Hadithi: Mtambo wa mauti

Nameless mjini dsm mnapatikana wapi nmtume mtu anichukulie hapo...
Vipo posta karibu na sanamu, kariakoo mtaa wa congo, kinondoni kituo cha kanisani na bunju. kwa maelezo zaidi piga simu namba 0712504985.
 
5

Kwa Insepkta Haroub Kambambaya alfajiri hiyo ilikuwa mbaya, ya kutisha na inayosikitisha kuliko alfajiri nyingine zote alizowahi kuishi katika uhai wake. Labda angeweza kuifananisha alfajiri hii na ile ya miaka kumi na sita iliyopita, wakati huo akiwa mwanafunzi wa kidato cha sita katika shule ya Mzumbe, mkoani Dodoma. Alikuwa katika likizo fupi, akijiandaa kwa mtihani wake wa mwisho, likizo ambayo aliitumia kukaa na mama yake mzee katika kimojawapo cha vijiji vya Shinyanga. Akiwa mtoto wa mwisho, asiye na ndugu, baada ya dada zake wawili na kaka zake wanne kufa kwa maradhi mbalimbali utotoni, baba yake pia akiwa marehemu tangu yeye anatambaa; mama yake, binti Kaundime, alikuwa kila kitu kwake. Alikuwa bibi, babu, mama, kaka, dada na zaidi ya yote rafiki. Waliishi kwa mapenzi makubwa na kuridhika kwa chochote walichokipata kutokana na jasho la mama huyu katika kijishamba chake cha mahindi.

Binti Kaundime alijinyima kila kitu na kujidhiki kwa kila hali ili kumpatia mwanae huyo wa pekee elimu. Kwa upande wake, Haroub hakuwa kipofu wa hali hiyo. Alifanya kila jitihada katika masomo yake ili apate elimu ya kutosha, ambayo ingempelekea kupata mshahara wa kutosha, ili aweze kuchukua jukumu la kumlea mama huyu.

Hivyo, alfajiri ile, wakati akiwa na hakika kuwa safari ya kutafuta uhakika wa maisha ilikuwa inafikia ukingoni, aligutushwa toka usingizini na kelele za watu walioizingira nyumba yao. Baadhi walikuwa wakiimba nyimbo za kuwalaani wanga, baadhi wakitukana kwa sauti huku wengine wakipiga milango na madirisha yao kwa miguu, mawe na magongo. “Toka nje mchawi wewe. Toka upesi, zako zimefika leo,” mtu mmoja alisikika akisema.

Kwanza Haroub hakuelewa kinachoendelea. Alipotoka chumbani kwake na kumfuata mama yake kwake alimkuta amejiinamia akilia kwa kwikwi.

“Kuna nini mama?” aliuliza.

Mama yake alipomtazama alizidi kulia. Akainuka na kumkumbatia mwanae huku akisema kwa sauti ya dhiki, “kwa heri mwanangu. Nimekulea, nilitegemea unilee. Shetani ametushinda nguvu. Kwa heri ya kuonana.”

“Kwani kuna nini mama?” Haroub aliuliza.

Mama yake alimtazama kwa mshangao. “Kwani hujaelewa tu?” alimuuliza. “Hao watu wanakuja kuniua.”

Haroub hakuyaamini masikio yake. “Unasemaje?... Kwa nini?” alihoji.

“Siku zote wamekuwa wakidai kuwa mimi ni mchawi. Wanadai kuwa mimi ndiye niliyemuua baba yako na wanangu wote waliotangulia. Majuzi amefariki mtoto wa jirani yetu yetu mmoja ambaye tuliwahi kugombea mpaka wa shamba. Naamini ni yeye aliyewatuma kwa kudhani kuwa nimehisika na kifo cha mtoto wake. Haroub baba, ningekuwa mchawi kweli ningeshindwa kukuarifu wewe mwanangu?”

Kabla Haroub hajaua afanye nini, ajibu nini mlango wa mbele ulipigwa jiwe kubwa lililofanya ufunguke. Ulifuatiwa na moshi mkubwa ulioashiriwa kuwa nyumba yao tayari ilikuwa imechomwa moto. Wakati huohuo kundi kubwa la watu waliofunika nyuso zao kwa matambara liliingia ndani na kuwatenganisha yeye na mama yake. Alijaribu kupigania roho ya mama yake kwa nguvu zake zote, lakini mikono yake ilikuwa dhaifu sana mbele ya umati huo wenye mikono iliyokakamaa kwa uhalifu. Aliburuzwa nje na kutupwa chini, ambako alishuhudia mama yake kipenzi akipigwa kwa michi, mawe na magogo hata akakata roho. Alishuhudia pia mama yake akimwagiwa mafuta ya taa na kuchomwa moto kabla ya watoa hukumu hao kuondoka zao huku wakiimba nyimbo za kujisifia.

Baada ya watu hao kuondoka ndipo majirani walipofungua milango yao na kumzoa Haroub ambaye alikuwa ameteguka mkono na kuumia mbavu kwa purukushani. Baadhi ya majirani walikimbilia polisi kutoa taarifa, taarifa ambayo haikuzaa matunda yoyote zaidi ya kuruhusu mwili wa marehemu uzikwe na ahadi ya “Upelelezi unaendelea.”

Ni tukio hilo lililomfanya Haroub Kambambaya afikie uamuzi wa; Nitakuwa polisi. Daima nitapambana na wahalifu wa aina zote na kuwatokomeza.

Alirejea shule na kufaulu vizuri masomo yake. Alijiunga na chuo kikuu cha Dar es Salaam na kusomea shahada ya sheria. Alipohitimu alikuwa miongoni mwa wasomi wachache wa awali walioona umuhimu wa kujiunga na jeshi la polisi.

Akiwa askari shupavu, mkakamavu na mwadilifu alijikuta akipanda cheo baada ya cheo hadi majuzi alipoteuliwa kukalia kiti hiki, ambacho uteuzi wake ulifanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, cheo ambacho madaraka yake yanawiana na yale ya Kamishna Mwandamizi wa Polisi au Mkuu wa Majeshi, ingawa kinafichwa kwa pazia la uinspekta. Naam, cheo ambacho kilimfanya akalie kiti hiki “Cha moto,” ambacho alfajiri hii alianza kuuonja.

Kufuatilia kwake nyendo za Joram Kiango ili aweze kuelewa kilichotokea pale hoteli ya Comfort na kusababisha kifo cha yule msichana mrembo, Mona Lisa, Kambambaya alichukua hatua kadhaa madhubuti kwa lengo la kumtia mikononi Joram Kiango.

Akiwa kingunge wa kitengo, Kambambaya alikuwa na siri nyingi ambazo wasaidizi wake wa karibu hawakuzifahamu. Moja ya siri hizo ni ile ya kujua namba ya simu na jina la bandia ambalo Joram Kiango alikuwa akitumia katika simu zake za mkononi. Akiwa na namba mbalimbali katika makampuni AIRTEL, TIGO na VODACOM, huku akizungumza au kuandika ujumbe wa maandishi kwa namna ya mafumbo, haikuwa kazi rahisi kuzinasa simu zao. Hata hivyo, wataalamu wa sauti waliwahi kushirikishwa kuthibitisha kuwa huyo hakuwa mwingine zaidi ya Joram Kiango.

Hivyo, lilipotokea hili, na Joram kutoweka Kambambaya aliitega mitego yake yote. Mmoja wa mitego hiyo ilifyatuka na kuinasa sauti yake pale alipotuma ujumbe wa maandishi kwenye namba fulani ambayo bila shaka iliorodheshwa kwa jina jingine la bandia. Kambambaya isingemchukua muda mrefu kumjua mtu huyo, lakini maadamu kwa sasa alichohitaji ni kumpata Joram Kiango mwenyewe, alichofanya ni kuwasiliana na kampuni ya simu iliyotumiwa ili kujua eneo ambalo ujumbe huo ulitokea.

Lilikuwa eneo la Manzese, lenye maelfu ya watu, maelfu ya majumba na maelfu ya vichochoro visivyo na mpangilio, eneo ambalo halina jina la mtaa wala namba za nyumba. Lakini hayo hayakumkatisha tamaa Kambambaya. Alitumia timu ya vijana wake sita, kuungana na polisi wa kawaida sitini, kulizingira eneo hilo usiku kucha na kumhoji kila atakayetiliwa mashaka hadi Joram Kiango atakapopatikana, operesheni ambayo aliichukulia kuwa ndogo sana na ya kawaida kabisa, hadi pale alipoamshwa usingizini na kupewa taarifa ya kuuawa kwa polisi wanne waliokuwa katika jukumu hilo.

Hakuyaamini masikio yake. “Wameuawa!” alinguruma katika simu yake ya mkononi, “Wameuawa vipi?... Nani kauawa?”

“Haijafahamika, afande. Ndio kwanza nafika katika eneo la tukio. Tuko katika vichochoro fulani, hatua kama mia moja hivi toka darajani. Inaonyesha…”

“Nakuja!” Kambambaya alisema akichupa toka kitandani. Alivaa shati na suruali ya karibu juu ya mavazi yake ya ndani, akaichukua bastola yake na kuitupia mfukoni. Dakika mbili baadaye gari lake lilikuwa likitafuna lami, toka Masaki kuelekea Manzese.

Alimkuta msaidizi wake, Chaku Chikaya, akimsubiri chini ya daraja, akiwa miongoni mwa askari wa kawaida wanne, wenye silaha. Chikaya akiwa mtu aliyekabidhiwa operesheni hii alimweleza Inspekta kwa tuo tukio zima lilivyokuwa.

“Marehemu hawa walikuwa na jukumu la kulinda vichochoro vyote vilivyotokea katika barabara kuu. Walikuwa wakitembea wawiliwawili. Inaonekana kama walioingia kwa bahati mbaya katika mtego wa adui. Askari waliokuwa mbali kidogo ya eneo hili walisikia milio ya risasi ikilipuka ghafla tu. Walipokuja eneo la tukio walikuta miili ya wenzao ikiwa imedondoka chini. Hawakumwona mtu wala kusikia mtu akikimbia.

“Ni wazi kuwa yeyote aliyefanya mauaji haya bado yuko katika eneo hilihili. Kwa ajili hiyo nimeongeza ulinzi na kupanua wigo.” Chaku alisema.

Kambambaya alitikisa kichwa na kuunga mkono hatua hiyo, “Walisikia mlio wa bunduki aina gani?” alihoji.

“AK-47, mzee.”

AK! Kambambaya alishangaa. Ile bunduki hatari iliyogunduliwa na Mrusi, Kalashnikov, kwenye vita kuu ya pili ya dunia! Basi hii ni vita! Aliwaza.

Chikaya alimwongoza hadi mahala ilipokuwepo miili ya marehemu. Walilaliana wawiliwawili, baadhi wakiwa wameziangukia silaha zao, mmoja silaha yake ikiwa mkononi kama anayejiandaa kufyatua. Haikuhitaji utaalamu wowote kubaini kuwa kifo kiliwakuta marehemu hawa bila ya wao kutegemea. Ama walivamiwa ghafla, au waliingia katika mtego wa mauti.

Kuiona miili ya vijana hao wasio na hatia, wakiwa hawapo tena duniani, kuliamsha hasira katika nafsi ya Kambambaya. Nani aliyewaua? Kwa nini amewaua? Afanye nini kuwapata haraka wahalifu hawa ili wafikishwe mikononi mwa sheria? Alijiuliza harakaharaka, swali baada ya swali, maswali ambayo yeye binafsi hakutegemea majibu yake yawe karibu kiasi hicho, jambo lililozidi kumpandisha hasira.

Kiasi fulani hasira hizo ziliambatana na hofu, si hofu ya kujua kuwa mahala fulani, katika mtaa fulani, kuna mtu au watu hatari, wenye silaha hatari, ambao wanaweza kuwaua polisi wanne bila ya kigugumizi chochote. Ndiyo, hilo lilimtisha, lakini hofu nyingine ilikuwa juu yake binafsi. Hatua yake ya kuamua kumwinda Joram Kiango kwa nguvu nyingi kiasi hiki ilionyesha kuwashangaza na kutoungwa mkono na wasaidizi wake. Wanavyomjua Joram hawakuona kama ni mtu wa hatari kiasi hicho, wengine hawakuona umuhimu. Lakini maadamu yeye alikuwa na madaraka, alilotaka liwe, likawa. Hivyo, sasa ilimtisha kwa kutojua atauambia nini umma wa Watanzania umwelewe; kwamba Joram Kiango alishukiwa kuua msichana hotelini! Kwamba kwa ajili hiyo alituma kikosi kikubwa cha askari kumtafuta! Kwamba katika purukushani hizo askari wanne wameuawa kinyama! Nani atamwelewa? Nani atamsikiliza?

Wakati akiwaza hayo Kambambaya alikuwa akiendelea na uchunguzi wa eneo hilo. Akiongozana na Chikaya, na askari wengine wawili, walipita uchochoro hadi uchochoro, wakiikagua nyumba baada ya nyumba. Ikiwa alfajiri ya siku ya kazi, baadhi ya wakazi wa eneo hilo walianza kuamka. Walishangazwa kuona mitaa yao ikiwa ‘imevamiwa’ na polisi wenye dalili za madaraka makubwa. Kambambaya hakutaka kuwabugudhi raia kwa wakati huo. Aliwahoji wawili watatu, maswali mawili matatu, lakini wote walionekana kama wanaoulizwa, “Wewe ni mwanamume?” wakati anajiona ni mwanamume au “Wewe ni mwanamke?” wakati kila mtu anaona kuwa ni mwanamke. Kambambaya aliachana nao na kuendelea na uchunguzi wake.

Uchochoro mmoja uliwafanya watokee kwenye hospitali ya Daktari Omari. Alishangazwa na umati wa watu walioukuta umezingira hospitali hiyo, kila mmoja akiwa anatokwa na machozi ya hofu.

“Kuna nini hapa?” alihoji.

“Daktari ameuawa,” mmoja wa majirani alimjibu.

“Daktari yupi?”

“Dokta Omari, mwenye hospitali hii. Wagonjwa waliokuja kupata sindano za masaa wamemkuta akiwa amelala kifudifudi, tundu kubwa likivuja damu toka kisogoni mwake.”

Kambambaya hakusikiliza zaidi. Alipenya umati huo wa watu hadi ndani. Mwili wa Daktari Omari ulikuwa bado umelala sakafuni, katikati ya mlango wa kutokea ofisini kwake kuelekea wodini. Risasi iliyomuua ilikuwa imemfumua kisogo na kupotelea katika ubongo wake ilikuwa tayari imeganda na kufanya kichwa chake kiungane na sakafu.

Kambambaya alitupia macho mezani. Majalada, vitabu, magazeti na vikorokoro vingine vya kiganga vilikuwa katika hali ya mpangilio mzuri. Viti na meza pia vilikuwa katika utaratibu wake maalumu, hali ambayo ilimfanya apate hisia kuwa kifo kilimkuta marehemu bila purukushani yoyote.

“Mzee unaona pale?” msaidizi wake mmoja alimzindua.

Kambambaya akamtazama. Kisha akayafuata macho ya askari huyo yalikoelekea. Yalikuwa yakitazama ukuta mmoja uliokuwa na tundu dogo ambalo lisingekuwa limesababishwa na kitu kingine zaidi ya risasi. Kambambaya alitoa kisu chake na kukipenyeza ndani ya tundu hilo. Baada ya kuchokonoa kwa muda risasi kubwa ilidondoka. Akaiokota na kuitazama. Kama alivyotegemea, ilikuwa ya bastola aina ya AK.45, ambayo mara nyingi hutumiwa na maafisa wa polisi na jeshi pekee.

Risasi ukutani! Kambambaya aliwaza. Ilikuwa ya onyo au mpigaji alikosa shabaha? Kwa jinsi mwili wa marehemu ulivyokuwa, Kambambaya hakuona kama muuaji alihitaji kumtisha au kukosea shabaha!

Aliirudia meza na kuanza kupekua majalada hadi alipopata lile ambalo alikuwa akilitafuta, jalada lenye kumbukumbu ya wagonjwa wote walioingia na kutoka siku hiyo. Alilipitia jina kwa jina, akitazama aina ya maradhi yaliyowaleta, umri na taarifa nyinginezo. Wengi hawakuwa watu wa kutilia shaka. Majina yalikuwa ya kawaida, magonjwa ya kawaida. Lakini alipochukua jalada la wagonjwa waliolezwa na kukutana na mgonjwa mmoja tu mwenye jina la ajabuajabu mara moja alijikuta akisisimkwa na mwili wake:

Sheriff Mkono wa Birika!

Miaka sitini na mitano!

Maradhi yasiyoeleweka!

Vipimo baadaye!

Kambambaya alipiga hatua za harakaharaka kukiendea chumba cha wagonjwa waliolazwa. Kama alivyotegemea alikuta chumba hicho kikiwa kitupu.

“Joram alikuwa hapa,” alinong’ona akimwelekea Chaku Chikaya. “Amelala katika chumba hiki. Tumechelewa sana. Tayari ametoweka tena.”

Chikaya hakumwelewa bosi wake. “Umesema Joram, afande? Una hakika?” alimuuliza.

“Bila shaka!” Kambambaya alimjibu. “Na kwa namna moja au nyingine anahusika na mauaji haya. Sasa umuhimu wa kumpata ni mkubwa zaidi na wa haraka zaidi. Lazima apatikane katika saa ishirini na nne zijazo,” aliamrisha.

Wakati huo ikikaribia saa kumi na mbili za asubuhi, uwanja wa hospitali hiyo ulikwishafurika watu. Minong’ono ya hapa na pale iliendelea na, hivyo, kuzidi kuvuta watu wengine. Kambambaya alitoa maelekezo kwa wasaidizi wake, “Eneo hilo lifungwe; taratibu za kawaida, ikiwa pamoja na kuchukuliwa alama za vidole na ripoti ya daktari zifuatwe.”

Kisha alilirudia gari lake ambalo lilimpeleka nyumbani kwake ambako alioga, akavaa mavazi yake rasmi, akanywa kikombe chake cha kahawa chungu, kisha akarejea ofisini kwake.

Kwa muda fulani Kambambaya aliduwaa ofisini, akiwa ameiinamia meza yake. Hakujua aanzie wapi, aishie wapi katika kulitafakari suala hili lililojaa utata, suala ambalo lilianza na kifo cha msichana mmoja tu hotelini, likafuatiwa na kutoweka kwa mtuhumiwa nambari moja na sasa tayari askari wanne na daktari mmoja ni marehemu.

Msaidizi wa ofisi yake alimletea kahawa nyingine ambayo aliinywa. Alipoingia tena alimletea jalada lililokuwa na taarifa ya daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu aliyeuawa hoteli ya Comfort.

Kambambaya alikuwa na mzigo mzito kichwani mwake zaidi ya jalada hili. Alikuwa na jukumu zito la ‘kuhalalisha’ vifo vya askari wale wanne na daktari wa Manzese. Ulikuwa wajibu wake, tena wa haraka, kupata ufumbuzi au kiini cha mauaji hayo. Aidha, jukumu la kumnasa au kuwanasa wahalifu kwa kiasi kikubwa lilikuwa mabegani mwake. Kila dakika iliyopotea, kabla ya kupiga hatua yoyote katika hayo, ilimtisha zaidi. Hata hivyo, kutokana na ukweli kuwa msichana yule, ambaye hata jina lake lilikuwa halijafahamika, alikuwa wa kwanza katika mlolongo huo wa vifo, Kambambaya alijikuta hana jinsi, isipokuwa kulisoma jalada hilo kwa tuo.

Taarifa ya daktari ilikuwa na kurasa tatu zilizoandikwa kwa mtindo wa kitabibu. Juu ya ripoti hizo ziliambatanishwa picha kadhaa za marehemu zilizopigwa na polisi. Mojawapo ya picha ilimvutia Kambambaya kiasi cha kufanya aamue kuiweka chini taarifa ya maandishi na kuzikodolea macho.

Alikuwa amewasikia wasaidizi wake wakizungumza uzuri wa msichana huyo aliyeuawa. Hakuwa amefikiria kuwa alikuwa mzuri kiasi hiki! Picha hii ikiwa imeandaliwa katika hali ya kumfanya msichana huyo asionekane kuwa amekufa, marehemu alikuwa amevalishwa nguo na kuketishwa kwenye kochi, macho yakiwa yamefumbuka. Alionekana msichana mzuri sana, ambaye hakustahili kufa kifo cha kinyama kiasi kile. Picha nyingine zilipigwa kabla hajaguswa, zikionyesha alivyolala chali kitandani, tundu la risasi kifuani, kitu kama tabasamu mdomoni. Nyingine, bila shaka ilipigwa Muhimbili, ilimwonyesha akiwa mtupu kama alivyozaliwa. Isipokuwa kwa tundu la risasi lililoutia dosari mwili huo ulikuwa mwili pekee, ambao Kambambaya hakupata kufikiria kama binadamu wa kawaida angeweza kuwa nao.

Baada ya kuzitazama kwa makini picha hizo Kambambaya aliirudia taarifa ya daktari. Kwanza aliisoma harakaharaka. Baadaye aliirudia taratibu, akiitafakari kipengele baada ya kipengele.

JINA: Halijafahamika

UMRI: kati ya miaka ishirini hadi ishirini na mitatu.

JINSIA: Mwanamke.

MUDA WA KIFO: kati ya saa saba hadi saa tisa usiku.

SABABU YA KIFO: kutokwa na damu nyingi katika tundu lililotoboa moyo.

MAELEZO MENGINE: Marehemu alikuwa mtu mwenye afya nzuri kabla ya kifo chake. Isipokuwa kwa harufu ya lotion na pafyumu mwilini mwake, marehemu alikuwa msafi. Hakuwa amefanya mapenzi na mtu yeyote. Kwa ujumla, alikuwa bado bikira.

Taarifa hiyo ya mwisho ilimchanganya Kambambaya. Marehemu alikuwa bikira! Marehemu, ambaye taarifa alizonazo zinaonyesha kuwa alikuwa na mpenzi wake, Joram Kiango, wakinywa, kula na kulala zaidi ya mara moja! Haikumwingia akilini. Kama wanamtafuta Joram Kiango, kwa tuhuma za kumuua mpenzi au hawara yake, vipi hawara huyu awe safi kiasi hicho!

Kambambaya akaichukua tena picha ile ya marehemu aliyeketishwa kwenye kiti. Akaitazama kwa makini kana kwamba alitarajia imwambie chochote. Haikumwambia. Alirejea katika jalada na kuendelea kufikiri. Mara akashikwa na hamu ya kumwona marehemu kwa macho yake mwenyewe. Akainuka na kutoka nje ya ofisi.

“Muhimbili,” alimwelekeza dereva wake wakati akiingia kwenye gari.

Dakika chachee baadaye alikuwa katika ofisi ya daktari wa uchunguzi wa maiti. “Naomba kumwona marehemu,” alisema baada ya kujitambulisha. Kambambaya alimwona daktari akibabaika kidogo kwa rai hiyo. “Vipi docta, mbona unawaza sana. Au kuna taratibu ambazo sijazifuata?”

“Hapana,” daktari alijibu.

Hakuona kama alihitaji kumwambia askari huyo tatizo lake. Ukweli ni kwamba pamoja na udaktari wake bado hakuwa mzoefu sana wa chumba cha maiti. Mara nyingi aliwategemea wahudumu wa chumba hicho, hasa Supa D ambaye alitekeleza majukumu yake kwa uhakika zaidi. Tatizo ni kwamba toka jioni jana Supa D alikuwa hajaonekana, jambo ambalo halikuwa la kawaida kwake.

“Twende,” alijikongoja daktari huyo baada ya kusitasita.

Chumba cha maiti kiliwalaki kwa ile harufu isiyoelezeka, harufu ambayo siku zote Kambambaya alishindwa kufahamu iwapo ilitokana na kuharibika kwa maiti, mchanganyiko wa madawa au yote kwa pamoja, harufu ambayo haizoeleki.

Alistahimili harufu hiyo kwa kusimama nyuma ya daktari alipovuta jokofu lililokuwa na taarifa za marehemu huyo. Mara Kambambaya alimsikia daktari huyo akitoa sauti ya mshangao, iliyofuatiwa na kutokwa na macho ya mshangao kama mtu aliyegusa waya wa umeme. Kambambaya akayafuata macho ya daktari huyo humo ndani ya jokofu. Yeye pia alipigwa na butwaa.

Badala ya msichana mrembo jokofu hilo lilikuwa na maiti ya mzee wa kiume, yenye ndevu nyingi zilizoachwa ovyoovyo. Ulimi wa marehemu huyo ulikuwa nje, shingo upande kama iliyovunjika huku damu ikiwa imeganda mdomoni, puani na masikioni.

Hatimaye, daktari alitokwa na sauti, “Supa D!” alisema kwa mshangao. “Jesus, kitu gani kimetokea hapa?”

Kambambaya hakumwelewa. “Ina maana umekosea na kufungua jokofu la maiti nyingine?” alimuuliza daktari huyo.

“Hapana, Inspekta. Jokofu hilihili ndilo lililohifadhi maiti ya yule msichana. Na huyu ambaye yumo sasa ni mfanyakazi wetu wa chumba hiki ambaye alikuwa akihudumia mwili huo. Toka jana jioni Supa D hajaonekana. Ametafutwa kila mahali bila mafanikio. Nashangaa kumkuta humu, tena akiwa maiti.”

Ndio kwanza ikampambazukia Kambambaya. “Yaani…” alitaka kumuuliza jambo, akasita. Badala yake aliuliza, “Kwa hiyo maiti tunayoyatafuta yatakuwa wapi?”

“Sijui.”

Kwa ushawishi wa Kambambaya daktari huyo alifungua majokofu yote. Kila maiti ilikuwemo, isipokuwa maiti moja tu, ya marehemu Mona Lisa.

Baada ya dakika nyingi za kuirudia tena na tena kazi hiyo na baada ya kupitia kumbukumbu za mapokezi mara mbilimbili, ilikuwa dhahiri Mona Lisa alikuwa ametoweka!
 
Mwanza tapataje hiki,roho ya paka ,mikononi mwa nunda,nyuma ya mapazia,salamu kutoka kuzimu,lazima ufe joram??etc
 
Back
Top Bottom