Elections 2010 Dk Slaa: Ni gharama kubwa kuiacha CCM i...

mrefu36

Member
Aug 16, 2010
71
22
Dk Slaa: Ni gharama kubwa kuiacha CCM iongoze nchi Send to a friend Tuesday, 24 August 2010 22:55 0diggsdigg

slaaaaaa.jpg
Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Dk Wilbroad Slaa

Elias Msuya
MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chadema, Dk Wilbroad Slaa amesema kuwa ni gharama kubwa kuiacha CCM iendelee kuiongoza nchi, huku akiweka bayana kaulimbiu ya chama hicho kwenye uchaguzi inayosema "2010 Hatudanganyiki".

Dk Slaa, ambaye amestua anga za kisiasa baada ya kuamua kugombea urais na kuliacha Jimbo la Karatu, alisema kwa miaka 49 tangu uhuru serikali ya CCM imeshindwa kuondoa kero walizonazo wananchi na pia imeshindwa hata kusimamia vyema vipaumbele ilivyojiwekea.

Alisema hayo jijini Dar es Salaam jana katika mahojiano maalum na gazeti hili kuhusu mchakato mzima wa kampeni za chama hicho na uamuzi wa kugombea nafasi hiyo ya juu nchini.

“Wakati tunapata uhuru, (rais wa serikali ya awamu ya kwanza) Mwalimu Nyerere alisema kuwa atapambana na maadui watatu ambao ni umasikini, ujinga na maradhi lakini cha kusikitisha ni kwamba baada ya miaka 49 maadui hao wako na taifa limeendelea kujiongezea maadui wengine. Adui wa nne aliyeongezwa ni ufisadi, huu ndio unavuruga kabisa nchi,” alisema Dk Slaa.

“Ufisadi na wizi ndio uliotawala katika serikali ya CCM. Hata chakula cha wafungwa magerezani kinaporwa na askari. Fedha za miradi ya maendeleo zinahamishiwa kwa watu binafsi.

Watanzania tunapewa pipi badala ya kilo ya nyama. Hayo ndiyo tunaambiwa maendeleo maana kila siku wanatulisha pipi. Ni sawa na kusema kuwa wanatupiga changa la macho! Kwa kweli ni gharama kubwa kuiacha CCM iendelee kututawala.”

Dk Slaa, ambaye amebobea kwenye sheria baada ya kusomea nyanja tofauti, alisema kuwa tangu mwaka 2001 hadi 2008 Watanzania ambao ni masikini wa kutupwa wameongezeka kutoka milioni 11 milioni hadi milioni 12.9.

Kwa upande wa elimu, alisema kuwa wakati wa Mwalimu Nyerere kulikuwa na kisomo cha manufaa kiasi cha Tanzania kusifiwa na Unesco kwa kufikia kiwango cha asilimia 70, lakini sasa kimeshuka hadi asilimia 40.

Alisema kwa takwimu za Mpango wa Maendeleo ya Sekondari, serikali ilitakiwa kujenga shule 22,000 lakini hadi sasa imejenga shule 300 tu.

“Tunahitaji kufanya mabadiliko ya haraka sana na mabadiliko hayo hayawezekani kufanywa na serikali ya CCM,” alisema.

DK Slaa, ambaye pia ni katibu mkuu wa Chadema, alisema kuwa kaulimbiu ya chama hicho kwenye kampeni za mwaka huu za uchaguzi mkuu ni "2010 Hatudanganyiki", ambayo inaelezea dhana nzima ya imani yao kuwa ni gharama kubwa kuiachia CCM iendelee kuitawala nchi.

Akitaja vipaumbele vyake endapo atapata urais na kuunda serikali, Dk Slaa alisema kuwa ataibadilisha katiba ya Jamhuri ya Muungano mara tu atakapoingia madarakani.

Alisema kuwa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inampa mamlaka makubwa mno rais, kiasi cha kufanya lolote analotaka.

“Tunataka kuwa na katiba itakayomwelekeza rais jinsi ya kuunda serikali. Siyo kumpa madaraka rais kuunda wizara anazotaka na kumchagua mtu anayemtaka.

Hii ni hatari sana kwani maamuzi makubwa ya nchi yamewekwa mikononi mwa mtu mmoja tu,” Dk Slaa alisema.

Alisema kwa kuwa rais ana mamlaka ya kuunda wizara ndiyo maana Tanzania leo tuna mawaziri na manaibu wake 48 ambao kimsingi wanaongeza mzigo kwa walipa kodi.

“Asilimia 60 ya kodi zinazokusanywa na serikali zinatumika kwa ajili ya kugharamia uendeshaji wa serikali na wala hazielekezwi katika maendeleo ya wananchi, vipi nchi hii itaendelea ikiwa mkurugenzi wa wizara anabadilishiwa samani za nyumbani kwake kila mwaka?

Vipi tutaendelea ikiwa viongozi wetu tunawanunulia mashangingi ambayo gharama zake tunaweza kujenga shule na zahanati kwa ajili ya wananchi,” alihoji Dk Slaa.

“Nikipata madaraka nitabadilisha katiba ili tuwe na mawaziri 20 tu au hata 15,” alisema Dk Slaa.

Alisema kuwa kazi kubwa ya manaibu waziri waliopo sasa ni kujibu maswali ndani ya Bunge ambayo, hata hivyo, alisema hushindwa kuyajibu.

Katika kipaumbele cha huduma za jamii, Dk Slaa alisema kuna ufisadi mkubwa unaoendelea katika Mpango wa Maendeleo wa Sekta ya Kilimo (ASDP), akisema kuwa asilimia 80 ya bajeti yake imepotea huku Tanzania ikiomba msaada wa chakula kila mwaka.

“Hii ni aibu kabisa. Kila mwaka tunaomba msaada wa chakula kutoka nje. Ni mwaka huu kwa sababu tu mvua zimenyesha sana. Tunaweza kujaza kabati kwa kauli mbiu za kilimo lakini hazijatusaidia kitu. Kwenye ASDP asilimia 80 ya fedha zimeliwa,” alisema.

Alisema kuwa Tanzania inaweza kulisha nchi nyingine za Afrika kama kutakuwa na utekelezaji mzuri wa mikakati ya kilimo.

“(Rais wa zamani wa Marekani, Bill) Clinton alipokuja Tanzania aliomba apewe bonde la Mto Rufiji ili ailishe Afrika. Naamini kabisa tunaweza kuwa na 'basket grain' (mfuko wa chakula) ya Afrika,” alisema.

Kuhusu miundombinu, Dk Slaa alisema kuwa Tanzania inapaswa kuwa na garimoshi linalotumia umeme na siyo kuendeleza garimoshi zinazotumia dizeli ambazo zimekuwa zikitumika tangu wakati wa ukoloni. Alisema kuwa usafirishaji kwa njia ya malori unaotumika sasa una hasara kubwa kwa serikali ukilinganisha na usafirishaji kwa njia ya reli.

Akizungumzia ndoa yake, Dk Slaa alisisitiza kuwa alishaachana na Rose Kamili ambaye amezaa naye watoto na akamtambulisha mchumba wake mpya Josephine katika mkutano wa hadhara wilayani Karatu,

“Mimi niko wazi na nilishaweka wazi masuala haya kwa wananchi wangu wa Jimbo la Karatu. Kama ningeficha nisingemtambulisha mke wangu mpya katika mkutano wa hadhara huko Karatu. Ni haya mambo ya uchaguzi tu yameingilia lakini tulikuwa tuko kwenye mchakato wa kuoana,” alisema Dk Slaa.
 
Elimisha sana labda utaeleweka. Maana wabongo akipewa pilau au khanga au fulana au kofia basi anatoa kura. Hafikirii kesho yake mwenyewe na kizazi chake.
 
Khanga,kofia na fulana thamani yake kwa ujumla haifiki ata laki moja but mtu anadiriki kurbuniwa na ivyo vitu na kujiingiza katika mateso ya miaka mitano.
Ivi tunaitaji malaika kutuelimisha juu ya ilo.
Keep it up Slaa ipo siku watanzania watakuelewa
 
Ni wangapi hapa Tanzania ambao hawafikiwi na ujumbe maridhawa kama huu. Tunatakiwa kufanya mipango ya kueleka elimu hii kwa watu vijijini ili waelimike na kuibeza sisiem kwa ahadi za uongo zisizotimizwa.
 
(Kuelimisha mpumbavu ni sawa na mwenye kuunga vigae). Ni kwa nini watanzania wengi tumekuwa na akili kama kigae, kikivunjika kinakuwa takataka.

Mabadiliko yanawezekana!!!
 
](Kuelimisha mpumbavu ni sawa na mwenye kuunga vigae). Ni kwa nini watanzania wengi tumekuwa na akili kama kigae, kikivunjika kinakuwa takataka.

Mabadiliko yanawezekana!!!

wengine wasema ni sawa na kumkanda mbwa kiuno
mix with yours
 
Back
Top Bottom