Dawa ya Babu wa Loliondo inatibu Lakini sio Ngeni

Exaud

JF-Expert Member
Oct 12, 2007
248
171
Wakuu,

Someni Makala hii mpate kuielewa vyema dawa anayoitoa Babu yetu wa kule Samunge Loliondo.

DAWA YA BABU WA LOLIONDO INATIBU LAKINI SIO NGENI – UTAFITI
Na Exaud G. Malya

Tangu mwezi Januari 2011 hadi sasa Watanzania, raia wa nchi jirani pamoja na raia wengine wa kigeni wamekuwa wakifurika kwa wingi kijijini Samunge Kata ya Digodigo, Tarafa ya Sale, Wilaya ya Ngorongoro, mkoani Arusha, umbali wa Kilometa kama 400 hivi kutoka mjini Arusha, kunywa dawa ya mitishamba inayoaminiwa kutibu magonjwa sugu hasa ya Ukimwi, Kisukari, Kifafa, Kansa, Pumu na maradhi mengineyo.

Dawa hiyo inayotolewa na Mchungaji Ambilikile Mwasapila au kwa jina maarufu "BABU" inatokana na mizizi na magamba ya mti unaoitwa "Muugamuryaga" au "Mugariga" kwa lugha ya kabila la Wasonjo wanaoishi Loliondo.

Dawa hii sio ngeni, imekuwa ikitumika tangu enzi za mababu zetu sehemu mbalimbali duniani ikitibu magonjwa mengi hasa ya zinaa. Hapa Tanzania tangu enzi za zamani imekuwa ikitumiwa na makabila ya Wambulu, Wabarabaig, Wasonjo na Wairaq kwa tiba za maradhi ya zinaa na magonjwa mengine ya moyo, pumu, kisukari, na maradhi mengine sugu kama tutakavyosoma kwenye makala hii.

Dawa hii inajulikana kwa majina mengi tofauti. Jina lake la kibotania ni Carissa edulis, majina yake mengine ya kienyeji ni Muugamuryaga kwa kabila la Wasonjo; Mtanda-mboo kwa lugha ya Kiswahili; Muyonza kwa lugha ya Kiganda; Emir kwa Kiarabu; Enkeldoring – noemnoem kwa lugha ya Kiafrikaans ya Afrika Kusini n.k.

Maelezo yake Kibotania

Mti wa Muugamuryaga (Carissa edulis) ni mfupi wenye wastani wa urefu wa meta 5, wenye miiba, matawi mengi, na utomvu wa maziwa. Gome lake ni laini lenye rangi ya kijivu, tawi lake changa huwa na ukubwa wa wastani wa sentimeta 2-5 kulingana na aina ya Muugamuryaga. Majani yake huwa ya kijani kibichi cheusi na yenye umbo kama la yai lililobenuka kwa juu kwa mzingo wa sentimeta 2.5-6 x 1.8-3.

Aina nyingine ya Muugamuryaga huwa na maua meupe yaliyochanganyika kidogo na rangi ya zambarau, nyekundu au rangi ya waridi. Maua hayo huwa na urefu wa sentimeta 1.8, pia una matunda yenye ukubwa wa sentimeta 1.1 yenye rangi nyekundu isiyokolea sana wakati yakiwa machanga, na yanapoiva huwa na rangi kama ya zambarau. Tunda lake lina mbegu kati ya 2-4 zenye umbo la bapa.

Mmea Tiba huu wa Carissa edulis unashabihiana sana na mti mwingine unaojulikana kibotania kwa jina la Carissa bispinosa. Tofauti yao kubwa ipo kwenye miiba. Miiba ya Carissa edulis imenyooka wakati ile ya Carissa bispinosa ina umbile la Y.

Kibaiolojia imethibitishwa kiutafiti kwamba huko Afrika ya Kusini maua yake huchipua kati ya mwezi Septemba na Desemba. Matunda hukomaa kati ya mwezi Novemba na January.


Ikolojia

Mmea Tiba wa Carissa edulis unapatikana kwa wingi kwenye maeneo ya kitropiki hususani nchi za Tanzania, Botswana, Namibia, Uganda, Kenya, Sudani, Senegal na Cameroon. Nchi nyingine ni Saudi Arabia, Nigeria, Afrika ya Kusini, Eritrea, Ethiopia, Ghana, Guinea, Cambodia, Japan, Myanmar, Thailand, Yemen, Vietnam na China.

Mmea Tiba huu hustawi zaidi kwenye mbuga za nyasi na vichaka zenye mwinuko wa kati ya mita 1,000-2,000 kutoka usawa wa bahari, na wenye wastani wa mvua kwa mwaka wa milimita 1,000-2,100 na joto la sentigredi 19-30 kwa mwaka. Mmea Tiba huu unastawi kwenye kila aina ya udongo.



Mazao ya Carissa edulis


Tiba mmea huu hutoa matunda, majani ya mifugo, kuni, sumu na dawa. Matunda yake ni matamu na mazuri ya kula. Huko Ghana huchanganywa na chakula kama kiamsha hamu cha kula chakula .

Vinega inaweza ikatengenezwa kwa kuyavundika na kuyachachua matunda ya mmea huu. Huko Sudani na Kenya hutumia matunda haya kutengeneza jamu. Mizizi yake huwekwa kwenye vibuyu kuwezesha kupata ladha nzuri inapochanganywa na supu au vyakula vingine vya nyama.


Majani yake hutumika kulishia mifugo kama vile mbuzi na ngamia, hasa kwenye maeneo makavu ya Sudani. Mti huu hutumika kama nishati nzuri ya kupikia. Mti huu pia ni sumu, huko Kenya kipande cha mzizi wake huwekwa kwenye paa la nyumba ili kufukuza nyoka.

Makabila mengine ya Kiafrika yamekuwa yakitumia utomvu wa mti huu kwa ajili ya kupaka kwenye ncha za silaha za jadi kama vile mishale na mikuki kwa ajili ya kuwindia na kupigana vita.


Mmea tiba huu umekuwa ukitumika kama tiba tangu zama za kale, umekuwa ukitibu magonjwa mengi kati yao yakiwa ni ya zinaa (Kaswende, Kisonono, Gonoria na Malengelenge), Saratani, Moyo, Pumu, Kisukari, Malaria, Maumivu ya meno, Nguvu za kiume, Tegu, vidonda vya tumbo, maumivu ya kifua na maradhi mengineyo.


Utafiti wa Dawa ya Carisa Edulis (Muugamuryaga)


Utafiti wa Tiba mmea huu umeshafanyika sehemu mbalimbali duniani; Utafiti umeonyesha pasipo shaka kwamba mizizi yake ina mchanganyiko uitwao Carissin ambao una uwezo mkubwa wa kutibu saratani.

Matawi yake yana mchanganyiko wa chembechembe za Quebrachytol na Cardioglycosides zenye uwezo mkubwa wa kutibu Tegu.

Huko nchini Guinea wao huchemsha majani ya tiba mmea huu na maji yake yanatumika kupunguza maumivu ya meno. Huko Ghana maganda ya mizizi ya tiba mmea husagwa na kuchanganywa na viungo vya vyakula na kuingizwa kwenye njia ya haja kubwa ya mgonjwa ili kumtibu maumivu ya kiuno na maumivu mengine ya mwili.

Mabaki ya mizizi huchemshwa tena ili kutibu matezi na uvimbe uchungu.

Utafiti wa hivi karibuni uliofanyika mwaka 2005 nchini Kenya, na Kituo cha utafiti wa dawa za mitishamba (Centre for traditional Medicine and Drug Research, Kenya Medical Research Institute).

Utafiti huo ulihusisha timu ya wataalamu 12 ikiongozwa na Mtafiti mkuu Bw. Festus M. Tolo akisaidiwa na Geoffrey M. Rukunga, Faith W. Muli, Eliud N. M. Njagi, Wilson Njue, Kazuko Kumon, na Geoffrey M. Mungai. Wengine walikuwa ni Charles N. Muthaura, Joseph M. Muli, Lucia K. Keter, Esau Oishi, na Mawuli W. Kofi-Tsekpo.

Utafiti huu ulidhaminiwa na shirika la Kimataifa la maendeleo la Japan (Japan International Cooperation Agency [JICA]). Utafiti ulipokelewa tarehe 26 July, 2005, ukaidhinishwa tarehe 24 August 2005 na kuwekwa kwenye mtandao tarehe 29 Septemba 2005(www.science.direct.com ).

Utafiti ulifanyika kwa nia ya kuthibitisha kama kweli dawa ya mitishamba inayotokana na mti wa Carissa edulis ina uwezo wa kutibu magonjwa ya zinaa hasa virusi vya malengelenge (Herpes Simplex Virus [HSV]).


Malengelenge humsababishia mtu kupata virusi vya ukimwi; Utafiti umeonyesha kwamba tiba mmea wa Carissa edulis unatibu mara moja malengelenge sugu kwa asilimia kubwa. Watafiti wa kituo cha utafiti wa dawa za mitishamba huko Kenya waliwatumia Panya ili kuthibitisha ubora wa tiba ya Carissa edulis.

Panya waliambukizwa virusi sugu vya malengelenge(HSV), na kugawanywa katika makundi mawili; Kundi la kwanza walitibiwa, na kundi la pili hawakutibiwa. Panya waliotibiwa walinyweshwa dawa yenye kipimo cha 250 mg/kg na iliwezesha kutibu malengelenge kwa zaidi ya asilimia 50%. Dawa hiyo iliwezesha pia muda wa matibabu kuongezeka kati ya asilimia 28% na 35%.

Vifo kwa panya walioambukizwa virusi vya malengelenge na kutibiwa kwa dawa ya Carissa edulis vilipungua kwa kati ya asilimia 70% na 90% ukilinganisha na asilimia 100% ya vifo vya panya walioambukizwa virusi vya malengelenge lakini hawakutibiwa. Kipimo cha dawa cha 250 mg/kg hakikuwadhuru panya wala kugeuka na kuwa sumu mwilini mwao.


Matokeo ya utafiti huu yamethibitisha pasipo shaka kwamba dawa ya mitishamba inayotokana na mti wa Carissa edulis au Muugamuryaga unaotumiwa na Babu huko Samunge, Loliondo unaweza kuponyesha magonjwa ya zinaa hasa virusi vya malengelenge na hata virusi vya ukimwi kwa kuwa ni kundi moja la magonjwa ya zinaa.

Utafiti wa kimaabara (Clinical Trial) unahitajika kufanyika zaidi kuweza kuelewa uwezo wa tiba mmea huu katika kutibu magonjwa sugu ya Ukimwi, Kisukari, Saratani, Pumu, Kifafa na mengineyo.


Makala hii imeandikwa na Exaud G. Malya, 0754 390402, E-mail: exaudmalya@yahoo.co.uk
 
Back
Top Bottom