Full Text: Hotuba ya Kambi ya Upinzani Bajeti 2013/2014 iliyosomwa na Freeman Mbowe

Molemo

JF-Expert Member
Sep 24, 2010
14,534
13,225
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Mh. Freeman Mbowe, atatoa hotuba yake leo kwa saa 1 bungeni, muda si mrefu kutokea sasa! Atazungumza vitu muhimu sana vyenye maslahi kwa Watanzania na taifa.

Afisa Habari a Chadema Tumaini Makene yupo bungeni kutuletea kila litakalojiri.Pia tunatajia Makene atatuwekea hotuba kamili muda sio mrefu.

Pia wabunge wa Chadema wamekwishaonya dhidi ya mbinu yoyote ya kukatisha hotuba ya Mbowe wakati akiunguruma.Tayari kuna hofu kuu upande wa serikali kufuatia hotuba hiyo inayosubiriwa kwa hamu na kila mpenda demokrasia nchini.

=========================

HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI OFISI YA WAZIRI MKUU, MHE.FREEMAN AIKAELI MBOWE (MB); KIONGOZI WA UPINZANI BUNGENI KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA 2013/2014

1. UTANGULIZI


Mheshimiwa Spika,
Kufuatia marekebisho kadhaa ya kanuni hususan zinazolenga kwa sasa Utaratibu wa Kutunga Sheria kuhusiana na mambo ya fedha, nasi kama Kambi Rasmi ya Upinzani tutafanya marekebisho katika utaratibu tutakaotumia katika kutoa maoni yetu kwa Serikali.

Kwa muda mrefu, kufuatia utaratibu wa mfumo wa bajeti ulivyokuwa huko nyuma, tulitumia muda mwingi kuishauri serikali namna bora ya kuboresha bajeti na utendaji wake wa kazi. Hata hivyo, kwa bahati mbaya sana, serikali hii imekuwa siyo sikivu vya kutosha hata kama pale ambapo ushauri unaotolewa uko wazi kwa masilahi na mustakabali mwema wa Taifa letu.

Aidha, pale ambapo Serikali imechukua maoni yetu, mara nyingi imekuwa haina ustaarabu wa kutambua, kukiri na kushukuru mchango wa Kambi ya Upinzani, bali mbele ya macho ya umma imeendelea kutoa kebehi kujaribu kuuaminisha umma kuwa vyama vya upinzani havina ufumbuzi mbadala kwa matatizo yanayolikabili Taifa.

Mheshimiwa Spika,
Tatizo kubwa la Serikali inayoongozwa na CCM ni kukosa weledi wa kutekeleza kikamilifu vipaumbele vyake pamoja na kuviainisha kupitia Mpango wake wa miaka 5, bajeti na programu mbalimbali. Hali hii inaweza kutafsiriwa kama uwezo duni wa kusoma alama za nyakati ikiwemo kubuni na kusimamia inachokiamini. Ni dhahiri vilevile unapolazimika kufanya jambo usiloliamini au lisilo kipaumbele chako, bali cha kulazimishwa na mazingira unatekeleza bila kujua undani wake na hatma yake ni kuharibu zaidi.

Mheshimiwa Spika,
Kwa kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu ni mtambuka, Mwaka huu tutajielekeza kuzungumzia mambo makuu machache ambayo sisi tunaamini ni vipaumbele muhimu ambavyo Waziri Mkuu na wasaidizi wake wanapashwa kuja na majibu ya kueleweka kwa Watanzania. Aidha, mengine yatawasilishwa kupitia hotuba zetu mbalimbali katika Wizara husika.

2. TUME YA MABADILIKO YA KATIBA, NA MCHAKATO WA KATIBA MPYA NA MSTAKABALI WA TAIFA


Mheshimiwa Spika,
Tarehe 18 Novemba, 2011 Bunge lako tukufu lilipitisha Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011. Kufuatana malalamiko mengi kuhusu utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa Sheria hiyo na kufuatia vikao kati ya Mheshimiwa Rais na Kamati Maalum ya CHADEMA pamoja na wadau wengine, Sheria hiyo ilifanyiwa marekebisho wakati wa Mkutano wa Sita wa Bunge hili uliofanyika mwezi Februari mwaka 2012.

Marekebisho hayo yalikuwa ni awamu ya kwanza ya awamu tatu za marekebisho ya Sheria hiyo kwa mujibu wa makubaliano yetu na Mheshimiwa Rais. Awamu nyingine mbili za marekebisho zilitarajiwa kukamilika kabla ya mwisho wa mwaka jana, yaani 2012. Hata hivyo, hadi nasoma maoni haya leo hii, Sheria ya Marekebisho ya Katiba haijafanyiwa marekebisho mengine yoyote.

Mheshimiwa Spika,
Mara baada ya marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kupitishwa mwaka jana, Mheshimiwa Rais alifanya uteuzi wa wajumbe na watendaji wakuu wa Tume na Tume yenyewe ilianza kazi mwezi Mei, 2012. Kwa maana hiyo, hadi kufikia leo Tume ya Mabadiliko ya Katiba imeshafanya kazi kwa karibu mwaka mmoja.

Kwa masikitiko makubwa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kulijulisha Bunge lako tukufu kwamba katika kipindi hiki mtiririko wa matukio kadhaa ndani na nje ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba imethibitisha kwamba haina weledi, dhamira au nia ya kusimamia mchakato huru usiofungamana na upande wowote.

Katika mwaka wa kwanza wa mchakato wa upatikanaji Katiba mpya, Tume ya Mabadiliko ya Katiba imethibitisha hofu tuliyokuwa nayo toka mwanzo kwamba lengo la mchakato wa Katiba Mpya uliowekwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ni kuhakikisha kwamba mabadiliko pekee yakayokuwepo ni yale yenye kulinda matakwa ya CCM na Serikali yake au yale pekee yatakayokuwa na Baraka za “Status Quo”.

Mheshimiwa Spika,
Kwanza, Tume haikuweka utaratibu wowote madhubuti wa kutoa elimu kwa wananchi juu ya masuala yote yanayohusu Katiba Mpya ili kuwaandaa wananchi kuchangia maoni yao kwa Tume wakiwa na uelewa wa kutosha. Badala yake, wakati wa mikutano ya Tume ya kupokea maoni ya wananchi, wajumbe wa Tume walipewa jukumu la kuwaeleza wananchi juu ya Katiba Mpya kwa muda usiozidi nusu saa!

Kwa kulinganisha, Tume ya Katiba ya Kenya ilifanya kazi ya kutoa elimu kwa umma kwa nchi nzima kwa muda wa miezi sita kabla ya kuanza kukusanya maoni ya wananchi wa Kenya juu ya Katiba Mpya. Matokeo yake ni kwamba mchakato wa Katiba Mpya wa Kenya umeiletea nchi hiyo Katiba Mpya ya mwaka 2010 ambayo imeanza kudhihirisha ubora wake kwa jinsi ambavyo mambo yatokanayo na Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo wa hivi karibuni yalivyotatuliwa.

Mheshimiwa Spika,
Pili, muda uliowekwa na Tume wa kukusanya maoni ya wananchi ulikuwa mdogo sana ukilinganisha na ukubwa wa nchi yetu na wingi wa Watanzania. Katika Majimbo karibu yote ya uchaguzi Tanzania Bara, Tume iliendesha wastani wa mikutano saba kwa kila jimbo kwa lengo la kukusanya maoni ya wananchi.

Katika mikutano hiyo wananchi walitakiwa kutoa maoni yao kuhusu Katiba Mpya kwa muda wa dakika tano kila mmoja na mikutano yenyewe ilichukua muda wa masaa matatu ikiwa ni pamoja na muda wa kutambulishana wajumbe wa Tume na mambo mengine yaliyo nje ya kuchukua maoni ya wananchi.

Mheshimiwa Spika, matokeo yake ni kwamba kwa mujibu wa maelezo ya Mwenyekiti wa Tume Jaji Joseph Sinde Warioba kwa waandishi habari tarehe 5 Januari mwaka huu, hadi awamu nne za kukusanya maoni ya wananchi zinakamilika tarehe 19 Desemba, 2012, Tume ilikwisha kufanya mikutano 1,776 kwa nchi nzima. Aidha, kwa mujibu wa maelezo ya Mwenyekiti Warioba, hadi kufikia kipindi hicho wananchi wapatao 64,737 walikwishatoa maoni yao kwa kuzungumza wakati wananchi 253,486 walitoa maoni kwa njia ya maandishi, na wengine 16,261 walitumia njia ya “posta, tovuti ya Tume, mitandao ya kijamii na ujumbe mfupi wa simu za mkononi....” Kwa hiyo, kwa mujibu wa taarifa hizi za Mwenyekiti wa Tume, kati ya Watanzania takriban milioni 45, ni Watanzania 334,484 ndio waliotoa maoni juu ya Katiba Mpya hadi kufikia tarehe 4 Januari, 2013. Idadi hii ni sawa na asilimia 0.7 ya Watanzania wote! Na hao ndio waliotoa maoni yao kwa muda wa dakika tano kila mmoja, wakiwamo waheshimiwa Wabunge wa Bunge hili tukufu.

Mheshimiwa Spika, ni wazi, kwa takwimu hizi za Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kwa vyovyote vile, Katiba Mpya itakayotokana na maoni haya haiwezi kuwa Katiba Mpya ya Watanzania wote. Utaratibu wa hovyo namna hii utazaa Katiba Mpya ya hovyo!!! Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba utaratibu huu wa hovyo hauwezi kutupatia Katiba Mpya yenye maridhiano ya kitaifa kwa ajili ya kutatua migogoro mingi ya kisiasa, kijamii na kidini ambayo inaikabili nchi yetu kwa sasa.

Mheshimiwa Spika,
Tatu, licha ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kutangaza kuwa Tume itakuwa huru katika utekelezaji wa majukumu yake, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaona kila dalili za Tume kutokuwa huru au kuutafsiri uhuru vibaya. Kwa mfano, kuna ushahidi kwamba Tume imekuwa na mawasiliano ya karibu na Serikali na Ofisi ya Rais kwa namna ambayo inaashiria Tume kutokuwa huru. Ndio maana katika hotuba yake ya kumaliza mwaka uliopita na kufungua Mwaka Mpya, Rais Jakaya Kikwete alilitangazia taifa ratiba ya kazi za Tume ambayo Tume yenyewe ilikuwa haijawahi kuitoa hadharani.

Katika hotuba yake hiyo, Rais Kikwete alitangaza sio tu kumalizika kwa awamu za kukusanya maoni ya wananchi, bali pia alitangaza ratiba ya Tume kuanza kuchukua maoni ya vyama vya siasa, taasisi nyingine na ‘makundi maalum’, tarehe ya kutolewa kwa Rasimu ya Kwanza ya Katiba Mpya, Mikutano ya Mabaraza ya Katiba na Bunge Maalum la Katiba na hata tarehe ya kura ya maoni na upitishwaji wa kura ya maoni kuihalalisha Katiba Mpya.

Mheshimiwa Spika, Rais asingeweza kufahamu ratiba hii yote bila kupatiwa taarifa ama na Tume yenyewe ama na watendaji au watumishi wake au na wajumbe wa Tume. Mbali na taarifa ya kwisha kwa awamu ya tatu ya zoezi la kukusanya maoni ya wananchi, taarifa hizi hazikuwa zimetolewa hadharani na Tume kabla ya hotuba ya Mwaka Mpya ya Rais Kikwete!

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imetambua siku zote kwamba msemaji rasmi wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ni Mwenyekiti wa Tume Joseph Warioba. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haijawahi kusikia wala kuona mahali popote ambapo Sheria ya Mabadiliko ya Katiba imempa Rais Kikwete jukumu la kuwa msemaji wa Tume. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inahoji kama Rais anaweza kupatiwa taarifa za kina namna hiyo kuhusiana na shughuli za Tume, kuna uhakika gani kwamba yeye au Serikali yake hawatoi kwa Tume maelekezo ya kichinichini juu ya nini cha kufanya, kwa namna gani na kwa wakati gani.

Mheshimiwa Spika,
Nne, wakati Tume ya Mabadiliko ya Katiba ikitoa taarifa za kina juu ya shughuli zake kwa Rais Kikwete na Serikali yake, Tume hiyo hiyo imetangaza wazi wazi kwamba haiwajibiki kwa Bunge kuhusu utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Sheria. Zaidi ya kumtuma Naibu Katibu wa Tume, viongozi wa Tume kama vile Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na wajumbe wa Tume wamekataa kuhudhuria vikao vya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala ili kuieleza Kamati juu ya utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Sheria na Katiba ya Nchi.

Katika hili, Tume imeungwa mkono na Serikali hiyo hiyo inayoelekea kupata taarifa za kina juu ya utekelezaji wa kazi zake! Hii ni licha ya kupatiwa jumla ya shilingi bilioni 33.944 za walipa kodi wa Tanzania zilizoidhinishwa na Bunge katika mwaka wa fedha 2012/2013 kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake. Kwa hiyo, wakati Tume inaharibu mchakato wa Katiba Mpya kama tulivyoonyesha hapa, Bunge – kwa kupitia kwa Kamati yake – limezuiliwa kuhoji shughuli za Tume kwa hoja kwamba Tume iko huru.

Mheshimiwa Spika, hii inaweza kuwa mara ya kwanza kwa chombo cha umma kinachotumia mabilioni ya fedha za umma kilichopewa majukumu ya umma na Sheria iliyotungwa na Bunge hili tukufu kukataa kuwa chini ya usimamizi wa kikatiba wa Bunge (parliamentary oversight)!

Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imesikitishwa sana na kushindwa kwa Kamati husika ya Bunge kudai madaraka yake ya usimamizi yasipuuzwe na Tume na/au Serikali. Udhaifu huu wa Bunge na Kamati unaweza kuligharimu Taifa endapo mchakato wa Katiba Mpya utachakachuliwa na kuliingiza Taifa katika machafuko ya kisiasa, kidini au kijamii.

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe kauli mbele ya Bunge hili tukufu juu ya uwajibikaji wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa matumizi ya mabilioni ya fedha za umma iliyoyaidhinishiwa mwaka jana na inayoyaomba mwaka huu wa fedha.

Mheshimiwa Spika,
Tano, Tume imetengeneza utaratibu wa mabaraza ya kikatiba ambao kwa ushahidi wa mwanzo tu unaonyesha kwamba hayo ni mabaraza ya CCM na sio mabaraza ya katiba ya Watanzania wote. Hili limefanyika kwa kupitia Mwongozo Kuhusu Muundo, Utaratibu wa Kuwapata Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya (Mamlaka za Serikali za Mitaa) na Uendeshaji Wake, uliotolewa na Tume mwezi Februari mwaka huu. Kwa mujibu wa Muundo huu, wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya watachaguliwa na Kamati za Maendeleo za Kata (maarufu kama ‘WDC’) baada ya kuwa wamechaguliwa moja kwa moja na wananchi katika vijiji na mitaa. Wajumbe wa WDC ni Madiwani wa Kata ambao ni Wenyeviti wake, Watendaji wa Kata ambao ni Makatibu na Wenyeviti wa Vijiji au Mitaa.

Mheshimiwa Spika, kwa kufuatana na chaguzi za vijiji na mitaa za mwaka 2009, zaidi ya asilimia 90 ya vijiji na mitaa inaongozwa na wenyeviti ambao ni wanaCCM. Aidha, kutokana na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, zaidi ya asilimia 80 ya Kata zote nchini zinaongozwa na madiwani wa CCM. Hawa ndio waliochagua wajumbe wa Mabaraza ya Wilaya ya Katiba tangu mwanzoni mwa wiki iliyopita. Matokeo yake, kwa taarifa ilizo nazo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kutoka sehemu mbali mbali za nchi yetu, kila mahali wagombea ambao hawakuwa wanaCCM walienguliwa katika ngazi ya uchaguzi wa vijiji au mitaa au wameenguliwa na WDC baada ya kushinda katika ngazi hizo.

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ina ushahidi kwamba viongozi wa kiserikali kama vile Wakuu wa Wilaya na wa Mikoa waliwahamasisha wenyeviti wa vijiji, mitaa na madiwani kuhakikisha kwamba wagombea wote wasiokuwa wa CCM, hasa wa CHADEMA, wanaenguliwa katika chaguzi za vijiji, mitaa au kata. Mfano mzuri ni wa Mkuu wa Wilaya ya Musoma Jackson Msome aliyeitisha mkutano wa wenyeviti wote wa mitaa ya Musoma Mjini na kuwapa maelekezo ya kuhakikisha kwamba watu wasiokuwa wanachama wa CCM hawapati nafasi katika Mabaraza ya Katiba ya Wilaya au Manispaa hiyo.

Mheshimiwa Spika, licha ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kupatiwa maoni ya wadau kwamba utaratibu huo utaharibu mchakato wa Katiba Mpya, Tume ilikataa kata kata kuubadilisha Muundo wa Mabaraza haya. Ni wazi kwamba Tume inafahamu inachokifanya.

Ni wazi vile vile kwamba Tume inafahamu matokeo ya hicho inachokifanya, yaani kuundwa kwa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ambayo ni ya wanaCCM. Na wala haihitaji shahada ya uzamivu kufahamu kwamba Mabaraza ya Katiba ya Wilaya yenye kutawaliwa kwa kiasi hicho na wanaCCM yatatoa maoni ya aina gani juu ya Rasimu ya Katiba Mpya yatakayoijadili. Itakuwa ni Katiba Mpya kwa jina tu, mambo mengine ya msingi yatabaki vile vile. Kwa maneno mengine, itakuwa ni Katiba ile ile, ya watu wale wale, wa chama kile kile.

Mheshimiwa Spika, Uchakachuaji wa mchakato wa Katiba Mpya wa aina hii ndio ulioiingiza Zimbabwe katika machafuko makubwa ya kisiasa toka mwaka 1998 na Kenya mwaka 2007/2008. Kwa utaratibu huu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, inaelekea Serikali ya CCM inaelekea kutotaka kujifunza kutokana na yaliyowakuta jirani zetu wa Kenya na marafiki zetu wa Zimbabwe.

Mheshimiwa Spika,
Sita, Serikali imekataa ama imeshindwa kuheshimu makubaliano iliyofikia na wadau mbali mbali ikiwemo CHADEMA, kufanya marekebisho zaidi ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Kwa sababu hiyo, bado haijulikani wajumbe mia moja na sitini na sita watakaotokana na taasisi mbali mbali zilizotajwa na Sheria hiyo watateuliwa kwa utaratibu gani na nani atakayefanya uteuzi huo.

Vile vile, bado hakuna muafaka juu ya uhalali wa idadi kubwa ya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kutoka Zanzibar kushiriki katika mjadala wa Katiba Mpya kwenye masuala yasiyokuwa ya Muungano ya Tanzania Bara wakati hakuna mjumbe hata mmoja wa Tanzania Bara anayeweza kushiriki katika mijadala ya kikatiba inayohusu masuala ya Zanzibar yasiyokuwa Mambo ya Muungano.

Zaidi ya hayo, bado hakuna majibu yanayotosheleza yanayompa Rais mamlaka ya kuliitisha upya Bunge Maalum la Katiba na kulielekeza ‘kuboresha’ masharti ya Katiba Mpya mara baada ya Bunge hilo kuipitisha. Aidha, haijulikani ni uhalali upi wa kisheria na kikatiba utakaoiruhusu Tume ya Taifa ya Uchaguzi kusimamia na kuendesha kura ya maoni ya kuhalalisha Katiba Mpya kwa sababu Katiba na Sheria za Uchaguzi za sasa hazitambui wala kuweka utaratibu wa kuendesha kura ya maoni.

Mheshimiwa Spika, kushindwa kwa Serikali kuleta Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ili kufanya marekebisho katika maeneo tajwa ni ushahidi wa wazi kwamba Serikali ya CCM haina nia ya dhati na dhamira safi ya kuhakikisha Tanzania inapata Katiba Mpya inayoistahili.

Aidha, si nia ya CHADEMA kuendelea kushiriki na kubariki mchakato huu kama ulivyo sasa kwani ishara zote ziko wazi kuwa Katiba inayokusudiwa ni ile tu itakayokidhi matakwa ya Wana- CCM na Washirika wake na hivyo kutokutimiza azma ya kuwa na Katiba itakayoponya majeraha mbalimbali na kurejesha uzalendo, mshikamano na upendo wa dhati miongoni mwa Watanzania na kisha mfumo wa Utawala utakaokidhi mahitaji ya wakati.

Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA inatangaza rasmi kwamba: CHADEMA itajitoa ushiriki wake katika mchakato wa Katiba Mpya endapo mambo yafuatayo hayatapatiwa ufumbuzi hadi kufikia mwisho wa mwezi huu, yaani tarehe 30 Aprili, 2013:

  • Kufutwa kwa uteuzi/uchaguzi wa wajumbe wa mabaraza ya wilaya ya Katiba uliofanywa na Kamati za Maendeleo za Kata, na badala yake wajumbe wa mabaraza ya katiba ya wilaya wachaguliwe moja kwa moja na wananchi wa Kata husika bila kuchujwa na WDC;
  • Serikali ilete mbele ya Bunge hili tukufu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba yatayofanyia maeneo yafuatayo marekebisho:
    • Vifungu vyote vinavyohusu uwakilishi katika Bunge Maalum la Katiba wa taasisi zilizoainishwa katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba;
    • Vifungu vyote vinavyohusu ushirikishi wa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kutoka Zanzibar katika mijadala inayohusu mambo yasiyokuwa ya muungano ya Tanzania Bara;
    • Vifungu vyote vinavyohusu mamlaka ya Rais kuitisha tena Bunge Maalum la Katiba baada ya Bunge hilo kuwa limeshapitisha Rasimu ya Katiba Mpya kwa lengo la kufanya marekebisho katika Rasimu kabla haijapelekwa kwenye kura ya maoni;
    • Vifungu vyote vinavyohusu mamlaka ya kikatiba nay a kisheria yatakayoiwezesha Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuendesha na kusimamia kura ya maoni;

3. ANGUKO LA ELIMU TANZANIA: ANGAMIZO LA KIZAZI NA JANGA LA TAIFA.


Mheshimiwa Spika,
Nianze kuzungumzia umuhimu wa elimu kwa kumnukuu Rais wa 55 wa Marekani, John F.Kennedy (1917 – 1963);
“Our progress as a nation can be no swifter than our progress in education. The human mind is our fundamental resource”

Mheshimiwa Spika,
Siku za karibuni kumekuwepo mjadala mzito sana kuhusiana na hali ya elimu nchini. Pamekuwepo na malalamiko mengi sana yakiwemo yaliyomtaka Waziri wa Elimu Mhe. Shukuru Kawambwa na Naibu wake Mhe Phillip Mulugo wajiuzulu kama ishara ya uwajibikaji wa kisiasa. Ni dhahiri kuwa elimu yetu kama Taifa imeporomoka kwa kiasi kikubwa cha sasa kuhatarisha mustakabali wetu kama Taifa.

Mheshimiwa Spika, ni mwaka mmoja tu umepita tangu Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA itoe angalizo kali kwa Serikali juu ya kasi kubwa ya kuporokoka kwa Elimu ya Tanzania na hivyo kuitaka Serikali kuchukua hatua madhubuti ili kuliepusha Taifa na balaa hilo. Hata hivyo, Serikali hii ya CCM imeendelea kupuuza ushauri mzuri inayopewa bure na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na matokeo yake ni kwamba anguko la mwaka huu ni kubwa kuliko maanguko yote yaliyowahi kutokea katika Historia ya Tanzania ambapo asilimia 60.6 (240,903) ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kidato cha nne wamepata daraja sifuri na wengine asilimia 26.02 (103,327) daraja la nne. Jumla ya kufeli huku ni zaidi ya asilimia 86.62 au sawa na

Mheshimiwa Spika, kufuatia kufeli huku kwa kutisha kwa wahitimu wa kidato cha nne mwaka 2012, wadau wengi walitaka baadhi ya viongozi wa sekta ya elimu akiwemo waziri kuwajibika. Ni bahati mbaya sana kuwa Waziri Mkuu ni mmoja wapo wa viongozi Wakuu aliyestahili kuchukua hatua za kuwawajibisha wahusika lakini hakufanya hivyo. Badala yake, akakimbilia kuunda tume ya uchunguzi, ilhali yeye mwenyewe Waziri Mkuu, Waziri wake wa elimu na serikali yake yote ikijua fika nini kinasababisha kuporomoka kwa elimu yetu. Yumkini, kama kweli serikali hadi leo haijui sababu ya kuporomoka kwa elimu yetu, basi haina tena sifa wala weledi wa kusimamia siyo tu elimu, bali maisha ya kila siku ya Watanzania.

Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa kufeli huku hakuwezi kuchukuliwa kama bahati mbaya hasa ikiwekwa maanani kuwa mserereko wa watoto wetu kufeli umeshika kasi chini ya utawala wa Serikali ya awamu ya nne hasa kuanzia mwaka 2007.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2007, ufaulu wa vijana wetu wa kidato cha nne ilikuwa (90.3%), 2008 (83.6%), 2009 (72.5%) na 2010 (50.4%). Kufuatia mserereko huu wa kufeli, serikali iliunda timu iliyoshirikisha wataalam kadhaa kubaini chanzo chake na tiba ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu. Timu hii iliyokuwa chini ya Uenyekiti wa Bw. Francis M. Liboy wa TAMISEMI ilikamilisha ripoti yake mwaka 2011 na kutoa mapendekezo kadhaa kwa serikali. Waziri wa Elimu Mhe. Shukuru Kawambwa anaijua ripoti hii kwani ndiye aliyeandika dibaji yake. (Angalia kiambatanisho A)

Mheshimiwa Spika, mbali na ushauri wetu wa mara kwa mara, serikali hii imebeza kwa nguvu zote juhudi mbalimbali zinazofanywa na wadau wengine wenye kuumizwa na kusikitishwa na kuporomoka huku kwa elimu. Watanzania ni mashahidi namna katika Mkutano wa Kumi wa Bunge, hoja binafsi ya Mheshimiwa James Mbatia (Mb) kuhusu udhaifu ulioko katika sekta ya elimu ilivyochukuliwa kimzaha na kutolewa majibu mepesi na Serikali kinyume na kanuni za bunge na hatimaye kuyazima maazimio ya bunge ya kuinusuru elimu ya Tanzania yaliyokuwa yamependekezwa katika hoja hiyo. Ni katika mkutano huohuo wa Bunge ambapo hoja binafsi ya Mheshimiwa Joshua Nassari (Mb) kuhusu Baraza la Mitihani linavyoathiri elimu ya Tanzania iliondolewa katika orodha ya shughuli za mkutano wa kumi wa Bunge bila ridhaa ya mtoa hoja kinyume na kanuni ya 58(5).

Mheshimiwa Spika, kitendo cha Serikali ya CCM chini ya mwavuli wa wingi wa wabunge wake bungeni, cha kuzivuruga hoja hizi na hivyo kusababisha maazimio ya bunge juu ya hoja hizi kutotekelezwa ni udhaifu mkubwa sana kwa chama kinacho tawala cha CCM na Serikali yake na ni ushahidi uliokamilika kwamba Elimu kwao sio kipaumbele cha taifa.

Mheshimiwa Spika, Serikali ambayo Elimu sio kipaumbele chake, haiwafai Watanzania kwa karne hii. Kuendelea kuukumbatia utawala na aina hii ni kukaribisha maafa yasiyoepukika kwa Taifa. Mbali na kulisababishia Taifa hili aibu kubwa mbele ya majirani zetu na jamii ya kimataifa kwa vijana walio wengi wa Kitanzania kuonekana kuwa na elimu ya mashaka na isiyoweza kuhimili ushindani wa soko la ajira, ubovu wetu wa elimu umedumaza uwezo wetu wa ndani wa kusimamia rasilimali za Taifa, Aidha kambi Rasmi ya Upinzani inawapa angalizo wananchi wote wa Tanzania kwamba haya yote yanatokea kwa kuwa Serikali ya CCM haijaiweka Elimu kuwa kipaumbele cha taifa na kwamba umefika wakati wa kufanya mabadiliko makubwa ya mfumo wa utawala kwa kuchagua chama chenye nia ya dhati ya kuleta mabadilko kitakachounda Serikali inayojali elimu ya watoto wao na bila shaka chama hicho hakiwezi kuwa CCM tena.

Mheshimiwa Spika, Taifa kupitia hotuba hii linataka kujua Serikali ina nini cha kusema kuhusiana na utafiti huu iliofanya mwaka 2011, imetekeleza mangapi kati ya mapendekezo 27 yaliyotolewa. Aidha ni kwa nini imeunda tume nyingine kwa kutumia fedha za walipa kodi wa nchi hii ingali ripoti nyingine inayohusu somo hilo hilo ikiwa mkononi.

3.1. UNYANYAPAA WA FIKRA VYUO VIKUU


Mheshimiwa Spika, pamoja na nia njema ya katiba ya nchi yetu kuheshimu haki ya uhuru wa mawazo kama ilivyowekwa bayana katika Ibara ya 18(a) na Ibara ya 20(1) kwa kutoa uhuru wa mtu kushirikiana na wengine, kumekuwepo na propaganda mbalimbali hasa kwenye taasisi za elimu ya juu, zenye kuminya nafasi na uhuru wa vyama vya upinzani kuendesha shughuli zake kwa usawa, uwazi na kwa haki katika ngazi ya elimu ya juu kama ambavyo chama tawala kimejiwekea na kujitengenezea mazingira hayo.

Mheshimiwa Spika, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisema hivi: "Lakini kutoa uongozi maana yake siyo kuwanyang'anya watu wenyewe mamlaka yao. Watu lazima wafanye uamuzi wao wenyewe kuhusu maisha yao ya baadae kwa kufuata njia za demokrasia. Uongozi hauwezi kuchukua nafasi ya demokrasi; uongozi lazima uwe sehemu ya demokrasi"

Mheshimiwa Spika, tafakuri ya nukuu hii imekuja wakati ambao ushiriki wa wanafunzi wa elimu ya juu katika siasa unaonekana kulemea upande moja tu wa kukipendelea na kukipa uwezo chama tawala katika shughuli zake kwenye taasisi hizo. CCM wamefikiri na kuamua kuanzisha mkoa maalumu kwa sasa wakitambua kuwa vyuo (hasa vyuo vikuu) haviruhusiwi kuendesha shughuli za siasa vyuoni, kama ilivyo majeshi, makanisa au misikiti na ili kuthibitisha hilo wameelekeza pia shughuli za mkoa maalumu ulioanzishwa zifanyike nje ya chuo. Lakini tujiulize na kutafakari zaidi kuhusu mshindo (impact) wa shughuli za mkoa maalumu wa kisiasa ndani ya himaya za vyuo vikuu na elimu ya juu nchini.

Mheshimiwa Spika, ni ngumu kuamini kuwa shughuli za siasa vyuoni, ambazo Tanzania Commission of University Act imeweka bayana kuwa ni kosa, zitaweza kudhibitiwa ikiwa vyama vingine vinajiwekea uhalali na mazingira ya kuingiza wanavyuo kwenye siasa, jambo ambalo udhibiti wake ni mgumu kwa mamlaka husika hasa vyuoni kwa kuwa wanavyuo hufanya vikao vya siasa kwa siri, na kwa nyakati ambazo uongozi wa vyuo hauna taarifa.

Mheshimiwa Spika, kwa uangalifu mkubwa, ningependa kutoa angalizo kuwa, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haitokubali unyanyapaa wa fikra wa aina yoyote utakaoendana na kujenga matabaka kutokana na utofauti wa mitazamo baina ya jamii ya wasomi kwa kuwa, kutoka taasisi mbalimbali za elimu ya juu , chimbuko la viongozi mahiri wa nchi hii pamoja na nchi nyingine mbalimbali duniani limechipukia. Kambi Rasmi ya Upinzani, itaendelea na juhudi zake za kuhakikisha kuwa taifa kwa kupitia wanafunzi wa elimu ya juu, wanapata fursa mbalimbali za kuikomboa jamii ya kitanzania ambayo inadumazwa kwa unyanyapaa wa fikra.

Mheshimiwa Spika, njia pekee ya kufuta unyanyapaa wa fikra kwa vijana waliopo kwenye elimu ya juu ni kwa Serikali kurejesha rasmi na kuruhusu uwepo wa siasa katika elimu ya juu na vyuo vikuu vyote nchini kama shughuli ambazo ni nje ya masomo ili kusaidia kujenga uwanja wa demokrasia katika serikali za vyuo na vile vile itasaidia katika kuweka mazingira ambapo wasomi wetu wanaanza kujifunza mbinu na utendaji wa kisiasa katika mazingira ya elimu ili waweze kujifunza kuishi pamoja, kupingana kwa hoja na kujua jinsi ya kuvumiliana katika mazingira ya tofauti mbalimbali za kiitikadi, imani, na mtazamo kama ilivyoainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CHADEMA ya mwaka 2010. Hapa nikisisitiza maneno ya baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere juu ya kuboresha maisha ya Watanzania:
"Tukiwasaidia watu wa Tanzania kuendelea, ndiyo tunaiendeleza Tanzania. Maana Tanzania Ni ya Watanzania Na Watanzania Ni wote, Hakuna mtu mwenye haki ya kusema "Mimi ndiyo watu". Wala hakuna Mtanzania mwenye haki ya kusema " Najua linalowafaa watanzania na wengine lazima wafuate".
INAENDELEA....
 

Attachments

  • Hotuba_April11-2013.pdf
    421 KB · Views: 932
Inaendelea hapa...

3.2 BODI YA MIKOPO YA ELIMU YA JUU

Mheshimiwa Spika, lengo la kuanzishwa kwa bodi ya mikopo ya wanafunzi wa elimu wa juu ni katika kusaidiakupunguza maumivu ya wazazi na walezi wa kitanzania katika kuhakikishsa vijana wetu wanapata elimu ya juu kwa kusaidiana na taasisi hii ya Serikali (HELSB), kwa kugawa mikopo kwa waombaji wenye vigezo sahihi na kuwapa mikopo kwa viwango vya madaraja ,balimbali ya uhitaji.

Mheshimiwa Spika,
Vigezo ambavyo vimekua vikitumika katika utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, vimekua vikilalamikiwa. Baadhi ya wanufaika wa mikopo hii, wamejikuta wakipewa asilimia chache huku wakiwa wametoka katika familia za kifukara ambazo hazina uwezo wa kuendesha maisha yao. Familia nyingi hazina uwezo hata wa kuhimili mlo mmoja kwa siku, je mzigo wa kuwasomesha watoto na vijana wao ngazi ya elimu ya juu nani ataubeba? Kutokana na udhaifu huu, vijana wameanza kujigawa katika matabaka ya 'wao'(matajiri na wenye nazo) na 'sisi'(masikini, wasionacho) na wamefikia mahali wananukuu maandiko ya dini kuwa "mwenye nacho huongezewa, asiye nacho hupokonywa hata kile kidogo walicho nacho".

Mheshimiwa Spika, Malalamiko juu ya bodi ya mikopo ya elimu ya juu yameendelea kuwa mengi, huku waombaji wakilalamikia mlolongo wa taratibu zilizowekwa ili muombaji aweze kufanikisha usajili wake katika bodi. Malalamiko haya yameendana sambamba na utaratibu mbovu wa utunzaji wa kumbukumbu za watu katika mfumo mzima wa elimu Tanzania ambao unajenga urasimu mgumu katika kupata taarifa za mwombaji na hivyo waombaji kulazimika kujaza taarifa upya kila mwaka mpya wa masomo unapoanza.

Mheshimiwa Spika, Bodi ya mikopo iliingia gharama ya kununua mfumo utakaotumika katika kuchambua viwango vya ukopeshaji kwa wanafunzi , kutoka kwa kampuni ya nchini Afrika Kusini ya ADBSC kwa gharama za dola za kimarekani shilingi 188,000 na marekebisho ya mtambo huu yaliigharimu bodi kiasi cha dola za kimarekani 42,000. Mfumo huu ulitarajiwa kupunguza malalamiko ya waombaji na badala yake malalamiko yanaongezeka kila kukicha.

Mheshimiwa Spika, Ongezeko la malalamiko mbalimbali juu ya ucheleweshaji wa mikopo kwa wanafunzi waliopo vyuoni hali ambayo imekua ikisababisha migomo ya mara kwa mara katika taasisi hizo nalo limekua tatizo lisiloisha. Na tumeshuhudia migomo hiyo ikiambatana na kusimamishwa ama kufukuzwa kwa wanavyuo, hali ambayo inajenga kizazi chenye hofu hasa inapokuja katika kutetea haki zao za msingi.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kifungu cha 19 (1) cha sheria No. 9 iliyoanzisha Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, ni wajibu wa kila mtu aliyenufaika na mikopo ya elimu ya juu kurejesha mkopo serikalini kupitia Bodi ya mikopo. Pamoja na changamoto ya urejeshwaji wa mikopo kwa walionufaika, bodi haijafanya kazi ya kutosha katika kufuatilia na kujua kuhusu wanufaika wa mikopo hiyo (tracking system).

Mheshimiwa Spika,ni dhahiri kuwa bodi ya mikopo haijaweka utaratibu na mfumo sahihi wa kuwafuatilia wadeni wake, na hivyo kuna asilimia kubwa ya wanufaika wa mikopo hiyo ambao wako makazini na wana ajira, lakini mpaka leo hawajawahi kukatwa marejesho ya mikopo wala kufuatiliwa na bodi kwa ajili ya taratibu za kuwaingiza katika mfumo wa marejesho.

Mheshimiwa Spika, n
i wazi kuwa kumekuwa na ubabaishaji mkubwa si katika marejesho tu, hata katika utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu. Pamoja na ushauri ambao Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ulitoa kwa Serikali katika uwasilishaji wa hotuba ya mwaka 2012/2013 kuanzisha na kutumia mfumo wa urejeshaji mikopo kwa kutumia technolojia ya kibenki kupitia mitandao ya simu kama M-PESA,TIGO PESA, Airtel Money, Z-Pesa, n.k, Serikali na bodi ya mikopo inaonekana kutofuata ushauri huu na hivyo kuendelea kuwanyima fursa wahitaji wa mikopo.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni inaitaka wizara husika pamoja na bodi ya mikopo kutoa maelezo juu ya utekelezaji wa mapendekezo haya, kama wamefanya tathmini juu ya uanzishwaji wa mfumo huu, faida na hasara zake na kama la! hawajafanya tathmini, wizara husika itoe kauli katika mkutano huu wa bunge, juu ya njia mbadala na mfumo utakaohakikisha wanufaika wanapata uraisi katika urejeshaji wa makato ya mikopo yao.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani, inaendelea kusisitiza juu ya utekelezaji wa mapendekezo yake, yaliyopo katika ilani ya CHADEMA ya kuivunja Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kutokana na uendeshaji mbovu, mfumo wake mbovu wa kisheria, na uongozi ambao umeshindwa kufanya elimu ya juu ipatikane kwa kila kijana na ambayo kutokana na uongozi usiofaa imeshindwa kukusanya madeni toka kwa wakopaji.

3.3 HATIMA YA WATOTO WANAOSHINDWA KUENDELEA NA MASOMO YA SEKONDARI BAADA YA KUMALIZA ELIMU YA MSINGI


Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa tafiti mbalimbali, watoto na vijana wa Kitanzania walio chini ya umri wa miaka 18 ambao wamefeli darasa la saba na au kidato cha nne, kwa sasa ni wastani wa watoto 800,000 kwa sasa. Kwa wengi wa watoto hawa ambao wengi hutoka familia masikini, hawana uwezo wa kujiendeleza na hawana sifa za kuajiriwa ikiwa ni pamoja na umri mdogo. Kundi hili ni kubwa na linakuwa kwa kasi.

Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha miaka 51 ya Uhuru, Serikali haijatengeneza sera yoyote au sheria ya kusaidia kundi hili kubwa ili liweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi ili waweze kujikimu wao wenyewe na kuchangia katika pato la taifa. Kundi hili lililo hazina kubwa ya nguvukazi ya Taifa letu siku za usoni limeachwa solemba huku likipewa majina ya kebehi ya kila aina ikiwemo wazururaji, vibaka, machinga nk.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza mbele ya Bunge hili, kwamba inampango gani wa kupunguza idadi hii ya watoto wanaobaki mitaani bila shughuli rasmi ya kufanya? Pili kwa wale ambao imeshindikana kabisa kuendelea na masomo, kuna mpango gani wa kisera wa kuweza kuwasaidia ili waweze kushiriki katika shughuli rasmi za kiuchumi ili kulinusuru taifa kuondokana na umasikini uliokithiri?

4. DEMOKRASIA, UTAWALA BORA NA HAKI ZA BINADAMU

4.1 DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA NA CHAGUZI ZA KIDEMOKRASIA NCHINI.



Mheshimiwa Spika, chaguzi huru na za haki ni kipimo muhimu cha demokrasia ya kweli. Kwa kutambua umuhimu huu katika chaguzi na hatimaye katika kuongoza nchi, ibara ya 5(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa haki ya kupiga kura kwa kila raia wa Tanzania aliyetimiza umri wa miaka kumi na minane.

Mheshimiwa Spika, ili kuweka utaratibu mzuri wa kila raia wa Tanzania mwenye sifa ya kupiga kura aweze kupiga kura, ibara ya 5(3) (a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa fursa kwa Bunge kutunga sheria ya Uchaguzi ambayo pamoja na mambo mengine, itaanzisha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kuweka utaratibu wa kurekebisha yaliyomo katika daftari hili.

Mheshimiwa Spika, Ni vyema kwamba Daftari la Kudumu la Wapiga kura lipo, lakini ni bahati mbaya sana pia kwamba utaratibu wa kurekebisha au kuboresha yaliyomo katika daftari hilo hauendi sawia na haki ya raia kupiga kura na mahitaji makubwa ya kukuza demokrasia katika chaguzi hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, mara kadhaa nimemuuliza Waziri Mkuu mbele ya Bunge hili juu ya mkakati wa Serikali kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Wakati wote majibu yamekuwa ni mepesi na yasiyokidhi hitaji hili muhimu la Kikatiba. (Tazama Taarifa Rasmi za Bunge (Hansard) za tarehe 19 Aprili, 2012 na 8 Novemba, 2012).

Mheshimiwa Spika, Waziri Mkuu akijibu swali langu la papo kwa papo juu ya Maboresho ya Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, katika Mkutano wa Tisa wa Bunge, tarehe 8 Novemba, 2012, alisema kwamba mfumo uliopo wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ni mzuri. Jambo hili linaibua mashaka makubwa juu ya utayari wa Serikali kulinda haki ya mwananchi ya kupiga kura kama ilivyotolewa na Katiba ya Nchi, kwa kuwa kumekuwa na malalamiko mengi kutokana na wanachi kukosa haki ya kupiga kura kutokana na Daftari hilo kutofanyiwa marekebisho. Aidha mtazamo huo wa Waziri Mkuu, hautoi fursa ya kulifanyia maboresho Daftari la Kudumu la Wapiga kura kwa wakati; na kwa maana hiyo haki ya kupiga kura na demokrasia ya uchaguzi katika Taifa hili vipo katika hatari ya kupotezwa au kupatikana kwa hisani ya watawala na siyo haki ya kikatiba.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tangu uchaguzi mkuu wa 2010, kumefanyika chaguzi ndogo mbili za Ubunge katika Majimbo ya Igunga Tabora na Arumeru Mashariki mkoani Arusha. Aidha, kata kadhaa zimerudia chaguzi nchini kwa sababu mbalimbali. Katika chaguzi hizi, daftari la Kudumu la Wapigakura halikufanyiwa marekebisho na hivyo kuwanyima wananchi wengi waliokuwa na sifa ya kuandikishwa na kupiga kura haki ya kushiriki katika chaguzi hizo.

Mheshimiwa Spika, Ni kilio cha muda mrefu ndani ya nchi hii kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), haiko huru na inafanyakazi zake kwa shinikizo la viongozi waliopo madarakani. Kilio hiki kimethibitishwa na Tume yenyewe pale walipokutana na Tume ya marekebisho ya Katiba wakati walipotoa maoni yao.

Mheshimiwa Spika, kuna mchakato wa maandalizi ya siri unaoendeshwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) wa kuandaa utambuzi wa wapiga kura kwa kutumia mfumo wa "biometric" kwa maana ya kumtambua mpiga kura kwa alama za mwili kama alama za vidole na au mboni ya jicho kama sehemu ya maandalizi ya Uchagizi Mkuu ujao wa 2015. Kwa mujibu wa taarifa tulizo nazo, tayari Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeshaanza maandalizi mengi ya msingi bila hata vyama vya siasa kujua

Aidha, mchakato huu unaofanywa kwa siri kubwa na unaokisiwa kutumia zaidi ya dola za kimarekani million 200 tayari umeanza kutafutiwa fedha.

Mheshimiwa Spika, teknologia hii kwa siku za karibuni imetumika katika chaguzi nchini Ghana na Kenya. Kote huko, ilifeli na chupuchupu ingeyaingiza mataifa hayo katika vurugu kubwa za uchaguzi. Mataifa haya yalilazimika kurudia mfumo wa upigaji na uhesabuji kura "manually" hali iliyosababisha hofu kubwa.

Mheshimiwa Spika, Si kwamba Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA haiafiki matumizi ya teknologia mpya kurahisisha na kuboresha mfumo mzima wa uchaguzi katika nchi yetu, bali inatambua athari kubwa zinazowezekana siku za usoni kama zoezi hili lililo "sensitive" halitafanywa katika misingi ya uwazi na ushirikishwaji wadau muhimu kama vyama vya siasa katika hatua zote la tangu awali kabisa. Ni kwa sababu hizi basi, tunaitaka Serikali kutoa maelezo ya kina kuwa ni sheria gani iliyotungwa na bunge inayoruhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa mfumo huu na ni bajeti ipi inatumika kutekeleza mpango huo? Na ni kwa nini mpango huo unafanyiaka kwa siri?

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali haioneshi dhamira ya dhati ya kusukuma mchakato wa kuleta marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi ili kuondoa ukomo wa kuboresha Daftari la Kudumu la Wapigakura (wa mara mbili kwa kipindi cha miaka mitano) na badala yake daftari hilo liwe huru wakati wote kuandikisha wapigakura wapya wanaotimiza masharti ya kupigakura na kuingiza marekebisho ya taarifa za wapigakura wengine, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kwa kusikiliza na kuzingatia sauti na utashi wa watu na uzingativu wa kutosha wa dalili za nyakati na mazingira ya nchi pamoja na kuheshimu maono na falsafa za waasisi wa taifa letu, inakusudia kuleta Hoja Binafsi kuhusu marekebisho ya sheria zote za uchaguzi nchini ili kuinusuru haki ya kikatiba ya raia wa Tanzania kushiriki kikamilifu katika chaguzi tena zilizo huru na za haki.

4.2 MFUMO WA KUKABIDHIANA MADARAKA KATIKA OFISI ZA VIONGOZI WAKUU WA SERIKALI.

Mheshimiwa Spika,
Pamoja na Taifa kuwa katika mchakato wa kuandika upya Katiba ya nchi yetu, hakuna "guarantee" kuwa katika hiyo itakuwa tayari kwa ukamilifu wake kabla ya uchaguzi mkuu wa 2015. Hivyo basi ni bora hatua zote za urekebishaji wa viashiria vya mvurugano kuendelea kushughulikiwa sambamba na mchakato wa Katiba Mpya.

Mheshimiwa Spika, Ni jambo la kiungwana kwa viongozi wanaoondoka madarakani kukabidhi madaraka na ofisi kwa wale watakaoingia madarakani na katika ofisi hizo.

Mheshimiwa Spika, pamoja na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoa muda wa siku saba, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano Ibara ya 42(1) kuwa "Rais Mteule atashika madaraka ya Rais mapema iwezekanavyo baada ya kutangazwa kwamba amechaguliwa kuwa Rais, lakini kwa hali yoyote itabidi ashike madaraka kabla ya kupita siku saba". Lakini utaratibu huo haujatungiwa sheria na ni utaratibu ambao ulikuwepo tangu enzi za chama kimoja na kwa misingi hiyo haukidhi mahitaji ya kipindi hiki cha vyama vingi endapo itatokea kwamba mgombea urais kutoka chama cha upinzani atashinda uchaguzi na kuapishwa kushika madaraka ya Urais.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa nchi mbalimbali duniani zimeanzisha sheria ya kipindi maalumu cha mpito cha kukabidhiana madaraka ya Urais baada ya uchaguzi mkuu wa Rais na wabunge,
Na kwa kuwa sheria kama hii huelekeza mtu atakayesimamia rasilimali za nchi ili kudhibiti ubadhirifu mkubwa ambao hufanyika katika kipindi hiki cha mpito;
Na kwa kuwa nchi yetu imeridhia kipindi cha uongozi wa u-rais wenye ukomo wa miaka kumi;
Na kwa kuwa mfumo wetu wa Siasa ya vyama vingi sasa umekomaa na hivyo kutoa nafasi ya uwezekano wa chama cha upinzani kutwaa madaraka ya Dola;
Hivyo basi ni jambo la busara sana kutunga sheria ya Kipindi cha mpito chenye kutoa muda wa kutosha na utaratibu utakaotumika kuruhusu kukabidhiana madaraka ya urais na serikali (Presidential Transition Act) kutoka utawala mmoja kwenda mwingine ili kuepusha migongano au hofu ya kutojua kitakachotokea.

Mheshimiwa Spika,
ni azma ya Kambi Rasmi ya Upinzani, CHADEMA kuleta hoja binafsi Bungeni ili Bunge liazimie kutungwa kwa sheria hii muhimu sana kwa Taifa letu siku za usoni.

4.3 UCHOCHEZI WA KISIASA: UDINI, UKABILA NA "UGAIDI"


Mheshimiwa Spika, nchi yetu kwa miaka mingi imesifika sana duniani kutokana na tunu yake ya "Amani na Utulivu." Hata hivyo, tunu hii ya amani na utulivu iko mashakani baada ya kuibuka kwa matukio kadhaa ya uvunjifu wa amani yenye sura ya udini.

Mheshimiwa Spika, matukio hayo ni pamoja na mgogoro kati ya waislamu na wakristo huko Geita, Tunduma na kwingineko juu ya uhalali wa kuchinja ambapo watu kadhaa walijeruhiwa na wengine kuuwawa. Matukio mengine ni kushambuliwa kwa viongozi wa dini akiwemo Katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Fadhil Soraga ambaye alimwagiwa Tindikali na watu wasiojulikana, Padre Ambrose Mkenda ambaye alinusurika kifo baada ya kupigwa risasa na kuvunjwa taya na Padre Evaristi Mushi ambaye aliuwawa kwa kupigwa risasi tarehe 17Februari, 2013.

Mheshimiwa Spika,
matukio haya ya kihalifu yenye sura ya kidini yalijumuisha pia kuchomwa moto nyumba za ibada hususan makanisa huko Zanzibar na Dar es Salaam na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali. Aidha matukio haya yalizua hofu kubwa miongoni mwa wananchi kwa kuwa hawakuwa na uhakika wa usalama wao.

Mheshimiwa Spika, mengi yamesemwa, mengi yameandikwa, mengi yamehubiriwa kwenye nyumba za ibada na vyombo vya habari. Lakini jambo moja ambalo halijasemwa wazi na ambalo tumekuwa na kigugumizi kulisemea, ni hili: Kwamba kwa kiasi kikubwa mgogoro huu wa kidini nchini, hasa mgogoro wa uchinjaji wa kitoweo, umechochewa na baadhi ya wanasiasa wa kutoka chama tawala.

Mheshimiwa Spika, Madhehebu ya dini yamekuwapo kwa muda mrefu nchini na katika kipindi chote hicho, hakujawahi kutokea mgogoro wa uchinjaji wa nyama kwa minajili ya kitoweo. Pamoja na kwamba Kambi Rasmi ya upinzani Bungeni, haina nia ya kutoa hukumu juu ya matukio haya, lakini ni vema Watanzania wakaelewa kwamba kwa vyovyote iwavyo, serikali ya CCM haiwezi kukwepa lawama katika kulikuza tatizo hili; na kwamba imeshindwa kujua wajibu wake wa msingi wa kuilinda nchi na raia wake na kuhakikisha jamii yote inaishi kwa upendo na kuvumiliana. Uhalifu wowote unaotokea dhidi ya nchi na raia ni dalili ya wazi kabisa ya udhaifu wa Serikali iliyoko madarakani katika kutimiza wajibu wake. Utawala unaotumia dini kuwagawa wananchi wake na kutafuta ushindi

Mheshimiwa Spika, uchochezi na propaganda za kidini na kikabila vilichagizwa kasi na CCM mara baada ya kuanza mfumo wa vyama vingi vya siasa kama mojawapo ya turufu yake ya kukabiliana na vyama vya upinzani. Uchochezi huu ulishika kasi katika uchaguzi wa mwaka 2005 na mwaka 2010. Vikundi kadhaa vya kidini vilifadhiliwa kuhubiri chuki dhidi ya dini nyingine waziwazi na kwa muda mrefu katika maeneo kadhaa ya nchi. Mihadhara, mahubiri na hata matamko ya hatari na uchochezi yalitolewa waziwazi hata kupitia vyombo kadhaa vya habari vya kidini na mitandao ya kijamii. Malalamiko mengi yalitolewa lakini Serikali ilifumbia macho tatizi hili kwani ilionekana kuwa mpasuko na hofu iliyo matokeo ya propaganda hizo ulikinufaisha zaidi chama tawala na baadhi ya viongozi wake.

Mheshimiwa Spika, chuki na hofu hii iliyopaliliwa kisiasa sasa ndiyo inayoitesa nchi yetu na hakika linastahili kuwa somo kwa wanasiasa wote walioasisi uhalifu huu dhidi ya mstakabali mwema wa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, kama vile hili halitoshi, sasa tunashuhudia kuibuka kwa uchochezi mpya wa kisiasa tena wenye ubia kati ya chama Tawala na vyombo vya dola na kinachoitwa "Ugaidi".

Mheshimiwa Spika, vitendo viongozi wa dini kujeruhiwa na kuuwawa kwa kupigwa risasi, kuchoma moto nyumba za ibada huko Zanzibar na Dar es Salaam ni Ugaidi kwa mujibu wa tafsiri ya Sheria ya Ugaidi ya Tanzania. Kambi Rasmi ya Upinzani inashangazwa sana kuona kwamba Serikali haikuyachukulia matukio haya ya wazi ya kigaidi kama ni ugaidi ila imekuwa hodari sana kuchukua suala la mtu aliyebambikiwa kesi ya ugaidi kwa ushahidi wa kughushi kuwa yeye ndiye gaidi. Pili, Kwa mujibu wa Sheria ya ugaidi mtu yeyote anayefanya mawasiliano na gaidi au magaidi, yeye pia anahamasisha ugaidi na hivyo naye anastahili kuunganishwa katika tuhuma hizo za mashtaka ya ugaidi.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inasikitika sana kuona wale wote waliokuwa wakiwasiliana na hao wanaoitwa magaidi ambao pia ni viongozi wa CCM na washirika wao hawajachukuliwa hatua yoyote. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaulaani mkakati huu wenye nia ovu ya kufifisha demokrasia hapa nchini. Aidha Kambi ya Upinzani inaamini kwamba, kamwe mpango huu haramu hautafanikiwa na naomba kuchukua nafasi hii kuonya kuwa vyama vya siasa vifanye siasa zake kwa ushindani wa sera na isiwe kwa mikakati ya kiharamia ya kudhuru, kubambikiza na kisha kutengeneza ushahidi kwa kutumia vyombo vya ulinzi na usalama. Hili nalo likiachiwa likakomaa litaliingiza Taifa letu katika hatari nyingine ya machafuko.


4.4 UHURU WA VYOMBO VYA HABARI

Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kwamba uhuru wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEKNOHAMA) ni kichocheo muhimu sana katika kujenga na kukuza demokrasia katika Taifa lolote linaloamini katika haki. Hali kadhalika, uhuru wa kujieleza na kupata habari ni miongoni mwa haki za msingi za raia. Ibara ya 18 ya Katiba yetu inaweka msisitizo kwamba, kila raia wa Tanzania anao uhuru wa maoni na kueleza fikra zake, uhuru wa kutafuta na kupokea habari na haki ya kufanya mawasiliano bila kuingiliwa katika mawasiliano yake.

Mheshimiwa Spika, matukio yaliyotokea mwaka jana peke yake katika tasnia ya habari ni kinyume cha katiba ya nchi lakini pia yanapingana na dhana ya Utawala Bora na kaulimbiu ya Serikali ya Uwazi na Uwajibikaji (Transparency and Accountability).

Mheshimiwa Spika, gazeti la MwanaHALISI limefungiwa kwa muda usiojulikana na serikali. Muda usiojulikana maana yake, ni hadi mtawala atakapotaka na au hadi waliolifungia gazeti watakapojisikia kutaka kulifungulia.

Mheshimiwa Spika, kwa taarifa zilizopo, gazeti hili limefungiwa bila wamiliki wa kampuni inayochapisha gazeti hilo kupewa haki ya kusikilizwa. Mbali na kitendo hiki kuwataabisha wafanyakazi kadhaa walioajiriwa na kampuni inayochapisha gazeti hili, kitendo hiki kimewanyima mamilioni ya Watanzania haki yao ya kupata habari kwa mujibu wa katiba. Kutokana na hali hiyo, ninaisihi serikali itafakari upya uamuzi wake wa kulifungia gazeti hili ili kuondoa kiza na malalamiko kuwa gazeti la MwanaHALISI limefungiwa kwa sababu ya kulinda uhalifu dhidi ya waliomteka na kumtesa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dr. Steven Ulimboka.

Mheshimiwa Spika, katika kadhia hiyo hiyo ya kuminywa kwa vyombo vya habari na uhuru wa habari, mwandishi wa habari Daud Mwangosi aliuawa kwa kupigwa kitu kilichohisiwa kuwa bomu na polisi. Utata mkubwa umezunguka tukio hili na polisi walewale ambao kwa mtazamo wa jumla ni watuhumiwa, wameachiwa mamlaka ya kuchunguza na kushtaki kuhusiana na kifo hiki.

Mheshimiwa Spika, kifo hiki kimelitia doa kubwa Taifa letu na zaidi kutokana na kitendo cha Serikali kuonekana kulinda wahalifu. Sina hakika kama watu walioshiriki katika kumpiga na kumuua Mwangosi wamekamatwa, ila nina hakika kuwa kifo chake kimepunguza wigo wa upatikanaji habari.

Ili serikali iweze kujinasua katika lawama, shutuma na tuhuma kwamba ilihusika katika kupanga njama za mauaji ya Mwangosi, ni vema itumie kupitia Rais, mamlaka yake ya kisheria kuunda tume huru ya kimahakama itakayochunguza kifo hiki na vingine kadhaa vyenye utata.

Mheshimiwa Spika, kilio hiki cha kuundwa kwa Judicial Commission of Enquiry kimekuwa cha muda mrefu na kila mwaka nazungumzia jambo hili katika hotuba zangu bila hatua zozote kuchukuliwa. Mara kadhaa, nimezungumza na wewe ndani na nje ya Bunge. Rais Jakaya Kikwete naye nimemwandikia na hata kuzungumza naye kuhusiana na haki hii ya msingi ya raia. Pamoja na wote kuahidi kuchukua hatua, hadi sasa hakuna hatua iliyochokuliwa hali inayoashiria serikali kujua ukweli na pengine kuhusika na hivyo kulindana katika mauaji.

Mheshimiwa Spika, napenda kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani kutoa pole kwa Ndg. Absalom Kibanda, Mwenyekiti wa Jukwaa la wahariri ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Mtanzania kwa maumivu na mateso makali aliyoyapata kutoka kwa watu wasiotaka kusikia uhuru wa kujieleza. Na kama ilivyo kwa matukio mengine kadhaa ya kuongezeka kwa utesaji wa aina hii, tunaitaka serikali itoe tamko rasmi la ni nani waasisi na watekelezaji wa mkakati huu wa kuzima uhuru wa wanahabari na vyombo vyao.

4.5 UWAJIBIKAJI WA KISIASA (POLITICAL ACCOUNTABILITY)


Mheshimiwa Spika, uwajibikaji wa kisiasa ni moja kati ya misingi ya utawala bora katika uendeshaji wa shughuli za Serikali. Serikali inayofuata misingi ya utawala bora huwa inawajibika kwa mema na mabaya yanayotokea chini ya utawala wake. Ni vyema ikaeleweka kuwa hitaji la kumtaka kiongozi wa kisiasa kuchukua hatua za uwajibikaji wa kisiasa, pale jambo linalosababishwa na uzembe wa ama yeye binafsi, walio chini ya mamlaka yake na hata mfumo anaousimamia, siyo jambo la chuki binafsi; bali ni kielelezo cha uongozi unaojali, unaojutia madhila yaliyosababishwa na ulio tayari kujirekebisha ili yaliyotokea yasijirudie tene siku za usoni.

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Tanzania siku zote hujikweza kama Serikali inayofuata misingi ya utawala bora. Lakini jambo la kushangaza ni kwamba kila mara viongozi wake wanakwepa kuwajibika kwa mambo mengi ya aibu yanayotokea chini ya utawala wake.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikipiga kelele ikiwataka mawaziri wa Serikali hii kuwajibika kwa kujiuzulu kwa kushindwa kutimiza wajibu wao wa kusimamia vyema kazi za Serikali lakini hakuna chochote kinachofanyika jambo ambalo limesababisha maovu kuendelea kufanyika na hivyo kuathiri ustawi wa Taifa.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani ilimtaka waziri wa Mambo ya Ndani na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini kujiuzulu kwa kushindwa kuzuia mauaji holela ya raia wasio na hatia yaliyofanywa na polisi maeneo kadhaa hapa nchini lakini hakufanya hivyo. Tulimtaka Waziri wa Elimu na Naibu wake kujiuzulu kwa kushindwa kusimamia mfumo wa Elimu hapa nchini jambo ambalo limepelekea kiwango cha wanafunzi wanaopata alama sifuri katika mitihani kuongezeka kila mwaka na hivyo kuweka hatarini mustakabali wa maisha ya wanafunzi hao na Taifa kwa jumla lakini bado wameng'ang'ania madaraka. Tuliitaka Serikali kuwawajibisha Makamanda wa Polisi wa Mikoa ya Morogoro na Iringa kwa kusimamia mauaji ya raia wasio na hatia lakini mpaka leo wanafurahia maisha kana kwamba hakuna kilichotokea.

Mheshimiwa Spika, Waziri Mkuu ndiye Kiongozi Mkuu wa shughuli zote za Serikali. Ofisi ya Waziri Mkuu ndiyo daraja kati ya Serikali Kuu na wananchi. Ni dhahiri kuwa Waziri Mkuu ndiye mtunza nidhamu na uwajibikaji mkuu katika Taifa hili. Ni nafasi ya uongozi inayostahili kuwa tayari kupokea lawama katika kufanya maamuzi magumu. Ni nafasi inayohitaji uwezo wa kufanya maamuzi hayo mazito na kwa wakati kwa maslahi ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, kwa idadi ya makosa ya kizembe yanayotokea katika nchi hii, na jinsi viongozi kadhaa wa serikali hii wasivyowajibika tena kwa kubeza na kukejeli malalamiko ya mara kwa mara ya wananchi; kitendo cha Waziri Mkuu kukaa kimya wakati mwingi bila kutumia rungu lake la madaraka kulitetea au kuliokoa Taifa ni kigezo tosha cha kutafakari kama upole nauungwana wa Waziri Mkuu leo ni tija au fedheha kwa Taifa?

Mheshimiwa Spika, napenda nimkumbushe Waziri Mkuu kwamba, Ofisi yake inategemewa sana kwa mustakabali wa maisha ya Watanzania. Kwa misingi hiyo, Waziri Mkuu hana budi kuwa mstari wa mbele katika kujibu kero na matatizo ya wananchi kwa haraka kuliko ilivyo sasa.

Mheshimiwa Spika, bado taifa liko katika msiba mzito uliosababishwa na kuporomoka kwa ghorofa katikati ya Jiji la Dar Es Salaam. Ofisi ya Waziri Mkuu imekalia kwa muda mrefu bila kuchukua hatua stahiki ripoti kadhaa zilizotahadharisha kuhusu ujenzi holela wa maghorofa katika nchi yetu. Mbali na waliopelekwa mahakamani, hakuna waliochukua hatua ya kuwajibika kisiasa / kiutendaji. Hili ni janga kuu na ishara ya watendaji na viongozi wengi wa Serikali kutokutambua kuwa nafasi zao za kazi ni dhamana waliyonayo kwa niaba ya Umma.

Mheshimiwa Spika, si nia yangu kutangaza mgogoro na Serikali kwa tabia hii ya kutowajibika, lakini napenda kuiasa Serikali kwamba kwa tabia hii inajitangazia mgogoro yenyewe na wananchi. Hili si jambo zuri kwani uvumilivu wa wananchi utakapofikia ukomo, Serikali isishangae kuona nguvu ya umma ikitumika kuwawajibisha viongozi wanaong'ang'ania madaraka huku wakiwa hawana sifa na weledi wa kufanya kazi za umma. Aidha, naomba kuwataka wananchi wasiendelee kutegemea "muujiza wa uwajibikaji" hivyo watafakari wenyewe uwezo walio nao kuchukua hatua muda muafaka ukifika.

INAENDELEA...
 
Inaendelea hapa....

===========

5.0 DENI LA TAIFA

Mheshimiwa Spika,
Mwaka 2012 takwimu zinaonyesha kuwa deni la taifa limeongezeka kwa asilimia 15.2. Ndani ya mwaka mmoja wa fedha kutoka shilingi bilioni 18,258.62 Desemba 2011 na kuwa shilingi bilioni 21,028.61 Desemba 2012 . Kati ya hizo deni la nje lilikuwa ni asilimia 75.97 na sababu inayotolewa kuwa ndiyo chanzo cha kuongezeka kwa deni hili kwa kasi namna hiyo ni pamoja na mikopo mipya kwa ajili ya kugharamia miradi ya miundombinu hususani ya Barabara na Umeme na malimbikizo ya riba.

Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inamtaka Waziri Mkuu ambaye ndiye Kiongozi Mkuu wa Serikali alieleze Bunge hili ni utaratibu gani uliotumika nje ya Bunge kuchambua na kuithinisha matumizi hayo kwani bajeti iliyopitishwa na Bunge kwa ajili ya miradi ya barabara ilikuwa ni shilingi trilioni 1, na bajeti nzima ya nishati ilikuwa shilingi bilioni 502 (bajeti 2012/2013) ilhali mkopo huu ulio katika deni la Taifa ni zaidi ya shilling trilioni 3? Ni miradi gani mikubwa hivyo ya barabara na umeme ambayo iligharimiwa na fedha hizo kama kweli zilikopwa kwa ajili ya kuhudumia miradi hiyo.

Mheshimiwa Spika,
Taarifa ya tume ya mipango iliyowasilishwa kwenye kamati ya Bunge zima na Waziri Stephen Wassira inaonyesha kuwa barabara zilizojengwa kwa kipindi hicho ni kilomita 170.6 ikilinganishwa na lengo na bajeti iliyopitishwa na Bunge ya kujenga kilomita 414 kwa mwaka 2012/2013 kwa barabara kuu kwa kiwango cha lami, hii ikiwa ni sawa na asilimia 41.2 tu ya lengo lililokuwa limepangwa.

Aidha ukarabati uliofanyika kwa barabara kuu ulikuwa kilomita 64.57, ikilinganishwa na lengo la kukarabati kilomita 135 kwa mwaka 2012/2013 na kwa upande wa ujenzi na ukarabati wa barabara zinazounganisha Mikoa na Wilaya ni ujenzi wa kilomita 8.2 tu ndio umekamilika ukilinganisha na lengo la kujenga kilomita 31.9 kwa mwaka kwa kiwango cha lami. Kwa upande wa ukarabati ni kilomita 99.45 tu zilikarabatiwa ikilinganishwa na lengo la kilomita 573.6 zilizokuwa zimepangwa kufanyiwa ukarabati ( chanzo: taarifa ya ofisi ya rais tume ya mipango).

Mheshimiwa Spika,
Aidha kwa upande wa miradi ya umeme ambayo ilitekelezwa ni pamoja na maandalizi kwa ajili ya ujenzi wa bomba la gesi ambayo yamekamilika ikiwa ni pamoja na kulipa fidia wanakijiji wapatao 3,092 na kwa upande wa mradi wa mgodi wa makaa ya mawe Kiwira kwa ajili ya kuzalisha MW 200 ni stahiki za wafanyakazi kulipwa pamoja na sehemu tu ya madeni ya CRDB, NSSF na PSPF ndio viliweza kulipwa.

Ni wazi kuwa taarifa hizi mbili yaani ya Waziri wa fedha na ile ya Tume ya mipango inaonyesha wazi kuwa kuna tatizo kubwa kuhusiana na suala la deni la Taifa, kwani upande mmoja unasema fedha hizo zilikopwa kwa ajili ya miradi ya umeme na barabara wakati upande wa tume ya mipango unaonyesha wazi kuwa hakuna miradi kama hiyo iliyoweza kutekelezwa kwa kipindi hicho.

Mheshimiwa Spika,
Taarifa ya serikali inaonyesha kuwa hakuna kitengo / idara ya madeni na sasa ndiyo serikali ipo kwenye mchakato wa kuanzisha idara ya madeni ambayo pamoja na mambo mengine itakuwa na jukumu la kujenga uwezo wa kufanya upembuzi yakinifu na kuhakikisha usimamizi madhubuti wa deni la Taifa. (Chanzo: Taarifa ya Waziri wa fedha juu ya mwongozo, matazamio na upeo wa bajeti ya serikali kwa Bunge 2013/2014, tarehe 25 machi 2013)

Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inamtaka Mhe Waziri Mkuu alieleze Bunge kwa kuwa haikuwepo idara kwa ajili ya uchambuzi juu ya mikopo hii, nani alikuwa anahusika na kusimamia ukopaji huu na hasa kuhusiana na riba kwani katika taarifa hiyo takwimu zinaonyesha kuwa fedha iliyolipwa kwa ajili ya deni la nje kama riba tu ilikuwa kiasi cha shilingi bilioni 66.1 wakati deni halisi tulilipa kiasi cha shilingi bilioni 35.5 na hivyo tulilipa jumla ya shilingi bilioni 101.56 kwa deni hilo.

Aidha kwa upande wa deni la ndani tulilipa kiasi cha shilingi bilioni 1,044.85 na kati ya fedha hizo tulilipia riba ya kiasi cha shilingi bilioni 210.7 tu.

Je, riba halisi kwa ajili ya mikopo hiyo tuliyochukua ilikuwa ni kiasi gani kwa mwaka? Na je madeni mapya riba yake iko kiasi gani kwa mwaka? Na ni kitengo gani kilihalalisha uchukuaji huu wa mikopo hiyo. Ni vyema sasa taarifa rasmi ya madeni ya Taifa yawe yanawekwa hadharani kwani kuna hisia ya kuwepo ufisadi wa kutisha kupitia akaunti ya madeni ya nje kama ilivyokuwa EPA.

6.0 GESI ASILIA
Mheshimiwa Spika;
Waziri Mkuu akiwa ndiye msimamizi na mdhibiti wa shughuli za kila siku za Serikali ndani na nje ya Bunge, anapaswa kutoa maelezo kuhusu hali inayoendelea hivi sasa katika sekta ndogo (sub sector) muhimu kwa nchi yetu ya gesi asili kuhusu mazungumzo yanayoendelea na makampuni mbalimbali ya kimataifa na mikataba inayozidi kusainiwa huku kukiwa na ombwe la kisera na udhaifu wa kiuongozi katika sekta hizo nyeti hali ambayo itakuwa na athari za muda mrefu sana kwa taifa.

Mheshimiwa Spika;

Mpaka sasa kwa mfano nchi haina sera ya gesi asili huku sera ya nishati ikiwa imepitwa na wakati, lakini mazungumzo yanaendelea na mikataba inazidi kusainiwa bila kuwa na mfumo thabiti wa kuhakikisha kwamba rasilimali za nchi zinanufaisha wananchi wa maeneo husika kwa ridhaa yao.

Aidha, kumekuwepo na ufisadi kama ambavyo ulielezwa pia katika taarifa iliyowasilishwa bungeni Novemba 2011 ambayo msingi wake ulikuwa pia madai ya Kambi ya Upinzani ya Julai 2011; hata hivyo mpaka sasa sehemu kubwa ya maazimio ya Bunge toka wakati huo mpaka sasa hayajatekelezwa kwa ukamilifu.

Wakati ufisadi huo ukiwa haujashughulikiwa, yameibuka madai mengine ya kasoro katika mkopo wa ujenzi wa Bomba la gesi, huku kukiwa pia na tuhuma za usiri katika mkataba huo ikiwemo kuhusu dhamana na masharti mengine yaliyoko kwenye mikataba ya ujenzi wa bomba husika.

Mheshimiwa Spika:

Kutokana na hali hiyo mwezi Februari 2013 katika maswali ya papo k wa papo bungeni, niliuliza swali kwa Waziri Mkuu iwapo mikataba hiyo sasa inaweza kutolewa kwa bunge na kwa wabunge na kuahidi kwamba wabunge wanaweza kupata nakala hiyo kwa kufuata masharti ya Sheria naomba ninukuu kauli yake " serikali imekwisha kubali kwamba, Bunge hili linayo fursa ya kupata mkataba wowote, kubwa ni kufuata utaratibu kupitia ofisi ya spika"

Kambi Rasmi ya Upinzani kupitia kwa Waziri Kivuli wa Nishati na Madini alitumia sheria ya kinga, haki na madaraka ya Bunge kuomba kuona nakala ya mkataba wa ujenzi wa bomba husika ili kutekeleza wajibu wa kibunge wa kuishauri na kuisimamia Serikali lakini toka wakati huo mpaka sasa mikataba hiyo imeendeelea kufanywa kuwa ni siri hata kwa wabunge.

Hata baada ya mazungumzo kati ya Rais wa Tanzania na Rais wa China masuala hayo yameendelea kufanywa kuwa siri; hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani kupitia Bunge hili inaitaka Serikali kuweka wazi masharti ya mikopo na dhamana zinazohusika kwa kuzingatia kwamba mwelekeo unaonyesha kuwa miradi ya chuma na makaa ya mawe ya Mchuchuma na Liganga imetumika kama sehemu ya mpango wenye kuacha maswali mengi kuhusu unyonyaji wa rasilimali za taifa katika sekta hizo muhimu.

Mheshimiwa Spika:

Udhaifu huo unapaswa kurekebishwa kwa kuongeza jitihada za kutekeleza ahadi za kuhakikisha kwamba matumizi ya gesi katika viwanda vya mbolea, viwanda vya bidhaa za kemikali zinazotokana na mafuta (petrochemicals), saruji na uzalishaji wa umeme katika mikoa ya Mtwara, Iringa, Ruvuma, Dar es Salaam na maeneo mengine yanayohusika.

Pamoja na Serikali kuingia makubiliano ya awali (MOU) na Kampuni ya kutoka nchini Marekani ya Symbion kuhusu uzalishaji wa umeme mkoani Mtwara, ieleze pia hatua ilizochukua katika kurekebisha kasoro zilizopo kwenye miradi ya Mchuchuma na Liganga na Mnazi Bay kwa kuzingatia ahadi ilizotoa mwaka 2004.

Mheshimiwa Spika;
Kambi Rasmi ya Upinzani pamoja na kutaka maelezo zaidi na vielelezo vya ziada kuhusu utekelezaji wa ujenzi wa bomba la gesi na matumizi ya gesi; inatoa mwito kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Watanzania kwa ujumla kufungua mjadala mpana zaidi wa kitaifa kuhusu gesi kwa kujikita katika suala la ubovu wa sera ya gesi na mchakato unaoendelea hivi sasa kuhusu rasimu ya sera hiyo na uozo wa mikataba kwenye utafutaji, uvunaji na usafirishaji wa gesi.

Serikali badala ya kuendelea kukimbilia kusaini mikataba mipya kuhusu utafutaji wa gesi asili na mafuta ishughulikie kwanza ubovu wa mikataba ya utafutaji wa mafuta na gesi kuweka hadharani ripoti ya uchunguzi kuhusu mikataba 26 ambayo ilikamilika tangu mwaka 2012 na kueleza hatua ambazo zimechukuliwa toka wakati huo.

Hatua hii ni muhimu kwa kuwa toka kusomwa kwa orodha ya mafisadi (list of shame ) tarehe 15 Septemba 2007 mpaka sasa yamekuwa yakitolewa madai mbalimbali kuhusu baadhi ya viongozi na watendaji kutuhumiwa kufanya ufisadi kupitia mikataba ya utafutaji na uvunaji wa gesi asili, utafutaji wa mafuta na uchimbaji wa madini na kufichwa kwa fedha katika akaunti za nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika:

Ziara ya Rais wa China ambayo ilihusisha usiri katika kusainiwa kwa mikataba 17 ya Sekta mbalimbali imedhihirisha kwa vitendo kwamba Serikali inayoongozwa na CCM isivyo na dhamira ya kutekeleza maazimio ya Bunge kuhusu usimamizi wa kibunge kwenye michakato ya mikataba.

Wabunge na wananchi wakumbuke kwamba mwaka 2008 kufuatia kashfa ya Richmond, Bunge lilipitisha azimio kwamba kamati za kisekta za Bunge zihusishwe kwa niaba ya wananchi kwenye maandalizi ya mipango na mikataba kuanzia hatua za awali ili kuishauri na kuisimamia Serikali; azimio ambalo halitekelezwi na hivyo kuibua migogoro kati ya wananchi na wawekezaji na maeneo mengine kufanya nchi kuingia mikataba mibovu.

Mathalani, wakati Tanzania imekopa mkopo mkubwa kutoka China kwa ajili ya ujenzi wa Bomba la gesi; miaka michache iliyopita kutokana na udhaifu wa mipango na mikataba ulifanyika ujenzi wa Bomba lingine kutoka Songosongo chini ya kampuni ya Songas kwa mkopo. Hata hivyo, katika mradi huo kulijengwa bomba lenye kipenyo kidogo na matokeo yake ni kwamba miaka michache baadaye taifa linaingia gharama kubwa ya mkopo mwingine kutokana na upungufu wa miundombinu ya gesi asili huku kukiwa na mzigo wa madeni makubwa ya mikopo ya awali. Serikali inapaswa kutoa maelezo kuhusu hatua ilizochukua kurekebisha hali hiyo toka wakati huo na kuhakikisha uwajibikaji wa viongozi na watendaji waliohusika ambapo wengine mpaka sasa bado wako katika ofisi za umma.

7.0 BUNGE KAMA MUHIMILI WA KUISIMAMIA NA KUISHAURI SERIKALI

Mheshimiwa Spika, mamlaka ya Bunge yameainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano Ibara za 62 hadi 64. Ibara hizi zote zinaeleza majukumu ya Bunge juu ya kusimamia utendaji mzima wa Serikali katika mchakato wa kuwapatia huduma za msingi wananchi.

Mheshimiwa Spika, jukumu hili kwa hali ilivyo sasa linashindwa kutekelezeka kutokana na ukweli kwamba Bunge linakosa taarifa au uelewa wa kutosha kuhusu sekta mbalimbali za kiutendaji. Kwa hali ya kawaida ni vigumu kumshauri au kumsimamia mtu bila ya kuwa na uelewa wa ziada kumzidi yule unaye mshauri au kumsimamia.

Mheshimiwa Spika, ili kukidhi matakwa ya Ibara ya 64 ni lazima Kurugenzi husika ndani ya Bunge kuwezeshwa kuwa na watendaji wanaoweza kuwasaidia waheshimiwa wabunge kutimiza matakwa ya Ibara hiyo.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka kuelewa toka kwa Mhe Waziri Mkuu, Miswada binafsi ya waheshimiwa wabunge Zitto Kabwe uliohusu mabadiliko ya sheria ya maadili ya viongozi na John Mnyika uliohusu uanzishwaji wa baraza la vijana la Taifa ambayo tayari imekwishawasilishwa Ofisini kwa Katibu wa Bunge ni lini italetwa rasmi Bungeni kwa utaratibu wa kuzifanya ziwe sheria za nchi?

Mheshimiwa Spika, Katika hotuba yangu ya mwaka jana nilieleza kuhusu Watendaji wa Serikali kushindwa kutimiza masharti ya kifungu cha 10 cha sheria ya Haki na Madaraka ya Bunge mwaka 1988 na marejeo yake ya mwaka 2002. Hali ya kutokuheshimu sheria hii bado inaendelea, Waheshimiwa wabunge wameomba kupatiwa nyaraka mbalimbali toka Serikalini kupitia kwa Katibu wa Bunge, lakini kwa bahati mbaya hadi sasa nyaraka hizo bado hazijatolewa.

Mheshimiwa Spika, katika hali kama hii, je Bunge linaweza kukidhi matakwa ya Ibara za 63? Utaishauri vipi na kuisimamia Serikali ukiwa huna taarifa za kutosha? Je, ni mara ngapi waheshimiwa Mawaziri wametoa majibu ya kudanganya na kupelekea waheshimiwa wabunge kukiambia kiti kuwa Waziri hajajibu swali lake? Mapungufu haya yote yanasababishwa na kutokuwepo kwa taarifa sahihi na za ziada kuwawezesha waheshimiwa wabunge kufanyakazi ili kukidhi matakwa ya Kikatiba.

Mheshimiwa Spika, Katika moja ya taarifa za asasi za kiraia zinazofuatilia mwenendo wa Bunge, pamoja na mambo mengine zimeonesha kuwa Bunge letu ni dhaifu na kuwa halitekelezi majukumu yake. Taarifa za Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na The Citizens' Parliament Watch (CPW) za Februari 13, 2013 zimeonesha kuwa
"…kumeendelea kuwa na mivutano yenye upendeleo wa vyama katika kujadili na kuchangia hoja na kuonekana Mh Spika, Naibu Spika na Wenyeviti wa vikao kutumia vibaya kanuni za Bunge kuwadhibiti Wabunge kulingana na vyama vyao. Ukiukwaji wa Kanuni za Bunge, matumizi mabaya ya muda na kukosa tija kumeendelea kuliathiri Bunge letu. Aidha baadhi ya Wabunge wamekuwa na matumizi ya lugha zisizostahili Bungeni na hata kushambuliana katika ubinafsi wao. Wakati wabunge wengine wakitumia muda wao nje ya Bunge kukutana na wananchi na kueleza ufanisi wao ndani ya Bunge, wengine wametumia nafasi hizo kupingana na wananchi na kulidhalilisha Bunge mbele ya jamii".

Mheshimiwa Spika
, Asasi hizi zinatukumbusha mambo muhimu sana kwa jamii yetu. Tuna kila wajibu wa kuwatendea haki watu wetu na kutafakari taarifa zinazotupima utendaji wetu na kuchukua hatua kurekebisha udhaifu huu.

8.0 MAMBO MUHIMU YA KUKUMBUSHA

Mheshimiwa Spika, mara kadhaa, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA imekuwa ikiitaka Serikali kutekeleza mambo ya msingi katika usitawi na maenedeleo ya Taifa hili lakini kwa masikitiko makubwa ni kwamba Serikali hii ya CCM inayojiita sikivu imeendelea kuziba masikio yake juu ya mahitaji muhimu kwa Taifa.

Kwa mfano, Kambi Rasmi ya Upinzani ilitoa pendekezo zuri la kuwapatia wazee wote pensheni (Universal Pension) sambamba na kuwa na mpango maalum wa kuwawezesha wazee wetu hawa kuishi maisha ya amani katika siku zao za uzeeni.

Licha ya Kambi ya Upinzani kuonesha njia ya kupata fedha za kuwalipa wazee hawa, lakini mpaka leo Serikali imekuwa na kigugumizi cha kutekeleza nia hii njema. Jambo hili linapelekea Kambi ya Upinani iamini kwamba Kauli aliyoitoa Waziri Mkuu, tarehe 01 Oktoba, 2009 wakati akiwahutubia wazee kwamba: "Wazee ni rasilimali na hazina kubwa katika kukuza uchumi wa nchi yetu na kuleta mabadiliko ya kiuchumi" ilikuwa ni kuwakejeli na kuwahadaa wazee waliovuja jasho kuijenga nchi hii hadi hapa ilipo. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali ieleze ukweli ili wazee hawa wajue kama Serikali imeamua kuwatupa wajitafutie utaratibu mwingine wa maisha.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikipiga kelele sana juu ya matumizi mabaya ya fedha za umma unaofanywa na Serikali kwa kisingizio cha uendeshaji wa shughuli za Serikali. Limekuwa ni jambo la kawaida kwamba katika bajeti ya Waziri Mkuu, na wizara nyingine, fedha za matumizi ya kawaida ni takribani asilimia 80 wakati fedha za maendeleo ni ni takriban asilimia 20 tu. Jambo la kushangaza hapa ni kwamba hata hii asilimia 20 ya fedha za maendeleo, zaidi ya nusu zinatoka kwa wahisani. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali iueleze umma wa watanzania: Kipi ni kipaumbele; kutumia fedha za walipa kodi wa Tanzania kwa matumizi ya ofisi, au kuwaletea wananchi maendeleo?

Aidha ni vyema Serikali ikaeleza Taifa ni njia gani inatumia kupunguza matumizi yasiyo ya lazima kwani kila siku tunaona kukua kwa kutisha kwa matumizi ya kawaida ya Serikali. Ni dhahiri hakuna uchungu na fedha za walipa koda kwa Serikali hii ya CCM.

Mheshimiwa Spika, Jambo jingine ambalo Kambi Rasmi ya Upinzani ingependa kuikumbusha Serikali ni kuhusu Sherehe za Kitaifa. Kwa muda mrefu sasa tumekuwa tukihoji matumizi yasiyofanyiwa ukaguzi ya sherehe za kitaifa. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuweka bayana matumizi ya fedha katika Sherehe za kitaifa kuwa kuwa fedha inayotumika ni fedha ya wananchi.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaikumbusha tena Serikali kusema ukweli kuhusu dhamira ya kuhamia Dodoma. Kambi Rasmi ya Upinzani inashauri tena Serikali kufuta mpango huu kwani ni upotezaji wa fedha za wananchi na fedha zinazopotezwa zielekezwe kwenye mipango mingine ya maendeleo na Dodoma iendelee kuwa mji wa Kibunge na Elimu kama ambavyo Kambi Rasmi ya Upinzani imekuwa ikishauri kila wakati.

9.0 MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI 2012/2013 NA UCHAMBUZI WA BAJETI YA 2013/2014

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/2013, Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake iliidhinishiwa kiasi cha shilingi bilioni 35.2 ikiwa ni matumizi ya kawaida. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 3.4 ilikuwa ni mishahara ya watumishi, shilingi bilioni 10.6 ikiwa ni ruzuku kwa taasisi, na shilingi bilioni 21.1 matumizi mengineyo. Hadi kufikia Februari 2013, shilingi bilioni 20.7 sawa na asilimia 59 zilikuwa zimepokelewa kutoka hazina.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Miradi ya Maendeleo, Ofisi ya Waziri Mkuu ilitengewa shilingi bilioni 91.7 lakini hadi kufikia Februari, 2013 ni kiasi cha shilingi bilioni 10.7 sawa na asilimia 11.7zilizokuwa zimetumika katika miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, kwa mchanganuo huo ni kwamba fedha za matumizi ya kawaida zinatumika zaidi kuliko fedha za maendeleo. Aidha, karibu asilimia 90 ya bajeti ya maendeleo, Ofisi ya Waziri Mkuu haikutekelezwa hadi kufikia Februari 2013.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inamtaka Waziri Mkuu atoe majibu kuwa inawezekanaje hadi kufikia "quota" ya 3 ya mzunguko wa bajeti, asilimia 90 ya bajeti ya maendeleo haijatekelezwa?

Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka huu 2013/2014 Ofisi ya Waziri Mkuu inaomba kuidhinishiwa shilingi bilioni 35.08 kwa matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 43.87 kwa bajeti ya maendeleo. Wakati matumizi ya kawaida yamepungua kwa asilimia 0.34 ukilinganisha na mwaka 2012/2013, bajeti ya maendeleo imepungua kwa asilimia 52.2 ukilinganisha na mwaka 2012/2013.

Mheshimiwa Spika, licha ya bajeti ya maendeleo kupungua kwa zaidi ya nusu ukilinganisha na mwaka jana bado imeendelea kuwa tegemezi kwa wahisani. Katika shilingi bilioni 43.87 za maendeleo, shilingi bilioni 37.87 sawa na asilimia 86.3 ni fedha za nje na shilingi bilioni 6 sawa na asilimia 13.7 ni fedha za ndani.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani haiamini kama tunaweza kupata maendeleo ya kweli kwa kutegemea fedha za wahisani katika bajeti za maendeleo.

Mheshimiwa Spika, katika miradi ya meaendeleo imetengwa shilingi bilioni moja kwa ajili ya uendelezaji wa kuzikia viongozi wa Kitaifa. Kambi ya Upinzani inataka kujua kama ni ombi la viongozi wa kitaifa kuandaliwa eneo maalumu la kuzikwa au ni utashi wa Serikali kufikiri kwamba viongozi wa kitaifa wanahitaji eneo maalumu la kuzikwa!

Kwa uzoefu ni kwamba waasisi wa Taifa hili walizikwa kwenye makazi yao. Kwa nini viongozi wa kitaifa walio hai sasa wasifuate mfano huo? Hivi kweli kuna mantiki yoyote ya kutumia shilingi bilioni moja ya kuandaa sehemu ya kuzikia watu ambao hawajafariki wakati kuna watu wenye njaa, wagonjwa, wamama wajawazito wanaojifungulia sakafuni ambao wanahitaji huduma ya matibabu na dawa ili wapone?

Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya maendeleo, Kitengo cha Maafa kimetengewa shilingi bilioni 1.8 kwa ajili ya kujenga uwezo wa kukabiliana na maafa. Mheshimiwa Spika, Watanzania wameshuhudia maafa makubwa katika nchi yetu hasa ya kuzama kwa Meli kwa mfano Meli ya MV Bukoba, Meli ya MV Skagit na Meli ya MV Spice Islanders huko Zanzibar na pia wameshuhudia kuporomoka kwa maghorofa na mengine kuungua moto. Katika ajali na maafa haya Watanzania wengi walipoteza maisha yao na daima waokoaji wa ndani wamekuwa na uwezo mdogo sana wa kuokoa watu na hivyo kutegemea zaidi waokoaji na vifaa toka nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaamini kuwa fedha hizi ni ndogo na hivyo ni vyema Serikali ieleze uwezo huo unaokusudiwa kujengwa ni upi!

Mheshimiwa Spika, katika kupunguza gharama za uendesha wa shughuli za Serikali, Kambi ya Upinzani imekuwa ikipinga matumizi mabaya ya fedha za umma na hasa posho za vikao (sitting allowances) kwa kuwa vikao ni sehemu ya majukumu yao ambayo wanalipwa mshahara. Kambi Rasmi ya Upinzani inazidi kusisitiza kuwa posho za vikao zifutwe kwani zinaongeza gharama za uendeshaji wa Serikali ambazo si za lazima.
 
Kama hoja za Mh. Mbowe ambazo huwa ni nyepesi sana zinaweza kulitikisa bunge, basi hili bunge linatakiwa kutokuwepo kabisa.

He's just there kama kiongozi wa upinzani bungeni by default
 
Kama hoja za Mh. Mbowe ambazo huwa ni nyepesi sana zinaweza kulitikisa bunge, basi hili bunge linatakiwa kutokuwepo kabisa.

He's just there kama kiongozi wa upinzani bungeni by default
hayo maneno yako in red naona kama dharau fulani... :eyeroll1:
 
31 Reactions
Reply
Back
Top Bottom