Duu,huu 'usafishaji' sasa ni kiboko!!!

Mtarajiwa

JF-Expert Member
Feb 29, 2008
440
11
Lowassa apokewa kifalme Monduli












BAADA YA KUJIUZULU…

::Watu 10,000 na magari 400 wampokea
::Akaribishwa kwa zulia jekundu Monduli
::Askofu Laizer amwombea, amtabiria mema
::Yeye apasua bomu, aichambua Richmond

Na Deodatus Balile, Monduli

WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu hivi karibuni, Edward Ngoyai Lowassa, jana amepokewa kama mfalme jimboni kwake Monduli.

Vikundi vya Morani wa kimasai, wanawake maarufu kama yeyo, vikongwe maarufu kama koko, mabinti maarufu kama ndito na wazee, wote walijitokeza.

Si hao tu, kwani maaskofu, mapadri, mashekhe na wachungaji walijitokeza kwa wingi kuungana na umati wa watu wanaokadiriwa 10,000 kumpokea Lowassa jimboni.

Maneno aliyokuwa anayatumia mwanasiasa maarufu kutoka Morogoro, hayati Thadeus Kasapira, kuwa haijapata kutokea, ndiyo yaliyotokea jana kwenye mji wa Monduli.

Magari zaidi ya 400 yakiwa mchanganyiko kati ya mabasi, magari madogo, malori kwa teksi, yaliufanya mji wa Monduli kulipuka kwa furaha jana.

Wananchi wa Mkoa wa Arusha waliokuwa wakionyesha furaha na bashasha ya hali ya juu walikuwa wamebeba mabango mengi yenye ujumbe mzito kwa Serikali na Lowassa katika sakata zima la Richmond .

Baadhi ya mabango hayo yalisomeka hivi: “Nyota yako bado inawaka, shujaa wetu umeonyesha mfano usife moyo, mtu kwao karibu nyumbani, tupo pamoja nawe usife moyo, wana Monduli tunakuamini, hongera mheshimwa Lowassa kwa usimamizi wa sekondari za Kata utakumbukwa.” Ukiacha mabango hayo, kubwa lililowaacha wengi midomu wazi ni bango lililosomeka hivi: “Mmasai haibi hela, anaiba ng’ombe.”

Lowassa yeye alitua katika Uwanja wa Ndege wa Arusha saa 6:55 mchana na kukuta umati mkubwa wa watu.

Akiwa katika shati nyeupe, tai yenye rangi nyeusi na mistari ya kijivu, huku suruali yake nyeusi na viatu vyeusi vikiwa vinang’aa, Lowassa aliyejiuzulu Uwaziri Mkuu, Februari 7, mwaka huu, akiongozana na mkewe Regina, alirejea Monduli kwa mara ya kwanza tangu aachie wadhifa huo huku mkewe akionyesha tabasamu la mwaka.

Lowassa hakuficha hisia zake alipopewa nafasi ya kuhutubia wananchi katika Ofisi za CCM, Monduli: “Siku hii nimeisubiri kwa hamu kubwa tangu yalipotokea haya yaliyotokea (akashangiliwa).”

Huku mkewe mama Regina naye akionyesha furaha ya dhati kutokana na wingi wa watu, alionekana kumuunga mkono mumewe na kufurahishwa na wingi wa watu na kupunga mkono muda mwingi.

Akiwa katika gari aina ya Land Cruiser maarufu kama shangingi namba T181 ATU, Lowassa aliwasili katika Viwanja vya Monduli saa 8:32 mchana, na kukuta umati uliokuwa ukimsubiri bila kujali jua kali lililokuwa likiwaka.

Wananchi wengi wakiwa wamevaa fulana zilizoandikwa ‘Karibu nyumbani shujaa wetu E. N. Lowassa- CWT Monduli,’ walionyesha nyuso za bashasha na matumaini makubwa juu ya mbunge wao, Lowassa.

Kama miujiza vile, wakazi wa Monduli walimwekea zulia jekundu, kuashiria mapenzi yao na utambuzi wa mamlaka aliyonayo kiongozi huyo katika jimbo lao na majukumu ya kitaifa.

Lowassa jana alisimikwa tena katika jamii ya Kimasai. Walimfunga mgolole, wakampa mundu, mkuki na kifimbo, huku wakiimba kuwa yeye ni Simba wa Yuda angurumaye katika nyika. Sehemu ya salamu za wana-CCM Monduli zilimtaka Lowassa kutokuwa na hofu: “Usiangalie nyuma kwa masikitiko, bali uangalie mbele kwa ushindi,” ilisema sehemu ya risala ya wana-Monduli.

Huku akipongezwa kwa kufungua ukurasa mpya wa uwajibikaji katika siasa za Afrika, Lowassa aliambiwa asiwajali wananchi wachache wenye masilahi binafsi wenye kumtembezea kejeli dhidi yake nchi nzima.

“Tunakupenda, tunakuamini na tunakupa moyo katika vita mpya kwa ajili ya mabadiliko,” alisema msoma risala na kushangiliwa kwa nguvu kubwa. Pia walimpongeza mama Regina kwa uvumilivu wa hali ya juu wakati huu wa shida.

Kwa mshangao wa wengi, wenyeji wa Kijiji cha Twatwatwa wilayani Kilosa, waliambatana na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Mvomero kuja Monduli jana kumpokea Lowassa na kueleza wanayoyakumbuka katika uongozi wake.

Pamoja na mambo mengine, walitaja maelekezo ya Lowassa kuwashauri wajenge shule maalumu kwa ajili ya watoto wa wafugaji, waliosema leo shule hiyo ina watoto 160 na kwao ni alama isiyofutika. Askofu Thomas Laiser wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), alikuwa mmoja wa watu waliohudhuria ujio wa Lowassa katika Jimbo la Monduli jana. Akizungumza kwa mamlaka makubwa na kuonyesha kwamba kweli maaskofu ni wawakilishi wa Mungu duniani kutokana na watu walivyokaa kimya wakati akihutubia jamii kutokana na sauti yake ya mamlaka, kwanza Askofu Laizer alimbariki Lowassa.

Alieleza mambo matatu ya msingi. Alisema umati ule ulikuwa umekusanyika kumpa pole kwa yaliyotokea, pili akamhakikishia kuwa wapo pamoja naye, na jambo la tatu, akasema kama kweli ulitokea ufisadi basi yeye anaungana na Rais Jakaya Kikwete kwa hatua alizochukua, ila akamalizia kwa kibwagizo: “Sisi Wamasai tunasema panya akiuawa anakuja kuozea kwenye nyumba ya mama yake.” Maneno haya aliyasema kwa Kimasai na kuyatafsiri hali iliyozua hamasa kubwa kwa wenyeji.

Mpendwa msomaji, kama ungekuwapo basi si ajabu na wewe ungekuwa mmoja wa watu waliotokwa na machozi baada ya Lowassa kusimama kueleza kilichotokea katika sakata la Richmond.

Tofauti na wiki mbili zilizopita, Lowassa akionyesha uchangamfu na sauti kali ya uchungu na matumaini ndani yake jana, alifafanua kilichotokea.

Alieleza mchakato mzima wa Richmond ulivyokwenda na ingawa hakutaja majina maelezo yake yalithibitisha kuwa aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Ibrahim Msabaha, alimwingiza mtegoni.

Kabla ya kufafanua kilichojiri wakati wa sakati la Richmond, alieleza jinsi alivyofikia uamuzi wa kujiuzulu: “Nilimweleza mke wangu, nikamwambia nataka kujiuzulu uko tayari? Yeye akaniuliza ‘wewe uko tayari?’ Nikamwambia niko tayari.

“Baada ya hapo nikaenda bungeni, kimya kimya watu wawili tu tulikuwa tukijua mimi na mke wangu, kwamba nakwenda kujiuzulu… maandiko matakatifu yanasema baba na mama wanakupa mali na urithi wa duniani, lakini mke mwema hutolewa na Mungu.” (akashangiliwa).

Alipofikia kuzungumzia sakata la Richmond, Lowassa alifafanua kuwa Net-Group Solutions kampuni iliyokuwa inaongoza manejimenti ya TANESCO walithibitika kuwa na nia ya kufanya hujuma katika mchakato wa kupata umeme wa dharura nchi ilipokumbwa na ukame mwaka 2006.

Alisema baada ya kubaini hilo kutokana na uzembe wa hali ya juu uliokuwa ukionyeshwa na watendaji wa Net-Group Solutions, yeye kama Waziri Mkuu chakaramu, asiyetaka mambo yaharibike akiangalia, aliamua kuondoa mchakato wa ununuzi wa mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura kutoka mikononi mwa TANESCO kwenda chini ya timu maalumu ya iliyoundwa na viongozi waandamizi wa Serikali.

Alisema timu hiyo iliundwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika, ambaye wakati wa kuhojiwa na Kamati ya Dk. Harrison Mwakyembe, alisema hajui lolote, Katibu Mkuu Hazina, Grey Mgonja, Mwakilishi kutoka Benki Kuu, TANESCO, Wizara ya Nishati na Madini.

Timu hii aliiundwa kwa nia ya kuharakisha mchakato wa kupata umeme wa dharura, lakini hata mambo yalipoonekana hayaendi alishauri mkataba kati ya Richmond na Serikali uvunjwe, ila maafisa wakuu wa Serikali walimkamtalia.

Kwamba je, nini kilitokea na Lowassa angefanyaje na ni hatua zipi alichukua usikose nakala ya Mtanzania kesho.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom