Elimu ya Uraia: Katiba ya Tanzania na Udhaifu wake

Kichuguu

Platinum Member
Oct 11, 2006
15,570
19,442
Katika wiki hii nitakuwa nyumbani full time kuanzia tarehe 24 Dec 2010 hadi tarehe 4 January 2011 kama mwenyezi mungu atanifikisha huko. Nimeamua kutumia muda huo kutumia thread hii kuandika somo la uraia kuhusu Katiba ya Tanzania na kuchambua udhaifu wake. Ingawa wengi wetu tunaijua Katiba yetu, kuna idadi kubwa ambao hawaijui sawasawa na hivyo kutokuelewa ulazima wa Tanzania kuwa na Katiba mpya.

Ninaomba mod asiunganishe thread hii na nyingine kusudi niweze kuwa na mtililiko mzuri wa mawazo.

Katiba inayotumika Tanzania iliandikwa mwaka 1977 na kufanyiwa marekebisho madogo kulingana na mabadiliko ya kisiasa kutoka chama kimoja hadi vyama vingi ambayo yote yalijumuishwa katika toleo la mwaka 2000. Ingawa kuna toleo la kiingereza la katiba hiyo, toleo kuu ni lile la kiswahili, kwa hiyo kukiwa na masigishano ya lugha kati ya toleo la kiswahili na kiingereza, basi lile la kiswahili linatawala.

katiba hiyo imegawanyika katika sura 10 zenye jumla ya ibara 152. Katiba ya Tanzania imaongelea karibu mambo yote ya muhimu kuwamo kwenye katiba na vile vile imejumuisha na mambo mengine ambayo siyo ya muhimu kuwamo kwenye Katiba.

Kabla ya kuanza kuangalia udhaifu wa ibara mbalimbali za Katiba, nitaanza na ule udhaifu wa jumla katika uandishi wa Katiba Yenyewe

Udhaifu wa Kwanza kabisa wa jumla katika uandishi wa katiba ya tanzania ni ule muundo wake; imeandikwa kwa mtindo wa kuzunguka zunguka kama vile ni kwa ajili ya wanasheria tu badala ya kuandikwa ikiwa imenyooka kwa ajili ya kusomwa na kueleweka na raia wote. Kwa mfano, ibara ya 2(2) inazungumzuia jambo linalohusu Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar bila kuwa imeelezea serikali hizo ni vitu gani. Inabidi mtu arukie ibara ya 151 kujua serikali hizo ni vitu gani.

Katika hizo ibara 152 za Katiba yetu kuna ibara ambazo hazina kitu kutokana na kuwa zilishafutwa lakini zimetunza namba zake; kwa mfano, ibara ya 10, 80, na 82. Kama ibara hizi zilishafutwa, hakuna umuhimu wa kuendelea kuziorodhoseha huku zikiwa tupu.
 
Ibara ya 2(2)

Kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano au Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Rais aweza kuigawa Jamhuri ya Muungano katika mikoa, wilaya na maeneo mengineyo, kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria au kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge: Isipokuwa kwamba Rais atashauriana kwanza na Rais wa Zanzibar kabla ya kuigawa Tanzania Zanzibar katika Mikoa, Wilaya au maeneo mengineyo.


Kifungu hiki kifutwe kabisa kwa sababu kwanza kinajenga mazingira ambamo rais wa jamhuri ya muungano anaweza kupingana na rais wa zanzibar. Pili shughuli ya ugawanyaji wa Wilaya na na Mikoa ni jukumu ambalo lingeachwa liwe linafanywa na Bunge kulingana na idadi ya watu baada ya sensa ya nchi. Kitendo cha Rais kuwa na madaraka ya kugawanya wilaya kwa utashi wake kinaweza kusababisha agawanye nchi katika wilaya nyingin sana ili aweze kutoa nafasi nyingi za u-DC kwa watu wake.



Ibara ya 3(1)

Jamhuri ya Muungano ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamaa, yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Kifungu hiki kiandikwe upya kwa kuondoa neno "kijamaa." Kwa vile Tanzania inafuata mfumo wa soko huru, ni makosa sana kwa Katiba kutangaza kuwa ni nchi ya kijamaa. Neno hili linaifanya katiba ionekane kama document yenye mambo yasiyokuwa na uzito wowote.
 
Kichuguu:

Nitakusiliza kwa makini mkuu. Suala la muundo mzima wa katiba limekuwa kikwazo cha watu kutosoma katiba hiyo. Kusoma katiba ya Tanzania is a real pain ...

Vilevile nimejaribu kufanya utafiti wa kipumbavu wa kuangalia matumizi ya maneno ya wenye nguvu kwa kutumia katiba ya Marekani na ya Tanzania. Katika utafiti huu nimehesabu matumizi ya neno Rais (noun, adjective) kwenye katiba ya Tanzania na neno President (noun, adjective) kwa katiba ya Marekani.

Katika katiba ya Tanzania neno rais limetumika mara 418. Katika katiba ya Marekani neno President limetuka mara 100. Pamoja na utafiti huu kuwa wa kipumbavu, unathibiti kuwa madaraka ya rais wa Tanzania ni makubwa sana. Anatajwa kuwa ndie atakayegawa mikoa. Anatajwa kuwa atateua hiki na kile.
 
Ibara ya 3(2)

Mambo yote yahusuyo uandikishaji na uendeshaji wa vyama vya siasa nchini yatasimamiwa kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii na ya sheria iliyotungwa na Bunge kwa ajili hiyo.

Kifungu hiki kiondolewe kwa vile hakina maana yoyote. Badala yake Katiba iwe na ibara maalum inayotoa mwongoza wa uendeshaji wa shughuli za vyama vya siasa katika lugha inayojitosheleza bila kuacha mwanya wa kuwepo kwa viraka vingine kutoka Bungeni.


Ibara ya 4(1)

Shughuli zote za Mamlaka ya Nchi katika Jamhuri ya Muungano zitatekelezwa na kudhibitiwa na vyombo viwili vyenye mamlaka ya utendaji, vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutekeleza utoaji haki, na pia vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma.


Ibara hii na vifungu vidogo vinavyofuatia vinaonyesha udhaifu wa muundo wa Muungano wetu, na itabidi viandikwe upya kutoa maelekezo thabiti. Inabidi Katiba iweke utaratibu ambamo kutakuwa na mamlaka moja ya utendaji, mamlaka moja ya kutunga sheria na mamlaka moja ya kutoa haki. Kuwepo kwa mamlaka mbili mbili kuakaribisha mgongano wa mamlaka. Kwa mfano Baraza la Wawakilishi la Zanzibar linaweza kutunga sheria inayokinzanana na sheria iliyotungwa na Bunge la jamhuri ya Muungano. Kwa vile zote ni mamlaka halali za kutunga sheria chini ya Katiba, inaweza kuwa na vuta nikuvute sana katika kufikia mwafaka, jambo ambalo lisingelazimika iwapo Katiba ingeonyesha wazi kuwa kuna mamlaka moja ya kutunga sheria. Kuhusu kuwepo kwa mamlaka inayohusu mambo ya zanzibar, ingekuwa ni jambo la maana sana iwapo Katiba itakuwa na ibara moja inayotoa mwongozo wa jinsi gani Serikali ya Zanzibar itakavyofanya mambo yake chini ya mamlaka kuu za serikali ya muungano. Chini ya ibara hiyo, swala la katiba ya Zanzibar liachiwe wazanzibari wenyewe huku wakijua kuwa kila wanalofanya linatakiwa liwe chini ya katiba ya Jamhuri ya Muungano



Ibara ya 4(2)
Vyombo vyenye mamlaka ya utendaji vitakuwa ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, vyombo vyenye mamlaka ya kutekeleza utoaji haki vitakuwa ni Idara ya Mahakama ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Idara ya Mahakama ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, na vyombo vyenye mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma vitakuwa ni Bunge na Baraza la Wawakilishi.


Udhaifu wa ibara hii ni kama ule niliotaja hapo juu kwa kuwa na mamlaka mbilimbili zinazotambuliwa na Katiba moja.


Ibara ya 4(3)

Kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za umma katika Jamhuri ya Muungano, na kwa ajili ya mgawanyo wa madaraka juu ya shughuli hizo baina ya vyombo vilivyotajwa katika ibara hii, kutakuwa na Mambo ya Muungano kama yalivyoorodheshwa katika Nyongeza ya Kwanza iliyoko mwishoni mwa Katiba hii, na pia kutakuwa na Mambo yasiyo ya Muungano ambayo ni mambo mengine yote yasiyo Mambo
ya Muungano.


Kifungu hiki hakina udhaifu mkubwa ila kingeorodhesha hapa moja kwa moja ni mambo yapi ni ya Muungano na ni yapi yasiyokuwa ya muungano na ni kwa vipi intersection ya mambo ya muungano na yasiyokuwa ya muungano itakavyoshughulikiwa.



Ibara ya 4(4)
Kila chombo kilichotajwa katika ibara hii kitaundwa na kutekeleza majukumu yake yake kwa kufuata masharti mengine yaliyomo katika Katiba hii.

Kifungu hiki hakina udhaifu wowote na wala siyo cha lazima kabisa katika katiba hii
 
Back
Top Bottom