Five killed in Barrick Tanzanian mine attack

Itafika mahali wananchi tutadai nchi yetu,sababu nnaona viongozi wanazidi kutufanya wananchi Kama watoto
 
Hao siyo inruders hao ni wenye mali wachoka na ujinga wa wezi wajimba madini kuiba kwa kushirikiana na viongozi wetu hivyo hawana mtetezi zaidi ya kujimibilise na kutumia mawe, nawapongeza kwa kwenda kushare kuchukua mali zao kwa majizi haya na hao waliokufa wamekufa kishujaa na wengige wauinge mkono vuguvugu hilo hasa kwenye migodi ya Buzwagi na Kahama mine

Ni kweli......hawa si intruders.....ni wenye mali na wamiliki halisi wa rasilimali ambao wanapigania haki ya watanzania ambayo inaibwa na wageni kwa kushirikiana na viongozi wa ccm ambao hawana uchungu na urithi wetu....

Kwa maana kama mrabaha wa mwaka jana zaidi ya 24 bill...hazieleweki ziko wapi....... sasa kweli kuna umuhimu wa kuwa na wawekezaji kama hawa... (ona link hii)http://www.corruptiontracker.or.tz/dev/index.php?option=com_content&view=article&id=150%3Atanzania-fails-to-account-for-24bn-in-mineral-revenues&catid=18%3Acurrent-issues-&Itemid=51&lang=en

Watu hawa wanahitaji support........shime ndugu zangu watanzania twendeni........tuungane nao kwa ajili ya hilo......tukasaidie......wenzetu....
 
Na Waandishi Wetu
POLISI wamewaua watu tisa kwa risasi na kuwajeruhi wengine kadhaa katika matukio mawili tofauti, likiwamo la watu 800 kuvamia mgodi wa North Mara Barrick, uliopo Nyamongo, wilayani, Tarime.Matukio hayo yametokea jana kwa nyakati tofauti katika mikoa ya Mara na Kilimanjaro.Huko Mara, watu watano kati ya zaidi 800 waliovamia mgodi wa North Mara uliopo Nyamongo kwa lengo la kuchukua mchanga wa dhahabu wameuawa na wengine sita kujeruhiwa katika mapambano makali kati yao na polisi wanaolinda mgodi huo.

Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Tarime-Rorya, Constantine Massawe alisema tukio hilo lilitokea jana kuanzia saa 11:00 alfajiri katika eneo la Kinu cha Dhahabu, watu wanaokadiriwa kuwa kati ya 800 na 1,000, wenye silaha za jadi na makombeo, walivamia eneo hilo ili wachukue mchanga wa dhahabu.

Waliouawa
Aliwataja watu waliouawa kuwa ni Chacha Ngoko (25), mkazi wa Kewanja Nyamongo, Emmanuel Magige Ghati (19), mkazi wa Kijiji cha Nyakunguru, Chacha Mwasi (23), mkazi wa Kijiji cha Bisarwi Komaswa na wengine wawili ambao majina yao hayakutambuliwa.
"Baadhi ya miili ya marehemu hao ipo chumba cha maiti katika Hospitali ya Wilaya Tarime ikisubiri kuchukuliwa na ndugu zao," alisema Kamanda Massawe.Alisema kati ya watu hao, watatu walikufa papo hapo na wawili walifia hospitali huku wengine wanane wakijeruhiwa kwa risasi.

Kamanda huyo alisema kwamba chanzo cha mauaji hayo ni kuzidiwa nguvu kiasi cha kumlazimu aongeze askari wengine ili kukabiliana na hali hiyo jambo ambalo pia lilishindikana.Alisema kabla ya mauaji hayo kutokea, polisi walijitahidi kuwadhibiti watu hao kwa risasi za mpira na mabomu lakini ilishindikana kwa kuwa nao walikuwa wakijibu mashambulizi kwa kuwatupia mawe kwa kutumia makombeo na marungu, hivyo wakatumia risasi za moto.

Mapambano makubwa
"Mapambano yalikuwa makubwa, maana kundi la watu kati ya 800 na 1,000 wakiwa na makombeo na mapanga na marungu walivamia eneo ili wachukue dhahabu,” alisema Kamanda Massawe."Polisi walijitahidi kuwatawanya kwa kupiga risasi hewani wakawa wanasonga kuwafuata askari huku wakiimba kuwa tunataka kuchukua mali yetu. Sasa katika kujihami, yakatokea mauaji hayo,” alisema.
Alisema kwa muda wa siku nne mfululizo, wananchi walikuwa wakivamia eneo hilo wakiwa na kombeo, silaha ambayo alisema waliwahi kuitumia kutungua ndege pia waliitumia kumpiga kiongozi wa Polisi wa Wilaya (OC-CID) katika paji la uso na kushonwa nyuzi nne.

“Ni hodari sana wa kurusha kombeo maana OC –CID alipigwa na kujeruhiwa usoni. Askari mmoja anaitwa Mrashani naye alipigwa mguu na anatembelea fimbo, walikuja wakijua ni kama kawaida, wakakuta tumejizatiti ndipo ikatokea hali hiyo,” alisema.
Alisema kuwa katika mapambano hayo yaliyochukua zaidi ya saa moja jana, askari wake mmoja alijeruhiwa.

Kamanda huyo pia aliwataja majeruhi ambao alisema wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya kuwa ni pamoja na Samwel Nyangoye (35), mkazi wa Sirari aliyepigwa risasi begani na kutokea kifuani ambaye hali yake ni mbaya.
Wengine ni Mwikwabe Marwa Mwita, Frank Joseph (20), mkazi wa Kewanja Nyamongo ambaye alipigwa risasi ya kiunoni, Nyangi Mkenye (30), mkazi wa Kijiji cha Matongo aliyepigwa risasi mguu wa kushoto na kuvunjika. Majeruhi wengine sita wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Sungusungu Nyamongo.

Askari waliojeruhiwa
Kamanda Massawe alisema kuwa askari wake waliojeruhiwa katika uvamizi huo tangu ulipoanza siku nne zilizopita ni wanne, akiwamo Mkuu wa Kitengo cha Kuzuia Wizi wa Mifugo Wilaya ya Tarime, SP Saimon Mrashan aliyepigwa mawe ya kombeo ubavuni. Alisema hali yake ni mbaya.

Mwingine ni ASP Hassan Maya aliyepigwa jiwe kichwani ambaye naye hali ni mbaya na askari wawili walipigwa mawe na kukatwa panga, huku magari ya polisi na ya walinzi wa mgodi huo yakiharibiwa vibaya kwa mawe na kuvunjwa vioo.
Kamanda Massawe alisema tukio hilo ni mwendelezo uvamizi mgodini hapo likiwamo la Mei 14, mwaka huu wakati kundi kubwa la watu wakiwa na silaha za jadi, mawe na marungu lilipovamia eneo hilo.

Diwani apinga mauaji
Diwani wa Kata ya Matongo, Bathlomeo Machage aliitaka serikali kutafakari njia mbadala ya kuimarisha ulinzi na kuwachukulia hatua askari wanaohusika na matukio katika mazingira yasiyoruhusu matumizi ya nguvu.

Meneja Uhusiano wa Kampuni ya African Barrick Tanzania, Teweli Teweli alikiri kutokea kwa tukio hilo lakini akasema suala hilo lipo mikononi mwa polisi. Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Tarime, Joyce Raymond alikiri kupokea maiti na majeruhi lakini pia hakutaka kuzungumza zaidi kuhusu suala hilo kwa kuwa alikuwa akitoa huduma kwa majeruhi hao.
Habari ambazo hazijathibitishwa zinasema kwamba idadi ya majeruhi inaweza kuwa kubwa zaidi kwa kuwa wengi hawakupelekwa hospitalini na idadi kubwa ya waliofikishwa huko ni wale waliokamatwa na polisi.

Mauaji mkoani Kilimanjaro
Mkoani Kilimanjaro, polisi wamewaua watu wanne baada ya kuwatuhumu kuwa walikuwa wanajiandaa kuvamia na kupora fedha katika klabu mashuhuri ya Malindi na duka la kuuza silaha la Tanganyika Arms Limited ya mjini Moshi. Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kilimanjaro, Lucas Ng’hoboko aliwaambia waandishi wa habari jana mjini Moshi kuwa watu hao waliuawa saa 7:00 usiku wa kuamkia juzi baada ya kupambana kwa kurushiana risasi na polisi.

Hata hivyo, tukio hilo limegubikwa na mkubwa kuhusu jinsi watu hao walivyouawa, wakati polisi wakidai kuwa waliwaua katika mapambano ya kurushiana risasi eneo la tukio, baadhi ya mashuhuda walidai kuwa watu hao walikamatwa wakiwa wazima katika eneo hilo na polisi wakaondoka nao.

Miongoni mwa waliouawa ni dereva wa teksi, Nicodemas Kinyaa (37), maarufu kwa jina la Samora, mkazi wa Pasua Matindigani, Moshi Mjini ambaye madereva wenzake wanadai kuwa hana kumbukumbu za uhalifu.
Wengine waliouawa katika tukio hilo wametajwa kuwa ni fundi seremala, Juma Sanga (27), mkazi wa Njoro makaburini, kondakta wa daladala, Musa Sekuye na Stephano Kivuyo (25) maarufu Msumbiji ama Dogooo.

Kuhusu Kinyaa, madereva wa teksi waliohojiwa walisema marehemu alikuwa amekodishwa bila kufahamu mienendo ya abiria wake na kusema kwamba kitendo cha polisi kumjumuisha kuwa ni jambazi na kumwua kwa risasi kilikuwa ni unyama wa hali ya juu.“Tunataka polisi watuambie walimkamata eneo gani na ni eneo gani walirushiana risasi… Watu wamekuja wamemkodi leo anageukaje kuwa jambazi?” alisema mmoja wa madereva hao.

Lakini Kamanda Ng’hoboko alisema mara baada ya watu hao kuuawa, walipopekuliwa walikutwa na bunduki moja aina ya short gun iliyokatwa kitako ikiwa na risasi nne. Alisema watu hao pia walikutwa na mapanga mawili na simu nne za mkononi wakiwa na gari dogo aina ya Toyota Corolla ambayo ni teksi.

Kwa mujibu wa Kamanda Ng’hoboko, gari hilo linamilikiwa na Roseline Shirima (37), Muuguzi katika Hospitali ya KCMC na dereva wake ni Evans Sebastian lakini siku ya tukio alikuwa amemkodishia dereva mwenzake (shanta) aliyeuawa na polisi. Kwa mujibu wa Ng’hoboko, Evans anashikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi.

Alisema majambazi hao wanatuhumiwa kuhusika katika matukio mbalimbali ya uporaji wa kutumia silaha, kupora na kubaka.Alisema polisi walipata taarifa za kuwapo kwa majambazi hao kutoka kwa raia mwema wakati majambazi hao wakiwa wanaondoka eneo la Malindi ndipo polisi walipowafuatilia na watu hao ndiyo walioanza kurusha risasi ovyo.

Ng’oboko alisema katika upekuzi wao pia walipata simu tano, kati ya tatu walizokamatwa nazo walikuwa wamezipora Mei 12 huko Soweto na pia walikuwa wamepora kiasi cha Sh1,276,600 kwa kutumia mtutu.


Source Mwananchi

Habari hii imeandikwa na Anthony Mayunga na Samson Chacha, Tarime na Daniel Mjema, Moshi
 
Inauma sana,
Hakuna mapinduzi bila ya damu kumwagika, hakuna asiyejipenda, ukiona watu wanavamia mgodi ujue wamechoka. Hivi kwanini ulale njaa uku ukijua ilipo chakula. Hawa watu walifukuzwa kwenye maeneo yao bila hata fidia ya kuridhisha, hali ni ngumu kimaisha. Ni hafadhali ufe leo ili wanao ajeapate mazingira mazuri.
Hivi serikali ya Tz inalinda maslai ya nani?
Hivi mapolisi hao si waTz?
 
Nchi inaongozwa kwa majungu na fitna,hii ni nchi ya dili, wote wanatafta madili hata kuuwa watanzania wenzao wao hilo ni dili kubwa...nawachukia polisi mana ni wanafiki wakubwa...wana njaa kali na hiyo laana ya kuuwa watanzania wenzenu haitawatyoka milele!! mlaaniwe na barick yenu na serikali ovu ya ccm!! siku yenu yaja mtalia sana.
 
wananchi sita wameuwawa huko tarime kwa kupigwa risasi na polisi, ikidaiwa kua wananchi hao walikua wanataka kuuvamia mgodi wa north mara, lakini wananchi wenyewe waliohojiwa wamesema kua sio uvamizi, bali walikua wanaenda kuomba kazi,,,lakini hata hivyo channel ten haijaitoa hii habari vizuri sana, na ndio source yangu, so who ever knowz much more atujuze.
 
Polisi yaua tena mgodini Tarime


na Ambrose Wantaigwa na Irene Mark


amka2.gif

JESHI la Polisi wilayani Tarime limeendeleza wimbi la mauaji katika mgodi wa dhahabu wa kampuni ya African Barrick Gold (ABG) safari hii limewaua kwa risasi watu watano wanaodaiwa kuvamia mgodi huo.
Hadi jana mchana kulikuwa na taarifa za kutatanisha kuhusu idadi kamili ya watu waliofariki wakati polisi waliokuwa doria katika eneo hilo walipolimiminia risasi za moto kundi la watu waliokuwa nje ya hifadhi ya mgodi huo kwa lengo la kuokota mchanga wa dhahabu.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kijiji cha Kewanja kilichopo kwenye mji mdogo wa Nyamongo wilayani hapa watu watano ambao hawajafahamika majina na makazi yao waliuawa katika vurumai hiyo iliyotokea jana saa 11 alfajiri.
Taarifa hizo zimetofautiana na zile zilizotolewa kwa vyombo vya habari na Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Tarime/Rorya ambapo limethibitisha vifo vya watu watatu kutokana na risasi za moto wanaodaiwa kuwa miongoni mwa kundi la wananchi waliotaka kuvamia mgodi huo.
Kamanda wa Polisi kanda hiyo Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Costantine Massawe aliwaeleza waandishi wa habari ofisini kwake jana kwamba watu hao ambao hawajatambuliwa walipigwa risasi wakiwa miongoni mwa kundi la watu zaidi ya 200 waliokuwa na silaha za jadi.
Alisema watu wengine watano waliojeruhiwa kwa risasi, wamelazwa katika hospitali ya wilaya wakiendelea na matibabu na kubainisha kwamba askari wawili walijeruhiwa kwa mawe wakati wa tukio hilo.
“Tukio hilo ni mfululizo wa mikakati ya kukabiliana na uhalifu maeneo hayo ambapo siku nne kabla tulikamata bunduki mbili aina ya SMG kutoka kwa watu wanaosadikiwa kuwa majambazi katika jaribio la kuvamia mgodi,” alisema ACP Massawe.
Aliwataja majeruhi waliolazwa kuwa ni Frank Emmanuel (25) mkazi wa Kewanja, Mwikwabe Mwita (30) mkazi wa mgumu, Samwel James (26) mkazi wa Tarime, Chacha Mwasi (23) mkazi wa Komaswa na mwingine ambaye hajatambuliwa.
Aidha, mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo Kiguku Ryoba, aliliambia gazeti hili kuwa askari polisi waliokuwa doria katika eneo hilo walianza kuwamiminia risasi watu hao baada ya kukaidi amri iliyowataka kuondoka maeneo hayo ambapo inadaiwa kuwa miongoni mwa kundi hilo kulikuwa na wanawake na watoto wa chini ya miaka 20.
“Tulisikia milio ya risasi mfululizo leo alfajiri na baadaye kila mtu alikimbia kutafuta hifadhi alivyoweza kabla ya kuona miili ya watu zaidi ya watatu ikiwa imetelekezwa eneo hilo na haikufahamika kama walikuwa hai au wamekufa,” alisema Kiguku Ryoba.
Kwa upande wake Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani Godbless Lema, ameeleza masikitiko yake kuhusu tukio hilo huku akiahidi kulizungumzia wakati wowote kuanzia leo.
“Nimesikitishwa na kitendo hicho… unajua polisi anatakiwa kuwa mlinzi wa raia na mali zake sasa anapogeuka kuwa muuaji wa anaowalinda kuna tatizo hapo.
“…Binafsi nimesikitishwa sana na taarifa hiyo, kwa nafasi yangu kama waziri kivuli naahidi kulizungumzia hili baada ya kupata habari kamili kutoka Tarime,” alisisitiza Lema ambaye pia ni Mbunge wa Arusha Mjini.
Naye Mbunge wa Tarime, Nyambari Nyangwine (CCM), amekemea kitendo hicho na kuahidi kushirikiana na vyombo husika kuhakikisha polisi waliofanya hivyo wanachukuliwa hatua kali.
“Hata kama wananchi wanavunja sheria polisi hawana ruhusa ya kuwaua… kwanza wananchi wenyewe hawakuwa na silaha walitakiwa kutumia mbinu nyingine kuwatawanya, kuua sio suluhisho.
“Kwa kuwa nimetoka huko jana (juzi), nitawasiliana na viongozi wa wilaya na mkoa kuhakikisha polisi walioua wanajulikana, wanakamatwa na hatua za kisheria kuchukuliwa kwa wahusika wote, hatuwezi kuvumilia hili maana si mara ya kwanza,” alisema Nyangwine na kuahidi kulishughulikia kwa karibu suala hilo.
Mratibu wa Haki za Binadamu wa Chama cha Wananchi (CUF) wilayani Tarime Abdallah Mrimi, amelishutumu jeshi la polisi kwa mauaji hayo na kusema linatumia nguvu kubwa kukabiliana na wananchi wasio na silaha huku akitahadharisha kuwa wahusika wanaweza kufikishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu The Hague, nchini Uholanzi. “Nchi yetu imetia saini mkataba wa kimataifa wa haki za binadamu na haikubaliki kumwadhibu mtu anayedaiwa kuvamia mgodi kwa kumuua, badala yake anapaswa kufikishwa katika vyombo vya sheria,” alisema Mrimi.
 
honestly, watanganyika tukubali kwamba Serikali hii si kwa ajili ya mtanganyika mlalahoi ila ipo kwa wageni wezi wa mali zetu. Naunga mkono 'jino kwa jino' hapo!! Naamini wakurya watadhihirisha u-kurya wao!!
 
Yaani sasa wale wa Tarime walio ichagua CCM ndipo watajua cha moto . Eneo lile CCM ililitaka kwa udi na uvumba wamelipata na sasa wanapokewa na maafa wacha tuone kitatokea kitu gani .
 
Hao intruders, si watanzania...
Dah, sad...
Hivi hawa polisi hawana mbinu mbadala, wanaona raha tu kuangamiza maisha ya watz..
Tanzanians will never be intruders in their own land. Their innocent people who have been alienated from ther land. Let them fight for the lost land and the resources.
 
HALI SI SHWARI WILAYANI TARIME


WAKATI serikali ikisema watu watano waliouawa na polisi wilayani, Tarime Mkoa wa Mara walikuwa ni wahalifu waliotaka kuvamia Mgodi wa North Mara Barrick, msafara wa Mbunge wa Jimbo hilo (CCM), Nyambari Nyangwine (pichani) umeshambuliwa katika mkutano wa kuzungumzia sakata hilo.

Tukio hilo lilitokea jana muda wa saa saba mchana mara baada ya mbunge huyo kuingia ghafla kwenye mkutano wa jamii maarufu kama Ritongo kwenye eneo la Mnada wa Matongo.Vurugu kubwa ziliibuka na kusababisha msafara wa mbunge huyo na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Amos Sagara kupondwa mawe. Katika tukio hilo, walinzi wa viongozi hao walijeruhiwa vibaya na baadhi ya magari kuharibiwa.

Mbunge asimulia alivyotimuliwa
Akisimulia tukio hilo, mbunge huyo alisema: "Mimi na mwenyekiti wa halmashauri, tulikwenda kutaka kuwafariji wenzetu wa eneo la Nyamongo ambao ndugu zao waliuawa na polisi wakati wakidaiwa kuvamia Mgodi wa North Mara mwanzoni mwa wiki hii na watu watano kuuawa."

Alisema walitaka kufanya mkutano na wananchi katika eneo la Stendi la Kewanja Nyamongo: "Tulifika na kuanza kukaa kabla hatujaanza kuhutubia lilijitokeza kundi kubwa la vijana zaidi ya 100 na kuanza kudai wanachama tulioongozana nao, wakiwa na sare za CCM wazivue na kuondoka maeneo hayo nikiwamo mimi."

Alisema baada ya tamko hilo, vijana hao walianza kuwashambulia viongozi hao kwa mawe.
Alisema katika tukio hilo, walinzi wake sita wakiongozwa na Godfrey Francis na Sutwa, walijaribu kupambana na kundi hilo ndipo yeye (Nyangwine) alipofanikiwa kupenya na kuingia katika gari na kuondoka. Hata hivyo, walirushiwa mawe yaliyowajeruhi baadhi ya walinzi hao na kuharibu magari yao.

Alisema katika msafara huo, magari yaliyoharibiwa kwa kuvunjwa vioo vyote na kupondwa mawe ni pamoja na lile la Idara ya Elimu aina ya Land Cruser, alilokuwa nalo mwenyekiti huyo wa halmashauri. Mengine ni Toyota RAV4 na Toyota Prado. Mbunge huyo alisema tukio hilo la kushambuliwa kwao lilitokea saa 5.00 asubuhi.

Baada ya kushambuliwa Mbunge huyo aliwaambia vijana hao: "Wananchi wa Nyamongo msikubali kutumiwa na baadhi ya wanasiasa wa vyama vya upinzani kuvamia Mgodi wa North Mara na kuwashambulia viongozi wa umma kwa kuwapiga mawe, suluhu inapatikana kwa pande zinazopingana kukaa pamoja wala si kurushiana mawe."

"Tumekuja kwa nia njema kuwafariji, lakini baadhi ya wanasiasa wamegeuza maafa haya kama mtaji wa kupandia, jambo ambalo ni hatari kwa jamii ya Kitanzania nakemea na kulaani kitendo hiki."

Alisema katika mkutano huo uliovurugwa, alitaka kuzungumzia masuala ya mauaji ya mara kwa mara kati ya wananchi wa vijiji vinavyozunguka mgodi huo na sababu za kuvamiwa kwa mgodi ambao wananchi wa maeneo hayo wamekuwa wakidai kutolipwa fidia ya mali zao.

Alisema serikali itaunda tume huru itakayowashirikisha wananchi, viongozi wa vijiji, wa serikali, wazee wa mila na wamiliki wa Mgodi huo wa North Mara Barrick.

Diwani naye aeleza kilichotokea
Diwani wa Kata ya Matongo (Chadema), Bathlomeo Machage alidai kuwa wananchi walihamaki kumwona mbunge huyo na timu yake iliyovalia sare za CCM ikiingia kwenye mkutano wa jamii ambao haukumhusu.

“Nilimkaribisha kiti kwa kuwa mimi ndiye nilikuwa kiongozi pekee zaidi ya wazee wa mila, tukasalimiana, lakini yeye akachukua kipaza sauti cha gari lake la matangazo maana walikuwa wanatoka kumpokea katibu mkuu wao wa taifa,” alisema.

Alisema kitendo hicho kiliibua mzozo huku wananchi wakisema mkutano huo haukuwa wa CCM na kuhoji iweje aende na sare za chama na kutaka kuwahutubia wakati hawakuwa wamemwalika.

“Alisema anakuja kuwapa pole, hapo ndipo wananchi wakachachamaa na kudai alikuwa wapi na hizo sare zake hazitakiwi. Alitulia kidogo, nikamwomba awasikilize wananchi maana ndiyo wenye mkutano, hakunielewa akataka kuzungumza,” alisema diwani huyo.

Alisema baada ya mabishano hayo kuliibuka hasira na wananchi wakaanza kupiga yowe iliyowavuta wengine na kuanza kukusanyika.

Baada ya kukusanyika diwani huyo anasema walianza kumrushia mawe mbunge huyo na wafuasi wake. Alisema baadhi ya vijana walifanikiwa kumnusuru na kumwingiza ndani ya gari ambalo pia lilishambuliwa pamoja na mengine katika msafara wake.

“Alishambuliwa gari lake na kupigwa vioo kwa nyuma, lakini lile la halmashauri limeharibiwa sana kwa kweli hali ilichafuka na mimi nikalazimika kukimbia eneo hilo,” alisema.

Machage alisema mara baada ya vurugu hizo kundi la vijana waliokuwa wamepandwa na jazba walijikusanya wakitaka kwenda kuvamia mgodi huo kwa lengo la kuuchoma moto.“Kwa kushirikiana na wazee wa mila tulifanikiwa kuzima jaribio hilo na kuwarudisha vijana na hali irejea kuwa ya utulivu,” alisema.

Sijawahi kuona ghasia kama hizi
Akizungumzia ghasia hizo, Mwandishi wa Habari wa ITV na Redio One, Mkoa wa Mara , George Marato alisema: “Sijawahi kuona tukio kama hilo tangu nizaliwe maana walinivamia hata mimi wakidai wapo waandishi wanaondika habari za upotoshaji na kupiga gari tulilokuwa nalo, wapo wanaonifahamu wakanitetea nikaachwa. Hapa nilipo nimepoteza baadhi ya vitu nimechafuka sana,” alisema.

Baadhi ya wananchi walisema wamekerwa na kitendo cha mbunge huyo kutokwenda kukutana na wananchi waliopiga kambi katika Hospitali ya Wilaya kwa siku mbili, wakiwa wamesusa kuchukua miili ya ndugu zao waliouawa kwa kupigwa risasi na askari polisi badala yake alikwenda kwenye mkutano wa CCM.Zaidi ya watu 200 walikusanyika nje ya chumba cha maiti katika Hospitali ya Wilaya Tarime wakitokea maeneo ya Nyamongo.

Kauli ya serikali kuhusu mauaji ya Tarime
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Balozi Hamis Kagasheki alisema, polisi waliamua kutumia nguvu baada ya kuzidiwa na kundi kubwa la watu hasa baada ya kupiga mabomu ya machozi bila mafanikio.

“Tukio hili limetokea katika mazingira haya kwa sababu walikuwa ni watu wengi na tunasikitika kwa sababu hakuna serikali inayopenda kuua raia wake. Ingekuwa askari waliwafuata watu hao katika maeneo yao ya kazi, hapo unaweza kusema jeshi la polisi lina uonevu.”

Alisema kabla ya tukio hilo la juzi, kulitokea mengine, Mei 7 na Mei 14, mwaka huu katika mgodi huo na watu walipora mali lakini hakukuwa na mauaji.Balozi Kagasheki alisema katika tukio la juzi, takriban watu 1,500 walivamia mgodi huo kwa nia ya kwenda kwenye kinu cha dhahabu na kusema katika tukio hilo, pia walivunja magari na kujeruhi polisi saba.

Alisema tayari Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), ametuma timu maalumu kwenda eneo hilo kufanya uchunguzi wa tukio hilo.Katika hatua nyingine, Kagasheki amesema ameshangazwa na baadhi ya watu kuligeuza tukio hilo mtaji wa kisiasa na kuwahamasisha wafiwa wakatae msaada wa serikali kwa ajili ya mazishi.Balozi Kagasheki alisema chama kimoja cha siasa kiliomba kibali cha kufanya maandamano na mkutano wa hadhara leo katika eneo hilo lakini kimenyimwa.

Alisema walikataa kutoa kibali hicho kwa sababu maandamano yaliyopangwa kufanywa, yanahatarisha amani.
“Tunakiri kwamba hawa ni wahalifu lakini bado ni Watanzania wenzetu ndiyo maana kama serikali tumeamua kutoa msaada wa mazishi,” alisisitiza.

Hata hivyo, alisema hadi sasa ni familia moja tu iliyokubali msaada wa mazishi kutoka serikalini lakini familia nyingine nne zimekataa.Naibu Waziri huyo aliwaonya wale wote watakaokwenda kinyume na kufanya shari katika eneo hilo, kwamba sheria itachukua mkondo wake.

Watu waliouawa katika tukio hilo ni Chacha Ngoko (25), mkazi wa Kewanja Nyamongo, Emmanuel Magige Ghati (19), mkazi wa Kijiji cha Nyakunguru, Chacha Mwasi (23), mkazi wa Kijiji cha Bisarwi Komaswa na wengine wawili ambao majina yao hayakutambuliwa.

Wabunge Chadema watinga Tarime
Wabunge wawili wa Chadema, Godless Lema (Arusha Mjini) ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani na Esther Matiko (Viti Maalumu na Waziri Kivuli - Uwekezaji), wamewasili Tarime na kukutana na ndugu wa waliofiwa wakitaka maiti zisichukuliwe hadi uchunguzi wa kina utakapokamilika.

Lema alisema matatizo hayo yanatokea kwa sababu ya mfumo mbovu wa utawala wa nchi kutotii Katiba na sheria zilizopo wakisema mauaji yaliyofanywa hayakustahili kwa kuwa watu walikuwa wanapigwa hadi vichwani.

Alisema chama kitatoa tamko lakini hakishabikii uvunjaji wa amani na kwamba hakipendi kuona watu wanauawa na polisi wenye dhamana ya kuwalinda.

“Hapa tukio si msiba, bali iwe alama ya kudai ukombozi mauaji yakome, maana kijana kama huyu Emanuel Magige kamaliza kidato cha sita anataka kwenda chuo kikuu, leo ameuawa ni hatari! Tunakwena wapi sisi?” Alisema na kuongeza:"Tunataka nchi za Afrika na dunia ziilaani serikali kwa mauji yanayofanywa na vyombo vya dola. Hili nalipeleka bungeni na tunataka iwe mwisho.”

Kwa upande wake, Matiko aliwataka wananchi kuendelea kushikamana kudai haki maana mauaji hayo hayapaswi kunyamaziwa. Alisema watahakikisha haki inapatikana ili iwe fundisho.Maiti zilizobaki ni nne na moja inadaiwa kuchukuliwa usiku kwa gari la serikali hata hivyo, madai hayo hayakuthibitishwa.Kutokana na hali ilivyokuwa Mjini Tarime na viunga vyake, Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mkama ameahirisha mkutano wake mjini hapo.


CHANZO: MWANANCHI MEI 19, 2011
 
Watu hawataki kabisa kuona sare za kijani siku hizi! Kwa upande wa CCM ni wenyewe hasa waliotaka kugeuza mauaji hayo kuwa mtaji wa kisiasa maana walivamia mkutano na mijisare yao bila kualikwa!
 
Safi sana, nguvu ya umma itaamua siku moja. Badala ya kuvaa nguo nyeusi kwa ajili ya maombolezo wao wanajivalia kijani, huyu Nyangwine pamoja na kuandika vitabu vyote hajaelimika tu. CCM mtatafunwa na dhambi ya kuua raia wasio na hatia kwa kutumia vyombo vya dola visivyojua wajibu wao wa kulinda usalama wa raia.
 
Ninachofahamu mkutano wa "Ritongo" unaihusu jamii au koo husika tu kwa sababu wakati mwingine wanazungumza mambo ya kimila, hivyo watu kutoka jamii au koo nyingine hawaruhusiwi, kama wataalikwa watapewa maelekezo muda wa kuingia na watakuwepo kwa muda maalum kulingana jukumu wanalopaswa kutekeleza. Sasa kama mkutano haukumuhusu Mheshimiwa aliweza kuhudhuria bila kualikwa? Hata kama yeye ni Mwakilishi wao kuna mambo ya kimila ambayo hayana uwakilishi na hata yeye hayafahamu kwa sababu sio wa jamii hiyo.
 
Huyu Nyangwine mtu wa ajabu sana. Waliouawa hatujui kama walikuwa wanaccm au chama chochote kile. Kwa nini uende kutoa pole ndani ya magwanda yako ya kijani? Au ndio chama linalotaka kugeuza msiba huo kuwa wa kisiasa aliloshindwa kulitaja Kagasheki!
 
Watu hawataki kabisa kuona sare za kijani siku hizi! Kwa upande wa CCM ni wenyewe hasa waliotaka kugeuza mauaji hayo kuwa mtaji wa kisiasa maana walivamia mkutano na mijisare yao bila kualikwa!

Maisha magumu,shida nyingi kweli watu wakiona ukekaa ki-chama chama lazima wakurukie tu.
 
ni kweli kwa nini uende kwa watu wenye majonzi na sare za chama la magamba na wakati hayo yote yamesababishwa na uonzi mchafu wa serikali yenu ya ccm
 
Wana jf naomba niseme siungi mkono watu kuvamia mgodini,lakini serikali ya ccm iltegemea nini inapowafanya wanatarime kuwa watumwa kwenye ardhi yao?haijifunzi migogoro mingi africa inatokana na unyonyaji wanaofanyiwa wazawa ilipo rasilimali kama vile madini yaliyopo tarime?hivi watu wanapoona wanaumizwa wanahitaji kuhamasishwa na nani kama sio ugumu wa maisha ndio umewafikisha hapo?nataka serakali ya ccm ijifunze kuwa migogoro mingi inakuja kwa sababu ukisikia kuna waasi ujue kuna dhuluma inafanyika,wanatarime wameona mgodi huo hauna faida zaidi ya kuwafanya watumwa kwenye nchi yao, kwanza nimesikitishwa kauli ya kagasheki kuwa wananchi wale wamehamasishwa na wanasiasa wa chama fulani cha upinzani,sio kweli hawanufaiki na mgodi na wamekata tamaa,"can't u imagine mtu anakwenda kupambana na mtu mwenye silaha ya moto akiwa amebeba panga?"hamuoni kuwa wamechoshwa?leo mmeu tarime mkimaliza hapo mtaenda wapi tunaomba ratiba,lakini hii hali itaendelea kama watu wanaozungukwa na rasilimali muhimu hawanufaiki "mungu azilaze mahali pema peponi roho za marehemu ambao walikuwa wakipigana kupinga utumwa kwenye ardhi yao lakini wakauwawa kama wanyang'anyi" naamini ndio kwanza wamepanda mbegu ya ukombozi katika ardhi yao kwa kuwawa kwa risasi za serikali ya ccm .
 
Mimi imeniuma sana kuona watanzania wenzangu wanapigwa risasi na askari wao, imeniuma sana lakini sasa tupige mawe viongozi wote wa ccm kama alivyopigwa nyambari nyangine,wakati ni sasa sisi kujikomboa tuliowatuma wametusaliti kwa kumwaga damu za ndugu zetu
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom