongeza wasiwasi kuhusu mwenendo wa uchumi, ni taarifa kwamba, serikali ilikuwa imetumia zaidi ya shilingi bilioni 900 (karibu trilioni moja) isivyo.
Hata kabla hilo halijabainishwa, taarifa ambazo wabunge walikuwa wamezipata kabla ya mkutano wao uliomaliza hivi karibuni, kwamba serikali ilikuwa ikikabiliwa na nakisi ya shilingi bilioni 650 katika bajeti yake, ni moja ya mambo ambayo yameendelea kuacha maswali mengi kuhusu mwenendo wa uchumi wa taifa.
Ripoti ya miezi mitatu ya BoT iliyoishia Septemba mwaka jana, iliyokuwa ikionyesha kuwapo kwa nakisi ya shilingi bilioni 341.1 katika bajeti, kiwango ambacho kilikuwa kimepungua kutoka nakisi ya shilingi 394.3 ya katika kipindi kilichokuwa kikimalizikia Juni mwaka 2006, nayo ilikuwa ni sehemu nyingine ya maswali kutoka kwa wabunge kwa serikali wakati wa kikao cha Kamati ya Fedha na Uchumi, mwezi uliopita.
Aidha, ripoti nyingine ya BoT ya mwenendo wa kiuchumi iliyokuwa ikiishia Desemba mwaka jana huo huo, kipindi cha miezi mitatu tu baada ya ile ya awali, ilikuwa ikionyesha kuwa, nakisi katika bajeti (ukiondoa misaada ya wahisani) iliongezeka hadi kufikia shilingi bilioni 367.9 kutoka kiwango cha shilingi bilioni 341.1 cha mwezi Septemba.
Aidha wasiwasi kuhusu mwenendo wa mambo ulibainishwa na wabunge hao wakati Waziri Meghji alipokutana na wajumbe wa kamati hiyo jijini Dar es Salaam.
Habari ambazo Tanzania Daima imezipata kutoka miongoni mwa wajumbe wa kamati hiyo zinaeleza kuwa, Meghji alilazimika kuwatoa wasiwasi huo wabunge baada ya mmoja wao kutaka kujua iwapo ni kweli, serikali ilikuwa ikikabiliwa na tatizo la nakisi katika bajeti yake iliyochangiwa kwa kiwango kikubwa na matumizi makubwa ya viongozi.
Taarifa ambazo baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo walizipata kabla ya Waziri Meghji kukutana nao, zilikuwa zikieleza kuwa matumizi yanayoweza kuzuilika ya serikali katika kipindi cha nusu ya kwanza cha mwaka 2006/7, yalikuwa yameongezeka kwa asilimia 25.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, ongezeko hilo ni kubwa zaidi kuliko kiwango cha asilimia sita kilichoainishwa chini ya Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupambana na Umaskini (MKUKUTA).
Mwenendo huo wa mambo ndiyo ambao sasa unaanza kuiweka Serikali ya Awamu ya Tatu iliyokuwa ikiongozwa na Mkapa ionekane kuwa mfano bora kabisa wa kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za serikali.
Mapokezi makubwa aliyoyapata Mkapa mwenyewe wakati alipowasili katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam kuhudhuria sherehe za Muungano Alhamisi wiki hii, ni sehemu tu ya ushahidi wa namna wengi wanavyoanza kutambua misingi imara ya kiuchumi aliyoiacha, ambayo sasa kumekuwa na wasiwasi kuwa imeanza kuyumbisha