Genge La Wahalifu... Laibuka Zanzibar

X-PASTER

JF-Expert Member
Feb 12, 2007
11,610
1,809
Genge la wahalifu wa kusafirisha binadamu laibuka Zanzibar

Na Salma Said, Zanzibar

GENGE la kihalifu linalodaiwa kusafirisha vijana kutoka Tanzania na kuwapeleka Israel kwa ahadi ya kuwapatia kazi na maisha bora, lakini badala yake kuwatumikisha kwenye shughuli mbalimbali na kuwatelekeza, limeibuka visiwani hapa.


Tayari vijana watano wa Zanzibar wamenusurika kufa baada ya kushambuliwa na askari wa Israel katika mpaka wa Misri wakati wakijaribu kuvuka kuingia Israel.

Mmoja wa vijana hao, Abdul Mohammed aliiambia Mwananchi katika mahojiano maalumu kuwa amekumbana na mazingira hatarishi ambayo hakutegemea kukutana nayo maishani mwake.

Kwa mujibu wa kijana huyo, genge hilo la wahalifu mara nyingi haliwaandai vijana kwamba watatakiwa kuvuka mpaka huo kwa kuruka seng'enge, kutambaa kama wanajeshi na kwamba pia wajihadhari kwa mashambulizi ya askari wa Israel ambao watawazuia kuingia nchini humo.

“Tuliambiwa safari yote itakuwa shwari, lakini mara tulipoingia Cairo (Misri) dalili za safari yenye hatari ilijitokeza kwa sababu watu waliotupokea walikuwa wamesheheni silaha na tuliwekwa kwenye nyumba na kufungiwa... hata kuchungulia nje hatukuruhusiwa kwa kweli ni hatari kubwa,”
Alisema kijana huyo huku akiinamisha kichwa kwa majuto.

Mkasa wa vijana hao unafunua kuwepo kwa genge ambalo linasafirisha watu kuwapeleka Israel kwa kupitia Misri, lakini bila ya kuwaeleza hatari wanayoweza kukabiliana nayo wakiwa njiani zaidi ya kuwadanganya kuwa kila kitu kitakwenda vyema na watapokelewa na askari wa mpakani mwa Israel pamoja na maafisa wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR na watu wa Msalaba Mwekundu (Red Cross).

“Watanzania tulikuwa wengi na walituambia kwamba tutasaidiwa na watu wa Red Cross, lakini kumbe tulipofika huko tukakutana na majeshi ambao wametuzuia kuingia na ndipo hapo tukajipitisha kwa nguvu lakini wengine wakapigwa risasi... sisi tukakimbia na tukasalimika,”
Alisema kijana mmoja kati ya waliosalimika.

Kijana huyo alieleza kwamba nyumba walizowekwa kusubiri safari ya kuvushwa hazina hata vyoo na tulikuwa tunajisaidia nje na kufunika vinyesi vyao kwa mchanga wa jangwani. Chakula wanachopewa mara nyingi ni mikate na fiwi zenye harufu ya kuoza jambo ambalo liliwasababishia maumivu ya tumbo mara kwa mara, alisema.

Kwa upande wa Zanzibar inaelezwa kwamba wanaoongoza katika harakati hizo za kusafirisha vijana wa Kizanzibari ni makampuni ya kitalii ambayo huwatoza vijana hao $ 2,800 za Kimarekani kwa kila mmoja kwa ajili ya safari hiyo kutoka Tanzania hadi Israel.

“Kwa kweli huja na maneno mazuri lakini safari hiyo ni ya hatari sana na unajikuta ukijuta wakati uko njiani na kutaka kurudi kwa kuwa watu walio tusindikiza walituambia hatua itakayo chukuliwa ni kutupiga risasi na kutuacha tuliwe na tai (eagle) jangwani,” alisema Rashad.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Mjini Magharibi, Bakari Khatib Shaaban alisema hana taarifa za genge hilo linalofanya kazi ya kuwasafirisha Watanzania kwa kuwa alisikia taarifa hiyo kupitia vyombo vya habari vya nje.

“Mimi sina taarifa hiyo hapa ofisini kwangu hakuna mtu aliyekuja kuripoti kuhusu madai hayo, lakini kama polisi tutachunguza na kufuatilia kabla ya kutoa taarifa kamili zenye uhakika kwa sababu hilo ni jambo baya katika nchi yetu.”
Alisema Kamanda Bakari akiwa ofisini kwake Madema Mjini hapa.

Rashad Abdallah ni miongoni mwa vijana walionusurika kufa katika safari hiyo anaeleza kwamba katika kundi lao walikuwa watu 40, lakini wanne kati yao walifariki mbele yao wakiwa njiani.

“Mmoja wetu alipigwa risasi; mmoja aliumwa na nyoka; mwingine akafa kwa kiu na mmoja akapukutika tunamuona mbele ya macho yetu akanyooka chini... unajua ni mazingira hatari sana,” alisema huku akitokwa na machozi.
Kabla ya kuvushwa, vijana hao hunyang'anywa hati zao za kusafiria kuvuliwa viatu na kulundikwa kwenye magari ya mizigo ambayo wakati mwingine hushehenezwa mavi ya ng'ombe juu wakati wao wako chini au kufichwa hata katika uvungu wa magari wanayopanda.

“Unajua ukielezewa huwezi kuamini, lakini ni balaa kwa sababu tunawekwa katika magari ya mizigo na ndani ya magari hayo hupakiwa mavi ya ngombe. Sisi tumo chini sasa humo baadhi yetu waliokuwa na roho nyepesi wanakufa, lakini sisi tena ndio Mungu ametuhifadhi mpaka tukaweza kupumua,” alisema.

Walieleza kwamba walipofika mpakani na kuonyeshwa mahala pa kuvuka, huachiwa wao na Mungu wao ili kuvuka mpaka kwa kutumia mbinu za kijeshi mbele ya askari wa Israel, jambo ambalo wengi walishindwa na kujikuta wakikamatwa.

Vijana hao walisema baada ya kupata matatizo hayo walikimbilia katika ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini Misri na kuwaeleza shida waliokumbana nayo na hatimaye balozi aliwasaidia kuwarejesha nyumbani.

Uchunguzi wa Mwananchi umegundua kwamba vijana wa kizanzibari wengi wao wamekuwa wakienda safari hiyo, lakini hii ni mara ya kwanza kuzuka kwa taarifa juu ya hatari ya safari hiyo na ukubwa wa kiwango cha uhalifu kinachoonekana kuhusika na mradi huo.

source: mwananchi
 
Back
Top Bottom