Diwani ‘amkwida’ Mwalimu Mkuu

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
WALIMU wa shule za msingi wa kata ya Olkokola, wilayani Arumeru, mkoani hapa wametishia kugoma kwa kitendo cha diwani wa kata hiyo, Joseph Laizer, kudaiwa kumkaba koo Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kitimu.

Mwalimu aliyekabwa koo ni Obed Keya baada ya kumrudisha nyumbani mwanafunzi wa shule hiyo, kwa kosa la kutolipa mchango wa Sh 2,000.

Mbali na kitendo cha kumdhalilisha mwalimu huyo, Diwani huyo anadaiwa kumporomoshea maneno makali na matusi huku akimtaka mwalimu huyo, ampe maelezo ya kina ya sababu za kumrudisha mwanafunzi huyo, ilhali akijua ni yatima.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kikao kilichoitishwa na walimu wa kata hiyo, walilalamikia hatua ya diwani huyo kunyanyasa walimu, huku akiwataka wafuate matakwa yake, kinyume na taratibu za mwajiri wao, wanapokuwa shuleni.

Taarifa zilizopatikana jana, kutoka kikao hicho zilisema, Diwani Laizer alimfuata mwalimu mkuu huyo, akiwa na mwanafunzi anayedaiwa kurudishwa nyumbani, na kumkwida shingo, huku akimtaka amrudishe mwanafunzi huyo darasani haraka iwezekanavyo.

Aidha inadaiwa Mwalimu Keya, ambaye alikuwa kwenye harakati za kwenda kusimamia mitihani katika shule nyingine jirani ya Lengijabe, alikumbwa na dhahama hiyo, iliyodumu takribani nusu saa, kabla ya mwalimu mwingine kujitokeza na kumnasua.

Kwa tukio hilo, walimu wote wa shule za msingi, zipatazo 10 za kata hiyo, walihamasishana na kutishia kugoma kufundisha hadi tatizo lao la kunyanyaswa mara kwa mara na diwani huyo litakapopatiwa ufumbuzi ikiwa ni pamoja na kuombwa radhi.

Walimwomba Mkurugenzi wa Halmashauri ya Arusha, Hilda Khalifa, ambaye ndiye mwajiri wao, kuwatafutia uhamisho haraka, hawataingia madarasani, mpaka diwani huyo aondoke.

Laizer alipoulizwa juu ya tukio hilo, alikiri kukwaruzana na mwalimu mkuu huyo, kiasi cha walimu wengine kutishia kugoma, ila alisema hakumpiga wala kumkaba shingo, isipokuwa yeye ndiye aliyetukanwa na mwalimu wa shule hiyo.

Alisema, alikwenda kwa Mwalimu Keya kwa lengo la kumwuliza sababu za kumrudisha nyumbani mwanafunzi huyo, lakini katika majibizano, alitokea mwalimu mwingine na kumtukana huku akimwita mlevi.

“Mimi sijamkaba wala kumnyonga, ila mimi ndiye nilitukanwa, wakati tukijibizana na mwalimu mkuu, alitokea mwalimu mwingine na kumwambia Mwalimu Keya kuwa aachane nami, kwa kuwa nilikuwa nimelewa,” alijitetea Laizer.

Diwani Laizer aliongeza kuwa mchango wa Sh 2,000 unaochangwa kwa wanafunzi wote shuleni hapo, yeye ndiye aliupendekeza, ila aliwataka walimu hao kutojihusisha na kukusanya fedha hizo, isipokuwa kamati ya wazazi.

Naye Khalifa alikiri kupata malalamiko juu ya uhusiano mbaya kati ya walimu na Diwani huyo.

“Nimepata malalmiko yao, ila sijasikia kama Diwani amemkwida mwalimu au kumpiga, hapana, bali hakuna maelewano mazuri kati yake na walimu, hivyo nimeagiza kamati za shule za kata wakae ili kupata utatuzi wa tatizo hilo na waniletee mapendekezo,” alisema Khalifa.

Kuhusu mwanafunzi kurudishwa nyumbani kwa kukosa mchango, alisema kuna taratibu za sheria, Diwani angezifuata na si kuanza ugomvi na kurushiana maneno na walimu.
 
Back
Top Bottom