Dk. Idris Rashidi alitabiri giza miaka miwili iliyopita

Lucchese DeCavalcante

JF-Expert Member
Jan 10, 2009
5,471
733
Mapema mwezi Machi, 2009 aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme (TANESCO) Dk. Idris Rashidi, alitoa taarifa ambayo kwa maslahi ya Taifa na kwa mjadala unaoendelea sasa kuhusiana na hali ya umeme, tunarejea taarifa hiyo ambayo itasaidia kuchochea mjadala zaidi na hatimaye kupata utatuzi.

Mwezi Disemba 2008 TANESCO iliwasilisha Wizara ya Nishati na Madini tathmini ya hali halisi ya uzalishaji ya umeme nchini kwa wakati huo, matarajio ya uzalishaji. Katika tathmini hiyo TANESCO iliwasilisha taarifa kwamba hali ya ukuaji uchumi unafanya kwamba mahitaji ya umeme yanaongezeka kwa megawati 745 kila mwaka. Kulingana na tathmini hiyo kwa hivi sasa nakisi ya mahitaji ikilinganishwa na uzalishaji ni megawati 150. Kwa maana hiyo ifikapo Disemba 2009 kwa hali ya uzalishaji wa sasa kama hapakuwa na ongezeko lolote nakisi hiyo itakuwa ni megawati 225 kwa uchache.

Aidha TANESCO ilizingatia kuwa katika kipindi hiki ilikuwa ni dhahiri kwamba ongezeko la uzalishaji uliotarajiwa kutoka vyanzo vya Kiwira na Tegeta visingeingia kwenye mtandao kwa muda uliokuwa umepangwa kwa sababu mbalimbali nje ya uwezo wa TANESCO. Kwa mfano Mradi wa Kiwira ambao megawati 200 toka 2009 umeathirika na malumbano ambayo yamewafanya wawekezaji wakubwa waliotarajiwa kushiriki kujitoa. Mradi wa Tegeta kwa megawati 45 ambao ulikuwa uanze uzalishaji mapema mwaka huu sasa utaanza uzalishaji mwezi Oktoba 2009.

Aidha tathmini ya hali ya mvua ndiyo chanzo cha umeme mkubwa kuliko wote na nafuu kuliko wote siyo ya kuridhisha. Utabiri wa hali ya hewa unaonyesha kwamba mvua za mwaka huu hazitolingana na viwango vya kawaida. Tayari mikoa ya Mbeya na Iringa ambayo ndiyo vyanzo vikuu vya maji ya Mtera mvua ni nvhini ya kiwango na katika maeneo mengine zimesimama.

Hali hii ilipelekea TANESCO kufanya tathmini ya kina kwenye ngazi zote na ndipo Menejimenti ikaomba Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika kulifikisha suala hili Wizarani kwa kuwa ilikuwa haitoshi kupeleka taarifa ya hali ya uzalishaji bila kwenda na mapendekezi ya ufumbuzi wa sula hilo. TANESCO ilifanya tathimini ya zabuni ya Dowans ya kuuza mitambo yake ilipotangazwa kwenye vyombo vya habari mwaka wa jana. Kwa wakati huo yaani Disemba 2008 baada ya kufanya tathmini ya masuala yake husika na mitambo hiyo, TANESCO ilipeleka Serikali ombi la kununua mitambo hiyo. Kwa kuwa manunuzi ya mitambo hii haikuwa ni ufumbuzi kamili TANESCO pia iliishauri Serikali kwa pamoja tukae na tubaini mpango wa haraka wa kuhakikisha kwamba uzalishaji wa nyongeza unaingia kwenye mtandao kwa kiasi ca megawati zisizopungua 200 katika miezi 24 ijayo kwa maana uzalishaji huo uwe umeingia kwenye mfumo kabla ya Disemba 2010 na ni zaidi ya megawati 105 zinazotarajiwa kuingia baada ya kumiliki mitambo ya Dowans.

Hatua hizi kwa muhutasari zilikuwa ni pamoja na Kuhakikisha kwamba megawati 45 za Tegeta na megawati 200 za Kiwira zinaingia kwenye mtandao, na ikibidi Serikali iongeze nguvu kwenye uwekezaji.

Uzalishaji wa chanzo cha maji cha Ruhuji ufanyiwe kazi haraka kwa kuwa uwekezaji wa mitambo ya maji unachukua miaka mingi na ili Ruhuji iongeze megawti 350 kwenye mfumo wa umeme ifikapo 2015 taratibu nyingi inabidi ziwe zimekamilika mwezi Machi 2009.

Mradi mwingine mkubwa na umeme utokanao na gesi asili ya Mnazi Bay megawati 300 ulitayarajiwa kuingia kwenye mtandao 2012 umekwama kutokana na matatizo ya kiuchumi duniani na taasisi za fedha ambazo zimewafanya wawekezaji wakubwa wa mradi huo kushindwa kuendelea.

Haya na mazingira mengine ya ndani na nje ya Taifa letu yakiwa pamoja na tathmini za masuala ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii, kiusalama, kisiasa kwa ujumla masuala mtambuka yanayohusu uzalishaji na matumizi ya nishati ya umeme ndiyo yaliyopelekea TANESCO kwenda Wizarani na kuwasilisha mapendekezo ya kununua mitambo ya Dowans ambayo kwa wakati huo zabuni yake ilikuwa imetangazwa. Aidha ni maoni yetu kwamba tukichukua tahathari mapema hatutoingia kwenye mtego usiokwepeka wa kukodi mitambo wakati nchi iko kwenye kiza huko siku za usoni.

Malumbano

Hivi karibuni kumekuwa na malumbano makubwa kuhusu suala zima la nia ya TANESCO kununua mitambo ya Dowans. Malumbano hayo kwa bahati sana, yamechukua sura tofauti kabisa na makusudio yaliolengwa wakati tunapeleka suala hili Serikali mwezi Disemba 2008. TANESCO iliwasilisha hoja zilizokuwa na misingi ya utaalamu, ya kiufundi na yaliozingatia mahitaji halisi na athari za kutokabili tatizo hili mapema. Tulifanya hivyo tukitambua, mazingira ya ukodishaji wa mitambo hiyo, lakini pia tumezingatia wajibu wetu wa kufanya tathmini ya masuala mapana zaidi yanayohusu mitambo hiyo ikiwa ni pamoja na ubora wake, na unafuu.

Unafuu wa kuipata mitambo hiyo pia ilikuwa inazingatia muda wa kununua hadi kupokea, kufunga na kuanza kutumia. Mitambo ya kununua toka kwa wazalishaji huchukua muda mrefu. Mfano halisi ni manunuzi ya mitambo mipya ya Ubungo ya aina ya Wartsila ya kuzalisha umeme wa megawti 100, uliofunguliwa mwezi Novemba 2008. Taratibu zote, kuanzia zabuni mpaka kupatikana kwa nishati ilichukua miezi 18.

Mitambo ya umeme hainunuliwi dukani kama ilivyo gari au trekta au mavazi. Huwezi kwenda kwa watengenezaji ukawaambia unataka mtambo ukaupata wakati huo huo au ndani ya wiki mbili kama baadhi ya watu, wakiwemo watu wazito wenye majukumu na dhamana kubwa wanavyosema. Taarifa hizi ziko mabli ki wa hali halisi, na zinalenga kwa makusudi kupotosha ukweli.

Uongozi wa TANESCO unaomba kuwasilisha kwa umma wa Watanzania masikitiko yake kuhusu kauli na taarifa mbali mbali ambazo zimekuwa zinatolewa kwenye vyombo vya habari. Tumehuzunika kwa taarifa hizi, nyingi ambazo katika nyakati nyingine wananukuliwa wanasiasa na wananchi wengine waandamizi “Senior Citizens” ambazo zimekuwa hazizingatii kabisa hoja tulizowasilisha bali zina mwelekeo wa kisiasa zaidi kuliko hali halisi ya upatikanaji wa umeme na kukua kwa matumizi.

Ukweli unapotoshwa

Hivi karibuni, kiongozi mmoja amenukuliwa akisema jitihada hizi ni za kuwasafisha mafisadi, ni kukiuka taratibu na sheria za nchi, na mwingine akasema akipatiwa fedha, anaweza akapata mitambo ya uwezo huu ndani ya wiki chache tu. Hizi ni kauli zinapotosha ukweli wala hazizingatii utaalamu bali zimejaa utashi wa kisiasa zaidi na zinachangia kuwavunja nguvu, mamia ya wafanyakazi wa TANESCO ambao wanafanya kazi kubwa, usiku na mchana ya kuhakikisha kuwa nchi inapata umeme wa uhakika. Kimsingi nia yetu ni kuhakikisha kuwa juhudi zetu za kujikwamua kiuchumi zinazotegemea mchango wa umeme hazikwami.

Sisi siyo wanasiasa, wala hatufanyi kazi zetu kwa kuweka mizani au kuangalia upepo wa kisiasa. Ni jambo la kuhuzumisha kwamba, miongoni mwa watu wanaotoa hoja za kupotosha umma, wengine wamepata nafasi ya kukaa nasi na kubadilisha nasi mawazo juu ya hali ya umeme. Mara zote, TANESCO tumeeleza kwamba tuko tayari kupokea maelekezo ya Wizara na kamati za Bunge kama taasisi za usimamizi na za uwakilishi wa wananchi. Katika kipindi hiki tumeona jinsi watu wengine wakiandika taarifa ambazo hazijafanyiwa tafiti yoyote, alimuradi mtu ana nafasi ya kuandika makala. Hii siyo sawa.

Ama cha kushangaza kabisa, ni kwamba hakuna wakati wowote ule, ambapo TANESCO imesema kwamba hatua za kununua mitambo hiyo hazitazingatia taratibu husika za kisheria au zinginezo, zinazofanyiwa kazi kuhusu tuhuma za ukiukwaji wa taratibu za kukodi mitambo hiyo awali. Tunashangaa kwanini watu wenye ufahamu mkubwa sana, wanachanganya mambo mawili haya. Ukweli ni kwamba hoja ya kununua mitambo haijahusisha masuala haya mawili tofauti.

Ni maoni yetu kwamba, tumewasilisha suala hili kwenye ngazi zote kwa ukweli uthabiti ambao umezingatia hali halisi ya sasa na inayotarajiwa. Tunaamini kuna hali inayozuia kuwa na mjadala wa uwazi na ukweli kuhusu masuala haya yenye misingi ya utaalamu. Masuala ya taaluma na ufundi, yanamezwa na hoja za kisiasa. Hali hii haina maslahi yeyote kwa mazingira haya tunayokabiliana nayo wala shirika la TANESCO.

Hitimisho

Kwa maana hii , kwa kuwa mwelekeo wa suala hili linatupeleka kwenye ugomvi wa wanasiasa, jukwaa ambalo sisi hatuna mamlaka nalo, TANESCO inatangaza rasmi kujitoa kwenye nia yake ya kununua mitambo hii. Ni imani yetu kwamba tumeishajieleza na kujenga hoja za kutosha, na wananchi wa Tanzania watafanya maamuzi yao hapo ambapo nchi itakapokuwa imegubikwa na kiza, mahospitali hayatoi huduma, viwanda havizalishi, wanafunzi vyuoni wanashindwa kusoma kwasababu tulishindwa kufanya maamuzi.

Kwa maamuzi haya, tunapenda kutoa taarifa kwamba TANESCO itaandika barua Serikalini kwa Waziri wa Nishati na Madini tukimfahamisha kuhusu maamuzi ya haya.
 
Back
Top Bottom