Hadithi: Mtambo wa mauti

2
UBONGO WA MWALIMU NYERERE! Joram alisoma kwa sauti maneno hayo na kuachia tabasamu jepesi. Aliinua uso wake kumtazama Mona Lisa ambaye aliketi kimya, upande wa pili wa kijimeza kilichowatenganisha, macho yake yakimtazama Joram kwa shauku.
“Hili ndio jina la kitabu chako?” Joram alimuuliza.
“Ndiyo. Jina la awali… kama kitafaa na kama kitapata mchapishaji, nadhani kwa kawaida atakuwa na uhuru wa kuchagua jina litakalofaha zaidi,” Mona alieleza.
Joram akatabasamu tena kabla ya kuongeza, “Sijasema kuwa halifai. Naliona kama jina kali na zito sana kwa riwaya ya kwanza kwa mwandishi. Lakini… ni riwaya yenyewe itakayoafikiana au kutofautiana na jina…” akawasha sigara nyingine. Kabla ya kuivuta alimeza fundo moja la wiski yake, ambayo kama kawaida aliinywa kavukavu. Kisha, akameza fundo la moshi na kuuhifadhi katika mapafu yake kwa muda wa robo dakika hivi kabla ya kuupeperusha angani, taratibu, huku macho yake yakiwa tayari yamezama na kupotelea katika msitu wa maandishi yaliyolala juu ya mapaja yake.

Ni usiku. Usiku wa manane. Isipokuwa kwa milio ya magari, mingurumo ya ndege angani na mashine ya kurekebisha hewa, jiji la London lilikuwa kimya, kama lililokufa. Kama taa za barabarani zisingekuwa ziking’ara kama ilivyo kawaida, tungeweza kusema kuwa mji huu maarufu duniani ulikuwa kuzimu.
Kama ilivyo tabia ya maumbile, utulivu huu uliwahusu hawa, uliwasahau wale. Katika jengo moja kongwe jijini humo, lililohifadhi hospitali maarufu ya St. Thomas, watu mbalimbali walikuwa wakitaabika. Wako waliokuwa wakitaabika kwa mateso ya maradhi, wako pia waliokuwa wakitaabika kwa kuhangaikia wagonjwa wao. Madaktari, manesi na wataalamu mbalimbali wa uhai wa binadamu pia walikuwa katika hekaheka kubwa.
Wengi kati ya hawa, hali haikuwaruhusu kujua kama huo ulikuwa usiku wa manane au mchana.
Miongoni mwao alikuwamo mgonjwa mmoja mashuhuri, Julius Nyerere. Alikuwa amelala kwa utulivu baada ya kuteseka sana. Saratani ya damu, iliyomvamia ghafla, ilikuwa imemtesa sana toka kijijini kwake Butiama, jijini Dar es Salaam hadi hapa Uingereza. Maradhi haya yalikataa kuitii kila aina ya dawa yaliyopatiwa. Yalikataa kuwaheshimu madaktari bingwa waliokesha usiku na mchana kumsaidia. Yalikataa kusikia maombi na kilio cha maelfu ya Watanzania waliomtakia kila la heri. Yalikataa katakata, angalao kuitii mizimu ya Wazanaki, ambayo Mwalimu hakuwahi kuipuuza.
Na sasa Mwalimu alilala kwa utulivu katika chumba cha wagonjwa mahututi, mabingwa wa maradhi hayo duniani wakiendelea kukuna vichwa vyao na kupekua tena na tena kamusi ya misahafu ya taaluma zao…

Joram aliinua uso na kumtazama Mona Lisa usoni. Msichana huyo, ambaye alikuwa akimtazama Joram kwa makini pindi akiyasoma maandishi yake aliyakwepa macho ya Joram Kingo kwa aibu. Badala yake alichukua glasi ya mvinyo aliokuwa akinywa na kumeza mafunda mawili matatu.
“Umeandika wewe, riwaya hii?” Joram aliuliza taratibu.
“Ndiyo… kwani inafaa?” aliuliza kwa sauti ya juu kidogo.
Joram akacheka. “Huko hatujafika,” alimjibu. “Niambie jambo moja! Ulikuwa London wakati wa maradhi ya Mwalimu Nyerere?”
“Ndiyo na hapana,” lilikuwa jibu la Mona Lisa.
“Una maana gani?”
“Maana yangu ni kuwa, kweli nimewahi kufika London. Na nilifika huko wakati wa maradhi ya Mwalimu Nyerere. Lakini pia sio kweli kwa maana unayofikiria wewe. Sikufika St. Thomas wakati Mwalimu akiwa amelazwa pale. Sikuhusika kwa namna yoyote na matibabu yake. Nilichoandika hapo ni utunzi tu wa kawaida kabisa, kwa lengo la kumuenzi kisanii.”
Joram alimeza funda jingine la wiski. Akawasha sigara nyingine. Kisha, akazama tena katika mswada huo ambao haikuwa siri tena kuwa ulianza kumvutia;

… Wakati Mwalimu akipambana kiume na maumivu hayo, pale nje, katika chumba cha mapumziko, kundi jingine dogo lilikuwa likipambana na mengi. Kundi hili lilijumuisha wapenzi na waumini wa Mwalimu.
Alikuwapo Mama Maria, siku ya tatu leo hajapata usingizi. Moyo wake uligubikwa na huzuni huku macho yake yakishindwa kuhimili machozi ambayo yalimtoka mara kwa mara. Kando ya Mama Maria binti yake… alitulia kimya, macho kayafumba akihesabu rozari. Ingawa sauti ilikuwa haitoki bado midomo yake iliashiria kuwa alikuwa katika sala ndefu, sala iliyoanzia Butiama, akaendela nayo hadi Dar es Salaam; akaruka nayo Bahari ya Atlantic na sasa anaendelea nayo katikati ya jiji la London.
Pembeni, ya kochi, alikuwepo Makongoro Nyerere na Mzee Kingunge Ngombale Mwiru. Walikuwa wakinong’ona kwa sauti ndogo; Makongoro, kiko akiwa amekisahau, Mzee Kingunge makeke yakiwa yamemtoka.
Hawa, pamoja na baadhi ya Watanzania waishio London, walijumuika katika mkesha huo, macho yao yakiwa yameelekezwa mlangoni, kumsubiri daktari kwa shahuku kubwa.

“Weitaa!” Joram aliita bila kuinua uso wake toka kwenye maandishi hayo. Kinywaji chake kilikuwa kimekwisha. Alimwelekeza mhudumu huyo kumletea kinywaji kingine kwa mkono, bila kutoa sauti.
Macho yake yalihama kutoka kwenye mswada huo pale tu alipoyainua kumtazama Mona Lisa, ambaye alitabasamu pia kwa aibu. Akayarejesha kwenye maandishi na kuendelea.

Nusu kilomita tu toka hospitalini hapo, katika moja wapo ya hoteli za Sheraton zilizotapakaa jijini humo, kundi jingine dogo lilijifungia katika chumba mahususi likijadili hatima ya Mwalimu. Hili lilikuwa kundi la wataalamu waliobobea katika fani mbalimbali. Mmoja wao alikuwa mtu mfupi, mnene mwenye kipara kilichong’ara kana kwamba hakuwahi kuota nywele toka utotoni. Kati ya kundi hili la watu wanne kati yao hakuna aliyemfahamu kwa jina. Walichofahamu ni kuwa alikuwa ameingia jijini humo usiku huohuo kwa ndege ya jeshi la anga la Marekani. Alijitambulisha kwa jina mola la Ignatius, ambalo lina asili ya Kigiriki kwa maana ya kitu kama moto au joto. Lakini kila mmoja alijua kuwa lilikuwa jina la bandia. Alijitambulisha pia kuwa alikuwa na ujumbe mahususi toka serikali ya Marekani, ingawa kila mmoja alihisi kuwa alikuwa mjumbe wa CIA.
Mwingine katika kundi hilo alikuwa daktari bingwa wa upasuaji wa vichwa na ubongo, Dkt. Brown Abraham. Katika dunia ya wanataaluma mabingwa wa upasuaji hakuna ambaye hakupata kumfahamu, sifa ambayo iliongezeka maradufu pale alipofanikiwa kuhamisha ubongo wa binadamu na kuupandikiza katika kichwa cha kondoo na ule wa kondoo akauweka kwa binadamu. Viumbe hao waliishi kwa saa ishirini na nne kabla ya kufa. Hata hivyo, inaaminika kuwa waliuawa na wanataaluma wenzao ili kuepusha kasheshe ambayo ingeweza kutokea. Dkt. Abraham mwenyewe aliadhibiwa kwa kupokonywa leseni yake kwa kipindi chote cha uhai wake. Hata hivyo, hatua hiyo haikufanya wanataaluma waliomheshimu wasite kumtumia kwa siri kila walipokwama…

Kinywaji cha Joram kikafika. Akainua glasi na kumeza funda la pili. Akawasha sigara nyingine na kupeperusha moshi angani. Akageuka kumtazama Mona Lisa. Macho yao hayakugongana. Mona Lisa alikuwa amegeuka kumtazama mlevi mmoja ambaye alikuwa ameiacha meza yake na kusimama katikati ya uwanja akicheza mayenu kwa nguvu kuliko muziki wenyewe ulivyoashiria.
Mona Lisa alicheka.
Joram akatabasamu.
Akarejea kwenye riwaya yake.

…Mwingine chumbani humo, ambaye hasa alichukua nafasi ya uenyeji alijitambulisha kama mtumishi wa ubalozi wa Marekani nchini humo, ingawa wajihi wake ulimweka miongoni mwa wale maafisa wa ubalozi wenye nyadhifa za ziada. Kwa mfano, ni yeye aliyetuma tiketi ya ndege na fedha zilizomwezesha Dkt. Abraham kuwa hapa leo toka Afrika Kusini alikokwenda kwa mapumziko. Ni yeye pia aliyekodi chumba hiki na kufanikisha kikao hiki. Yeye, kwa mujibu wa kadi yake, alitajwa kama Thomas MacBain, mwambata wa utamaduni.
Mtu wa nne na wa mwisho katika hafla hii alitajwa kama Dkt. Fabian Winston, bingwa katika matibabu ya kansa ya damu katika hospitali ya St. Thomas jijini humo.
“Ninachotaka kufahamu kabla ya yote,” Ignatius alikuwa akisema. “Ni iwapo, kwa utaalamu wako Dkt. Winston, ipo nafasi yoyote ya Julius Nyerere kupona.”
“Kwa hatua aliyofikia, nafasi hiyo ni finyu sana,” Dkt. Winston alieleza.
“Na katika hali kama hiyo Dkt. Abraham,” Ignatius aliendelea. “Ubongo wake bado uko katika kiwango chake kwa asilimia mia moja?”
Dkt. Winston alikuwa na tabia ya kukohoa na kisha kukuna kichwa kabla hajaingia katika uchambuzi wa kitaalamu. Alifanya hivyo. “Hakuna binadamu ambaye ubongo wake uko asilimia mia moja, Bw. Ignatius, awe mzima awe mgonjwa. Isipokuwa, katika hatua hii, ninachoweza kusema ni kuwa hakuna namna yoyote ambayo inaweza kufanya virusi vya kansa ya damu vishambulie ubongo wake. Taarifa ya kitaalamu aliyoileta Dkt. Winston hapa inaonyesha kuwa ubongo wake haujaathiriwa.
Ignatius alishusha pumzi ya faraja. “Kwa hiyo,” baadaye alisema. “Tunaweza kuendelea na mpango wetu bila wasiwasi wowote.”
“Unajua, hujatuambia hadi sasa ni mpango gani ulionao ambao umetukutanisha hapa ghafla, katika mazingira ya usiri kama haya,” Dkt. Abraham alisema.
“Tunauhitaji ubongo wake kabla hajafa.”
“Ubongo wa Julius Nyerere!” Dkt. Abraham na wengine wote chumbani humo walitokwa na macho ya mshangao.
“Siamini masikio yangu!” Dkt. Winston alisema. “Nadhani hujui hospitali ile inavyolindwa! Si hayo tu, muda wote amezungukwa na madaktari bingwa toka pembe zote za dunia. Hapa tunavyoongea wako wenzangu wamekizingira kitanda chake wakimhudumia.”
“Tunataka ubongo wake… kwa bei yoyote ile,” Ignatius alisisitiza, akamgeukia Dkt. Abraham, “Kazi hiyo inawezekana?”
“Bila hofu ya ulinzi mkali uliopo, bila vipingamizi vya daktari wenzangu, manesi na jamaa zake wanaokesha pale usiku na mchana, mimi nahitaji dakika ishirini tu kuhamisha ubongo wake na kuweka…”
Ignatius alimkatiza, “Achana na hofu ya ulinzi uliopo. Sahau madaktari waliomzunguka. Hayo mwachieni McBain. Anajua la kufanya. Kwa hili hakuna hata kujadili bajeti.
Amepewa uwezo wa kutumia kiasi chochote cha fedha zinazohitajika. Amepewa amri ya kutumia silaha yoyote atakayoona inafaa. Ikibidi hospitali nzima ipitiwe na usingizi wa pono kwa hizo dakika unazohitaji kukamilisha kazi yako. Akilazimika kuua kwa hili ruksa.”
Dkt. Abraham alitokwa tena na macho ya mshangao. “Kwa nini mnauhitaji kiasi hicho ubongo wa binadamu wa kawaida?”
Ignatius alitikisa kichwa kwa masikitiko na kusema, “Mie pia natimiza amri niliyopewa. Lakini kwa machache ninayoyajua juu ya Julius Nyerere hakuwa binadamu wa kawaida. Fikiria, Mwafrika gani wa kawaida aliyeweza kuiyumbisha CIA, BOSS, MOUSAD na wengineo kwa miaka nenda rudi hadi anaachia madaraka kwa hiari yake? Waulize akina Nkurumah, akina Lumumba, akina Mondlane na wengineo. Waulize kipi kiliwakuta.”
Haya, fikiria Mwafrika gani ameweza kufanya kile ambacho marais watano wa Marekani walishindwa kufanya. Aliweza kumng’oa Idd Amin na kuweka utawala aliotaka nchini Uganda. Sisi Marekani tulishindwa kufanya hivyo Vietnam, Kambodia, Iran na hata Congo.
Fikiria alivyoiyumbisha IMF na Benki ya Dunia hata zikashindwa kutekeleza sera zao katika nchi mbalimbali za Kusini mwa dunia kwa wakati muafaka hadi alipoachia madaraka.
Fikiria alivyoweza kuitawala Tanzania, nchi masikini yenye makabila zaidi ya mia na ishirini na dini mbalimbali kuwa kitu kimoja na kupata hadhi kubwa duniani. La… hakuwa mtu wa kawaida. Na tunauhitaji ubongo wake katika maabara zetu, kwa bei yoyote.




 
Una vitabu vipya vya aina ngapi? Ningependa kununua nakala mpya aina zote ulizonazo
VIPO AINA SITA
Napatikana kwa namba 0763044459 au 0712504985
 

Attachments

  • mtambo cover.jpg
    mtambo cover.jpg
    59.6 KB · Views: 254
  • najisikia.jpg
    najisikia.jpg
    8.6 KB · Views: 134
  • nunda.jpg
    nunda.jpg
    12.7 KB · Views: 143
  • roho.jpg
    roho.jpg
    8 KB · Views: 121
  • shetani.jpg
    shetani.jpg
    77.9 KB · Views: 195
  • tutarudi cover.jpg
    tutarudi cover.jpg
    70.1 KB · Views: 190
“Mpaka hapa riwaya yako inaonyesha matumaini makubwa,” Joram alimwambia Mona Lisa, akiitua mezani na kuanza kushughulikia sigara nyingine. “Ina mvuto na msisimko wa kutosha ingawa sifahamu dhamira yako kuu. Lakini lazima nikuonye mapema, mimi si mtaalamu wa lugha wala uhakiki. Hivyo, sitakusaidia sana kwa vitu kama tamathali za semi mfano: takriri, tashbiha, tafsida na kadhalika. Hata hivyo, kwangu mimi imefika mahala ambapo natakiwa nianze kuisoma kwa makini zaidi ili niwe katika nafasi ya kujaribu kutoa ushauri wangu mdogo.”
“Naamini hautakuwa mdogo kama unavyofikiria wewe. Kuna mengi humo ndani ambayo ama hayaaminiki ama hayawezekaniki, ambayo naamini kwa uzoefu wako hutasita kunidokeza ili a ma niyarekebishe kama yanarekebishika, au nikutupilie mbali kama hayarekebishiki,” Mona alimwambia kwa sauti yake yenye haya.
Joram alimzawadia tabasamu, bila shaka la kumtia moyo. “Sidhani kama suala la kukitupa litakuwepo,” alimwambia. “Kama kingekuwa kitabu cha kutupwa nisingesoma Zaidi ya kurasa mbili. Ningekinai zamani na kukurudishia…”
Mhudumu alitokea na kumwongezea Joram kinywaji. Mona Lisa alikataa kwa maelezo kuwa mvinyo aliokunywa ulikuwa unatosha.
“Nadhani nirudi mjini,” alimwambia Joram taratibu.
“Mara hii?” Joram aliuliza. “Una haraka gani, wewe msichana? Unajua nimeanza kukuzoea. Halafu, unajua kuwa hatujafahamiana hata kidogo? Nilidhani tutakaa, tuongee, tule chakula cha usiku pamoja na ikiwezekana tuingie muziki.”
Mona aliachia moja ya zile tabasamu zake za kusisimua, tabasamu ambalo lilimfanya Joram aanze kujutia mzaha wake. “ nashukuru sana kwa ofa yako. Nivile tu sikujiandaa, ningechangamkia. Nitakupitia kesho kutwa nione umefikia wapi kwenye riwaya yangu.”
“Kesho kutwa! Kwa nini isiwe kesho!” Joram alisema akiinuka. Akauchukua mkono wa Mona Lisa na kuufinya kidogo, kabla hajaubusu. Kisha, aliutua taratibu huku akisema, “Kumbe! Haya nimeelewa.”
“Nini?” Mona Lisa aliuliza kwa mshangao.
“Nimeelewa kwa nini umekataa ofa yangu ya kuingia muziki.”
“Umeelewa nini?”
“Unaogopa!”
“Naogopa nini?”
“Mchumba wako.”
Mona Lisa akaangua kicheko. “Mchumba! Mchumba gani? Mie bado niko single. Sina mume wala mchumba,” alisema.
“Umeanza kuwa mwongo,” Joram alimwambia. “Pete hiyo hapo inakusuta. Kama si ya uchumba ni ya ndoa.”
Mona alicheka tena. “Watu wengi wanasema hivyo,” baadaye alisema. “Kila mtu anadhani hii ni pete ya uchumba. Hii naivaa kama mapambo tu, jamani,” alisema akiishikashika.
Joram alionyesha kutomwamini.
“Kama huamini,” Mona alisema akiivua. “Nitakuachia uivae hadi kesho kutwa nitakapokuja.”
Joram aliipokea na kuitazama. Ilikuwa pete kubwa, iliyotengenezwa kwa mchanganyiko wa madini ya Tanzanite na ruby. Kwa ndani ilikuwa na kito kinachong’ara, ambacho Joram hakuweza kujua mara moja kama ilikuwa almasi au kioo.
“Hii ni pete ya thamni kubwa,” Joram alisema baada ya kuitazama. “Unaiacha kwa roho nyeupe?”
“Bila wasiwasi.”
“Mchumba wako utamwambiaje?”
“Si nimeshakwambia sina mchumba?”
“Uliipata wapi basi peteb ya bei mbaya kama hii?”
“Ni hadithi ndefu. Tuiache hadi kesho kutwa nitakapo kuja.”
Huku akimshika mkono, Joram alimwuliza, “Bado umeng’ang’ania kesho kutwa. Mimi nakuhitaji hapa kesho.”
“Kesho! Ilikuwa zamu ya Mona Lisa kushangaa. “Kurasa mia mbili na arobaini utakuwa umezimaliza kesho!”
Joram alicheka. “Bila shaka,” alisema. “Nina tabia ya kuamka saa kumi za alfajiri na kufanya mazoezi hadi saa kumi na mbili. Toka hapo kazi yangu huwa ni kusoma magazeti yote yaliyochapishwa nchini siku hiyo. Kama naweza kusoma magazeti ishirini na tatu, yenye Zaidi ya kurasa kumi na sita kila moja,nitashindwa kusoma na kuimaliza riwaya tamu kama hii kabla ya saa nne asubuhi?”
Mona Lisa alimtazama kwa mshangao. Hakuelekea kuamini. Hata hivyo, alisema, “Nitajitahidi kuja kesho jioni basi, kama nitapata wasaa.”
“Nitakuwa juu ya kiti hikihiki nikikusubiri,” Joram alimwambia.
Mona akaendea mojawapo ya magari ya kukodi yaliyokuwa nje ya hoteli na kutokomea.
Mara tu Mona Lisa alipotoweka machoni mwake hisia za upweke zikamjia Joram Kiango. Alihisi hali ambayo hakupata kuhisi huko mbeleni, hali ya kitu kama unyonge au kupungukiwa kitu Fulani.
“Nimeanza kuwa mzee, nini?” alijiuliza akiichezea pete aliyoachiwa. Jana alimtazama Mona Lisa kwa namna iliyofanya ajiwe na hisia za mapenzi na kiujenga matumani ya mahaba mazito toka kwake, hisia zilizomfanya hata afikie hatua ya kumkumbatia na kumbusu, lile busu moja tu, busu la kwanza, ambalo lilimloga Zaidi.
Leo alijitahidi vilivyo kuziweka nyuma ya kisogo chake hisia zile ingawa hakufanikiwa sana. Huyu ni msichana mdogo tu, Joram. Alijinong’oneza mara kwa mara. Ndiyo, ni mzuri… na mwili wake unafariji… lakini bado ni mdogo tu, tena anahitaji msaada wako. Uko wapi ule ushujaa wako?... Uko wapi ule msimamo wako usiotetereka?Ni hayo ambayo muda wote yalikuwa yakipiga kengele katika kichwa chake hadi pale Mona Lisa alipoinuka na kuaga. Vipi sasa ajisikie kama anavyojisikia? Vipi afikie hatua ya kukubali kubaki na pete yake?

Nadhani ni kweli… Uzee unaninyemelea, alinong’ona tena, akiagiza kinywaji kingine.
“Leta chupa nzima… Huchoki kuleta hivi vitoti? Alimwamuru mhudumu.

***
“Mpenzi nimerudi,” sauti ilimzindua Joram Kiango. Ilikuwa ile sauti tamu, ambayo muda mfupi uliopita ilikuwa ikimfariji.
Joram aliinua uso wake kumtazama Mona Lisa. Kama muda mfupi uliopita alikuwa mzuri sasa alikuwa malaika. Alikuwa amejipulizia pafyumu nyepesi iliyofanya hewa iliyomzunguka ijae hisia za mahaba. Kama awali uso wake uling’ara, sasa ulimeremeta kwa aina ya poda au mafuta aliyoyatumia. Nywele zake, ambazo awali zilifungwa kichwani sasa ziliachiwa na kujimwaga hadi mabegani mwake na, hivyo, kufanya suala la kujua kama msichana huyu ni Mbantu, Mhindi au Muajemi liwe tatizo. Kilichohitimisha u-malaika wake katika ujio wake huu lilikuwa vazi lake. Alivalia vazi la usiku, nguo laini, iliyofichua vilivyo ubora wa umbile lake.
Joram alihamisha macho yake toka juu ya umbo hilo la kuvutia na kuitazama saa yake, tano na dakika arobaini. Saa tatu zilikuwa zimepita toka Mona Lisa alipoondoka hapo kwa ahadi ya kurudi kesho. Dakika ishirini zilibakia kabla ya kuingia siku mpya ya Jumamosi. Na zilisalia saa kumi na mbili kabla ya kufikia miadi yao. Kulikoni?
Mona Lisa alikuwa kama anayeyasoma mawazo ya Joram.
“Naona hujaridhika na ujio wangu,” alisema. “Samahani sana kama nitakuwa nimekuudhi. Hisia za upweke zilinibana nikashindwa kuvumilia. Naweza kuondoka kama…”
“Hapana, hapana,” Joram alisema akiinuka kumkaribisha. “Ujio wako umenifurahisha sana . ni vile tu sikukutegemea hadi kesho. Keti, tafadhali… jisikie uko nyumbani,” alisema akimshika kiuno na kumkumbatia. Akambusu, busu ambalo lilijibiwa kwa mbwembwe zote.
“Utakunywa nini?”
“Kama hutojali nitapenda kuonja hicho ulichokunywa wewe. Ni John Walker, sio?”
“Ndiyo.”
Joram aliagiza glasi ya pili. Tayari alikuwa amemaliza chupa nzima ya wiski hiyo, jambo ambalo aliamini kuwa lilitokana na hisia za upweke toka pale Mona Lisa alipoondoka. Hivyo, kichwa chake alikiona chepesi huku macho yake yakiwa mazito kiasi. Lakini hilo halikumfanya ashindwe kuiona tabia ya kinyonga katika msichana huyu. Ama nusu glasi aliyokunywa ilikuwa imemaliza hay azote, ama alikuwa akinywa toka alipoondoka hapa.
Alikuwa hazungumzi sana. Lakini alichekelea kila kauli ya Joram huku akitia neno hapa na pale, jambo ambalo lilimfanya Joram acheke. Aidha, aliongea kwa maneno na vitendo. Mara kwa mara mikono yake iliruka na kutua hapa na pale katika mwili wa Joram. Mara achezee vidole vyake. Mara mkono utue na kutulia juu ya paja lake.
Ukiwa usiku mwingi, upepo mwanana wenye marashi ya karafuu ukiwapepea toka visiwani. Kama binadamu, kama mwanamume rijali Joram hakuwa na uwezo wa kustahimili hali ile. Bila kutegemea alijikuta yeye pia akiingia katika mchezo wa mikono. Alimshika hapa na pale. Mona alionekana kuridhia. Taratibu walianza kubusiana.
Mara Mona aliinuka na kumshika Joram mkono. “Twende zetu,” alimwambia.
“Wapi?”
“Kwani huna chumba?”
Ilimshangaza Joram kuona kuwa pamoja na mwili wake kusisimkwa na matarajio, roho yake ilikuwa nzito. Hisia Fulani, ambazo hakuweza kuzifafanua ziliashiria shari badala ya heri. Hivyo, wakati akiongozwa kupelekwa chumbani kwake, alihisi kama mwanakondoo anayepelekwa madhabauni kutolewa kafara, badala ya kijana mzuri, aliyefuatana na msichana mzuri, anayetarajia kuufurahia ujana wake.

‘Umeanza kuwa mzee, Joram…’kitu Fulani kilianza tena kumnong’oneza, kauli ambayo ilimezwa pale kitanda kipana kilipowapokea na kuwakumbatia.
***
Muda mfupi baadaye.
“Joram!”
“Na…am!”
“Unajua unachokifanya?”
“Si…jui.”
“Ni kweli hujui… Hujui kuwa unabaka! Na unambaka afisa wa ngazi za juu wa Jeshi la Polisi,” sauti ya Mona ilisema, ikisindikizwa na kicheko.
“Sikujua,” Joram alijibu. “Nilidhani mimi pia nimebakwa.”
Kicheko.
“Ni wazii kuwa hujaipitia sharia ya ubakaji. Mwanaume habakwi, anabaka. Unaijua adhabu yake?”
“Siijui.”
“Miaka ishirini na nane jela. Lakini kwako wewe adhabu hiyo haikutoshi. Utafungwa kifungo cha maisha, pingu mkononi.”
Kicheko.
“Naanza lini kuitumikia adhabu hiyo?”
“Toka sasa uko chini ya ulinzi. Huruhusiwi kukutana na mwanamke mwingine. Huruhusiwi kuoa wala kuolewa…”
Kicheko. Usingizi uliwachukua huku wakiwa wamekumbatiana, wakiwa bado wanacheka.








3
Ni kitu kama unyevunyevu uliomgusa ghafla ubavuni, ambacho kilimfanya Joram Kiango aamke toka katika usingizi wa pono, uliokuwa umemchukua. Akiwa bado ameyafumba macho yake aliuondoa mkono wake toka kifuani mwa msichana aliyelala kando yake na kuutuma kuupeleleza unyevunyevu huo. Vidole vyake viligusa kitu kama maji mazito mithili ya uji uliopoa. Kitu gani hiki? Alijiuliza akiutoa mkono wake huko ulikokuwa na kuuleta puani ili kuunusa.
Ilikuwa harufu ngeni, lakini aliyoifahamu vilivyo. Harufu ya damu! Mara moja akayalazimisha macho yake, ambayo aliyaona mazito kuliko kawaida yake, kufunguka.

Damu! Mkono wake ulikuwa umejaa damu!
Hakuamini. Akakiinua kichwa chake kizito kumtazama msichana aliyelala kando yake. Alikuwa amelala kwa utulivu kupita kiasi. Uso wake ulikuwa na tabasamu lililofanya kama kusahauliwa pale. Kifuani alikuwa na tundu kubwa lililokuwa likiendelea kuvuja damu ambayo ilianza kuganda, damu nzito ambayo ndiyo iliyokuwa imetambaa hadi kuutembelea ubavu wa Joram.
Hii ni ndoto, au… Joram alijiuliza akiinuka harakaharaka. Kwa dakika moja au mbili aliduwaa wima, katikati ya chumba hicho, akimtazama kiumbe aliyepoa pale kitandani. Kiumbe ambaye muda mfupi uliopita alikuwa hai, hai kuliko uhai wenyewe, wakacheka na kucheza pamoja hadi usingizi ulipowatenganisha, kiumbe ambaye sasa alikuwa marehemu.
Katika kipindi hicho kifupi cha kuduwaa mbele ya maiti, mambo elfu na moja yalipita katika kichwa cha Joram Kiango. Yalimjia mfululizo, bila mpangilio, kiasi cha kufanya ashindwe kujua aanzie wapi aishie wapi katika kuutafakari mkasa huo mzito uliomsibu. Kwanza, alishangazwa na uzito wa ubongo wake katika kufikiri. Aliiona akili yake kama iliyoduwaa, kinyume cha kawaida yake anapokuwa katika masaibu hayo. Pia, aliduwazwa na udhaifu wa mwili wake. Hata macho yake alihisi kuwa anafanya kuyalazimisha kuwa wazi. Vinginevyo, alijisikiakama mtu aliyekuwa tayari kuendelea kupiga usingizi wake, hadi wakati muafaka, atakapoamka na kisha kuanza kujiuliza nini kinachotokea.

Changamka Joram! Uko hatarini! Hatari yenyewe kubwa kuliko unavyofikiria! Amka! Chemsha ubongo wako! Sauti Fulani, toka nyuma ya kisogo chake ilimhimiza.
Joram aliitii. Dakika iliyopita alikuwa ameduwaa, ubongo ukiwa umeduwaa. Dakika iliyofuata akili yake ilikuwa makini. Alianza kwa kujikumbusha kuwa kwanza alihitaji kutuliza akili yake. Katika hali hiyo ya utulivu aliitazama saa yake. Ilimwambia kuwa ilikuwa alfajiri, saa 11:45. Hata alipotupa amcho nje aliona miale ya mwanga wa jua ikianza kuashiria mapambazuko.
Baada ya hapo Joram aliutupia macho tena mwili wa marehemu. Hakuhitaji daktari kuthibitisha kuwa alikata roho kitambo. Hali kadhalika, hata kipofu angejua kuwa kifo chake kilitokana na tundu la risasi iliyopenya kifuani mwake na kusababisha damu nyingi imwagike toka mwilini mwake.
Nani aliyemuua? Kwa nini amemuua? Aliwezaje kuingia chumbani humu na kufanikiwa kumuua msichana huyu asiye na hatia bila yeye kujua? Na ilikuwaje yeye Joram, mwenye maadui lukuki akaachwa hai? Hayo ni miongoni mwa mamia ya maswali yaliyokisumbua kichwa cha Joram Kiango. Hata hivyo, hakuona kama ulikuwa wakati muafaka kujaribu kutafuta majibu. Kitu Fulani kilikuwa kikimnong’oneza kuwa yeyote aliyefanya mauaji hayo ya kinyama alikusudia yeye aonekane kuwa ndiye muuaji, jambo ambalo lingemfanya achukue miaka, huku akiwa mahabusu, kuihakikishia dunia vinginevyo.
Joram hakuwa na wasaa huo, wasaa wa kukaa gerezani huku mtu Fulani anayeitwa wakili akiipigania roho yake. Alikuwa mtu wa kujipigania, mtu wa kisasi kwa yeyote aliyekatisha maisha ya Mona Lisa, msichana mwenye umbo la malaika.
Harakaharaka, Joram alianza kukusanya vifaa vyake muhimu. Aliliendea begi lake. Lilikuwa wazi. Na, kama alivyotegemea, bastola iliyotumika kumuulia Mona Lisa ilikuwa humo. Ilikuwa bastola kubwa, maalumu kwa majeshi ya polisi na usalama; K45. Joram akaifungua. Ilikuwa na risasi tano. Moja tu ilikuwa imetumika. Bila shaka ni ile iliyomuua Mona. Joram aliitia mfukoni mwake na kuifunga mifuko ya siri ya begi lake hilo.
Ilikuwa mitupu!
Silaha zake zote zilikuwa zimechukuliwa!
Akauacha mfuko huo na kuiendea meza ndogo ya chumbani humo. Macho yake yalikwenda moja kwa moja pale alipouweka mswada wa marehemu; UBONGO WA MWALIMU NYERERE.

Nao ulikuwa umetoweka!
Katika mtoto wa meza Joram aliipata simu yake ndogo ya mkononi. Akaichukua na kuitia katika mfuko wa suruali yake nyepesi ambayo aliivaa. Pia akavaa shati jeusi, viatu na kofia yake ya kawaida. Alifikiria kufuta alama za vidole vyake katika mwili wa marehemu na kila kitu chumbani humo. Wazo ambalo alilipuuza mara moja kwa kuzingatia kuwa uongozi wa hoteli ulikuwa na kumbukumbu zake zote, aidha wateja wote wa hoteli hiyo walimwona pindi akiburudika na msichana huyo ambaye sasa ni marehemu. Isitoshe, jaribio la kufuta alama hizo ni dalili ya kwanza kabisa ya mauaji ya kukusudia kwa mpelelezi mzoefu.
Mlango wa chumba ulikuwa wazi. Joram hakuutumia. Alimtupia marehemu jicho la mwisho. Huyo, akapenya dirishani kudondokea nje.
Dakika tano baadaye alikwishaliacha eneo la hoteli na kuingia katika mitaa iliyomwelekeza mjini.
 
Nameless japo tunapata burdan but tu nakumbuka mbali ni furaha ndani ya majonzi utunzi kama huu adhwimu kuupata kwa watunzi wa miaka hii hakuna.Mzee Ben,mzee ganzel na mzee musiba watabaki kuwa watunzi bora katika akili yangu.
 
Katika uhai wake wote wa kimatibabu Daktari Omari Shaka, hakupata kupokea mgonjwa wa aina hii, mgonjwa ambaye alijileta mwenyewe hospitali, huku akigugumia kwa maumivu, lakini akakatalia vipimo na dawa zote isipokuwa ‘kitanda’ na ‘vidonge vya usingizi tu.’ Mgonjwa huyohuyo alionekana mchovu kiafya na kiuchumi, bila kudaiwa, alitoa shilingi 50,000 kama malipo ya awali ya gharama za matibabu yake.
Daktari alichukulia siku hiyo kama siku mpya, ambayo ilianza na maajabu.
Ilikuwa ndio kwanza anaingia kazini, kushika zamu ya daktari mwenzake ambaye alimaliza saa kumi na mbili asubuhi. Ikiwa hospitali yao binafsi, mpya, iliyojengwa katika eneo la watu wenye kipato cha chini, siku zote kwao wagonjwa waliendelea kuwa bidhaa adimu. Si kwa kuwa magonjwa yalikuwa yamepungua, la; isipokuwa gharama za matibabu ndizo zilizokuwa zikiwakimbiza. Wengi waliugulia majumbani na kupoteza maisha. Wengi walikimbilia kwa waganga wa jadi ambao waliwapokonya hadi senti za mwisho bila uhakika wa tiba. Wengi, kati ya wachache waliokuja hospitalini hapo, waliondoka na madeni makubwa na, hivyo, kutorejea tena.
Hivyo, anapokuja ‘mgonjwa’ mwenye shilingi elfu hamsini mkononi, na madai ya kuujua vizuri ugonjwa wake, kwamba anachohitaji ni kitanda cha mapumziko na vidonge vya usingizi, baada ya hapo ndipo atakubali vipimo, nani amkatalie?
Alilitupa chini gazeti alilokuwa akilisoma na kuvuta jalada jipya ambalo aliliandika tarehe na kisha kumgeukia mgonjwa wake.
“Jina lako?”
“Sharif Mkono wa Birika.”
“Umri?”
“Miaka sitini na tano.”
“Unakoishi?”
“Kinondoni B”
“Mjumbe…” na kadhalika na kadhalika.
“Una hakika kuwa usingependa kupimwa walao presha? Unajua tuna taratibu zetu…”
“Daktari vipimo vyote utachukua. Lakini baada ya mapumziko yasiyopungua masaa ishirini na nne. Najifahamu, Daktari. Niwahishie kitanda, tafadhali.”
Alipatiwa kitanda katika chumba pekee maalumu hospitalini hapo.kilikuwa chumba chenye vitanda vitatu, yeye akiwa mgonjwa pekee, jambo ambalo lilimfurahisha sana. Baadaye nesi alipomletea vidonge viwili vya piritons, alivipokea na kusingizia kuvimeza. Alikunywa maji matupu, akamrejeshea nesi glasi na kisha kujifunika gubigubi. Muda mfupi baadaye alisikika akikoroma kwa mbali.
Joram alikuwa amejisingizia ugonjwa ilia pate nafasi ya kujificha, akiwa ametulia, ili aweze kupata fursa ya kufikiri na kutafakari kwa kina kitu gani kinamtokea, nini kinachofuata na achukue hatua zipi kukabiliana na hali hiyo.
Kutoweka lilikuwa jambo la awali na muhimu sana. Alijua kwa vyovyote usingepita muda kabla ya mauaji hayo kuarifiwa polisi nay eye angekuwa mtuhumiwa wa kwanza. Kwa tabia ya polisi wa Tanzania, nap engine kote duniania, alijua ambacho wangefanya ni kumkamata kwanza na kuanza upelelezi baadaye. Akiwa na pingu mkononi, nyuma ya nondo kubwa, Joram alijua kuwa huo ungekuwa mwisho wa ndoto yake ya kukielewa kiini cha mkasa huo na mwisho wa dhamira yake ya kumwadhibu yeyote ambaye amemuua msichana mpole kama yule, mzuri kama yule, malaika asiye na hatia yoyote.
Uamuzi wa kujificha hapa kwa muda aliuchukua mara alipotoka pale hotelini. Alijua fika kuwa pindi taarifa za mauaji zitakapowasilishwa kwenye vyombo husika, na yeye kutajwa kama mtuhumiwa, msako kabambe dhidi yake ungetangazwa. Nchi jirani n azote zilizo katika mkataba wa INTERPOL pia zingeusishwa. Hoteli na majumba yote ya wageni yangepekuliwa, madanguro na magenge yote yangekaguliwa. Hata magari mabovu na magofu yote jijini yangechunguzwa. Joram alikuwa na hakika kuwa mahala pa mwisho ambapo polisi wangepafikiria kumtafuta, ni hapo, wodini.
Kichwani mwake hakuona kama ni jambo jema sana kujisingizia ugonjwa, akichelea kuwa unaweza kumchukiza Mungu ukajikuta umekuwa mgonjwa kwelikweli.
Aliwahi kusoma mahala Fulani, juu ya mtu mmoja kule Harare, wakati ule wa shida kubwa ya mafuta kufuatia vikwazo vya kiuchumi dhidi ya nchi ile, kwamba walisubiri mgao wa mafuta tangu saa mbili usiku na kuja kuyapata saa tisa alfajiri. Magari pekee yaliyotiliwa maanani yakiwa yale yaliyobeba wagonjwa au maiti. Hivyo jamaa Fulani walilazimika kununua jeneza na sanda, mmoja wao akijilaza katika jeneza hilo na kuvishwa sanda. Wakapatiwa mafuta na kuondoka zao. Lakini walipofika mbele ya safari na kusimamisha gari ili wamtoe mwenzao walimkuta tayari amekufa kikweli kweli. Msiba wa kusingizia ukaanza upya.
“Yasije yakanitokea hayo…” Joram aliwaza huku akicheka kimoyomoyo ndani ya shuka zake za hospitali alimojifunika.
Akaituma akili yake kuanza kufikiri kwa makini Zaidi. Jambo la awali ambalo hakuona kuwa lilihitaji kumpotezea muda ni vipi muuaji alivyoweza kuingia chumbani mule na kumuua Mona Lisa kwa risasi, yeye akiwa kwenye usingizi wa pono. Bila shaka muuaji huyo aliwapulizia dawa ya usingizi na, hivyo, kuingia chumbani humo na kufanya mauji yake kwa kutumia bastola yenye kiwambo cha kuzuia sauti bila yeye kuwa na habari.
Alihisi dawa hizo hadi sasa bado ziliufanya ubongo wake ushindwe kufanya kazi yake kwa kiwango chake halisi.
Hata hivyo, akiwa kitandani hapo, taratibu aliona kama utandu katika ubongo wake ukianza kudondoka na mambo kadhaa aliyokuwa akiyaona katika hali ya ukungu yakianza kutoweka na kuonekana katika hali yenye uhalisia Zaidi.
Kilichozindua akili yake ni pale alipokumbuka kumwona Daktari Omari, wakati akimwandikia cheti, aliandika kitu kama jumatatu, tarehe 25 Septemba! Hata gazeti lililolala pale mezani pake lilikuwa la Jumatatu.
Jumatatu! Joram alishangaa. Alikumbuka vizuri sana, kwamba alikutana na Mona Lisa siku ya Jumamosi na aliingia naye chumbani mle usiku mwingi wa Jumamosi ileile. Ilikuwaje aamke, akiwa amemkumbatia Mona Lisa yuleyule, au maiti yake, siku ya Jumatatu? Inawezekana kuwa walilala chumbani mule kwa takribani saa ishirini na nne? Inawezekana!
Joram aliituma akili yake kufikiri. Alizirudisha fikra zake kama mkanda wa picha toka pale Mona aliporejea ghafla na kumwambia “Mpenzi nimerudi…” kinyume cha rai yake ya awali kurudi kesho yake. Aliufikiria uchangamfu wake uliomfanya ajikute yuko naye chumbani. Aliufikiria utundu wake kitandani uliopelekea ajione kuwa yuko peponi anayeburudishwa na malaika halisi. Akaifikiria ile kauli yake ya mwisho, kabla usingizi haujampitia.
Muda mfupi baadaye.

“Ni kweli hujui… Hujui kama unabaka. Na unambaka afisa wa ngazi ya juu wa Jeshi la Polisi…”
Kicheko.
“Sikujua… nilidhani mimi pia nimebakwa.”
Kicheko.
“Ni wazi kuwa hujaipitia vizuri sheria ya ubakaji. Mwanaume habakwi, anabaka. Unaijua adhabu yake?”
“Sijui.”
“Miaka ishirini na minane jela. Lakini kwako wewe adhabu hiyo haitoshi. Utafungwa kifungo cha maisha, pingu mkononi.”
Kicheko.
“Naanza lini kuitumikia adhabu hiyo?”
“Toka sasa uko chini ya ulinzi. Huruhusiwi kukutana na mwanamke mwingine. Huruhusiwi kuoa wala kuolewa…”
Kicheko. Usingizi…

Kwa mujibu wa kumbukumbu iliyomjia Joram hayo yalikuwa maongezi yake ya mwisho na Mona Lisa kabla hajaamka na kujikuta akiwa amekumbatia maiti yake, tundu kubwa la risasi kifuani pake likiendelea kuvuja damu.
Huo ulikuwa usiku wa Jumamosi au alfajiri ya Jumapili. Kilichomshangaza ni hii hadithi mpya ya kuwa leo ni Jumatatu. Ukweli ni upi, Jumapili au Jumatatu?
Joram hakuona kama alikuwa na haja ya kuupoteza muda wake kufikiria kama leo ilikuwa Jumapili au Jumatatu. Kama daktari ameandika tarehe ya Jumatatu na kama hata gazeti lilikuwa la Jumatatu, kwa vyovyote siku ya leo ni Jumatatu. Alichohitaji kufanya ilikuwa ni kukusanya akili yake ili imwambie kitu gani kilimtokea hata akalala kwa saa ishirini nan ne bila kujua kinachoendelea.
Ilikuwaje? Alijiuliza.
Taratibu, ule utandu uliokuwa ukiudumaza ubongo wake ukaanza kumtoka na picha mpya kuingia akilini. Ilikuwa kama mkanda wa video ambao unarudishwa nyuma na kuchezeshwa upya.
Sasa alikumbuka vizuri kabisa kuwa mara baada ya Mona kumwambia, “Huruhusiwi kuoa wala kuolewa…” na usingizi kuwachukua, Mona Lisa alitoweka.
Joram alibaini kutoweka huko pale alipoamka na kushituka mida Fulani baina ya saa tatu au nne na kujikuta peke yake. Ubavuni mwake, pale alipolala Mona Lisa, sasa palikuwa na mto ambao yeye, Joram, aliukumbatia. Hakujali, akijua kuwa msichana huyo alikuwa ameondoka kimyakimya kwa kuchelea kumsumbua. Akaurudia usingizi wake ambao aliuchapa hadi saa saba za mchana huo. Baada ya kuoga, kunywa supu na chupa mbili za club soda alirejea chumbani kwake ambako alijilaza chali na kuendelea na mswada wa Mona, UBONGO WA MWALIMU NYERERE.
Ilikuwa riwaya tamu. Ilimvutia na kumsisimua kiasi kwamba alijikuta amezama moja kwa moja katika msitu huo wa maneno yaliyopangiliwa kisanii. Ilimwia vigumu Zaidi kuamini kuwa mbunifu mwenyewe alikuwa msichana mpole na mrembo kama yule. Ufundi wa matumizi ya lugha, hila katika mpangilio wa matukio na Zaidi ya yote uhalisia wa matukio ya mambo katika hadithi hiyo ni miongoni mwa mambo yaliyomfanya Joram amezwe moja kwa moja, bila kujua kuwa muda umekwenda, hadi aliposikia mlango wake ukigongwa.
Kabla ya kuinuka kuufungua aliitazama saa yake ya mkononi. Tatu kasoro! Hakuamini. Alipoufungua mlango umbile zuri la Mona Lisa lilikuwa limesimama pale, tabasamu lenye hayahaya na kutojiamini likiwa limechanua usoni pake.
Darling! Karibu sana,” Joram alisema akimshika mkono na kumvuta ndani ambako alimkaribisha tena kwa busu jingine.
Kiasi fulani Mona Lisa alionyesha kushangazwa na mapokezi hayo. Alimtazama Joram kwa muda, kisha akayakwepa macho yake na kujiinamia. Joram pia alishangazwa na hali hiyo. Muda mfupi tu uliopita ulikuwa mchangamfu kuliko mie, mara hii umebadilika tena! Achana na tabia hizo za kinyonga! Alitamani kumweleza. Lakini hakufanya hivyo. Badala yake alimwambia taratibu, “Chumba hiki chako, chagua kukaa ama kitandani, ama kwenye kochi.”
Mona aliliendea kochi na kuketi.
“Kitabu chako kimenishika kwelikweli,” Joram alimwambia. “Sikujua kama muda umeisha kiasi hiki. Nikuagizie chakula na kinywaji gani?”
Mona alitabasamu, “Kizuri?”
“Kitu gani?”
“Kitabu. Ni kizuri kweli?”
Joram akatabasamu. “Kizuri kama alivyo mtu aliyekiandika. Kikitoka utapata washabiki kila pembe ya dunia. Utakula nini?”
“Unaamini kitakubaliwa?” Mona alihoji tena kwa shahuku.
“Ni mchapishaji kipofu wa taaluma peke yake anayeweza kukataa kitabu kama hiki. Ingawa kuna mambo mawili matatu atakayoyatoa na kuyaongeza. Hata hivyo, sijafika mwisho,” Joram akasita, “Hujaniambia utakula nini na utakunywa nini.”
Ilikuwa dhahiri kuwa akili za Mona hazikuwa kwenye chakula wala kinywaji, bali kwenye maandishi yake, hali ambayo ilimshangaza Joram. Jana hakukitaja kabisa kitabu hicho, leo hataki kusikia jambo lolote Zaidi ya kitabu.
Kinyonga!
“Siwezi kukaa hapa na msichana mrembo kama wewe, bila kumkirimu walao maji ya uhai. Nawapigia jikoni watuletee kuku mzima, chupa mbili za wiski na tonic. Sawa?”
Joram alisubiri jibu la Mona Lisa.
“Samahani sijisikii kula wala kunywa chochote.”
“Kwa nini? Za jana bado zipo kichwani?”
“Jana!” ilikuwa zamu ya Mona Lisa kushangaa. “Jana nimekunywa wapi! Sijawahi kunywa pombe toka nizaliwe.”
Joram hakuyaamini masikio yake.
“Wacha mzaha Mona,” akamwambia akicheka. “Jana umerudi hapa ukanipa company ya nguvu, ukanywa kiasi cha kunifariji hapo kitandani hadi ulipotoweka bila kuniaga!”
Kilichofuata baada ya hapo Joram hakukitegemea. Joram alimwona Mona Lisa akisimama na kumtumbulia macho ya mshangao, akiwa ameusahau mdomo wake wazi, huku akitetemeka mwili mzima. Taratibu mshangao ulianza kutoweka katika macho yake na nafasi yake kuchukuliwa na hasira, hasira za mwanamke, hasira ambazo Joram, pamoja na ujabali wake wote hakupata kuziona kwa mwanamke yeyote yule. Lakini hali hiyo pia ilitoweka taratibu katika macho yake na nafasi yake kuchukuliwa na kitu kama msiba au maombolezo, jambo lililofuatiwa na kilio cha kwikwi, kwa sauti ndogo, huku machozi mengi yakimtoka.
Kwa Jpram Kiango ile picha ya kusisimua ilikuwa imerudi, picha ya msichana mpole, mrembo, mwenye maumivu Fulani rohoni mwake, picha ya malaika anayeteseka! Ambayo mwanaume yeyote asingeivumilia. Hivyo, bila ya kujipa wasaa wa kutafakari Zaidi alimwendea na kumkumbatia. Akamvuta taratibu hadi kitandani ambako alimketisha na baadaye kumlaza huku akiwa amemkumbatia, mkono wake wa pili ukijipa kazi ya kumfuta machozi.
Mona alinyamaza kidogo na kumuuliza Joram kwa sauti ya mnong’ono, “Unaniambia kweli, Joram?”
“Kwamba?”
“Kwamba jana nimerudi hapa na kuwa nawe hadi asubuhi ya leo?”
“Kwa nini nikudanganye?” Joram alimjibu kwa swali vilevile. “Kwani kulikoni, Mona, mbona sikuelewi!”
Mona akaanza kulia tena. Baadaye alinong’ona tena kama anayezungumza peke yake. “Hata wewe! Hata Joram Kiango! Nifanye nini jamani?”
“Kuna nini?” Joram alihoji tena. “Kuna jambo gani la muujiza wewe kurudi hapa na kuwa name?”
“Hujui Joram, hujui; huelewi. Na uwezi kuelewa,” Mona alisema na kuongeza, “Hujui kuwa tayari nimeyaweka maisha yako hatarini. Sijui kitu gani kinachonitokea. Lakini naamini nimekuweka katika hatari kubwa sana katika maisha yako.”
“Hatari gani?”
“Ya kifo.”
Joram akaangua kicheko. “Yaani kufurahi na wewe usiku mmoja kwangu ni hukumu ya kifo! Acha mzaha Mona. Mie sio mshirikina kiasi hicho!”
“Joram, hufahamu,” Mona aliongeza. “Kwanza, hukulala na mimi. Halafu, suala la ushirikina halipo.”
Joram akacheka tena. Akasema, “Kwa hiyo tuachane na ushirikina. Twende kwenye elimu ya akhera. Ni kwamba nimelala na jini linalotumia sura yako, jini ambalo baadaye linatiua, sio? Usinichekeshe Mona”
“Huwezi kuelewa,” Mona alinong’ona tena. Ingawa sasa kile kilio cha kwikwi kilikoma, machozi yaliendelea kutiririka juu ya mashavu yake laini, Joram akiendelea na kazi ya kuyafuta na kumfariji.
Kuna ugonjwa Fulani. Ugonjwa adimu, ambao ni madaktari wachache hadi sasa wanaoufahamu. Ni aina fulani ya matatizo ya akili ambapo mhusika hujikuta amesahau yeye ni nani na kujihisi kama mtu mwingine kabisa mwenye jina na tabia tofauti. Akiwa katika hali hiyo anaweza kufanya chochote, hata kuua bila kujua analolifanya.
Maradhi hayo yanaweza kumfanya mtu kuwa na nafsi mbili au tatu zenye majina na tabia tofauti. Anaweza kuwa Amina, Asha au Aisha kivitendo na kitabia kwa nyakati tofauti. Wakati mwingine Amina au Asha huyo anaweza kuchukiana au hata kuoneana wivu na Aisha, kwa kutegemea wakati huo mgonjwa yuko katika taswira ipi.
Zipo kesi kadhaa za aina hiyo, baadhi zikihusisha hata mauaji, lakini watuhumiwa wakaachiwa huru na mahakama baada ya kuthibitisha kuwa wanaugua ugonjwa huo.
Joram aliamini kuwa Mona Lisa alikuwa na tatizo hilo. Aliamini kuwa alipomfuata jana na kunywa, ambako anaapa kuwa hajawahi kunywa maishani, alikuwa katika taswira yake mpya amabayo yeye binafsi haifahamu, taswira ya msichana wa kileo, sister doo, asiye na haya na mwingi wa mbwembwe.
Ni hilo lililomfanya aamue kumfariji na hata pale Mona Lisa alipoomba kuondoka Joram alikataa katakata kwa maelezo kuwa asingemruhusu kuondoka katika hali hiyo.
“Joram, mara hii naona unafanya jambo ambalo hujui hatma yake. Laity ungenisikiliza…” Mona alimtahadharisha.
“Najua… Usijali…”
Wakiwa katika hali hiyohiyo ndipo usingizi ulipowapitia. Na ndipo Joram Kiango alipozinduka alfajiri na kujikuta akiwa amekumbatia maiti ya aliyekuwa Mona Lisa huku tundu la risasi katika kifua chake likiendelea kuvuja damu.
Ndivyo ilivyokuwa.



 
Utunzi maridhawa kabisa Huu.
Utaileta yote ama n do itatubidi tusake copy ?
 
dah nitakupigia kesho kama kutakuwa na uwezekano tukutane posta nichukue kitabu cha hii stori... Mimi ni mtumwa katika kusoma vitu kama hivi.. Mngekuwa mpo ofisini ubungo mpaka saa mbili ningekuja usiku ningekuja leo leo
 
dah nitakupigia kesho kama kutakuwa na uwezekano tukutane posta nichukue kitabu cha hii stori... Mimi ni mtumwa katika kusoma vitu kama hivi.. Mngekuwa mpo ofisini ubungo mpaka saa mbili ningekuja usiku ningekuja leo leo
Hakuna shida. Karibu.
 

“Sio kazi yako kutuuliza,” mwingine alimjibu. Wewe endelea na kazi yako. Siye tutakuwa hapa kuhakikisha unaifanya kwa usahihi.”
“Lakini… lakini…”
Kofi likatua barabara shavuni mwake. Lilikuwa kofi kali ambalo lilimtia kizunguzungu. Kofi la pili lilimfanya pombe zote zimtoke.
Sasa utafanya kazi yako kwa adabu. Sawa?”
Huku akitetemeka aliitikia kwa kichwa.

***
Kama siku ilikuwa imeanza kwa maajabu basi ilimmalizikia Daktari Omari Cheka kwa maajabu zaidi.
Utaratibu waliojiwekea na mshirika wake ulikuwa wa kufanya kazi saa ishirini na nne. Hivyo, toka alipoingia kazini jana asubuhi alikuwa bado yuko zamu, akihudumia wagonjwa. Kwa kuwa wagonjwa walikuwa adimu kazi kubwa aliyoifanya ilikuwa kupitia magazeti yote yaliyomfikia, na wakati mwingine kuyarudia. Hiyo ilimsaidia kupunguza usingizi.
Ikiwa tayari ni usiku wa manane kazi ya kupambana na usingizi ilikuwa ngumu kuliko hata kupambana na Jibril anapotaka kupokonya roho ya mgonjwa wake.
Usiku wa leo hospitali ilikuwa na mgonjwa mmoja tu, yule mgonjwa wa ajabu aliyetoa fedha nyingi na kuomba kitanda peke yake. Kutwa nzima mgonjwa huyo alikuwa amelala! Hadi sasa, usiku wa manane bado alikuwa amelala! Daktari Omari alikwenda kumtazama mara kadhaa na kumkuta akiwa anakoroma kwa utulivu. Alitamani kumwamsha ili ajadiliane naye juu ya maradhi yake. Lakini kwa mujibu wa taaluma yake, usingizi pia ni dawa. Hivyo, alimwacha aendelee kulala, naye akaendela kusubiri; gazeti mkononi, sigara mdomoni.
“Dakta!” sauti laini, ya mnong’ono ilimzindua. Daktari Omari alishituka na kuinua uso wake. Macho yake yalikutana na sura ya kike iliyokuwa ikimwangalia kwa tabasamu jepesi. Ilikuwa sura nzuri, ya kuvutia, pengine kuliko sura zote nzuri ambazo Daktari Omari alipata kuziangalia katika maisha yake yote. Umbile lake pia lilikamilika. Kiuno kilicho katika kike kabisa na kukifanya kiwe daraja baina ya kifua kilichojaa na mapaja yaliyojaza, kilimfanya Daktari Omari ahisi kuwa alikuwa hamtazami binadamu wa kawaida. Kama sio jini huyu ni malaika! Aliwaza, akiwa ameduwaa wima.
“Dakta, mbona hunikaribishi? Mimi ni mgeni wako,” mgeni huyo alihimiza.
“Ka-ri-bu!” omari alijikongoja kutamka. “Karibu kiti, tafadhali.”
“Sikai,” msichana huyo alisema taratibu. “Nimepata taarifa kuwa mzee wangu amelazwa hapa kwako. Nimekuja kumwona mara moja.”
“Mgonjwa wako! Anaitwa nani?”
“Sharif Mkono wa Birika.”
“Ameletwa lini?”
“Leo alfajiri.”
“Yupo,” Daktari Omari alijibu. Lakini amelala. Kwa nini usimwone kesho asubuhi?”
“Ni muhimu nimwone leo Dakta,” Mgeni huyo alisisitiza. “Kesho nitakuwa safarini. Na siwezi kuondoka bila kujua hali yake.”
Hakuwa msichana wa kukataliwa ombi lolote lile. Sauti yake ilishawishi. Macho yake yalilazimisha. “Ngoja nikaone kama anaweza kukuona,” Daktari Omari alisema. “Nimwambie unaitwa nani?” aliuliza.
“Mona.”
“Mona?”
“Mona Lisa.”
Daktari aligeuka na kuanza kuondoka. Hivyo, hakuiona bastola kubwa, ambayo ilichomoza ghafla na kumlenga kisogo. Kilichomshangaza ni maumivu ya ghafla, ya risasi iliyopenya kisogoni hapo na kukifumua kabisa kichwa chake. Aliduwaa kwa sekunde moja, akitamani kugeuka ili amtazame mwuaji wake. Hakufanikiwa, sekunde ya pili alikuwa tayari akidondoka kama kiroba huku ubongo wake uliochanganyika na damu ukifumka na kutembea sakafuni.
Mlio wa pili wa risasi ulifuatiwa na kuzimika kwa taa za umeme katika jengo zima na kiza totoro kuchukua nafasi yake. Wakati huohuo ving’ora vya magari ya polisi vilisikika ghafla huku na huko katika eneo hilo.

***
Tangu aliposikia vishindo vya kike vikiingia katika chumba cha Daktari Omari, Joram Kiango tayari aliinuka na kukiacha kitanda chake. Alinyata taratibu hadi nyuma ya mlango ambapo aliweza kuyasikia maongezi baina ya Daktari na mgeni uyo. Yalikuwa maongezi ya kushangaza. Mgeni alijiita Mona Lisa! Mona Lisa ambaye sasa ni marehemu kwa takribani saa ishirini na nne! Bastola yake ikiwa tayari mkononi, Joram Kiango aliusogelea mlango na kutafuta upenyo ili aweze kuchungulia na kumwona mgeni huyo.
Ni wakati akiwa katika jitihada hizo mlio wa bastola kubwa uliposikika ghafla na kufumua kichwa cha Daktari Omari. Joram Kiango alichupa angani kutoka mlangoni hapo. Hata kabla hajatua sakafuni bastola yake ilikwishalenga na kulipua taa ya umeme chumbani humo, kitendo kilichofuatiwa na umeme kukatika nyumba nzima. Alijibiringisha tena hadi dirishani ambako alilifungua taratibu na kuchupa hadi nje. Huko alitambaa taratibu kufuata uchochoro wa nyuma la jengo hilo.
Ving’ora vya polisi vilivofuatia milipuko ya bastola zile ilimshangaza zaidi Joram. Polisi! Wako hapa kufanya nini? Alijiuliza akizidi kujichimbia katika uchochoro huu.
Toka alipokuja hapa alfajiri ya jana yake na kujisingizia ugonjwa kwa jina la bandia, Joram aliamini kuwa si kwamba kuna mtu ambaye angeweza kujua kuwa yuko hapa tu, bali hata kufikiria kuwa anaweza kuwa hapa. Hivyo, kitendo cha mwanamke kutokea saa kama hizo, akimtafuta kwa jina la bandia aliloliandikisha, huku mwenyewe akijiita Mona Lisa, kilimshangaza sana. Aidha, kuwepo kwa polisi katika eneo hilo kulimshangza zaidi.
Maswali yalikuwa mengi kuliko majibu. Joram hakuona kama muda huo ulimtosha kuketi kuyatafuta, akiwa eneo la hatari kama hilo, aliendelea kunyata toka uchochoro hadi uchochoro, nyumba hadi nyumba; hadi akawa ameiacha hospitali kwa mita mia tatu au zaidi.
Uchochoro aliokuwa ameufuata ulimfanya atokee Barabara ya Morogoro. Mara moja aliyaona magari mawili ya polisi yakiwa yamesimama na askari kama wanne au zaidi wakipita huku na huko, bunduki mikononi, katika hali ya hadhari kubwa. Polisi hawa walikuwa katika mkao wa kuua kwanza na kuuliza maswali baadaye. Joram hakuwa tayari kufa ili ajieleze baadaye. Taratibu, kama kivuli, akaurudia uchochoro wake na kupenya hapa na pale kuelekea upande mwingine.
Kitongoji cha Manzese kikiwa kimejaliwa vichochoro lukuki, haikuwa kazi kubwa kwa Joram Kiango kupenya hadi kuifikia barabara iendayo Mabibo. Alichungulia kwa makini kabla ya kujitokeza barabarani. Kwa mara nyingine uangalifu wake ulimwokoa. Polisi wawili, wenye silaha walikuwa wamesimama hatua kadhaa mbele yake. Mmoja alikuwa akizungumza katika radio call, mwingine akivuta sigara.
Joram alikuwa amechoka kuishi vichochoroni. Juu, akiwa amevaa lile koti kuu kuu ambalo alilitumia kumlaghai Daktari Omari, na ndevu za bandia zenye mvi, baragashia kichwani, aliamini angeweza pia kuwalaghai polisi hao. Akajitokeza mtaani kwa mwendo wa mzee wa miaka sabini na kuwasogelea polisi hao.
“Simama!” askari mmoja alitoa amri huku akimwelekezea bunduki. Yule aliyekuwa akizungumza katika radio call pia aliacha na kujiunga na mwenzake kumkabili Joram Kiango.
“Weka mikono yako juu!”
Joram alitii.
“Wewe ni nani, unatoka wapi na unakwenda wapi saa hizi?” Mmoja wao aliuliza maswali kwa mfululizo mara walipomfikia.
“Naitwa Sharif Mkono wa Birika,” Joram aliwajibu.
“Unatoka wapi?”
“Nyumbani.”
“Unakwenda wapi?”
“Nyumba ndogo.”
Polisi mmoja alicheka. Mwenziwe alimkazia Joram macho ya mashaka. “Nyumba ndogo! Huo ni uzinzi mzee, umemuaga vipi mkeo?”
“Ah… nimemwambia nawahi sala ya alfajiri,” Joram alijieleza.
“Una kitambulisho chochote?” polisi yule alisisitiza.
Joram akacheka. “Kitambulisho! Nitakipata wapi mie? Biashara yangu genge la nyaya, miaka nenda rudi,” aliwajibu.
“Basi mzee, leo una bahati mbaya. Hutalala nyumbani kwako wala hutafika nyumba ndogo. Utalala polisi.”
“Kwa nini?”
“Tuna amri ya kumkamata mtu yeyote anayetia mashaka katika eneo hili, usiku wa leo. Wewe huna kitambulisho, halafu huna hoja ya msingi ya kutembea usiku.”
Joram alijifanya kaduwaa.
“Sogea hapa!” polisi alitoa amri. “Na endelea kuiweka mikono yako juu!” Aliamuru na kumsogelea ili kumkagua. Aliiweka bunduki yake mgongoni na kuipeleka mikono yake katika mifuko ya suruali ya Joram.
Kosa! Polisi huyo hakujua alipigwa na nini. Alihisi kitu kama nyundo kikiangukia upande mmoja wa kichwa chake na kumfanya aanguke chini kama mzoga. Polisi wa pili aliduwaa. Hata kabla hajajua afanye nini teke la punda lililompata barabara shingoni lilimfanya apepesuke. Teke la pili lilimmaliza. Yeye pia alianguka kama mzoga, juu ya mwili wa mwenziwe, fahamu zikiwa zimemtoka.
Dakika iliyofuata Joram alikuwa hatua elfu moja na moja nje ya eneo hilo, akifuata njia na vichochoro vya mkato kuelekea Mabibo na baadaye Mburahati.
Mburahati Joram aliikuta baa moja yenye kibali cha kuchekesha ikiendelea kuhudumia wateja wachache waliokuwepo. Aliketi na kuagiza Club soda baridi ambayo ilimsaidia kukata bia. Soda ya pili aliinywa kwa kuichanganya na toti mbili za konyagi. Ilipotimu saa tisa za usiku aliiendea moja ya teksi chache zilizokuwa zikisubiri abiria nje ya baa hiyo.
“Nifikishe town,” alimweleza dereva.
Town ipi?”
“Twende tu nitakueleza.”
Waliifuata Barabara ya Kigogo, wakaingia Ilala, Kariakoo na kuishia Mnazi mmoja ambako Joram alishuka na kumlipa dereva huyo ujira wake. Kisha alianza kuikata mitaa kwa miguu, akichukua kila adhari kuwa hakuna mtu anayemfuata wala kumfuatilia. Alipenya zaidi ya mitaa saba kabla ya kuifikia hoteli ya New Africa ambako alibahatika kupata chumba cha bei mbaya, baada ya kujieleza sana kwa karani ambaye awali alimtilia shaka.
“Jina lako, mzee?” Karani wa mapokezi alihoji akinukuu katika fomu zake.
“Kondo Mtokambali.”
“Kabila?”
“Mtanzania”
Karani huyo alimtazama kwa mshangao. “Mtanzania ni kabila mzee?”
“Si umeniuliza kabila? Mimi ni Mtanzania. Andika kama nilivyokuelekeza,” Joram alimwamrisha.
“Unakotoka?”
“Dar es Salaam.”
“Unakokwenda?”
“Dar es Salaam.”
Na kadhalika na kadhalika. Muda mfupi baadaye Joram akawa katika chumba kikubwa, chenye kila hitaji muhimu; bafu na vyoo vya ndani kwa ndani, televisheni kubwa, kitanda kipana na sofa pana za kukalia. Aliwasha mashine ya kurekebisha hewa, kabla ya kuvua nguo zake na kwenda bafuni ambako alioga vizuri, akapaka lotion na kuzichana nywele zake. Kisha aliingia katika jitihada za kuzisafisha nguo zake ambazo ndio kwanza aliona zilivyochakaa kutokana na purukushani za vichochoroni. Baada ya kulikamilisha jukumu hilo ndipo alipowasha tv na kukiendea kitanda ambako alikusudia kujilaza kwa nusu saa tu kabla ya kuamka na kuiacha hoteli hiyo.
Hakujua kama lepe la usingizi lilikuwa limempitia au la. Kilichomzindua ni mlio wa simu chumbani humo. Aliitazama kwa mshango. Kisha akaitazama saa yake, kumi na moja na robo alfajiri! Alikuwa amelala kwa takribani saa nzima bila kujua!
Simu iliendelea kulia. Joram aliitazama kwa mshangao. Watumishi wa hoteli hii wana kichaa? Alijiluliza. Alfajiri yote wanamtakia nini, wakati ndio kwanza tu ameingia. Akainua mkono wake na kukwanyua mkonga wa simu hiyo.
“Nani?” alikoroma.
“Samahani mzee,” ilikuwa sauti ya yule karani aliyempangisha. “Kuna mgeni wako hapa mapokezi. Amesema unamtarajia. Kwamba lazima akuone mara moja.”
“Mgeni wangu!” joram alihoji kwa mshangao.
“Amekwambia anamhitaji nani?”
“Ametaja jina lako mzee,” alijibu. “Amesema Kondo Mtokambali. Hata namba ya chumba chako alikuwa amekariri.”
Joram akazidi kushangaa.
“Ni mwanamke au mwanaume?”
“Msichana, mzee.”
“Amekwambia anaitwa nani?” Joram alihoji tena.
“Anaitwa Mona Lisa…”
Joram hakuyaamini masikio yake. “Mona Lisa, Tena! Marehemu! Ni kitu gani hichi kinachotokea? Alijiuliza. Ujio wa kwanza wa mtu aliyejiita Mona Lisa ulisababisha maafa makubwa muda mfupi tu uliopita pale Manzese. Ujio huu wa pili utazua lipi? Alijiuliza tena, hasira zikianza kumpanda, hasira za kuishi gizani, bila kujua kinachoendelea huku ukiwa umebebeshwa zigo zito ambalo hujui namna ya kulitua.
“Vipi mzee? Nimwambiaje?” sauti ya upande wa pili ilimzindua.
“Eh… ndiyo…. Hapana. Ngoja nizungumze naye,” joram alisema. Sauti iliyofuatia katika simu ilikuwa ya kike. Sauti nzuri, sauti nyepesi, sauti ambayo Joram aliifahamu sana na aliipenda sana. Ilikuwa sauti ya Mona Lisa!
“Joram, lazima nikuone mara moja, tafadhali. Nije au unakuja?”
“Mona! Mbona sikuelewi?”
“Utaelewa tu, nakuja,” ilijibu sauti hiyo, ikifuatiwa na kukatika kwa simu.
Joram alivaa harakaharaka. Akaichukua bastola yake na kuikagua. Risasi moja tu ilikuwa imetumika. Akaiweka katika mifuko yake ya siri. Baada ya hapo aliliendea dirisha na kuchungulia kwa makini huku masikio yake yakiwa kazini kunasa sauti yoyote isiyo ya kawaida.
Kama alivyotegemea joram aliliona gari moja, teksi ikisimama mbele ya hoteli hiyo. Ilikuwa na abiria wawili ambao walishuka na kufungua boneti ya gari hilo kwa namna ya watu walioharibikiwa. Kwa jinsi walivyopaki gari hilo bila tatizo lolote, na kwa jinsi walivyokuwa wakiutazama mlango wa hoteli kwa hila mara kwa mara, Joram alijua fika kuwa walikuwa na jukumu maalumu. Jukumu ambalo halikuwa jingine zaidi ya kuua. Gari la pili lilifika na kusimama mlangoni. Abiria watatu walishuka na kuingia hotelini. Gari likaondoka.
Joram alihitaji sana kukutana ana kwa ana na kiumbe huyu ambaye tayari amemtokea mara mbili akijiita Mona Lisa. Alihiaji kupata jibu la kitendawili hiki, cha mtu ambaye amekufa mbele ya macho yake kumtokea, tena akiwa mafichoni. Ndiyo, alihitaji kumwona ili kama ni aina fulani ya fumbo au aina mojawapo ya tamthiliya ifikie tamati. Lakini zaidi ya jibu la fumbo hilo Joram aliupenda uhai wake. Alikuwa na hakika kuwa watu walioingia hotelini humo, na wale waliobaki nje kwa kisingizio cha kutengeneza gari walikuwa wajumbe wa kifo. Ama walihitaji roho yake, ama ya huyo binti anayejiita Mona Lisa.
Akiwa tayari amechoka kuwa mkimbizi katika nchi yake mwenyewe, joram alifikia uamuzi wa kushambulia kabla hajashambuliwa. Mona Lisa au yeyote anayejiita Mona Lisa anaweza kusubiri. Alinyata na kuliendea dirisha ambalo alilifungua taratibu na kisha kuchupa nje. Kwa kutumia vidole vyake vya mikono na miguu. Aliambaa na ukuta hadi chini ambako alitua katika kichaka cha maua, huko alitumia lango la uani ambalo alilifungua na kutokea barabarani.
“Risasi ya kwanza ilisikika wakati akivuka barabara. Ilifuatiwa na mlipuko wa bomu ndani ya hoteli hiyo iliyofanya vioo vivunjike hovyo. Joram hakurudi nyuma. Alilifuata gari lile kwa kasi.

 
Aisee!?? Hakika Ben Ntobwa alikuwa ni Hazina Ya Utunzi katika Nchi Hii... Pumzikeni kwa Amani wewe na mzee mwenzio Elvis Musiba
 
Dah sasa huyu Monalisa ni jini au??? anajuaje hadi majina bandia wakati hakuwepo?? au aliweka kinasa sauti kwa siri kwenye mwili wa Joram??? Nitafanya kila njia nikipate na hiki kitabu this weekend!!! Thanks Nameless girl.
 
Dah sasa huyu Monalisa ni jini au??? anajuaje hadi majina bandia wakati hakuwepo?? au aliweka kinasa sauti kwa siri kwenye mwili wa Joram??? Nitafanya kila njia nikipate na hiki kitabu this weekend!!! Thanks Nameless girl.
mi mwenyewe hata sijui. Pengine mzimu ;)
 
Back
Top Bottom