Hadithi Jinsi Ilivyo Ndefu

Mi nikupongeze kwanza kwa ujumbe mzito pili kwa uwasilishaji wako wa kifasihi, nadhani kama wamekupa shahada hawajakupendelea! Big Up!
 
Paukwaaaa....! Pakawaaaa...!

Alitokeani... Naaam Twahib!

Alitokea chanjagaa... kajenga nyumba kakaaa... Na kilango cha kupita... Mwanangu mwana wa Siti Vijino kama Chikichi!

Mtambaji huanza hadithi yake na huendelea kwa mbwembwe na manjonjo mengi. Katika hadithi hizi wahusika hupatwa na janga, tatizo na misukosuko mingi, mmoja wao hulazimika kutafuta njia ya kuisaidia jamii yake ili iondokane na janga husika. Baada ya ujasiri mwingi, hekima, uvumilivu na mara nyingine mmoja mhusika hufanikiwa na kuibuka shujaa na hatimaye jamii ile huishi raha mustarehe!

Hizi ni hadithi za zamani za kale na mtambaji huyu mwenye mbwembwe pia ni wa zamani ingawa si kale. Kwani watambaji wa siku hizi hawajui hizo mbwembwe, na wasikilizaji wake husinzia na yeye mwenyewe kuishia katika kuonekana kituko maana hadithi inatambwa kina tirivyogo haswa!

Hata hivyo kuna hadithi hii ndefu inatuhusu sote mimi na nyinyi. Ila sina hakika kama wenzangu bado mnasikiliza maana mimi imenichosha. Hadithi yenyewe inahusu umaskini na ujinga wa jamii yetu. Tatizo lililopo hivi leo, hatuna tena mtambaji mahili ila tuna watambaji wengi, kiasi sisi adhira tunachanganyikiwa tumsikilize yupi.

Yule mtambaji tuliye mzoea na kumuona ni bingwa leo amepwaya na sauti yake inaanza kukauka. Mtambaji huyu hata akisimulia mambo ambayo ni 'nyeti kabisa'. Simulizi zake hazina radha tena... zimekuwa ni za kulazimisha.

Mtambaji huyu alisababisha vijana wengi wa enzi zile, kuamua kudandia nyumba zinazoelea baharini wakatokomea ughaibuni... Wakati mtambaji anaendelea na hadithi zake nami niliamua kumwacha kidogo kimawazo kwa vile nilitaka amalize hadithi na mimi ni hadhira nitazua matata. Niliamua kujisogeza mbali kidogo kimawazo.

Nikakumbuka kuwa walala hoi wengi kima cha chini enzi hizo mia sita. Walikuwa wanajitahidi kukabiliana na kile wakivunacho kwa kila hali. Ikapelekea nchi tukufu ya Tanzania kujibatiza jina jipya, jina ambalo ndio limekuwa maalufu miongoni mwa walalahoi wengi wa nchi hii tukufu. Hapo ndipo jina la nchi ya BONGO Likazaliwa rasmi.

Ajabu hali hii aikumstua mtambaji huyu mahili asiye choka na hadithi zake za paukwa pakawa. Wasikilizaji wamesinzia mpaka wameamka hadithi ni ile ile siasa za ujamaa na kujitegemea. Japokuwa sasa mtambaji kabadirisha kidogo uchezaji... Lakini bado anaimba kijamaa, ila uchezaji ni wa kibepari zaidi...!

Hali ikaanza kubadilika taratibu... Walalahoi wachache wakaamua kuvuna wasicho kipanda... Tatizo wengi wao wanaishi kutolewa muhanga na wengine wa upande wa pili kuchomwa moto. Yote hii ni kuonyesha kuwa adhira imechoka na ipo dhorfi hali. Walala hoi wengi hivi sasa wanajitahidi kusomesha watoto wao kadri ya uwezo wao kwa kujua kuwa wakisoma watapata ajira na watapunguza umaskini. Lakini mbona hao wanao wategemea kuwafundisha watoto wao nasikia ni vilaza...!? Na wengine wana majina na sifa mpya...! Eti wakina cha pombe. Ah! Wakati mwingine huwa nasikia kichefu chefu nisikiapo Ngano na Hadithi kama hizi.

Sasa kumekuja watambaji wapya na hadithi zao za Ali Nacha... Ahadi kem kem, kila mtambaji anavutia kwake, majasho yanawatoka kwa kuzunguka huku na kule, na simulizi zao zisizo na mwisho...! Najua kuwa wako watambaji mahili... Lakini Je utambaji wao unamsaidia vipi yule Mzee wangu kule kijijini... karne hii ya ishirini na moja bado anatumia kilimo cha jembe la mkono? Hivi hawa watambaji wanaijua hii hadithi vizuri au nao wamesimuliwa na mtambaji asiyefuzu?

Haya! sasa kumekuja kisa kipyaaa cha mafisi mafisadi... sic. Nafikiri hawa watambaji hawaijui hii hadithi vizuri, labda waliisikia huku wakipita nyuma ya nyumba ya watu hivyo hawajui ilianzia wapi na ilianzaje.

Kazi ya utambaji mimi sina ujuzi nayo. Lakini kisa cha wananchi hawa na kijua. Sitaki simulia hapa leo kwa vile yule mtambaji pale bado anaendelea na hadithi yake. Labda nigusie kidogo tu kuwa kama hakuna tofuati kati ya fisadi papa wala nyangumi. Hivi hadithi hii ya mafisadi inawasaidia vipi Wananchi hawa walala hoi? Je wakishajuwa kuwa fulani ni fisadi zaidi ya fisadi mwingine kutawapunguzia matatizo yao ya kukosa elimu, matibabu na mambo mengine ya msingi? Je kutawafanya waishi kwa raha mstarehe? Je kutawapatia matibu na elimu bora? Je kutasaidia kupambana na umaskini uliokithiri.

Elimu hii inawasaidia kiasi gani kuupunguza au japo kuutia ganzi umaskini walio nao? Nashangaa jana eh! Na zaidi namshangaa leo hawa watambaji kama wana macho na masikio na iwapo yanafanya kazi sawasawa.

Ninataka kuwaambia watambaji waache hadithi za Ali Nacha... Kwani walikuwa wapi miaka yote kuyajuwa haya? Mbona ni kesho tu walala hoi wataanza kupewa vitenge na kupikiwa wali ulio changanywa na nyama, ili wale wali waliwe...! Je watambaji wako wapi kuwazinduwa walala hoi hawa waliokata tamaa ya maisha?

Basi watie japo wimbo kidogo, wasikilizaji waamke ili wapate wa kuwasikiliza... Hivi watambaji hawa wanafika kule Lindi vijijini? Mahenge, Sikonge, Isongole, Kisegese, Chemba, Dalai, Farkwa, Mchesi, Mchoteka, Maweni, Mgandu, Sangabuye, Chakwa, Wete nk, nk, nk...!? Au watambaji wamepata wimbo mpya wanasahu hatari iliyoko mbele yao?

Nataka kuwaamba watambaji wapya waache kuwaadaa walalahoi na nyimbo zao, sisizo na msisimko. Waamke sasa ili adhira nayo ihamke. Hizi safari zao za miji mikubwa kama Dar, Arusha na Mwanza hazina msisimko tena, waende kule kwenye shina la Mtanzania halafu watambaji waendelee na hadithi zao, tena wahakikishe hadithi zenye kuleta tija na faraja ili kumkomboa mlalahoi, hapo labda hadithi zinaweza kunoga.

Lakini Je hawa watambaji sijui kama watanisikiliza... na mimi ni mfupi na
niko huku nyuma, sijui kama wataniona. Maanake maandishi tu pekee kwenye hii kompyuta hayatoshi.

Je JF inasomeka kule kunakolimwa mahindi, viazi, ufuta, kule kunako vuliwa samaki wa aina mbali mbali... Hivi babu yangu kule kijijini anakusoma au kukusikia vile unavyo hadithia simulizi zako? Au mbele ya kipasa sauti chako kumeshindiliwa matambara...?

Nyinyi mlio jisogeza ughaibuni mnamsoma...Je yule mlalahoi anayehadithiwa habari za mafisadi papa na nyangumi anawakusoma? Au mpo hapa kujisoma wenyewe kwa wenyewe?

Nina mengi ya kuhadhiri lakini nachelewa kusema kuwa hii si fani yangu... Naogopa naweza kupata hasira nikapiga teke kama si ngumi hiki kisekandi hendi cha mkono wa pili kama si watatu... eti wanakiita tarakilishi, Mi nachoka kabisa....!

Basi na tusubiri watambaji waliovuka umri wa kustahafu hata ule alioondokea madarakani hayati Mwalimu Nyerere. Waendelee kutamba... Mwalimu Nyerere alig'atuka akiwa na umri wa miaka 63" Je mtambaji yupi yupo tayari kufuata nyayo zake?

Jamani nyie warefu nisaidieni, kama hamuwezi kuniinua basi waambieni watambaji, tunataka hadithi hii iishe kama zile za babu na bibi zetu.

"Yaani wakaishi raha mustarehe".

Wakatabau ndimi, niliyenyuma ya tarakilishi, ninayetaka uwakilishi.

X-Paster
 
Back
Top Bottom