Sam GM
JF-Expert Member
- Mar 3, 2008
- 535
- 28
JF imekuwa ni mahali pa kupashana habari na kuweza pia kuzungumzia mambo ya historia yetu na mwelekeo wa nchi.
Kuna Huyu bwana anajulikana kama marehemu Dr Kleruu, mie nimekuwa nikimsikia katika wimbo wa Mbaraka Mwinshehe kuwa alikuwa mwanamapinduzi.
Je, kuna yeyote anaweza kutupatia taarifa kumhususu huyu Dr Kleruu alikuwa nani hasa na uana mapainduzi wake ulikuwa vipi katika historia na siasa za Tanzania?
Mnara wa kumbukumbu kifo cha Dr. Kleruu kijijini Isimani
Mtoto wa Said Mwamwindi
=== Historia ya Dr. Kleruu kwa ufupi ===
HISTORIA: MKULIMA ALIYEMUUA MKUU WA MKOA SIKU YA KRISMASI-
ILIKUWA siku ya Sikuku ya Noeli almaarufu Christmas mnamo mwaka 1971. Mkuu mpya wa Mkoa wa Iringa aliyehamishiwa hapo akitokea Mtwara, Dkt. Wilbert Kleruu, msomi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) wa Uchumi wa kijamaa katika Kilimo aliuawa na Mkulima aitwaye Said Mwamwindi.
Kipindi hicho kulikuwa na kampeni ya kutaifisha mashamba ya wakulima wakubwa na kuyafanya mashamba ya kijiji. Na Dkt. Kleruu alipelekwa Iringa ili akatekeleze kazi hiyo kwani kipindi hicho Iringa ilikuwa na wafanyabiashara wakubwa waliomiliki mashamba makubwa ya Kilimo hasa maeneo ya Isimani.
Katika eneo hilo la Isimani kulikuwa na mkulima mmoja aliyekuwa anamiliki takribani hekari 400 za mashamba na mfanyabiashara aliyekuwa anamiliki majumba Iringa mjini - Said Mwamwindi-
Kwa wakati ule ilishauriwa angalau kila mtu awe na shamba lisilo zidi hekari 4. Jambo ambalo lilileta mvutano mkubwa kati ya wakulima wakubwa na Serikali.
Sasa siku hiyo ya Christmas, Dkt. Kleruu alikwenda Isimani akiwa katika utekelezaji wa sera ya kutaifisha mashamba. Moja kwa moja alikwenda hadi shambani kwa Mwamwindi, na kumkuta analima.
Mkuu huyo wa Mkoa akamuuliza mbona unalima shamba lako mwenyewe na si la kijiji? Mwamwindi akajibu, sioni tatizo hakuna mtu shambani, leo ni Jumapli tena ni sikukuu.
Maneno yale yalimuudhi Dkt. Kleruu, ambaye alikuwa akisifika kwa ukali, kutekeleza sera za serikali na maneno makali au kutukana watu hadharani pale wanapo fanya makosa.
Dkt. Kleruu baada ya kuudhika alimtukana Mwamwindi tusi lililomlenga mama yake ambaye tayari alikuwa marehemu. Mwamwindi alihoji inakuwaje anamtukania mama yake, huku akimuonyesha kaburi alimozikwa?
Mkuu wa Mkoa, aliendelea kuja juu, huku akisema kaburi ndio nini? Huku akilipiga mateke kaburi la Mama yake Mwamwindi. Kwa kabila la wahehe makaburi yana heshima yake, kwani ndipo nyakati nyingine hutumika katika sala, matambiko na mila kadha.
Kitendo kile kilimghadhabisha Mwamwind, na kuanza kukimbia kuelekea nyumbani. Mkuu wa Mkoa akadhani Mwamwindi anamkimbia, akaamua kumfuata.
Alipofika nyumbani, tayari Mwamwindi alisha ingia ndani na kuchukua bunduki yake, Dkt. Kleruu baada ya kuona hali ile mara moja alianza kumuomba msamaha, lakini hasira zilimuwaka Mwamwindi kama moto wa nyika; hakuwa na msamaha, alimfyetulia risasi kichwani Dkt. Kleruu na kumuua.
Baada ya kumuua, Mwamwindi aliuchukua mwili ya Mkuu wa Mkoa na kuuweka ndani ya gari (inadaiwa kwenye boneti) alilokuja nalo Mkuu huyo wa Mkoa.
Kisha alichukua kofia ya Dkt. Kleruu na kuivaa, akaingia ndani ya gari na kuanza safari ya kuelekea Iringa mjini tena akipita njia isiyo ruhusiwa kwani barabara ilikuwa 'one way'.
Alipo karibia mjini, askari walishangaa ni nani anaye pita njia isiyo ruhusiwa, ila mara waligundua ilikuwa gari ya RC wa Iringa, hivyo walidhani amepata dharura.
Gari lilipowasili kituoni, Polisi walijiandaa kupiga salute, mara alishuka Mwamwindi akiwa na bunduki yake na kuelekea ndani (counter). Askari walipigwa na butwaa.
Alipofika aliwaambia "Nendeni mkachukue Nguruwe wenu ndani ya gari," na Kisha akakabidhi bunduki yake.
Lilikuwa tukio la kustaajabisha, na kushangaza na lililofanyika kwa haraka sana.
Baada ya taarifa kuenea, msako wa polisi ulianza mara moja. Ila katika msako huo, Polisi waliwakamata baadhi ya watu walio kuwa wakinywa bia kwa furaha, shangwe na nderemo baada ya kusikia Dkt. Kleruu ameuawa. Kwani wanadai alikuwa na dharau.
Kesi ya Mwamwindi alipelekwa haraka sana na ndani ya miezi kadhaa, Juni 1972, Mwamwindi alihukumiwa kunyongwa hadi kufa, ikiwa ni moja ya hukumu chache za kunyongwa zilizo wahi kuidhinishwa.
Inadaiwa Mwalimu. Nyerere alihuzunishwa sana na kifo hicho, na hata kesi ya Said Mwamwindi ilipoisha na kupewa hukumu ya kifo, Inasemekana Nyerere hakusita kusaini, na ni mojawapo ya hukumu tatu tu za kifo zilizotekelezwa wakati wa utawala wa Nyerere
MICHANGO YA WADAU:
-----------------------------
Habari nyingine inayohusiana na habari hii fuatilia
- Binti wa Dkt. Wilbert Kleruu atoa ya moyoni
Viongozi na Wanasiasa wengine waliowahi kukumbana na matukio ya kupigwa riasasi
- DODOMA: Tundu Lissu ajeruhiwa kwa risasi, akimbizwa Hospitali
- Simulizi: Kisa na Mkasa wa Mauaji ya Jenerali Imran Kombe (Mkurugenzi Mstaafu wa Idara ya Usalama wa Taifa-TISS)
- Kifo chenye utata cha Waziri Nicas Mahinda
- John Mwankenja auawa kwa risasi
- Wakili mtetezi wa ICTR Prof. Jwani Mwaikusa auawa Tanzania
- TANZIA - Waziri Salome Mbatia afariki dunia, maswali yaibuka!
- Iringa: Mwandishi Mwangosi auawa katika vurugu kati ya Polisi na CHADEMA
- Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka ashambuliwa kwa risasi na Watu wasiojulikana
- Askari polisi aliyepigwa risasi na majambazi Tanga afariki

Dr Wilbert Kleruu alikuwa mzaliwa wa mkoa wa Kilimanjaro sehemu iitwayo Mamba (au Mwika), Moshi vijijini ambako siku hizi kunaitwa Vunjo. Alisomea uchumi wa kijamaa hadi ngazi ya PhD, na hasa alikuwa agricultural economist.
Alifanya kazi kwa karibu sana na Mwl Nyerere ambaye alimpenda sana, maana alimwona ni muumini wa siasa yake ya ujamaa na kujitegemea. Alijituma na kuiamini kwa moyo wake itikadi hiyo, kwamba ukombozi wa nchi utapatikana kwa mapinduzi ya kilimo cha kijamaa (ndio uanamapinduzi anaozungumziwa).
Alijitahidi pia kutekeleza itikadi hiyo kwa vitendo, na ndiyo iliyomgharimu maisha yake mwaka 1971 alipokuwa mkuu wa mkoa wa Iringa. Siku moja ya jumapili (hakuwa na jumapili huyu mjamaa) alikwenda kwenye shamba la mkulima mmoja aliyeitwa Saidi Mwamwindi, ambaye alikuwa na shamba kubwa sana, kwa lengo la kufuatilia maagizo yake aliyokuwa ametoa kuhusu shamba hilo, ndipo alipokorofishana na mkulima huyo maana yeye hakuzikubali hata kidogo hizo sera za kijamaa. Mwamwindi alikwenda nyumbani kwake akachukua gobore lake, akamfuata Dr Kleruu alipokuwa akampiga risasi na kumwua, kisha akapakia mwili wake kwenye Land Rover yake (pick up short chassis) na kupeleka kwenye kituo cha polisi ambako pia alijisalimisha.
Nyerere alihuzunishwa sana na kifo hicho, na hata kesi ya Saidi Mwamwindi ilipoisha na kupewa hukumu ya kifo, Nyerere hakusita kusaini, na ni mojawapo ya hukumu tatu tu za kifo zilizotekelezwa wakati wa utawala wa Mwl Nyerere.
Wengine wataongezea, lakini kama hapo ulipo unaweza kupata vitabu, tafuta kitabu kiitwacho "The Egalitarian Moment: Asia and Africa 1950-1980" kilichoandikwa na Donald Anthony Low (1995), habari hii ya Dr Kleruu iko kwenye ukurasa wa 52-53, kwenye chapter yenye heading "Richer Peasants and the State".
Unaweza pia kusoma journal article iliyoandikwa na Phillip Raikes mwaka 1979: Agrarian Crisis and Economical Liberalisation in Tanzania kwenye jarida la Journal of Modern African Studies Vol 17(no.2) pg 309-316, ambayo nimejaribu kukuwekea link yake hapa chini. Kifo cha Dr Kleruu kiliwahuzunisha watu wengi hasa wakulima wadogowadogo wa huko Iringa ambao walikuwa wakifurahia alivyokuwa ananyang'anya mashamba kwa wakulima wakubwa ili yalimwe kijamaa. Pia alikuwa ana tabia ya kuwafokea watumishi wa serikali hata wakurugenzi kwenye mikutano ya hadhara, pale alipoona sera zake za kijamaa hazijafuatwa kama alivyotaka, yaani alikuwa na ule ujamaa wa kibabe hasa uliokuwa Urusi (ajabu ni kwamba huyu alisomea Marekani!). Kwa namna fulani (ama kiasi kikubwa) alikuwa na 'ukali' kama ule wa Marehemu Sokoine. Raikes (1979) anaandika hivi kuhusu kifo cha Dr Kleruu kwenye rejea niliyotaja:
"...the emergence of the assassin of the Regional Commissioner as a 'folk hero', seems to me a misreading. Dr Wilbert Kleruu had achieved a certain local popularity largely because of his habit of abusing civil servants in public. His expro- priation of the 'rich' peasants also seems to have been quite popular, especially of course with those who received the land. As for the various stories which went the rounds in the aftermath of the murder, I can only go by second hand gossip...." (uk 315).
Anaendelea:
"The point stressed was that Mwinyi killed Kleruu for calling him a dog (said to be an unallowable insult among the Hehe) in front of his wife (which made it the more unforgivable). In short, it was seen by Mwinyi as a means to preserve his honour, and this would help to explain why he gave himself up immediately" (uk 316). Mwamwindi alijulikana pia kama "Mwinyi" kwa maana ya "Lord"
Historia ya Isimani imejaa a lot of hardship. Wakulima waliohamia huko walikuta ni pori tuu na wakaclear mashamba na kuanza kulima kwa tabu sana, maji yanachotwa mbali, chakula shida, wanyama pori nao tele, etc.
Babu yangu alikuwa mmojawapo wa wakulima wa mwanzo huko Isimani; mama yangu anasimulia walivyokuwa wanaenda mbali sana kufuata maji ya kunywa na kupikia. Maisha yalikuwa duni na magumu sana. Ikumbukwe hii ni kabla ya sera ya vijiji vya ujamaa, azimio la Arusha nk. Sera hizi zilivyoingia mkoani Iringa, serikali iliwataka watu wote wahamie katika vijiji vya ujamaa na kuwe na communal farming. Hii iliwakuta wakulima wengi mahala pabaya sana manake mashamba waliotoil kuyalima yangechukuliwa kuwa ya vijiji vya ujamaa. Hatimaye walikubali ila ikaonekana kwamba kijiji cha ujamaa Isimani kina mashamba mengi tayari, na wakulima wengine wakakubaliwa waendelee kuyashughulikia mashamba yao zile siku ambazo sio za kijiji, na jumapili ndio siku isiyo ya kijiji na Mwamindi na wakulima wale wa mwanzo kule Isimani wakawa wanatend mashamba yao siku za jumapili.
Kutoka Iringa mjini Kleruu ameamua kwenda Isimani bila ya mlinzi/dereva. Ikumbukwe pia ameshakuwa very unpopular na wanyalukolo na word was out kuwa yeyote atakayempata kwanza ammalize (haya ni maneno ya wanyalukolo wa enzi hizo) Alipopita kwa Mwamindi na akamuona Mwamindi yupo shambani kwake ndipo akamfuata huko huko na kuanza kumkejeli. Inasemekana Kleruu alikuwa ana kifimbo kama kile cha Mwalimu na akaanza kumchomachoma kifuani Mwamindi huku akimwambia"wewe nani kakupa ruhusa kulima jumapili? Si ulitakiwa kulima kwenye shamba la kijiji cha ujamaa tuu?" etc etc.
Mwamindi akaingia ndani akachukua shot gun yake(nadhani ilikuwa zile wanaziita two-two rifle, popular sana enzi hizo) na akatokea kwa nyuma (nyumba za waHehe zina mlango/dirisha mdogo kwa nyuma) na akamtwanga risasi na kikafuata kilichoelezwa hapo juu. Ila alipofika Iringa alikwenda kwanza kwa wake zake na kuwaambia alichofanya ndipo akaenda police station. Kuna mzee mmoja alipishana na Land Rover ya Kleruu na akashangaa kumuona Mwamindi anaendesha, na hapo hapo akajua soo limetokea, akapita shambani kwa Mwamindi na akaelezwa kilichotokea. Vilevile, kule mtaani watu walishangaa Mwamindi anaendesha kari la mkuu wa mkoana limepaki kwake! Waliokuwa wanajua walielewa mara moja nini kimetokea!
Siku ile pale Isimani, the current popular mayor of Iringa was present as a very young boy. Maggid muulize atakupa story yote ya the first political assassination in Tanzania. Ya Karume ilikuwa next the following year, I think.
-----------------------------
Jana Jumamosi jioni nilikuwa na mazungumzo marefu na Bw. Amani Mwamwindi. Mstahiki Meya wa Iringa aliyemaliza muda wake. Huyu ni mwana wa marehemu Saidi Mwamwindi ambaye simulizi juu ya kilichotokea kule Isimani mwaka 1971 tumeifuatilia.
Bw. Amani Mwamwindi alikubali kufanya mazungumzo nami hiyo jana nyumbani kwake Mlandege hapa Iringa. Ni simulizi ya kusikitisha, kusisimua na yenye kutoa mafunzo. Inahusu pia maarifa ya uongozi na dhana nzima ya utawala bora. Naandika haya saa saba za usiku Jumapili. Ngoje nikapumzike. Baadae Jumapili ya leo nitaanza kuwasilimua niliyosimuliwa.
Kumekucha. Jumapili saa kumi na mbili asubuhi. Naanza kusimulia nilichosimuliwa;
Nimefika Nyumbani kwa Amani Mwamwindi. Ni majira ya saa kumi na nusu jioni. Ni nyumba ya kawaida sana katikati ya eneo wanaloishi watu wengi, karibu kabisa na soko. Ni kata ya Mlandege.
Nagonga mlango mkuu. Anayenifungulia ni Amani Mwamwindi.
" Karibu Bwana Mjengwa". Tunafahamiana, tumewahi kukutana kabla. Miguuni hana viatu, amevaa soksi nyeusi.
Ananikaribisha kiti sebuleni. Anaagiza nilitewe kinywani. Naye anakaa kitini. Mazungumzo ya ana kwa ana. Kichwani najiuliza; unaanzaje mahojiano na mtu aliyefiwa baba yake kwa kunyongwa miaka arobaini iliyopita?
"Bw. Mwamwindi, pole sana kwa tukio lile la mwaka 1971. Mimi nimelifuatilia kiasi. Kuna simulizi nyingi mitaani. Nimeanzisha mjadala bloguni. Vijana wengi wanaonyesha kuwa na kiu ya kutaka kujua ukweli hasa wa tukio lile. Kwa vile uko hai, nikaona nikutafute tusikie kutoka kwako."
Mwamwindi ananiangalia usoni.
" Alaa!" Anatamka. Kisha kinafuata kimya.
Nakumbuka, kuwa nimetoa maelezo ya utangulizi, sijauliza swali.
" Je, ni kweli kuwa Dr Kleruu alikwenda Isimani kwa marehemu mzee Mwamwindi kuhimiza suala la kilimo ndipo akakutana na kifo chake? " Namwuliza kwa staili ya kurusha mshale bila kulenga hasa ninachotaka kupiga. Namjengea mazingira ya kuogelea katika kile anachokijiua. Na swali hili kwake analiona zuri sana.
" Swali zuri, umeuliza kama Kleruu alikwenda kuhimiza kilimo. Hapo ndipo lilipoanzia tatizo."
Nakumbuka swali muhimu kabla hajaendelea.
" Mzee Mwamwindi, hivi ulikuwa na umri gani siku hiyo ya tukio?"
" Nilikuwa na miaka 21, na marehemu mzee alikuwa na miaka 42."
Nauliza tena.
" Tunasoma kuwa ilikuwa siku ya Krismasi. Je, ilikuwa ni Jumapili au siku gani? Na wewe ulikuwapo nyumbani kwa mzee?"
" Ni kweli ilikuwa siku ya Krismasi, Desemba 25, 1971. Ni siku ya Jumamosi" Anajibu Mwamwindi.
" Turudi kwenye tatizo lilipoanzia" Namwomba Mzee Amani Mwamwindi.
" Kulikuwa na tofauti ya kimtazamo. Na ugomvi ulianzia siku ya Alhamisi, Desemba 23 kwenye ukumbi wa welfare pale Mshindo. Kleruu aliwakusasanya wakulima wakubwa wa Isimani. Nataka ujue kuwa Isimani ilikuwa na wakulima wakubwa sana na mmoja wao ni marehemu baba yangu. Mle ukumbini kulitokea malumbano makali sana baina ya wazee wale na mkuu wa mkoa Kleruu.
Wazee hakukubaliana na Kleruu kuwaita pale kuzungumzia kilimo cha eka mbili au tatu wakati wao kila mmoja ukubwa wa shamba ulianzia eka mia mbili. Na tayari walikuwa na ushirika wao. Mimi nikiwa na miaka 21 nilikuwa karani wa chama cha ushirika.
Siku ile Mzee alitoka kwenye mkutano ule na kuja nyumbani kwangu hapa tulipo, Mlandege. Akanieleza juu ya mkutano ule na jinsi walivyokosana kimazungumzo na Kleruu. Akaniambia, kuwa mle mkutanoni alimwambia Kleruu ni vema akawasaidia wale ambao hawajaanza hata kutembea kuliko kuhangaika na watu wenye uwezo wa kutembea na kukimbia. Na baba yangu hakwenda shule.
Kwenye Umoja wao wa wakulima wa Isimani, baba na wenzake walijipanga vema. Walishaanza kuzungumzia haa uwezekano wa kumlipa mwanasheria, hata kama ni wa kutoka Uingereza, aje kuwatetea katika uovu ule wanaotaka kufanyiwa. Hawakukubaliana na utekelezaji wa sera za Ujamaa kwa staili ile aliyotaka Kleruu. Kuingia kwenye ushirika na wengine wakati wao walishaanza zamani. Fikiri, wao walifyeka mashamba yao tangu miaka ya hamsini. Hoja yao ni kuwa mapori yalikuwa hayajaisha kwa wengine kwenda kufyeka na kulima. " Anazungumza Mzee Mwamwindi. Anaonekana kuwa na mengi sana, na hamu ya kusimulia zaidi. Nabaini pia, kuwa kwake yeye mkuu yule wa mkoa ni Kleruu na hamtaji kama ' Dr Kleruu'. Namwacha aendelee.
" Sasa baada ya ile alhamisi, mzee akashinda Ijumaa. Jumamosi ikawa siku ya Krismasi. Kwa vile wafanyakazi wake wa shambani walikuwa mapumziko ya krismasi. Na yeye ni mwislamu, na alikuwa mchapa kazi kweli, basi, alikwenda shamba lake la jirani akiwa na mdogo wangu, sasa ni marehemu, anaitwa Mohamed. Wakawa wanalima kwa trekta.
Siku hiyo Kleruu, pamoja na kuwa ni Mkristo, aliamua kutokula Krismasi. Alivaa kofia yake ya pama. Inaaminika alibeba pistol yake pia. Kleruu akaendesha mwenyewe gari lake la mkuu wa mkoa aina ya Peugeot Injection, rangi ya bluu. Katika orodha yake, Kleruu alikuwa na watu watatu wa kuwashughulikia miongoni mwa wakulima wale wakubwa wa Isimani. Target nambari moja alikuwa Bw. Rashid Juma wa Nyangólo. Nambari mbili ni marehemu baba. Namba tatu simjui.
Kleruu alipofika Nyang'olo hakumkuta mkulima Rashid Juma. Siku hiyo ya Krismasi Rashidi Juma alipata habari, kuwa kuna ng'ombe wake walipotelea milimani. Alikwenda huko milimani kusaka ng'ombe wake. Hivyo, Kleruu akafunga safari kurudi kwa target namba mbili, baba yangu Mzee Mwamwindi. Ni njia hiyo hiyo, Nyang´'olo iko mbele ya ilipokuwa ngome ya mzee." Anasema Mwamwindi akionekana kuzama katika simulizi inayomgusa. Nami namsikiliza kwa makini.
"Basi, Kleruu akafika kwa Mzee. Baba akiwa shambani akaliona gari la Kleruu limesimama nje ya mji wake. Kisha akamwona Kleruu akitembea kumfuata shambani. Baba alihisi tu, kuwa Kleruu amekuja na shari.
Kleruu akamwuliza Mzee kwa ukali, " Mbona mnafanya kazi leo siku ya Krismasi?". Baba akamwomba Kleruu waende wakuzungumze nyumbani. Akamwambia mdogo wangu Mohammed aendelee kulima. Mzee akatangulia mbele, nyuma anamfuatia Kleruu. Kabla ya kufika kwenye nyumba yake wakayapita makaburi. Kleruu akamtamkia baba mzee Mwamwindi; " Hapa ndipo unapozika mirija yako?" Alitamka hivyo huku akimtomasa tomasa mzee na kifimbo alichoshika mkononi.
Jambo hilo lilizidi kumkasirisha marehemu mzee. Akafika nyumbani kwake. Mlangoni alisimama mke wake mdogo. Inaonekana mzee alishafanya uamuzi. Jana yake alikwenda kuwinda. Hakupata mnyama. Bunduki yake moja aia ya riffle kati ya bunduki zake mbili ilikuwa bado ina risasi. Akamwambia mke wake mdogo huku Kleruu akiwa anasikia;
" Kanichulie bunduki yangu"
" Je, aliposikia hayo Dr Kleruu alifanyaje?"
" Nadhani alipigwa na butwaa. Hakuamini kama baba angefikia hatua hiyo"
"Na ilikuwaje basi Mwamwindi alipoletewa bunduki?"
" Ilienda haraka, Mzee Mwamwindi akainua bunduki yake. Tayari ilikuwa loaded na risasa tangu jana yake alipotoka kuwinda. Kleruu aliinua mikono yote miwili kama mtu anayesalimu amri. Mwamwindi akampiga risasi ya kwapani. Kleruu akabaki hai. Akapiga risasi nyingine. Ikamwua pale pale." Anasimulia Mzee Amani Mwamwindi.
Kinafuatia kimya. Anainama, namwona usoni, kuwa huzuni imemjia. Bila shaka, ni kitendo kile cha baba yake kumpiga risasi na kumwua Dr Kleruu ndicho kilichoashiria mwanzo wa ukurasa mgumu katika familia ya Mwamwindi , Isimani na pengine Iringa kwa ujumla.
Nafikiria kumwuliza swali lifuatalo; Risasi ya pili ya Mzee Mwamwindi ilimpiga Dr Kleruu katika sehemu gani ya mwili? Nasitisha swali hilo. Litasubiri mara nyingine. Mzee Amani Mwamwindi anaendelea kunisimulia;
" Mdogo wangu Mohammed akiwa shambani alisikia mlio wa bunduki. Alidhani kuwa baba amepigwa risasi. Alikimbia kurudi nyumbani. Na pale ilipowekwa kumbukumbu ya Kleruu nyuma yake ndio ilipokuwa nyumba ya mzee. Hivyo, pale ulipowekwa mnara ni mbele ya nyumba. Kwa sasa nyumba hiyo haipo.
Alipofika nyumbani, Mohammed akamkuta baba amesimama, na Kleruu amelala chini, amekufa. Mzee alichukua kofia ya pama ya Kleruu, akaivaa. Akaingiza mkono mifukoni mwa Kleruu, akachukua funguo za gari la Kleruu. Mzee alimwambia mdogo wangu amsaidie kumwinua Dr Kleruu. Mzee alimshika miguuni na mdogo wangu Mohammed alimshika kwenye mikono. Wakamwingiza kwenye buti la gari.
Baba akaendesha mwenyewe gari lile la Mkuu wa Mkoa Kleruu, Peogeot Injection, rangi ya bluu likiwa linapepea bendera ya taifa. Aliendesha kuelekea mjini Iringa. Njiani kuna walioshangaa kumwona Mwamwindi akiendesha gari la Mkuu wa Mkoa huku akiwa kichwani amevalia pama la Kleruu.
Mzee alipoingia mjini Iringa breki ya kwanza ilikuwa hapa tulipo, nyumbani kwangu Mlandege. Kama nilivyosema, wakati huo nilikuwa kijana wa miaka 21. Nilishakuwa na mji wangu, nilijenga kibanda changu hapa tulipo. Nilifanya kazi kama karani wa Ushirika. Siku ile ya tukio nami nilikwenda kwenye shamba langu Ifunda.
Basi, Mzee alipofika hapa nyumbani akaambiwa kuwa nimekwenda shamba Ifunda. Alisikitika sana." Anasema Mzee Mwamwindi huku naye bado akionyesha huzuni machoni. Miaka 40 baada ya tukio.
Alipotoka hapa alipita nyumbani kwake pale Mshindo, na baadae akasimama kwa binamu yake. Ile nyumba ya njano nyuma ya benki ya CRDB, si unaijua?" Ananiuliza.
" Ndiyo" Namjibu.
" Pale alikuwa anakaa binamu yake na baba. Basi, alipofika pale akakutana n abinamu yake. Binamu yake yule alishangaa kumwona mzee akiwa na damu kwenye nguo zake. Akashangaa pia kumwona akiwa na gari la Kleruu lenye bendera ya taifa ikipepea. Akamwuliza nini kimetokea? Mzee hakuweza kuongea akaeleweka. Alitamka; " Nimeenda kwa Amani ( Mimi) nimeambiwa kaenda shambani kwake Ifunda". Alionekana kuchanganyikiwa.
Akaingia kwenye gari. Akaendesha moja kwa moja hadi Kituo cha polisi. Akamkuta polisi kijana. Akashuka, akamwambia; " Njoo chukua mzigo wako". Akaweka chini pia kofia ya pama ya Kleruu.
Polisi alipofungua buti ya gari akashangaa kuona mzigo wenyewe ni mwili wa Mkuu wa Mkoa, Dr Kleruu. Mzee akawa amejisalimisha.
Niliporudi nyumbani kutoka Ifunda nikazikuta habari hizo mbaya. Nikaenda moja kwa moja hadi nyumbani kwa Mzee pale Mshindo. Nikawakuta akina mama wanalia. Ilikuwa ni kilio. Hiyo bado ilikuwa ni Jumamosi, siku ya Krismasi. Nikauliza; kuna aliyekwenda kumwona baba pale polisi? Jibu likawa hapana. Nikaenda moja kwa moja polisi ili nikamwone baba na nimsikie kauli yake.
Nilipofika polisi nikaanza kujieleza kwa askari polisi kuomba ruhusa ya kuongea na Mzee. Wakati nikifanya hivyo mzee nae alisikia sauti yangu. Akatamka; " Mwanangu huyo, mruhusu niongee nae". Nikaongea na Mzee.
Chanzo: Majid Mjengwa
Mwanzoni mwa miaka ya 1970 Mkulima said Mwamwindi alikabiliwa na shitaka la kumwua Dr Wilbert Kleruu, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa wakati huo.
Mshitakiwa Mwamwindi alijitetea kuwa alipokuwa anamwua marehemu Kleruu alirukwa na akili . Hivyo, akapotewa na fahamu ya kuweza kuelewa kile alichokuwa anakitenda. Jaji Onyiuke kutoka Nigeria aliukataa utetezi wa Mwamwindi kwa kutilia maanani kwamba baada ya mshitakiwa kughadhibishwa ndipo alipokwenda ndani kuchukua bunduki ambayo aliitumia kumwua marehemu.
Mwezi Oktoba mwaka 2010, nikiwa njiani kwenda Dodoma na Arusha, nilipita kijijini Isimani. Hapo ndipo yalipokuwa makazi ya Mwamwindi. Ni umbali wa kilomita zipatazo 40 kutoka Iringa Mjini. Kijijini Isimani Saidi Mwamwindi bado anaonekana ni shujaa kwa kukataa kunyanyaswa na Mkuu wa Mkoa. Inasimuliwa, kuwa ilikuwa siku ya Jumapili , tena siku ya Krismasi, pale Mkuu wa Mkoa, Dr Kleruu, alipofika Isimani na kumkemea Mwamwindi mbele ya wake zake kwa vile alifanya kazi za shamba siku ya Sikukuu.
Inasimuliwa, kuwa Dr. Wilbert Kleruu alifikia hata hatua ya kuanza kudhihaki makaburi ya mababu zake Mwamwindi akimwambia Mwamwindi: "Humu ndimo mlimozika mirija yenu". Alifanya hivyo huku akionyesha makaburi yake kwa kutumia fimbo aliyoshika mkononi. Mwamwindi alikasirika sana. Akaficha hasira yake. Kutoka makaburini, Mwamwindi aliongozana na Kleruu hadi nje ya nyumba yake. Akamwomba Mkuu huyo wa Mkoa abaki nje. Mwamwindi akaingia ndani chumbani.
Mke wake Mwamwindi alimwona mume wake akichukua bunduki na kusimama dirishani. Mama huyo alidhani mumewe amepanga kwenda kuwinda. Kumbe, Mwamwindi alitokea dirishani na kumwelekea Kleruu aliyedhani Mwamwindi angetoka nje kwa kupitia mlangoni.
Basi, Mwamwindi akamlenga Mkuu wa Mkoa sawa kichwani. Dr kleruu alinyosha mikono juu na kuomba asemehewe. Mwamwindi alikaa kimya. Kisha akafyatua risasi. Kishindo kilisikika kijijini. Baada ya hapo, kwa mikono yake, Mwamwindi akaubeba mwili wa Mkuu wa Mkoa na kuuweka nyuma ya boneti ya gari alilojia mkuu huyo wa mkoa.
Mwamwindi alichukua kofia ya pama aliyovaa Kleruu. Akaivaa kichwani na kuanza kuendesha gari hilo hadi kituo cha polisi Iringa. Waliokutana na Mwamwindi njiani walimshangaa akiendesha gari hilo la Mkuu wa Mkoa akiwa amevalia kofia ya mkuu huyo. Hatimaye Mwamwindi akafika kituo cha Polisi.
Akatoka na kwenda mapokezi. Hapo akaripoti tukio kwa kutamka; " Nendeni mkamchukue mbwa wenu nyuma ya gari!".
Tukio lile bado linatuachia maswali? Je, ni kwanini Dr Kleruu alikwenda nyumbani kwa Mwamwindi siku ya Jumapili na hususan siku ya Krismasi?
Je, yawezekana Mwamwindi na Dr Kleruu walikuwa na ugomvi mwingine kabla ya tukio?
Kuna waliokuwepo na wanasimulia kana kwamba ilikuwa ni jana tu. Mmoja wa watu hao ni mwana wa Mkulima Said Mwamwindi aitwaye Amani Mwamwindi ambaye ndiye Meya wa Manispaa ya Iringa kwa sasa. Amani Mwamwindi anakumbuka nini juu ya siku hiyo?
hi wana JF,
Nimewasili jana jioni toka shamba kwenye shughuri zangu za kujitafutia Riziki, njiani nilinunua Gazeti la Mwananchi. Duh, lina bonge la Makala isomekayo MKULIMA ALIYEMPIGA RISASI,KUMUUA RC KLERUU. Kwa wale wanaopenda kufahamu Histori ya Nchi hii, nawashauri Mtafute gazeti la Mwananchi la tangu Juzi (tar. 20 June, 2016) ili muweze kufahamu ujasiri wa Mzee Mamwindi.
Nawatakia usomaji mwema.
View attachment 358893View attachment 358894