Dawa za kulevya Dar zauzwa kama njugu

Mbaha

JF-Expert Member
Nov 26, 2010
697
73
DAWA za kulevya zinauzwa kama njugu kwenye mikusanyiko ya watu hususan vijana, katika miji mikubwa ikiwamo Dar es Salaam.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa bangi, cocaine na mirungi, huuzwa zaidi katika viwanja vya michezo, vituo vya mabasi, klabu za pombe za kienyeji, nyumba za kulala wageni na kwenye baa. Biashara hiyo haramu, ambayo inawashirikisha pia vijana walio na umri chini ya miaka 18 kwa kuuza na kutumia, sasa inafanyika waziwazi, mchana kweupe.

Uchunguzi umebaini kuwa dawa za kulevya zinauzwa kama bidhaa nyingine halali huku baadhi ya wauza sigara wakitumika kuzisambaza kwa wateja.

Imebainika kuwa baadhi ya wafanyabiashara wakubwa na wanasiasa ndio vinara wa biashara hiyo, wakishirikiana na mtandao wa vigogo wa biashara hiyo nje ya nchi.

Kikwete na orodha ya wauza unga

Mwaka 2006 Rais Jakaya Kikwete alikabidhiwa orodha ya majina ya vigogo wanaofanya biashara ya dawa za kulevya wakiwamo, wabunge na baadhi ya wafanyabiashara maarufu nchini ili aifanyie kazi. Watu wanaojiita wanaharakati na wazalendo walitoa orodha ndefu ya vigogo hao wa dawa za kulevya nchini na kueleza kuwa wamewasilisha Ikulu kufanyiwa kazi.

Hata hivyo, Rais Kikwete mwaka 2006 alitangaza kuwa ana majina ya vigogo wa dawa za kulevya nchini na akawataka wanaojihusisha na biashara hiyo kujisalimilisha vinginevyo watanaswa na msako mkali utakaoanzishwa dhidi yao.

Alisema sasa umefika wakati kwa 'Wazungu wa Unga' kuamua kujisalimisha kwa kuachana na biashara hiyo au wakabiliane na mkono wa dola.

Lakini, uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa jijini Dar es Salaam, dawa hizo bado zinauzwa katika klabu za usiku na katika maeneo mbalimbali ya viwanja vya kuchezea mpira.

Biashara hiyo hufanyika katika vibanda vya kuuzia bidhaa ndogo hasa nyakati za usiku katika maeneo ya Ubungo, Manzese, Magomeni, Mwananyamala, Kinondoni, Posta Mpya na maeneo ya Posta ya zamani.

Katika baadhi ya klabu za usiku zilizoko maeneo ya Kinondoni, Sinza na katikati ya jiji (majina tunayo), dawa hizo zinauzwa nje ya majengo ya klabu hizo na watumiaji wake baadhi yao kuzitumia ndani wakiwa wanaendelea na kinywaji.

Mkoani Mwanza, maeneo ambayo biashara hiyo imeonekana kushamiri ni kwenye klabu karibu zote za usiku zilizopo maeneo ya Kirumba, Mtaa wa Rufiji, Uhuru na Mabatini.

Habari zilizopatikana kutoka katika jiji hilo, zilieleza kuwa mirungi huingizwa nchini kwa meli za mizigo kupitia mpaka wa Sirari na Ziwa Victoria.

Na ikifika Mwanza, mirungi huuzwa kwa Sh5,000 na wateja huitumia hadharani. Hata hivyo, vigogo wa biashara hiyo imekuwa vigumu kuwatia mbaroni kutokana na kujiwekea mtandao ambao unawalinda.

"Kontena (mtu ambaye anakwenda kuleta kutoka Pakistani au Afghanistan), anayemjua ni yule aliyemtuma sio zaidi ya hapo na 'pusher' (muuzaji mdogo) hamjui kigogo wa dawa hizo," alisema mtu mmoja ambaye aliwahi kutumika kusafirisha dawa hizo kutoka nje ya nchi.

Alisema: " biashara hiyo ni hatari kwani iwapo ukibainika kutoa siri inayoweza kusababisha vigogo hao kukamatwa au kufanya ujanja wa kudhulumu, basi ujue kwamba lazima watakuua."

Polisi wadaiwa kuneemeka na dawa za kulevya

Mmoja wa wauzaji wadogo jijini Dar es Salaam alilidokeza gazeti hili kuwa ingawa hawajui wafanyabiashara wakubwa wanaoingiza dawa hizo, anaamini baadhi ya polisi wanashiriki na wanautumia mzunguko huo wa dawa za kulevya, kujipatia fedha.

Habari zaidi zinasema baadhi ya nyumba zinazotumika kuuzia dawa za kulevya katika mitaa ya Livingstone, Mwanyamala na Magomeni, zimegeuzwa mradi wa kujipatia fedha na baadhi ya askari polisi jijini Dar es Salaam.

Zinaeleza kuwa askari hao huenda kuchukua fedha kwa wauzaji dawa za kulevya na kwamba askari hao ndio wanaowavujishia wafanyabiashara hao taarifa za msako wa kuwakamata.

Hata hivyo, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Nonosius Komba alilieleza gazeti hili kuwa, hana taarifa za kuzaagaa kwa dawa hizo. "Sina taarifa, lakini kwa vyovyote vile nitajitahidi kufuatilia suala hilo kwa karibu zaidi," alisema Kamanda Komba.

Uchunguzi unaonyesha kuwa msokoto mmoja ya bangi huuzwa kwa Sh250 katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha huku mirungi ikiuzwa Sh5,000 kwa fungu. Katika mji wa Moshi imebainika kuwa mirungi huingia nchini kupitia mipaka ya Horohoro, Holili na Namanga.

Kamanda aliyekuwa anahusika na kitengo cha dawa ya kulevya nchini, Godfrey Nzowa, aliwahi kukiri kukithiri kwa dawa za kulevya aina ya heroine, cocaine, na mirungi katika miji mikubwa nchini.

Alisema dawa hizo huingizwa nchini na wageni hasa kutoka nchi moja ya Mashariki ya Kati ambao wana uhusiano wa karibu na baadhi ya vijana wa Kitanzania wanaojihusisha na biashara hiyo.

Chanzo: Mwananchi 5/02/2011
 
tafakari ni kwa nini hata siku moja muingiza madawa hajawahi kukamatwa...vinakamatwa vidagaa tu!:twitch:
 
Hii biashara ina long chain kila siku wanavumbua njia mpya za kuingiza na kutoa popote pale
 
Back
Top Bottom