Habari Leo laasa kuhusu Takukuru.........utanashati wa majengo...........

Rutashubanyuma

JF-Expert Member
Sep 24, 2010
219,470
911,172
Uzuri wa Takukuru usiishie kwenye majengo ya kisasa

Imeandikwa na Mhariri; Tarehe: 15th December 2010 @ 23:59

KASI ya ujenzi wa ofisi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) imekuwa kubwa, kiasi cha kila baada ya kipindi kushuhudia ufunguzi wa ofisi za makao makuu ya mkoa au wilaya.

Baada ya kushuhudia jengo la kisasa la makao makuu la taasisi hiyo lenye thamani ya Sh bilioni 4, wananchi waliendelea kuona majengo bora katika mikoa na wilaya.

Na haikushangaza juzi kuona Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo, Dk. Edward Hosea akifungua jengo la kisasa la ghorofa kwa matumizi ya idara hiyo, katika wilaya ya Iramba lililogharimu Sh milioni 726.8.

Hakuna shaka kwamba, ubora wa jengo hilo ni kielelezo tosha kwamba, Takukuru ni moja ya taasisi zenye majengo ya kisasa zaidi nchini.

Si majengo tu, bali pia taasisi hiyo imewezeshwa kwa mambo mengi, ikiwa ni pamoja na vitendea kazi vya uhakika na hata kupewa sheria inayowapa meno zaidi katika utekelezaji wa majukumu yao.

Ni dhahiri kwamba, kama ilivyo imani ya serikali, wananchi nao sasa wanatarajia mengi mazuri kutoka kwa taasisi hii nyeti inayopaswa kudhibiti vitendo na mianya ya rushwa, hali ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa kudumaza miradi mingi ya maendeleo iliyotengwa kwa ajili ya ustawi wa nchi.

Katika majengo haya yanayogharimu fedha nyingi za walipa kodi, hatutegemei kusikia mikanganyiko isiyo ya lazima kuhusu kukwama kwa mafaili ya kesi kati ya ofisi za Takukuru na zile za mamlaka nyingine za sheria nchini, mikanganyiko ambayo wakati mwingine haileti taswira nzuri mbele ya jamii.

Kutoka katika majengo mapya ya Takukuru, sasa tunategemea kuona kasi kubwa ya kushughulikia kero zinazopigiwa kelele kila kukicha na hatimaye, bila kuwafumbia macho, wahusika wafikishwe katika mikono ya sheria kukabiliana na maovu yao.

Ni kwa mtaji huu, wananchi hawatayajutia mabilioni ya fedha zao zinazotumika katika kuisuka taasisi hii, kwani watakuwa wamepata majibu ya kweli ya madudu, hasa ya ulaji wa fedha za umma kama ambavyo Rais Jakaya Kikwete aliwahi kusema siku za nyuma kuwa, kuna wakati karibu asilimia 30 ya fedha za maendeleo zilikuwa zinapotea kimiujiza.

Ndani ya majengo haya mapya, wafanyakazi wa Takukuru wawe na ujasiri na uthubutu wa kuchimbua na kutaja majina ya watu wanaoiingiza nchi kwenye mikataba ya hovyo, iliyojaa kamisheni za asilimia kumi na yenye kuibakiza nchi pale pale ilipo, miaka nenda miaka rudi.

Tungependa kuamini kuwa makazi mapya ya TAKUKURU sasa yatamfanya mkuu wake, Dk. Hosea asiishie tu, kila baada ya muda, kuwataka wananchi wakae mkao wa kusikiliza kesi kubwa za rushwa, bali wasikie na kuona kweli mambo yakitendeka.

Watakapofanya yote haya na mengine yanayohusiana nayo, Takukuru itakuwa imestahili majengo mapya na hata kodi ya wananchi iliyotumika na inayoendelea kutumika kuyajenga itakuwa imetumika kihalali, kinyume cha hapo, ni dhahiri serikali itaonekana inafanya matumizi yasiyo ya lazima.

Wasifikishwe mahali pa kuona ni afadhali fedha hizo zingetumika kuongeza idadi ya madarasa, madawati na madawa, bali wafanyakazi waendane na majukumu yanayostahili majengo mapya, tena ya kisasa.
 
Back
Top Bottom