Fanyia kazi haya ambayo

emma115

Senior Member
Apr 28, 2012
135
167
UCHAMBUZI WA KITABU; THE TOTAL MONEY MAKEOVER

Kwa dunia ya sasa, hakuna siku inayopita bila ya wewe kuhitajika kutumia fedha. Fedha ni sehemu muhimu ya maisha yetu ya kila siku, kwani kila tunachofanya kwenye maisha yetu, kinahusisha fedha. Hata unapokwenda kwenye nyumba za ibada, unategemewa kutoa sadaka au zaka kulingana na utaratibu wa imani yako

tmmo_hardcover.jpg

Licha ya umuhimu huu wa fedha kwenye maisha yetu ya kila siku, bado watu wengi sana wanateseka na fedha. Watu wengi wanaishi maisha magumu kutokana na kukosa elimu na maarifa sahihi juu ya fedha. Watu wengi wamefundishwa kitu kimoja tu, namna ya kupata fedha.

Lakini kuna vitu viwili muhimu wanakosa, namna ya kutumia fedha hizo na namna ya kuzifanya ziwafanyie kazi.

Mwandishi na mwendeshaji wa vipindi vya redio na tv Dave Ramsey, alipitia hili kwenye maisha yake. Kutokana na kukosa elimu sahihi ya fedha, aliweza kuwa milionea mara mbili kwenye maisha yake lakini akafilisika kabisa. Ni baada ya kukaa chini na kutafuta dawa ya matatizo yake, aliweza kuandaa mwongozo wa uhakika wa kumfikisha kwenye uhuru wa kifedha, yaani utajiri.

Kupitia kitabu chake hichi cha THE TOTAL MONEY MAKEOVER, Ramsey anatushirikisha mwongozo huu. Nitakuchambulia mwongozo huu hapa na ukiweza kuuishi na kufanyia kazi kwenye maisha yako, hutabaki hapo ulipo sasa. Utasahau kuhusu madeni na utakuwa na maisha bora na yenye furaha.
Karibu sana tujifunze kwa pamoja.

Matatizo yako ya fedha unasababisha wewe mwenyewe.

Mwandishi Dave Ramsey anasema kwamba matatizo yako ya fedha hayasababishwi na serikali, uchumi, bosi au kitu kingine chochote. Bali matatizo yako ya kifedha yanasababishwa na wewe mwenyewe. Ramsey anasema kujua hili ndiyo kulimpa uhuru mkubwa sana wa maisha yake.

Anasema ukitaka kumwona adui wako wa kifedha, simama mbele ya kioo, utamwona adui huyo anakuangalia.

Matatizo yako ya kifedha kwa asilimia 80 yanasababishwa na tabia zako na asilimia 20 yanasababishwa na kukosa maarifa sahihi. Hivyo kama unataka kuweka mambo yako ya fedha sawa, pamoja na kujifunza, bado una kazi kubwa ya kuweka tabia zako sawa.

Na kweli ukiangalia, kwa nini watu wanaingia kwenye madeni? Jibu ni rahisi, watu wanataka kununua vitu ambavyo hawawezi kuvimudu. Unataka kitu ambacho huna uwezo wa kukilipia, hivyo unashawishika kukopa uje kulipa baadaye. Hii inakuwa tabia na mwishowe unakuwa na madeni sugu.


Anza kufanyia kazi tabia zako kuhusu fedha, wakati huo pata maarifa sahihi ya kifedha. Hii ndiyo njia yako ya kuelekea kwenye utajiri.

Unahitaji mapinduzi makubwa ya kifedha.

Ili kutoka hapo ulipo sasa kifedha, mwandishi anasema unahitaji vitu vitatu vikubwa.
Kwanza unahitaji kuwa tayari kuishi tofauti na wengine wanavyoishi sasa, ili baadaye uweze kuishi tofauti na wengi wanavyoishi. Mwandishi anasema watu wengi kwenye jamii wanaishi kwa kuangalia wengine, wananunua vitu ili waonekane nao wanakwenda na wakati. Huu umekuwa mzigo mkubwa kwa wengi.

Pili unahitaji kuweka juhudi kubwa, unahitaji kuwa na vipaumbele na kuvifanyia kazi bila ya kuchoka. Kuna wakati utahitajika kufanya kazi masaa mengi zaidi ya kawaida. Kuna wakati utahitaji kufanya kazi zaidi ya moja. Na pia kuna wakati utahitaji kusema hapana kwa mambo yenye faida ya haraka lakini baadaye siyo mazuri.

Tatu unahitaji muda. Mwandishi anasema mwongozo wake siyo njia ya kutajirika haraka, hivyo kama unatafuta njia ya kutajirika haraka umeshapotea. Mpango wake unahitaji miaka saba mpaka kumi ya kuweza kufikia utajiri ambao utadumu nao kwenye maisha yako yote.
Je upo tayari kwa vitu hivi vitatu? Kama ndiyo karibu tuanze na vikwazo vitano vinavyowazuia watu kufikia utajiri.

Kikwazo cha kwanza; kukanusha kwamba una tatizo la fedha.

Mwandishi anatuambia watu wote wanaoingia kwenye matatizo ya kifedha, huwa wanakana kwamba hawana matatizo ya kifedha. Wengi huwa wanajiona wapo vizuri kabisa kifedha, kabla ya kujikuta kwenye matatizo makubwa sana kifedha.

Anatupa mfano wa mwajiriwa ambaye mshahara wake ni mzuri, na hivyo kutumia mshahara huo kukopa gari na nyumba. Anaona kila kitu kipo sawa kwake kifedha mpaka siku anapofukuzwa au kupunguzwa kazi. Hapo anajikuta kipato chake kimekauka na huku ana madeni ambayo bado hajakamilisha kulipa.

Mwandishi ametoa mifano ya wengi na hata kwake binafsi, kununua vitu vingi kwa mkopo na hivyo kujikuta na mikopo mingi. Kabla ya matatizo kutokea, watu huona mikopo siyo tatizo kwao. Mwandishi anatuma njia ya uhakika ya kuweza kuondoka kwenye mikopo hii na kuwa na uhuru wa kifedha, ila kwanza lazima tukiri tuna matatizo ya kifedha.
Je unakubali hapo ulipo kifedha kama bado hujajijengea uhuru wa kifedha upo hatarini? Kama ndiyo basi tuendelee kujifunza. Kama unaona haupo kwenye hatari yoyote, unaweza kuishia hapa kwa sasa, mpaka pale utakapokutana na hatari halisi ndiyo utakumbuka kurudi hapa, lakini pia utakuwa umechelewa sana.

Kikwazo cha pili; imani mbovu kuhusu madeni.

Mwandishi anasema uongo ukisemwa mara nyingi, na kurudiwa rudiwa kila mara watu wanaanza kuuamini kama ukweli.

Anasema moja ya uongo ambao umeshasemwa na sasa watu wanauamini ni kuhusu madeni. Watu wanaamini madeni ni sehemu ya maisha ya kila siku. watu mpaka wanasema kabisa, huwezi kuishi bila madeni, au bila kukopa huwezi kufanikiwa au kufanya makubwa.

Mwandishi anarudi nyuma na kutukumbusha ya kwamba mtu anapokopa anakuwa mtumwa wa yule ambaye amemkopesha. Na katika biashara ya ukopeshaji, yule anayekopesha ananufaika mara dufu kuliko anayekopa.

Mwandishi anasema watu wanatumia fedha ambazo hawana, kununua vitu ambavyo hawavihitaji, kuwafurahisha watu ambao hawana muda nao. Yaani mtu ananunua vitu kwa mkopo ili aonekane na yeye ana vitu hivyo au ana uwezo, wakati wale anaowaonesha wala hawajali.


Mwandishi anatukumbusha kwamba mkopo hasa ambao hauzalishi, haujawahi kuwa na faida hata siku moja kwa mkopaji. Kama unapoka ili kununua gari ya kutembelea, au nyumba ya kuishi, au vyombo vya ndani, nguo na vinginevyo, jua tu umewanufaisha wengine na wanakunyonya wewe.

Kazi kubwa ya kwanza tunayopaswa kufanya ni kuvunja imani hii mbovu kuhusu madeni na kuondokana nayo kabisa.

Kikwazo cha tatu; imani mbovu kuhusu fedha.

Mwandishi anatuambia hakuna kitu kinawazuia watu kutajirika kama imani mbovu ambayo watu wanayo kuhusu fedha. Anasema watu wengi wanapotea sana kwa kuamini ipo siri kubwa ya utajiri, siri ambayo wao hawajui ila matajiri wanaijua. Wanaamini wakijua siri hiyo basi watakuwa matajiri kwa haraka na kwa urahisi.

Mwandishi anasema ukienda sehemu inapochezwa michezo ya bahati nasibu au kamari, wengi waliopo ni masikini. Wengi wanaamini ipo siku watapata bahati na kuwa matajiri.

Imani nyingine mbovu ambayo watu wanayo kuhusu fedha, hasa waajiriwa ni kuamini kwamba wakishastaafu basi watapata pensheni zao na maisha yatakuwa safi sana. Lakini muda unapofika ndipo wanagundua walikuwa wakijidanganya wao wenyewe.

Mwandishi anatukumbusha ya kwamba hakuna siri ya utajiri ambao watu wachache pekee ndiyo wanaijua. Kanuni za utajiri ni zile zile, unahitaji kuweka juhudi kubwa, unahitaji kujipa muda wa kutosha ili kufika pale unapotaka kufika.

Kikwazo cha nne; ujinga, kukosa maarifa sahihi kuhusu fedha.

Hakuna mtu aliyezaliwa anajua chochote, kila kitu tumejifunza hapa duniani. Lakini kwenye swala la fedha, wengi wamekuwa wajinga kwa sababu hawajifunzi. Wanajua kidogo na wanatumia kidogo hicho kutaka kufanya makubwa. Wanashindwa na kuishia kupata matokeo mabaya.

Mwandishi anasema watu wamefundishwa namna ya kupata fedha, kupitia kazi mbalimbali walizojifunza kufanya. Lakini wakishapata fedha hizo, hawajafundishwa wanapaswa kuzitumiaje ili waweze kutajirika. Wengi wanaishia kwenye madeni na maisha yao yanakuwa magumu mno.

Kikwazo cha tano; kuishi maisha ya kuiga.

Mwandishi anasema hakuna kitu kinawarudisha watu nyuma kama kuishi maisha ya kuiga. Watu wananunua vitu ambavyo hawawezi kuvimudu ili tu waonekane nao wapo, waonekane wana uwezo.

Mwandishi anatuambia kama tunataka kutoka kwenye matatizo ya kifedha ambayo tunayo, lazima tuache kuiga maisha ya wengine. Lazima tuchague kuishi maisha yetu wenyewe. Lazima tuwe tayari kuchekwa na kuonekana washamba au wa chini lakini sisi tunajua ni wapi tunaenda.

Mwandishi anatukumbusha kama tutakuwa tayari kuishi tofauti na wengine wanavyoishi sasa, baadaye tutaweza kuishi tofauti na wengine wanavyoweza kuishi.

Hivyo ndiyo vikwazo vitano vinavyowafanya wengi kubaki kwenye umasikini. Ni muhimu kuvijua na kuviangalia hapo ulipo sasa ili uweze kuondokana navyo.

Hatua saba za kuelekea kwenye uhuru wa kifedha.

Mwandishi anatushirikisha hatua saba za uhakika kabisa za kufikia uhuru wa kifedha au utajiri kwenye maisha yetu. Hatua hizi ni rahisi na yeyote anaweza kuzifuata, bila ya kujali anaanzia wapi. Karibu tujifunze hatua hizi saba;

Hatua ya kwanza; weka akiba ya milioni moja kama fedha ya dharura.
Mwandishi ameshauri kwa dola za marekani elfu moja, ambapo tukizileta kwa fedha za Kitanzania ni kama milioni mbili. Mimi nakushauri uanze na milioni moja.

Mwandishi anasema hivi; popote pale ulipo sasa, pambana vyovyote uwezavyo, uweze kuweka akiba ya milioni moja. Pambana usiku na mchana, ongeza muda wa kufanya kazi, ongeza biashara ya pembeni na punguza matumizi yasiyo muhimu. Lengo ni uwe na akiba ya milioni moja, hii ni fedha ya dharura.

Fedha hii unaihitaji sana kabla hujaenda hatua ya pili kwa sababu bila fedha hii hatua ya pili inaweza kukushinda. Mwandishi anasema usiweke mpango mwingine wowote kama hujaweka akiba hii ya milioni moja.
Akiba hii iweke kwenye akaunti maalumu ambapo haitakuwa rahisi kwako kuchukua fedha hiyo.

Hatua hii ya kwanza itakuchukua mwaka mmoja kukamilisha. Inaweza kuwa chini ya hapo pia kulingana na juhudi zako.

Hatua ya pili; lipa madeni yako yote, kasoro deni hili moja.

Mwandishi anatupa hatua ya pili ya kuelekea kwenye utajiri, hatua hii ni kulipa madeni yote ambayo mtu unadaiwa. Anasema kwenye hatua hii lazima ulipe madeni yote kasoro deni la nyumba kama ulikopa. Madeni mengine madogo madogo yote yalipe kwenye hatua hii.

Mwandishi anatufundisha kwamba tuchukue karatasi na kalamu na kuorodhesha madeni yote ambayo mtu unadaiwa, yapange kwa kuanza na madeni madogo na kuenda makubwa. Bila ya kujali riba, anza na yale madogo. Ukishayaorodhesha anza kulipa yale madogo. Anasema kwa kufanya hivi utaanza kuona matokeo mapema. Kadiri unavyolipa madeni yako utapata hamasa ya kuendelea zaidi.


Mwandishi anatuambia ikiwa katika hatua hii umejikuta umepata dharura na kutumia ile fedha ya dharura na ikawa chini ya milioni moja, basi acha hatua hii na rudi kuijazia fedha ya dharura mpaka ifikie milioni moja.

Wakati unafanya zoezi hili la kulipa madeni, kamwe kamwe usikope, kwa vyovyote vile usikope. Sasa unaondoka kwenye madeni, usiyakaribishe tena. Tumia njia yoyote mbadala kuepuka kukopa.

Madeni makubwa kama ya nyumba yana hatua yake mbeleni ya kuyalipa. Katika hatua hii yasikuumize kichwa, maliza yale madogo madogo kwanza.

Hatua hii ya kulipa madeni inaweza kukuchukua miaka miwili mpaka mitatu, inategemea na madeni yako na juhudi zako katika kuyalipa.
Hatua ya tatu; kamilisha mfuko wako wa dharura.

Ukishamaliza kulipa madeni yote unayodaiwa, kasoro deni kubwa la nyumba, sasa rudi kukamilisha mfuko wako wa akiba ya dharura. Ile milioni moja uliyoweka kama akiba ya dharura siyo kwamba umemaliza.

Washauri wa fedha na uchumi wanasema mtu anapaswa kuwa na akiba ya kuweza kuendesha maisha yake kwa miezi mitatu mpaka sita hata kama hana kipato kabisa. yaani iko hivi, ikitokea leo kipato chako kimekatika kabisa, basi unahitaji uwe na akiba ya kuendesha maisha yako kwa miezi sita bila wasiwasi wowote.

Hivyo angalia matumizi yako yote kwa mwezi ni kiasi gani, kisha zidisha mara sita na hiyo ndiyo akiba unapaswa kuwa nayo kama dharura. Kama matumizi yako kwa mwezi ni laki tano, basi unahitaji kuwa na akiba ya milioni tatu kama dharura. Kama matumizi yako ni milioni moja kwa mwezi, basi unahitaji kuwa na akiba ya milioni sita kama fedha ya dharura.

Mwandishi anasisitiza ni muhimu sana uwe na fedha hii ya dharura, maana hii ndiyo itakuzuia kurudi kwenye madeni na umasikini. Dharura zinatokea na mbaya zaidi zinatokea wakati ambapo hutaki kabisa zitokee, ni sawa na huna kazi halafu unapata ugonjwa unaohitaji fedha nyingi za matibabu. Hapa ndipo watu wanajikuta wamerudi tena kwenye madeni.

Iwe umeajiriwa, umejiajiri au unafanya biashara, unahitaji mfuko wako wa akiba ya dharura uwe na kiasi cha fedha kukuwezesha kuishi miezi sita ikitokea kipato chako kimeathiriwa. Hii itakupa amani ya moyo na kukupa uhuru wa kuweka juhudi za kuelekea kwenye utajiri.

Hatua hii inaweza kuchukua mwaka mmoja mpaka miwili. Kama umeshamaliza madeni, basi unaweza kufanya hatua hii kwa muda mfupi zaidi.

Hatua ya nne; wekeza kwa ajili ya kustaafu kwako.

Najua unajua kwamba hutaweza kufanya kazi unayofanya kwa miaka yako yote. Kuna wakati utachoka na kuhitaji kupumzika. Mwandishi anatuambia tuanze kujiandaa sasa kwa wakati huo.
Mwandishi anatuambia hatua ya nne ya kuelekea kwenye utajiri ni kuwekeza asilimia 15 ya kipato chako cha kila mwezi kwenye akaunti yako ya kustaafu. Kwa nchi kama marekani zipo akaunti maalumu za kujiandaa kustaafu. Achana na ile mfuko ya kijamii. Hapa kwetu akaunti hizi siyo maarufu, hivyo utahitaji kutengeneza uwekezaji wako mwenyewe.

Wekeza kwenye hisa, vipande, hati fungani, ardhi na hata majengo. Pia unaweza kuwekeza kwenye biashara mbalimbali, lengo ni baadaye uwekezaji huu ukuwezeshe kuishi maisha yako vizuri hata kama hufanyi kazi. Yaani uwekezaji uwe unakuzalishia faida ya kukutosha kuendesha maisha yako.

Mwandishi anatukumbusha kutotegemea moja kwa moja fedha za mafao za mifuko ya kijamii, nafikiri umekuwa unaona namna wengi wanasumbuliwa na mafao yao, na kadiri kila siku sheria za mafao zinabadilishwa. Sasa wewe jiandae ki vyako kwa ustaafu wako, ikitokea umepata mafao basi una faida mara mbili, na ukiyakosa, maisha yako hayatakuwa mabaya maana ulijiandaa.
Hili ni zoezi endelevu ambapo kila mwezi tenga asilimia 15 ya kipato chako na wekeza. Isiwe chini ya hapo, maana utachelewa kufikia uhuru wa kifedha. Pia isiwe zaidi ya hapo, maana kuna mengine muhimu bado unahitaji kuyafanya.

Hatua ya tano; lipa ada ya chuo kwa watoto wako.

Mwandishi anatukumbusha ya kwamba hakuna kitu kinasumbua kama mikopo ya elimu hasa kwenye elimu ya juu. Hivyo anatukumbusha kuanza kujiandaa mapema. Kama una watoto, anza kuwekeza kwa ajili ya elimu zao. Hakikisha unajiandaa kiasi cha kuweza kumsomesha mtoto wako mpaka chuo kikuu. Usitegemee kuja kupata mkopo wa kumsomesha, jiandae na msomeshe mwenyewe.

Mwandishi pia anatukumbusha tunapopeleka watoto vyuoni tuwapeleke kwa lengo la kuelimika na waweze kuchagua maisha yao. Tusiwapeleke kama vitega uchumi, kwamba unamsomesha mtoto ili apate kazi na baadaye akulipe fadhila. Mambo haya walifanya wazazi wako, wewe usiyafanye kwa watoto wako. Mambo yamebadilika sana, kusoma siyo tiketi ya kupata kazi au mafanikio.
Hii pia ni hatua endelevu na inategemea umeianza wakati gani.

Hatua ya sita; lipa deni la nyumba, au deni kubwa lingine ambalo unalo.

Kama ulikopa nyumba, kitu ambacho ni maarufu kwa nchi za wenzetu, deni hili huwa ni kubwa na la muda mrefu, kama miaka 15 mpaka 30. Mwandishi anasema gharama ya deni hili ni kubwa sana. Anashauri mtu upange upya kulipa mkopo huu ndani ya muda mfupi kuliko ulivyopanga kulipa.

Hivyo kama una mkopo mkubwa ambao unalipa kwa muda mrefu, zaidi ua miaka mitano au kumi, kaa chini na wale wanaokudai kisha panga kulipa haraka ziadi. Maliza mkopo huo kwa nusu ya muda uliopanga kulipa. Kwa mfano kama mkopo ulikuwa wa miaka kumi, basi ulipe ndani ya miaka mitano.

Hatua hii ni ya kukamilisha usafi kwenye nyumba yako mpya ya utajiri. Unafuta kila aina ya deni kwenye maisha yako, na unakuwa tajiri wa ukweli, tajiri ambaye hana deni.

Kuanzia hatua ya kwanza mpaka hii hatua ya sita, inakuchukua miaka saba mpaka tisa kukamilisha hatua hizi. na Baada ya hapo sasa ipo hatua ya saba na ya mwisho, ambayo ni kutengeneza utajiri kama kichaa.

Hatua ya saba; TENGENEZA UTAJIRI.

Baada ya kuondokana na changamoto zote za kifedha, hapa sasa ndipo safari ya utajiri inapoanza rasmi. Hapa ndipo unakuwa umeondokana kabisa na mambo yote yaliyokuwa yanakurudisha nyuma na kukuzuia kufanikiwa.

Mwandishi anatuonya kwamba wengi wakifika hatua ya sita huwa wanajisahau na kujikuta wamerudi tena nyuma. Hatua hii ya saba ni muhimu sana katika kufikia uhuru kamili wa kifedha kwenye maisha yetu.
Katika hatua hii ya saba, mwandishi anatuambia matumizi ya fedha ni matatu tu;

Moja; kufurahia maisha, hakuna maana kukazana upate fedha nyingi halafu ushindwe kuyafurahia maisha yako. Tumia fedha zako kuyafurahia maisha, hii itakupa hamasa ya kupata nyingi zaidi.

Mbili; kuwekeza, utajiri siyo kilele kwamba ukishafika basi ndiyo umefika, unahitaji kuendelea kuwekeza ili uendelee kubaki kwenye utajiri wako. Hivyo ni muhimu sana kuendelea na uwekezaji.

Tatu; kuwasaidia wengine, wewe kupata fedha na kuwa tajiri, kunapaswa kuwa msaada na neema kwa wengine. Wasaidie wale wenye uhitaji na utabarikiwa zaidi na zaidi kwenye utajiri wako.

Hizo ndizo hatua saba za kutoka popote ulipo na kufikia utajiri, ishi hatua hizo kila siku na maisha yako yatakuwa bora kama utakavyo.

Jambo muhimu kabisa kukumbuka ni kwamba juhudi zinahitajika, na uvumilivu ni muhimu. Inahitaji muda kuweza kufika hapo, na yeyote ambaye yupo tayari, hakuna kitakachoweza kumzuia kufika kwenye utajiri.

Umeshavijua vikwazo vitano vinayokufanya usiwe tajiri, na umezijua hatua saba za kuelekea kwenye utajiri, swali ni je utaanza safari hii ya kuelekea kwenye utajiri?

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom