Dhana ya UHURU na KAZI: Tuwekeze kwenye Elimu ya Watu wetu

Shayu

Platinum Member
May 24, 2011
608
1,653
Ni jambo muhimu sana kwetu kama tunataka kukua kiakili kila wakati kukumbushana na kuelimishana kuhusu mambo muhimu ambayo yana uwezo wa kujenga akili zetu na tabia zetu kuwa bora Zaidi lakini pia kujenga taifa letu. Leo nimeamua tuzungumzie kuhusu uhuru na kazi pamoja na uhuru na kujitegemea.

Kama raia ambaye umepevuka kiakili huwezi kufikiri kuhusu wewe tu kila wakati. Utafikiri kuhusu taifa lako na kuhusu jamii yako pia. Lakini pia majaliwa yako binafsi na majaliwa ya taifa lako. Na kushiriki kutoa mawazo ambayo unadhani yatakuwa na umuhimu katika ujenzi wa taifa lako. Na mimi nafanya hivyo kadiri niwezavyo. Napenda taifa hili na napenda watu wa taifa hili. Na kulitakia mema taifa hili kila wakati.

'' Kuna mambo mawili ambayo Nyerere alizungumzia ‘’Uhuru ‘’ Alafu na ‘’ Kazi’’. Ni wajibu wetu kujua maana ya ndani ya nadharia hizi mbili na mahusiano yake na maendeleo ya nchi yetu. Tusipojua nadharia hizi tutakuwa tunafanya jambo ambalo hatuna uhakika nalo kwamba malengo yake yalikuwa nini.

Dhana hizi mbili Uhuru na Kazi. Na Uhuru na kujitegemea zinaendana. Kwahiyo majadiliano yetu yatakuwa juu ya dhana hizi mbili ndio hoja yangu nitajengea hapo.

Uhuru ambao aliokuwa akizungumzia Nyerere ni uhuru tuliupata kutoka kwenye kutawaliwa kwetu na wakoloni. Uwezo wa kujiamulia mambo yetu na mwelekeo wetu kama taifa. Yaani uhuru wa kisiasa. Lakini kuna uhuru mwingine ambao taifa lolote linapaswa kuwa nao. Nao ni uhuru wa kiuchumi, ambao ndio unapelekea taifa lolote kujitegemea. Uhuru wa kiuchumi na uhuru wa kisiasa lazima uendane. Uhuru wa kisiasa ni uwezo wa nchi kujiamulia mambo yake na mwelekeo wake na kuwa na fikra huru zinazojitemea kama taifa.

Wanaposema UHURU na KAZI maana yake nini? Ni lazima kuwe na lengo, watu hawawezi kufanya kazi bila malengo. Ni lazima kuwepo na lengo katika jitihada ambazo watu wanafanya kwa kufanya kazi. Na lengo hilo lilikuwa ni kujitegemea. Kulifanya taifa letu kuweza kujitegemea. Kulifanya taifa letu kuwa na uhuru wa kiuchumi. Taifa letu kuwa na uwezo wa kuzalisha na kutumia kile inachokizalisha bila kutegemea msaada kutoka nje, au kuhitaji msaada kidogo sana kutoka nje, katika kuendesha mambo yake.

Toka uhuru mpaka sasa hivi tunaweza kujiuliza tumefanikiwa kwa kiasi gani katika dhana hizi mbili. Uhuru wa kisiasa tunao, ambao unatupa nafasi kufanya mambo yetu bila kuingiliwa. Jitihada ambazo zilitakiwa kufanyika ilikuwa ni kupata uhuru wa kiuchumi kwa nguvu ile ile ambayo tuliifanya katika kudai uhuru wa kisiasa. Na hii haikuwa ni kazi ya kizazi kimoja au viwili ilikuwa ni jitihada za muendelezo na kiu isiyofifia ya kupata ukombozi wa kiuchumi kama taifa. Lakini kwa kiwango kikubwa tulisinzia na tunaendelea kusinzia. Wakati wenzatu wakizidi kuchanja mbuga.

Maendeleo yetu hayalingani na miaka ambayo tumepata uhuru. Bado tuko nyuma katika maswala ya afya, elimu, miundo mbinu na hata kilimo. Hali yetu bado sio nzuri sana. Bado hatujajitegemea kwa kiwango kikubwa sana, bado tupo chini .

Mambo haya yote yanahitajika kuangaliwa upya na kujitathmini upya kama taifa. Changamoto tulizonazo hazitoondoka kama hatutakuwa na hamasa ile ile ambayo tuliyokuwa nayo katika kudai uhuru wa kisiasa kupata uhuru wa kiuchumi. Adui ni yule yule ila katika sura tofauti. Huwezi kujitawala kama hujajitegemea. Kujitegemea ni uwezo wa nchi kutimiza mahitaji yake.

Kwa kiwango kikubwa bado tunategemea vitu kutoka nje lakini sisi wenyewe hatuzalishi vya kutosha pamoja na kwamba tuna malighafi nyingi. Bado tunatumia vitu vingi vilivyotengenezwa nje. Na elimu yetu haijawezesha watu wetu kujitegemea hata kwa fikra. Na elimu ndio ilipaswa kuwa chachu ya kujitegemea kwetu.

Hatuwezi kutengeneza utajiri wa nchi yetu kama hatuzalishi na kutegemea vitu kutoka nje. Hatutaendelea kama hatutazalisha na hili sio jukumu la mtu mmoja ni la taifa.

Kwahiyo nataka mjue changamoto tulizonazo na kwamba tuna uwezo wa kukabiliana nazo kama tukiamua. Ni jambo ambalo liko chini ya uwezo wetu kama tukiwa na nia ya kubadili maisha yetu kama taifa. Lakini changamoto hizi zinahitaji umoja wetu na kujitolea kwetu.

Tunahitaji kubadili mwenendo wa siasa zetu ili kukabiliana na changamoto hizi. Na kama tunalipenda taifa hili tutakuwa tayari kubadili aina ya siasa tunazofanya. Ili taifa hili liwe lenye kuzalisha na lenye uwezo wa kujitegemea.

Naamini watu wetu wana akili, wamekosa siasa bora. Na misingi imara katika elimu yetu. Hatuwezi kuendelea kuingiza kila kitu ndani ya nchi yetu pasipo sisi wenyewe kuzalisha na kutengeneza, kwa vizazi vyetu vyote. Ni lazima tuzalishe tena kwa wingi. Ni lazima tuwekeze katika elimu ya watu wetu. Ni lazima tutengeneze.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom