EPA na mambo yake

Kada wa CCM alikiri kuchota mamilioni BoT’
Shadrack Sagati na Neema Mgonja
Daily News; Thursday,November 20, 2008 @21:15

Upande wa mashitaka katika moja ya kesi za ufisadi umeiambia mahakama kuwa mmoja wa washtakiwa katika kesi ya ufisadi, Rajabu Shaban Maranda, alikiri kushirikiana na maofisa watatu wa Benki Kuu (BoT) kuchota mamilioni ya fedha.

Maranda ambaye ni Mweka Hazina wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Kigoma anashtakiwa kwa kuiba Sh milioni 207 kutoka katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) kwa kutumia kampuni ya Rashhas.

Akisoma maelezo ya awali, Wakili wa Serikali Boniface Stanislaus aliiambia mahakama hiyo kuwa mshtakiwa baada ya kukamatwa na kuhojiwa na vyombo vya dola alikiri kufanya wizi huo wa Sh milioni 207.3.

Akielezea mwanzo wa kampuni iliyotumika kuchotea mamilioni hayo ya fedha, wakili huyo alidai kuwa Maranda kwa mara ya kwanza alisajili kampuni ya Rashhaz Tanzania Ltd kwa msajili wa kampuni na Mkurugenzi mwenzake aliyetajwa kuwa ni Maranda Rajabu Maranda.

Alidai kuwa ukusanyaji wa madeni haikuwa kazi ya kampuni ya Rashhaz tangu isajiliwe na haikuwahi kubadili kazi zake ambazo zimeandikishwa Brela. Aliendelea kudai kuwa Desemba 10, 2004 Maranda aliwasilisha waraka Benki Kuu ukimtaja

Jaffer Hussein Jaffer kuwa ni mmoja wa wakurugenzi wa kampuni ya Rashhas (T) Ltd na kwamba kampuni hiyo ilikuwa imeteuliwa na kampuni ya General Marketing ya India kukusanya deni la dola za Marekani 1,252,480.48.

Mbele ya Hakimu Mkazi wa Kisutu Hezron Mwankenja, wakili huyo alidai kampuni ya Rashhaz na Rashhas ni vitu viwili tofauti; lakini Maranda kwa kutumia udanganyifu alidai kuwapo kwa mabadiliko ya wakurugenzi na kumwingiza Jaffer kuwa ni mmoja wa wakurugenzi wa Rashhas wakati ni uongo.

Alidai miezi saba baadaye Maranda Julai 14, 2005 alitumia jina la Jaffer kama mmoja wa wakurugenzi wa Rashhas akaandika barua kwa Gavana wa BoT akimjulisha kuwa kampuni yake hiyo imepewa jukumu na kampuni ya General Marketing ya India kudai rupia 8,141,123.09.

Agosti 11 maofisa wawili wa BoT waliokuwa Kitengo cha Madeni Iman Mwakyosa na Esther Mary Komu waliidhinisha deni hilo kulipwa kwa kampuni feki ya mshtakiwa. Alidai maofisa hao waliidhinisha kwa makusudi malipo hayo licha ya kuwa barua iliyoandikwa na kampuni ya Rashhas iliomba ilipwe dola za Marekani wakati fedha iliyokuwa inadaiwa katika akaunti ya EPA ilikuwa ni rupia ya India.

Kwa upande wa mshtakiwa wa nne Bosco Kimela ambaye alikuwa Katibu wa BoT inadaiwa aliidhinisha malipo hayo kufanywa na akashauri barua ya maombi iandikwe na iombe kulipwa fedha za rupia na sio dola za Marekani kama ilivyokuwa katika barua ya awali.

Alidai Agosti 12, 2005 Mwakyusa na Komu walimtaarifu Maranda kuwa maombi yake yamekubaliwa na BoT, lakini wakamshauri akaandike barua inayoonyesha kutaka alipwe fedha za rupia 8,141,123.09 na aiwasilishe haraka na sio malipo ya dola.

Baada ya kuelezwa hivyo siku hiyo hiyo Maranda akitumia jina la Jaffer kama Mkurugenzi wa Rashhas aliwasilisha barua mpya BoT ya maombi ikionyesha kuwa ilisainiwa mjini Mumbai, India Julai 12, 2004 na kushuhudiwa na wakili aliyetajwa M.V Shinde wa Mahakama Kuu ya Mumbai, India.

Lakini barua hiyo haikuwa imesainiwa na ofisa yeyote wa Rashhas lakini Maranda akaithibitishia benki hiyo kuwa nyaraka hiyo ilikuwa halali kisheria. Baadaye Agosti 15, 2005 BoT iliidhinisha malipo kwa kampuni halali ya Rashhaz na kupitishia fedha hizo katika akaunti zake ambazo Maranda alizichukua katika mikupuo minne.

Hata hivyo washtakiwa wote wanne walikubali majina yao na nafasi zao lakini walikana maelezo yote yaliyosomwa na Wakili wa Serikali. Mshtakiwa wa pili alikana kuwa na cheo cha Kaimu Mkuu wa Idara ya Madeni BoT. Upande wa mashitaka umeiambia mahakama hiyo kuwa unatarajia kuwaita mashahidi 16 akiwamo Naibu Msajili wa Kampuni (Brela) Andrew Mkapa kutoa ushahidi katika kesi hiyo.

Miongoni mwa mashahidi hao yumo Twilumba Tawara wa Benki ya Kenya (KCB) na Ronald Manongi wa Commercial Bank of Afrika (CBA) ambako BoT ilipitishia fedha hizo kwa ajili ya kulipwa kwa Maranda. Wamo pia maofisa wa BoT ambao ni Emmanuel Boazi, Tamali Mwakilema, Elisa Kisangya, Peter Noni, Rashid Mwanga, Samwel Mark, Athumani Mtengeti na Stela Chaula.

Wengine ni maofisa wa Polisi SP Mkonyi na ASP Salumu Kisali. Pia wengine ni mmoja wa wakurugenzi wa Rashhaz, Jaffer Hussein Jaffer ambaye jina lake lilitumiwa kufanyia wizi huo na Joseph Sheffu Mkaguzi wa Hesabu wa Kampuni ya Ernst and Young. Upande wa mashitaka uliiambia mahakama kuwa aliyetoa taarifa za wizi huo ni Sheffu ambaye ni mkaguzi ambaye kampuni yake iligundua wizi huo. Kesi hiyo itaanza kusikilizwa Januari 20.
 
Je wamewashtaki na sheria ya uhujumu uchumi (1984)? make hiyo sheria inasema hakuna mambo ya blah blah za dhamana. Kwa mtizamo wangu naona kama hii sheria nayo ilikuwa inaingia katika makosa wanayoshtakiwa. Mwendesha mashtaka makini unapanua wigo wako wa mashtaka hili mwisho wa siku unakuwa umejiweka katika mazingira mazuri kikesi.

Au ndo dili kama Mama Mia anavyosema hapo juu kwamba watu wanastruck dili kuwapumbaza wadanganyika?

Kazi kweli kweli.
 
kwa wastani wa laki laki, then ni watu 1040 waliomchangia, sasa ukiirekebisha hiyo hesabu, kwa kuwa umesema watu wengine walitoa elfu kumi kumi, unaweza kukuta watu kama elfu mbili mpaka tatu au hata zaidi walimchangia.

Mzee usikute hii kikao ilikuwa diamond...........
 
Watuhumiwa wa ufisadi waonyesha jeuri ya fedha
Neema Mgonja
Daily News; Friday,November 21, 2008 @20:10

Pamoja na masharti magumu yaliyowekwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, dhidi ya washitakiwa wa kesi za wizi wa mabilioni ya fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), ni washitakiwa wawili tu kati ya 20 wamebaki rumande bila kudhaminiwa.

Baadhi ya washitakiwa katika kesi hiyo wamelazimika kutoa mamilioni ya fedha taslimu mahakamani kukidhi sharti la dhamana ili waweze kuwa nje; huku wengine wakiwasilisha hati za mali zenye thamani ya mabilioni ya fedha.

Kada wa CCM Shaban Maranda, ambaye kesi yake ilihitaji alipe fedha taslimu za dhamana, alitimiza sharti hilo kwa kuweka Sh milioni 104 hivyo mahakama kumpa dhamana baada ya kukaa rumande kwa takribani wiki mbili.

Juzi aliyekuwa Kaimu Katibu wa BoT, Bosco Kimela naye alipata dhamana baada ya kuwasilisha fedha taslimu Sh milioni 104 ambazo zilitosha kumweka nje. Washitakiwa hao wawili pamoja na aliyekuwa Mkurugenzi wa Madeni ya Nje Ester Mary Komu, ambao kesi yao iko mbele ya Hakimu Mkazi Hezron Mwankenja, ndio ambao masharti ya dhamana yalitamkwa yawe ya fedha taslimu.

Komu tayari alishaweka kiasi hicho cha fedha tangu wiki iliyopita na sasa yuko nje kwa dhamana. Mshitakiwa aliyebaki katika kesi hiyo inayoelezwa kuwa ndio pekee yenye sharti gumu ni Iman Mwakyosa anayedaiwa alikuwa Mkuu wa Kitengo cha Madeni, cheo alichokikana juzi.

Mshitakiwa mwingine katika moja ya kesi hizo za ufisadi ambaye hajapata dhamana ni Farijala Hussein, ambaye katika kesi yake anashitakiwa pamoja na Maranda na maofisa wengine watatu wa BoT. Katika kesi hiyo iliyoko mbele ya Hakimu Mkazi Wariaulwande Lema, Farijala na mwenzake Maranda wanadaiwa kuiba Sh bilioni 2.3. Katika kesi hiyo washitakiwa hao wanadaiwa kushirikiana na maofisa wa BoT Komu, Mwakyosa na Sofia Joseph.

Tayari Sofia, Komu na Maranda wameshapata dhamana kwenye kesi hiyo baada ya kuwasilisha hati zenye thamani ya kiasi hicho kinachodaiwa kuibwa. Lakini Farijala na Mwakyosa bado wanaendelea kusota rumande.

Sharti la dhamana katika kesi hiyo ni kuwasilisha hati ya mali yenye thamani nusu ya fedha wanazodaiwa kuiba. Farijala alishindwa kupata dhamana jana kutokana na barua ya mmoja wa wadhamini wake kukataliwa na mahakama kutokana na kuwa na dosari kadhaa ambazo hazikidhi sifa ya kumdhamini mtuhumiwa.

Washitakiwa wengine ambao wako nje kwa dhamana ni Jeetu Patel, Amit Nandy, Ketan Chohan, Vinodbhai Patel, Bahati Mahenge, Davies Kamungu, Manase Mwakale, Eddah Mwakale, Japhet Lema, Ajay Somani, Jai Somani, Johnson Lukaza, Mwengesi Lukaza, Godfrey Mosha na Davis Kamungu
Washitakiwa hao ni miongoni mwa watu wanaodaiwa kumiliki kampuni 12 ambazo zilitumiwa kuchota mabilioni hayo ya fedha na ambao tayari wameshitakiwa.

Kampuni hizo ni Bina Resorts Ltd, Maltan Mining Company Ltd, Bencon International Ltd, Njake Hotel &Tours Ltd, Money Planners & Consultants, Mibane Farm, Changanyikeni Residential Complex Ltd, Liquidity Services Ltd, Kiloloma and Brothers, KARNEL Ltd, M/S Rashtas (T) Ltd na Navy Cut Tobacco (T) Ltd, Wamiliki wa kampuni 10 ambao hawajafikishwa mahakamani ni Kagoda Agriculture Ltd, G & T International Ltd, Excellent Services Ltd, Malegesi Law Chambers, VB & Associates Company Ltd, Bora Hotels & Apartment Ltd, B.V. Holdings Ltd, Venus Hotel Ltd, Ndovu Soaps Ltd, VB & Associates Company Ltd na Clyaton Marketing Ltd.

Umma wa Watanzania unasubiri kwa hamu kuona hatua zitakazochukuliwa kwa kampuni hizo ambazo baadhi yake zimekuwa zinaelezwa zinamilikiwa na baadhi ya vigogo wa kisiasa nchini. Wakati huo huo, kesi inayowakabili washitakiwa Jeetu Patel, Amit Nandy Devendra Patel na Ketan Chahan ilitajwa jana mahakamani hapo na itaanza kusikilizwa Januari 18, mwakani
 
Kifupi mchezo uliochezwa na Kikwete ni mkubwa kuliko wanavyofikiria hawa samaki wadogo (mafisadi)....
Kesi hizi zitakwenda weee ,mwisho wake watashindwa kesi watatumikia kifungo..na fedha hizo zitachukuliwa ama niseme zimekwisha chukuliwa.
Kesi za vigogo wa chama hazitafika mahakamani kwa sababu wao itasemekana walikwisha lipa hivyo hakuna haja..
Wananchi Wadanganyika tumepigwa bao majina yao hayatakuwa hadharani isipokuwa kwa wale mnaowafahamu kupitia JF na baadhi magazeti.. Ni tuhuma tu..
Hivyo kwa msemo wake JK - ni win win situation!
 
Mtaalam,
Ninachosema mimi fedha ndio inatakiwa na Kikwete zaidi ya wahusika kwa sababu ukienda deep hata yeye mwenyewe yawezekana kabisa anahusika. Kwa hiyo kuondoa dukuduku la wananchi ktk kundi hili wameisha fika pale wanapopataka.
Jeetu nani kwa Mdanganyika mkuu wangu, watu wanauza ndugu zao, wamezitoa roho za vipenzi wao bungeni itakuwa Jeetu..nani alijua Kikwete na Lowassa wanaweza tenganishwa kirahisi hivyo!
Kufikishwa Jeetu mahakamani tu yaonyesha wazi wameanza kumtema.. Wabongo kwenye ngawila wala sina imani nao..
 
Mtaalam,
Ninachosema mimi fedha ndio inatakiwa na Kikwete zaidi ya wahusika kwa sababu ukienda deep hata yeye mwenyewe yawezekana kabisa anahusika. Kwa hiyo kuondoa dukuduku la wananchi ktk kundi hili wameisha fika pale wanapopataka.
Jeetu nani kwa Mdanganyika mkuu wangu, watu wanauza ndugu zao, wamezitoa roho za vipenzi wao bungeni itakuwa Jeetu..nani alijua Kikwete na Lowassa wanaweza tenganishwa kirahisi hivyo!
Kufikishwa Jeetu mahakamani tu yaonyesha wazi wameanza kumtema.. Wabongo kwenye ngawila wala sina imani nao..

well said!!
Wabongo kwenye ngawila wala sina imani nao..
 
Nadhani kwa hao watumishi wa BoT, huu unaweza kuwa ushahidi wa kutosha kuwaweka hatiani kama upande wa mashitaka utaweka juhudi kidogo tu kujua hizo mali na pesa mamilioni walizitoa wapi.
 
eti wakuu,hebu nipeni msaada wa kisheria hapa..nimewahi kusikia eti ukiwa na kesi inayohusisha pesa nyingi kama hii ya EPA, kitendo cha kuweza kulipa dhamana kubwa kinaweza kutumiwa na mwendesha mashtaka/mahakama kukutia hatiani? --admission of guilty??
 
Kifupi mchezo uliochezwa na Kikwete ni mkubwa kuliko wanavyofikiria hawa samaki wadogo (mafisadi)....
Kesi hizi zitakwenda weee ,mwisho wake watashindwa kesi watatumikia kifungo..na fedha hizo zitachukuliwa ama niseme zimekwisha chukuliwa.
Kesi za vigogo wa chama hazitafika mahakamani kwa sababu wao itasemekana walikwisha lipa hivyo hakuna haja..
Wananchi Wadanganyika tumepigwa bao majina yao hayatakuwa hadharani isipokuwa kwa wale mnaowafahamu kupitia JF na baadhi magazeti.. Ni tuhuma tu..
Hivyo kwa msemo wake JK - ni win win situation!

Dhamana haichukuliwi hata kama ukishindwa kes, inarudishwa.
 
eti wakuu,hebu nipeni msaada wa kisheria hapa..nimewahi kusikia eti ukiwa na kesi inayohusisha pesa nyingi kama hii ya EPA, kitendo cha kuweza kulipa dhamana kubwa kinaweza kutumiwa na mwendesha mashtaka/mahakama kukutia hatiani? --admission of guilty??

Ni haki yako kuweza kutoa dhamana, the fact kua umetoa dhamana kubwa cant be used gainst you. Labda procecution ilete ushahidi mwengine, lakini nadhani watakua at least wamefanya money laundering fulani, otherwise its pretty stupid.
 
Pia ningepeda kujua kiasi cha dhamana kinapangwaje Tanzania?
Kwa kuwa hawa watuhumiwa wameshasalimisha Passport zao na sio hatari kwa jamii wakiwa nje kwanini dhamana imekua juu hivyo? Tukumbuke kuwa kisheria mtu yuko innocent until proven guilty.
 
Pia ningepeda kujua kiasi cha dhamana kinapangwaje Tanzania?
Kwa kuwa hawa watuhumiwa wameshasalimisha Passport zao na sio hatari kwa jamii wakiwa nje kwanini dhamana imekua juu hivyo? Tukumbuke kuwa kisheria mtu yuko innocent until proven guilty.

Kang.
1. Yes kila mtuhumiwa ni innocent until proven guilty as a matter of general legal principle japo kuna pia exception ambapo katika mashtaka mengine mshtakiwa anachukuliwa kuwa guity until athibitishe innocence.Kadhalika generally bail is a right and not a priviledge
2. However -kuna situations mtu anaweza kunyimwa bail - kuna baadhi ya makosa ni unbailable kama murder, robbery with violence, causing grievous harm ambapo hali ya aliyejeruhiwa ni mbaya na kuna uwezekano wa kupoteza maisha, kama mshtakiwa ametenda kosa akiwa nje kwa dhamana kwa shtaka jingine au kama ni kwa usalama wa mshtakiwa kuwekwa rumande e.g kama umma au waliotendewa kosa wana hasira ya kuweza kumdhuru mshtakiwa etc.Vile vile dhamana inaweza kufutwa kama mshtakiwa ataruka dhamana ( kutofika shaurini siku iliyopangwa bila taarifa,) au kama mdhamini ataamua kujitoa na mshtakiwa akakosa mdhamini mwingine etc
3.Bail conditions depends on the nature of the offence.Mahakama ( hakimu au jaji) anaweza kuweka masharti ili kuhakikisha mshtakiwa hatoroki. Hivyo basi hakuna checklist/schedule/manual ya kurejea kuona masharti ya dhamana.Ni busara ya mahakama hutumika.Kwa mfano katika kesi ya EPA nadhani tunaona kiasi cha pesa inayosemekana kuibiwa ni nyingi sana.Uwezekano wa kutoroka pia ni mkubwa.Hivyo basi pamoja na kuchukua passports zao bado inatoa nguvu kuweka bond kubwa ambayo kama atatoroka itakuwa forfeited.

BTW: Tusisahau pia kuwa mshtakiwa akionekana na hatia, pamoja na kufungwa bado hakimu anao uwezo wa kuamuru mshtakiwa arudishe kiasi hicho cha fedha iliyoibiwa.Ni vizuri kuwa wameweza " kuonyesha uwezo mkubwa wa kudeposit kiasi kikubwa che fedha" kama bond mahakamani japo wengine wamechangiwa na ndugu zao.Labda cha kutafakari ni je? hii inatuambia nini?
 
Huyu jamaa kumbe kafikishwa Kisutu kimya kimya wakati concentration yote iko kwa Mgonja:

Mwingine BoT kortini wizi wa EPA (Habari Leo)

Aliyekuwa mfanyakazi katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Jonathan Munis, ambaye sasa ni mfanyabiashara, jana alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kwa tuhuma za wizi wa Sh bilioni 2.6, mali ya BoT kupitia katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).

Akisomewa mashitaka yanayomkabili mbele ya Hakimu Mkazi Addy Lyamuya, Wakili wa Serikali Boniface Stanislaus alidai Munisi anatuhumiwa kuwa Oktoba 25, 2006 akiwa Dar es Salaam, aliiba fedha hizo kwa kutumia Kampuni ya Njake Enterprises, aliidanganya kuwa amenunua deni kutoka kwenye Kampuni ya E.ltoh ya Japan.

Wakili Boniface alidai kuwa katika siku hiyo, mshitakiwa akiwa Arusha, kwa kutumia akaunti ya kampuni hiyo, alijipatia ingizo la Sh bilioni 2.6. Mshitakiwa alitakiwa kutoa fedha taslimu au mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh bilioni 1.3 ambayo ni nusu ya fedha zinazodaiwa kuibwa pamoja na kuwa na wadhamini wawili watakaomdhamini kwa Sh milioni 30.

Upelelezi haujakamilika na kesi hiyo iliahirishwa hadi Desemba 30, mwaka huu. Tangu kuanza kwa kesi hiyo, Munisi ni mtuhumiwa wa 21 kupandishwa kizimbani ambapo tayari walishapandishwa kizimbani katika kesi hiyo watuhumiwa 20 ambao ni Jeetu Patel, Amit Nandy, Ketan Chohan, Vinodbhai Patel, Bahati Mahenge, Davies Kamungu na Manase Mwakale.

Wengine ni Eddah Mwakale, Farijala Hussein, Rajab Maranda, Japhet Lema, Ajay Somani, Jai Somani, Johnson Lukaza, Mwengesi Lukaza, Bosco Ndimbo Kimela, Sofia Joseph Lakila na Ester Mary Komu, Godfrey Mosha na Imani Mwakyosa. Watuhumiwa hao 20 wako nje kwa dhamana.
 
EPA yaikoroga CCM

na Esther Mbussi
Tanzania Daima~Sauti ya Watu​

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeandaa jarida mahususi linaloelezea historia ya wizi wa fedha katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Jarida hilo ambalo linaratibiwa na uongozi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam likiwa na lengo la kukisafisha chama hicho tawala na kashfa hiyo ya EPA linatarajiwa kuzinduliwa keshokutwa Alhamisi.

Viongozi kadhaa wa juu wa CCM waliozungumza na Tanzania Daima jana akiwamo Katibu wa chama hicho Mkoa wa Dar es Salaam, Ng’enda Kirumbe, walisema wanakusudia kulisambaza jarida hilo katika maeneo mbalimbali nchini bure.

Kwa mujibu wa Kirumbe na viongozi wengine kadhaa wa CCM, jarida hilo ambalo linaonyesha kuwa ni mkakati wa chama hicho kujipanga kwa ajili ya chaguzi kadhaa zijazo, linakusudia kueleza namna kisivyokuwa na mkono wowote katika sakata hilo ambalo hadi sasa limesababisha watuhumiwa 21 kufikishwa mahakamani.

Ili kufanikisha lengo hilo, jarida hilo linaelezwa kuwa na maandishi yanayokusudia kukanusha madai ambayo yamekuwa yakitolewa na wanasiasa kadhaa wa vyama vya upinzani kuwa CCM ilitumia sehemu ya fedha miongoni mwa shilingi bilioni 133 zilizoibwa EPA kwa ajili ya kampeni na ushindi wake kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.

Habari ambazo Tanzania Daima inazo zinaonyesha kuwa, tayari viongozi mbalimbali wa CCM wameshaanza kuzungumza na wanachama wao kuhusu jarida hilo.

“Hivi karibuni kumeibuka matukio mengi ya upotoshaji kutoka kwa wapinzani, yenye lengo la kukichafua chama, yakiwamo ya Richmond, ufisadi na mengineyo, chama chetu hakikumbatii wala hakilei ufisadi na ndiyo maana serikali imechukua hatua kwa wote walioshiriki,” alisema kiongozi mmoja wa CCM alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kuzinduliwa kwa jarida hilo.

“Kwa hali hiyo, wote wasiojua undani wa EPA, watapata fursa ya kusoma jarida hilo, ndipo mtakapojua ukweli wa wizi huo na jinsi CCM inavyochafuliwa kuhusika na wizi wa fedha za EPA,” alisema kiongozi huyo wa CCM.

Akizungumza na Tanzania Daima jana, Kirumbe alisema jarida hilo liko katika hatua za mwisho za kuchapwa baada ya kuhaririwa wiki chache zilizopita.

Alisema jarida hilo litatolewa bure kwa viongozi na baadhi ya wanachama watakaopenda kujua na kuelewa kwa undani historia ya EPA.

“Baadhi ya wanasiasa wa upinzani kwa makusudi au kutojua historia ya EPA wamekuwa wakiwapotosha hata kuwagawa wanachama kwa kuwaambia kwamba CCM ilihusika katika kuiba fedha hizo ndani ya BoT, hivyo tumeona ni busara kuwafafanulia Watanzania ili kuelewa kuwa CCM haikuhusika.

“Na kuanzia sasa kila suala ambalo litaonekana kuleta utata miongoni mwa wanachama na wananchi, chama kimeandaa jarida hili ili kutoa ufafanuzi kuepusha migongano na mfarakano usio wa lazima ndani ya chama,” alisema Kirumbe.

Hata hivyo, alisema ufafanuzi zaidi kuhusu suala zima la jarida hilo atautoa siku ya Alhamisi wiki hii wakati wa uzinduzi wake ambao bado haujajulikana namna utakavyofanywa.

Kashfa ya wezi wa fedha za EPA kwa mara ya kwanza ilifichuliwa kupitia katika mtandao wa intaneti kabla ya kupelekwa bungeni na Mbunge wa Karatu, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa.

Kuibuka kwa kashfa hiyo ya EPA bungeni, kulisababisha mtafaruku mkubwa baada ya wabunge kadhaa wengine wa upinzani wakiwamo Hamad Rashid Mohamed (CUF) na Zitto Kabwe (CHADEMA) kuishikia bango serikali kutokana na sakata hilo.

Kuibuka kwa sakata hilo kulisababisha Dk. Slaa afikie hatua ya kuandaa hoja binafsi kuzungumzia wizi wa fedha ndani ya BoT, uamuzi ambao hata hivyo ulizimwa na Spika wa Bunge, Samuel Sitta, ambaye aliamua kumzuia.

Tangu wakati huo hadi leo hii, viongozi wa upinzani na hususan wale wa CHADEMA wamekuwa wakiitaja Kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd ambayo ilichota kiasi cha shilingi milioni 40 katika akaunti hiyo ya EPA kuwa iliundwa mahususi kwa ajili ya kusaidia kampeni za urais na ubunge za CCM.

Tuhuma hizi za kuihusisha CCM na wizi huo wa EPA mara kadhaaa na kwa njia tofauti zimekuwa zikikanushwa bila ya mafanikio na viongozi na makada mbalimbali wa chama hicho tawala.
 
Back
Top Bottom