Dr Slaa: Lowassa ni sehemu ya matatizo yanayoikabili nchi kwa sasa

CHASHA FARMING

JF-Expert Member
Jun 4, 2011
7,789
8,914
Sunday, 26 June 2011

ASEMA anawakejeli Watanzania, ni sehemu ya matatizo


Hussein Issa na Fidelis Butahe

KATIBU Mkuu wa Chedema Dk Wlibroad Slaa ameunga mkono kauli ya Mbunge wa Monduli,Edward Lowassa na kumponda kuwa mbunge huyo ni sehemu ya matatizo yanayoikabili Tanzania hivi sasa.

Dk Slaa alisema kuwa Lowassa hakupaswa kutoa kauli hiyo kwa kuwa naye ni mmoja wa viongozi waliokuwa madarakani katika Serikali ya awamu ya nne, ambao hawakufanya vizuri hadi alipoamua kuachia madaraka kwa kujiuzulu.

Dk Slaa alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa Chuo kikuu cha Ualimu Dar es Salaam (DUCE), katika ukumbi wa TCC Changómbe Dar es Salaam. "Naiunga mkono kauli yake, lakini sio yeye, kwa sababu yeye mwenyewe ni miongoni mwa viongozi waliokuwa madarakani kipindi kile."

Alisema kimsingi ni kweli kuna matatizo ya usafiri wa reli, msongamano na makontena bandarini na ujenzi wa bandari na taifa kukabiliwa na mgawo wa mara kwa mara wa umeme uliodumu tangu mwaka 2006, lakini akasema kuna watu waliotakiwa kuyazungumza siyo Lowassa. Akizungumza katika mahojiano na Mwananchi Jumapili baada ya mkutano huo, Dk Slaa alisema kauli ya Lowassa ni kama kejeli kwa Watanzania na kwa viongozi walioko madarakani kwa sababu na yeye ni miongoni mwa waliokuwa madarakani

Aliongeza kwamba, kauli ya Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli kusema Serikali inasumbuliwa na ugonjwa wa woga katika kutoa uamuzi mgumu ni ya kejeli kwa kuwa hata yeye alikuwa mtendaji mkuu wa serikali. Lowassa, ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa kwanza katika utawala wa awamu ya nne, aliitaka Serikali hiyo kubadilika na kuwa na maamuzi magumu alitoa kauli hiyo bungeni wakati akichangia hotuba ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya mwaka 2011/2012.

Alisema kuwa ni bora kulaumiwa kwa kufanya uamuzi mgumu kuliko kulaumiwa kwa kutofanya uamuzi na kwamba, Serikali inapaswa kufanya uamuzi bila kujali matokeo yake. "Ni bora kulaumiwa kwa kufanya maamuzi kuliko kulaumiwa kwa kutofanya maamuzi kabisa," alisema Lowassa.

Aliongeza, "Kuna ugonjwa wa kutokutoa maamuzi hapa na lazima tukubali kubadilike. Ni heri mtu ukosee kutoa maamuzi kuliko kukaa kimya kabisa, heri uhukumiwe kwa kutoa maamuzi mabya kuliko ulaumiwe kwa kushindwa kutoa maamuzi." Naye Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Azaveri Rwaitama alisema kwamba kauli ya Lowassa ni sawa na kiini macho kwa sababu yeye mwenyewe ni wa upande huo wa Serikali. Alisema wakati wa kipindi chake uwaziri mkuu, Lowassa aliyaona matatizo yote ya nchi, lakini alishindwa kuyakabili.

Rwaitama alisisitiza: Anachokisema Lowassa ni kiini macho." Alisema Watanzania hawataki kuongozwa na watu wanaotaka umaarufu bali wanataka kuongozwa na wachapa kazi na siyo vinginevyo. Alisema kauli ya Lowassa inaonyesha wazi kuwa kuna ushindani unaendelea ndani ya serikali hali aliyodai inaweza kuleta mtafaruku mkubwa baadaye. "Mimi sina chama, awali nilikuwa TANU, lakini niliirudisha kadi baada ya kuona hakuna maelewano mazuri ndani ya chama, hivyo kwa sasa nipo tu bila ya chama'' alifahamisha Aliongeza kwamba haitakiwi kuruhusu vikundi ndani ya tabaka tawala kwani linaweza kuharibu nchi kabisa. Alisema huu sio muda wa kuongozwa na viongozi wanaotaka kuchukua nchi kiujanjaujanja kwani matokeo yake yatakuwa sio mazuri hapo baadae.

Maandamamo
Katika hatua nyingine, Dk Slaa amewaambia wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ualimu Chang'ombe (DUCE) kuwa kuandamana ni haki yao na ya kila raia wa Tanzania. Dk Slaa ametoa kauli hiyo huku taifa likiendelea kukabiliwa na migomo na maandamano maeneo mbalimbali. Hata hivyo alisema kwamba ingawa yeye hawezi kuchochea vurugu, lakini wananchi kufanya maandamano si jambo la ajabu, pale wanapoona kuwa haki na amani havifuatwi katika nchi yao. Alisisitiza kwamba kila mtanzania ana haki ya kuishi, kuheshimika, kusema na kushiriki katika maamuzi. "Tatizo sisi tukisema ukweli tunaambiwa tunachochea wanafunzi na wananchi kuandamana…., sasa tusiposema ukweli huu tutausemea wapi; hiyo ndio kazi ya siasa, Serikali na Jeshi la Polisi wanatakiwa kulijua hili.

Hata hivyo aliwaonaya wanafunzi hao akisema: "Ukiandamana kwa ushabiki wangu wewe hufai kuitwa mwanachuo."

Dk Slaa ambaye alikuwa akitoa mifano mbalimbali inayoweza kumsukuma mtu kuandamana alisema kuna upotoshaji mkubwa katika upimaji wa maendeleo ya nchi.

Alisema siku zote anayeambiwa ukweli huumia huku akilishukia Jeshi la Polisi nchini kuwa kupiga marufuku maandamano ni upuuzi kwa kuwa kupitia maandamano baadhi ya mambo yamewekwa sawa ikiwa ni pamoja na bei za bidhaa mbalimbali. Huku akitoa mfano wa baadhi ya vitabu vilivyoandikwa na Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1968 vilivyogusia haki, amani na usawa, alisema amani sio ukosefu wa nchi kuwa na mapigano bali ni Watanzania kujitawala wenyewe kuwa na uhuru wa kufanya mambo yao bila kuingiliwa na mtu.

Alisema: "Kujenga barabara, nyumba za kifahari na shule sio maendeleo bali hivyo ni vyombo vya kuleta maendeleo tena kama vyombo hivyo vitatumika kweli kuleta maendeleo."


SOURCE: Mwananchi newspaper.
 
Yeah nimesimama imara mkono wake wakuume! Hizi ni kauli zenye tija na zenye mashiko toka kwa kiongozi thabiti chaguo la aliyejuu!!
 
Kwakweli mtifuano wa madaraka ndani ya ccm ni hatari kubwa kwa taifa kwani hivi ni vita vikubwa kati ya kambi tatu kwasasa kati ya mweenyekiti na kanbi yake mpya na mapacha watatu wa ufisadi na mapacha wengine watatu wa CCJ. CCM ISIPOONDOLEWA MAPEMA ITATUPELEKA MAHALI PAGUMU SANA
 
Mbona Lowasa hajakosea kabisa au mimi ndio sijaelewa?
  1. Mbona serikali inalaumiwa kwa kushindwa kufanya maamuzi magumu ya kumchukulia Lowasa hatua! huu ni uongo jamani?
  2. Serikali imeshindwa kufanya maamuzi magumu ya kufukuzakazi ndugu na marafikize Lowasa waliovurunda katika idara za serikali kumlinda kama Edwardo Heseah wa PCCB, mbona huu sio uongo Lowasa anasema ukweli kabisa.
  3. CCM ili ahidi kumfuka Lowasa, R. Azizi na Chenge lakini Serikali ya Kikwete imeshindwa kufanya maamuzi hayo hata hii mna taka kusema Lowasa kadanganya kweli jamani?
Ebu fakarini maneno ya Lowasa kwa mapana yake, maana kama serikali ya Kiwete hisinge kuwa ni serikali ya kushindwa kuchukuwa hatua leo hii Lowasa hasingelikuwa Bungeni hata siku moja.
 
Dr. kafanya vyema sana kuwafafanulia watanzania mbinu za huyu fisadi kutaka kuwahadaa wananchi, na mi naomba liwe somo kwa JK, kuwa majority ya wana magamba wapo against him, na sasa wameanza kuonyesha live!
 
Naona Slaa ananza kumponda mapemaa mpinzani wake kwenye urais 2015!
My take: At least tunafahamu utendaji wa Lowasa, je utendaji wa Slaa tutaupima vip? Hajawahi kushika nyadhifa kubwa serikalini!! Au tukamuulize baba askofu?
 
Jamani kwani Lowasa kusema vile ni kosa? Kwani c ukweli serikali imeshindwa kufanya maamuzi magumu ya kumfukuza yeye na wezi wenzake?so Lowasa yupo sahihi2.
 
Naona Slaa ananza kumponda mapemaa mpinzani wake kwenye urais 2015!
My take: At least tunafahamu utendaji wa Lowasa, je utendaji wa Slaa tutaupima vip? Hajawahi kushika nyadhifa kubwa serikalini!! Au tukamuulize baba askofu?

Mkuu huyo Dr Slaa amekuwa mbunge.
Amewahi kuwa mwenyekiti wa kamati za bunge.
Hakuwa serikalini kwani alikuwa upande wa upinzani ,michango yake bungeni ilikuwa ya manufaa kwa taifa.
Dr Slaa ni mtu makini na serikali inataka mtu makini sio kufanya kazi kwa mazoe tu.
 
Kitendo cha Lowassa kusimama kwenye chombo cha kutunga sheria yaani bunge na kuanza kukosoa serikali huku akitoa mapendekezo ya nini kifanyike, na wapi is increadibly scary! Assume Office ya Waziri mkuu itachukuwa ushauri aliotoa Lowassa wa (a) kuwafanya maamuzi bila woga na hata kukopa bila kujali madhara yake na (b) kuvunja vunja muundo wa office ya waziri mkuu na kupunguza idadi ya wizara/idara. Je, nani anauhakika kwamba Lowassa kweli ana nia njema ya kuleta ufanisi ndani ya serikali na sio janja yake ya ku-hodhi nguvu (powers) ili atimize azma yake - whatever that azma is?

Ikumbukwe kuwa wakati akiwa Waziri mkuu Lowassa aliwekeza (kwa kasi ya ajabu) TAMISEMI na hata sasa serikali inapata matatizo maana wako watendaji wengi (RC, DC etc) wanawajibika kwake yeye Lowassa-literally, pamoja na kwamba alijiuzulu uwaziri mkuu. Na kwanini yeye Lowassa hakugawa hizo wizara/idara alipokuwa waziri mkuu? why now? au ameshindwa 'kum-fix' Pinda? au anahofia list mpya wa TAMISEMI yaani RC, DC, DED etc ikitangazwa inaweza kuondoa 'waumini' wake?

Ukiangalia vizuri kauli ya Lowassa kuwa 'ni afadhali ulaumiwe kwa kufanya maamuzi kuliko kutofanya maamuzi kabisa' unaweza kuona ni kwa jinsi gani huyu Mheshimiwa na 'ngozi' ngumu. Ina maana Lowassa anaona ni afadhali (yeye) kulaumiwa kwa kutuletea hili jinamizi la RICHMOND-DOWANS ambalo sasa limezaa Symbion na bado nchi iko kwenye giza? Hivi inakuwaje kiongozi/msimamizi mkuu wa shughuli za serikali anashinikiza kampuni HEWA ipewe tender ya kutoa huduma kwa sekta muhimu, pengine sekta mama kama umeme? Huu ujasiri wa kutoona kadhia aliyowapa watanzania kautoa wapi Lowassa? kwa nabii Joshua?

Nimalizie, wabunge woooote waliokuwa wanamshangilia wakati anatoa hizi nasaha zake mpya wanaweza kutumbia ni kwa nini hasa walifanya hivyo? Au walishukiwa na roho mtakatifu maana mtoa nasaha katoka kwenye maombi maalum Nigeria? Wanaweza pia kutuelea walijisikiaje mionyo mwao walinyanyuwa mikono na kuanza kugonga meza ndani ya bunge wakati huyu mheshimiwa anaongea?
 
SIKU moja baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kuwashambulia viongozi wa serikali ya Rais Kikwete kuwa waoga wa kutochukua maamuzi magumu, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibroad Slaa, amesema serikali inawadanganya wananchi kwa takwimu zisizo na ukweli.

Slaa, alisema serikali ya Rais Kikwete imekosa umakini wa kuchukua maamuzi magumu yenye manufaa kwa taifa na matokeo yake Watanzania wanaendelea kuwa masikini ilhali nchi ina rasilimali lukuki.

Kauli hiyo aliitoa jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (DUCE), ambapo alisema Watanzania hivi sasa wamekata tamaa kutokana na ugumu wa maisha huku serikali ikishindwa kuchukua maamuzi magumu ya kuboresha hali za wananchi wake.

Alibainisha kuwa serikali imekuwa ikiwadanganya wananchi kwa takwimu mbalimbali kwa lengo la kuwapa imani, matumaini na ahadi ambazo haiwezi kuzitekeleza, kwa sababu ya kutokuwapo kwa kiongozi wenye uwezo wa kusimamia maamuzi magumu.

Alisema katika kampeni za Uchaguzi Mkuu zilizofanyika mwaka jana, alikuwa akizinadi sera za CHADEMA pamoja na kuahidi kusimamia maamuzi magumu juu ya mgawanyo wa rasilimali za taifa ambazo sasa zinawanufaisha watu wachache pamoja na wawekezaji.

“Mara nyingi katika kampeni zangu wakati nilisema CHADEMA ikiingia madarakani itafanya maamuzi magumu ili Watanzania waweze kunufaika …sasa Lowassa juzi katoa kauli kama yangu kwa chama chake na viongozi wa serikali iliyopo madarakani, naungana naye,” alisema.

Alibainisha kuwa maisha hivi sasa yamekuwa magumu zaidi na serikali inayoongozwa na CCM imekuwa kwenye matatizo ya kifedha kwa sababu fedha nyingi za umma ilizitumia kusaka madaraka kwenye Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwaka jana na kutawaliwa na mizengwe ya hapa na pale.

Alisema mgawo wa umeme kwa nchi nzima uliotangazwa hivi karibuni na Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO), umesababishwa na ombwe la uongozi uliopo ambao ulitumia fedha nyingi katika uchaguzi na mambo yasiyo na tija kwa taifa.

Aliongeza kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, anapaswa kujiuzulu kutokana na tatizo hilo kujitokeza mara kwa mara huku yeye akiendelea kutoa sababu zisizo na mashiko kwa jamii.

Alisisitiza kuwa Ngeleja, anatakiwa kutoa kauli kwa umma na bungeni kwa mujibu wa kanuni ya 49 ya Bunge kuhusu mgawo mkubwa wa umeme unaoigusa mikoa 18 inayopata nishati hiyo kupitia Gridi ya Taifa.

Alisema kutokana na ombwe la uongozi lililopo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ameshindwa kuingilia kati ili kupunguza muda uliotajwa na TANESCO kuhusu mgawo huo unaoathiri uchumi wa taifa na mtu mmoja mmoja.

Alisema maelezo ya kwamba mgawo huu umesababishwa na mitambo ya IPTL kuzalisha megawati 10 badala ya 100 kutokana na upungufu wa mafuta mazito (HFO), yanatosha kwa serikali kuwajibika kutokana na uzembe wenye kulitia hasara taifa.

Alisema mahitaji ya mafuta ya mitambo ya IPTL au mingineyo si jambo la dharura, bali lilikuwa linajulikana mapema lakini halikuchukuliwa kwa umakini, kwa sababu ya uongozi mbovu uliopo.

Alibainisha kuwa tatizo kubwa la mgawanyo usiozingatia masilahi ya wananchi ni miongoni mwa mambo yanayowafanya wananchi waendelee kudidimia katika lindi la umaskini ambalo chanzo kikubwa ni mikataba mibovu na viongozi kukwepa kuchukua maamuzi magumu.

Alisema mgawo wa rasilimali za nchi kwa kiasi kikubwa zinashikiliwa na watu wachache na wawekezaji wenye kumiliki uchumi huku idadi kubwa ya Watanzania ikiendelea kuwa mashuhuda wa zinavyowanufaisha wenzao.

“Mgawanyo wa rasilimali kati ya Watanzania na wawekezaji hauko imara na sawa, serikali inadanganya katika takwimu za vitabuni na kuwataka Watanzania waamini hivyo, haya mambo ni lazima yabadilike,” alisema.

Katika hatua nyingine, Dk. Slaa alimpongeza Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, kwa kuwasema viongozi wa serikali, kwa kuogopa kuchukua maamuzi magumu yenye manufaa kwa taifa.

Alisema Lowassa amefanya jambo la msingi, kwani kama maamuzi magumu hayatachukuliwa na viongozi, Watanzania wataendelea kuwa maskini zaidi na hivyo kutishia mustakabali wa taifa.

“Wananchi wamekata tamaa, viongozi wanaogopa kuchukua maamuzi magumu kama alivyosema Lowassa, mnadhani amani na utulivu vinavyoimbwa hivi sasa vitaendelea kuwapo?” alihoji.

Juzi, Lowassa wakati akichangia hotuba ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya mwaka 2011/2012, alisema serikali inasumbuliwa na na ugonjwa wa woga katika kufanya maamuzi magumu, ndiyo maana mambo mengi hayaendi kama yanavyopaswa na kuitaka ibadilike.

Katika hatua nyingine, Dk. Slaa alizindua tawi la CHADEMA katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuwataka vijana kutumia elimu watakayoipata kueneza amani na uhuru uliopo kwa masilahi yao na vizazi vilivyopo na vijavyo.

“Mwalimu Nyerere alikuwa akizungumza mengi kuhusu amani, utulivu na uhuru tulionao kwamba umepatikana kwa elimu yetu …hivyo kuna kila sababu ya kueneza haya bila woga, kwa kuwa vijana wa chama hiki ndio tegemeo letu kwa kila kitu,” alisema Dk. Slaa.
 
Naona Slaa ananza kumponda mapemaa mpinzani wake kwenye urais 2015!
My take: At least tunafahamu utendaji wa Lowasa, je utendaji wa Slaa tutaupima vip? Hajawahi kushika nyadhifa kubwa serikalini!! Au tukamuulize baba askofu?

Kaka Lowasa hawezi kuwa mpinzani wa Dr. Slaa kwenye uchaguzi ujao katika nafasi ya urais. Fahamu kuwa tutafanya uchaguzi chini ya katiba mpya ambayo kwanza itaweka uwanja sawa kwa kila mgombea, pili itaweka wazi vigezo vya mgombea urais.

Kwa vigezo hivyo tutagundua kuwa Lowassa anatakiwa kusubiri kujibu mashitaka ya uhujumu uchumi na kufanya a series of criminal acts za kupanga uhalifu ambao kwa sasa unalicost taifa kwa kukaa gizani 12 hours in any one day.

Sasa mtu huyu hawezi kuwa kwenye calibre ya kiongozi wa ngazi yoyote ile, anatakiwa kuwa jela akisubiri mashtaka yanayomkabili. Hakutakuwa na dhamana kwa sababu uhalifu alioufanya umesababisha watu wengi kufa hapa Tanzania kwa kukosa madawa, ajali zinazosababishwa na barabara mbovu, n.k.
 
nILIKUWEPO, kwa kweli 2015 ni mapigano ya kweli, na si kazi ya Dk Slaa tu, tupambane kuikomboa Tanzania!
 
Kwahiyo Lowassa kusema ni tatizo? hivi haki yake kikatiba inaanzia wapi? Halafu km alishakubali kujiuzulu kwa uwajibikaji tunataka tumuadhibu kiasi gani? Tunahitaji maoni yenye maana au watu wenye kutoa maoni ht km hayana maana? Tunapata shida gani.kujadili alichosema lowassa? Tukianza kumtazama kila mtu kimaadili hakuna atakayesimama
 
Kwahiyo Lowassa kusema ni tatizo? hivi haki yake kikatiba inaanzia wapi? Halafu km alishakubali kujiuzulu kwa uwajibikaji tunataka tumuadhibu kiasi gani? Tunahitaji maoni yenye maana au watu wenye kutoa maoni ht km hayana maana? Tunapata shida gani.kujadili alichosema lowassa? Tukianza kumtazama kila mtu kimaadili hakuna atakayesimama
umsimtetee huyo msanii hana hoja kama anaweza atuambie richmond n ya nan?tunamwelewa malengo yake yenu,mtashindwa tu
 
Tatizo sio aliyoyasema Lowasa. Yupo sahihi kabisa. Tatito yametoka kwa mtu ambaye tunamashaka kama anamaanisha anachokisema. Alipata nafasi ya kuongoza serikali lakini maamuzi magumu aliyochukua ndio yaliyozaa Richmund. Sasa kama hayo ndio maamuzi anataka serikali iyachukue, tutazidi kupotea. Ningefurahi kama angetaja areas ambazo maamuzi magumu yanahitajika. Hilo lingesaidia sana.
 
Tumtendee haki Lowassa. Katika mawaziri wote wa JK, ni yeye pekee aliyekuwa akithubutu kuamua mambo mazito na kuyafuatilia kwa commitment kama mambo yake binafsi.

Tumeona ya City water, hakuogopa kuwatimua wale majizi na kuvunja mkataba wao, japo walitushitaki potelea mbali lakini uamuzi ulifanywa na badiliko likawepo.

Alithubutu kwenye shule za kata, na sasa tunaziona. Japo si nzuri sana lakini kila kitu kina mwanzo, ninaamini hazitafungwa hizi shule wananchi wataendelea kuziboresha. Uamuzi. Alithubutu kusimamia suala la umeme, ndipo akauingia ule mkenge wa Richmond. lakini ndiyo matokeo ya kuthubutu. Unapothubutu, unachukua risk. Wanaoogopa risk ndio hawa tunaowaona legelege tu hakuna wanachofanya.

Mi namsapoti Lowasa, ni jasiri anathubutu na matokeo yapo hata kama mengine ni mabaya, ni bora kuliko zero. Mimi nafananisha uthubutu wa Lowassa na ule wa Simba wa Vita Hayati Rashidi Kawawa; alithubutu kutenda na hakuzikimbia lawama zilizotokana na uthubutu wake.

Ninaamini hata JK anajua kuwa kipindi kile Lowasa ndiye alikuwa rais, sasa hivi kuna ombwe, hakuna rais, kuna kundi la watu waoga ambao wanajadili mambo kwa hofu tu bila kuamua chochote!
 
Nafikiri hatumtendei haki Lowasa kwa kumshambulia baada ya kutoa maoni. Inawezekana baada ya kukaa nje ya game, amepata muda mzuri wa kutafakari, kujifunza na , kufanya utafiti. Sasa anajua ni wapi alikosea na anajua ni nini cha kufanya illi kusaidia maendeleo ya nchi.

Swala la richmond hakukosea chochote. Maana richmond ndo ilikuwa iuzie umeme Tanesco kwa bei ya chini kuliko kampuni nyingine yoyote ile. Angeiacha kampuni hii pia asingeeleweka. Kushindwa kwa richmond ni matokeo ya kawaida ya kibiashara. Sidhani katika nchii hii ni mradi pekee wa richmond ulioshindwa kutekelezeka kwa wakati. Richmond walileta mitambo ingawa ilichelewa.

Kuchelewa kwa project kubwa kama hii ni jambo la kawaida. Sakata la Richmond limekuzwa tu kisiasa kwa sababu baada ya mitambo kufika kampuni ya dowans iliichukua na kuanza kuzalisha umeme kwa makubaliano na richmond. Ila kwa ushabiki wa kisiasa mkasitisha mkataba na dowans.

Eti sheria ya manunizi ilikiukwa. Tatizo la watanzania wanafikiri sheria zote ni nzuri. Moja ya sheria mbaya na ambazo zinaliingizia hasara taifa hili ni hii sheria ya manunuzi. Licha ya kuwa na urasimu mkubwa pia hai guarantee anayeitumia kupata kitu bora.

Katika crisis kama ile iliyokuwepo Waziri mkuu yeyote mchapa kazi na asiyeogopa kufanya maamuzi angeenda hata through single source iki umeme upatikane.

Simtetei Lowassa katika mambo mengine, ila katika hili la Richmond.
 
Tumtendee haki Lowassa. Katika mawaziri wote wa JK, ni yeye pekee aliyekuwa akithubutu kuamua mambo mazito na kuyafuatilia kwa commitment kama mambo yake binafsi.

Tumeona ya City water, hakuogopa kuwatimua wale majizi na kuvunja mkataba wao, japo walitushitaki potelea mbali lakini uamuzi ulifanywa na badiliko likawepo.

Alithubutu kwenye shule za kata, na sasa tunaziona. Japo si nzuri sana lakini kila kitu kina mwanzo, ninaamini hazitafungwa hizi shule wananchi wataendelea kuziboresha. Uamuzi. Alithubutu kusimamia suala la umeme, ndipo akauingia ule mkenge wa Richmond. lakini ndiyo matokeo ya kuthubutu. Unapothubutu, unachukua risk. Wanaoogopa risk ndio hawa tunaowaona legelege tu hakuna wanachofanya.

Mi namsapoti Lowasa, ni jasiri anathubutu na matokeo yapo hata kama mengine ni mabaya, ni bora kuliko zero. Mimi nafananisha uthubutu wa Lowassa na ule wa Simba wa Vita Hayati Rashidi Kawawa; alithubutu kutenda na hakuzikimbia lawama zilizotokana na uthubutu wake.

Ninaamini hata JK anajua kuwa kipindi kile Lowasa ndiye alikuwa rais, sasa hivi kuna ombwe, hakuna rais, kuna kundi la watu waoga ambao wanajadili mambo kwa hofu tu bila kuamua chochote!
mkubwa,

hata kukubali kuongeza wingi wa vyuo vikuu lowassa alisaidia. sasa hata hawa vijana vilaza ambao zamani wasingegusa lecture theatre sasa wanasoma.
kila siku sasa wanashinda kwenye siasa. wamshukuru lowassa wangekuwa wanalima vijijini.
 
Tumtendee haki Lowassa. Katika mawaziri wote wa JK, ni yeye pekee aliyekuwa akithubutu kuamua mambo mazito na kuyafuatilia kwa commitment kama mambo yake binafsi.

Tumeona ya City water, hakuogopa kuwatimua wale majizi na kuvunja mkataba wao, japo walitushitaki potelea mbali lakini uamuzi ulifanywa na badiliko likawepo.

Alithubutu kwenye shule za kata, na sasa tunaziona. Japo si nzuri sana lakini kila kitu kina mwanzo, ninaamini hazitafungwa hizi shule wananchi wataendelea kuziboresha. Uamuzi. Alithubutu kusimamia suala la umeme, ndipo akauingia ule mkenge wa Richmond. lakini ndiyo matokeo ya kuthubutu. Unapothubutu, unachukua risk. Wanaoogopa risk ndio hawa tunaowaona legelege tu hakuna wanachofanya.

Mi namsapoti Lowasa, ni jasiri anathubutu na matokeo yapo hata kama mengine ni mabaya, ni bora kuliko zero. Mimi nafananisha uthubutu wa Lowassa na ule wa Simba wa Vita Hayati Rashidi Kawawa; alithubutu kutenda na hakuzikimbia lawama zilizotokana na uthubutu wake.

Ninaamini hata JK anajua kuwa kipindi kile Lowasa ndiye alikuwa rais, sasa hivi kuna ombwe, hakuna rais, kuna kundi la watu waoga ambao wanajadili mambo kwa hofu tu bila kuamua chochote!
Nakuunga mkono mtu B, at least yeye kuna aliyoyafanya kwa muda ule mfupi mpk leo tunayahesabu. binafsi namshukuru sana kutumalizia kero yetu ya shekilango road. kama ingekuwa ni msanii Pinda mpaka leo tungekuwa tunaogelea kwenye yale mahandaki
 
Back
Top Bottom