HESLB Wanavyotafuna Mikopo na Uchunguzi wa Bodi 2011

Hivi hii ripoti naweza kuichapisha na kumtumia kiongozi mmoja hivi au ndio mambo yana haki za kunakili?


Kwa memory zangu Mzee Mwanakijiji alishawahi kuruhusu huko nyuma. Ila nadhani angependa unampa nani.. Kama sivyo tafadhali anisahihishe
 
Haya mambo ya ukabila ukabila hata sielewi hivi ndio kubadili mada kiujanja nini? Mimi nataka kujua kama hawa wanafunzi wamepewa au kugawiwa mikopo zaidi ya mara moja, ni nani yuko kwenye huo mgao?
 
Sasa itakuwaje kama watu wa bodi wakaona hii ripoti na kuamua kufunga zile batch zao walizoweka kwenye mtandao?
 
Nimeipitisha hii ripoti mikononi mwa watu wachache hapa DDM midomo ilivyokuwa imeachama utadhani watu wameona mzuka. Kazi nzuri sana, ila walikuwa wanauliza umepataje majina haya?
 
..balaaa tupu kama ni kweli,lakini ujanja kama huo upo siku nyingi sana pale TZ kuanzia hapo mpaka wizara ya Fedha kwa wanafunzi wa IFM ,kule hakuna haki kabisa maana mikopo ukijua mtu tuu unatoa kidogo dogo unapata au any bosi ukimjua umepeta...huku wenye Division one wakipigwa nje...rushwa tupu na hao PCB ndio wajinga kazi yao ni kutumia pesa za unga za polisi kukamata ambavyo najua haitasaidia chochote in long run,ile nchi inabidi isafishwe kwa kutumia Technology kwenye system yetu kubana holes kama hizo...tukitegemea kina MSOLA hatutafika popote
 
Nasikia Msolla amepata ripoti na ana iplay down kuwa ni makosa ya kibinadamu tu. Kuna watu wamempania kweli.
 
Mwanakijiji,
.....umefanya kazi nzuri sana. Nategemea juhudi zako zitawezesha hawa vijana walioko Ukraine wapate udhamini wa serikali.

Mimi naamini hawa vijana wamekwenda huko kutafuta ELIMU. Vijana wangekuwa na nia ya kutafuta "maisha" au "kuukata," basi wangekwenda nchi za magharibi.
 
Thanks Mwanakijiji!.Naomba uniwie radhi kwani nimeipitisha Ripoti hii kwa baadhi ya Wabunge bila idhini yako ili wambane huyu Msolla atakaposoma Bajeti yake Alhamis,ni vizuri pia Spika aione Ripoti hii kabla ya hiyo Alhamis.Kuna baadhi ya Wabunge wanadai Bajeti ya huyu Muungwana Profesa itakuwa na vikwazo vingi!Shukran Mkuu kwa Ripoti hii.
 
Haya ndo mambo Mkuu Mwawado!
Lakini wabunge wataweza kumbana au ndo yale yale ya kuitwa chemba na Lowassa na kupigwa mkwala?
 
UTETEZI WA BODI YA MIKOPO, MAJIBU YAO YATHIBITISHA UFISADI.

MJENGA HOJA

Kwanza kabisa sina budi kutoa shukrani za dhati kwa Mkurugenzi wa Bodi ya Mikopo Bw. George Nyatega kwa kitendo chake cha kujaribu kutoa majibu ya makala yangu niliyoandika wiki iliyopita yenye kichwa cha habari “Twaweza kumuamini Prof. Msolla – Bodi ya mikopo kilele cha ufisadi”. Jaribio lake hilo ambalo bila ya shaka liliandikwa kwa uangalifu mkubwa limenigusa moyo na kunionesha kuwa sisi kama Watanzania tunaweza kuwa na mjadala wa wazi katika kujaribu kuisogeza mbele kimaendeleo nchi yetu. Licha ya sehemu chache katika majibu yake ambapo anahoji nia na uzalendo wangu nina uhakika Bw. Nyatega na wenzake wanaelewa kuwa lengo langu siyo kuichafua bodi hiyo au majina ya watu bali kuonesha uchafu wa bodi hiyo na kutaja majina ya watu ambao wanahusika na uchafu huo. Hivyo siyo lengo langu hata kidogo kuwachafua, bali kunyoosha kidole dhidi yao na kusema wamechafuka, wasafishwe. Hata hivyo, kwa vile amehoji nia na kusudi la makala yangu na kwa kukosea amehitimisha kuwa lengo langu ni “kuchafua majina ya watu” ninapenda kutumia nafasi hii kueleza ni kwanini niliandika makala zangu mbili zilizotangulia kuhusu Prof. Msolla na baadaye kuihusu Bodi.

Kwanza kabisa lengo la makala yangu ni kuonesha kuwa kuna tatizo kwenye bodi ya mikopo, tatizo ambalo limechangia kupotea kwa mamilioni ya fedha kutokana na mfumo mbaya wa utoaji mikopo. Mifano niliyotoa (nitaelezea tena baadaye) ilikuwa na lengo la kuonesha kuwa madai ya kuwa bodi ni chafu na ina mfumo mbaya siyo madai ya mtu asiyejua nini kinaendelea bali yanatokana na uchunguzi yakanifu.

Pili, na kubwa zaidi lengo langu ambalo Bw. Nyatega hakujaribu kulikanusha ni kuwa uongozi wa Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu umeshindwa kabisa kuipa uongozi bodi hii licha ya wao (wizara) kukiri mapungufu mbalimbali (angalia makala yangu ya kwanza). Kinara wa ukosefu wa uongozi huo ni bosi wa Bw. Nyatega yaani Waziri Prof. Peter Msolla. Ni madai yangu kuwa matatizo mengi yanayotokea kwenye bodi leo hii na yaliyotokea hadi sasa yametokana na uzembe wa Prof. Msolla na kiburi cha kutotaka kuyakabili matatizo hayo moja kwa moja. Licha ya kwamba anayajua matatizo ya bodi Prof. Msolla na wasaidizi wake wameshindwa kabisa kutafuta mbinu ya kuyatatua. Tatu na mwisho kabisa, katika kuandika makala yangu nilitaka kuonesha kuwa ni kutokana na uchafu wa bodi na kushindwa kwa Prof. Msolla kuongoza ndio maana leo hii tuna watoto wetu waliokwama Ukraine, kwa kisingizio cha “waliondoka wenyewe”. Hili “nitaliibua” tena baadaye.

Hayo ndiyo yalikuwa malengo ya makala zangu zilizotangulia na yanaendelea kuwa malengo ya makala hii ya sasa. Hata hivyo jambo moja limenisikitisha katika majibu ya Bw. Nyatega. Katika majibu yake yote ya ukurasa wa nane, Bw. Nyatega ameshindwa kuonesha uungwana wa kunishukuru kwa kumsaidia kuiangalia kwa ukaribu bodi anayoingoza na kusahihisha makosa au mapungufu niliyoyaonesha. Jinsi alivyoandika ni kana kwamba mimi nina kusudio baya na bodi au nchi yangu na ni yeye ndiye mzalendo pekee aliyebakia. Kwa vile nimewasaidia kutambua makosa na matatizo mengine angeonesha angalau uungwana wa kushukuru badala ya kudhihaki juhudi zangu kwani wakati yeye analipwa kufanya anachofanya mimi nafanya kwa kujitolea. Hata hivyo, kama hamaanishi shukrani hizo, sizihitaji lakini nitaendelea kufafanua mambo mengine bila kutarajia shukrani yoyote kwani walisema waswahili kwa usahihi kabisa kuwa “shukrani ya punda ni mateke”. Nina uhakika hata hivyo kuna watu ambao wananishukuru kwa kuthubutu kusema “mfalme hajavaa nguo”.

Baada ya kusema hayo, hebu tuangalie majibu ya bodi hii na kama majibu haya yanaweza kuingia akilini mwa mtu yeyote mzima na kama katika majibu yao wamejibu kwa uhakika hoja nilizojenga. Ndugu zangu, majibu ya Bw. Nyatega ni ya mtu aliyekurupushwa, yenye kujikanganya, yasiyo na ukweli na kwa hakika ni majibu yenye lengo la kuipotosha jamii na yenye kujaribu kujisafisha. Ni majibu ya mtu anayejaribu kupaka makaburi rangi za kumeremeta kumbe ndani yake ni mifupu mitupu! Kwa bahati mbaya, wamekosea mtu wa kumjibu kwani wakati wengine wanakubali majibu ya bodi kama walivyokubali majibu ya Hosea, Gesimba, na Balali, sisi wengine majibu yao ndio yanatupa maswali mengi zaidi na ya kina kwani majibu hayo siyo majibu bali ni majaribio ya kujibu maswali magumu. Ni majaribio yaliyoshindwa na nitumie nafasi hii kuonesha ni jinsi gani majibu ya Bw. Nyatega hayana mantiki na yenye kukusudia kuficha kitu.

Kutengewa mikopo na kugawiwa mikopo (loan allocation & loan disbursement)
Bw. Nyatega katika jaribio lake la kujibu hoja zangu anajaribu bila mafanikio kutumia maneno ya Kiingereza kutofautisha mambo mawili lakini hata hivyo ameshindwa kuonesha uhusiano wa mambo hayo. Je mtu anaweza kutenga kitu ambacho hana? La hasha! Na je mtu anaweza kuwagawia watu kitu ambacho hajakitenga kwa ungalifu? La hasha. Katika kuelezea hili suala Bw. Nyatega amedhihiria udhaifu mkubwa wa bodi, anasema hivi kuhusu suala la kutengewa mikopo na kugawiwa mikopo, “kupangiwa kupewa mkopo (Loans Allocation) hufanyika mwanzoni mwa mwaka wa masomo, baada ya Bodi kupata matokeo ya udahili kutoka vyuo vya elimu ya juu na pia kutoka kwa Kamisheni ya Vyuo Vikuu Tanzania (Tanzania Commission for Universities - TCU). Baada ya uchambuzi wa waombaji, kulingana na vigezo, Bodi hupanga mikopo kwa kila mwombaji kwa kila Chuo na taarifa hiyo hutolewa kwa njia ya tovuti ya Bodi ili iwafikie wahusika wote.” Na baada ya hapo Bw. Nyatega anasema “Bodi huendelea na uchambuzi zaidi kabla ya kufanya malipo “Disbursements”.

Kwa maneno mengine ni kuwa wao wanatumia majina yaliyotumwa na vyuo na TCU kupanga mikopo hiyo na baadaye wakiishayachambua ndio wanagawa hizo fedha. Katika majibu yake hayo bila ya shaka tunakutana na mambo mawili makubwa. Wanapopatiwa majina ya waombaji na wanapokubali kuwatengea fedha kabla ya kuhakikisha waombaji ni kina nani, wamefungulia ghala la ufisadi. Hii inajibu swali la mwanafunzi mmoja aliyeomba vyuo vitatu au vinne kukubaliwa mikopo mara hizo zote. Kwa kitendo cha bodi kutenga fedha hizo kwa kila mwombaji aliyeyedailiwa bila kuhakikisha kama ni “multiple allocations) ina maana fedha hizo zipo na zinatengwa zaidi ya mara moja. Huwezi kutenga fedha au kupanga matumizi ya fedha ambazo hauna. The board does not allocate fanthom money! Hivyo wanapompangia Juma Mdoe (jina la kubuni) aliyeomba mkopo kwenye vyuo vitatu Shs milioni 3 kwenye kila chuo, basi Juma atakuwa ametengewa/amepangiwa/amekuwa “allocated” milioni tisa. Sasa kama Juma ataamua kwenda chuo kimojawapo na siyo vile vingine, basi kuna Shs. Milioni sita ambazo zitakuwa hazikutumika. Swali kubwa ni nini kinafanyika kwa fedha hizi? Ni kutokana na uchunguzi wangu ndio nimeonesha kuwa kuna zaidi ya wanafunzi 500 ambao kwa mwaka uliopita wa 2006/2007 walitengewa mikopo zaidi ya mara moja.

Hili linatuleta kwenye neno la pili nalo ni “kugawa mikopo” (Loan disbursement). Kwa mujibu wa Bw. Nyatega uchambuzi hufanyika na baadaye wanafunzi wanapewa mikopo hiyo. Na kwa ujasiri mkubwa akaniambia kuwa ningetumia taarifa za waliogawiwa mikopo kuonesha kama wamepewa au la. Kwa kutumia ujanja amejaribu kulifanya jambo la “loan allocation” kuwa ni “non-issue”. Jaribio lake hilo lilifanywa pia na Prof. Msolla kwenye jibu lake Bungeni mapema kwenye kikao kinachoendelea sasa Dodoma. Swali kwetu ni kuwa lipi ni jambo kubwa, loan allocation au loan disbursement? Jibu langu ni hilo la kwanza. You can not disburse money you haven’t allocated! Ili waweze kugawa pesa ni lazima wawe wamezitenga. Hivyo ufisadi hauanzii kwenye kugawa bali kwenye kutenga. Kwa maneno yake yeye mwenyewe bodi imewalipia watu ambao hawako vyuoni, na waliweza kufanya hivyo baada ya kuwatengea. Ufisadi mkubwa katika bodi hauko kwenye kugawa pesa kwani ni rahisi kugawa fedha kwa mtu wanayemtaka kuliko kuangalia wamemtengea nani fedha. Hivyo tatizo ni zile pesa ambazo ziliombwa kwa mwanafunzi zaidi ya mmoja na zikatengwa lakini hazikutumiwa zilifanyiwa nini? Je, Bw. Nyatega anataka kuwahakikishia Watanzania kuwa hakuna afisa wake hata mmoja ambaye “amejipongeza” kwa mikopo ya wanafunzi? Isipokuwa kama Bw. Nyatega atasema kuwa fedha zinapotengwa haina maana kuwa zipo.

Of course, hawezi kusema hivyo kwani yeye mwenyewe anasema hivi “Bodi inakiri kwamba kutokana na mkanganyiko wa “Double Admissions” katika vyuo vikuu mwanzoni mwa mwaka wa masomo wa 2006/2007 kulitokea ‘Double Loan Allocations’ ambazo hata hivyo yalisahishwa kwa kiwango kikubwa wakati wa kufanya malipo (Loan Disbursements).” Na anasema “yalisahihishwa kwa kiwango kikubwa” kwa maana ya kwamba hayakuondolewa yote. Hivyo kupuuzia tatizo la “double allocation” kana kwamba siyo jambo zito ni ufunguzi wa double payment. Kwa maneno mengine, Mkurugenzi wa bodi anakubaliana na mimi kuwa kuna tatizo la ufisadi kwenye bodi anayoiongoza.

Hata hivyo Bw. Nyatega anajaribu kuelezea chanzo cha tatizo hilo (la double allocation) na anapofanya hivyo anaendelea kuthibitisha maneno yangu kuwa bodi jinsi ilivyo sasa ni “kilele cha ufisadi”. Anataja sababu tatu lakini zote ziko nusu nusu. Sababu yake ya kwanza kuwa chanzo cha tatizo ni udahili wa zaidi ya mara moja ni tatizo linaloonesha kuwa bodi haina utaratibu wa kuzuia jambo hilo kutokea tena mwaka huu. Anaposema kuwa bodi ilipata majina baadaye ya wanafunzi halisi anashindwa kutuambia kama walipata majina hayo baada ya kugawa fedha au baada ya wanafunzi kuhamia vyuo vingine? Na kama walishagawa pesa zaidi ya mara moja, wana uhakika gani kuwa fedha hazikuishia mifukoni mwa watu wachache katika bodi yake au vyuo husika?

Chanzo cha pili anachodai ni kuwa tatizo ni muda mfupi wa kuchambua majia ya waombaji. Hili nalo ni uthibitisho wa uzembe wa bodi. Kama bodi haina muda wa kufanya uchambuzi wa kina kwanini basi wakubali kupokea mabilioni ya fedha za walipa kodi wa Tanzania na kuzigawa kama nyugu? Kama hawana muda wa kufanya uchambuzi unaostahili kwanini tuwaamini kuwa majina waliyoyapatia fedha ni majina halali?

Katika chanzo cha tatu Bw. Nyatega analaumu mfumo mbaya wa kutokuwa na namba za kuwatofautisha wanafunzi. Madai kuwa kutokuwepo kwa namba maalum za kutofautisha wanafunzi zimechangia sana kwenye tatizo ni kujaribu kuficha ukweli. Kila mwanafunzi anayemaliza kidato cha sita Tanzania anapatiwa namba ya mtihani na kituo alichofayia mtihani; kwanini wasitumie namba hiyo? Je, wasomi wote wizara ya Elimu ya Juu na hapo Bodi wameshindwa kabisa kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo na matokeo yake wameamua kufanya mambo bila uwezo wa kutofautisha waombaji? Ina maana kwa mamilioni yote ya fedha wanazotengewa na serikali wameshindwa kutafuta program ya kompyuta ambayo inaweza kutoa alama nyekundu pale majina yanafanana au namba zinazofanana zinapojitokeza na hivyo kulazimisha manual oversight? Kama huu siyo ubovu na uchafu tuupe jina gani? Kwa kuwaambia kwamba hapa kuna tatizo kwanini wafikirie lengo langu ni kuchafua jina la mtu? Wiki chache zijazo nitaandika jinsi ya kuiboresha bodi yetu ya mikopo baada ya kuivunja hii ya sasa. Lengo siyo kuonesha uchafu tu bali pia kutoa mawazo ya jinsi ya kuundoa uchafu huo.

Hata hivyo hakuna kitu cha kufurahisha kama maelezo ya Mkurugenzi huyo kwenye kipengele cha 2.2 cha majibu yake. Hapa nitamnukuu neno kwa neno. Bw. Nyatega katika kuelezea jinsi bodi ilivyo makini kuhusu matatizo niliyoyaanisha kwenye makala yangu anasema “Serikali kupitia Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, imeshachukua hatua ya kubainisha kama kulikuwa na ulipaji hewa wa mikopo ya wanafunzi au “Double Payments” na kazi hii imepewa Taasisi ya Kuzuia Rushwa (Prevention of Corruption Bureau– PCB) ambayo inaendelea na uchunguzi na endapo itagundulika kuwa kweli basi hatua zifaazo zitachuliwa ipasavyo.” Kwa hili nawapongeza sana, hata hivyo hatua hii imeanza kuchukuliwa lini? Baada ya makala yangu au kabla? Kama ni kabla ni kitu gani kiliwasababishia kutaka kufanya uchunguzi huo? Kama ni baada ya makala yangu ina maana hoja zangu zilikuwa na uzito na siyo za kuchafua watu! Na kama ilikuwa kabla mbona watanzania hawakuambiwa kuhusu suala hili, kwanini lilifanywa kwa usiri hadi makala yangu ilipotoka ndipo Bodi inakiri kuna uchunguzi?

Maelezo kuwa PCB wameombwa wafanya uchunguzi ni maelezo duni. Watanzania hawaiamini PCB isipokuwa viongozi wa serikali tu. Kama uchunguzi wao wa Richmond, BOT n.k ni ishara yoyote, basi ni rahisi kujua Bw. Hosea atatoka na taarifa ya namna gani. Kwa vile sitaki watanzania wasubiri muda mrefu matokeo ya uchunguzi huo, ngoja niwapatie preview ya maelezo kuhusu ufisadi bodi ya mikopo. PCB itakapotoka na uchunguzi wake watagundua kuwa kulikuwa na matatizo ya kimfumo na kimuundo ya hapa na pale na matatizo madogo madogo ya kiutendaji. Hata hivyo watagundua kuwa matatizo yote hayo hayana maana ya ufisadi na hivyo watasema kuwa hakukuwa na double payments na hakukuwa na rushwa ya aina yoyote. Vyombo vyetu vya habari vitapiga makofi, Msolla atashingiliwa na yote yataisha kinyemela. Kwa ufupi hakuna atakayewajibishwa kwani hakuna ufisadi bodi ya mikopo. Wakija na jibu tofautina hilo nililosema nitawaomba msamaha.

Mifano niliyotoa na majibu ya bodi
Katika majibu ya bodi nimefurahi kuwa kuna mambo kadhaa ambayo wameyakiri. Kwanza suala la Yesse C Msechu na Allawi R Kihalla. Bodi inakiri kuwa vijana hawa walikubaliwa mikopo mwaka 2005/2006 siyo 2006/2007 na bodi inaeleza kwa uhakika kuwa wanafunzi hawa ni “halali” na kuwaelezea kuwa “kwa mwaka 2006/2007 hao ni wanafunzi wanaoendelea na masomo.” Kwa mtu ambaye anaweza kumiss point anaweza kufikiri kuwa wanafunzi hawa ni wa mwaka wa pili. Tatizo ni kuwa wanafunzi hawa wako mwaka wa kwanza. Sasa kama walikubaliwa mikopo mwaka 2005/2006 iweje mwaka 2006/2007 wawe wanafunzi wa mwaka wa kwanza? Wanapotafuta jibu wakumbuke kuwa wanafunzi wale wengine waliowakana wapo vyuo hivyo hivyo na wanawahafamu wenzao “walioneemeshwa” na bodi.

Zaidi ya yote, wakati Bw. Nyatega anasema kwa uhakika kuwa wanafunzi hawa walikubaliwa mkopo mwaka 2005/2006 na sasa wako Ukraine, bodi yake ikamtengea tena Yesse Shs. 840,000 kwa mwaka wa kwanza hapo UDSM katika bajeti ya 2006/2007 (Batch 9). Bila ya shaka atasema hawa ni watu wawili tofauti na wamepiga simu UDSM na kuhakikisha kuwa kuna mwanafunzi mwenye jina hilo yupo. Nawapa changamoto UDSM wamlete hadharani mwanafunzi huyo na nitakiri nimekosea.

Tukibakia kwenye suala hili hili, kama wanafunzi hawa walikubaliwa mwaka 2005/2006 na siyo 2006/2007 na mikopo yao ikaheshimiwa kwanini wanafunzi wenzao waliokuwa nao kwenye batch zile zile wamekataliwa? Bila ya shaka Bw. Nyatega atasema hawa 24 “hawakukamilisha taratibu” fulani. Hata hivyo hadi leo hii siyo yeye, siyo Gesimba wala siyo Msolla ambaye ameweka hadharani taratibu hizo ambazo watoto wetu 24 hawakuzikamilisha. Ni taratibu gani hizo ambazo zilikuwa ngumu kiasi hicho hadi kusababisha vijana wasipewe mkopo na kutelekezwa? Inawezekana kuwa vijana hawa hawakutaka kuomba fedha za nauli toka bodi ili wasijiongezee deni na badala yake wakajitafutia nauli zao wenyewe na hivyo kuwanyima watu ulaji? Na kitendo cha wao kuondoka bila “nauli” za bodi kiliwaudhi kina Mbegu, Ruta, na Temu? Kwa wanafunzi wengi wanaosoma nje ya nchi suala la nauli ni suala ambalo limewapa ulaji mwingi watu wa bodi. Ningekuwa na muda ningeanza kuchambua hilo, ninawawekea kiporo kwa sasa.

Mwanafunzi Adiel Daniel Mushi. Bodi inasema kuwa mwanafunzi huyu yupo UDSM ambako malipo yameshafanyika. Na anasema madai yangu ni “uzushi”. Kama hilo ni kweli je mwanafunzi aliyeomba mkopo kwenda kusoma Ukraine na akatengewa milioni 3 (batch 10) ni nani huyo? Kwa vile Bw. Nyatega amesema kuwa COET wamethibitisha mwanafunzi huyo yupo, naomba kutoa changamoto nyepesi kuwa pindi wakisoma makala hii wamlete Adiel Daniel Mushi hadharani na siyo mtu anayejiita hivyo, na ale kiapo kwa kuonesha hati ya kuzaliwa kuwa ni yeye na hajulikani kwa jina jingine mahala kwengine; wakifanya hivyo nitakiri nimekosea. Kama bodi haitafanya hivyo, naomba COeT wamlete mwanafunzi huyo hadharani ndani ya siku tatu tangu kusoma makala yangu. Na zaidi ya yote, Bw. Nyatega anaweza kuelezea iweje mtu huyo huyo atengewe tena fedha nyingine kwenye chuo hicho hicho na kozi hiyo hiyo na hakuna mtu wa bodi aliyeshtuka? Kama huo siyo uzembe na kilele cha ufisadi tuuite jina gani?

Mwanafunzi Davis Dennis Kanyika. Mwenyekiti wa bodi anasema kuwa kijana huyu alikuwa asafiri mapema mwaka jana na ilikuwa kabla ya bajeti mpya. Sasa fedha alizotengewa zilitoka bajeti gani kama siyo ya 2005/2006. Ni kitu gani kilisababisha kijana huyo apewe mkopo wa 2005/2006 mwaka 2006/2007 na wale vijana 24 wanyimwe? Bw. Nyatega una mengi ya kujibu. Kama alikubaliwa 2005/2006 na hakuweza kuanza masomo wakati ule ilikuwaje bodi imlipie kwa mwaka wa 2006/2007

Kina Charles J Temba. Mwenyekiti wa bodi anasema kuna wanafunzi wawili kwenye vyuo viwili tofauti (SUA na MIST) ambao majina yao yanafanana na wote wameshalipiwa fedha zao. Na anasema kuwa kuna mwanafunzi mwingine mwenye jina hilo ambaye alipangwa kusomea Mzumbe ambako alipelekewa fedha. Hata hivyo anakiri kuwa mwanafunzi huyo hakutokea huko Mzumbe na fedha zimerudishwa kwenye Bodi. Je, fedha hizo zimerudishwa baada ya mimi kusema jina lake hadharani au kabla? Mkurugenzi wa bodi anakiri kuwa vyeti vilivyotumika kumdahili Charles Temba wa SUA ndivyo vilivyotumika kumdahili yule wa MIST lakini anasema kama asiye na uhakika wa ufisadi kuwa “Ikibainika kwamba kulikuwa na udanganyifu, hatua za kisheria zitachukuliwa.” Je nikimwambia kuwa kuna Charles J. Temba mmoja tu atakataa, kama anabisha naomba amlete yule wa MIST na yule wa SUA hadharani. Akifanya hivyo kwa ushahidi unaoweza kusimama mahakamani nitakubali nimepotoka.

Charles B. Temba wa Arusha. Kwa mujibu wa Bw. Nyatega ni kuwa mwanafunzi huyo ni tofauti na Charles J Temba na anakiri kuwa amelipiwa karibu shilingi milioni 2 huko Arusha. Ninapendekezo jepesi kwa Bw. Nyatega. Wakutanishe wanafunzi hawa watatu hapo MAELEZO. Vinginevyo kiri kuna ufisadi kwenye bodi unayoongoza na wewe na Prof. Msolla hamstahili kuendelea kushikilia usukani.

Mwanafunzi Salim Chadoe aliyetengewa fedha mara mbili wanasema kuwa kwa sasa yuko Algeria. Je, zile fedha alizotengewa UDSM zimetumika vipi? Maelezo ya Chadoe yanalingana na maelezo ya bodi kuhusu wanafunzi Alistidia J. Rupia, Kazinja Patrick E, Ligunda Mary, Sophia Sokoni na Mohamed Matwera. Katika maelezo ya bodi ni kuwa wanafunzi wote hawa wote wako Algeria baada ya kukatisha masomo yao ya Udaktari hapo Tanzania. Wanafunzi waliacha masomo hayo ili waende kusoma “Kifaransa” huko Algeria. Bw. Nyatega bila ya shaka anatuona watanzania ni wavivu wa kufikiri. Nitawaacha wengine watafute hoja za suala hili maana kwangu haliingii akilini kabisa. Ili kutuliza maswali yangu ati anadai wanafunzi hawa watakatwa fedha hizo kwenye malipo yajayo. Sasa wakiwakatia fedha si watawasababishia mapungufu. Nashauri pesa hizo zikatwe kwa maofisa wa bodi hiyo waliozembea hadi kusababisha tatizo hilo, na ili kuonesha mfano wa kwanza awe ni Bw. Nyatega mwenyewe.

Mwanafunzi Exaud Chengule. Kwa ufupi Bw. Nyatega anasema kuwa huyu mtu hayupo na wanatafuta fedha alizokopeshwa zimeenda wapi. Je nikiwaambia kuwa mtu huyo hakuwahi kuwepo isipokuwa katika mawazo ya watu wa bodi atakataa. Na uchunguzi wa kumtafuta ulianza lini? baada ya mimi kuwaripotia au kabla. Je kwa kuwaonesha uchafu na uozo huo nimechafua majina yao au nimewasaidia kuwarahisishia kazi yao? Wajifunze kuonesha shukrani siyo kubeza juhudi za watu wanaowasaidia.

Wanafunzi Emmanuel Richard Kizigha na Emmanuel Richard Kizigha. Bw. Nyatega anasema kuwa wanafunzi hawa ni wawili tofauti lakini inaonekana kuna mmoja anatumia vyeti vya kufoji. Kama kuna mtu kafoji na wanagundua hilo baada ya mimi kuwatajia majina wanajua ni wangapi wanatumia majina ya kufoji na vyeti vya kufoji ambao sijawataja? Kumbuka nimewaambia ninao 500! Kama nisingewapatia hilo jina wangeweza hata kuanzisha uchunguzi? Kama huo wote sio uzembe na kilele cha ufisadi tuupe jina gani? Next time, kila ninapowapatia majina ya wanafunzi wenye mashaka na wakigundua kuna tatizo itabidi wanilipe! Uzalendo utanishinda na bodi inazo pesa bwelele.

Suala la wanafunzi waliotelekezwa Ukraine na serikali ya Kikwete
Bw. Nyatega kama walivyofanya kina Gesimba, mama Kabaka, na Prof. Msolla amerudia maneno yale yale ya kilaghai kuhusu suala la hawa wanafunzi ili kuzima tuhuma dhidi yao. Bw. Nyatega anasema kuwa wanafunzi hawa “walichagua kwenda Ukraine kwa taratibu zao wenyewe baada ya kushauriwa kutofanya hivyo. Suala hili limeshatolewa ufafanuzi na serikali na bodi ya mikopo mara kadhaa, hivyo, bodi haina haja ya kutoa maelezo ya ziada”. Kwa bahati mbaya sana, haja ya kufanya hivyo bado ipo.

Kama waliweza kuwapa mikopo vijana Yesse Msechu na Alawi Kihalla waliokubaliwa mikopo 2005/2006 kwenye batch zile zile na hawa 24 ni kitu gani kiliwafanya washindwe kuwapa mikopo hawa wengine? Madai ya kuwa vijana hawa 24 hawakutimiza taratibu fulani licha ya kutengewa mikopo, Bw. Nyatega awaambie watanzania ni taratibu gani hizo ambazo hawakuzitimiza?Na wao kama bado walishindwa vipi kuwasaidia vijana hawa kutatua matatizo hayo ili wasipate matatizo?

Kama vijana hawa waliweza kutafuta tiketi zao na hawakutaka kutumia mikopo ya tiketi, je hilo ni kosa kubwa la kusababisha wasipewe mikopo. Kama mimi ningekuwa Nyatega ningewashukuru vijana hawa kwa kuonesha mfano kuwa familia inaweza kupunguza deni la elimu ya juu kwa kuwatafutia vijana wao nauli badala ya kusubiri mkopo wa serikali. Bw. Nyatega, mwaka 2005/2006 mliwatengewa vijana hawa fedha, na baadaye kwa sababu mnazozijua nyinyi mkawanyima baada ya vijana hawa kununua tiketi zao na kwenda kuanza masomo, tunaomba uwaambie watanzania fedha zao mlizowatengea mwaka ule kiasi cha 72,000,000 ziko wapi?

Bodi na serikali imeendelea kudai kuwa vijana hawa “walishauriwa” wasiende huko Ukraine, lakini hadi hivi sasa haijatolewa sababu ya kwanini walishauriwa hivyo. Sababu ya Bilateral Agreement haiwezi kusimama kwani Yesse na Alawi walienda na wako vyuo hivyo hivyoj walivyokubaliwa vijana hawa. Iweje hiyo Bilateral Agreement iwahusu wanafunzi wote wa kitanzania walioko Ukraine isipokuwa hawa 24. Hawa vijana hawajakubaliwa kusoma sayari Zebaki ambako hatuna Bilateral Agreement nao!

Na katika kudai kuwa bodi iliwashauri wasiende hakuna kiongozi hata mmoja aliyetayari kusema ushauri huo ulitolewa lini, wapi, na nani. Namuuliza Bw. Nyatega na Prof. Msolla, ni barua gani waliyopewa wanafunzi hawa kuwa wasiende Ukraine? Ni tangazo gani la habari na kwenye chombo kipi lililowataka wasiondoke? Je yawezekana kuwa ushauri huo ulitolewa kwa mdomo (verbal) na hakuna maandishi yoyote? Kama lililotolewa kwa mdomo bila maandishi kwanini tusiamaini kuwa ahadi ya wao waendelee na safari nayo iliyotolewa kwa mdomo? Nakupa changamoto bw. Nyatega na wenzako wekeni hadharani ushauri huu ulikuwa upi, ulitolewa lini, wapi, na nani na ulitumwa kwa nani.

Suala la malipo yaliyofanyika Ukraine – uthibitisho wa ufisadi
Katika majibu yake Bw. Nyatega anasema vitu hivi kwamba kuna malipo yaliyofanyika kumhusisha Alawi Rajabu Kihalla yaliyofanyika tarehe 18/4/2006 kwa kupitia hundi namba 193426 yenye thamani ya Shs. 87,772,800 na yakihusisha wanafunzi wengine waliotangulia. Hata hivyo Bw. Nyatega anasema tena kuwa kuna malipo mengine yaliyofanyika 22/3/2006 (mwezi mmoja kabla ya yale ya Kihalla) kwa mwanafunzi David Dennis Kanyika (yakihusisha wanafunzi wengine) yenye thamani ya Shs. 87,772,000 kwa kutumia hundi yenye namba 193426. Jumla ya malipo hayo yote ni Shs. 175,544,800. Kwa kuangalia namba hizo tunakutana na matatizo yafuatayo.

- Namba za cheki zilizotumika ni zile zile. Hilo haliwezekani isipokuwa kama kuna mtu anataka kufanya malipo hewa.
- Kiasi cha fedha kilicholipwa kinakaribiana. Tofauti ni Shs. 800 tu.
- Wanaolipwa ni watu wale wale. Inawezekana vipi uandike cheki mbili zenye kiwango sawa na zenye namba sawa kwa wanafunzi wale wale isipokuwa kama unataka kuweka kiasi kingine pembeni?

Kama hiyo haitoshi, Bw. Nyatega anasema pia kuwa tarehe 19/1/2006 malipo yalifanyika yaliyomjumuisha Yesse Msechu (na wanafunzi wengine) kwa kupitia hundi namba 149736 yenye thamani ya Shs. 80,097,600. Kwa maneno mengine ndani ya miezi minne bodi yetu ya mikopo ililipa Shs. 255,642,400 kwa wanafunzi wasiopungua 85. Tukumbuke kuwa malipo haya yanatokana na bajeti ya 2005/2006. Je. Bw. Nyatenga anaweza kutupa orodha ya wanafunzi wote waliokuwa kwenye mgao wa mikopo ya mwaka 2005/2006 kule Ukraine? Je ana uhakika kuwa hakuna fedha zilizoishia mikononi mwa watu ambao siyo wanafunzi.

Tricky tricky!
Namuomba Bw. Nyatega awaeleze watanzania Bw. Francis kutoka Ubalozi wetu Moscow ni nani na anahusika vipi na malipo ya mikopo. Zaidi ya ya yote awaambie watanzania Bw. Constantine Mkami wa Ukraine anahusika vipi katika mchakato mzima wa wanafunzi wanaosoma pale Ukraine. Asipofanya hivyo kwa ukweli na uwazi nitamsaidia.

Suala la Sera.
Bw. Nyatega anasema kuwa Bodi yake haiko tayari kuwasaidia vijana hawa kwa sababu ya sera. Kuwa ni sera ya CCM kutowasaidia vijana hawa wa Kitanzania ambao walishakubaliwa mikopo kama Kihalla, Msechu Na Kanyika. Anasema kuwa ni sera ya CCM kutambua baadhi ya wanafunzi kwenye kwa sababu ya makubaliano ya nchi mbili na kuwakataa wengine kwa vile hawakutaka mikopo ya tiketi zao. Bw. Nyatega anachosema ni kuwa ni sera ya serikali ya Rais Kikwete kuwabagua vijana hawa kwa vile wameonesha manung’uniko yao hadharani na kudai haki yao hadharani. Na jinsi nilivyomuelewa Bw. Nyatega ni kuwa ni sera ya wana CCM na wabunge wao kutowatetea vijana hawa na kuwatafutia haki yao kwa vile tu wapinzani wamejitokeza kuwasaidia.

Ndugu zangu, sera hii ni ya kibaguzi, kibabe, na ya kizandiki. Ni sera ambayo haina budi kupigwa vita na kila mtanzania mwenye kuthamini elimu na mwenye kujali haki za wananchi. Haiwezekani watu wachache waje na sera mbovu kama hii na sisi tukawafumbia macho. Binafsi nasikitika kuwa hadi hivi sasa hakuna kiongozi yeyote wa CCM aliyejitokeza kuwatetea vijana hawa, hakuna mchungaji, askofu, walimu, NGO, n.k ambao wametaka serikali iwatimizie ahadi yao vijana hawa. Inaonekana tumekubali serikali iwabague vijana wetu kwa vile tu “hawakukamalisha taratibu fulani” za kusadikika. Sera hii ya CCM lazima ivunjwe na iondolewe vitabuni vinginevyo chama chetu kitakuwa kimetiwa tope kubwa na watu wa bodi. Nawashauri viongozi wa CCM waikane sera hii na kuwatendea haki vijana wetu. Vinginevyo, wajiandae kulipa gharama kubwa ya kisiasa.

Siwezi kuamini kabisa kuwa Rais Kikwete, Makamu wake na Baraza zima la Mawazirila serikali yetu limevumilia sera hii ambayo ina harufu ya nchi ya kibaguzi. Siwezi kuamini kuwa Rais anayetaka watu wasome elimu ya juu anafumbia macho suala hili na kuwaacha watuhumiwa wa ufisadi kumpa maelezo ya kilaghai ili kutetea unga wao. Kwa mara nyingine tena, natoa wito kwa Prof. Msolla kujiuzulu, Bodi ya Mikopo kuvunjwa mara moja na tume huru kuundwa kuchunguza ufisadi katika bodi hii. Ni wazi kuwa ni vigumu kwa serikali yetu kufanya hivyo lakini nimekunja vidole vyangu nikiamini kuwa kuna mtu mwenye dhamira safi Ikulu ambayo hakubali uonevu au ufisadi. Vijana hawa wanaonewa na wametelekezwa bure na watu wa bodi. Prof. Msolla anajua hivyo, Mama Kabaka na mama Katunzi wanajufa hivyo, Bw. Mbegu anajua hivyo, na Bw. Nyatega anafahamu hivyo. Na hatimaye leo hii, kila mtanzania anafahamu hivyo.

Kwa vile Bw. Nyatega amenitafutia majibu ya majina niliyoyaweka mwanzoni, nimeonelea nimuongezee majina mengine ili ayatolee ufafanuzi. Kila jina moja waweke kwenye akaunti ya wanafunzi wa Ukraine Shs. Milioni moja.

Rabson Mahenge, alitengewa (allocated) shilingi laki 980,000 pale Muhimbili kusomea Pharmacy (batch 12) na akatengewa shilingi 1,665,000 (batch 10) kwenye chuo hicho hicho kwa kusomea Pharmacy hiyo hiyo. Sasa Bw. Nyatega anaweza kutuambia kuwa pesa ililipwa mara moja. Sawa. Kwanini watenge mara mbili, aidha kuna uzembe wa kiutendaji au kuna mtu anataka “chenji”

Sifa Anyimike, ametengewa shilingi 295,000 kusomea Elimu hapo UDSM (Batch 10), lakini akatengewa 1,320,000 kusoma hapo hapo UDSM (batch 8). Huyo huyo Anyimike wetu, akakubaliwa kiasi kingine cha Shs. 540,000 kusoma chuo hicho hicho tena (Batch 6).

Helena Yomo. Kwa huyo nayo ni yale yale. Katika Batch 10 alitengewa Shs. 1, 320,000 kusomea Elimu hapo UDSM. Kwa vile bodi yetu ina makengeza ikatenga tena kiasi kama hicho kwenye batch 8. Na kama hiyo haikutosha mwanafunzi huyo huyo chuo kile kile akatengewa tena Shs 540,000 (Batch 6). Inawezekana Bodi yetu ya Bw. Nyatega watakuja na kusema hao UDSM kuna wanafunzi watatu wote wanaitwa Helena T Yomo na wote wanasomea Elimu, na bila ya shaka watasema wamezungumza na chuo na kuthibitishiwa kuwa wanafunzi wote watatu wapo.

Upendo V Chubwa. Huyu katika Batch 10 alitengewa na Bodi ya Nyatega Shs 295,000 kusomea Elimu hapo UDSM na wakati huo huo kwenye mwaka huo huo alitengewa 1,320,000 (batch 8) kusomea elimu hapo hapo UDSM. Na kwa vile kina Nyatega na wenzake hawajui jinsi kuendesha bodi hiyo wakaona hiyo haitoshi wakaamua kumuongezea tena 540,000 kwenye chuo hicho hicho kwenye kozi hiyo hiyo (batch 6).

Hivi kama si uzembe na uvivu unaweza kuelezea vipi kumtengea fedha mtu mmoja mara mbili kwenye batch ile ile huku jina lake likijirudia. Hii imetokea kwa wanafunzi wawili, Hamisi Mganda ambaye alitengewa Shs. 2,640,000 (DUCE) na Mwaveso Mbwana ambaye alitengewa kiasi kama hicho kwenye batch 10. Sasa kama majina mawili yanayofanana hayawashtui, nini kitawashtua?

Arton Kayombo. Huyu katika Bodi yetu hii ametengewa Shs. 1,320,000 hapo DUCE kusomea Elimu (batch 10) na kupitia bodi hiyo hiyo akatengewa tena kiasi hicho hicho kwenye batch 8. Sasa inawezekana kabisa kuwa mfumo wanaotumia ni mbovi kiasi cha kwamba majina yanajirudia rudia kwa bahati mbaya. Kama hili ni kweli ni kitu gani kinazuia watu wachache kujipongeza kwa fedha za umma?

Ndugu zangu bodi ya Mikopo ina matatizo na uongozi wake mzima hadi Waziri ni mbovu na unaohitaji kubadilishwa. Unganeni nami kumtaka Prof. Msolla na Bw. Nyatega na bodi nzima wakiongozwa na Bw. Mkono wajiuzulu kwa kuzoea uzembe, kuvumilia ufisadi, na kushindwa kuiongoza bodi hiyo ipasavyo. Mimi na wenzangu tumeanzisha utiaji sahihi wa ombi la kutaka Prof. Msolla ajiuzulu. Unaweza kuingia kwenye http://www.jamboforums.com kwa maelezo ya kuweza kusaini ukurasa huo wa kwenye mtandao.

Niandikie: mjengahoja@jamboforums.com
Nitumie ujumbe: + 1 248 686 2010
 
Just for the heck of it,send a copy to Ikulu na kwa Waziri Mkuu with a caption: Rais Jakaya Mrisho Kikwete Aione na Waziri Mkuu, Edward Lowasa aione.
Not that it makes any difference, but hey, what do we loose!

Very good work.
 
mbona umewashika nyeti zao kwikwikwi ehe ehe,mwaka huu haponi mtu,pamoja na misemo yao ya kelele hazimuzuii mwenye nyumba kulala.
sasa watatoka tu.si unajua nyoka akiingia shimoni wewe weka mafuta ya taa,atatoka bila kelele wala mikwaruzo.sasa kazi kwao
 
Mzee MKJJ...HONGERA SANA!
JF TUNAKANDAMIZA.........
ALUTA KONTINUA...
Kweli umewashika pabaya..........................aahaaaaa
I would be happy to hear from Hon Presidaa....alipotoshwa????
 
Back
Top Bottom