Dk. Mwakyembe afunguka! Aeleza mkakati wa kumuua ulivyopangwa...

Kiganyi

JF-Expert Member
Apr 30, 2012
1,242
765
attachment.php


  • Muuaji wake alitoa taarifa za mpango
  • Profesa Mwandosya asema wote walipimwa yaleyale
  • Sugu amtaka Dk. Mwakyembe CHADEMA
  • Sitta aponda siasa za Tanzania

Raia Mwema | Toleo la 260 | 26 Sep 2012

SHUHUDA zilizotolewa wakati wa ibada ya shukrani ya Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, zilikuwa ujumbe tosha kuhusu kuwapo kwa mitandao ya kiharamia iliyolifikisha Taifa pabaya.

Ibada hiyo ya shukrani ilifanyika katika Kanisa la Kiinjili la Moravian Tanzania, Usharika wa Nduli katika Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya Jumapili iliyopita, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali, wakiwamo mawaziri, wabunge na viongozi wa Serikali na vyama vya kisiasa mkoani Mbeya.

Kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, wananchi wamekuwa na hamu ya kufahamu hasa ugonjwa uliomsibu mwanasiasa huyo huku ikiaminika miongoni mwa wengi, wakiwamo viongozi wa kisiasa, kwamba ulitokana na sumu ambayo hata hivyo mazingira ya kupewa kwake imebaki kuwa ni kitendawili hadi leo.

Kila aliyepata nafasi ya kuzungumza alibainisha utukufu wa Mungu ulivyodhihirika katika matukio mbalimbali nchini, hususan, yaliyohusu mikasa dhidi ya baadhi ya viongozi wa kisiasa nchini, hivyo kufichua dhambi ambazo waliamini kuwa hazikufahamika, na wananchi kutoufahamu ukweli wa madhila yaliyowasibu viongozi wao.

Dk. Mwakyembe aliamua kumshukuru Mungu kutokana na mambo makuu aliyosema alimtendea katika miaka mitatu iliyopita ikiwa ni pamoja na kumuokoa kwenye ajali mbaya ya gari iliyotokea mkoani Iringa, Mei 2009, na njama za kumuua yeye pamoja na baadhi ya viongozi wengine wa kisiasa, dini na watu mashuhuri nchini, matukio yote hayo yakiwa yametolewa taarifa katika Jeshi la Polisi lakini yakiachwa bila kufanyiwa kazi.

Lakini lililoshtua zaidi ni ugonjwa wa ajabu uliompata mwaka jana kiasi cha Serikali kulazimika kumkimbiza katika Hospitali ya Apollo nchini India ambako walifanikiwa kubaini kuwapo kwa kemikali kwenye ute katika mifupa yake (bone marrow), ambazo ndizo zilikuwa zikisababisha kuharibika kwa ngozi yake pamoja na kunyonyoka nywele.

Katika ushuhuda wake, Waziri Nchi, Ofisi ya Rais, Profesa Mark Mwandosya ambaye naye alihudhuria ibada hiyo, alisema pamoja na mambo mengine kwamba kilichomshangaza ni kuona vipimo alivyofanyiwa Dk. Mwakyembe ni vile vile alivyofanyiwa yeye na hivyo kubainisha kuwapo kwa mahusiano katika ugonjwa waliougua.

Profesa Mwandosya ndiye aliyetangulia kwenda katika Hospitali hiyo ya Apollo nchini India, ambapo awali alitarajia kutumia juma moja tu asifahamu ukubwa wa tatizo lililokuwa likimkabili. Akiwa hospitalini hapo ilibainika Waziri huyo kukabiliwa tatizo kubwa zaidi ya alivyotarajia hivyo kulazimika kukaa kwa zaidi ya miezi sita akitibiwa.

"Nikiwa India nikampigia simu kumuomba msamaha kwa kutomuaga, na nikamuomba anapokuja jimboni kwake apitie na Busokelo (Jimbo la Rungwe Mashariki kwa Profesa Mwandosya), lakini baadaye kidogo nikashangaa kuambiwa naye kaletwa India kwa matibabu," alisema Mwandosya na kuongeza: "Siri ambayo sikuwahi kuieleza ni kwamba, vipimo walivyomfanyia ni vile vile walivyonifanyia mimi."

Kuugua kwa mawaziri hao wawili kwa wakati mmoja, tena wenye kutambulika kama mtu na ndogo wake, wakiwa wanatoka mkoa mmoja, majimbo yaliyo jirani yenye kukaliwa na watu wa jamii moja, kulizua sintofahamu ambayo hadi sasa haifahamiki iwapo wananchi wa Mkoa wa Mbeya wamesamehe.

Hali halisi, pamoja na kutowekwa bayana, ni kwamba wananchi walio wengi mkoani humo hawana imani na Serikali yao pamoja na chama tawala, mazungumzo yao yanathibitisha hilo, hususan, pale wanapohoji kulikoni kila mzawa wa Mkoa huo anapoibuka, hukutwa na masahibu ya kutisha.

Mazungumzo kuhusu madhira yanayowakuta wazawa wa mkoa huo ni jambo la kawaida kuyakuta maofisini, vijiweni na maeneo mbalimbali ya mikusanyiko, ambapo huyataja majina kuanzia marehemu Stephen Kibona, waziri wa fedha wa zamani, ambaye hadi leo hawaamini kwamba kifo chake kilikuwa ni cha kawaida.

Hawaishii hapo, wanayakumbuka majina ya kina marehemu Profesa Jwani Mwaikusa aliyeuawa kikatili kwa kupingwa risasi nyumbani kwake jijini Dar es Salaam, Profesa Mwandosya na Dk Mwakyembe walionusurika kifo kutokana na ugonjwa wa ajabu uliowakuta, na hivi karibuni zaidi, Dk Stevev Ulimkoka, aliyeongoza mgomo wa madaktari akaishia kutekwa na kufanyiwa ukatili wa kutisha akinusurika kufikwa na mauti katika mazingira ya kimiujiza.

Mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa Kituo cha Channel Ten mkoani Iringa na Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoani humo, marehemu Daudi Mwangosi, yamezidisha hasira ya wananchi hao dhidi ya Serikali, wakiamini kuwa ni mpango mahsusi wa kuwamaliza wazawa wa mkoa huo wenye kujitokeza na kujenga majina nchini.

"Mwaka 2009 nilipata ajali mbaya kati ya Makambako na Iringa mjini. Kitu ambacho sitokisahau milele ni kwamba niligongwa na lori," alisimulia Dk. Mwakyembe Jumapili.

Alisema pamoja na tukio hilo na matukio mengi mengine yaliyomwandama na kuyaripoti katika Jeshi la Polisi, lakini amekuwa akishangazwa na watendaji katika jeshi hilo kwa kuyasemea matukio hayo pasipo kuyafanyia uchunguzi jambo ambalo limekuwa likimkera na kupoteza imani kwalo.

Dk. Mwakyembe ambaye alitumia nafasi hiyo kuwaelezea wananchi wa jimbo lake namna anavyoandamwa kuuawa pamoja na ugonjwa wa ajabu uliompata ghafla na kusema matukio yote hayo yamekuwa yakipotoshwa vibaya na watendaji wakuu wa ndani ya Polisi.

Aidha, alisema miongoni mwa walioshuhudia ajali hiyo ni Mkurugenzi wa Taasisi moja ya elimu yenye kuendesha shule za sekondari na vyuo katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, Mboka Mwambusi, ambaye akiwa na mchumba wake wakati huo wakielekea jijini Dar es Salaam walimkuta Dk. Mwakyembe akiwa mahuttuti huku dereva wake, Jose Msuya akitokwa damu, na kuwakimbiza hospitali ya Mkoa wa Iringa.

"Polisi tuliyemkuta aliniambia niondoke, kwani Dk. Mwakyembe hakuwa mzima tena, alishafariki. Namshukuru ndugu yangu Jose, alinisisitizia kuwa alikuwa hai, nimharakishe hospitali, nikamshusha abiria niliyekuwa naye, nikashusha michele na ndizi, tukampakia na kumkimbiza hospitali," alisimulia Mkurugenzi huyo.

Kwa mujibu wa Mwambusi ajali hiyo ya Dk. Mwakyembe aliyoipata Iringa, ni miongoni mwa matukio ambayo hatayasahau katika maisha yake, akisema litaendelea kudumu katika kumbukumbu zake milele.

Lakini lililoshitua wengi waliohudhuria katika ibada hiyo ni simulizi ya Dk Mwakyembe kuhusu jinsi alivyofuatwa na mtu aliyepangwa kumuua, hiyo ikiwa ni Desemba 28, mwaka 2009.

Alisema: "Niliandaliwa mpango wa kuuawa kati ya Iringa na Mbeya. Aliyepangwa kuniua ni mhalifu sugu, lakini Mungu alijiinua, muuaji alinifuata akaniambia unaenda safari ya Kyela, usiende, ukienda nitakuua."

Katika maelezo yake hayo ambayo yaliwaacha wahudhuriaji wa ibada hiyo ya shukrani wakiwa wamepigwa butwaa, alisema muaaji huyo alimweleza mpango mzima wa mauaji ulivyopangwa na kumpa uhuru wa kumrekodi maelezo yake, ambayo ameyahifadhi hadi leo.

Katika matukio yote yaliyomsibu ndani ya miaka hiyo mitatu, Dk. Mwakyembe alisema amekuwa akilitaarifu Jeshi la Polisi, lakini anasema pia kwamba wakati wote hawakuchukua hatua zozote zaidi ya kuendesha juhudi za kuficha ukweli.

Pengine lililowaumiza walio wengi ni ugonjwa aliougua, ambao anasema katika mazingira ya kushangaza kumekuwapo na juhudi za kuupotosha umma.

"Mwaka 2011 niliugua, cha kusikitisha niliugua wakati huo huo na kaka yangu Profesa Mark Mwandosya. Mungu ni mwema, alitunyanyua vitandani, leo tunatembea. Mimi na kaka yangu Mwandosya ni ushahidi juu ya utukufu wa Mungu," alisema Dk. Mwakyembe.

Katika kile kinachosababisha wananchi wengi, akiwamo yeye mwenyewe, waamini kuwa ugonjwa uliomsibu ni wa ajabu, hali aliyokuwa nayo alipofikishwa India anasema iliwatisha hata madaktari waliokuwa wakimhudumia.

"Daktari aliyenitibu, aliniambia amefanya kazi yake hiyo ya udaktari kwa zaidi ya miaka 27, lakini hakuwahi kuona ugonjwa wa aina ile," alisema Dk. Mwakyembe.
Aliongeza: "Sitta alipofika kuniona, nilisikitika sana kwa nini alikuja. Ndiyo maana aliporudi alikuja na kilio kwa Polisi akiwataka wachunguze, wakamgeuzia kibao... walisau kuwa Sitta (Samuel) ni mwanasheria aliyebobea."

Katika ushuhuda wake, Waziri wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta alihitimisha ibada hiyo kwa kuhoji: "Mungu hapendi uongo, na ukweli hauna tabia ya kujificha, ipo siku utadhihirika. Ikiwa Polisi walikuwa wanachunguza ugonjwa uliomsibu Dk. Mwakyembe, kwanini hawakwenda kwenye hospitali aliyokuwa akitibiwa?"

Waziri Sitta aliendelea kufichua udhaifu wa ndani ya siasa za Tanzania akisema: "Tatizo la nchi zetu hizi za Afrika ni siasa ya kiwango cha chini, viongozi wanajali maslahi yao na si maslahi mapana ya umma. Wapo watu, tunasheherekea hapa wao wamenuna, na wanafahamika, tutapambana na ubinafsi, tutapambana na ufisadi."

Ibada hiyo ilikusanya watu mbalimbali mashuhuri na miongoni mwa waliozungumza ni pamoja na Mbunge wa Kahama, James Lembeli, ambaye alibainisha kuwa matatizo yote aliyoyapata Dk. Mwakyembe yalitokana na tabia yake ya kuwa mkweli.

Kauli hiyo iliungwa mkono na Mbunge wa Mbarali, Modestus Kilufi na Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangala, huku Kilufi akibainisha kuwa tatizo la siasa za Tanzania ni kwamba wenye kusimamia ukweli huwa hawapendwi.

Akizungumza katika ibada hiyo, Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi alimshauri Dk. Mwakyembe kuachana na Chama cha Mapinduzi (CCM) na badala yake ahamie chama chake cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) akidai kuwa misimamo yake (Dk. Mwakyembe) haiendeni na ile ya chama chake.

"Kitu chochote ambacho hakijakuua, kinakupa nguvu zaidi. Kinachotuunganisha mimi na Dk. Mwakyembe, wote tuna ambition sawa, kusimamia maslahi ya Mbeya na Taifa letu kwa ujumla," alisema Mbilinyi.

Kiasi cha shilingi milioni 41.8 zilipatikana katika ibada hiyo ya shukrani kama sadaka kwa Mwenyezi Mungu, ikiwa ni sehemu ya waliohudhuria ibada hiyo kumuunga mkono Dk. Mwakyembe katika shukrani yake kwa Mungu kwa mambo makuu aliyomtendea, ikiwamo kumwepusha na kifo katika vipindi tofauti.

Kiasi hicho cha fedha kilichokusanywa wakati wa ibada hiyo ya shukrani, kimeelekezwa kutumika kwenye kukamilisha ujenzi wa jengo jipya la Kanisa la Usharika huo wa Nduli pamoja na ukarabati wa jengo la zamani litakalotumika kuendesha miradi ya maendeleo ya kina mama kijijini Ikolo, ikiwamo upishi na ushonaji.

Viongozi wengine waliohudhuria ibada hiyo ni pamoja na Naibu Waziri wa Elimu, Philip Mulugo, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba, aliyekuwa waziri wa maliasili na utalii, Ezekiel Maige na Mbunge Viti Maalumu, Hilda Ngoye.
 

Attachments

  • 093.JPG
    093.JPG
    250.7 KB · Views: 664
  • 698793425.JPG
    698793425.JPG
    44.5 KB · Views: 2,276
Mwakyembe yaonyesha kuwa unatambua kuwa zamu yako ya kunyolewa imefika, hivyo unakiroweka maji kichwa chako.
 
Mwigulu nchemba ajifunze siasa zenye kuwajali wananchi angalau kama hizi!
Sio yeye anapeleka mamluki kuwafanyia fujo wapinzani kisiasa kumbe wanaoumia ni wapiga kura.
 
Vipi huyu Mwakyembe hajafunguka tu?AU kagundua ni vipodozi vyake ndo vilivyomzuru!
vipodoz gani nawewe, sikuhizi mzee wawatu sijui anajipaka kiwi kichwani hadi usoni? Nampa pole sana kwa yaliyomkuta na hongera sana kwa kupona na kutoa shukrani
 
safi sana mh Sugu.....huu ni mfano bora kabisa wa siasa za upinzani nje ya bunge....baba cdm..mama ccm...watoto cuf...jioni mnakula meza moja......
 
AhaAa wanafiki wa Chadema mnapongeza Sugu geuzeni santuri iwe Zitto ndio kaandama na Sitta naona mziki wake JF pangekuwa hapatoshi
Chama
Gongo la mboto DSM
 
AhaAa wanafiki wa Chadema mnapongeza Sugu geuzeni santuri iwe Zitto ndio kaandama na Sitta naona mziki wake JF pangekuwa hapatoshi
Chama
Gongo la mboto DSM

Huyu Hapa!


Mbunge wa jimbo la Kigoma kaskazini Kabwe Zitto (kulia) akizungumza na mkuu wa wilaya ya Ikungi Manju Msambya wakiwa kwenye mazishi ya baba wa mbunge wa jimbo la Singida mashariki,Tundu Lissu.(Picha zote na Nathaniel Limu).
 
Hongera kwa uponyaji na kumkumbuka Muumba wako. Sikujua hii kitu ilikuwa serious kiasi hichi! Mpaka kucha zimekuwa nyeusi kabisa!
Mungu awasamehe waliohusika na tukio hili ovu zaidi duniani
 
Huyu Hapa!


Mbunge wa jimbo la Kigoma kaskazini Kabwe Zitto (kulia) akizungumza na mkuu wa wilaya ya Ikungi Manju Msambya wakiwa kwenye mazishi ya baba wa mbunge wa jimbo la Singida mashariki,Tundu Lissu.(Picha zote na Nathaniel Limu).

Safi sana.
 
AhaAa wanafiki wa Chadema mnapongeza Sugu geuzeni santuri iwe Zitto ndio kaandama na Sitta naona mziki wake JF pangekuwa hapatoshi
Chama
Gongo la mboto DSM
Siyo kweli ndugu,CDM imekuwa mfano wa mambo mengi ya kuigwa nchini,Sugu umetuwakilisha vyema kwa mheshimiwa sana Mwakyembe,
 
kibonde as an individual hauwezi mziki wa sugu,kapambana na clouds na ikulu nzima mpaka wame surrender na kuachia ile studio aliyotoa jk
 
Huyu Hapa!


Mbunge wa jimbo la Kigoma kaskazini Kabwe Zitto (kulia) akizungumza na mkuu wa wilaya ya Ikungi Manju Msambya wakiwa kwenye mazishi ya baba wa mbunge wa jimbo la Singida mashariki,Tundu Lissu.(Picha zote na Nathaniel Limu).

wakigoma wamekutana
 
Back
Top Bottom