Familia 289 za waathirika wa mafuriko zatua Mabwepande

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,299
33,079
Hama(1).jpg

Mmoja wa waathirika wa mafuriko, Stephen Katumba, akiwa na familia yake, Sophia Kioza na mtoto Angela Stephen, wakitua mizigo muda mfupi baada ya kuwasili katika makazi mapya ya Mwabwepande, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam jana. (PICHA OMAR FUNGO)


Waathirika wa mafuriko waliokuwa wamehifadhiwa kwenye makambi ya Mbweni JKT na baadhi waliokuwa kwenye kambi ya JKT Mgulani, wamehamishiwa rasmi jana kwenye makazi mapya katika eneo la Mabwepande, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika eneo hilo, Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, Said Meck Sadick, alisema jumla ya kaya 289 zenye idadi ya watu 750 zilihamishiwa Mabwepande.

“Leo ndio tumeanza safari ya kukamilisha agizo la Rais la kuwapatia waathirika wa mafuriko makazi mbadala ya kuishi, ili waishi maisha ya kiutu zaidi, hivyo leo tumeanza rasmi zoezi la kuwahamishia hapa, baada ya kwanza kuwatoa kule mashuleni, kwenye kambi za awali, na baadaye kwenye kambi za JKT Mgulani, JKT Mbweni na kule Ubungo Maziwa,” alisema.

Sadick alisema leo zoezi la ujenzi wa kambi kwa ajili ya waathirika ambao hawajahamishwa litaanza na litakapokamilika waathirika wanaoendelea kuishi katika kambi ya JKT Mgulani na Ubungo Maziwa watahamishwa.

Aidha, Sadick alisema zoezi hilo linatarajiwa kukamilika katika kipindi cha wiki moja na jumla ya kaya 556 zinazotarajiwa kuhamia hapo zimekwisha hakikiwa ili kuepuka watu kugawiwa viwanja zaidi ya mara moja ingawa katika uhakiki wa kwanza jumla ya kaya zilizojiandikisha ili kupewa viwanja hivyo ilikuwa ni 659.

Sadick alifafanua kuwa utaratibu uliotumika kugawa viwanja hivyo ni wa kupiga kura na kugawa namba, hivyo hata kama mtu atakuwa wa mwisho kuhamishiwa eneo hilo, atakikuta kiwanja chake kikimsubiri.

Alisema mtu akishapewa eneo lake anapigwa picha pamoja na familia yake na kupewa hati yake, na viwanja vyote ni vizuri kwani vimepimwa na vipo sawa.

Kuhusu chakula, Sadick alisema utaratibu wa kuwapikia chakula cha pamoja utaendelea, lakini kuanzia leo kila kaya itaanza kujipikia, kwani watapewa mgao wao wa chakula.

Akizungumzia huduma ya maji, Sadick alisema, maji yapo ya kutosha, kwani kuna matanki ya lita 5,000 ya kutosha na yatakuwa yanajazwa kila baada ya siku tatu na kwamba kuna visima vitatu tayari vimechimbwa ambavyo maji yake yamepelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ili yapimwe na kuona kama ni salama, na wanategemea kupata majibu mapema iwezekanavyo.

Aidha, alisema Shirika la Umeme nchini (Tanesco), wamekwisha weka nguzo na nyaya za umeme na wameahidi ya kuwa umeme utapatikana katika kipindi cha wiki mbili zijazo.

Sadick alisema wanafunzi wote, wataanza kwenda shule kuanzia leo katika Shule ya Msingi Mabwepande na Sekondari, na amekwishaongea na Ofisa Elimu ili aongeze idadi ya walimu kwenye shule hizo, sambamba na ongezeko la wanafunzi pamoja na ujenzi wa madarasa mapya, na kwamba Kampuni ya Home Shopping Center, imekwishaanza ujenzi wa shule ya sekondari ambayo wamemhakikishia kuimaliza baada ya wiki mbili.

Akijibu swali la mwandishi wa habari aliyetaka kujua juu ya huduma za afya na mustakabali wa waathirika ambao ni wapangaji, Sadick alisema kuna jengo tayari wamelikodi ambalo litatumika kama zahanati, na tayari mpango wa kuleta madaktari upo mbioni.

“Tumeanza kutekeleza agizo la Rais kwa kuwaangalia hawa wenye nyumba kwanza, baada ya hapo tutawaangalia wale waliojenga kwenye mabonde, ili na wao wapate viwanja, na baadaye tutawaangalia wapangaji, ingawa zoezi kwa upande wao litakuwa gumu kwani katika nyumba zilizojengwa mabondeni, wengi wao wanakiri kuwa walikuwa wanaishi kwenye chumba kimoja mpaka watu kumi, sasa hapa itatupa shida kidogo, sasa hawa wote tutawapa viwanja wakati jumla yao inafikia watu 3,000?,” Alihoji.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema wakati wanasubiri kituo cha polisi kujengwa, hema moja litatumika kama kituo cha polisi, na polisi hao watafanya kazi ya ulinzi usiku na mchana watatumika kama walimu wa kufundisha ulinzi shirikishi.




CHANZO: NIPASHE
 
Eh?
Naona mipango chungu mbovu, hongera wahusika kwa mlichokifanya!
 
Back
Top Bottom