Candid Scope
JF-Expert Member
- Nov 8, 2010
- 11,888
- 6,885
Waziri Mkuu Pinda Na Mbunge Halima Mdee Bungeni
Wakijadili Hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya Ardhi
Mdee aonya machafuko kugombea ardhi
Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee aliitahadharisha Serikali kuwa kuipuuza sekta ya ardhi kutasababisha watu wa taifa hili kuchinjana."Sekta ya ardhi ndiyo uhai wa nchi hii. Sekta hii tukiipuuza... na ninaiambia Serikali tukiipuuza watoto wetu, wajukuu wetu watakuja kuchinjana na hatutaki kutengeneza Tanzania ya kuchinjana katika kipindi," alisema Mdee.
Akizungumzia kuhusiana na Kampuni ya Agri Soil ambayo imepewa eneo la uwekezaji katika Wilaya ya Mpanda, Mdee alisema mbali na upungufu wake imekiuka sheria."Imekiuka sheria ya nchi, sheria zetu zote ziko wazi na hili namwambia Mheshimiwa Waziri Mkuu asiposhughulikia vizuri anaweza akaanguka nalo kabisa kwa sababu kuna ushahidi wa moja kwa moja kuwa ofisi yake ilihusika tutumie busara tuokoe nchi," alisema.
Mdee alisema sheria inasema kama kuna ushirikiano unamhusu raia na kwamba sheria ya uraia haijatambua halmashauri na kuhoji kuwa Serikali iwaambie wabunge ni raia gani anamiliki hekta zaidi ya 200?
Mgogoro wa shamba hilo uliibukia kwa mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Pudenciana Kikwembe ambaye aliitaka serikali kutoa asilimia 25 ya hisa katika shamba hilo kwa wazawa na kwa sababu madiwani walishirikishwa katika suala la Agro Soil basi waamue gawio la faida litakwenda katika mradi gani.
Mwananchi
Halima Mdee, Serukamba jino kwa jino
MBUNGE wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba, amemponda Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) kuwa ni muongo na anapeleka siasa uchwara bungeni.
Mdee amemjibu Serukamba kwa kumweleza kuwa, anamuonea huruma kwa kuwa hajui kama mwaka 2015 Mbunge huyo atarudi bungeni.
Serukamba alisema, wabunge waache kutafuta umaarufu kwa kusema uongo bungeni na kwamba, wananchi wa Kigoma ndiyo wanaofahamu hali halisi ya mambo yao. "Huo uzalendo uchwara unaoletwa leo hatuutaki Kigoma, tunataka maendeleo' amesema Serukamba alipoomba kutoa taarifa wakati Mdee anachangia bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Mdee amesema, hatafuti umaarufu kwa kuwa yeye tayari ni maarufu, anataka kufanya kazi. Mbunge huyo amesema, hazungumzi kitu ambacho hana ushahidi nacho hawafanyi uchochezi. " Hatutafuti umaarufu wa kisiasa, upo tayari, tunataka kuijenga nchi yetu" amesema Mbunge huyo kijana, Waziri Kivuli wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Amemtahadharisha Waziri Mkuu awe makini katika kushughulikia mkataba unaodaiwa kummilikisha mwekezaji eneo kubwa la ardhi mkoani Rukwa, kwa kuwa inadaiwa kuwa ofisi yake imehusika. Kwa mujibu wa Mdee, mkataba huo umekiuka sheria za nchi na kwamba, Pinda asipokuwa makini ‘ataanguka nalo'. Amewataka wabunge waache ushabiki, hilo ni tatizo kubwa.
Baada ya Mdee kusema hivyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Mary Nagu aliomba kutoa taarifa, akasema, hakuna sheria iliyovunjwa Rukwa, na hakuna mwekezaji aliyemilikishwa ardhi mkoani humo.
Mdee amesema bungeni kuwa haitaki taarifa ya Nagu, na anashangaa kuona kuwa wanaopaswa kutekeleza sheria wanatetea uhalifu. Mbunge huyo amesema, anataka haki itendeke kwa wananchi wa Kwembe na Mabwepande mkoani Dar es Salaam na atakuwa na wananchi hao hadi mwisho. "Sisi tutakufa na wananchi wetu, liwe jua, iwe mvua"amesema Mbunge huyo na kusema, Serikali inapaswa kuweka utu kwanza, iache siasa zifanywe na vyama.
Ameiomba Serikali itumie busara kushughulikia mgogoro wa ardhi eneo la Chesimba, na amewatuhumu baadhi ya wenyeviti wa mitaa na madiwani wasio waaminifu kuwa wanauza maeneo. Amedai kuwa, maeneo ya wazi yakiwemo yakiwemo yaliyotengwa kwa shughuli maalum yanauzwa, na kwamba, wakubwa wanajenga ‘mabangaloo'. Amesema, ardhi ndiyo mhimili wa nchi na kwamba, sekta hiyo ikipuuzwa baadaye wananchi watachinjana.
"Sekta hii ikipuuzwa Watoto wetu, wajukuu wetu watakuja kuchinjana, hatutaki kutengeneza Tanzania ya Watanzania kuja kuchinjana" amesema Mdee.
Source Habari Leo.