Dar kinara wa TB nchini

Mahesabu

JF-Expert Member
Jan 27, 2008
5,971
3,827
NA EPSON LUHWAGO
“HATUWEZI kupambana na ukimwi kama hatutilia mkazo katika mapmbano dhidi ya kifua kikuu.”
Hiyo ni kauli ya Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Mzee Nelson Mandela, aliyoitoa katika Mkutano wa Kimataifa wa Ukimwi, Julai 14, 2004 nchini Thailand. Kauli hiyo inasadifu na hali halisi ya sasa ambapo tatizo la ukimwi na kifua kikuu bado liko juu na linazidi kuitikisa dunia. Taarifa zinaeleza kuwa zaidi ya watu bilioni mbili duniani wana kifua kikuu (TB) na zaidi ya milioni 33 wanaishi na virusi vya ukimwi na miongoni mwao wanaishi na virusi vya ukimwi (VVU) na kuugua ukimwi. Aidha, watu milioni 11, kwa mujibu wa
Shirika la Afya Duniani (WHO), wana maambukizi ya VVU na TB. Kutokana na hali hiyo halisi, zinahitajika juhudi kubwa za kupambana na kifua kikuu ili kuweza kudhibiti na kupambana na ukimwi, kama alivyosema Mandela. Kauli ya Mandela inawakumbusha wadau wa afya duniani kote, hususan leo, ambapo dunia inaadhimisha Siku ya Kifua Kikuu. Wakati maadhimisho hayo yanafanyika duniani kote, Tanzania inakabiliwa na changamoto kubwa katika mapambano ya ugonjwa huo ambao umeleta athari kubwa.
Miongoni mwa athari hizo ni vifo miongoni mwa watu pamoja na nguvu kazi kupukutika. Asilimia kubwa ya watu wanaougua TB ni wale wenye umri wa miaka 24 hadi 49, ambao ni tegemeo kubwa katika uzalishaji mali. Kwa miaka ya karibuni, tatizo la kifua kikuu limechangiwa au kukua kwa kasi kutokana na ongezeko la maambukizi ya VVU na ukimwi miongoni mwa wagonjwa.
HALI TANZANIA
Taarifa iliyotolewa na Mwanasayansi Mtafiti wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa wa Binadamu (NIMR), Dk. Bernard Ngowi, hivi karibuni mjini Bagamoyo, inaonyesha kuwa Tanzania ni moja ya nchi 23 duniani zenye tatizo hilo kwa kiwango cha juu.
Dk. Ngowi katika taarifa hiyo ambayo aliiwasilisha katika warsha juu ya kifua kikuu, alisema wastani wa watu 340 kati ya 100,000 nchini, wana kifua kikuu wakati Uganda ni watu 342 kati ya 100,000.
Alizitaja nchi zingine kuwa ni India, China, Indonesia, Cambodia, Nigeria, Bangladesh, Pakistan, Philippines, Ethiopia, Afrika Kusini, Russia, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Vietnam, Kenya, Brazil, Thailand, Msumbiji, Myanmar, Afghanistan, Zimbabwe na Peru.
DAR KINARA
Wakati Tanzania ikiwa moja ya nchi zenye maambukizi makubwa ya kifua kikuu duniani, Dar es Salaam inaongoza kuwa na watu wengi wanaokumbwa na ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa takwimu, asilimia 24 ya maambukizi na watu wenye kifua kikuu wanatoka katika jiji hilo lenye wakazi wengi kuliko mji wowote nchini.
Mkoa huo unafuatiwa na Tanga, Mwanza na Arusha yenye asilimia saba kila mmoja, Iringa na Mbeya (asilimia sita) na Morogoro asilimia tano. Kilimanjaro, Arusha na Dodoma zina asilimia nne kila moja wakati mikoa mingine iliyobaki ina asilimia tatu na kushuka chini.
Sababu kubwa ya kuwepo kwa kiwango kikubwa cha maambukizi ya TB pamoja na wagonjwa katika jiji la Dar es Salaam ni hali halisi ya eneo lenyewe.
Msongamano wa watu katika meneo ya mikusanyiko ni mkubwa, jambo ambalo ni rahisi watu kuambikizana kifua kikuu.
Watu katika mikusanyiko kama vile Kariakoo na vituo vya mabasi, wamekuwa wengi kiasi cha kushindwa kupata hewa ya kutosha. Kwa kawaida, kifua kikuu huambukizwa na bakteria kwa njia ya hewa.
Vile vile hali ya usafiri katika jiji la Dar es Salaam si ya kuridhisha. Watu wamekuwa wakibanana katika magari hasa daladala, jambo ambalo linaweza kuwafanya baadhi yao kuambukizwa magonjwa yatokanayo na hewa, kifua kikuu kikiwemo.
Kwa upande wa watoto hasa wanaosoma, nao wako katika hatari ya kuambukizwa kutokana na kulundikana madarasani na kwenye mabasi wanayosafiria kwenda shule na kurejea nyumbani.
Sababu nyingine inayofanya Dar es Salaam kuwa kinara ni pamoja na msongamamo wa watu katika magereza na mahabusu za Ukonga, Segerea na Keko.
Vile vile, ujenzi holela wa makazi ya watu ni chanzo cha kuwepo kwa hali hiyo. Maeneo mengi, kama vile Manzese, Tandale, Mwanayamala, Buguruni, Kigogo na Mabibo yamejengwa holela kiasi cha kutokutoa nafasi ya kuwepo kwa hewa ya kutosha.
Matokeo ya kuwepo hali hiyo ni mgandamizo wa hewa hivyo kuwepo uwezekano wa kuambukizana magonjwa kwa njia ya hewa na uchafu. Kifua kikuu ni rahisi pia kuibuka miongoni mwa wakazi wa maeneo hayo.
Katika mikoa kama Iringa na Mbeya, ongezeko la kifua kikuu ni kubwa kutokana na kiwango cha juu cha maambukizi ya VVU.
Mikoa hiyo kwa sasa ndiyo iliyo juu kwa mambukizi ya virusi vya ukimwi, hivyo kama wataalamu wanavyosema kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya ukimwi na kifua kikuu.
NINI KIFANYIKE?
Kuwepo kwa hali hiyo ambayo si ishara nzuri kwa maendeleo ya watu, hivyo jitihada zinahitajika ili kuhakikisha tatizo la kifua kikuu linapungua.
Jambo la msingi la kuzingatia ni elimu kwa umma juu ya kifua kikuu. Kupitia elimu hiyo, watu watapata uelewa juu ya ugonjwa wenyewe, jinsi unavyoambukizwa na namna ya kujikinga nao.
Watu watakapoelewa yote hayo, watakuwa na uwezo wa kufika katika vituo vya tiba pindi wanapoona dalili za ugonjwa huo, ambazo baadhi ni kukohoa kwa muda mrefu, kutoa jasho jingi kupita kiasi na kupungua uzito ghafla.
Serikali kwa upande wake, inapaswa kutatua tatizo la ukosefu wa wataalamu wa afya na dawa ili wananchi waweze kupata huduma na ushauri wa kitaalamu bila matatizo.
 
Back
Top Bottom