S. S. Phares
JF-Expert Member
- Nov 27, 2006
- 2,138
- 82
Nimesoma ripoti ya CCM inayobainisha mafanikio ya Serikali ya Mkapa (1995 - 2005) nimekuta mambo mengi sana ya kujivunia. Isipokuwa ripoti hii imenizidishia maswali zaidi ya majibu....swali mpja kuu ni kuwa kwa nini bado bajeti yeti inategemea wafadhali kwa 50%..!!???
Hizi ni baadhi ya yaliyomo kwenye ripoti nzima inayopatikana hapa: http://www.ccmlondonuk.org/iyu.html
Hizi ni baadhi ya yaliyomo kwenye ripoti nzima inayopatikana hapa: http://www.ccmlondonuk.org/iyu.html
8. Mafanikio hayo ni kama yafuatavyo:-
(a) Mafanikio Katika Uchumi
(i) Pato la Taifa limeongezeka kutoka Dola (za Kimarekani) 5.6 bilioni mwaka 1995 hadi Dola 9.8 bilioni mwaka 2004 likiwa ni ongezeko la asilimia 75.
(ii) Pato la kila mtu limeongezeka kutoka Dola 160 mwaka 1995 hadi Dola 260 mwaka 2004 likiwa ni ongezeko la asilimia 62.5.
(iii) Ukuaji wa Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 3.6 mwaka 1995 hadi asilimia 6.7 mwaka 2004.
(iv) Mfumuko wa bei umeshuka kutoka asilimia 27.1 mwaka 1995 hadi asilimia 4.2 mwaka 2004.
(v) Asilimia ya Watanzania wanaoishi kwa kipato cha chini ya Dola moja ilishuka kutoka 50 mwaka 1995 hadi 20 mwaka 2004.
(vi) Utekelezaji wa Sera ya Ubinafsishaji wa Mashirika ya Umma umeweza kuiondolea Serikali mzigo mzito wa kuendesha uchumi moja kwa moja. Ubinafsishaji umeanza kujenga mazingira ya ongezeko la tija na ufanisi katika uzalishaji wa bidhaa za viwandani. Baada ya kubinafsishwa makampuni na mashirika hayo sasa yanaipatia Serikali mapato makubwa badala ya kuendeshwa kwa ruzuku ya Serikali.
(vii) Mauzo ya nje ya bidhaa yameongezeka kutoka thamani ya Dola 682.9 milioni mwaka 1995 hadi Dola 1,165.9 milioni mwaka 2004, likiwa ni ongezeko la asilimia 70.7
(viii) Akiba ya fedha za kigeni kwa ajili ya kuagizia bidhaa kutoka nje imeongezeka kutoka uwezo wa kukidhi mahitaji ya mwezi 1.6 mwaka 1995 hadi mahitaji ya miezi 9 mwaka 2004.
(ix) Ruzuku ya Serikali Kuu kwa Serikali za Mitaa ambazo ni chombo cha wananchi wenyewe cha kusimamia maendeleo yao kule kule waliko, imeongezeka kutoka Shilingi 12.3 bilioni mwaka 1995/96 hadi shilingi 392.2 bilioni mwaka 2004/05. Hili ni ongezeko la asilimia 3,088.6(yaani zaidi ya mara 30).
(x) Kutokana na mafanikio ya utekelezaji wa mikakati ya kuweka mazingira mazuri ya kuvutia vitega uchumi na kupambana na rushwa, hivi sasa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoongoza katika Afrika katika kuvutia uwekezaji. Mwaka 2004 Tanzania ilipata tuzo ya kuwa nchi ya kwanza Afrika kwa uwekaji wa mazingira mazuri ya uwekezaji. Uwekezaji wa moja kwa moja wa mitaji kutoka nje umeongezeka kutoka Dola 50.2 milioni mwaka 1995 hadi Dola 247.8 milioni mwaka 2004 sawa na ongezeko la asilimia 394.
(xi) Kutokana na mafanikio ya utekelezaji wa mikakati ya kupambana na rushwa na kuziba mianya ya ukwepaji wa kulipa kodi pamoja na zoezi la ubinafsishaji wa mashirika ya umma, hatua ambayo imeboresha uzalishaji, makusanyo ya mapato ya Serikali yameongezeka kutoka wastani wa shs. 25 bilioni kwa mwezi, mwaka 1995 hadi wastani wa sh. 160 bilioni kwa mwezi, mwaka 2005. Hili ni ongezeko la asilimia 540.
(xii) Tanzania ilitimiza masharti ya Mpango wa Kuzifutia Madeni Nchi Zenye Madeni Makubwa (HIPC) na hivyo kuingizwa katika Mpango huo mwaka 1999. Kutokana na hali hiyo, kuanzia mwaka 2002/2003 hadi 2004/2005, Tanzania ilitekeleza Mkakati wa Kupunguza Umaskini (MKU) ambapo fedha ambazo zingetumika kulipia madeni ya nje yaliyofutwa, sasa zilielekezwa katika sekta teule za huduma za jamii na kiuchumi na miundombinu zinazowagusa moja kwa moja wananchi wa kawaida kwa manufaa ya pamoja. Sekta hizo ni elimu, afya, maji, barabara za vijijini, kilimo na utawala bora, hususan Mahakama.
(xiii) Kutokana na juhudi za makusudi za kuimarisha utalii kwa lengo la kuchangia katika ukuaji wa uchumi na kuongeza ajira, idadi ya watalii walioingia nchini imeongezeka kutoka watalii 295,000 mwaka 1995 hadi 582,000 mwaka 2004. Hili ni ongezeko la asilimia 97.3 Aidha, mapato yatokanayo na utalii nayo yameongezeka kutoka Dola 259 milioni mwaka 1995 hadi Dola 746 milioni mwaka 2004, likiwa ni ongezeko la asilimia 188.0. Nafasi za ajira kwenye Sekta ya Utalii zimeongezeka kutoka 96,000 hadi 160,750 swa na ongezeko la asilimia 67.4.
(xiv) Kutokana na utekelezaji wa sera za makusudi za kuvutia wawekezaji wakubwa na teknolojia ya kisasa katika uchimbaji wa madini, hasa dhahabu, imefunguliwa migodi mikubwa Nzega, Geita, Kahama, Mara n.k. Kutokana na maendeleo hayo, uuzaji wa madini umeongezeka kwa kiasi kikubwa kutoka thamani ya Sh. 452.0 milioni mwaka 1995 hadi Sh. 22,786.0 milioni mwaka 2004 likiwa ni ongezeko la asilimia 4,941.
(xv) Kutokana na utulivu wa mazingira ya kisiasa na kiuchumi, biashara imechangamka nchini. Mchango wa Sekta ya Biashara kwa Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 2.4 mwaka 1995 hadi asilimia 16.8 mwaka 2004. Mchango wa Sekta ya Fedha umeongezeka kutoka asilimia 5.9 hadi asilimia 12.1 katika kipindi hicho. Mchango wa Sekta ya Viwanda nao uliongezeka kutoka asilimia 4.5 hadi 8.7. Aidha, mchango wa Sekta ya Madini kwa Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 0.1 mwaka 1995 hadi asilimia 3.0 mwaka 2004.