H. MDEE apasua; Migogoro ya ardhi tishio la amani, wawekezaji sawa na majambazi wanaopora benki

Tumaini Makene

JF-Expert Member
Jan 6, 2012
2,642
6,070

HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI BUNGENI, WIZARA YA ARDHI NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI MHE. HALIMA JAMES MDEE (MB) KUHUSU MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2011/12 MA MAKADIRIO YA MATUMIZI YA WIZARA YA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI MWAKA WA FEDHA 2012/13.



UTANGULIZI Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwepo hapa leo kuwasilisha maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusu Wizara ya Ardhi, Nyumba Na Maendeleo ya Makazi .

Mheshimiwa Spika
, pia nikushukuru wewe kwa kuniruhusu kutoa maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusu Wizara hii kwa mujibu wa Kanuni ya 99 kanuni ndogo ya (7) , ya Kanuni za Bunge Toleo la Mwaka 2007.

Mheshimiwa Spika, pili ningependa kutoa shukrani zangu za dhati kwa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na wananchi wa Jimbo la Kawe ( wapiga kura wangu) kwa imani yao kwangu, makamanda wote (vijana, wazee na akina mama wa vyama vyote) kwa kuendelea kuniunga mkono katika kuhakikisha Jimbo letu linapata huduma zote za msingi zinapatikana katika viwango stahili. Ahadi yangu kwenu ni kuwatumikia kwa uwezo wangu wote kwa kadiri Mwenyezi Mungu atakavyoniwezesha!

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutoa shukrani za dhati kwa CHADEMA kikiwa chini ya Mtendaji wake mkuu (KATIBU MKUU-TAIFA), Mhe. Wilbroad Peter Slaa. Hakika kila Mtanzania anaona kazi unayoifanya ya kuhakikisha chama chetu kina kuwa juu na Watanzania wote wanatuunga mkono. Mungu akupe uhai, naamini ipo siku tutaifikia Nchi ya Ahadi!

Mheshimiwa Spika,
sina budi kumshukuru Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Mhe. Freeman Aikaeli Mbowe, kwa kuniamini na kuniteua tena kuwa Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani katika Wizara hii. Shukrani pia ziende kwa wasaidizi wa Kiongozi wa Kambi, Kabwe Zitto (Naibu Kiongozi wa Kambi) na Tundu Lissu (Mnadhimu wa Kambi) kwa kutuongoza vyema katika shughuli hii ngumu ya kuwatetea wanyonge. Shukrani pia ziwafikie wabunge wenzangu wote wa Kambi kwa ushirikiano wao kwangu.

Mheshimiwa Spika, kipekee niishukuru sana familia yangu yote, wazazi wangu Prof. James Salehe Mdee na Theresia Kisenga Ngowi kwa upendo wao na kwa upekee nimshukuru kaka yangu Joseph James Mdee,kwa msaada na ushauri mkubwa katika kuhakikisha natimiza majukumu yangu ya kibunge ndani na nje ya Bunge. Asanteni sana!!!

HOJA ZA KAMBI YA UPINZANI 2011/12

Mheshimiwa Spika,
kufuatia hotuba ya Kambi ya Upinzani Bungeni ya mwaka 2011/12 Kambi ya upinzani inatambua hatua zilizochukuliwa na serikali katika hoja kadhaa ambazo ziliwasilishwa kwake hususan suala la ada ya ukodishwaji wa mashamba na vitalu ambapo serikali ilikuwa inatoza shilingi 220 tu kwa eka. Kauli ya serikali kupitia Naibu Waziri wa ardhi wakati akichangia hotuba ya mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya matumizi ya fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu 2012/2013 imeonyesha nia ya serikali kuongeza ada husika ili kuiongezea serikali mapato.

Kambi ya Upinzani
inatambua pia hatua ambazo serikali imeahidi kuzichukua katika mwaka huu wa fedha 2012/13 kwa kutenga fedha za fidia kwa wananchi wa Kurasini Mabwawani. Serikali imeeleza kwamba fidia zitalipwa kwa viwango vipya kuendana na thamani ya soko! Halikadhalika, Kambi ya Upinzani inatambua hatua zitakazochukuliwa na serikali kuhusiana na mwekezaji Agrisol , ili kuiepusha nchi kuingia kwenye mkataba mbovu usiozingatia maslahi na sheria za nchi.

Kambi ya upinzani imefarijika na Kauli ya Waziri Mkuu wakati akihitimisha hotuba yake ya bajeti ambapo, pamoja na mambo mengine alitamka kwamba mchakato wa Agrisol haujaanza, hawajaingia makubaliano/mkataba "wowote" na kwamba mchakato ukianza ndipo wataingia kwenye mambo ya msingi waone wanapangiana vipi, uwiano utakuwaje na kwamba halmashauri imiliki kiasi gani cha hisa!


Mheshimiwa Spika,
rai ya Kambi ya Upinzani ni kwa serikali kusitisha mpango wake wa kuligawa eneo la Mishamo na Katumba lenye ukubwa wa zaidi ya hekta 325,000 au ekari 760,728 kwa AGRISOL. Kuna taarifa kwamba tayari serikali ilishaligawa eneo la Lugufu lenye ukubwa wa hekta 10,000 kwa AGRISOL (kwa kuwa mikataba inaendeshwa kwa usiri mkubwa.) Ni imani yangu Serikali itatupa jibu juu ya mustakabali wa Lugufu.

Mheshimiwa Spika
, wakati serikali ikitafakari, ni muhimu Bunge hili tukufu likaelewa kwamba aliyekuwa mshirika muhimu wa Agrisol IOWA State University College of Agriculture aliyekuwa mhimili muhimu wa mwekezaji huyu hasa katika kuwasaidia wakulima wadogo wadogo kama ilivyoainishwa katika kipengele cha 4.7 cha MoU baina Halmashauri ya wilaya ya Mpanda na AGRISOL ENERGY TANZANIA LIMITED alijitoa baada ya kugundua kwamba mwekezaji huyu hana dhamira ya kuisaidia nchi na wakulima wadogo zaidi ya kujinufaisha kibiashara.

Mheshimiwa Spika,
kwa maelezo ya IOWA State University College of Agriculture, ilijitoa baada ya kugundua ilitumiwa na mmiliki wa AGRISOL bwana Bruce Rastetter ili aweze kupata uhalali wa kukubalika kirahisi kama mwekezaji mahiri! Ukweli ni kwamba nia ya mwekezaji huyu haikuwa kuisaidia nchi balikuendeleza mashamba makubwa ya zao mojamoja,.. matumizi ya viwango vikubwa vya kemikali na pia kuomba mabadiliko katika kanuni za kitaifa za usalama wa kibiolojia ili mazao yenye viinitete yaweze kupandwa.

Mheshimiwa Spika,
madhara ya GMO ni makubwa sana, moja kubwa ni kufifisha kabisa matumizi ya mbegu za asili. Mwekezaji akizitumia kwenye eneo lake, madhara yanasambaa pia kwa mashamba ya jirani, inajenga utegemezi wa wakulima kununua mbegu kutoka kwa wakulima wakubwa.

Mbali na utegemezi wa mbegu, GMO zina madhara makubwa sana kiafya. Tafiti zimeonyesha kwamba nchi zilizoendelea ziko katika vita kali sana za kuzuia matumizi ya GMO lakini sisi tunayapokea makampuni makubwa kwa misamaha lukuki ya kodi, tukiamini tunaalika wawekezaji waje kuijenga nchi, kumbe wanakuja kutengeneza taifa la utegemezi na lenye maradhi lukuki.


Mheshimiwa Spika,
ni muhimu ikaeleweka kwamba katika wilaya ya Mpanda ardhi ambayo iko wazi kwa matumizi ya binadamu (arable land) ni 19% tu ya eneo lote! Nyingine iliyobaki ni hifadhi za taifa: i) 18% hifadhi ya wanyama, ii) 59% hifadhi ya misitu iii) 4% hifadhi ya maji.

Mheshimiwa Spika,
badala ya kila kitu kuwategemea mabeberu, inawezekana kabisa serikali ikawekeza katika eneo husika. Taarifa zinaonyesha kwamba AGRISOL walitarajia kuwekeza $100 milioni (shilingi bilioni 150) katika kipindi cha miaka 10, kwa matarajio ya kupata faida ya $272 milioni (shilingi bilioni 408) ndani ya mwaka mmoja baada ya uwekezaji huo kwa kulima hekta 200,000 tu za mahindi, kiasi ambacho kinalingana kama sio kuzidi bajeti ya Wizara ya Kilimo!

Mheshimiwa Spika, kama Agrisol wangepata/watapata hadhi ya mwekezaji wa kimkakati,(stratergic investor). Wangepata/watapata pia msamaha wa kodi ya shirika (corporate tax) ambayo ni 30% ya shilingi bilioni 408 (ambayo ni bilioni 122)!

Hivi kweli serikali makini, mbali ya kuwa na vivutio vya utalii vilivyosheheni, na hivyo kuwa nchi ya nne ya uzalishaji wa dhahabu Afrika, nchi pekee yenye madini tofauti tofauti zaidi ya 15 na kwa upekee ni madini ya Tanzanite, tuna urani ya kutosha, hivi karibuni tumegundua gesi yenye thamani ya tsh trilioni 626.7, tuna tani milioni 86 za makaa ya mawe, tuna kila dalili ya kupata mafuta n.k inashindwa kuwekeza kwa faida ya nchi na wananchi wake? Tunawezaje kuokoa kizazi cha vijana waliogeuka wazururaji kwa sababu serikali yao haijawapa fursa?


Mheshimiwa Spika,
katika bajeti ya mwaka 2011/2012, Kambi ya Upinzani ilielezea kwa kina matatizo sugu ya migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini ambayo imekithiri kufikia hatua ya uvunjifu wa amani kunakopelekea umwagaji damu na wakati mwingine vifo kutokea. Mwaka mmoja umepita bado hakuna hatua dhahiri zilizochukuliwa na serikali hususan kuhusu:-

i) Mgogoro wa ardhi unaowahusisha wakulima wa kijiji cha Nzasa, ambapo Wizara ya Maliasili na Utalii wanataka kuwaondoa wananchi katika ardhi yao halali kwa madai kwamba wanaishi ndani ya hifadhi ya Msitu wa Kazimzumbwi.

ii) Mustakabali wa maeneo ya yaliyokuwa mashamba ya Ngano, Hanang (Hanang Wheat Complex (HWC) na Dakawa Ranch. iii) Tatizo la ukodishwaji wa mashamba unaofanywa na wawekezaji dhidi ya wananchi wenyeji. Hususan shamba la mpunga la Mbarali na Kapunga, yote yakiwa wilaya ya Mbarali na mwekezaji RAI group anayemiliki mashamba ya Setchet, Murjala na Gidagamowd ambaye alikuwa anawakodisha wananchi $10 kwa ekari.

Kambi ya Upinzani ina taarifa za kuendelea kwa ukodishaji wa mashamba unaofanywa na wawekezaji. Shamba la hekta 1 hukodishwa kwa shilingi laki moja mpaka laki moja na nusu katika mashamba ya Kapunga na Mbarali. Hoja ya Kambi ya Upinzani imethibitishwa pia na timu ya wataalam wa Consolidated Holding Corporation (CHC) katika taarifa yao ya ufuatiliaji wa mashamba na viwanda vilivyobinafsishwa[1] ambayo inabainisha kwamba katika shamba la Mbarali Rice Farm mwekezaji analima sehemu ya shamba na sehemu nyingine ya shamba anakodisha kwa wananchi kwa utaratibu maalum.

iv) Kambi ya Upinzani inataka kujua mustakabali wa kijiji cha Kapunga, kilichopo wilaya ya Mbarali ambacho kiliuzwa kwa mwekezaji! Mkataba wa mauzo na Hati miliki ya shamba (certificate of title) zinaonyesha kuwa shamba lina ukubwa wa hekta 7,370. Wanakijiji wanadai kuwa shamba linatakiwa kuwa na ukubwa wa hekta 5,500 kulingana na barua ya maombi ya ardhi kutoka kwa NAFCO na muhtasari wa mkutano wa kijiji ulioidhinisha utoaji wa eneo husika.

v) Mashamba ya Gawal na Warret yaliyopo Hanang yalitakiwa kurejeshwa kwa wananchi lakini hayajarejeshwa.

vi) Mgogoro wa ardhi baina ya Jeshi la Wananchi (JWTZ) na wananchi wa Bukanga na Buhare (Mgaranjab) Musoma Mjini.

vii) Mgogoro unaohusu shamba namba 299 (iliyokuwa NARCO Ranches) lenye ukubwa wa hekta 49,981. Halmashauri ya wilaya ya Mvomero. Mgogoro huu uliwahusisha vigogo wakubwa wastaafu wa Chama cha siasa na serikali.

viii) Mgogoro baina ya Simba Motors na wanakijiji wa Mapinga, kitongoji cha Undindivu, wilaya ya Bagamoyo.

ix) Mgogoro baina ya wakulima na wafugaji wa jamii ya Wamasai katika eneo la vijiji vya Izava (Chamwino) na Chitengo (Kongwa).

x) Uvamizi wa maeneo ya wazi Mkoa wa Dar es salaam; viwanja vingapi vimerejeshwa kwa matumizi ya umma? Na viwanja vingapi bado vipo mikononi mwa wavamizi?

MATATIZO YA TATHMINI NA MALIPO YA FIDIA


Mheshimiwa Spika, imekuwa ni jambo la kawaida sana kwa zoezi la fidia kuendeshwa kihenyeji na pasipo kuzingatia sheria na taratibu tulizojiwekea! Na hata wananchi wakilalamika serikali inaendelea na miradi! Kambi ya Upinzani inataka majibu ya hoja zifuatazo ambazo licha ya kuzungumzwa katika bajeti ya 2011/12 bado serikali haijazipatia majibu:

a) Hatma ya wanakijiji wa kijiji cha Mabwepande ambao miaka mitano iliyopita serikali ilifanya tathmini na kuwaagiza wasifanye maendeleo yoyote ili kupisha ujenzi wa chuo cha IFM. Pia baada ya mafuriko makubwa yaliyolikumbwa jiji la Dar es salaam maeneo yao yalichukuliwa na serikali kwa ajili ya kugawa viwanja kwa waathirika! Mpaka sasa hakuna fidia yoyote iliyolipwa!

b)
Hatma ya Wananchi wa Kigamboni.

c)
Hatma ya wananchi 1600 wa wilaya ya Mbarali waliotakiwa kuondoka kupisha upanuzi wa mbuga ya Taifa ya Ruaha.

UTEKELEZAJI WA BAJETI 2011/12

Mheshimiwa Spika, mpango wa Taifa[2] umeainisha wazi kwamba, pamoja na mambo mengine kufanikiwa kwake kunategemeana sana na mipango bora ya matumizi ya ardhi. Na chombo pekee cha kuweza kufanikisha hili ni Wizara ya Ardhi kupitia taasisi yake ya Tume ya Taifa ya Mipango. Kati ya majukumu ya Tume ni:-

i)
Kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi ya vijiji.

ii) Utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Matumizi ya Ardhi kwa kutekeleza programu za kilimo, mifugo na maji kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo, Maji na Kilimo.

iii) Kusaidia kupatikana kwa ardhi kwa ajili ya utekelezaji wa KILIMO KWANZA.

iv) Kufanya utafiti katika masuala yanayohusiana na ardhi hasa katika maeneo yenye migogoro, uhamiaji mijini kutoka vijijini, ushirikishwaji wananchi katika kuendeleza ardhi mijini, viwango vya matumizi ardhi mijini na vijijini.

v) Kufuatilia na kutathmini mipango ya matumizi ya ardhi iliyokwisha andaliwa na katika maeneo yenye migogoro sugu. Mheshimiwa Spika, ni wazi kwamba majukumu yao yangekuwa yanachukuliwa kwa uzito unaostahili, leo tungekuwa hatuzungumzii hoja za migogoro ya ardhi ambayo kwa sasa ni tishio la amani ya nchi, bali mafanikio ya matumizi endelevu ya rasilimali kubwa ya ardhi tuliyobarikiwa na mwenyezi Mungu!

KUPUUZWA KWA MIRADI YA MAENDELEO

Mheshimiwa Spika, licha ya umuhimu na ukubwa wa majukumu yake, Wizara ya Ardhi ni kati ya wizara ambazo zinapewa fedha ndogo sana za kutekeleza miradi ya maendeleo! Na mbaya zaidi, licha ya ufinyu wa fedha, fedha zimekuwa hazipelekwi zote! Mwaka wa fedha 2010/11 Wizara iliidhinishiwa jumla ya shilingi 22,265,078,000/- kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Hadi mwaka unaisha, wizara ilipokea jumla ya shilingi 4,673,383,000/- tu! Ambapo fedha zilizotumika kutekeleza miradi ya maendeleo ni shilingi 3,931,581,086/- zilitumika kutekeleza miradi ya maendeleo! [3]

Hali kadhalika, katika mwaka wa fedha 2011/12, wizara iliidhinishiwa jumla ya shilingi 22,010,437,000/ kwa ajili ya miradi ya maendeleo . Hadi Mei 2012, Wizara ilipokea shilingi 3,663,685,463.96/- tu kwa jili ya miradi ya maendeleo!

Mheshimiwa spika,
uzembe wa aina hii hauwezi kuvumilika! Kambi ya Upinzani inaitaka serikali ilieleze Bunge lako tukufu, ni kwa nini kwa miaka miwili mfululizo fedha za maendeleo zimekuwa hazitolewi kama zilivyopangwa! Sambamba na hilo, ni miradi mingapi imekwama kutokana na upungufu huo?

KUPUUZWA KWA MAELEKEZO YA WAZIRI MKUU


Mheshimiwa Spika,
kwa kuzingatia changamoto za kimapato zinazoikabili Wizara ya Ardhi, serikali kupitia kauli ya Waziri Mkuu iliridhia kuipatia wizara kibali cha kubakia na makusanyo yao asilimia 100. Naomba kumnukuu:

'Mheshimiwa Naibu Spika,lakini nasema hivi, jana tukiwa kwenye Cabinet tumemuidhinishia huyu mama kwamba wewe mama ile fedha yote ambayo utakuwa unakusanya kutokana na shughuli zako za ardhi baki nayo yote, chukua yote ili ikusaidie wewe katika uendeshaji wa wizara hiyo.Kwa hiyo tunatambua changamoto alizonazo na naamini tutamsaidia vizuri sana na najua ataweza' Mwisho wa kunukuu.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, hadi Mei 2012 , Wizara ilikusanya jumla ya shilingi bilioni 16. Kinyume na maelekezo ya Waziri Mkuu, wizara ilipokea kiasi cha bilioni 9.4 tu, sawa na asilimia 59 ya kilichokusanywa! Kutokana na upungufu huo wizara ilishindwa kuongeza gawio la fedha za retention kwa Halmashauri mpaka kufikia 30% badala ya gawio la sasa la 20%! Kambi ya Upinzani inaitaka serikali itoe maelezo juu ya mustakabali wa kiasi cha retention ambacho bado hakijapelekwa Wizarani!

MATUMIZI YANAYOHITAJI MAELEZO MISHAHARA

Mheshimiwa Spika, imekuwa ni utaratibu wa Bunge lako tukufu kupitisha mafungu mbali mbali kama yalivyoombwa na wizara na idara mbalimbali za serikali. Tafsiri ikiwa kila wizara au idara ya serikali ina ufahamu wa makadirio ya fedha ambazo ina tarajia kutumia katika fungu husika. Kwa miaka miwili mfululizo wizara ya ardhi imekuwa ikitumia fungu la mshahara kuliko kiasi kilichoidhinishwa na Bunge.

Katika mwaka wa fedha 2010/11, wizara iliidhinishiwa jumla ya shilingi 6,423,295,000/- kwa ajili ya mishahara. Lakini katika kipindi cha Julai 2010 hadi Mei 2011 kiasi cha shilingi 8,499,539,334/- zilitumika kulipa mishahara.

Hali kadhalika katika mwaka wa fedha 2011/12 wizara iliidhinishiwa shilingi 7,531,409,000/- kwa ajili ya matumizi ya mishahara. Hadi Mei 2012 kiasi cha shilingi 9,765,774,300/- zilitumika kulipa mishahara! Kambi ya Upinzani inaitaka serikali itoe maelezo, hiyo tofauti (ya zaidi ya shilingi bilioni mbili) ya kiasi kilichoidhinishwa na Bunge na kiasi kilichotumiwa na wizara kwa miaka miwili mfululizo imetokana na nini!


MIPAKA YA KIMATAIFA

Mheshimiwa Spika,
Serikali ilikuwa katika mchakato wa kuandaa andiko la kuomba eneo la nyongeza nje ya ukanda wa kiuchumi baharini . Andiko hili liliwasilishwa Umoja wa Mataifa tarehe 18 Januari 2012. Kwa mwaka wa fedha 2010/11 na 2011/12 kiasi cha shilingi 431,572,872/- na 171,920,854.59/- zilitumika kuandaa andiko husika! Kambi ya Upinzani inaitaka serikali kutoa mchanganuo wa matumizi husika na kuainisha ni kwa namna gani ANDIKO limeweza kuigharimu serikali zaidi ya shilingi milioni mia sita!

MASHAMBA YALIYOBINAFSISHWA AMBAYO HAYAJAENDELEZWA


Mheshimiwa Spika, wakati akihitimisha bajeti ya ardhi mwaka jana, Waziri wa ardhi aliliahidi bunge lako tukufu kwamba baada ya bunge la bajeti wizara ingekwenda kufanya ukaguzi huru wa nani ametelekeza mashamba. Alisisitiza kwamba wawekezaji wote waliotelekeza mashamba the honeymoon is over.[4]

Mheshimiwa Spika
, Kambi ya Upinzani inaitaka kupata idadi ya mashamba yaliyokaguliwa na wizara na mahali yalipo toka ahadi husika ilipotolewa na ni hatua gani ambazo zimeshachukuliwa na serikali dhidi ya wawekezaji husika.

Mheshimiwa Spika, wakati Kambi ya Upinzani ikisubiri taarifa toka kwa waziri wa ardhi juu ya ukaguzi huru iliyofanywa na wizara kuweza kuwabaini waliotelekeza mashamba, kambi ya upinzani inataka serikali itoe msimamo juu ya taarifa ya ufuatiliaji wa mashamba na viwanda vya bidhaa na kilimo iliyofanyiwa kazi na CHC kufuatia maelekezo waliyopewa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC).

Taarifa husika imebainisha kwamba mashamba 13 yenye ukubwa wa hekta 71,184 yalikuwa yameendelezwa kwa kiasi, wakati mashamba 14 yenye ukubwa wa hekta 44,764 yalikuwa hayajaendeleza kabisa/yametelekezwa! Mengi ya mashamba yakiwa ni mashamba ya Mkonge! Mashamba hayo ni:-

1) Ndungu Sisal Estate, shamba hili lenye ukubwa wa hekta 1,230. 9 liliuzwa kwa L.M investiment ya Tanga mwaka 1997 kwa bei ya shilingi milioni 278 . Mpaka sasa 2012, miaka 15 baada ya kukabidhiwa shamba, mwekezaji ameendeleza 52% tu ya shamba lote!

2) Mkumbara Sisal Estate , shamba hili lenye ukubwa wa hekta 1,734 liliuzwa mwaka 1997 kwa M/S D.D Ruhinda & Company LTD kwa bei ya shilingi 100 milioni. Mpaka sasa (miaka 15 baada ya kukabidhiwa shamba) mwekezaji ameendeleza 52% tu ya shamba lote. 3) Toronto Sisal Estate, shamba lenye ukubwa wa hekta 6,023 lililobinafsishwa kwa Highland Estate Limited kwa bei ya shilingi milioni 265.4 mwaka 1998.

Mpaka Septemba 2011, ni 50% tu ya shamba lilikuwa limeendelezwa! Taarifa zilizopo ni kwamba mwekezaji husika hana hati miliki ya shamba kutokana na kudaiwa riba hivyo kushindwa kupata mkopo wa kuliendeleza shamba.


4)
Magunga Sisal Estate, shamba lipo wilaya ya Korogwe, lina ukubwa wa hekta 6,520. Katika shamba hili ambalo linamilikiwa kwa ubia na kuendeshwa kwa kilimo cha mkataba kati ya wakulima wadogo wa mkonge na Katani Limited limeendelezwa kwa 19% tu .

5)
Mgombezi Sisal Estate , shamba liko wilaya ya Korogwe na lina ukubwa wa hekta 6,480 ambapo hekta 3881 zimegawiwa kwa wakulima. Shamba linaendeshwa kwa kilimo cha mkataba kati ya wakulima wakubwa na wa kati. Eneo lililopandwa mkonge ni hekta 1301.6 tu!

6) Hale Mruazi Sisal Estate, shamba lina ukubwa wa hekta 4,180, ambapo hekta 1,136 tu ndizo zilizopandwa Mkonge.

7) Manzabay Sisal Estate, shamba liliuzwa kwa Chavda Group mwaka 1998. Mwekezaji alitumia hati miliki kupata mkopo ambapo hakutumia mkopo husika kuendeleza shamba, shamba husika lilishikiliwa na CRDB mpaka mwaka 2001 alipoiuzia Mbegu Technologies ambaye naye amelikodisha kwa Omari Mduduma. Shamba halijaendelezwa!

8) Kwashemshi Sisal Estate, shamba lina ukubwa wa hetka 1498.5,shamba liliuzwa kwa Chavda Group mwaka 1998, mwekezaji alitumia hati miliki ya shamba kupata mkopo, ambao hakuutumia kuendeleza shamba. Shamba hilo lilishikiliwa na NBC mpaka 2003 lilipouzwa kwa Mathew Upanga Mnkande. Shamba limeendelezwa kwa 35% tu!

9) Ubena Sisal Estate, shamba lenye ukubwa wa hekta 4,227 ambalo lipo wilaya ya Bagamoyo, mkoa wa Pwani liliuzwa kwa Highlands Estates Ltd mwaka 2007 kwa kiasi cha shilingi 278 milioni. Jumla ya hekta 499 ambayo ni sawa na 12% tu imepandwa mkonge.

10) Kingolwila /Pangawe Sisal estate, shamba lenye ukubwa wa hekta 3703 liko wilaya ya Morogoro, mkoani morogoro, liliuzwa kwa Highland Estates limited kwa bei ya shilingi milioni 210.2 kupitia PSRC mwaka 2007. Jumla ya hekta 800 kati ya hekta 3703 ambazo ni sawa na 22% ya eneo lote ndio limepandwa mkonge!

11) Msowero Sisal Estate, Shamba lenye ukubwa wa hekta 5200 lipo wilaya ya Kilosa Morogogo , shamba liliuzwa na mamlaka ya Mkonge Tanzania kwa kampuni ya Noble Azania Agricultural Enterprises mwaka 1993. Shamba limepandwa mkonge hekta 900 tu ambazo ni 17% ya shamba lote na alizeti na mtama zimepandwa hekta 200 tu. Hekta 4100 hazijaendelezwa toka mwaka 1993!

12) Rudewa Sisal estate, shamba lina ukubwa wa hekta 6351, liliuzwa kwa kampuni ya Farm land mwaka 1992. Kampuni husika iliuza shamba kwa kampuni ya China State Farms Agribusiness (Group) corporation Tanzania Limited (CSFACOT) kwa kiasi cha dola za kimarekani milioni 1.2 mwaka 2000. Mwekezaji ameweza kuendeleza 32% tu kwa kupanda mkonge hekta 2018 !

13) Kimamba Fibre Estate, shamba lenye ukubwa wa hekta 5743 liliuzwa kwa kampuni ya ANCO ltd mwaka 1998. Mwaka 2009 Kampuni ya ANCO ltd iliuza hekta 3,043 kwa kampuni ya Sino na kubakiwa na hekta 2700. Mustakabali wa shamba walilouziwa Sino haujulikani, ila shamba lililobaki ANCO ltd limeendelezwa kwa 46.3% tu!

Mheshimiwa Spika, mashamba ambayo hayajaendelezwa kabisa ni:

1) Kikulu Sisal estate ,lenye ukubwa wa hekta 5900 lililouzwa kwa Chavda Group, mwekezaji alieka dhamana shamba,kama kawaida yake akachukua , mkopo hakuendeleza shamba.

2) Kibaranga Sisal Estate lenye ukubwa wa hekta 6,900, liliuzwa kwa kampuni ya katani ltd, iliposhindwa kuendeleza serikali ililiweka chini ya PSRC na bodi ya Mkonge.

3) Kwamngwe sisal estate, lenye ukubwa wa hekta 3700, liliuzwa kwa Chavda Group mwaka 1998, alichukua mkopo, hakuendeleza shamba.

4) Kwafungo Sisal Estate, lenye ukubwa wa hekta 2310, liliuzwa kwa Chavda Group mwaka 1998, mwekezaji alitumia hatimiliki ya shamba kuchukua mkopo, ambapo hakutumia kwa kusudi la kuendeleza shamba. Shamba hilo bado linashikiliwa na CRDB.

5) Bombuera Sisal Estate, lenye ukubwa wa hekta 2370, lipo Korogwe, liliuzwa kwa Chavda Group mwaka 1998. Mwekezaji alitumia hatimiliki ya shamba kupata mkopo. Hakuliendeleza shamba. Mwaka 2002 CRDB iliuza shamba kwa AMC Arusha Ltd.

6) Hale Mwakiyumbi Sisal Estate, lenye ukubwa wa hekta 4,309. Shamba liliuzwa kwa Chavda Group, 1998. Alitumia hatimiliki kupata mkopo ambao hakuutumia kwa kusudi lakuendeleza shamba na kulitekeleza. Shamba linashikiliwa na CRDB.

7)
Allidina Sisal estate, lenye ukubwa wa hekta 2300, liliuzwa kwa Noble Azania Agriculture Enterprises mwaka 1993. hakuna uwekezaji wowote uliofanyika!

8) Msowero (Godes) Farm, lenye ukubwa wa hekta 5,000. lilikuwa linasimamiwa na wizara ya Kilimo chini ya Tanzania Livestock research organization (TALIRO) Mwaka 1993 serikali ya CCM ilipanga kujenga chuo cha mifugo. Mpango ambao haukukamilika ,shamba likabaki bila usimamizi wowote.

9) Rutindi Sisal estate,lina ukubwa wa hekta 1,087. Shamba liko Morogoro, linamilikiwa na kampuni ya Noble Azania Agricultural Enterprises. Shamba halijaendelezwa na mwekezaji toka amelinunua.

10) Magole Sisal Estate, lina ukubwa wa hekta 1,149. Lipo Dumira, kilometa 65 toka Kilosa. Lilikuwa la serikali chini ya mamlaka ya mkonge Tanzania. Japo halijabinafsishwa liko katika hali mbaya.

11) Mauze Sisal Estate , lina ukubwa wa hekta 2,842.5. Shamba lilikuwa na deni la shilingi milioni 1.36 kutoka benki ya NBC. Benki ilishikilia Hati miliki na kuliweka chini ya ufilisi wa LART kutokana na kuongezeka kwa deni mpaka milioni 10. Kwa sasa kuna vijiji vya Kilangali na Mabwembele vilivyoanzishwa na vimesajiliwa ndani ya shamba. Halmashauri za vijiji hivyo zinakodisha maeneo katika shamba hilo kwa wanavijiji na watu kutoka nje ya vijiji kwa gharama ya shilingi 3,000 kwa ekari moja!

12)
Myombo na Kilosa Sisal estate. Mashamba haya yenye ukubwa wa hekta 2,024 (Kilosa) na 1843 (Miyombo). Mashamba yalibinafsishwa na mamlaka ya Mkonge kwa Kampuni ya Katani mwaka 1998. Baada ya kampuni ya Katani Limited kushindwa kuyaendesha ,iliyakodiha kwa kampuni ya Agro-Focus. Mwaka 2005 Baraza la Mawaziri liliagiza kuwa mashamba haya yatafutiwe mwekezaji mwenye uwezo kwani kampuni ya Agro- focus LTD imeshindwa kuyaendeleza.

Hata hivyo, kinyume na maagizo mwaka 2009 Bodi ya Mkonge iliyauza mashamba haya kwa Agro-Focus. Matokeo yake mpaka sasa hakuna uwekezaji wowote uliofanywa. Sehemu kubwa ya shamba ni pori na sehemu iliyobaki imekodishwa kwa wananchi kwa ajili ya kulima mahindi.


13) Madoto sisal estate, shamba lina ukubwa wa hekta 3,200. Shamba lilinunuliwa na kampuni ya SUMAGRO Ltd ambayo nayo ililiuza kwa East African Breweries mnamo mwaka 2009. Hakuna uwekezaji wowote uliofanyika !

14) Kivungu Sisal Estate, shamba lina ukubwa wa hekta 2,200. Shamba lilinunuliwa na kampuni ya SUMAGRO Ltd. Mwaka 1998, ililiuza kwa East African Brewaries mwaka 2009. Hakuna uwekezaji wowote uliofanyika!

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka serikali kuyarejesha mashamba yote ambayo wawekezaji wameshindwa kuyaendeleza, kama ambavyo taarifa hii imevyoainisha. Hali kadhalika kwa wale wawekezaji ambao wameweza kuendeleza sehemu ndogo na hawana uwezo wa kuendeleleza shamba zima warejeshe sehemu ya mashamba waliyoshindwa kuendeleza ili wapewe wananchi wenye uhitaji!

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inapendekeza serikali iangalie hatua za kuchukua dhidi ya wawekezaji katika mashamba 13 ambao wafuatao wameshindwa kuendeleza mashamba kwa 100%. Pamoja na wawekezaji katika mashamba 14 ambao wameshindwa kabisa kuendeleza mashamba waliyonunua, kama ambavyo yameorodheshwa hapo juu.

Mheshimiwa Spika, kwa tathmini hii fupi iliyofanywa na CHC utaona ni kwa namna gani zoezi la ubinafsishwaji mashamba lilifanywa kiholela na kwa hujuma, pasipo kuzingatia maslahi ya umma. Katika hali ya kawaida , watu wote walioshiriki katika zoezi hilo wana kila sababu ya kuchukuliwa hatua, hakika hawana tofauti na wahujumu uchumi. Kwa mfano huyu 'mwekezaji' anayejiita Chavda Group, aliuziwa shamba kwa bei ya kutupa mashamba saba, yenye ukubwa wa hekta 25,000, katika maeneo tofauti ya nchi hii.

Kikubwa alichokifanya ni kutumia hati za shamba kuchukulia mikopo, kisha kutelekeza mashamba!! Hivi kweli unahitaji kuwa na akili nyingi kuyaona haya? Nyuma ya Chavda Group wako akina nani?

Mheshimiwa Spika, ikumbukwe ni familia hii hii ya Chavda ( V.G Chavda na kaka yake P.G Chavda),[5] waliojitwalia mkopo wa $ 3.5m mwaka 1993 chini ya DCP (Debt Conversion Program) wakiahidi kufufua mashamba ya mkonge Tanga ndani ya miaka 10, na kupata $42 milioni. Walipopata hayo mapesa, hawakufanya lolote, na hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi yao!

Mheshimiwa Spika, kwa utaratibu huu, lazima tuwachukulie wawekezaji wa aina hii kama ni 'waporaji' na hawana tofauti na majambazi yanayoiba benki kwa kutumia nguvu!
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka serikali, kupitia Wizara ya Ardhi yenye jukumu pana la kusimamia sekta ya ardhi kuhakikisha kwamba maeneo yote ambayo hayajaendelezwa na wawekezaji yanarejeshwa serikalini bure bila fidia kwa ajili ya kutafuta wawekezaji wengine wenye mtaji wa kutosha watakaoyaendeleza mashamba hayo.

Hali kadhalika, kwa yale mashamba ambayo tayari yana wakulima wadogo wadogo wanaoendesha shughuli zao za kilimo, serikali ipange utaratibu wa kuwamilikisha wananchi maeneo husika, ili kuondokana na ile dhana ya 'uvamizi' au kukodishwa ardhi kwa ajili ya kilimo. Zoezi hili lazima lifanywe kwa uwazi ili kuepuka udanganyifu uliotokea katika maeneo mengine ya nchi ambapo vigogo na watu wenye nafasi zao walijitwalia ardhi wakijifanya na wao ni sehemu ya wanakijiji!

MASHAMBA YALIYOPENDEKEZWA KURUDISHWA KWA WANANCHI MKOA WA ARUSHA


Mheshimiwa Spika,
tarehe 17/6/1997 aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Arusha, Ndugu D. Ole Njoolay aliitisha kikao kilichohudhuriwa na Ndugu Kileo – katibu tawala Mkoa, Ndugu P.H Muhale- Afisa Maendeleo ya ardhi (M), ndugu E. K. E Makere – Afisa Ardhi na Ndugu Z.M.S Meirish – Afisa Ardhi. Kikao husika kilichofanyika saa 4.35 asubuhi kilikuwa mahsusi kwa kuchambua mapendekezo yaliyoletwa kutoka wilayani kuhusu taarifa za mashamba makubwa mkoani Arusha.

Mheshimiwa Spika, mashamba yaliyojadiliwa na kufikia maamuuzi mbali mbali yalihusisha wilaya sita: a) wilaya ya Arumeru- Mashamba 18 b) wilaya ya Ngoro Ngoro- Mashamba 10 c) wilaya ya Babati – Mashamba 11 d) wilaya ya Simanjiro – Mashamba 2 e) wilaya ya karatu –Mashamba 6 f) wilaya ya Monduli – Mashamba 36 (Nakala ya Majina ya Mashamba pamoja na hatua zilizopendekezwa nimeziambatanisha kama sehemu ya hotuba hii). Kambi ya upinzani inaitaka serikali kulieleza Bunge hili tukufu nini mustakabali wa mashamba 83, na hatua zilizochukuliwa kufuatia kikao husika.

Mheshimiwa Spika
, mwaka 1999, ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, kupitia barua yenye kumb. Na. RC/AR/ CL 2/3 Vol IV/19 ilimwandikia Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Arumeru ikimtaarifu juu ya mashamba 11 ambayo yamepata kibali cha Rais kufuta miliki. Taarifa ambayo ofisi ya mkuu wa mkoa ilipata toka kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi kwa barua yenye kumbu kumbu namba CL/46/VOL III ya tarehe 1 Juni 1999 .

Mashamba hayo:
1) Shamba namba 78 na 79 - NAIC , Usa River 2) Shamba namba 90 na 91- Madiira Coffee ltd 3) Shamba namba 98/2/1 – Duluti New – Duluti Lodge 4) Shamba namba 218/2- Maua limited 5) Shamba la Oljoro – Salama estate 6) Shamba la Unit 15 Oljoro – Iman estate 7) Karangai Sugar Estate ( Tanzania Plantaion) 8) Shamba Namba 3 – Milimani pharmacy 9) Shamba la Nduruma- Lucy estate 10) Shamba la Nduruma – Umoja Sisal Estate 11) Shamba la DOLLY – DOLLY ESTATE- FLYCATCHERS (ambalo limegeuzwa uwanja wa Gofu na shamba la wanyama kinyume na maagizo ya Rais)

Kambi ya upinzani
, inaitaka serikali itupe maelezo ya kina kuhusu mashamba haya!

MIGOGORO YA ARDHI


Mheshimiwa Spika,
kama ambavyo tulifanya katika mwaka wa fedha 2011/12, Kambi ya Upinzani itakuwa na utaratibu wa kila mwaka wa fedha kuianishia serikali migogoro mbali mbali ya ardhi inayolikumba taifa letu! Ni jukumu la Serikali kupitia vyombo vyake kuhakikisha kwamba inafuatilia migogoro hii kwa kina na hatimaye kuyatafutia ufumbuzi:

BAGAMOYO- MKOA WA PWANI


Mheshimiwa Spika, wananchi wa kijiji cha Milo chenye vitongoji vitano:- Milo, Relini, Kengeni, Kisiwani na Migude, kilichoandikishwa chini ya sheria ya kijiji (chenye shule ya msingi na zahanati na kijiji) wanailalamikia Kampuni ya Noble-Azania Agricultural Enterprises Limited ambayo inadai ni wamiliki halali wa eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 3000. Eneo ambalo limekimeza kitongoji cha migude na sehemu ya kijiji cha milo. Kwa upande mwingine, Kampuni ya Azania, inadai wanakijiji hao ni wavamizi kwa kuwa wao wana umiliki halali wa eneo husika kupitia umiliki namba 36911.

WILAYA YA MPANDA – KATAVI

Mheshimiwa Spika, mkoa mpya wa Katavi, anakotoka Waziri Mkuu, ni kati ya maeneo yenye migogoro mingi sana ya ardhi, mingi ikiwa ni migogoro sugu, ambayo imeshindwa kutafutiwa ufumbuzi licha ya malalamiko kufika ngazi za juu serikalini pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Migogoro inazihusu kata za Kabwe na Korogwe, kijiji cha Nkungwi[6], kijiji cha Kabange, Kijiji cha Mbuguni, mgogoro baina ya hifadhi ya Ubende na vijiji kumi na nane.

Mheshimiwa Spika, nitawasilisha mezani kwako nyaraka mbali mbali za migogoro hii, kama serikali itaona inafaaa, iyafanyie kazi! Mheshimiwa Spika, kutokana na muda, nitaelezea mgogoro mmoja sugu, ambao unahusisha watendaji serikalini.

Mgogoro ambao unaambatana na vitisho kwa wananchi, mpaka kufikia hatua wananchi kufunguliwa kesi za jinai[7] ili kuwatisha. Wananchi wa Kata ya Sibwesa, wilaya ya Mpanda wanalalamikia mtandao ambao umeundwa na watumishi wa serikali, ambao ni waajiriwa wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda, wanaofahamika kama Cletus Siwezi, Andrea Malando (Kitengo cha Ardhi) na Bwana Galus Kasonso (Meneja wa mradi wa maji katika Halmashauri ya Mpanda ).

Mheshimiwa Spika, watumishi hawa wanalalamikiwa na wananchi, wakituhumiwa kuwanyang'anya mashamba yao kwa kutumia nafasi zao. Mheshimiwa Spika, mtumishi huyu wa Serikali (kupitia kwa bwana Ramadhani), alishindwa kuthibitisha umiliki wake katika baraza la ardhi la Kata, walikimbilia Baraza la Ardhi na Nyumba la Sumbawanga ambapo ilitolewa hukumu ya upande mmoja!

Baada ya hukumu hiyo ya upande mmoja kumekuwa na hujuma dhidi ya wananchi na kuna malalamiko kwamba kuna mbinu ya kuandikwa hati ya kukamata heka mia tatu na sitini (360) kutoka mbuga ya Mwamapuli, kijiji cha Kabage na mbinu yake ya kuendelea kufanya mipango ya kukamata watu bila ya kuwa na kosa kwa kutambua kuwa hawana uwezo wa kukabiliana na kesi za jinai.

Jeshi la polisi linahusishwa pia katika mazingira mawili, la kwanza kufungua kesi za kubambikiza, hali kadhalika kumlinda mhalifu!
Mheshimiwa Spika, yanayotokea Mpanda, yanafanyika pia kwenye maeneo mengi ya nchi hii, kwa watu ambao wamepewa dhamana kutoa huduma hii muhimu kwa wananchi, kutumia fursa hiyo kujilimbikizia ardhi, na pale ambapo wananchi wa kawaida wenye uhitaji wa huduma hiyo kukumbana na urasimu mkubwa uliotawaliwa na rushwa!

Mheshimiwa Spika
, Kambi ya Upinzani inaitaka serikali ijipime kwa kuangalia ni hatua gani stahili itawachukuliwa watumishi hao wa halmashauri kama ushahidi ulivyotolewa, na pengine inaweza pia kubaini mambo mengi mazito yaliyojificha!

MKOA WA MANYARA- BABATI

Mheshimiwa Spika, mgogoro huu unahusu hifadhi ya Taifa Tarangire na Vijiji vya Gijedabung, Ayamango[8] na Gedamar[9]. Mheshimiwa Spika, vijiji hivi vilikaliwa na wananchi toka miaka ya 1960. Hifadhi ya Tarangire ilianzishwa mwaka 1970 kwa kuzingatia tangazo la Serikali (GN) Na. 160. Mipaka yake ilitambulishwa kwa barabara iliyozunguka hifadhi nzima na kuipatia umbo linaloonekana katikati yake kupitia Sheria ya mwaka 1974 ya Vijiji na Vijiji vya ujamaa, mpaka ambao wananchi wote waliutambua na kuuheshimu.

Mheshimiwa Spika, mgogoro ulianza baada ya uongozi wa hifadhi ya Tarangire ulipotekeleza zoezi lake la kuhakiki mipaka yake kwa nia ya kufanya tafsiri yakinifu kwa kutumia vifaa vya kisasa. Wataalam walibaini kwamba ule mpaka wa miaka yote wa barabara, ulioliwekwa na
Mamlaka ya Hifadhi yenyewe
haukuzingatia vipimo halisi na hivyo kusababisha eneo lenye ukubwa wa ekari 16,249.10325 kuingizwa kwenye mamlaka ya vijiji kimakosa. Kwa mantiki hiyo hifadhi iliamuru wananchi waliokuwa wakiishi kwenye ardhi hiyo kuhama mara moja na kusitisha matumizi yote juu ya ardhi hiyo.

Mheshimiwa Spika, kutokana na amri hiyo, wananchi wengi wa maeneo haya wako katika hali mbaya sana kiuchumi kutokana na ardhi waliyokuwa wanaitegemea kuchukuliwa na serikali! Wananchi wamezuiwa kufanya kitendo chochote cha kufanyia matengenezo makazi yao walioishi kwa zaidi ya miaka 50. Ikumbukwe kwamba wananchi hawa hawakuvamia eneo hili bali waliwekwa na mamlaka ya wilaya kwa makosa pasipo kukusudia. Pamoja na serikali kutaka kuwahamisha wananchi hao haijafanikiwa kuwapatia makazi mapya na mashamba ya kulima.

Mheshimiwa Spika,
usumbufu wa Askari wa Hifadhi ya Tarangire wanaofanya vitendo vya unyanyasaji ni kero kubwa kwa usalama, utulivu na ustawi wa wananchi wa maeneo husika. Kambi ya upinzani haidhani kwamba hifadhi ni muhimu zaidi kuliko watanzania waliokiweka CCM madarakani. Ni rai yangu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano awatazame wananchi wa maeneo haya kwa jicho la huruma!

Awatazame wananchi wa maeneo haya kwa jicho la huruma kutokana na kwamba hawana maeneo mbadala ya kuishi ili kuendeleza maisha yao! Rais wa Jamhuri ya Muungano ana mamlaka ya kuhawilisha ardhi ya Hifadhi ya Taifa ya Tarangire inayokaliwa na wananchi wa vijiji tajwa ili iwe ardhi ya kijiji, ombi ambalo lilisha wasilishwa Wizara ya Ardhi Nyumba na Makazi, lakini mpaka leo hakuna majibu!


MKOA WA KAGERA- wilaya ya Karagwe

Mheshimiwa Spika, muda sasa Kambi ya Upinzani, pamoja na wabunge wengi, wamekuwa wakizungumzia juu ya mgogoro baina ya wakulima na wafugaji, kutokana na serikali kutokuwa na mpango endelevu wa kutenga maeneo ya wakulima na wafugaji. Mwaka jana katika hotuba ya Kambi, tulielezea juu ya mgogoro wa wakulima na wafugaji wa jamii ya Wamasai katika eneo la vijiji vya Izava (Chamwino) na Chitego (Kongwa).

Mgogoro huu mpaka leo hujapatiwa ufumbuzi. Kimsingi mgogoro ulisababishwa na ubabe na maamuzi mabovu ya mkuu wa wilaya. Katika hotuba hii, Kambi ya Upinzani inafikisha mbele ya Bunge lako Tukufu kilio cha wanavitongoji vya Karugwebe, kijiji cha ITEERA na kitongoji cha MTAKUJA kijiji cha CHANYA, Karagwe.

Mheshimiwa Spika, wananchi wanalalamikia kufukuzwa kwenye maeneo yao ya kilimo na kupewa wafugaji matajiri bila wao kuhusishwa! Baada ya kufukuzwa hawakupewa hifadhi, kitu ambacho kimewafanya wawe wahamiaji wasio rasmi ndani ya nchi yao! Ikumbukwe wananchi hawa walikuwa wanafanya shughuli za kilimo kwa kipindi cha zaidi ya miaka 20. Madiwani walipohoji katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika ntarehe 31/2/12, walipata vitisho kutoka kwa Mkuu wa wilaya ya Misenyi aliyekuwa anakaimu ukuu wa wilaya ya Karagwe!

Mheshimiwa Spika
, Kambi ya Upinzani inataka kauli ya serikali kuhusiana na matukio haya mawili; hali kadhalika serikali ilitaarifu Bunge lako tukufu, ni lini Serikali itaandaa mpango rasmi wa matumizi ya ardhi kwa wakulima na wafugaji ili kuepuka migogoro isiyokwisha! MKOA WA

DAR- ES- SALAAM
Maeneo ya Pembezoni

Mheshimiwa Spika, miaka ya hivi karibuni serikali imekuwa na mikakati, inayoitafsiri kama mikakati kabambe ya kuendeleza maeneo yaliyomo pembezoni mwa jiji la Dar es salaam. Mipango hiyo imeleta msiba mkubwa sana kwa wananchi wa maeneo hayo! Kwa sababu ya muda, tutazungumzia miradi ya Luguruni na Kwembe Kati, Kinondoni Dar es salaam.

Mheshimiwa Spika
, katika maeneo haya, wananchi wameporwa ardhi yao yote kwa fidia ndogo sana, wamebomolewa makazi yao na kutimuliwa kutoka kwenye ardhi yao kwa nguvu ya dola, wakiwa wamemaskinishwa kupindukia baada ya kuporwa rasilimali ardhi yao, na wakiwa na fidia duni mkononi, wakihamia kwingineko kuanzisha makazi yasiyopimwa na ya kimasikini kupindukia!

Miradi hiyo imegubikwa na utendaji wenye kupindisha sheria, ubabe, usio na utawala bora, ulioteteresha viwango vya ramani na upimaji uliochakachua fidia, uliofanya ofa na hatimiliki kuwa uyoga, uliojaa dhuluma na hujuma dhidi ya hakiardhi ya wananchi. Hapo Luguruni tarehe 22/5/2007 Mkurugenzi wa Makazi na Ardhi alitangaza utwaaji wa ardhi wa 5% ya Ardhi kwa ajili ya miundombinu. Hali hii ilibadilika kufikia 100% na waliofanya hivyo ni watendaji wa mradi baada ya mkurugenzi husika kustaafu.

Mheshimiwa Spika, hali kadhalika kinachofanyika Kwembe Kati, kwa maeneo ya miundombinu, biashara na makazi yalitwaliwa na Mradi na kutangazwa kuwa mali ya serikali, licha ya tamko la Waziri wa Ardhi Mhe. Chiligati Bungeni la tarehe 18/06/2009 na tamko la Naibu Waziri wa Ardhi Mhe. Goodluck Olemedeye Bungeni tarehe 12/11/2011 kusisitiza ya kwamba baada ya Rais kutwaa ardhi na Miundombinu albaki ya ardhi kwa ajili ya makazi na biashara ibakie mikononi mwa wananchi wamiliki wa ardhi, waiendeleze wao wenyewe ili waweze kujikomboa kiuchumi.

Katika maeneo yote hayo, baada ya ardhi yote ya wananchi kutwaliwa kwa fidia duni chini ya 20% ya bei ya soko kinyume hata na matakwa ya sheria ya ardhi, namba 4 ya mwaka 1999, sehemu ya II, kifungu cha 3 kinachoelezea misingi mikuu ya sera ya ardhi ya Taifa, wananchi walitimuliwa kimabavu baada ya makazi yao kubomolewa kwa tingatinga. Mfano dhahiri ni wa eneo la Luguruni; fidia iliyolipwa kwa mita moja ya mraba ilikuwa ni shilingi 1,977, ardhi hiyo hiyo iliuzwa kwa tshs 30,000 mita moja ya mraba bila maendelezo yoyote! Hivyo kuzalisha faida ya 1500% …Huu ni wizi na unyonyaji mkubwa.


Mheshimiwa Spika, inasikitisha sana pale watendaji wa wizara ya Ardhi, wanapotumia mgongo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutengua toleo la hatimiliki halali za wananchi wamiliki wa ardhi, kupora ardhi yao kwa mtindo huu, kupima viwanja vipya juu ya viwanja vya awali.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inataka serikali hii ya CCM, kuacha kufanya mambo kibabe, na kusitisha kile kinachoendelea katika maeneo ya Luguruni na Kwembe Kati. Ulipaji fidia unakuwa na mianya lukuki ya ubadhirifu wa fedha, hivyo kuhitaji ukaguzi na udhibiti wa makini sana wa masuala yote ya malipo na matumizi ya fedha kwenye miradi ya Luguruni na Kwembe Kati.

Viwango vya fedha vinavyohusika hapa ni vikubwa sana kutokana na wingi wa watu wanaohitaji kufidiwa na kutokana na mauzo ya viwanja vilivyopatikana katika mchakato mzima wa kutwaa na kuuza ardhi, kuna uhitaji mkubwa wa ukaguzi na udhibiti mahsusi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu.
Suala la ukaguzi ni muhimu kutokana na tuhuma kwamba malipo ya fidia yamefanywa bila kutumia nyaraka halali za matayarisho na ulipaji fedha.

Tatizo la Uvamizi wa Maeneo ya watu

Mheshimiwa Spika, kuna tabia iliyozuka kwa kasi sana, katika manispaa ya Kinondoni, hususan maeneo ya pembezoni, na katika jimbo la Kawe; ninaloliwakilisha tabia hii imekithiri sana kata za Bunju, Mabwepande na Wazo. Kumekuwa na genge la watu wenye silaha wanaovamia maeneo ya watu, kuharibu mali, kugawa viwanja na kuwauzia watu (wapya) viwanja kwa bei ya kutupa.

Hilo genge, baada kufanya uharibifu eneo moja, huhamia eneo lingine! Hali hii imesababisha uvunjifu wa amani, na katika mazingira mengine kusababisha vifo!


Mheshimiwa Spika,
hofu ya wananchi inaongezeka kutokana na kutokupata ushirikiano kutoka kwa mamlaka zenye jukumu la kuhakikisha wananchi na mali zao wako katika hali ya usalama. Kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya na Mkoa wa Dar es salaam zote zina taarifa ya genge hili la majambazi wa ardhi, vyombo mbalimbali vya habari vimetoa taarifa kuhusu genge hili la majambazi, hakuna hatua zilizochukuliwa na wala hakuna dalili kama kuna dhamira ya dhati ya kuweza kutafuta suluhu!

Mheshimiwa Spika,
ni dhahiri kwamba serikali ingejipanga katika matumizi bora ya ardhi na kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata ardhi kwa gharama nafuu bila urasimu walarushwa, hili genge la majambazi wa ardhi lisingepata wateja!

Kambi ya Upinzani
inaitaka serikali ieleze Bunge ina mipango gani ya muda mfupi na mrefu kuweza kukomesha kabisa suala la uvamizi wa maeneo ya wazi! Nikiwa mbunge wa Kawe, napenda kuwasisitizia wamiliki wote wa ardhi Jimbo la Kawe, serikali ya wilaya kupitia kamati yake ya ulinzi na usalama imeshindwa kuwapa ulinzi wenu na mali zetu. Niendelee kuwashawishi kila mmoja kwa nafasi yake mmoja mmoja au kwa vikundi kuweka walinzi binafsi kwa ajili ya kulinda mali zao! Na chochote kikitokea mbunge wenu nitawalinda kwa sababu nilishatoa taarifa kuanzia ngazi ya wilaya, mkoa mpaka serikali kuu!

Majiji ya Viungani (setelite towns)

Mheshimiwa Spika, Mwaka 2006/07 Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ikishirikiana na Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam na Manispaa zake tatu ilianzisha Mkakati wa kuanzisha miji midogo sita itakayokuwa na vituo vya huduma za kijamii na za kibiashara. Kutokana na ukubwa wa mpango huo iliamuliwa kuwa utekelezaji uanze katika eneo la Kibamba Luguruni ambalo lilipaswa kuwa eneo la mfano ambapo uzoefu katika uendelezaji ungetumika kwa maeneo mengine ya Jiji na nchi nzima kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, Uanzishwaji wa Mji wa Kibamba uligawanywa katika maeneo makubwa matatu: Eneo Kitovu cha Mji cha Luguruni, eneo la makazi mbadala la Kwembe Kati na uendelezaji wa eneo linalozunguka kituo. Hata hivyo miaka zaidi ya mitano imepita bila uendelezaji huo kukamilika na hivyo sehemu kubwa ya maeneo tajwa kurejea kuwa mapori na kuanza kurejea kwa migogoro ya ardhi katika maeneo tajwa.

Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza matokeo ya tathmini ya utekelezaji wa mpango huo na kueleza bayana kasoro na matatizo yaliyojitokeza sambamba na kuharakisha ujenzi wa mji husika ili kuwa mfano kwa mipango ya ujenzi wa miji mingine ambayo maandalizi yake yanaelezwa kutaka kufanyika katika mwaka wa fedha 2012/2013.

Mheshimiwa Spika,
wakati zoezi la wa Luguruni, Kwembe Kati na Kigamboni yakitawaliwa na malalamiko makubwa sana kutoka kwa wananchi, Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi imeandaa mpango mpya wa Makongo. Mradi huu utasimamiwa na mtendaji aliyeendesha zoezi la kihuni la ujenzi mpya wa mji wa Kigamboni!

Kambi ya Upinzani inaona mradi huo umeanza vibaya kwani msimamizi wake mkuu haaminiki kutokana na miradi aliyoisimamia huko nyuma. Hivyo basi inaitaka Serikali ikutane na wananchi na majirani zake wa Makongo tulijadili hili kwa kina! Kutumia mabavu hakutasaidia! Wananchi wa makongo wanataka maendeleo, lakini yasiwe maendeleo yenye lengo la kuwapa mzigo, ufukara na kuwahamisha wale ambao hawatakuwa na uwezo wa kukidhi matakwa ya mradi! Nasisitiza mimi ni mbunge wako, njoo tuzungumze!

UWINDAJI, UFISADI NA UKIUKWAJI WA SHERIA ZA MATUMIZI YA ARDHI


Mheshimiwa Spika,
kwa muda mrefu sasa Ardhi ya Tanzania imegeuzwa shamba la bibi na kikundi cha mafisadi! Kambi ya Upinzani imeshuhudia mkataba ulioingiwa baina ya kampuni za Uranium resourses PLC, Western Metals Limited na Game Frontiers of Tanzania Limited. Mkataba ambao umetengenezwa na Kampuni ya Kitanzania ya REX ATTORNEYS. Na ulisainiwa tarehe 23.3.2007.

Mheshimiwa Spika, mkataba husika,ambao vipengele vyake vinaainisha kwamba unatakiwa uwe wa SIRI unaihusu kampuni ya uwindaji, inayofahamika kwa jina la Game Frontiers of Tanzania Limited inayomilikiwa na Bwana Mohsin M. Abdallah na ndugu Nargis M. Abdallah. Kampuni hii ya uwindaji, imeingia mkataba na kampuni mbili za kigeni, za kufanya utafiti wa uchimbaji wa madini ya Uranium katika kijiji cha Mbarang'andu kwa malipo yafuatayo:-

a)
Malipo ya $ 6,000,000/- za kimarekani, ambazo zitalipwa kwa awamu mbili ya malipo ya $3,000,000. Malipo ya kwanza yatafanyika pale uzalishaji wa urani utakapoanza.

b) Malipo ya $ 250,000/- baada ya kampuni za madini kukamilisha utafiti wa madini ya urani na kupata kibali cha uchimbaji wa madini.

c) Malipo ya $ 55,000 kila mwaka kama fidia ya kushindwa kufanya biashara na usumbufu unaotokana na shughuli za machimbo kwenye kitalu! Malipo hayo yatafanyika kila tarehe 31Machi.

d) Malipo ya $ 10,000 kwa vijiji vitakavyoathiriwa na utafiti huo wa urani. Malipo ambayo yametokana na makubaliano baina ya kampuni ya uwindaji na kampuni za madini! Mheshimiwa spika, nimepitia sheria za uhifadhi wa wanyamapori, The wildlife Conservation Act, 1974 (Sheria ya zamani) na Sheria mpya The wildlife Conservation Act, Act no 5 of 2009. Sheria hizi zinamruhusu mtu aliye na leseni ya uwindaji, kuwinda wanyama tu!

Mheshimiwa spika,
hali kadhalika, Sheria ya Ardhi ya Mwaka 1999, Sheria namba 4 ya mwaka 1999 na Sheria ya Ardhi ya vijiji, sheria namba 5 ya mwaka 1999 inatamka bayana kwamba ardhi inajumuisha vitu vyote vilivyo juu ya ardhi na chini ya ardhi isipokuwa madini au mafuta……… Na kwa mujibu wa sheria za Tanzania linapokuja suala la madini, umiliki unatoka kwa mtu binafsi na kurudi serikalini! Na ni Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini ndiyo pekee yenye mamlaka ya kutoa leseni ya kutafuta madini kwa kampuni za madini!

Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inaitaka serikali ilieleze Bunge lako tukufu uhalali wa mkataba kati ya Game Frontiers na Uranium Resourses PLC na Western Metals! Ni sheria ipi inayoipa kampuni ya uwindaji haki ya kualika kampuni ya nje kwenye eneo ambalo haina umiliki kufanya utafiti na hatimaye kuchimba madini hatari kama urani?

Nini mustakabali wa Watanzania wanaoishi kwenye vijiji vinavyozunguka mbuga hiyo ambao wanaishi maisha yao ya kila siku pasipo kujua kama kuna utafiti wa madini hatari ya urani unaoendeshwa kwa siri kubwa? Ni serikali ya aina gani, yenye uwakilishi mpaka ngazi ya kitongoji na usalama wa taifa mpaka ngazi za chini kabisa za utawala inashindwa kuyaona haya?


MCHAKATO WA KUTOA ARDHI KWA WAWEKEZAJI


Mheshimiwa Spika
, uchunguzi uliofanywa na haki ardhi umebaini kuwa katika wilaya ya Kilwa, mwekezaji alikuwa na kampuni iitwayo Bioshape kutoka nchini Uholanzi. Kampuni hii ilipewa ardhi yenye ukubwa wa hekta 80,000 kwa lengo la kulima zao la mbono kaburi, ardhi hiyo ilihusisha vijiji vinne ambavyo ni Mivuji, Migelegele, Liwili na Inokwe. Mwekezaji hakutumia eneo lote na kulima hekta 800 tu katika kijiji cha Mavija ambazo ziligeuka kuwa pori baada ya mwekezaji kutelekeza shamba, vifaa na wafanyakazi.

Mheshimiwa Spika, katika wilaya ya Kisarawe, mwekezaji alikuwa ni kampuni inayoitwa SunBiofuels kutoka nchini Uingereza. Kampuni ilipewa ardhi ya ukubwa wa ekari zipatazo 9000 iliyojumuisha ardhi za vijiji 11 ambavyo ni Marumbo, Muhaga, Mtamba, Mzenga A, Kurui, Chakenge, Mitengwe, Paraka, Kidugalo, Vilabwa na Chakaye.

Mwekezaji huyu hakulima shamba lote bali alilima shamba la mfano katika eneo la ekari zipatazo 3000 lililopo kijiji cha Mtamba ambalo lilikuwa na mazao ambayo mengi yameanza kuzaa matunda huku yakiwa tayari kwa kuvunwa, pia Bagamoyo kampuni iliyohusika inaitwa Sekab Bioenergy Tanzania Limited.


Mheshimiwa Spika
, ieleweke kuwa katika maeneo yote ardhi zilikuwa za aina mbili; zilizomilikiwa na wanakijiji na zile za vijiji ambazo zilipaswa kuhawilishwa kwanza na kisha kutolewa kwa mwekezaji. Kwa jumla, wananchi katika vijiji, watendaji wa vijiji, wajumbe wa kamati za vijiji kwa pamoja walisema hawakuridhika na mchakato uliotumika kutoa ardhi kwa wawekezaji.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inasikitikamchakato kujaa mizengwe, hadaa, utapeli kwa wananchi na hata harufu ya rushwa kwa baadhi ya watendaji wa vijiji, maofisa ardhi katika wilaya na vigogo wa juu katika wilaya na halmashauri. Hata pale ambapo wananchi walirubuniwa kutoa ardhi zao kwa kuelezwa kuwa mwekezaji ataleta neema katika maeneo yao, bado fidia hazikuwafikia, zilichelewa au fidia iliyotolewa ilikuwa ndogo, huku zoezi la kutathmini mali zilizopo katika ardhi zao likiwa siyo la wazi na shirikishi. Hata vigezo vya tathmini kwa ardhi na mazao havikuwekwa bayana kwa pande husika.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani kwa niaba ya wananchi inaitaka serikali kuzingatia sheria na kusimamia utekelezaji wake kwa ngazi mbalimbali kwa kuwatendea haki wananchi kuwapa huduma zenye uhalali kisheria ikizingatiwa fidia zilizotolewa hazikurandana na hali halisi ya soko kwa wakati husika.

Mheshimiwa Spika,Serikali katika hotuba yake hapa bungeni kupitia Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi mwaka wa fedha 2011/12 ilikiri kuwa na changamoto ya kutokuwa na mfumo thabiti na utunzaji wa kumbukumbu za sekta ya ardhi na kutoa ahadi ya kujenga mfumo mmoja wa kuhifadhi kumbukumbu za ardhi kwa njia ya kielekroniki (Integrated Land Management System) utakaounganisha mifumo yote ya utunzaji wa kumbukumbu za sekta ya ardhi. Kambi ya Upinzani inaitaka serikali kueleza wananchi mfumo huu umefikia wapi na utekelezaji wake uko je?

Mheshimiwa Spika, kutokana na tatizo la ardhi kwa maana ya uwekezaji na matumizi mbalimbali ya serikali kutopatikana kwa urahisi mijini na vijijini, serikali kupitia wizara iliahidi hapa bungeni kuanzisha chombo kitakachosimamia hazina ardhi (Land Bank) ili kurahisisha upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya miradi ya uwekezaji na kuunda mfuko wa kulipa fidia(Land Compensation Fund) kwa mujibu wa sheria za ardhi ili kuiwezesha serikali kulipa fidia timilifu na kwa wakati inapotwaa ardhi kwa maslahi ya umma. Kambi ya Upinzani inataka kupata majibu kutoka kwa serikali ni hatua gani ziliendelea kuchukuliwa ikizingatiwa kuwa tatizo la fidia limeendelea kuwepo na kuwa kero kwa wananchi?

SEKTA YA NYUMBA

Mheshimiwa Spika,
sekta hii ni sekta pekee inayoweza kuleta na kutekelezwa kwa dhana nzima ya maisha bora kwa kila Mtanzania. Nchi yetu na Watanzania kwa ujumla bado tuna matatizo makubwa ya nyumba bora na za bei nafuu kutokana na bei kubwa ya simenti na bati- bidhaa muhimu katika kutimiza azma ya ujenzi.

Mheshimiwa Spika, tulisema na tunasema kuwa bei ya simenti na bati inaweza kuwa chini ya shilingi elfu saba, kama serikali itakuwa na utashi wa kuwahudumia wananchi kwa dhati. Bei ya simenti Uturuki na Paksitani ukinunua tani 600,000 bei ya tani moja ni dola za Marekani 70 hadi bandarini. Guangzhou –China tani moja ni dola za marekani 26. Kwa hesabu za kawaida kwa mfuko mmoja ni dola 3.5 sawa na shilingi 5250/- kama ukinunua Pakstani au Uturuki. Ukinunua China bei itakuwa dola 1.3. sawa na shilingi 1950/-

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani bado inasisitiza kuwa kama Serikali ina dhamira ya kweli mfuko wa simenti hauwezi kuuzwa zaidi ya shilingi 7,500. Hivyo basi tunaitaka Serikali itueleze kwa nini bei ya simenti inauzwa zaidi ya shilingi 14000 Dar es salaam na nje ya Dar es Salaam bei ni zaidi ya hapo, wakati malighafi zinapatikana hapa hapa nchini na kiwanda kikubwa cha simenti kinatumia gesi asili ili kupunguza gharama za umeme.

Mheshimiwa Spika, Serikali ina mkakati gani wa kupunguza gharama hizi na ni faida kiasi katika kodi tunayopata kwa kuwalangua Watanzania. Serikali haioni kwamba ina wajibu wa kuondoa hizi kero wananchi wajenge nyumba bora na kwa bei nafuu?

SHIRIKA LA NYUMBA LA TAIFA

Mheshimiwa Spika,
Shirika la Nyumba la Taifa, lilipoanzishwa mwaka 1962, moja kati malengo yake ilikuwa ni kujenga nyumba za bei nafuu kwa ajili ya Watanzania wafanyao kazi mijini . Hata hivyo kwa kadiri siku zilivyosonga mbele, shirika hili liligeuka kutoka kuwahudumia masikini na watu wenye kipato cha kati na badala yake linawahudumia watu wa kipato cha juu.

Mheshimiwa Spika
, Shirika la Nyumba la Taifa linahudumia asilimia 0.5 tu ya watanzania wote wa nchi hii. Swali la msingi ni je Serikali imeweka mikakati gani ya kuhakikisha kuwa shirika hili linahudumia Watanzania wengi zaidi kwa kuwapatia nyumba za bei nafuu?

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/2012 Kambi Rasmi ya Upinzani imepata taarifa kuhusu ujenzi inaoendelewa kufanywa na Shirika la Nyumba katika maeneo mbalimbali nchini. Kambi rasmi ya upinzani inataka Wizara kutoa maelezo kwa umma kuhusu migogoro iliyojitokeza kati ya shirika na wapangaji na hatua ambazo zimechukuliwa kushughulikia malalamiko yaliyotolewa hususan katika maeneo ya Chang'ombe, Ubungo na mengineyo."

KODI YA ONGEZEKO LA THAMANI (VAT) NA ONGEZEKO LA MTAJI (CAPITAL GAIN TAX) KWENYE MAUZO YA NYUMBA ZINAZOJENGWA NA SHIRIKA

Mheshimiwa Spika,
changamoto kubwa inayowakabili Watanzania wengi ni kuweza kupata nyumba za bei nafuu. Suala hili tulilizungumza mwaka jana, na tutaendelea kulizungumza! Kwa sheria zetu za kodi, nyumba mpya iliyojengwa kwa ajili ya kuuzwa inapaswa kutozwa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) pale inapouzwa, na anayelipa kodi hiyo ni mnunuzi!. Mheshimiwa Spika, suala la msingi ni kuwa nyumba hiyo wakati inajengwa vifaa vyote vya ujenzi vililipiwa kodi hiyo, hivyo kitendo cha mnunuzi kulipa kodi ya VAT wakati wa kununua nyumba hiyo ni kulipia kodi mara mbili (DOUBLE TAXATION).

Je, serikali haioni kama haimsaidii mwananchi kuweza kuishi kwenye nyumba nzuri na kwa gharama iliyo nafuu?
Mfano dhahiri ni kwamba kwa mwaka wa fedha 2010/11 shirika lilitarajia kujenga nyumba 49, zenye jumla ya thamani ya shilingi bilioni 4.08. Kwa gharama iliyotumika, wastani wa nyumba moja ililigharimu shirika shilingi milioni 83.4.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa Kazi za Shirika la Nyumba la Taifa kuanzia Julai 2010 hadi Mei 2011 walitarajia kupata shilingi bilioni 6.3 kutokana na mauzo ya nyumba hizo, yaani faida ya shilingi bilioni 1.9 Kwa tafsiri nyingine nyumba moja itauzwa na shirika la nyumba kwa shilingi milioni 129.2, wakati gharama halisi za ujenzi ni shilingi milioni 83. Kwa kila nyumba iliyouzwa shirika limepata faida ya shilingi milioni 46.

Mheshimiwa Spika,
sheria ya mikopo yaani "Government Loans, Guarantees and Grants Act 1974 and amendments 2003" inalifanya shirika la nyumba la taifa kulazimika kupata kibali kutoka Wizara ya Fedha hata pale ambapo halihitaji kupata dhamana ya serikali na pia hata kwa mikopo ya ndani ya nchi. Wote tunafahamu rasilimali ambazo shirika hili linazo. Pamoja na kufahamu yote, bado tumeamua kuliweka shirika hili katika urasimu mkubwa wa kiserikali wa kupata vibali kutoka wizara ya fedha bila ya sababu za lazima.

Je, serikali imedhamiria kutekeleza ahadi zake katika ujenzi wa nyumba na kuliwezesha shirika kujiendesha kibiashara kama sheria yake inavyolitaka? Kambi ya Upinzani inaitaka serikali itoe ufafanuzi ni lini inatarajia kuanzisha mchakato wa kurekebisha sheria hiyo?

MAMLAKA YA/WAKALA WA KURATIBU BEI ZA PANGO LA NYUMBA


Mheshimiwa Spika,
katika hotuba ya Kambi ya Upinzani kwa mwaka wa fedha 2011/2012 tuliitaka serikali kuanzisha chombo kitakachoweka utaratibu utakaotambulika kisheria ili kiwe kinatoa miongozo ya kudhibiti gharama za kodi za nyumba kwa ujumla wake. Kwa maana nyingine ni kuanzisha mamlaka ya udhibiti itakayoitwa"Real Estate Regulatory Authority". Tunarudia tena kusisitiza ushauri wetu huo.

Mheshimiwa Spika,
sekta hii ambayo imejaa changamoto ambazo kama zikifanyiwa kazi ni dhahiri pato la taifa litaongezeka na pia tatizo la ajira linaloikabili nchi yetu linaweza kupungua kwa kiasi kikubwa kama si kuondoka kabisa. Swali muhimu la kuuliza ni kwa vipi Serikali itabadilidha changamoto kuwa fursa? Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kuangalia kwa makini kuwa mamlaka ya udhibiti ndiyo inayoweza kubadilisha changamoto zilizopo katika sekta hiyo kuwa fursa.

Mheshimiwa Spika, ninawashukuru waheshimiwa wabunge wote kwa kunisikiliza na naomba kuwasilisha.
................................................
Halima James Mdee(Mb)
Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani- Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi.
11.07.2012


[1] Consolidated Holding Corporation, United Republic of Tanzania , Taarifa ya ufuatiliaji wa Mashamba na viwanda vya bidhaa za kilimo, Januari 2012, pg X

[2] The Tanzania Long Term Perspective Plan ( LTPP) 2011/12-25/26 . The Road Map to a Middle Income Country , April 2012, pg 28

[3]Taarifa ya utekelezaji wa Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2010/11 na makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2011/12 kwa kamati ya Kudumu ya Bunge Ya Ardhi, Maliasili na Mazingira , Tarehe 1 Juni ,2011

[4] Majadiliano ya Bunge, Taarifa Rasmi ( Hansard) , Mkutano wa Nne, Kikao cha arobaini na Nane , tarehe 16 Agosti ,2011

[5] Corruption ,Politics and societal Values in Tanzania. An Evaluation of the Mkapa Administration's Anti –Corruption Efforts, Dr Bruce heilman and Dr Lauren Ndumbaro Vol 7 (2002)

[6] Katika kijiji hiki wanakijiji waliporwa ardhi (Heka 3000) na kikundi kinachojiita Mpairo.Ni mgogoro ambao unaendelea kutokota chini kwa chini lakini kwa mujibu wa wananchi unaweza kuzua mauaji kwa sababu unashabihiana na mgogoro uliosababisha mauaji ya kutisha ya tarehe 21/05/2012 kati ya kikundi cha nguvu kazi kinachoendeshwa na Galas Kasonso chini ya kivuli cha baadhi ya wakubwa wilaya ya Mpanda.

[7] Kesi namba CC .204/2011CC.207/2011 NA PI 16/2011. Rejea pia barua toka ofisi ya Mkurugenzi wa mashtaka yenye kumb. Na J/C .110/9/322 kwenda kwa wakulima wa kijiji cha Sibwesa , Kitongoji cha Kabange, unaohusu wananchi kubambikiwa kesi ya mauaji!

[8] Kijiji kilisajiliwa tarehe 1/4/1976 kwa usajili namba AR KJ 26

[9] Kilisajiliwa tarehe 1/4/1976 kwa usajili namba AR. KJ 43
 
Bruce Rastetter ana kasheshe huko USA pia

Atalima mahindi ili kutengeneza Ethanol.
Kampuni yake ya AgriSol Energy inajishughulisha na hilo.
Mahindi ya kutengeneza Ethanol hayafai kula.
Ni modifaidi hayana radha.
Yana sura ya mahindi lakini si mahindi.
Ni raw material ya Ethanol,plastic na cone sugar.
Poleni zake zikichanganyika na mahindi yetu ndiyo mwisho wa ugali as we know
Millionea huko Aiwa,Republican wanamwogopa

Hog, ethanol baron Bruce Rastetter now a Republican kingmaker
Emails show ISU swapped expertise for scholarship funds in AgriSol partnership | Ames Tribune
 
ukitaka kunisaidia hapa niwekee video clip, utakua umenikwamua sana..
manake hii duh, kama kwa ocampo
 
Cha kushangaza kambi ya upinzani haiongeleai ardhi kubwa inayomilikiwa na taasisi za kidini ambayo hairudishwi kupewa wananchi waiendeleze.

Taasii za kidini zinamiliki ardhi kubwa baada ya Serikali Tanzania hii na 90% ya ardhi hiyo haijaendelezwa kwa miaka mingi sana. Kulikoni mnaifumbia macho?
 
Back
Top Bottom