Haya si matokeo ya kushangalia

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,319
33,125
Jana Baraza la Mtihani la Taifa lilitangaza matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha nne uliofanyika mwaka jana. Matokeo hayo yanaonyesha kuwa kiwango cha kufaulu mwaka 2011 kimeongezeka kwa wastani wa asilimia 3 ikilinganishwa na mwaka juzi, yaani 2010. Shule zilizofanya vizuri kwa mwaka jana ni zile zile, yaani za binafsi.
Mwaka juzi matokeo yalikuwa ni mabaya mno kwani nusu ya wanafunzi waliofanya mtihani huo walifeli, kelele nyingi zilipigwa juu hali hiyo ambayo inaonyesha dhahiri kuwa ubora wa elimu nchini unazidi kuporomoka.
Wanafunzi waliofanya mtihani mwaka jana ni 426,314 kati yao asilimia 53.37 wamefaulu kuanzia daraja la kwanza hadi la nne; waliopata daraja la kwanza ni wanafunzi 3,671, daraja la pili ni wanafunzi 8,112, daraja la tatu 21,794 na daraja la nne ni wanafunzi 146,639.
Ukizitazama takwimu hizi kwa jicho kali zinathibitisha kitu kimoja, kwamba bado hali ya elimu yetu ni mbaya. Ingawa wanafunzi waliofaulu ni 189,216, kimsingi wenye nafasi ya kuendelea na masomo ya juu ni wale wa daraja la kwanza, pili na tatu tu, hawa ni sawa na wanafunzi 33,577 sawa na asilimia 9.98, idadi hii ni ndogo sana ikilinganishwa kwa mfano na wale waliopata daraja la nne ambao ni 146,639.
Tafsiri ya takwimu hizi inaeleza kuwa hata kama kuna ongezeko la asilimia tatu katika kiwango cha kufaulu, bado hali yetu si nzuri. Asilimia tatu ni sawa na tone la maji katika bahari kuu, hasa kutokana na ukweli kuwa idadi kubwa ya wanaoelezwa wamefaulu wako katika daraja la nne sawa na asilimia 81.36 ya wote waliofaulu.
Mwaka jana baada ya taifa kutikiswa na matokeo mabaya pengine kuliko yote yaliyowahi kutokea nchini, kulikuwa na rai mbalimbali juu ya hatua za kuchukuliwa ili kukabiliana na hali ya kuendelea kuporomoka kwa ubora wa elimu nchini, miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na kuelekeza rasilimali nyingi zaidi kwenye sekta ya elimu.
Ni vigumu kusema kwa hakika ni kwa kiwango gani serikali imeitikia wito huo, lakini matokeo ya mwaka jana ni kielelezo kingine kwamba bado hali yetu si nafuu sana ikilinganishwa na tulivyokuwa mwaka juzi.
Kwa muda mrefu sasa juhudi za kukabiliana na janga la kutetereka kwa ubora wa elimu ya nchi hii ama zimekuwa za stahili ya zima moto au ahadi za maneno matupu ambayo kimsingi hazitatui tatizo lenyewe.
Matokeo yake hata pale kunapokuwa na ongezeko la idadi ya wanafunzi shuleni, hakuna hatua nyingine inayopigwa kwa mfano kuhakikisha kwamba mafanikio si idadi tu, bali ni ubora wa mchakato wa utoaji elimu yenyewe.
Tumesikia mara kadhaa serikali ikisema kuwa imeongeza ajira kwa walimu, tumesikia ahadi kuwa kila anayetaka kusomea ualimu katika ngazi ya elimu ya juu anahakikishiwa mkopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa asilimia 100, lakini pia tumeona upanuzi mkubwa wa vyuo vya elimu ya juu kwa ajili ya kuzalisha walimu wengi zaidi; hizo zote kwa ujumla wake hazionyeshi kuwa na matokeo chanya kiasi cha kutosha ndiyo maana sasa shule zetu zinageuka kutoka kituo cha kutafuta maarifa kuwa kituo cha kwenda kukua kwa watoto wa taifa hili.
Hakina wakati umefika sasa kutambua kwamba taifa linakabiliwa na janga kubwa katika sekta ya elimu, haikubaliki na kwa kweli si haki kuweka watoto wa taifa hili shuleni kwa miaka minne, lakini mwishowe eti asilimia 9 tu ndiyo tu inafanikiwa kuvuka kigingi cha kwanza kuingia hatua nyingine ya mfumo wa elimu yetu.
Kila tunapotazama hali hii, na kwa kweli tukiwapongeza kwa moyo wetu wote wanafunzi waliofanya vizuri na shule zao pamoja na walimu wao, tukiwatakia kila la heri na kuwataka wakaze kamba kwa mafanikio hayo, tunatoa changamoto kwa serikali kujitazama kwa makini zaidi juu ya hali ya elimu nchini.
Tunaweza kudhani kuwa hili ni tatizo dogo, lakini ikumbukwe kuwa dunia ya sasa imegeuka kuwa kijiji, tutake tusitake ushindani hauna mbadala, ni lazima kushindana katika nyanja zote, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) nayo inatulazimu kufungua kila mlango na dirisha, kila kitu, haya yote tutayamudu vipi kama tunaicha elimu yetu ikiwa hoi kiasi hiki? Tunajitafakari zaidi.



CHANZO: NIPASHE
 
hapa ndipo huwa na choka kabisa kwanini huwa hawaongelei ongezeko la shule na idadi ya wanafunzi katika takwimu zao hasa za ujumla..

yaani shule zimeongezeka lazima kiwango nacho kiongezeke lakini wao ndo kwanza wanakuambia kiwango cha ufaulu kimeongezeka na je hao waliongezeka walikuwepo mwaka ulioita. mwenye ufahamu juu ya hili naomba maelekezo..
 
Shule ya kata nayopiga mzigo one na two hamna three mbili, four hamsini na moja zero Mia kumi na nne.... Na sisi tulitegemea zero zote sababu wanafunzi wenye we hawajishughulishi, wazazi hawajali wanafkiria elimu ni kulipa Ada tu, serikali imewatupa hamna walimu, vitabu hata madawati na walimu tushajichokea hatuna morale hata kidogo...tutegemee matokeo mabaya zaidi ya hayo unless mitihani wa form two urudishwe
 
Back
Top Bottom